Jumatano, 5 Novemba 2014

Nikajimwaga Kwa Mwenye Mali!

Naitwa Salome Shemazua mkazi wa Pongwe Jijini Tanga nina umri wa kati ya miaka 35, ni mshichana mwenye umbo zuri la kibantu ambalo linaweza kumvutia mwanaume yeyote mwenye akili timamu na mwenye kupenda wanawake wenye uasilia yaani wale wasiopenda wanawake vimbaumbau wale wanaoijifanya eti wana menteini na kukondesha vipaja vyao kaa kuku wa kisasa, mimi ni kibonge bwana umbo nambari nane lakini hata hivyo sijaolewa. Hiyo sio shida kwani wote tunajua kuwa kuolewa nako ni majaliwa.


Hata hivyo katika kubangaiza hapa na pale katika shughuli za maisha nilitokea kupendwa na baba mmoja hivi wa makamo sikuwa na muda hata wa kuuliza umri wake ingawa alionekana kama angeweza kunizaa na huenda pia ningeweza kuwa mwanae wa pili au watatu hivi, nilikutana na baba huyu pale Texas motel moja ya baa maarufu hapa Pongwe, baba huyu aliyekuwa anafanya kazi saruji kiwanda cha simenti kilichopo karibu na mji wa Pongwe alitupa ndoana yake kwangu nami bila ya fedheha sikuwa na hapana  nilimkubalia, wenyeji wangu walikwisha kunipa stori kuwa wanaume wa saruji wana pesa kama njugu kutokana na mishahara mizuri wanayolipwa na kiwanda hicho ambacho huchangia mapato ya kutosha katika jiji la Tanga niliona nami nimepata wangu wa kumchuna,

 Nilijitahidi sana kumpagawisha baba Yule kimapenzi kama unavyojua hapa Tanga waja leo waondoka leo  nilimpagawisha na mambo ya kipwani, nilijituma hasa nikijua kuwa hii ndio nafasi ya kumfanya baba huyu ajikite kwangu na kumsahau bi mkubwa,  hasa ukichukulia kuwa Alisha mwaga malalamiko kibao kuhusu bi mkubwa kuwa hajitumi na ni mshamba na kuwa hata kimaumbile mimi nimemzidi bi mkubwa kwa kila idara alidai mzee huyu kuwa bi mkubwa huyo ni kafupi na kamekomaa na ukikaona ni kuwa hata mkononi hakajai sikujua kwanini sasa alimuoa au alilazimishwa lakini niliona vyovyote iwavyo shuhuda hizi zinanipa ujasiri wa kujituma kuliko, na kumuonyesha kuwa na sisi wenye maumbile ya kibantu mchezoni nasi hatujambo nikijipindua hivi na vile kuonyesha manjonjo  kwa ujumla nilifanikiwa sana kumroga Baba Yule wa bara huko, hapa simaanishi maswala ya kishirikina namaanisha jinsi nilivyofanikiwa kumfisadi kimapenzi baba Yule,


Kujituma kwangu hakukuwa bure kwani alinihamisha kwenye nyumba ya kupanga na kunijengea kajumba kangu kazuri maeneo ya Ambangulu kwa wale wanaoijua Pongwe kule Tanga, nilijengewa kajumba potabo kwani kana vyumba vitatu na kila kitu ndani yaani selfu konteini  niliendelea kujidekeza na kupewa kila kitu nilichokitaka  ingawa nilimsikia Buzi wangu akilalamika kuwa ana maswala ya Ada ya watoto na kuwa na majukumu mengine huko kwa bi mkubwa, mi sikujali kwani niliendeleza ufisadi wangu bila kujali kuwa kuna kafamilia kanaumia  ingawa kaubinadamu kanaponijia  huwa najiuliza je ningelifanyiwa miye ingekuwaje? Lakini Mapepo ya ukatili yaliponivaa sikujali nilijitia moyo acha huyo bi mkubwa akome, 

Mungu ametuleta duniani tukomeshe wanawake wachovu wasiojituma kwa nini amtese baba wa watu ? mtu unapata bahati ya kuolewa halafu uinaichezea kweli upele anapewa asiye na kucha nilijitia moyo kuhalalisha upashikuna wangu na ufisadi kiwembe na nilitiwa moyo kwani wanawake wengi pale Pongwe hizo ndo issue zetu wengi ni nyumba ndogo.


Siku moja iliyopelekea kuelezea kisa hiki kama waswahili wasemavyo  “Mwizi zake arobaini” au za mwizi arubaini, Nilipatana na mzee wangu Yule  kwamba tukatese huko maeneo ya Raskazone njia ya kwenda hospital kuu ya Mkoa bombo karibu na daraja upande wa kulia ambako kuna hotel moja maarufu siku hizi nyuma kidogo ya shule ya sekondari ya mkwakwani sipendi kutaja jina la hoteli hiyo kwa maslahi ya mwenye hoteli hata hivyo kwa wenyeji wa Tanga watakuwa wamenipata vilivyo lakini hata kabla ya kwenda hoteli, Bwanangu Yule aliniambia nitangulie mjini na kupitia saluni kisha yeye angenipitia akitokea Saruji anakoishi  akiwa na usafiri wake, Nilitangulia na rafiki zangu kadhaa waliokuwa wakienda mjini nao kwenye mishemishe zao tuliingia saluni moja karibu na stendi kuu ya mji wa Tanga katika barabara maarufu kama Taifa rodi, saluni hii inapendwa na watu wengi sana hususani wakiwemo wale wanaotokea Pongwe hasa kwa sababu ya utaalamu wao pia wa kusuka rasta, na pia kuandaa maharusi, kama iliyo ada tulikutana na wanawake wengine kadhaa wengine wakihudumiwa na wengine wakisubiri, tulipofikia hatua ya kuhudumiwa  kama unavyojua mambo ya umbeya wa saluni tulianza na mada mbalimbali za kisiasa, umbeya udaku na mengineyo kedekede na baadaye ilikuja mada ya uchunaji mabuzi, hapo ndipo nilipodakia kama nimefikishwa kwani mimi sio mzuri sana kwenye maswala ya siasa za Tanzania nilizichoka kwani niliona kama tunazugwa tu  hivyo sikuwa na interesti na siasa tangu alipostaafu Mkapa na hata kufatilia Bunge nilifuatilia alipohutubia Kikwete ile hutuba yake ya bungeni ya kwanza kabisa, kwa hiyo eneo hili utafikiri nilipewa maiki nilieleza kuwa kuchuna mabuzi kunalipa, kulikuwa na mama mmoja mfupi aliyeonekana kama amekomaa hivi alionekana kupinga mada ya maswala ya waume za watu na kuonya kuwa inatesa sana wale walioolewa. Nilimkatisha mama huyo na kuanza kumsomesha kama mtoa mada mkuu huku nikiungwa mkono kwa herufi kubwa mada hii ilinigusa utafikiri ndio mwenyekiti wa kamati Fulani huko Bungeni  nilionyesha faida kadhaa za kufaidika kutokana na kuchuna mabuzi, huku nikitamba juu ya kajumba nilikojengewa  na aina ya simu maarufu kama blakiberi niliyonunuliwa na buzi na nilionyesha wazi jinsi wanaume wa saruji wanavyojua kuhonga na kuwa hata pale saluni buzi wangu atanipitia kwenda kutesa maeneo ya Rasikazone na kuwa atalipa hata hela ya gharama yote ya pale saluni, nilitoa mada siku hiyo utafikiri kungwi wa kicheni pati niliwaponda sana wanawake wachovu na kueleza pia kuwa buzi wangu anasema kuwa ka mwanamke kake kamekondeana na kukomaa kama nyigu na kuwa hata kwenye mkono hakajai hakana intateiniment na kwa mkwara mkubwa wakati mwingine niliwasiliana naye kumuulizia hani kuwa yuko wapi na mbona anachelewa ili mradi tu kuwapagawisha wanasaluni pale, Mama Yule kimbaumbau  aliyekuwa na nywele nzuri sana nyingi lakini kanyimwa nyama mwenye uso uliionekana kama ana mapito hivi kama wasemavyo watu wa dini Fulani ambao hujidai wanaimani kali,  alinyamaza kimya kama amelowa maji, nilimwaga sera na hatimaye alionekana kuunga mkono kama mbunge aliyepotea kutoka kambi ya upinzani, hilo lilinipa kichwa na kujiona kama ninatawala saluni kwa muda wana saluni wenyewe walikuwa bize kutushughulikia wakiwa kimya  na wengi walikuwa wakinisikiliza jinsi nilivyojimwaga na kumkandia mke mwenza ambaye nilikuwa simfahamu. Mwisho ikawa kama wote tumeshughulikiwa na wengine walikaa vitini kwaajili ya kuhudumiwa.


Niliinua simu yangu aina ya blakiberi niliyohongwa na kumjulisha dalingi wangu kuwa niko tayari na kuwa aje alipe tuondoke, kwa kawaida anaijua saluni hiyo kwani hiyo haikuwa mara ya kwanza, lakini kwa vile siku ile nilijimwaga sana kila mmoja alikuwa na hamu ya kumuona huyo buzi ni wa aina gani, alikuja mzee Yule na gari yake ya kifahari aina ya mark tu saluni grandi alipoteremka  aliingia mojakwamoja saluni na  nilimkimbilia kwa busu na mdeko wa nguvu “hai hani karibu umekuja nchukua eh njoo basi hani unlipie kisha ndo tuondoke”, jambo la kushangaza siku ile ni kuwa baba Yule katika hali isiyokuwa kawaida yake alikuwa kama ananitaaliza, au kunishushua kwa lugha za kitanga, Busu langu la siku ile lilikuwa pia limechanganyika na ishara ya kuwaonyesha kuwa huyu nitakayembusu ndiye kama vile alivyofanya mtume mmoja wa Bwana Yesu aliyeitwa Yuda Iskariote, lakini kama nilivyokugusia awali mwitikio wa shuga dady Yule ulikuwa kama amepigwa ganzi na ghafla mama Yule kimbaumbau alisimama kama afande  na kuanza kuteremsha matusi mazito sana  yakielekea kwa baba Yule  huku akilalamika kuwa watoto wamefukuzwa ada wameshindwa kwenda shule, nyumbani tunashindia dagaa na maharage tu kumbe wewe unajengea Malaya zako, kila mmoja alikuwa anashangaa na idadi ya watu ilianza kuongezeka pale saluni matusi yalimwagika kama mvua na hatimaye nikageukiwa miye na  yalimwagikia upande wangu  na nilipojaribu kujibu huku nikiwa nashangaa nilipokea mkong’oto mkali nikiambiwa Malaya wewe firauni mkubwa nikiambiwa ukome wewe kuchukua waume za watu nilishangaa mama huyu niliyekuwa naye saluni inakuwaje ana mamlaka kubwa kiasi hiki ndipo akili ilianza kunijia kuwa huku ndio kufumaniwa, Viungo vilinilegea kipondo kile kilipelekea kuchaniwa nguo  kiasi cha kuwa uchi, watu niliokuwa nao saluni walianza kupata majibu kuwa kumbe mwenye mali halisi alikuwa ni mwanamke Yule nilizomewa kama paka mwizi, ilikuwa ni aibu ya mwaka siwezi kusahau jamani  umbeya wa saluni bwana kumbe nilikuwa najimwaga kwa mwenye mali, wanaume za watu shoga nimekoma, unataka kujua yaliishije we mbeya sana mijimacho ka chura mbona ulipoacha kunyonya maziwa ya mamako mi sijakuuliza? Si uliacha bila kuambiwa sasa ulitaka niendelee kusumbua nyumba za watu mkong’oto ule ulikuwa kama zile stori za betina na zena katika magazeti ya sani zamani. kwa sasa nimeamua kujishughulisha na shughuli ndogondogo za kibiashara, nimeachana na maisha ya kupenda dezo kumbe bure ni gharama.

Na Rev. Innocent Kamote
Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima
0718990796
0784394550

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni