Jumapili, 31 Januari 2016

SOMO: JINSI MUNGU ANAVYOCHAGUA VIONGOZI



Mstari wa Msingi: 1Samuel 16:7 “Lakini Bwana akamwambia Samuel, Usimtazame uso wake wala urefu wa kimo chake ; kwa maana mimi nimemkataa. Bwana haangaliikama binadamu aangaliavyo; Maana wanadamu huitazama sura ya nje, bali bwana huutazama moyo”

      Mfalme Daudi alipatikana kwa Mapenzi ya Mungu na sui kwa shinikizo la Wanadamu
 
Utangulizi:
Hivi Karibuni Nchi yetu itakuwa na uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge na madiwani, na kwa upande wa uchaguzi wa Rais ni wazi kuwa nafasi hii inahitaji Rais mpya kwa mujibu wa utaratibu tuliojiwekea, ni wazi kuwa kwa Tanzania, Marais hutokana na vyama vya kisiasa na hivyo vyanzi vinavyoweza kuleta Rais ni vyama vya siasa, na iko wazi kuwa kuna vyama vya siasa kama CCM, CUF, NCCR, CHADEMA, UDP, DP, ADC, na kadhalika, wote tunakubali kuwa moja ya chanzo kikubwa kinachoweze kutupatia viongozi katika Tifa hili ni CCM, hili halina ubishi kutokana na mfumo mzima ulivyo kwa taifa hili, ingawa inaweza kutokea tofauti wakati mwinginine lakini kwa Tanzania sio sasa

Katika wakati huu wa uchaguzi kuna mambo mengi ya kujifunza, au ambayo tunaweza kuwa wote tumejifunza na ni dhambi kuyakalia kimya bila kuyatafakari, vinginevyo Historia itatuhukumu!

Katika chaguzi za nyuma zilizopita, vituko kadhaa vilivyopata kushuhudiwa ilikuwa ni pamoja na kutabiriwa kumwagika kwa Damu, tetesi za vita, maonyo dhidi ya taifa, na pia baadhi ya watu kutabiri kuwa Fulani ndio chaguo la Mungu n.k.

Uchaguzi wa mwaka huu pia kupitia ndani ya mchakato wa CCM wengi wetu, tuliona na kushuhudia watu walionyesha wazi kuwa ni nani amechaguliwa na Mungu kuiongoza Tanzania kupitia CCM, watumishi wa Mungu, wachawi, wanajimu na Mashehe kila mmoja alikuwa na majibu kuwa ni nani anafaa kuwa kiongozi wa Taifa hili wakati Kikwete akiondoka Madarakani
Neno la Mungu lina majibu ya kutosha kuondoa utata huo uliojitokeza, kwa kurudia Historia ambayo watanzania lazima tuikumbuke kila wakati na kujifunza kutoka katika Neno lake namna na jinsi MUngu anavyojipatia viongozi.

Biblia imejaa Mifano mingi jinsi Mungu alivyojipatia viongozi wa aina mbalimbali wengi wao wakiwa ni hodari, viongozi hao wanaume kwa wanawake, wafalme, waamuzi, makuhani, manabii na Mitume Je Mungu aliwapataje viongozi hao ni mfumo gani Mungu aliutumia kupata viongozi? Njia hii ya Mungu kujipatia viongozi ikitumika katika taifa letu tutaona viongozi wazuri na watakaotimiza mengi makubwa katika Taifa letu wakiendelea kupatikana

Jinsi Mungu anavyochagua viongozi
Katika Mstari wetu wa msingi pale juu tunaona kuwa Daudi ni moja ya mfano wa viongozi waliopata kuiongoza Israel na kuiletea heshima kubwa sana, aliongoza Israel kwa miaka 40, Isamuel 16. Israel walikuwa chini ya utawala wa Saul ambaye sasa alikuwa anafikia ukingoni, Na Mungu anamtuma Nabii Samuel katika Familia ya Yesse akimueleza wazi kuwa amejipatia mfalme katika wanawe ! 1Samuel 16:1. Hakuna mtu alimjua si Samuel wala hata Yese mwenyewe ambaye alikuwa ndio chanzo kikuu cha kumleta mfalme!
Kumbuka kuwa hakukuwa na uteuzi wa kiofisi, hakukuwa na Kampeni, wala mijadala wala kujitangaza kwa mbwembwe, wala kwa kueleza sera mipango na mikakati au nini wataufanyia utawala wa Israel, Bali Mungu mwenyewe aliangalia na kuchagua ni nani atakuwa mrithi wa Sauli, sio hivyo tu lakini hebu chunguza njia ambayo Mungu anaitumia kumpata kiongozi ambaye ni chagua lake!
Wakati Samuel anafika nyumbani kwa Yese, Yese ambaye ni chanzo kikuu cha kutoa kiongozi anawaleta mbele ya nabii wanae wote wakubwa akiwa na furaha sana, Kumbuka kuwa hata Samuel hakuwa anajua kuwa ni nani atakuwa mfalme licha ya kuwa Nabii mkubwa na mwenye uzoefu na ujuzi kuhusu sauti ya Mungu Mungu alimwambia wazi “USIMTAZAME USO WAKE,WALA UREFU WA KIMO CHAKE, KWA MAANA MIMI NIMEMKATAA” Ni maneno magumu sana haya kutoka kwa Mungu hasa kama yanaelekezwa kwako kukataliwa Mh? Ni kama ukatili Fulani hivi lakini Mungu yuko kazini tena makini kuhakikisha kiongozi bora anapatikana, kwa sababu yeye haangalii mbwembwe za nje anaangalia Moyo!

Ni wazi kuwa wana wote wa Yese waliopitishwa kwa Samuel Mungu aliwakataa Mstari 8-10 Mungu anauwezo wa kuchunguza moyo Ayubu 34:21, Waebrania 4:13, 1Yohana 3:10.  Mungu ana namna yake ya kuangalia mambo katika namna iliyo njema kabisa nay a kiungu, na hivyo wana wote wa Yese waliopitishwa hawakuwa wanafaa kwa kwa nafasi ya Ufalme, Mwisho Yese alimuita mwanae mdogo Daudi ambaye hakuna hata mmoja alidhania kuwa angefaa hata kuletwa mbele ya Samuel

Hakika Mungu huchagua viongozi katika namna tofauti kabisa na sifa na mitazamo ya kibinadamu
Kila mahali katika Biblia tunaweza kuona mifano hii ya jinsi Mungu alivyojipatia viongozi, Musa aliyekuwa na miaka 80 akichunga kondoo wa mkwewe jangwani, Malaika wa Bwana alimtokea na kumuagiza awaongoze Israel kutoka Misri Kutoka 3. Elisha alikuwa akilima kwa ngo’mbe kwa jozi 12 na Eliyanabii alipita na kumtupia vazi kama ishara ya kuwa mrithi wake (1Wafalme 19:15-21) kumbuka kuwa Eliya aliambiwa watu ambao alipaswa kuwatia mafuta ambao Mungu alikuwa amewachagua, wakiwemo wafalme wa Israel na Syria 

Katika agano jipya mitume walichagua mtume mwingine ili kujaza nafasi ya Yuda aliyemsaliti Yesu, kwa kura lakini waliomba Mungu awaonyeshe ni nani aliyemchagua kati ya wawili waliopendekezwa Matendo 1:24-25 waliomba Mungu anayejua mioyo ya watu awaonyeshe. Hilo ni la Muhimu sana!

Mungu pia aliamua kumchagua mtu mwingine aliyeitwa Sauli ili awe Mtume yeye mwenyewe Matendo 9 Sauli yaani Paulo alitambua mara moja kuwa alikuwa akiwatesa watu wa Mungu, aliokoka na kubatizwa na akawa mtume mkubwa sana ilileta mashaka sana kwa watu wa kanisa wakati huo lakini kumbuka maneno haya Matendo 9:15 “ Lakini Bwana akamwambia  Nenda tu kwa maana huyu ni chombo kiteule kwangu alichukue jina langu mbele ya mataifa , na wafalme na wana wa Israel”

Mtu anaweza kudai kuwa hawa walikuwa viongozi wa kiroho, na labda Mungu hajihusishi na uchaguzi wa viongozi wa kisiasa na wakuu wa serikali kwa nnjia hizo! Jibu ni Hapana Mungu pia hujihusisha kuchagua viongozi wa kisiasa kama tulivyoona kuhusu mfalme wa Israel na Syria pale juu Biblia iko wazi kabisa kuwa aliye juu ndiye anayetawala katika falme za wanadamu Daniel 4:17 “hukumu hii imekuja kwa agizo la walinzi, na amrihii kwa neno la watakatifu: kusudi walio hai wapate kujua ya kuwa Aliyejuu anatawala katika ufalme wa wanadamu naye humpa amtakaye tena humtawaza juu yake aliye  myonge (myenyekevu)”

Hata inapotokea kuwa wanadamu wanalazimisha kiongozi wa aina wanayemtaka Bado Mungu huchagua yeye mwenyewe lakini mabaya yatakayowapata yatakuwa ni matokeo ya kutaka kwenu, Mungu aliwafanyia Israel walipotaka ufalme kama mataifa mengine kinyume na Samuel 1Samuel 10:23-24 Mungu akiruhusu wanadamu wakajichagulia atakuacha upate somo kuwa uchaguzi wa mwanadamu ni wa kipuuzi na tutaumia! 1Samuel 9: 15-17
Ni muhimu kufahamu kuwa Mungu anapochagua wala haiitajiki kampeni wala uchaguzi kwa vile sio DEMOCRACY lakini ni THEOCRASY yaani sio Mfumo ambao watu wengi au wote wanapata nafasi ya kuchagua MKUMBO bali ni mfumo ambao Mungu anaibua kiongozi kwa jicho lake kutoka kusikotarajiwa, uchaguzi wa Mungu hautokei chini kwenda juu bali juu kuja chini, HIVYO SAUTI YA WENGI SIO SAUTI YA MUNGU! Nakazia tena  SAUTI YA WENGI SIO SAUTI YA MUNGU mwisho wa kujinukuu.

Kampeni na uchaguzi wa kupiga kura uko kwaajili ya kuendeleza tabia ya kiongozi na kutekeleza mapenzi ya Mungu, lakini ukweli Mungu anapochagua huitaji kuwashawishi wanadamu kwa namna yoyote wala kwa sera na mipango utakayoifanya Mungu anawaweka katika ofisi na watu wanatakiwa kumfuata.

JINSI GANI VIONGOZI WANAWEZA KUFANIKIWA?
Hili ni swali muhimu Je kila kiongozi anayetokana na Mungu anaweza kufanya vizuri jibu ni ndio ikiwa wataendelea kumfuata Mungu na maagizo yake “Yoshua 1:5-9, 1Wafalme 1:1-3” Hata baada ya kufa kwake Daudi ingawa aliwahi kufanya dhambi katika maisha yake anasifiwa na Mungu kama mtu aliyeupendeza Moyo wa Mungu Matendo 13:22, Musa pamoja na makubwa aliyoyafanya na madhaifu aliyokuwa nayo anatajwa kuwa mtu mnyenyekevu zaidi kuliko wote waliokuwa juu ya uso wa duni Hesabu 12:3, Mungu hutuchagulia viongozi wazuri wenye kuleta ufanisi mkubwa, wenye moyo na uzalendo atakaowatumia kwa namna ya kupita kawaida na kuleta mafanikio makubwa ambayo kila mtu anayataka na watu hupata faraja kubwa na kufurahi
Mithali 29:2 “ wenye haki wakiwa na amri watu hufurahi bali mwovu atawalapo watu huugua”
Je ungependa nani akuchagulie kiongozi ? Mungu huchagua viongozi

Kumbuka.
·         Kiongozi anayetoka kwa Mungu ni vigumu kumtambua mpaka Mungu amfichue, Samuel alikuwa nabii mkubwa lakini ilikuwa ngumu kwake kujua Mungu anamtaka yupi katika shina la Yese
·         Tuwasamehe viongozi wote wa dini waliotabiri na kutamka kuwa mtu Fulani ni chagua la Mungu na wengine Fulani asipokuwa Raisi mniue kwa vile hao ni wanadamu na huenda hawajui Mungu anajipatiaje viongozi
·         Tuwasamehe watabiri na wanajimu kwa vile inawezekana uwezo wao wa kuona uliishia kwenye nyumba ya Yese yaani walitabiri wale walioishia kwenye tano bora ua wengine waliokatwa mapema tuwasamehe kwa vile ni wanadamu na hawajui mapenzi ya Mungu

·         Tuache kujivuna na kujifikiri kuwa sisi ni watu maalumu tunayoweza kuyajua mapenzi kamili ya Mungu aidha tuache kwenda kwa Mkumbo kwa vile Mungu hachukuliwi na umati wa watu
·         Acha kuwaombea na kuwalilia wale ambao Mungu amewakataa Mungu hutazama Moyo, wajibu wetu siku zote ni kumuomba Mungu atuonyeshe ni nani aliye katika mapenzi yake na kujiandikisha na kwenda kupiga kura ya kumkubali Yule ambaye Mungu amemchagua, Niliwahi kusema katika mahubiri yangu kuwa Yule ambaye anatoka kwa Mungu atakuwa ni Yule ambaye wanadamu hawakumtarajia wala kumfikiria.
Haya ndio niliyojifunza katika mchakato mzima wa kupatikana kwa wagombea Urais katika Taifa letu na huku tukiyaangalia mapenzi ya Mungu Mungu ibariki Afrika Mungu ibariki Tanzania

Mkuu wa wajenzi Mwenye Hekima
Rev. Innocent Kamote.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni