Alhamisi, 18 Februari 2016

Maombi Yenye Matokeo:-




Utangulizi

Biblia inatufundisha Kanuni kadhaa wa Kadhaa ambazo tukifanikiwa kuzifahamu na kuzitumia Maombi yetu yataambatana na mafanikio makubwa sana, Mungu wetu anataka wote tufanikiwe, na anataka wote tujibiwe maombi, katika kusisitiza swala la maombi Yesu alisema “Kila aombaye Hupokea…..” Mathayo 7;7 lakini katika halia halisi tunaweza kuona kuwa si kila aombaye hupokea yaani wengine hawapokei majibu ya maombi yao,sasa ili maombi yajibiwe ni muhimu kuzingatia kanuni zifuatazo:-
  
1.        MAOMBI LAZIMA YAAMBATANE NA IMANI.
Biblia inatufundisha kuwa ili maombi yajibiwe ni lazima Imani iwepo Yakobo 1:5b-7 Ila na aombe kwa imani pasipo shaka yoyote” Biblia inasisitiza kuwana Imani katika maombi watu wengine hawapokei majibu yao kwa sababu wanaona mashaka mashaka ni kinyume cha imani tunapoamini kuwa Mungu atatufanyia kile tuilichokiomba mara moja kinakuwa chetu katika ulimwengu wa roho. Marko 11:12-14, 20-24  “Yoyote myaombayo mkisali aminini ya kwamba mnayapokea nayo yatakuwa yenu” Mafundisho ya Yesu kuhusu maombi yanakazia pia kuambatanisha na Imani, Imani ndio msingi mkuu wa Ukristo na uhusiano wetu na Mungu, shetani anapokuja kutushambulia kwa mashambulizi ya aina yoyote ile anachokilenga ni kutuharibia Imani yetu Yeye anajua wazi kuwa msingi wa Msimamo katika imani yetu una uweza mkubwa sana kutupatia maswala ya kiungu, Yesu alitambua ya kuwa imani ndio msingi mkuu wa maisa ya kiriho na hivyo alimuombea Petro asipungukiwe na Imani “Luka 22:31-32” “…Lakini nimekuombea ili Imani yako isitindike” Petro baadaye alifahamu kuwa imani ni msingi wa mambo mengine ambayo Mkristo anapaswa kuwa nayo linapokuja swala la kukua Kiroho 2Petro 1:5-8 Katika imani yenu tieni na wema…” Kujibiwa kwa Maombi yetu hakutokani na wingi wa siku tunazofunga au urefu wa maombi tuombayo bali imani tuliyonayo, Mungu ili atupe ni lazima tuwe na Imani kuwa anaweza kufanya lile tumuombalo Mathayo 9:27-29 Kwa kadiri ya imani yenu mpate!Yesu alitumia Muda mwingi kuwafundisha wanafunzi wake kuamini Yohana 11:14-15 sikuwako huko ili mpate kuamini.. Yesu alijua wazi kuwa tukiamini Kazi azifanyazo tutazifanya naam na kubwa kuliko hizo Yohana 14:12-14. Maisha yetu ya Maombi na Ukristo yatakuwa na maana kubwa sana kama kama tutaambatanisha Imani.

2.        MAOMBI NI LAZIMA YAAMBATANE NA SHAUKU.
Mungu huangalia sana shauku yetu kabla ya kujibu maombi yetu, shauku inajenga uzito wa kila unachotaka kufanyiwa, Tunapoomba pia ni kama tunampelekea Bwana shauku tuliyonayo katika mioyo yetu Kibiblia tunaweza kuiita njaa na kiu ya Haki, au uhitaji lengo au tamaa isiyo mbaya Mathayo 5:6 “Heri wenye njaa na kiu ya haki maana hao watashibishwa” Shauku ndio huwa kama tairi linalobeba Imani na kumsukuma Mungu afanye Marko 10:46-52, Wataka nikufanyie nini? Maombi yetu ni lazima yaambatane na shauku yaani kile unachokitazamia, kile unachotaka Bwana akufanyie, Mwandishi wa zaburi aliweka wazi kuwa Yeye alitaka neno moja tu kukaa nyumbani mwa Bwana  Zaburi ya 27:4 wewe unataka nini?Kama hakuna unachohitaji maombi yanakuwa hayana uzito, yanaweza kubaki kama ibada ya kawaida, Nyakati za agano la kale mtu alipoingia kwa mfalme kama alikubwaliwa mfalme alimtaka kueleza shida yake Nehemia 2:2-5 Una haja gani unayotaka kuniomba? Ni lazima iwepo haja Esta 7:2-3, Bwana ambaye ni mfalme wa wafalme angependa kujua haja za moyo wako naye hujalia au hutupatia kwa kadiri ya haja ya moyo Zaburi 20:4 akujalie kwa kadiri ya haja ya moyo wako, maombi yeje haja yenye shauku yenye uhitaji humgusa na kumsukuma Mungu kufanya kitu
Haja zenu na zijulikane na Mungu Wafilipi 4:6, Na tumtwike yeye fadhaa zetu zote 1Petro 5:7 Mungu anataka haja zetu ziwe wazi mbele zake.

3.        MAOMBI LAZIMA YAAMBATANE NA BIDII / HISIA KALI.
Neno bidii linaloweza kutumika katika kingereza ni Fervent ambalo maana yake kwa mujibu wa Oxford Dictionary – having or showing very strong and sincere feelings about something, Yakobo 5:16-18, Aliomba kwa Bidii Earnestly (heartfelt, continued)  Haya ni maombi yenye kuonyesha bidii na yenye kuguswa na hisia kali strong feelings kuhusu kile unachokiombea aina hii ya maombi huonyesha matokeo haraka Waebrania 5:7, Yesu alikuwa akisikilizwa na Mungu kwa sababu aliunganisha maombi yake na hsia kali sana alilia alilowa machozi Yohana 11:33-35,43. Tunapoomba maombi yenye hisia kali, ya bidii Mungu huguswa nakuachilia kile tukiombacho Isaya 38: 1-6 Biblia Inaeleza wazi jinsi ambavyo Hezekia alisikilizwa na Mungu licha ya kuwa ni Mungu mwenyewe ndiye aliyemtangazia kifo kupitia nabii Isaya biblia inasema hivi Isaya 38:1-6 .  “1. Siku hizo Hezekia aliugua, akawa katika hatari ya kufa; na Isaya nabii, mwana wa Amozi, akaenda kwa mfalme, akamwambia, Bwana asema hivi, Tengeneza mambo ya nyumba yako; maana utakufa, wala hutapona. 2. Basi Hezekia akajigeuza, akaelekeza uso wake ukutani, akamwomba Bwana, 3. akasema, Ee Bwana, kumbuka haya, nakusihi, kwamba nimekwenda mbele zako katika kweli na kwa moyo mkamilifu, na kutenda yaliyo mema machoni pako. Hezekia akalia sana sana.    4. Ikawa, neno la Bwana likamjia Isaya, kusema,  
4.        Enenda ukamwambie Hezekia, Bwana, Mungu wa Daudi, baba yako, asema hivi, Mimi nimeyasikia maombi yako, nimeyaona machozi yako; tazama, nitaziongeza siku zako, kiasi cha miaka kumi na mitano. 6. Nami nitakuokoa wewe, na mji huu, na mkono wa mfalme wa Ashuru, nami nitaulinda mji huu.” Luka 19:41-44 Yesu alilia kwaajili ya Yerusalem Muda Usingeweza kutosha kuangalia mifano mingi ya kuomba kwa bidii, kwa hisia, kwa machozi, kwa kendelea bila kukoma ambako kunaleta matokeo makubwa. Luka 18:6-8

5.        MAOMBI YENYE MATOKEO LAZIMA YAWE ENDELEVU/BILA KUKOMA
Bilia inatufundisha juu ya maombi endelevu, maombi ya kudumu maombi yasiyokoma Luka 18:1-5 Yesu alifundisha kuwa muombaji hapaswa kuchoka wala kukata tamaa, fundisho hili liko wazi hata kwa mitume walifundisha kuomba bila kukoma 1 Wathesalonike 5:17, Ni marufuku kukata tamaa katika swala la kuendelea kumuomba Mungu, 1Wafalme 18:41-45, Eliya alipokuwa akiomba mvua ni muhimu kukumbuka kuwa haikuwa rahisi lakini aliomba na kuitarajia hata mara saba na kwa dalili ndogo tu aliamini kuwa Mungu amekwisha kujibu, Kumuomba Mungu mpaka upate matokeo wakati mwingine unapaswa kuwa kama kinganganizi, Aidha katika kuomba kwetu bila kukoma hatupaswi kuangalia hali yetu na historia yetu kwa Mungu mwanamke mfonike alipokuwa akimuomba Mungu hakujali Historia yake na wayahudi yeye alikazania akijua kuwa Mungu hana upendeleo na ni wa wote Marko 7: 24- 30 Mwanamke huyu alipokea Maombi yake kwa vile hakukatishwa tamaa kuwa yeye ni mataifa na Mungu alimsikiliza na kupokea haja yake.

6.        MAOMBI YENYE MATOKEO NI LAZIMA YAENDANE NA KUSAMEHE.
Mafundisho ya Biblia yanasisitiza sana maombi yanayoendana na kusamehe wengine, kutokusamehe ni kizuizi kikubwa sana cha maombi, Lakini Msamaha una nguvu kubwa sana Yesu alirudia mara kadhaa kuhusu kusamehe kabla ya Maombi, Mathayo 6:12,14-15  kwa hiyo msamaha ni wa Muhimu kila linapokuja swala la maombi Mark 11:25, Kutokusamehe kunafunga milango ya Baraka na kusikilizwa na Mungu, Hakikisha kuwa hakuna uchungu wa aina yoyote ili kusudi maombi yako yasizuiliwe Waefeso 4:31-32,  Aidha pia ukiwakosea wengine bila kushughulika kutafuta amani nawe kuna uwezekano wa kuzuia kwa kiwango kikubwa kwa maombi yako, Yesu alisisitiza kwamba ni muhimu kupatana na mshitaki wako upesi Mathayo 5: 25-26, Yesu anaelezea hali halisi katika ulimwengu wa Kiroho kuwa kuna uwezekano wa kufungiwa jambo na usilipate milele kama hujafanya mapatano na mshitaki wako, Katika ulimwengu wa kiroho mtu anapokuwa na kinyongo nawe anakufunga usipate Baraka zinazokusudiwa na Mungu kwako Mfano Mwanzo 20:1-18, Abimeleki alikusudiwa kuuawa na Mungu na pia nchi yake nayeye mwenyewe walifungwa katika utasa kwa sababu,alimkosea Abrahamu katika unyinge wake na kuogopa kudhuriwa naye kama Mfalme. Dua za Abimeleki zilisikilizwa alipoweka mambo yake sawa na Ibrahimu.

7.        MAOMBI YENYE MATOKEO NI LAZIMA YAENDANENA KUMSIFU MUNGU.
Maombi yenye matokeo kibiblia ni lazima yaanze na kumsifu Mungu ama yajumuishe kumtukuza Mungu, waombaji wengi sana wa nyakati za biblia walitambua umuhimu wa kumsifu Mungu, Mungu anaposifiwa hujifunua kwa wanadamu kwa kiwango kikubwa na cha kushangaza, Wakatoliki wana sala inayoitwa atukuzwe “Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu” maono yao makubwa ni kuhakikisha kuwa Mungu katika ukamilifu wake anapewa sifa na utukufu kwa mambo yote makubwa anayostahili na aliyotutendea katika maisha yetu Zaburi ni moja ya kitabu chenye Nguvu sana katika Maisha yetu lakini ndio kitabu kinachoongoza kwa kumsifia Mungu
·           Zaburi 9:1-2
·           Zaburi 19:14
·           Zaburi 71;8
·           Zaburi 8:9
·           Zaburi 96;4
·           Zaburi 118:28
Kwa nini kuna umuhimu wa kumsifu Mungu?
Kumsifu Mungu ni tofauti na kushukuru, hapa kwa dhati kabisa kutoka moyoni unakubali kutambua ukuu wake, uweza na utendaji wake wa ajabu, Kushukuru kunaletwa na matendo yake makuu neema na rehema na fadhili alizotutendea lakini kusifu kunaletwa na utambuzi rasmi moyoni kumtambua Mungu ni nani Zaburi 18:3 Mungu anastahili Kusifiwa na Biblia imetuamuru kufanya hivyo Isaya 43:21

8.        MAOMBI YENYE MATOKEO NI LAZIMA YAENDANENA UTII ULIOTIMIA.
Mafanikio makubwa ya kiroho na katika mazingira mengine yote ya kukubaliwa na kujibiwa maombiyetu na Mungu nilazima yaendane na utii, Yesu alijibiwa Maombi na kupendwa na Mungu kwa sababu alikuwa mtii kwa maagizo yote ya Mungu Luka 3 :21-22, Yesu alikuwa na uhakika kuwa Mungu anamsikia, utii unaongeza kusikiwa na Mungu Yohana 9:24-3, Mungu hawasikii wenye dhambi Maana yake Mungu hawasikii wasiotii hajibu maombi ye wenye kuvunja Sheria zake.
a.       Mungu  aliwaambie Israel kuangalia kuyatii maagizo yake yote Torati 11:22-25
b.      Kutokutii kunafananishwa na dhambi ya Uchawi 1 Samuel 15:23
c.       Hasira za Mungu huwajia wana wa uasi Efeso 5:6
d.      Mungu anatamani kama lau tungemsikiliza na kutii amri zake anaetubarikia sana Isaya 49:18-19, watu wengi sana wamezuilia kusikiwa na Mungu kwa kukosa utii, ni lazima tujifunze kuishi maisha ya utii na ndipo tutakapofanikiwa katika maisha ya maombi na kusababisha matokeo makubwa.

9.        MAOMBI YENYE MATOKEO NI LAZIMA YAENDANE NA MATUMIZI YA DAMU YA YESU
Moja ya njia Nzuri sana katika kuomba na ambayo inasababisha matokeo ni kutumia damu ya Yesu utaniuliza kwa nini na kwa vipi?
Damu ya Yesu inazungumza kwa niaba yetu, Ni damu ya Mwanakondoo wa Mungu asiye na Dhambi Waebrania 12:24 Inasema Na Yesu mjumbe wa agano jipya , na damu ya Kunyunyizwa, mInenayo mema kuliko ile ya Habili. Biblia inaonyesha kuwa damu inazungumza na inauwezo wa kulia Mwanzo 4:10, Damu ya ndugu yako inanililia kutoka katika ardhi ni kwa sababu ya kilio cha damu ya Habili Kaini alilaaniwa, Damu ndiyo iliyowafanya Israel kuwa salama kule Misri na kuokolewa Kutoka 12, Makuhani waliitumia Damu kila wakati kuwaombea watu Msamaha kwa Mungu Damu ya Yesu ilikuwa ni upatanisho wa Dhambi zetu kwa Mungu na inazungumza msamaha kwaajili yetu, tunaambiwa kuwa tutamshinda Shetani kwa Kwa Damu ya mwana kondoo na neno Ufunuo 12:11, Tunaambiwa kwa kupigwa kwake sisi tumepona Isaya 53:5, Tunahitaji kuitumia damu ya Yesu kwa Imanikatika maswala kadhaa wa kadhaa ya Maisha yetu ikiwa ni pamoja na Maombi.

10.   MAOMBI YENYE MATOKEO NI LAZIMA YATUMIE JINA LA YESU.
Yohana 14:13-14 Ni muhimu kuwa na ufahamu wa kutosha kuhusu kuomba kwa jina la Yesu maana yake ni nini, Kuomba kwa jina la yesu maana yake ni kutoa maombi kwa Mungu kupitia huduma aliyoifanya Yesu, ina maana kwamba mtu anayeomba kupitia au kwa jina la yesu lazima awe amaeokoka yaani Yesu ni Bwana na mwokozi wako Yohana 1;12 wote waliompokea aliwapa uwezo kufanyika wanawe, lazima uwe umehesabiwa haki Warumi 3:28,51, hii inamaana ya kuwa umekuwa kiumbe kipya 2Wakoritho 5:17, umezaliwa na Mungu Yohana 14:23, Aliyezaliwa mara ya pili au kuokolewa kupitiaKazi za Yesu ana haki ya kufanya maombi kupitia Kristo aliyeishi maisha makamilifu 1Petro 2:22 na kutuondolea Dhambi zetu,1Petro 2:24. Kuomba kwa jina lake pia inamaanisha kuomba kwa kutumia mamlaka yake kwa baba na nadio maana watu wengi hupenda kumalizia maombi kwa kusema Katika Jina la Yesu amen, wanachokusudia ni kuwa wanamuomba baba kupitia au kwa kutegemea kazi kamili ya ukombozi iliyofanywa na Yesu au Mungu alipokuwa katika mwili Yohana 1;1, 14,Wakolosai 2:9.
Kuomba kwa jina la Yesu ni kuomba kwa mamlaka yake Matendo 4:7, 10, kuomba kwa jina la yesu maana yake ni kutumia mamlaka yake na tunapoitumia mamlaka yake  maana yake tumekubaliana na kazi zake zote alizozifanya msalabani na kuwa tumesamehewa dhambi na hivyo tuna haki ya kusikiwa na Mungu na kujibiwa. 

11.   MAOMBI YENYE MATOKEO NI LAZIMA YASIMAME SAWA NA NENO LA MUNGU Maombi yenye matokeo ni muhimu yakiendana sawa na Neno, kwa ujumla katika neno la Mungu kuna rekodi ya maombi, kwa hiyo neno la Mungu ni rekodi ya maombi, tunaona watu wengi walimuomba Mungu na wakafanikiwa, Maombi ndio njia pekee ya uhakika wa maswala ya rohoni katika mwili, Hata nyumba ya Mungu huitwa nyumba ya sala, lakini hata hivyo ili maombi yetu yawe na Nguvu na yenye matokeo ni muhimu ni muhimu kuyahusisha maombi yetu na ujuzi kuhusu Neno la Mungu Yohana 15:7 “Ninyi mkikaa ndani yangu, na maneno yangu yakikaa ndani yenu ombeni mtakalolote nanyi mtatendewa” Mungu amezificha ahadi zake katika neno na maombi, ni kwa njia ya neno lake tunaweza kusababisha mambo makubwa, Neno lake linakuwa msingi mkuu wa maombi yetu, Kulitumia neno la Mungu ni kama kumtumia Mungu mwenyewe, Neno lake ni msaada mkubwa katika maombi, 1Timotheo 4:4-5 Kupitia neno la Mungu tunaweza kutakasa hata kitu kisifaa kuliwa na kikaliwa

12.   MAOMBI YENYE MATOKEO NI LAZIMA YAJAWE NA SHUKURANI.
Ni muhimu kufahamu kuwa Mungu wetu anapendezwa sana na shukurani, Mafundisho yote ya Biblia yanayokazia kuhusu maombi pia yanaonyesha kuwa tunapaswa kushukuru, 1Wathesalonike 4: 17-18, Wakristo ni lazima tujifunze kuwa watu wa shukurani, shukurani katika Maombi ina nguvu ya kipekee sana hata kusababisha miujiza mikubwa  Yohana 11:38-42, Yesu alimfufua Lazaro kwa Maombi ya kushukuru, kushukuru ni sehemu ya imani, Yesu aliwalisha watu mikate kwa Maombi ya shukurani Yohana 6:10-11, Mungu anamtaka kila mmoja wetu awe na Moyo wa shukurani, Yesu aliwaponya watu 10 lakini ni mmoja tu aliyerudi kutoa shukurani wengine wote waliishia Luka 17:11-19, Muda usingeliweza kutosha kuangalia kuhusu shukurani Lakini Biblia inaonyesha kuwa Mtume Paul alikuwa mtu wa shukurani, inasemekana kuwa Paulo ameonyesha shukurani mara 186 katika maandiko yake na waraka wa wakolosai umejaa shukurani Mfano (Wakolosai 1: 3, 12; 2:7; 3:15, 17; 4:2) tunahitaji kushukuru,kumshukuru Mungu ni kwa muhimu kuna nguvu ni kutambua, kuwa Mungu ni kila kitu, ni kumuheshimu, ni kuonyesha kuwa tunamtegemea na kutambua fadhili zake na kuto kushukuru ni kumvunjia Mungu heshima ni kiburi, ni kuonyesha kuwa tunaweza kwa nguvu zetu, Mashujaa wote wa Biblia walikuwa wamejawa na shukurani Zaburi 100:1-5


13.        MAOMBI YENYE MATOKEO LAZIMA YAWE KATIKA MAPENZI YA MUNGU.
Ili maombi yaweze kuwa yenye matokeo ni muhimu kuomba sawa na Mapenzi ya Mungu, Fundisho la kibiblia linamtaka kila mmoja kuomba, sawa na Mapenzi ya Mungu 1Yohana 5:14-15 Mungu humsikia kila mtu anayeomba katika mapenzi yake tunaweza kwenda mbele za Mungu kwa ujasiri na tukifahamu kuwa anatusikia kama tutaomba sawa na Mapenzi yake, Tunawezaje kujua kuwa tunaomba sawa na Mapenzi yake, ukweli ni kuwa pale tunapoomba katika mstari wake au sawa na Neno lake Mungu hutusikia, Kama neno la Mungu likikaa kwa wingi maana yake ni kuwa tuko katika mapenzi yake Yohana 15:7, watu wengi sana ahawapokei kutoka kwa Bwana kwa sababu wanaomba vibaya, kuomba vibaya ni kuomba kwa nia mbaya au kwa tamaa wrong motive Yakobo 4:2-3. Yesu aliomba sawa na Mapenzi ya Mungu Marko 14:36, Ikiwa hatujui kuomba sawa na Mapenzi ya Mungu Roho Mtakatifu atatusaidia kuomba sawa na Mapenzi yake ikiwa tutamshirikisha Warumi 8:26-27 kwa sababu sisi hatujui kuomba  kama itupasavyo kuomba.


14.        MAOMBI YENYE MATOKEO NI LAZIMA YAONYESHE UNYENYEKEVU (PRAY WITH HUMILITY)
Biblia iko wazi kuwa Mungu huwapinga wenye kiburi na kuwapa neema wanyenyekevu, ili maombi yetu yaweze kupata kibali na kujibiwa Vema na Mungu ni lazima yatanguliwe na unyenyekevu 1Petro 5: 5-7…..Mungu huwapinga wenye kiburi bali huwapa neema wanyenyekevu, nyenyekeeni chini ya mkono wa Mungu ulio hodari ili awakweze kwa wakati wake, huku mkimtika yeye Fadhaa zenu zote kwa maana yeye hujishughulisha sana kwa mambo yenu. Mapema sana katika Injili ya Luka Yesu alifundisha mfano wa watu waliopanda Hekaluni kuomba Luka 18:9-14, Mungu hapendezwi na watu wenye kujihesabia haki wanaojifikiri Moyoni kuwa wao ni bora, hawajawahi kumkosea Mungu, Ili maombi yetu yaweze kuwa na Nguvu ni muhimu kuwa na moyo wa unyenyekevu, Hanna aliomba kwa unyenyekevu na alijua Tabia ya Mungu kuwa ana uwezo wa kuinua wanyonge na kuwaponda wenye kiburi Mungu anazo njia zake 1 Samuel 2:1-10. Muda usingeliweza kutosha kuwapitia wote katika Biblia ambao walijibiwa Maombi baada ya kujidhili yaani kujinyenyekeza, Daniel alijua namna ya kumuendea Mungu kwa unyenyekevu Daniel 9:1-9, Tunamuomba Mungu kama watu tunaobembeleza na sio tunaotaka ni lazima kujifunza kumfanya Mungu ashawishike kujibu Maombi yetu kwa kunyenyekea. Tukubali kujishusha tuache kuijihesabia haki, twende mbele zake kama watu tusiostahili Mungu atatukubali kwa Rehema zake na sio kwa haki yetu, “God never work on our godliness” Mungu hafanyi kazi kwa sbabau ya utauwa wetu bali kwa neema yake Matendo 3:11-16. Mungu ana njia za kushughulika na wale wanaojivuna Daniel 4:36-37, 28-33

15.        ILI MAOMBI YAWEZE KUWA YENYE MATOKEO NI LAZIMA TUTUNZE VYNYWA VYETU
Ni muhimu kwa kila muombaji kuwa na ufahamu kuwa katika kitendo cha kuomba kinywa ndicho hutumika kunena na kuzungumza na Mungu na kukiri maandiko na kukiri imani yetu, kwa msingi huo basi ni muhimu sana kila Muombaji akaelewa umuhimu wa kutunza kinywa kuna uhusiano mkubwa kati ya kuomba na matumizi ya kinywa Biblia inasema Mungu husikiliza maombi ya watu wasiotumia ndimi zao kunena mabaya au kunena kwa hila 1Petro 3:10-12. Mwandishi wa zaburi alikuwa akiomba na moja ya maswala aliyoyajua kuwa yanaweza kuzuia Maombi yake ni kinywa aliomba Mungu aweke ulinzi kwa kinywa chake Zaburi 141:1-3, Mungu hufurahia midomo inayonena haki na kusema yaliyo sawa Mithali 16:13, kupitia maombi yetu  tunatamka mambo ambayo baadaye yataumbika kuwa jambo halisi, tumeumbwa kwa mfano wa Mungu na Mungu aliuumba ulimwengu kwa neno na kutukabidhi sisi wanadamu, ulimwengu huu hivyo tunapoomba tunamshirikisha Mungu kwa vinywa vyetu na kumruhusu kufanya kitu hapa duniani kwaajili yetu hivyo ndimi zetu ni za muhimu kwa maombi yetu kuleta Matokeo Maombi ni jambo zuri na mtu mzuri anapaswa kutoa maneno mazuri Mathayo 12;34-37. Yakobo 1:26 Mcha Mungu wa kweli lazima ajue kuuzuia ulimi wake, waombaji wote wanapaswa kulikumbuka hili, ili maombi yao yajibiwe na ndimi zao zijae mamlaka ya kiungu na kuweza kutamka neno na likatimia, Ukiyajua hayo heri wewe ukiyatenda

Rev. Innocent Kamote
Mtumwa asiye na faida.

Endapo umebarikiwa na somo hili Niandikie Maoni, 0718990796 au ikamote@yahoo.com


 







Maoni 7 :

  1. Barikiwa mtumishi wa Mungu kwa maarifa haya🙏

    JibuFuta
  2. Barikiwa mtumishi wa Mungu

    JibuFuta
  3. Ubarikiwe Sana baba Mch,KWA Somo lenye Upana.By Israel Andrew

    JibuFuta
  4. Ubarikiwe sana mtumishi, hakika nmejifunza na kuomba wap nlkuwa nakosea, mungu aendelee kutumia Zaidi 🙏🙏🙏🙏🙏

    JibuFuta
  5. Akika mimi nimejazwa sana na mambo yenye umetupea nimefatilia sana ninaona nikibadilika naombatu ubarikiwe sana

    JibuFuta
  6. Shukrani baba kwa mafundisho adhimu kabisa

    JibuFuta
  7. Barikiwa kwa ufahamu huu wa neno la mungu

    JibuFuta