Jumanne, 16 Februari 2016

PALE TUNAPOFANYA HARAKA KUHUKUMU !


Ni tukio ambalo bado mpaka leo nalikumbuka, ilikuwa ni mwaka 2009, kipindi hicho lile wimbi la walemavu wa ngozi (alibino) kuuawa na kukatwa viungo ndio lilikuwa limeshika kasi kwelikweli hapa nchini. Siku moja alikuja nyumbani kwangu akanikosa, bali alimkuta mke wangu Mama Ngina. Hakukaa muda mrefu akaondoka lakini alimjulisha mke wangu kuwa simu yake imeibwa na hana mawasiliano labda mpaka hapo atakaponunua simu nyingine.

Niliporudi mke wangu alinipa zile salama, lakini kuna jambo alidai anataka tujadili juu ya rafiki yangu, mimi nikashtuka, na kumuuliza, ni jambo gani hilo? Akaniambia kuwa kutokana na hili wimbi la watu wenye lemavu wa ngozi kuuawa na kukatwa viungo vya mwili, inawezekana huyo rafiki yangu akapatwa na tatizo halafu ikatuletea shida, tukawa suspect

                                                                            wrong suspected


Nilishtushwa sana na kauli ile ya mke wangu, nilikaa kimya kwa muda kidogo, nikitafakari kisha nikamuuliza, Sasa unataka nimkataze asije hapa nyumbani

Hapana, sio lengo langu kuvunja urafiki wenu, lakini jaribu kupunguza ukaribu wenu na hasa kutembeleana, ikiwezekana mwambie unasoma na utakuwa unaishi Hostel kwa muda ili asiwe anakuja hapa nyumbani, mwenzio mimi naogopa,
alijibu mke wangu kwa sauti ya upole. Sikukubaliana naye na tulibishana sana na hatukufikia muafaka wa jambo hilo. Haikupita wiki yule rafiki yangu alikuja na akashinda kwangu kutwa, ilikuwa ni siku ya jumamosi na tulizungumza mambo mengi sana kuhusiana na mradi ambao tulitaka kuuanzisha, lakini pia alinijulisha kuwa huenda wiki inayofuata angesafiri kwenda Morogoro mara moja kuna kitu anafuatilia kule kwa rafiki yake ambaye alisoma naye.

Siku iliyofuata asubuhi alikuja mdogo wake na yule rafiki yangu na kuniuliza kama kaka yake alikuwa pale kwangu, kwani tangu alipoondoka jana asubuhi kuja kwangu kama alivyoaga hakurejea hadi asubuhi, na simu yake haipatikani kabisa... mke wangu alinitupia jicho kali kama la kunisuta, nilibabaika kidogo. Nilimjulisha kwamba ni kweli alikuja kwangu na aliondoka mchana kurudi nyumbani kwao. Basi yule kijana akaondoka, lakini huku nyuma mke wangu alinibadilikia na kuanza kunishambulia kuwa mimi sio msikivu na sana nitapata matatizo asipopatikana huyo kijana wa watu, nilibaki kimya na sikujibu aliendelea kunishambulia huku akilia kwa uchungu kuwa nimejitafutia matatizo. Ilibidi niwe mkali kidogo na kumuonya juu ya fikra zake potofu. Ghafla nikawa nimekumbuka kuwa yule rafiki yangu aliniaga kuwa huenda angesafiri kwenda Morogoro kwa rafikiye aliyesoma naye, hivyo nikamtoa mke wangu wasiwasi kuwa huenda kaenda Morogoro na simu yake imeisha chaji na ndio maana haipatikani.

Ilipofika jioni, nilipata wageni tena, na hawakuwa wengine, bali wazazi wa yule rafiki yangu, wakiwa wameambatana na watu wengine wawili, ambao sikuwafahamu, waliingia ndani na walinijulisha kuwa mtoto wao hajulikani alipo na wanahisi kuwa huenda nahusika na kutoweka kwake. Mimi niliwajulisha kwamba, ni kweli jana alifika kwangu na alikaa mpaka mchana akaondoka, na nikawajulisha kwamba mtoto wao alinidokeza kuwa angesafiri kwenda Morogoro kwa rafikie waliyesoma naye kwani kuna jambo analifuatilia huko. Wazazi wa yule kijana walikanusha kujua lolote juu ya safari hiyo. Lakini wakati bado wakiendelea kuniuliza, mama wa yule kijana alidakia kuwa nipelekwe kituoni nikatoe maelezo, kwani inawezekana nafahamu kilichompata mtoto wao. Nilipinga kupelekwa kituoni, likazuka zogo mle ndani mpaka majirani zangu wakaja kusikiliza kulikoni!

Miongoni mwa majirani zangu alikuwepo dada mmoja wa Kichaga, ambaye hakuwa na maelewano mazuri na mke wangu, na aliposikia zile tuhuma, alianza kusema kishabiki kuwa tupelekwe kituoni kwani lazima tunajua aliko mtoto wao. Alianza kulizungumza jambo lile kwa dhihaka akisema,;watu wanajifanya wana hela na kujitia ufahari kumbe wanauza viungo vya albino! Alikuwa anaongea kwa sauti na kwa ushabiki akitumia lafudhi ya Kizaramo iliyochanganyika na ya Kichaga, alinikera sana.

Baada ya mvutano mkali mke wangu alinishauri nikubali kwenda kituoni kutoa maelezo, kwa kuwa sikuhusika na kupotea kwa kijana yule. Nilitoka nje uso wangu ukiwa umesawajika kwa fedheha ile. Siku hiyo ndio niliwafahamu majirani zangu kwa rangi zao halisi.

Nilifuatana na wazazi wa yule kijana pamoja na baadhi ya majirani zangu waliokuwa wameguswa na jambo lile, kwani pia wapo waliokuwa wakinipa moyo kuwa nisiwe na wasiwasi kwa kuwa sikuhusika, basi kila kitu kitafahamika kule kituoni. Mke wangu mama Ngina alikuwa amefuatana na mimi akiwa analia na alionekana wazi akiwa na wasiwasi sana.

Wakati tuko njiani kuelekea kituo cha Polisi simu ya yule baba wa kijana iliita, alipoitoa mfukoni , alisita kidogo kuipokea, mkewe akamuuliza kuwa ni nani anapiga simu, yule mzee hakuipokea simu ile alibaki kuikodolea macho akiwa ameishika mkononi. Mmoja wa wale watu aliofuatana nao ambaye nilikuja kuambiwa kuwa ni shemejiye, aliichukua ile simu na kuipokea, haloo, nani anaongea....aah mjomba, uko wapi?

Wakati anaongea na simu ile wote pale tukajua kuwa alikuwa ni yule kijana aliyekuwa akitafutwa, na watu wote tulikuwa kimya..yule mjomba hakumwambia kuwa anatafutwa, ila alimdanganya kuwa mama yake yu mgonjwa na anahitajika nyumbani haraka. Alikata simu na kusema, ;Ni Msakuzi, ni kweli yuko Morogoro na simu yake iliisha chaji akawa amekosa chaji tangu jana na leo kutwa. Wote tulishikwa na butwaa, na wazazi wa yule kijana waliniomba radhi kwa usumbufu wote uliotokea
Kumbe tunapofanya hukumu kwa haraka tunaweza kunyonga wasiostahili kunyongwa na kufunga wasiostahili kufunga hukumu ya haki ina Mungu tu.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni