Jumamosi, 19 Machi 2016

Mafundisho Kuhusu Ubatizo:-



Ni muhimu kufahamu kuwa Mafundisho kuhusu Ubatizo katika nyakati hizi tulizonazo yamechakachuliwa sana,  na hivyo kuliweka kanisa katika wakati mgumu wa kuamua watu wabatizwe vipi kutokana na kila mtu kubatiza katika namna anayoiona kuwa iko sahii na kujenga hoja za kibinadamu hata kuliko kuliangalia Neno la Mungu linasema nini kuhusu Ubatizo, Mungu na ampe neema kila mmoja wetu na moyo uliopondeka ili wote kwa pamoja tuache tofauti zetu na kuliangalia neno la Mungu linasema nini kuhusu Ubatizo, tuchukulie kana kwamba tumeokota Biblia na sisi wote hatujui Neno la Mungu na tunaisoma hiyo Biblia na tunagundua kuwa tunaweza kumuamini Mungu na tukabatizwa je unafikiri tungebatizwa vipi?  Hii ndio aina ya ubatizo ninayotaka kuizungumzia sawa na Neno la Mungu linavyojieleza na sio sawa na tamaduni za watu na historia za kipagani.

 watu wengi sana hubatizwa pale alipobatiziwa Yesu mto Jordan (Jordan river) huko Israel.

Kwa msingi huo leo tutachukua Muda pamoja na mkuu wa wajenzi mwenye hekima kuchambua kwa kina somo kuhusu ubatizo kwa upana na urefu, ili tuweze kufahamu kwa undani kuhusu ubatizo na kuondoa utata ulioko miongoni mwa jamii ya Kikristo.

Yesu aliamuru kwamba wote watakaomuamini na kubatizwa wataokoka, Biblia inasema katika Mathayo 28:18-20 “18. Yesu akaja kwao, akasema nao, akawaambia, Nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani. 19. Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu;    20. na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi; na tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku zote, hata ukamilifu wa dahari.” Unaweza pia kuona katika Marko 16:15-16 “Akawaambia, Enendeni ulimwenguni mwote mkaihubiri injili kwa kila kiumbe, aaminiye na kubatizwa ataokoka asiyeamini atahukumiwa

Ni muhimu kwetu basi tukachukua muda kuchambua agizo hili la Yesu la kubatiza na kuangalia kwa undani kile tuilichoagizwa ili kukifanyia kazi kama Mungu alivyoagiza. Tutajifunza somo hili Mafundisho kuhusu Ubatizo kwa kuzingatia Vipengele vitano vifuatavyo:-


  • ·         Maana ya Neno Ubatizo
  • ·         Maana na Historia ya Ubatizo
  • ·         Kanuni na jinsi ya kubatiza
  • ·         Sifa ya mtu anayestahili kubatizwa
  • ·         Namna ya kubatiza.


Maana ya Neno Ubatizo:-

Kwa kuwa tunazungumzia ubatizo ni vema kwanza tukaelewa asili ya neno Ubatizo neno Ubatizo tulilo nalo kwa Kiswahili katika kiingereza wanatumia neno “Baptize” au “Baptisms” ambalo kwa asili limetokana na Neno la kiyunani yaani KIGIRIKI  BaptizoBatizo,  ambalo maana yake ni Kuzamisha au kudumbukiza, “to dip or sink” or “immerse” pia ubatizo unaweza kufananishwa na kuchovya kama mtu anavyoweza kudumbukiza tonge la ugali katika mchuzi, nyakati za Biblia pia lilitumika kumaanisha kuchovya na kufyonza kabisa asili ya kitu kwa mfano nguo ya kitani ilipowekwa katika rangi ili kuibadili iwe na rangi ingine ilidumbukizwa katika rangi na nguo hiyo ilitoka ikiwa imebadilika kutoka weupe wake wa asili kuingia katika rangi iliyodumbukizwa kwayo tendo hilo pia liliitwa Ubatizo unaweza kuona, hii ndio maana halisi ya ubatizo hata kwa mujibu wa “Strong concordance” na “NAS Exhaustive Concordance”  na vyanzo vingine vya Lugha za kiyunani.

Maana na Historia ya Ubatizo:

Kama tulivyoweza kuona maana ya Ubatizo hapo juu ni wazi kuwa hii ndio maana halisi ya ubatizo na maana hii imathibitishwa na hata kukubaliwa kuwa ndio maana halisi ya ubatizo kwa mujibu wa wataalamu na wasomi wa Lugha ya kigiriki yaani kiyunani, na wanahistoria waliobobea katika maswala ya kanisa, ingawa ni muhimu pia kufahamu kuwa wayahudi walioishi nyakati za Kanisa la kwanza walibatiza pia kwenye maji mengi au kwa kuzamisha kwa kusudi la kuwabadilisha wale waliokuwa mataifa wa kawaida walioamini katika dini ya kiyahudi ambao waliitwa “Proselyte’s” ubatizo wao ulikuwa na maana ya kuwa wameacha miungu yao na kumuamini Mungu wa wayahudi, kitamaduni inaelezwa kuwa mwongofu alisimama katika maji na kisha kuzamisha kichwa chake katika maji huku sheria au Torati ya Musa ikisomwa, na tendo hilo pia lilimuhesabu kuwa ametakaswa na  na ameanza kuishi maisha mapya  kama mtu wa watu wa agano la Mungu.

Katika tamaduni za kiyunani pia kulikuwako na biashara zilizoshamiri za uuzaji wa nguo za rangi ya zambarau soma Matendo 16:11-14 nguo hizi zilikuwa mfano wa batiki zilizamishwa katika sufuria za maji yenye rangi na hivyo nguo hizo zlifyonza maji na rangi kabisa na kusababisha rangi kupenya katika nguo na nguo ilitoka ikiwa na rangi iliyokusudiwa kitendo hiki pia kiliitwa UBATIZO.

Ni wazi kutokana na maana na historia na tamaduni, swala la kunyunyizia maji au kumwagia maji binadamu kwa madai kuwa unabatiza haliko katika historia nzima ya kubatiza, lakini liko katika tamaduni za kitorati za kutakasa kitu au vitu, pia kibiblia swala hilo halimaanishi ubatizo, Kibiblia kuhani alitakasa vitu au vyombo vilivyotumika kwa kazi maalumu hekaluni, lakini linapokuja swala zima la Ubatizo kubatiza kwa kunyunyizia hakuna mashiko ya kihistoria wala ya kimaandiko, kuna uwezekano tu kuwa aina hii ya ubatizo ilifanywa kwa wagonjwa mahututi ama ambao walikuwa hawawezi kuelekea eneo la Ubatizo na pia ama kwa kuheshimu watu wenye nyadhifa kubwa kama wafalme, au pia kwa sa babu ya kubatiza wakristo waliokimbilia mafichoni wakati wa mateso, hata hivyo kwa sababu zozote zile kama zilizoainishwa hapo juu, haziwezi kuhalalisha ubatizo huo kuwa wa kibiblia ama wa kihistoria, na kwa vyovyote vile ubatizo huo sio agizo la kibiblia na uko uwezekano kuwa uliingizwa kwa mitazamo ya kipagani au kwa kuweko na mwingiliano wa kipagani.
Iko wazi kuwa ubatizo wa kimaandiko kabisa ambao hata wapagani yaani watu wasio na dini wakiokota biblia leo wakajifunza neno na kubatizana basi ni wazi ubatizo halisi utahitaji maji mengi na ya kuzamisha, ambayo ndio maana halisi ya kibiblia kwa mujibu wa Maandiko Warumi 6:1-4.
Ubatizo unafanana na tendo la kuzika mwanadamu Warumi 6:1-4
Ubatizo ni picha ya wokovu
Ubatizo ni kivuli cha kufanana na Bwana Yesu kiroho
Ubatizo ni alama ya kuoshwa ni alama ya kile ambacho kimekwisha kufanyika ndani ya moyo Matendo 22:16
Ubatizo ni ushuhuda Wagalatia 3:27
Umuhimu wa ubatizo, kanisa halipaswi kupuuzia swala zima kuhusu ubatizo, hata ingawa ubatizo wenyewe hauokoi, wala hauna nguvu ya kuokoa, watu hawabatizwi ili waokoke, lakini wanabatizwa kwa sababu wameokoka, kwa hiyo ubatizo sio tiketi ya wokovu lakini ni tendo muhimu katika kumkiri Yesu hadharani na ni muhimu katika kuonyesha utii, kama vile Rais anapoteuliwa anathibitika kuwa Rais kamili pale anapoapishwa, tunapokuwa tumemuamini Yesu kuwa ni bwana na mwokozi wetu, kokote pale tunamkiri Yesu kuwa ni bwana na Mwokozi hadharani kwa kukubali kubatizwa.

Kanuni na Jinsi ya kubatiza

Ni muhimu kufahamu kuwa kanini kuu ya kubatiza ni kile kilichoagizwa na Bwana Yesu tu Mathayo 28:19 Kubatiza kwa jina lka Baba na la mwana na la Roho Mtakatifu. Haya ndio Maneno yanayopaswa kutamkiwa mtu anayebatizwa sawa na Yesu alivyoagiza, mtu anapomwamini Yesu anakiri hadaharani kwa njia ya ubatizo na mbatizaji atatamka maneno haya Kwa kuwa Fulani…….bin Fulani…..umemwamini Bwana Yesu Kristo kuwa alikufa msalabani kwaajili ya ondoleo la dhambi na kuwa amekuwa bwana na mwokozi wa maisha yako kwa mamlaka niliyopewa na Mungu mimi nakubatiza kwa jina la baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu amen!, Maneno wakabatizwa kwa jina lake Yesu Kristo yaliyotumiwa na petro katika Matendo 2:28, hayawakilishi kanuni ya kubatizia, bali yanazungumzia Mamlaka ya ubatizo mara baada ya mtu kumuamini Yesu Kristo, kwa Mfano “Didache” yaani maandiko ya nyakati za zamani wakati wa mitume yaliyoandikwa mika 100 baada ya Kristo (100 AD) yanataja Ubatizo ulioagizwa na Yesu kama Ubatizo wake Yesu Kristo lakini katika ufafanuzi wake jinsi walivyobatiza walitumia kanuni ya kubatiza kwa Jina la Baba na la Mwana na la Roho Mtakataifu, Hivyo kanuni iliyotumika kubatiza ilizingatia utatu wa Mungu. Paulo anapozungumzia ubatizo wa wana wa Israel katika bahari ya shamu anataja Ubatizo wake Musa hii haimaanishi Paulo alikuwa anataja juu ya Kanuni bali mamlaka ya Musa kwa vile kila mmoja baada ya kuvuka bahari ya shamu alikubali wazi kuwa Musa ni mjumbe wa Mungu wa Mbinguni kwaajili yao, “1Koritho 10:2” ni katika mtazamo huohuo unapozungumzia ubatizo wa Yesu Kristo unazungumzia sio kubatizwa kwa jina lake Yesu tu, bali kubatizwa kwa Mamlaka au agizo lake Yesu Kristo baada ya kumkubali na kumuamini kama kiongozi wetu mkuu wa wokovu wetu, kubatizwa kwa jina lake Yetu kungemaanisha vilevile kama alivyoagiza, kubatizwa kwa Jina la Baba , Mwana na Roho Mtakatifu, hivyo si sahii katika kanuni ya ubatizo kutaja jina la Yehova tu au jina la Yesu tu, kanuni ya ubatizo inabaki kubatizwa kwa jina la Baba, mwana na Roho, Mtakatifu.
Uatatu wa Mungu ulikuwa ni jambo muhimu sana kutajwa katika nyakati za mitume kwaajili ya kuwakilisha upatikanaji wa neema na ushirika na upendo 2Wakoritho 13:14. Aidha tendo la ubatizo nyakati za Biblia na kama ilivyo maana halisi kibiblia ilikuwa ni lazima lihusishe maji mengi  Yohana 3:22-23”
Ubatizo kwa kuwa ulifanyika katika maji mengi ulihusisha kupandana kushuka kutoka majini, wakati wote Biblia ilipotaja swala la ubatizo au mtu kubatizwa lugha za kushuka na kupanda kutoka kwenye maji zilitawala kama unavyoweza kuona katika mazingira yafuatayo:-

-          Marko 1:9-11
-          Mathayo 3:16
-          Matendo 8: 36-39
-          Matendo 16:13-15
-          Matendo 16:30-34

Sifa ya mtu anayestahili kubatizwa:

Watu wenye sifa ya kubatizwa ni wale ambao kwa moyo wa dhati wametubu dhambi zao kwa kumaanisha kuziacha na wanaishi maisha ya utakatifu sawa na injili ya Bwana Yesu Kristo, ni watu waliomwamini Yesu na wameisikia injili na kuiamini, hao wana sifa ya kubatizwa, Nyakati za kanisa la Kwanza swala la ubatizo liliambatana na maswala makuu matatu yafuatayo;-
1.       Kumwamini Yesu kwa moyo wako wote kuwa ndiye Mwana wa Mungu Matendo 8:36-39
2.       Kuliitia jina la Bwana yaani kuomba Matendo 22:16
3.       Kujiweka wakfu kutoka matendo maovu na kuishi kwaajli ya Mungu 1Petro 3:20-21
Kwa msingi huo mtu mwenye sifa ya kubatizwa anapaswa kuwa na sifa za kuweza kuisikia injili, kusikiliza mahubiri, na kisha kuyaamini na ndipo inapowezekana mtu huyo kubatizwa Marko 16:15-16Akawaambia Enendeni ulimwenguni mwote mkaihubiri injili kwa kila kiumbe, aaminiye na kubatizwa ataokoka asiyeamini atahukumiwa” Mtu aliye na sifa za kubatizwa ni lazima awe na uwezo wa kusikia injili na kuipambanua na kuikubali yaani kuiamini na kutubu dhambi zake yeye mwenyewe, ni lazima ahubiriwe, ni lazima aamini ni lazima akiri ni lazima aliitie jina la Bwana, ni lazima asikie kutoka kwa muhubiri Warumi 10:10-17 “10. Kwa maana kwa moyo mtu huamini hata kupata haki, na kwa kinywa hukiri hata kupata wokovu. 11. Kwa maana andiko lanena, Kila amwaminiye hatatahayarika. 12. Kwa maana hakuna tofauti ya Myahudi na Myunani; maana yeye yule ni Bwana wa wote, mwenye utajiri kwa wote wamwitao; 13. kwa kuwa, Kila atakayeliitia Jina la Bwana ataokoka. 14. Basi wamwiteje yeye wasiyemwamini? Tena wamwaminije yeye wasiyemsikia? Tena wamsikieje pasipo mhubiri? 15. Tena wahubirije, wasipopelekwa? Kama ilivyoandikwa, Ni mizuri kama nini miguu yao wahubirio habari ya mema! 16. Lakini si wote walioitii ile habari njema. Kwa maana Isaya asema, Bwana, ni nani aliyeziamini habari zetu? 17. Basi imani, chanzo chake ni kusikia; na kusikia huja kwa neno la Kristo.Utaweza kuona sifa za namna hiyo zikijirudia kwa mkazo katika maandiko unaweza kusoma Matendo 8:36-39, Matendo.2:38-41, Matendo 16:14-15, Matendo 16:29-34. Kwa Msingi huo basi watu wenye sifa ya kubatizwa ni wale wenye uwezo wa kupambanua injili moyoni wenye uwezo wa kujua mema na mabaya. Kwa kuwa watoto wadogo hawana dhambi na hawana ujuzi au wezo wa kupambanua jema au baya na hawana uwezo wa kuamua kuamini au kutokuamini ni wazi tu kuwa ubatizo wa maji mengi hauwahusu  kwa ufupi watoto hawabatizwi, hii haimaanishi kuwa tunawazuia kuja kwa Kristo au kuingia katika ufalme wa Mungu hapana Yesu alisema watoto kama hawa ufalme wa Mungu ni wao, kwa msingi huo wanayo tiketi ya kuingia katika ufalme wa Mungu Mathayo 19:13-14 watoto wadogo huwekwa wakfu kwa Mungu katika ibada lakini hawabatizwi wao hubarikiwa tu.Luka 18:15-16.

Namna ya kubatiza.

Yeye anayebatiza na wanaobatizwa watafika nga’mbo ya maji yenye uhai yaani yaliyo safi na yanayotembea na kama ni kisima kiwe kina uwezo wa kuruhusu maji kuingia mapya na yaliyotumika kutoka, wataimba kama sehemu ya ibada na baada ya nyimbo maandiko kadhaa au mojawapo yanayohusiana na ubatizo yatasomwa na kisha Maji yatabarikiwa na eneo la kubatizia litawekwa wakfu, mbatizazi ataingia katika maji mengi na kuhakikisha kuwa anasimama vema mahali ambapo ataweza kuwazamisha wanaobatizwa, wabatizwaji wanaweza kuwa na mavazi maalumu ya kubatiziwa au kuwa na nguo za kubadilisha mara baada ya kubatizwa, aidha ni vema wakaweko wahudumu wenye nguo maalumu ambao watawahifadhi wanaobatizwa mara baada ya kupanda kutoka majini kuwazinga kwa nguo hizo na kuwasindikiza mahali pa kubadilisha nguo kavu, mbatizaji atakapokwisha kuyatakasa maji kwa kuyaweka wakfu, wanaobatizwa watajipanga mstari na kuanza kubatizwa kwa zamu ni vema wahudumu wakawa karibu kabisa na anayebatiza kwaajili ya kutoa msaada wa huduma zinazojitokeza wakati wa ubatizaji kama woga wa maji, kujazwa Roho Mtakatifu wakati wa kubatizwa na kuondoka kwa Pepo wabaya wakati wa kubatizwa haya ni matendo ya kawaida ambayo hujitokeza wakati watu wanabatizwa.
Wanaobatizwa waelekezwe namna ya kujihami wasinywe maji au maji kuwaingia puani, waelekezwe namna ya kuwa wepesi na kutokusababisha kuangukia majini tendo la ubatizaji lifanyike kwa utaratibu bila papara.

Mbatizaji atauliza majina kamili ya anayebatizwa nakama kuna jina jipya analotaka kulituimia kubatizwa kama alitokea katika uislamu na imani nyinginezo
Mbatizaji atamuuliza anayebatizwa kama amemkubali Yesu kuwa Bwana na mwokozi na kama anaamini kazi aliyoifanya Yesu Msalamabani ikiwa ndivyo mbatizaji atatamka yafuatayo
Kwa kuwa …………………..Umemkubali Yesu Kristo kuwa Bwana na mwokozi wa maisha yako na kuiamini kazi aliyoifanya Msalabani kwaajili yetu

Mimi kwa mamlaka niliyopewa nakubatiza kwa jina la Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu na kisha atamzamisha kwenye maji, mfano wa mtu anayezikwa ardhini na kisha atamtoa katika maji, wakati huu kila sehemu ya mwili wa anayebatizwa itapaswa kuzama kabisa katika maji mfano wa marehemu anavyolazwa, baada ya kitendo hicho utamuinua kwa haraka na kusimama katika hali ya kawaida na kisha utamuombea neema kwa maisha yake na kumbariki katika sehemu ya maisha yake ya wokovu  na kumuacha aende zake.

Maoni 2 :

  1. Shalom, ningependa kuuliza, kwangu nini ni lazima ubatizo ufanyike kwenye maji yanayotembea? Nini umuhimu wa maji yanayotembea? Na kama mtu amebatizwa kwenye kisima pasipo maji kutembea, je, ubatizo huo si sahihi? Na kama si sahihi, je anahesabiwa kama hajabatizwa? Natamani nielewe zaidi kuhusu ulazima au maana ya maji yanayotembea, msaada tafadhali, shukrani in advance.

    JibuFuta
  2. Naombeni kujua kwa ndani kuhusu ubatizo maana trh 27 na mimi naenda kubatizwa

    JibuFuta