Jumanne, 17 Mei 2016

Ujumbe: Hutamtoa Mtakatifu wako aone Uharibifu!



Zaburi 16:10 “Maana hutakuachia kuzimu nafsi yangu, wala hutamtoa Mtakatifu wako aone Uharibifu”

Zaburi ya 16 ni moja ya Zaburi ambazo mtunzi wake Ni Daudi, Katika zaburi hii kuna Ufunuo mkubwa sana ambao ni Matokeo ya kumuamini Mungu tuwapo Duniani, Mwandishi anaonekana Kumtegemea Mungu katika maisha yake, Kama mnitakavyoelezea Baadaye kwa kina.

Kabla sijazama ndani sana katika kuchambua aya hii, ni Muhimu kufahamu kuwa Mtume Petro aliutumia Mstari huu kuzungumzia habari za Kufufuka kwa Masihi Matendo 2:25-31 “25. Maana Daudi ataja habari zake, Nalimwona Bwana mbele yangu siku zote, Kwa kuwa yuko upande wa mkono wangu wa kuume, nisitikisike. 26. Kwa hiyo moyo wangu ukapendezewa, ulimi wangu ukafurahi; Tena mwili wangu nao utakaa katika matumaini. 27. Kwa maana hutaiacha roho yangu katika kuzimu; Wala hutamtoa Mtakatifu wako aone uharibifu. 28. Umenijuvisha njia za uzima; Utanijaza furaha kwa uso wako. 29. Waume, ndugu zangu, mniwie radhi, niseme kwa ujasiri mbele yenu habari za baba yetu mkuu, Daudi, ya kuwa alifariki akazikwa, na kaburi lake liko kwetu hata leo. 30. Basi kwa kuwa ni nabii, akijua ya kuwa Mungu amemwapia kwa kiapo, ya kwamba katika uzao wa viuno vyake atamketisha mmoja katika kiti chake cha enzi; 31. yeye mwenyewe akitangulia kuyaona haya, alitaja habari za kufufuka kwake Kristo, ya kwamba roho yake haikuachwa kuzimu, wala mwili wake haukuona uharibifu.” Paulo Mtume pia aliutumia mstari huu kumuhusu Masihi yaani Bwana wetu Yesu na Kufufuka Kwake Matendo 13:34-3734. Tena ya kuwa alimfufua katika wafu, asipate kurudia uharibifu, amenena hivi, Nitawapa ninyi mambo matakatifu ya Daudi yaliyo amini. 35. Kwa hiyo anena na pengine, Hutamwachia Mtakatifu wako kuona uharibifu, 36. Kwa maana Daudi, akiisha kulitumikia shauri la Mungu katika kizazi chake, alilala, akawekwa pamoja na baba zake, akaona uharibifu. 37. Bali huyu aliyefufuliwa na Mungu hakuona uharibifu.
Ni wazi kabisa Zaburi hii ilikuwa inahusu kufufuka kwa Yesu Kristo kwa sababu kuna maneno makuu mawili yanayotumika katika Mstari huu wa Msingi “Maana hutakuachia KUZIMU nafsi yangu, wala hutamtoa Mtakatifu wako aone UHARIBIFU” 

Neno Kuzimu katika Lugha ya kiibrania ni Sheol na kiyunani ni Hades ambayo yalimaanisha Kaburini au sehemu Fulani katika ulimwengu wa waliokufa, Na neno Uharibifu lilimaanisha KUOZA. 


Pichani ni Mwili wa Mtakatifu John Neumann, aliyefariki Dunia Mwaka 1860 huko Philadelphia akiwa na umri wa mika 48. Mwili wake baadaye uligunduliwa kuwa haukuharibika, Alikuwa ni Askofu wa Kwanza wa Marekani kutangazwa kuwa Mtakatifu, mwili wake umehifadhiwa katika jeneza la kioo katika madhabahu isiyofunikwa Katika kanisa la Mtakatifu Petro Mtume huko 5th and Girard Streets in the Northern Liberties section of Philadelphia.

Yesu Kristo Bwana wetu aliishi maisha Matakatifu bila ya dhambi, aliposulubiwa aliwekwa Kaburini na kabla hajaoza Mungu alimfufua kutoka kwa wafu, kwa hoiyo lugha hutakuachia kuzimu nafsi yangu ina maana hutaiacha nafsi yangu Kaburini, na neno wala Mtakatifu wako kuona uharibifu maana yake wala mtakatifu wako Kuoza

Yesu alifufuka kutoka kwa wafu Yu hai, Paulo mtume na Petro walitafasiri vema kabisa kwa sababu jambo hili lilizungumzwa na Daudinkama Nabii, lakini Daudi alipokufa alizikwa na hakutoka Kaburini na mwili wake ulioza kama ilivyokuwa kwa manabii wengine kwa hiyo ilikuwa ni sahii kabisa kwa Petro na Paulo kuona unabii huu unamhusu Yesu Kristo

Hata hivyo Pamoja na hayo Leo nataka twende mbele zaidi, kwa kulitumia andiko hili kwetu sisi Daudi hata kama alikuwa ni nabii na alizungumza kinabii Kuhusu Yesu Kristo  lakini zaburi nzima inatufunulia Imani na ujasiri aliokuwa nao Daudi na ambao unaweza kumuhusu kila mmoja wetu.

Zaburi 16: 1-2 “1. Mungu, unihifadhi mimi, Kwa maana nakukimbilia Wewe. 2. Nimemwambia Bwana, Ndiwe Bwana wangu; Sina wema ila utokao kwako.”
Yalikuwa ni maombi ya Daudi yakiomba Hifadhi kwa Mungu kwa sababu amemkimbilia Yeye, Daudi alimfanya Mungu kuwa ndiye Bwana hata pamoja na kujitambua kuwa hakuwa na wema wa kutosha lakini alijikinga kwa Mwenyezi Mungu na kumtegemea yeye, inawezekana ulikuwa wakati mgumu na wakati wa mapito mbalimbali lakini aliendelea kutambua kuwa Mungu ndie kimbilio lake na msaada uonekanao tele wakati wa Mateso Zaburi 46:1.

Zaburi 16:3-4 Daudi alionyesha kuwapenda watu wanaishi maisha ya utakatifu na kumtumikia Mungu, huku akitabiri kuongezeka kwa huzuni za watu wasiomuabudu Mungu wa kweli na kuabudu miungi mingine , Daudi alichukizwa zaidi na watu waliokuwa wakiabudu miungu na kutoa sadaka za damu kwa miungu hiyo alikiri kutokuwataja hata majina yako vinywani mwake Isaya 57:5, watu walitoa watoto wao sadaka kwa miungu Daudi alichukizwa nao sana hakufurahishwa na Ushirikina hata kidogo

Zaburi 16:5-9 Daudi anaonyesha kuwa yeye Kwake Bwana ndiye fungu lake yaani amemchagua Bwana, kama ni uamuzi wa kuchagua Basi yeye angelimchagua Bwana Mungu ameshika kura ya Daudi, anaamini kumchagua Bwana ni kuangukia mahali pema, ni urithi Mzuri, kuliko kawaida na kuwa atamhimidi Bwana, aliyempa shauri na kumfundisha amemweka Bwana mbele Daima na hataondoshwa moyo wake unamfurahia bwana na  kumtumaini.

Matokeo ya Imani ya Daudi.

  • · Daudi aliamini katika kumtegemea Mungu
  • · Aliamini na kuwapenda watu wanaomtumikia Mungu badala ya kuchukizwa nao
  • · Alimchagua Bwana na kumfanya kuwa fungu lake na alikataa kushiriki ibada zisizofaa wala kutoa sadaka za kuua watoto na kutoa Damu yake alipingana na ushirikina
  • · Aliamini kuwa akifanya hayo atapata furaha kuu hata kama atakuwa katika hali ya kifo, Mungu hatakubali au kumuacha afe na akifa Mungu hatakubali kumuacha aone uharibifu yaani aoze!


Hutamtoa Mtakatifu wako aone Uharibifu! Zaburi ya 16:10-11
Hatujui kuwa daudi alikuwa na ufahamu gani kuhusu maisha baada ya kufa, lakini ni lazima tuamini na kukaa katika kumuamini Mungu kama Daudi, Daudi kwa kusema Maneno hayo alimaanisha Lazima Mungu atamfufua tu, Biblia iko wazi kuwa iko siku miili ya watakatifu itafufuka Isaya 26:19 “Wafu wakowataishi” Daniel 12:2-3 “wengi wa hao waliolala katika Mavumbi wataamka” Yesu alieleza wazi kuwa kuna maisha baada ya kufa Marko 12:26-27 Biblia inasema hivi “26. Na kwa habari ya wafu ya kwamba wafufuliwa, hamjasoma katika kitabu cha Musa, Sura ya Kijiti, jinsi Mungu alivyomwambia, akisema, Mimi ni Mungu wa Ibrahimu, na Mungu wa Isaka, na Mungu wa Yakobo?  27. Yeye si Mungu wa wafu, bali wa walio hai. Hivyo mwapotea sana.  Ni wazi kuwa Yesu alifufuka yeye alikuwa ni Malimbuko tu ni alama ya kuwa kila amuaminiye yeye atamfufua Yohana 11:23-25, Biblia inasema hivi “23. Yesu akamwambia, Ndugu yako atafufuka. 24. Martha akamwambia, Najua ya kuwa atafufuka katika ufufuo siku ya mwisho. 25. Yesu akamwambia, Mimi ndimi huo ufufuo, na uzima. Yeye aniaminiye mimi, ajapokufa, atakuwa anaishi Unaona Daudi hakuwa anazungumzia Ufufuo wa Yesu Kristo Pekee Yesu Kristo ni Ufufuo na Uzima maana yake ndiye anayefufua na ndiye atakayefufu, Daudi alikuwa akizungumzia imani yake kuwa atafufuliwa hata kama ameoza lakini iko siku Mungu atamuinua tena, Daudi pia alikuwa anazungumzia ufufuo wa kila mmoja wetu kuwa sisi sote tutafufuka Yesu atakapokuja tena na kama atakukuta unaishi huku unamuamini basi hutakufa kabisa.

Hutamtoa Mtakatifu wako aone uharibifu ni muhimu kufahamu pia kuwa uharibifu sio kifo pekee Bilia inaeleza kuwa mwivi haji ila aibe kuchinja na kuharibu, Yohana 10:10  hivyo muharibifu ni Shetani,  Kama tutamutmaini Mungu na kuachana na ushirikina, na kumfanya yeye kuwa fungu letu ni wazi kuwa Mungu atatulinda hatutaona uharibifu wa aina yoyote katika maisha yetu, Mashambani, Biashara, Ndoa, Uchumba,  kazini, afya magonjwa mabaya, mimba kuharibika,  mashambulizi ya kishetani, Umasikini na udhaifu katika taifa letu, tukimtumaini Mungu atatupa neema na uzee mwema na tutaondoka Duniani kwa wakati tukiwa tumeshiba miaka, na Mungu akitukuzwa sana na maisha yetu. Mungu akupe neema usione uharibifu katika jina la yesu Kristo amen

Na Mkuu wa Wajenzi mwenye Hekima
Rev. Innocent Kamote.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni