Jumapili, 26 Juni 2016

Bwana Ndiye Mchungaji wangu!


Zaburi 23:1-6 Biblia inasema
 1. Bwana ndiye mchungaji wangu, Sitapungukiwa na kitu. 2. Katika malisho ya majani mabichi hunilaza, Kando ya maji ya utulivu huniongoza. 3. Hunihuisha nafsi yangu; na kuniongoza Katika njia za haki kwa ajili ya jina lake. 4. Naam, nijapopita kati ya bonde la uvuli wa mauti, Sitaogopa mabaya; Kwa maana Wewe upo pamoja nami, Gongo lako na fimbo yako vyanifariji. 5.Waandaa meza mbele yangu, Machoni pa watesi wangu. Umenipaka mafuta kichwani pangu, Na kikombe changu kinafurika. 6. Hakika wema na fadhili zitanifuata Siku zote za maisha yangu; Nami nitakaa nyumbani mwa Bwana milele.”

 Bonde la Wadi Quelt linalotajwa na daudi kama Bonde la Uvuli wa Mauti katika Zaburi 23.

Zaburi hii ni moja ya zaburi muhimu sana na Yenye maneno ya maana sana yenye usalama, Ingawa maandiko yake ni machache lakini yamebeba maana pan asana na nzito mno isiyoweza kupimika kuhusu Upendo wa Mungu kwa watu/mtu wake, Ni zaburi ambayo inaweza kutufunulia kwa kina upana na urefu wa Hali halisi ya uhusiano wa Mfalme Daudi na Mungu. Tutajifunza Zaburi hii kwa kutafakari vipengele vitatu vifuatavyo:-

·         Historia ya Zaburi hii
·         Bwana ni Mchungaji wa Ajabu
·         Sitaogopa Mabaya

Historia ya Zaburi hii:-

Zaburi ziko za Aina mbalimbali, lakini zaburi hii inaangukia katika Kundi la Zaburi za kujitia moyo, Katika moja ya chanzo yaani Commentary ambayo niliiisoma, inatuhakikishia wazi kuwa zaburi hii ni ya Daudi aliyekuwa mfalme wa Israel, Lakini sababu ambazo zilipelekea Daudi kuandika zaburi hiii ambayo inaonekana aliiandika kabla ya kuwa mfalme inazungumzia mazingira ya Bonde liitwalo kwa Kiarabu Wadi Quelt unaweza kugoogle jina hilo katika wikipidia, Bonde hili liko katika ukanda wa Magharibi yaani West Bank wa Mto Jordani Karibu na Yerusalem njia ya kuelekea Yeriko karibu na bahari ya Chumvi, Eneo hilo lilikuwa ni eneo hatari sana na lenye majabali ambapo kama mtu angeangukia huko kifo tu ndio kingekuwa zawadi yake, ni Bonde la Kutisha sana na njia yake pia ilikuwa na vibaka na majambazi na huenda ilikuwa ni simulizi na maonyo kutokupita eneo hilo hatari lililoogopewa sana, Bonde hilo lenye kutisha lilikuwa ni halisi na ni halisi hata sasa kwa vile liko hata leo, Kwa vile lilikuwa ni Bonde lenye kuogopesha wengine waliliita Pango la Jabali au Bonde la Mauti, kuna uwezekano kuwa watu wengi walipoteza Maisha katika eneo hilo na hata wachungaji walipoteza mifugo yao huko na walishindwa kuiokoa.

Bwana Ni Mchungaji wa Ajabu:-

Daudi anataka kumfunua Mungu anayemjua Yeye na mwenye uhusiano naye Jinsi alivyomkuu na alivyo na ujasiri kumtegemea, anataka kuionyesha jamii kuwa yeye anaweza kupita katika Bonde hilo lenye harufu ya kifo na akatoka salama, kule ambako jamii nzima inaogopa yeye angeliweza kupita tu kwa  sababu hakuna jambo lolote lenye kuogopesha linaweza kulinganishwa na Mungu wa Daudi na Mchungaji mwema, Kuweza kufahamu kila Daudi anakizungumzia ni lazima tufanye uchambuzi wa Maneno mazito yaliyomo katika zaburi hii.

1.       Bwana ni Mchungaji wangu – Kwa ufupi sana Daudi anatumia Mfano huu (Metaphor) ambao mara nyingi umetumiwa sana na waandishi wa Biblia hususani katika Agano la kela kuonyesha jinsi Mungu anavyojali na kujihusisha na watu wake (Zaburi 28:9, 79:13, 80:1, 95:7 Isaya 40:11Yeremia 31:10 na Ezekiel 34:6-19) Yesu mwenyewe alikuja kuuweka wazi kabisa kuwa Yeye ndiye huyu Mchungaji mwema anayetajwa katika zaburi hii na maandiko mengine  Yohana 10:11-16, Ukweli unaofunuliwa hapa ni sisi ni watoto wa Mungu Mungu ni Baba na ni mwangalizi mkuu wa Maisha yetu, Yeye hutujali na kutuangalia kwa upendo mkubwa sana kuliko wachungaji wanavyoangalia mifugo, Jambo kubwa la Msingi ili kunufaika na Bwana kama ilivyokuwa kwa Daudi ni lazima uwe na uhusiano wa kudumu na Mungu wetu.

2.       Sitapungukiwa kitu – Mungu kama Mchungaji mwema yuko tayari kurupatia malisho, huu ndio ulikuwa wajibu mkuu wa wachungaji wa wanyama walipaswa kuhakikisha kuwa Konndoo wanashiba ipaswavyo, ni wazi kuwa Mungu hushughulkika na mahitaji yetu kiasi ambacho hatutapungukiwa na kitu

3.       Kando ya malisho ya majani mabichi hunilaza – Ulikuwa ni wajibu mwingine wa Mchungaji kuhakikisha kuwa anawapa raha mifugo yake, ikiwa Mungu ni Mchungaji mwema na sisi tu Kodnoo zake yeye hutupa kustarehe pia Yesu alisema Njooni kwangu ninyi nyote wenye kuelemewa na Mizigo nami nitawapumzisha “Mathayo 11:28” haingekuwa hekima ya kawaida common wisdom kwa Mchungaji kuwazungusha mifugo kutwa nzima bila kuwapa pumziko, Mungu anajua kuwa tunahitaji pumziko, ingawa tunapitia changamoto za aina mbalimbali katika ulimwengu huu, Mungu atatupa nyakati za Kuburudika, Acha kusema kuwa utapumzika Kaburini, au au Heri wafu wafao katika Bwana, hayo maneno Daudi hakuyatamka hata kidogo yeye alljua kuwa Mungu atampa pumziko sawa kuna hilo la baadaya lakini hapahapa duniani pia tutafaidika na kazi za Mchungaji mwema, Mungu atalitumia neno lake kama chakula kutulisha na kututia nguvu,Yohana 6:32

4.       Kando ya maji ya utulivu huniongoza. – Ni wazi kuwa Maji yanawakilisha uwepo na faraja ya Roho Mtakatifu, kwa wale wakristo amabao wamejazwa Roho mtakatifu wanafahamu jinsi anavyoburudisha na kuleta utulivu mioyoni mwetu hata kama twapitia majaribu ya aina mbalimbali, Yeye ndio Chemichemi ya uzima acha kujichimbia visima vyako Yeremia 2:13 Roho wa Mungu yuko kutupa faraja ya kweli, ambayo haipatikani kwa Pombe au zinaa au uvutaji wa Bangi kila aina ya burudiko na bubujiko lililo bora utalipata kwa Roho wa Mungu

5.       Hunihuisha nafsi yangu – katika ulimwengu huu tulio nao yako mambo mengi ya kukatisha tamaa na kuvunja Moyo na kuifanya nafsi kuinama, Mungu wa Daudi aliweza kumtia nguvu alimtia Moyo, Zaburi 42:11, Tunapokutana na wakati mgumu wa kukabiliana na changamoto mbalimbali kama tumemfanya Yehova kuwa Mchungaji wetu atatufariji na kuzihuisha nafsi zetu, Daudi alilifahamu hilo vema aliona wema wa Mungu ukifanya hayo katika maisha yake

6.       Huniongoza Katika njia za Haki – Ni muhimu kufahamu kuwa ni Mungu kupitia Roho wake mtakatifu ndiye anayetuongoza katikia njia ya haki Warumi 8;14, Kwaasili mwanadamu havutiwi sana na kutembea katika haki, moyo na nia ya kuhakikisha kuwa tunatembea katika haki hupatikana kwa msaada wa Roho Mtakatifu, na ndio maana ni muhimu ikaeleweka wazi kuwa haki tuliyo nayo haitokanani na uweza wetu na uamuzi wetu ni haki ya Yesu Kristo na tunatembea katika hiyo kwa neema na uongozi wake Daudi alilijua hili wazi,Warumi 8:5-14, alitambua nia ya mwili siku zote inafanya uadui dhidi ya Mungu na kuwa kama anatembea katika haki ni kwa sababu ya utii wake wa kukubali kumsikiliza Mchungaji mwema na so sauti ya Mgeni Yohana 10:3-4, 5.

7.       Kwaajili ya Jina lake:-  Mungu hutufanyia miujiza mikubwa na kutisha na kushangaza kwaajili ya jina lake, wema wote anaotutendea Mungu hufanya ili apate utukufu Zekaria 2:8Kwa maana Bwana wa majeshi asema hivi, Ili nitafute utukufu amenituma kwa mataifa wale waliowateka ninyi; maana yeye awagusaye ninyi aigusa mboni ya jicho lake” Mungu hututetea kwaajili ya Utukufu wake Daudi alijua wazi kuwa kuna kitu cha ziada ndani yake jina la bwana linatukuzwa na hivyo kamwe Mungu hataacha kumuongoza katika njia za haki kwa sababu ya Jina lake takatifu aliloliweka ndani ya Daudi, Mungu akiweka kitu ndani yetu atatuongoza kwaajili yake

8.       Naam, nijapopita kati ya bonde la uvuli wa mauti, Sitaogopa mabaya; Kwa maana Wewe upo pamoja nami:- Daudi sasa analitaja lie Bonde la Wadi Quelt Bonde lenye kutisha sana, ni wazi kuwa Daudi analitumia Bonde hilo kuonyesha kuwa kuna magumu katika ulimwengu huu kuna mambo ya kutisha katika ulimwengu huu, Mungu hatatuacha tusipitie katika magumu, na majaribu, kwamba iwe ni nyakati za hatari, Magumu au hata hatari za kifo Yeye hataogopa mabaya kwa sababu Mungu atakuwa npamoja nayeYeye ni Mlinzi wetu,na ni Mwaminifu kamwe hawezi kutuacha Mathayo  28:20 Nami nitakuwa pamoja nayi hata ukamilifu wa Dahari Mungu ataendelea kuwa pamoja nasi

9.       Gongo lako na fimbo yako vyanifariji.:-  Fimbo na gongo vinawakilisha Mamlaka na silaha za Mungu pia humaanisha kutia nidhamu, au kurudi, kuadhibu, pia inawakilisha nguvu na utendaji wa Mungu Kutoka 21:20, Ayubu 9:34 fimbo ilitumika katika kumrudisha kondoo katika njia au kundi sahihi na iliwaadhibu pale walipokuwa kinyuma na matakwa ya Mchungaji, Mungu huwadhibu wale wampendao ili kuwapa nidhamu yeye mwenyewe lakini pia huwalinda na kuwatetea Gongo liko kwaajili yanulinzi na Usalama wa Kondoo.

10.   Waandaa meza mbele yangu, Machoni pa watesi wangu. Umenipaka mafuta kichwani pangu, Na kikombe changu kinafurika.:- Ukweli ni kuwa wanadamu hawafurahii mafanikio ya wanadamu wengine hata siku moja, kutokana na ubinadamu wao ndani yao kuna wivu na hivyo ni rahisi kuwa na maadui unapobarikiwa na Mungu, Lakini sio hivyo tu Mashetani majini na mapepo hayafurahii uhusiano wetu na Mungu, Daudi alifahamu wazi swala hilo lakini kutokana na ukuu na wema wa Mungu Daudi anamuona mungu kuwa ni mwenye kujali sana , ni mwenye kujali na kulata usalama kiasi ambacho pamoja na hatari ya mashetani na majini na mapepo na madui wa kibinadamu, Bado Mungu anatoa neema na Baraka za Kutosha anakubariki na kukufanikisha mbele ya wanaokuchukia, na hata wale waliokubali kutumiwa na shetani kututesa, Licha ya Baraka zake dhidi ya wanaotuchukio Mungu aliendelea kuonyesha kuwa Daudi ni Mtumishi wake tu ni mtumishi maalumu aliyemchagua amempaka mafuta! Hii ilikuwa ni Dalili ya wazi kuwa yeye amechaguliwa na Mungu na ana upendeleo maalumu na wa kipekee ana uhusiano na Roho Mtakatifu ulio wa Pekee  na kwa sababu hiyo hapungukiwi na kitu, Kikombe kilichofurika kinazungumzia mabalasi yenye uwezo wa kuchukua Galoni 40 za maji, Daudi alimaanisha kuwa kombe lake linafurika ukiwa na Mungu huna shaka maana Balasi lako halipungui, Ukimtegemea Mungu hutapungukiwa na kitu neema na rehema na kufurika roho wa Bwana kutaendelea kububujika siku zote za maisha yetu.

11.   Hakika wema na fadhili zitanifuata Siku zote za maisha yangu; Nami nitakaa nyumbani mwa Bwana milele:- Mchungaji siku zote aliandamana na kondoo kila walikokwenda uhusiano ulistawi waliwapenda na kuwa kitu kimoja, Daudi amabaye ana ujuzi mkubwa wa Kuchunga anaelewa wazi kuwa Mungu yuko pamona naye anafuatana naye akiwa na uso wa wema akiwa yuko tayari kufadhili,alijua kuwa Mungu akiambatana nawe siku zote atatoa msaada wenye kudumu, wema na fadhili bila kujali nini kitatokea mbele yako, Mchungaji hufanya shughuli zake zote kwaajili ya kondoo wake, daudi anamalizia kwa kuonyesha kuwa Lengo lake kuu la kuambatana na mchungaji huyu mwema ni ili siku moja autazame uso wake amtumikie na kumuabudu yeye milele.

Sitaogopa Mabaya:-



Nataka kuhitimisha ujumbe huu kwa kukazia kuwa ukimjua Mungu katika viwango ambayo Daudi alimfahamu Mungu, Hutaogopa chochote katika maisha yako, Mungu ndio zindiko letu, yeye ndie Mwamba ngao na kimbilio hatupaswi kuogopa lolote unapotamka Neno hilo Bwana ndiyo Mchungaji wangu! Kifurushi hicho cha Bwana ndiye Mchungaji wangu kinabeba maswala kadhaa  Nina uhusiano wa kipekee na Mungu, Yeye ndio anayenitunza, yeye ndiye starehe yangu na faraja yangu, Yeye ni faraja yangu, yeye ndiye mlinzi wangu, yeye ni mwaminifu, atanishindia majaribu, nimewekwa wakfu kwake, amanibariki, amanipa upako, ananitosheleza, niko naye milele mpango wangu ni kutokumuacha haya yote yatakufanya usiogope kitu chochote katika maisha yako na yeyote atakayejifanya kuwa ni adui yako atashangaa ukiandaliwa Meza machoni pake, kwaajili ya utukufu wake.
 


Ujumbe na Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima
Rev. Innocent Kamote!

Maoni 2 :

  1. TUMSIFU YESU KRISTO!!
    Ahsante sana na mungu mwenyezi akubariki.

    JibuFuta
  2. Amina ubarikiwe mtumishi

    JibuFuta