Waamuzi 9:8 – 13. Biblia inasema hivi:-
“8. Siku moja miti ilitoka ili
kuutia mmoja mafuta uwe mfalme juu yao; ikauambia mti mzeituni, Tawala wewe juu
yetu. 9. Lakini huo mzeituni ukaiambia, Je! Niache mafuta yangu, ambayo kwangu
mimi watu wamheshimu Mungu na wanadamu, ili niende nikayonge-yonge juu ya miti?
10. Kisha miti ikauambia mtini, Njoo wewe, utawale juu yetu. 11. Lakini huo
mtini ukaiambia, Je! Niuache utamu wangu, na matunda yangu mazuri, niende
nikayonge-yonge juu ya miti? 12. Kisha miti ikauambia mzabibu, Njoo wewe,
utawale juu yetu. 13. Huo mzabibu nao ukaiambia, Je! Niiache divai yangu,
ambayo humfurahisha Mungu na wanadamu, ili niende nikayonge-yonge juu ya miti?”
Leo tutachukua muda kutafakari kwa kina na upana na
marefu kuhusu mti wenye kuleta Heshima kwa Mungu na wanadamu, Ninazungumza
jambo muhimu sana litakaloifaa jamii ya leo ambayo imejaa watu wanaoteseka kwa
kukosa maarifa, kama utafuatilia somo hili kwa moyo maisha yako yatabadilika na
utakuwa na furaha maishani mwako, Leo nataka kuzungumzia kuhuzu mti wa Mzeituni
(Olive Tree) lakini kwanza nataka ufahamu jambo hili
Mwanzo kabisa Mungu alipouumba ulimwengu alitoa
zawadi ya mimea na miche pamoja na miti kwa wanadamu kama chakula na zawadi
soma Mwanzo 1:29 “ biblia inasema
29. Mungu akasema, Tazama,
nimewapa kila mche utoao mbegu, ulio juu ya uso wa nchi yote pia, na kila mti,
ambao matunda yake yana mbegu; vitakuwa ndivyo chakula chenu; 30. na chakula
cha kila mnyama wa nchi, na cha kila ndege wa angani, na cha kila kitu
kitambaacho juu ya nchi, chenye uhai; majani yote ya miche, ndiyo chakula
chenu; ikawa hivyo.
Miche na miti katika biblia ya kiingereza huitwa Herbs tuangalie Biblia ya
Kiingereza tafasiri ya King James Bible inasema:-
"And God said, Behold, I have given you every herb bearing seed, which is upon the face of all the earth, and every tree, in the which is the fruit of a tree yielding seed; to you it shall be foe meal"
Ni wazi kuwa miti na mimea ndio chakula cha kwanza
walichopewa wanadamu kabla ya kuongezewa nyama katika Mwanzo 9:3 baada ya gharika wakati
wa Nuhu, Moja ya mti muhimu sana unaotajwa katika Biblia ni mti wa Mzeituni na
tunda la zeituni na mafuta ya mzeituni huu ni moja ya mti muhimu sana katika
uumbaji wa Mungu, Wayahudi na waarabu na wakristo wa zamani sana walifahamu
sana umuhimu wa mmea wa mzeituni ukilinganisha na nyakati tulizonazo katika kizazi
hiki, ni kwasababu hiyo leo Mkuu wa wajenzi ninataka kuchukua muda kueleza
maswala kadhaa muhimu kuhusu mti huu wenye kuleta Heshima kwa Mungu na
wanadamu.
Mmea wa Mzeituni ni mmea unaomea kwa wingi sana
katika nchi ya Israel, Hata leo, mashamba ya mizeituni
yametapakaa kutoka sehemu za chini ya Mlima Hermoni upande wa kaskazini hadi
viunga vya Beersheba upande wa kusini. Mizeituni bado inapatikana kwenye pwani
ya Uwanda wa Sharoni, vilima vyenye mawemawe vya Samaria, na mabonde yenye
rutuba ya Galilaya lakini pia ni mmea unaostawi na kuzalishwa kwa wingi katika inchi ya
Hispania (Spain) Nchi hii kwa sasa ndio inayoongoza kwa uzalishaji
wa Mafuta ya Mzeituni na sehemu nyingine nyingi duniani, Mungu ameupa mmea huu
uwezo wa ajabu sana kama tutakavyoweza kuona mbeleni lakini pia mmea huu kwa
tabia zake ni mmea ambao hauwezi kuharibiwa,Unapoukata mzeituni unauwezo wa
kutoa machipukizi mapya na ukaendelea kuwepo mara moja, Matunda yake yanauwezo
wa kutoa au kuzalisha mafuta mengi ambayo hutumika kwa shughuli mbalimbali,
ikiwa ni pamoja na kupikia, kujipaka, kuwashia taa, na kutibu wanadamu, katika
shughuli za Ibada mmea huu ni mmea wa kikuhani kwa vile unatumika kutangaza
rehema za Mungu na unatumiwa katika ishara ya amani, kuweka wakfu viongozi wa
kisiasa, kijamii na kidini yaani Wafalme, Makuhani na manabii. Aidha mti huu
mafuta yake na matawi yake hutumika katika kufukuza Mapepo (Mashetani na
Majini) kwa jina la Yesu.
Katika kuwatia Moyo Israel katika safari yao ya
kwenda Kanaani moja ya vitu vyenye mvuto sana kwa wana wa Israel ambavyo Mungu
alimtumia Musa kuvitaja ilikuwa ni pamoja na Mizeituni yenye mafuta. Kumbukumbu 8:7-8 biblia inasema
7. Kwa kuwa Bwana, Mungu wako,
yuakuingiza katika nchi nzuri, nchi yenye vijito vya maji, na chemchemi, na
visima, vibubujikavyo katika mabonde na milima; 8. nchi ya ngano na shayiri, na
mizabibu, na mitini, na mikomamanga; nchi ya mizeituni yenye mafuta, na asali;
·
Sifa za Mzeituni
·
Historia ya Kibiblia kuhusu Mzeituni
·
Matumizi ya Mzeituni
Sifa za Mzeituni.
Kwa kawaida Mzeituni ni mti usio na
Mvuto ukiuona kwa mara ya kwanza. Si mrefu kama mierezi fulani yenye kuvutia ya
Lebanoni. Mbao zake hazina thamani kama mbao za mberoshi, na maua yake
hayavutii kama maua ya mlozi ambayo ilitumika kujengea Nyumba katika Israel
kama maandiko yasemavyo katika wimbo ulio bora
Wimbo
Ulio bora 1:17 Biblia inasema hivi:- “Nguzo za
nyumba yetu ni mierezi, Na viguzo vyetu ni miberoshi”. Na Amosi 2:9 9. “Lakini
nalimwangamiza Mwamori mbele yao, ambaye urefu wake ulikuwa kama urefu wa
mierezi, tena alikuwa na nguvu kama mialoni; lakini naliyaangamiza matunda yake
toka juu, na mizizi yake toka chini”.
Sehemu muhimu zaidi ya mzeituni
haionekani—iko chini ya ardhi. Mizizi yake mingi, ambayo hufikia kina cha meta
sita chini ya ardhi na kwenda hata mbali zaidi kuelekea upande-upande, ndiyo
hasa hufanya mti huo uzae sana na kustahimili hali ngumu.
Mizizi hiyo huiwezesha mizeituni kwenye
vilima vyenye mawemawe istahimili ukame wakati ambapo miti iliyo kwenye bonde
imekwisha kauka kwa kukosa maji. Mizizi huiwezesha kuendelea kuzaa zeituni kwa
karne nyingi, ingawa huenda shina lisilovutia likaonekana kuwa lafaa tu kwa
kuni. Mti huo usiovutia huhitaji tu nafasi ya kukua na udongo wenye hewa, bila
magugu au mimea mingine inayoweza kuwa na wadudu waharibifu. Mahitaji hayo
sahili yakitimizwa, mti mmoja utatoa lita 57
za mafuta kila mwaka.
Historia ya Kibiblia kuhusu
Mzeituni.
Kibiblia Mzeituni unatajwa kwa mara ya kwanza katika
Kitabu cha Mwanzo 8:6-12 “6. Ikawa baada ya siku
arobaini, Nuhu akalifungua dirisha la safina, alilolifanya; 7. akatoa kunguru,
naye akatoka akaenda huko na huko, hata maji yakakauka juu ya nchi. 8. Kisha
akatoa njiwa, aone kwamba maji yamepunguka usoni pa nchi; 9. bali yule njiwa
hakuona mahali pa kutua kwa wayo wa mguu wake, akamrudia Nuhu safinani, maana
maji yalikuwa juu ya uso wa nchi yote; naye akanyosha mkono, akamtwaa,
akamwingiza mle safinani. 10. Akangoja na siku saba tena; kisha akamtoa yule
njiwa katika safina mara ya pili, 11. njiwa
akamjia jioni, na tazama, alikuwa na jani bichi la mzeituni kinywani mwake, ambalo
amelitunda, basi Nuhu akajua ya kwamba maji yamepunguka juu ya nchi. 12.
Akangoja na siku saba tena, akamtoa yule njiwa; naye asimrudie tena kamwe.”
Mzeituni unatajwa kama mti ulioashiria amani baada
ya Hasira za Mungu alipoangamiza dunia kwa maji, Nuhu alituma ndege Kunguru
ambaye alizurura bila kutoa ripoti na njiwa ambaye alirejea na kijitawi cha
jani la mzeituni Tangu wakati huu mzeituni ulipata umaarufu mkubwa sana na
kitendo cha njiwa kurudi na Jani bichi la Mzeituni kinywani mwake kuliashiria taarifa
ya amani kwa Nuhu na familia yake.
Alama ya “V” ya vidole inayotumika sehemu nyingi
sana Duniani ni matokeo ya njiwa huyu aliyekuja na jani la mzeituni katika
safina, aidha matumizi ya tawi la mzeituni kama alama ya AMANI/shalom/salaam,
yalitumika sana na watu wa Magharibi Karne tano hivi kabla ya Kristo, Wayunani
wa kale waliutumia mti huu, kama alama ya uzao na masimulizi na historia
zinaonyesha pia waliutumia kufukuzia pepo wachafu, kwa jina la mungu
aliyejulikana kama Eirene au Irene ambayo maana yake ni Shalom/Salaam au amani,
wapagani wa Kirumi pia walitumia matawi ya Mzeituni kumaanisha mungu mke wa
amani ambaye alijulikana kama PAX na katika Coins za zamani za Kirumi iliwekwa
nyuma ya fedha maana hizi hazitofautiani sana na maana ya asili iliyotumiwa na
waandishi wa Biblia.
Fedha ya zamani sana
(Coin) ya Kirumi ikiwa na tawi la Mzeituni
Mara nyingi waandishi wa Biblia
walitumia mzeituni kama mfano. Sehemu mbalimbali za mzeituni zilitumika
kufananisha rehema ya Mungu, ahadi ya ufufuo, na maisha ya familia yenye
furaha. Kuuchunguza mzeituni kwa makini kutatusaidia kuelewa marejeo hayo ya
Kimaandiko na kutafanya tuuthamini sana mti huu wa pekee ambao pamoja na
uumbaji mwingine wote, ni moja ya mti wenye matunda unaofanya kazi ya kumsifu
Mungu Zaburi 148:7,9.
Matumizi
ya Mzeituni na Mafuta ya Mzeituni.
Bila shaka, zeituni zilipendwa sana na
Waisraeli kwa sababu ya mafuta yake yenye thamani. Walitumia katika nyumba zao
taa zenye tambi zilizotumia mafuta ya zeituni. Pia Mungu aliagiza wana wa
Israel kuleta mafuta ya mzeituni kwaajili ya Taa yenye vinara saba iliyopaswa
kuwaka Daima katika nyumba ya Mungu.
Taa yenye vinara Saba
iliwaka katika nyumba ya Bwana Daima ikitumia Mafuta ya Mzeituni
Mambo ya walawi 24:2 “1. Kisha BWANA akanena na Musa, na kumwambia, 2. Waagize
wana wa Israeli kwamba wakuletee mafuta ya zeituni safi ya kupondwa kwa ajili
ya ile nuru, ili hiyo taa iwake daima. 3. Hapo nje ya pazia la ushahidi, ndani
ya hema ya kukutania, Haruni ataitengeza tangu jioni hata asubuhi mbele za
BWANA daima; ni amri ya milele katika vizazi vyenu.”
Mafuta ya zeituni yalikuwa muhimu katika
upishi. Yalikinga ngozi dhidi ya miali ya jua, na Waisraeli waliyatumia
kutengenezea sabuni. Mazao muhimu ya nchi yalikuwa nafaka, divai, na zeituni.
Hivyo, ungekuwa msiba mkubwa kwa familia ya Waisraeli mizeituni ikikosa
kuzaa.
Kumbukumbu
la Torati 7:13 Biblia inasema. “naye atakupenda
na kukubarikia na kukuongeza tena ataubarikia uzao wa tumbo lako, na uzao wa
nchi yako, nafaka zako na divai yako, na mafuta yako, maongeo ya ng'ombe zako,
na wadogo wa kondoo zako, katika nchi aliyowaapia baba zako kuwa atakupa.”
Kubarikiwa kwa Divai na Mafuta yanayotajwa hapo ni Mafuta ya Mzeituni Habakuki 3:17 Ilikuwa ni laana nzito ni
adhabu kama Bwana ataipiga nchi kiasi cha kufikia Mzeituni kuzaa kwa shida “Maana mtini hautachanua maua, Wala mizabibuni hamtakuwa
na matunda; Taabu ya mzeituni itakuwa bure, Na mashamba hayatatoa chakula;
Zizini hamtakuwa na kundi, Wala vibandani hamtakuwa na kundi la ng'ombe;”
Hata hivyo, kwa kawaida mafuta ya
zeituni yalikuwa mengi. Yaelekea kwamba Musa aliliita Bara Lililoahidiwa ‘nchi
ya zeituni’ kwa sababu mizeituni ilipandwa kwa wingi sana katika eneo hilo.
Mtaalamu wa mambo ya asili, H. B. Tristram, wa karne ya 19 aliutaja mzeituni
kuwa “mti wa kawaida wa nchi ya Kanaani yaani Israel.” Kwa sababu ya thamani
yake na wingi wake, mafuta ya zeituni yalitumika katika eneo lote la
Mediterania yakiwa kama fedha ya kimataifa. Yesu Kristo mwenyewe alitaja deni
ambalo lilikadiriwa kuwa “vipimo mia vya bathi vya mafuta ya mzeituni.” Luka
16:5-6 “5.Akawaita wadeni wa bwana wake, kila
mmoja; akamwambia wa kwanza, Wawiwani na bwana wangu? 6. Akasema, Vipimo mia
vya mafuta. Akamwambia, Twaa hati yako, keti upesi, andika hamsini”.
“Baraka kuu zililinganishwa Kama
Miche ya Mizeituni”
Mzeituni wenye mafaa ni mfano ufaao wa
baraka za Mungu. Mtu anayemcha Mungu angethawabishwaje? “Mkeo atakuwa kama
mzabibu uzaao, vyumbani mwa nyumba yako,” mtunga-zaburi akaimba. “Wanao kama
miche ya mizeituni wakiizunguka meza yako.” Zaburi128:3 “Mkeo atakuwa kama mzabibu
uzaao, Vyumbani mwa nyumba yako. Wanao kama miche ya mizeituni Wakiizunguka
meza yako”.“Miche ya mizeituni” ni nini, na kwa nini mtunga-zaburi
anailinganisha na wana?
Mzeituni ni wa pekee kwa kuwa
machipukizi mapya huchipuka daima kutoka kwenye shina lake. Wakati shina kuu
liachapo kuzaa kama zamani kwa sababu ya uzee, wakulima wanaweza kuacha miche
au machipukizi mapya yakue na kuwa sehemu muhimu ya mti huo. Baada ya muda, mti
wa awali utazungukwa na mashina machanga matatu au manne yenye nguvu, kama wana
wanaoizunguka meza. Miche hiyo inatumia mzizi uleule, nayo hutoa mazao mazuri
ya zeituni.
Hali hiyo ya mzeituni ni mfano ufaao wa
jinsi imani ya wana na binti iwezavyo kuwa thabiti kwa sababu ya mizizi ya
kiroho yenye nguvu ya wazazi wao. Watoto wakuapo, wao vilevile huzaa matunda na
kuwategemeza wazazi wao, ambao hufurahi kuona watoto wao wakimtumikia Mungu
pamoja nao. Mithali 15:20
“Mzeituni Unafundisha kuwa Yako
Matumaini ”
Baba mzee-mzee anayemtumikia Mungu
hupendezwa na watoto wake wenye kumcha Mungu. Lakini watoto haohao huomboleza
wakati hatimaye baba yao ‘anapoenda njia ya ulimwengu wote.’ (1Wafalme 2:2). Ili kutusaidia
kuvumilia msiba kama huo wa familia, Biblia hutuhakikishia kwamba kutakuwa na
ufufuo. Yohana 5:28-29, 11:25
Aubu, aliyekuwa baba ya watoto wengi,
alifahamu vizuri kwamba maisha ya mwanadamu ni mafupi. Aliyalinganisha na maua
ambayo hunyauka upesi. (Ayubu 1:2, 14:1,2). Ayubu alitamani
sana kufa ili aepuke maumivu, akiliona kaburi kuwa mahali pa kujificha ambapo
angeweza kutoka. “Mtu akifa, je! atakuwa hai tena?” Ayubu akauliza. Kisha kwa
uhakika akajibu: “Mimi ningengoja siku zote za vita vyangu, hata kufunguliwa
kwangu kunifikilie. Wewe ungeita, nami ningekujibu; ungekuwa na tamaa ya kazi
ya mikono yako.”Ayubu 14:13-15
Ayubu alionyeshaje imani kwamba Mungu
angemwita kutoka kaburini? Kwa kutumia mti ambao kutokana na jinsi
anavyoufafanua, yaelekea ni mzeituni. “Yako matumaini ya mti,” Yobu akasema. “Ya
kuwa ukikatwa utachipuka tena.” Ayubu
14:7 Mzeituni unaweza kukatwa, lakini kufanya hivyo hakutauharibu. Utakufa
tu uking’olewa. Mizizi isipong’olewa, huo mti utachipuka tena ukiwa na nguvu
mpya.
Hata ikiwa ukame wa muda mrefu
unanyaukisha mzeituni wa zamani, shina lililonyauka laweza kuchipuka tena.
“Ijapokuwa mizizi yake huchakaa mchangani, na shina lake kufa katika udongo;
lakini kwa harufu ya maji utachipuka, na kutoa matawi kama mche.” Ayubu 14:8-9 Ayubu
aliishi katika nchi kavu na yenye vumbi ambako yaelekea aliona mashina mengi ya
mizeituni iliyozeeka ambayo yalionekana yamenyauka na bila uhai. Hata hivyo,
mvua iliponyesha mti huo “mfu” ulichipuka tena na mizizi yake kutoa shina jipya
kana kwamba ni “mche.” Uwezo huo wa kipekee wa kuchipuka tena ulifanya mkulima
mmoja wa bustani wa Tunisia aseme: “Kwa kweli mizeituni haiwezi kufa.”
Kama vile mkulima anavyotamani kuona
mizeituni yake iliyonyauka ikichipuka tena, ndivyo Mungu anavyotamani kufufua
watumishi wake waaminifu. Anangojea kwa hamu wakati ambapo watu waaminifu kama
Abrahamu na Sara, Isaka na Rebeka, na wengine wengi watafufuliwa. Mathayo
22:31-32 Itakuwa ajabu kama nini kuwakaribisha wafu na kuwaona wakiishi tena
maisha kamili yenye manufaa!
Mzeituni wa Mfano
Sifa ya Mungu ya kutobagua na pia
uandalizi wake wa ufufuo hudhihirisha rehema yake. Mtume Paulo alitumia
mzeituni kuonyesha jinsi ambavyo Yehova huwarehemu watu bila kujali rangi au
malezi yao. Kwa karne nyingi Wayahudi walijivunia kuwa wachaguliwa wa Mungu,
“uzao wa Abrahamu.” Yohana 8:33, Luka
3:8
Haikuwa lazima uwe mzaliwa wa taifa la
Kiyahudi ili kupata kibali cha Mungu. Hata hivyo, wanafunzi wote wa kwanza wa
Yesu walikuwa Wayahudi, na walikuwa na pendeleo la kuwa wanadamu wa kwanza
kuteuliwa na Mungu kufanyiza mbegu ya Abrahamu iliyoahidiwa Mwanzo 22:18 Wagalatia 3:29. Paulo
aliwalinganisha wanafunzi hao Wayahudi na matawi ya mzeituni wa mfano.
Wengi wa Wayahudi wa asili walimkataa
Yesu, wakijinyima pendeleo la kuwa washiriki wa “kundi dogo,” au “Israeli wa
Mungu.” Luka 12:32: Wagalatia 6:16 Hivyo
wakawa kama matawi ya mzeituni wa mfano yaliyokatwa. Ni nani wangechukua mahali
pao? Mwaka wa 36 Baada ya Kristo., wasio Wayahudi walichaguliwa kuwa sehemu ya
mbegu ya Abrahamu. Ilikuwa kana kwamba Yehova alipandikiza matawi ya
mzeituni-mwitu kwenye mzeituni wa bustani. Wale ambao wangefanyiza mbegu ya
Abrahamu iliyoahidiwa wangetia ndani watu wa mataifa. Wakristo wasio Wayahudi
sasa wangeweza kuwa ‘washiriki wa mzizi wa unono wa mzeituni.’Warumi 11:17
Lingekuwa jambo lisilowazika na lililo
“kinyume cha asili” kwa mkulima kupandikiza tawi la mzeituni-mwitu kwenye
mzeituni wa bustani. Warumi 11:24 “Pandikiza mti mzuri
kwenye mti wa mwituni, na, kama vile Waarabu wasemavyo, ule mzuri utashinda
ule wa mwituni,” chaeleza kitabu The Land and the Book, “lakini
huwezi kupandikiza mti wa mwituni kwa mti mzuri ukafanikiwe.” Wakristo Wayahudi
hali kadhalika walishangaa wakati ambapo Yehova ‘kwa mara ya kwanza alielekeza
uangalifu wake kwa mataifa ili achukue kutoka kwayo watu kwa ajili ya jina
lake.’ Matendo 10:44-48, 15:14 Hata
hivyo, hiyo ilikuwa ishara ya wazi kwamba kutimizwa kwa kusudi la Mungu
hakukutegemea taifa moja tu. La, kwa kuwa “katika kila taifa mtu ambaye humhofu
na kutenda uadilifu akubalika kwake.” Matendo
10:35
Paulo alionyesha kwamba kwa kuwa
“matawi” ya mzeituni ya Wayahudi wasio waaminifu yalikatwa, mtu yeyote aweza
kukatwa vivyo hivyo akikosa upendeleo wa Yehova kwa sababu ya kiburi na
kutotii. Warumi 11:19,20 Kwa kweli
jambo hilo laonyesha kwamba hatupaswi kupuuza fadhili isiyostahiliwa ya Mungu 2Wakoritho 6:1.
Kupaka Mafuta kwa Maombezi ya
Mgonjwa
Maandiko yanarejezea kihalisi na kwa
mfano matumizi ya mafuta ya zeituni. Zamani, majeraha na machubuko
‘yalilainishwa kwa mafuta’ ili yapone haraka. Isaya 1:6 Kulingana na mojawapo ya mifano ya Yesu, Msamaria
aliyekuwa jirani mwema alipaka mafuta ya zeituni na divai kwenye majeraha ya
mtu aliyemkuta kwenye barabara ya kwenda Yeriko Luka 10:34.
Mtu huburudika na kupata kitulizo
apakapo mafuta ya zeituni kichwani. Zaburi
141:5 Wazee Wakristo wanaweza
‘kumpaka mafuta mtu ambaye hawezi wanaposhughulika na ugonjwa wa mwili na kiroho.na Kuomba kwa Jina la Yesu
Yakobo 5:14 Ushauri wenye upendo wa
wazee unaotokana na Maandiko na sala zao za kutoka moyoni kwa niaba ya mwamini
mwenzao aliye mgonjwa kiroho zinalinganishwa na mafuta ya zeituni yenye
kutuliza. Yapendeza kwamba kuna usemi wa Kiebrania ambao wakati mwingine
humwita mtu mzuri “mafuta safi ya zeituni.”
‘Mzeituni Unaostawi Katika
Nyumba ya Mungu’
Kwa kuzingatia mambo ambayo yametajwa,
si ajabu kwamba watumishi wa Mungu wanaweza kulinganishwa na mizeituni. Daudi
alitamani kuwa kama “mzeituni mbichi, unaostawi katika nyumba ya Mungu.” Zaburi
52:8 “Bali mimi ni kama mzeituni Umeao katika
nyumba ya Mungu. Nazitumainia fadhili za Mungu milele na milele.”
Kama vile mara nyingi familia za Waisraeli zilivyokuwa na mizeituni
iliyozingira nyumba zao, vivyo hivyo Daudi alitaka kuwa karibu na Mungu na kuzaa
matunda kwa sifa ya Mungu.
Ufalme wa Yuda wa makabila mawili
ulikuwa kama “mzeituni wenye majani mabichi, mzuri, wenye matunda mema” wakati
walipokuwa waminifu kwa Mungu. Yeremia
11:15-18 “15. Mpenzi wangu afanya nini
nyumbani mwangu, ikiwa amefanya uasherati? Je! Nadhiri zako na nyama takatifu
zitakuondolea hatia? Ufanyapo maovu, ndipo uonapo furaha. 16. Bwana alikuita
jina lako, Mzeituni wenye majani mabichi, mzuri, wenye matunda mema; kwa kelele
za mshindo mkuu amewasha moto juu yake, na matawi yake yamevunjika. 17. Kwa
maana Bwana wa majeshi, aliyekupanda, ametamka mabaya juu yako, kwa sababu ya
maovu ya nyumba ya Israeli, na ya nyumba ya Yuda, waliyoyatenda juu ya nafsi
zao wenyewe kwa kunikasirisha, wakimfukizia Baali uvumba. 18. Tena Bwana
akanijulisha haya, nami nikayajua; ndipo uliponionyesha matendo yao.”
Lakini watu wa Yuda na Israel walipoteza hali hiyo ya kupendelewa ‘walipokataa
kusikia maneno ya Mungu; wakafuata miungu mingine. Yeremia 11:10 “Wameyarudia maovu ya baba zao, waliokataa kusikia maneno
yangu; wamewafuata miungu mingine na kuwatumikia; nyumba ya Israeli, na nyumba
ya Yuda, wameyavunja maagano yangu niliyoyafanya na baba zao.”
Ili kuwa mzeituni unaostawi katika
nyumba ya Mungu, ni lazima tumtii Mungu na kuwa tayari kukubali nidhamu ambayo
yeye hutumia “kutupogoa” ili tuweze kuzaa matunda zaidi ya Kikristo.Waebrania 12:5-6 Isitoshe, kama vile
mzeituni wa kawaida huhitaji mizizi mingi ili kustahimili ukame, twahitaji
kuimarisha mizizi yetu ya kiroho kusudi tuvumilie majaribu na mnyanyaso Mathayo 13:21, Wakolosai 2:6-7.
Mzeituni unafananisha vizuri na Mkristo
mwaminifu, ambaye huenda asijulikane katika ulimwengu bali anatambuliwa na
Mungu. Mtu kama huyo akifa katika mfumo huu, ataishi tena katika ulimwengu mpya
unaokuja. 2Wakoritho 6:9, 2Petro 3:13.
Mzeituni ambao ni kama hauwezi
kuharibiwa, ambao huendelea kuzaa matunda mwaka baada ya mwaka watukumbusha
ahadi hii ya Mungu: “Kama siku za mti ndivyo zitakavyokuwa siku za watu wangu,
na wateule wangu wataifurahia kazi ya mikono yao muda wa siku nyingi.” Isaya 65:22 Ahadi hiyo ya kiunabii itatimizwa katika ulimwengu mpya wa
Mungu 2Petro 3:13.
Jinsi
ya Kutumia Mafuta ya Mzeituni kwa shughuli (Mahitaji) Mbalimbali.
1. Kuweka
wakfu Kiongozi Mafuta ya mzeituni hutumika wakati wa kumuweka wakfu Kiongozi wa
Kisiasa, Kidini na kijamii, Katika Israel Nabii, Mfalme na Kuhani waliwekwa
wakfu kwa ibada maalumu na kupakwa mafuta unapompaka mtu mafuta kwa mujibu wa
nafasi aliyo nayo utatangaza kupitia neno la Mungu Je Bwana Hakukupaka Mafuta
Ili………………..(Unaeleza Kusudi la kumpaka mafuta hayo) kisha unamiminia na
kumuombea neema kwaajili ya kazi hiyo kupitia Jina la Yesu Mfano 1Samuel 10:1 “
Ndipo Samweli akatwaa kichupa cha mafuta akayamimina kichwani pake akambusu
akasema Je Bwana hakukutia mafuta [Uwe mkuu juu ya watu wake Israel? Nawe utawamiliki
watu wa Bwana na kuwaokoa na mikono ya adui zao kisha hii itakuwa ishara kwako
ya kuwa Bwana amekutia Mafuta ] uwe mkuu juu ya urithi wake”
Unapompaka mafuta kiongozi lazima utangaze kusudi la kupakwa kwake mafuta nay
ale yatakayonenwa yatampata.Kama anayepakwa Mafuta ni Mchungaji , Kuhani padre
au nabii utasoma Kutoka 29:7 na
kumuombea nneema ya majukumu yake na kumpaka mafuta,
Ibada ya kumpaka mtu mafuta yaweza kufanyika hata Faragha
2. Ikiwa
unahitaji Mafuta haya kwaajili ya kumpokea Roho Mtakatifu utasoma Luka 4:18-19 pia 1Samuel 16:13 kisha ingia katika maombi ya kuhitaji kujazwa Roho
mtakatifu na utashangaa nguzu za Mungu zitakushukia na utaanza kusema kwa lugha
nyingine
3. Ikiwa
unatumia mafuta kwaajili ya kuondoa msongo wa mawazo, kujilinda na maadui wa
kibinadamu na mashetani utachukua mafuta ya mzeituni utasoma Zaburi ya 23 yote na kisha utajipaka au
utampaka mtu mwenye stresses Msongo wa mawazo na kisha utaomba neema na rehema
huku ukiyasambaza mafuta hayo katika upaji wa uso kwa kutumia jina la Yesu na
mtu huyo atapokea amani na furaha tangu wakati huo
4. Ikiwa
ni kwaajili ya kuombea Mgonjwa ambaye hawezi utachukua kichupa cha mafuta ya
mzeituni, utaongena na mgonjwa na kumtia moyo na kumfariji kisha utasoma pamoja
naye Yakobo 5:14-15 na Marko 16:17-18
5. Ikiwa
ni kwaajili ya kukemea vifungo vya shetani ba kutoa pepo chukua mafuta ya
mzeituni kisha soma maandiko yafuatayo na weka mkono wako juu ya mtu mwenye
pepo omba rehema kwaajili yake na kukemea kwa jina la Yesu Luka 4:18-19, na Marko 16:17-18
6. Ikiwa
ni kwaajili ya kujilinda na maadui wa aina yoyote yaani wakimwili na kiroho
jipake mafuta ya mzeituni na kabla ya kujipaka utasoma maandiko haya kisha
utajipaka na kujiombea au kumuombea mwenye uhitaji huo Zaburi 27:1-6, 1Samuel 2:10
7. Ikiwa
ni kwaajili ya nguvu za kiume au za kike utajipaka mafuta hayo ya mzeituni
wakati unapokuwa unakwenda kulala katika sehemu ya via vya uzazi kisha utaomba kisha
utaisema Zaburi ya 103:1-5 utasubiri
kwa dakika tano nguvu zitakushukia kufurahia uumbaji wa Mungu
8. Kwaajili
ya kujitibu Mafua utajipaka katika eneo la pua na tundu zake mara tatu kwa siku
ukitumia Marko 16:17
9. Kwaajili
ya kuua wadudu wabaya walioko tumboni utayaombea mafuta hayo na kunywa kijiko
cha chai 1X2 kwa siku kwa mfululizo siku saba Marko 16:17-18
10. Kwaajili ya
kutunza kumbukumbu na kuponya ugonjwa wa kusahau chukua mafuta ya zeituni
jipake katika paji la uso soma Zaburi ya
103:1-5 kisha muombe Mungu kwa jina la Yesu na utakuwa wa ajabu
11. Kwa mtu
alitepooza atachua eneo lililopooza mara mbili kila siku, mwenye pepo la
Degedege atapaka mwili mzima kwa siku mara mbili maombi yatatangulia na Marko 16:17-18 itasomwana kuomba katika
jina la Yesu
12. Kwaajili ya
kutunza Ngozi isizeeke kuondoia mikunjo, kuondoa alama za kuungua na jua,
kukinga mionzi ya jua kulainisha mishipa, kukinga na saratani ya ngozi,
kupambana na sumu kwenye ngozikilinda ngozi kupatwa na sumu,kuondoa mabaka kuondoa
ukavu kwenye ngozi soma Zaburi 103:1-5
kisha omba nap aka mafuta haya mwili mzima kama mafuta ya kawaida hutazeeka
haraka
13. Ikiwa una
kesi na hoja ngumu zinakukabili Mahakamani soma Isaya 54:17 kisha fanya maombi ya ushindi na ujasiri jipake mafuta
ya mzeituni Bwana atakupigania nawe utanyamaza kimya
14. Mafuta
ya Mzeituni yanaweza kutumika hata kwa kuukanda mwili Massaging na kusababisha
mwili ku- relax kupata ahueni nakuondoa uchovu. Pia mizeituni huleta usingizi mzuri
15. Mafuta ya mzeituni yanaweza pia kutumika kwa kuvunjia mikataba ya aina mbalimbali yaani nira na maagano ambayo ulijiingiza na kama unataka kujikomboa
Mafuta ya Mizeituni hupatikana katika maduka mbalimbali supermarket, na sehemu nyinginezo kumbuka ni muhimu kupata mafuta Original na sio yaliyochanganyika na kitu kwa vila mengine utaweza kula, kujipaka na kadhalika huitaji msaada wa Mchungaji au kiongozi wa dini kuona matokeo ya mizeituni zaidi ya kujifunza, kuamini na kutendea kazi.
Matumizi ya neno la Mungu na mafuta
yanaweza kutumika katika maeneo mengi zaidi ya haya itategemea na ufunuo wako
na maandiko utakayoweza kuyatumia utayatumia kulingana nauhitaji wako, Hakuna
utata wa kimaandiko kuhusu matumizi ya mafuta,sio lazima upewe na manabii au Mchungaji kanunue mwenyewe hata ndoo nzima kwa matumizi yako ingawa mafuta haya ni ghali, kwa muda mrefu sana nilimtumikia
Mungu na kuombea watu bila ya matumizi ya mafuta, sikupanda kabisa kutaka
kuyatumia, kwa zaidi ya miaka 20 ya kumtumikia Mungu sikutaka kuamini katika
swala hili, nilisubiri kupata ufunuo kamili wa swala hili na dhamiri yangu
kuhusu matumizi ya mafuta na Mungu aliponithibitishia kuwa Inatenda kazi
naliona vema kama mkuu wa wajenzi kuweka fundisho hili wazi, Jambo kubwa la
msingi usiyatumia mafuta kama Biashara, wala usiyatumie kama uganga bali
yatumia kwa imani na maombi na neno la Mungu na utaweza kuona Mafanikio, Kwa
maandiko zaidi kuhusu Mafuta katika Biblia soma mistari kadhaa ifuatayo:-
Kutoka 25:6, 29:7, 29:2,
29:29,30:3,22-26,40:9, 40:15, Walawi.8:10,8:12,4:3,5,16,6:20,
Zaburi.132:10,1Sam.16:13,2Sam.24:4,1Nyakati.16:22;Zab.105:15,1Wafalme-19:16 1Nyakati.16:22, Zab.105:15, Isa. 21:5,Luke 7:38-40, Kumb.
28:40, Ruth 3:3,2Samuel 14:2,
Zab.104:15,
109:18, Isaiah 1:6,Mark 6:13, Yakobo. 5:14, Mark 14:8,Luka. 23:56, Zab. 2:2;
Dan. 9:25, 26,
Isa. 61:1, Zab. 45:7; Heb. 1:9, John 1:41; Mdo. 9:22; 17:2, 3;
18:5, 28, 1 Yoh. 2:20, Matt. 25:1-13
Nimepata kitu
JibuFutabarikiwa sana nimeongeza maarifa nitatumia ii nakala kwa kuwa najiombeazaidi amina
JibuFutaBarikiwa sana, nimejifunza kitu
JibuFutaAsantee san
JibuFuta
JibuFutaNimebarikiwa sana na nimefurahi ufafanuzi natamka MUNGU akuinue na akutumie zaidi wewe na uzawa wako akupe baraka in je sus mighty name
Naitaji mafuta hayo original
JibuFutaNimepanda mche wa mzeituni hapa nyumbani kwangu toka mwezi March 2023.Mche unaendelea kukua vizuri. Nitarajie matunda baada ya muda gani?
JibuFutaNakushuru sana MTU wa Mungu barikiwa sana kwa elimu nzuri Mimi ni muuza wa mafuta mzeituni lakini nilikuwa sijui kazi take kama nikubwa hivyo asante sana naitwa Lidya samweli
JibuFuta