Jumatatu, 18 Julai 2016

Ujumbe: “Si kwa Uwezo, wala si kwa nguvu bali ni kwa Roho yangu”


Kiini: Umuhimu wa Kumuachia Roho wa Mungu atawale

Andiko la Msingi: Zekaria 4:6-10

.6. Akajibu akaniambia, akisema, Hili ndilo neno la Bwana kwa Zerubabeli, kusema, Si kwa uwezo, wala si kwa nguvu, bali ni kwa roho yangu, asema Bwana wa majeshi. 7.Nani wewe, Ee mlima mkubwa? Mbele ya Zerubabeli utakuwa nchi tambarare; naye atalileta lile jiwe la kuwekwa juu kabisa pamoja na vigelegele vya, Neema, neema, ilikalie. 8. Tena neno la Bwana likanijia, kusema, 9. Mikono yake Zerubabeli imeiweka misingi ya nyumba hii, na mikono yake ndiyo itakayoimaliza; nawe utajua ya kuwa Bwana wa majeshi amenituma kwenu. 10. Maana ni nani aliyeidharau siku ya mambo madogo? Kwa kuwa watafurahi, nao wataiona timazi katika mkono wa Zerubabeli; naam, hizi saba ndizo macho ya Bwana; yapiga mbio huko na huko duniani mwote. ”


Utangulizi:

Zerubabel alikuwa ni Liwali wa Jiji la Yerusalem baada ya Wayahudi kurudi kutoka Uhamishoni, Jina Zerubabel ni muungano wa Maneno mawili ya Kiibrania Zeri na Babilon ambalo maana yake ni Mzizi au Chipukizi kutoka Babeli, aliteuliwa kuwa liwali wa Yuda na Mfalme Artashasta, liwali huyu alikuwa anakabiliwa na kazi ngumu ya Ujenzi wa Hekalu, Kazi hii ilikuwa ni Mapenzi ya Mungu kabisa na Mungu alikuwa ameweka moyoni mwake  Mzigo wa kulijenga Hekalu, wakati huu kazi ya Ujenzi ilikuwa ngumu sana kuliko wakati wa Suleimani ni muhimu kufahamu kuwa ni kazi rahisi sana kujenga kitu mara moja lakini ni kazi ngumu sana kukirudia, Kazi ilikuwa ngumu na yenye upinzani mwingi sana, Kama ilivyokuwa kwa Nehemia Mungu alipoweka Moyoni mwake kuujenga ukuta wa Yerusalem kulikuwa na upinzani mkubwa sana, Zerubabel hali kadhalika alikutana na upinzani mkali wakati wa kulijenga Hekalu.

Hali halisi ya upinzani ilikuwa Hivi:-

1.      Watu waliokuwa wakiuzunguka mji walijaribu kuwakatisha tamaa, waliwatisha, waliiba baadhi ya vifaa vya ujenzi,
2.      Kila mara tunapojihusisha na kazi yoyote ya Mungu ni lazima shetani atatumia kila mbinu na hila kuharibu kabisa mikakati na mipango ya kimungu na kutukatisha tamaa.
3.      Shetani anaelewa wazi nini kinatokea watu wanapokuwa wamekata tamaa na kujichokea
4.      Watu wanapokata tamaa kumuamini Mungu kunapungua, Mambo yoyote yale yakifanyika katika hali ya hofu na kutokumcha Mungu mafanikio huwa ni madogo sana, Biblia inasema Mungu hakutupa Roho ya woga “2Timoth 1:7” watu waliokata tamaa hudumaa, hawawezi kufanya jambo lolote lile Duniani, ukiwa na jeshi la wanajeshi waliokata tamaa hata uwe na vifaa vya kisasa vya aina yoyoteile ushindi unaweza kuwa ni hadithi ya kusikiliza tu

5.      Shetani licha ya kututishia bali pia atashambulia na kuiba furaha tuliyonayo
6.      Watu walimuacha Zerubabeli peke yake na kila mtu akaanza kuangalia mambo yake na kujenga nyumba yeke mwenyewe na unjezi wa hekalu ukawa umesimama watu walikufa moyo “Mathayo 6:33” Kumbuka jinsi Israel walivyokufa moyo baada ya wapelelezi kuleta habari mbaya ya kuvunja Moyo, walisahahu kabisa kuwa Mungu yuko Pamoja nao, walianza kutumia akili
7.      Zerubabel alikata tamaa kwa sababu alikuwa haoni njia tena maono yake yalianza kufifia na moyo wake ulianza kupoteza matumaini jaribu lilionekana ni kubwa na tayari ujenzi wa Hekalu ulionekana kuwa mzigo na mlima mkubwa ambao sio rahisi kuusawazisha

Ndipo Mungu alipomuinua Nabii Zekaria kwaajili ya kumtia moyo Zerubabel  Na nabii Hagai kwaajili ya kuwatia Moyo wayahudi, Nabii Zekaria alimueleza wazi Zerubabel ujumbe kutoka kwa Mungu kwamba si kwa nguvu si kwa uweza Bali kwa Roho yangu asema Bwana, Mungu aliukemea mlima uliokuwa unamkabili Zerubabel na kuutabiria kuwa utakuwa Tambarare Mungu alimuahidi kuwa macho yake yanazunguka kuangalia duniani kote ni nani anamtumaini yeye na kila anayemtumaini yeye hatata tahayarika

Inawezekana hali kama ya Zerubabel inajitokeza katika Maisha yako, umeanza kukata tamaa,umeshambuliwa na kukosa msaada umeanza kutumia akili zako katikakutatua majaribio yako lakini wiki hii ninazo habari njema kwako kuwa Bwana amenituma nikuambie umtegemee yeye Machjo yake yanaangalia ni nani anamtegemea naye atamruhusu Roho wake mtakatifu kukutia nguvu na kukuwezesha atalikemea kila tatizo linaloonekana kuwa gumu katika maisha yako na litakuwa tambarare, Bwana akubariki na kukuongeza kwa utukufu wake katika Jina la Yesu amen

Ujumbe Na mkuu wa wajenzi mwenye Hekima
Rev. Innocent Kamote.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni