Jumanne, 23 Agosti 2016

Kuutetea Urithi wako!


Andiko la Msingi: 1 Wafalme 21:1-4

1. Ikawa baada ya hayo, Nabothi Myezreeli alikuwa na shamba la mizabibu katika Yezreeli, karibu na nyumba ya kifalme ya Ahabu mfalme wa Samaria. 2. Ahabu akasema na Nabothi, akamwambia, Nipe shamba lako la mizabibu nilifanye shamba la mboga, maana ni karibu na nyumba yangu; nami nitakupa badala yake shamba la mizabibu lililo zuri zaidi; au ukipenda, nitakupa fedha sawasawa na thamani yake. 3. Nabothi akamwambia Ahabu, Bwana apishe mbali nikupe wewe urithi wa baba zangu. 4. Basi Ahabu akaenda nyumbani kwake, ana moyo mzito, tena amekasirika, kwa sababu ya neno lile aliloambiwa na Nabothi Myezreeli, akisema, Sitakupa urithi wa baba zangu. Akajilaza kitandani pake, akageuza uso wake, akakataa kula.”

    
 Naboth aliuawa akijaribu kuutetea urithi wa Baba zake kutokana na tamaa ya mfalme Ahabu na malikia muovu Yezebeli

Utangulizi:

Ni muhimu kufahamu kuwa Biblia inazungumzia kwa undani sana kuhusu UMUHIMU WA URITHI, Katika Israel Urithi ulitambuliwa kama moja ya maswala muhimu sana na kama mtu aliuza urithi alizarauliwa sana katika jamii ya kiebrania na kuitwa jina la dharau kama mtu asiyemcha Mungu au mwesharati Katika Waebrania  angalia kwa mfano Waebrania 12: 16-17 Biblia inasema hivi;-

16. Asiwepo mwasherati wala asiyemcha Mungu, kama Esau, aliyeuuza urithi wake wa mzaliwa wa kwanza kwa ajili ya chakula kimoja. 17. Maana mwajua ya kuwa hata alipotaka baadaye kuirithi baraka, alikataliwa (maana hakuona nafasi ya kutubu), ijapokuwa aliitafuta sana kwa machozi.”

Angalia kwa makini jinsi Esau alivyoitwa katika maandiko, alidharaulika kama mtu asiyemcha Mungu na mwesharati kwa nini? Kwa sababu aliuza urithi wake

Ni nini maana ya neno Urithi?

Urithi kwa asili ni Baraka kutoka kwa Mungu, ambazo zinaweza kutafasirika katika ulimwengu wa kimwili na kuhusisha fedha, mali, mashamba, mtaji karama, vipawa, maisha yako ya baadaye, Elimu, Kazi, Mume, mke watoto,zawadi na kadhalika.

Baraka hizo zinaweza kuweko duniani au kwa mtu toka kizazi hata kizazi, mtu anaweza kupokea urithi kutoka kwa Mungu, Roho Mtakatifu, wazee wetu, na Baraka hizo na mali zikadumu, urithi kwa kawaida hauwi mali ya mtu mmoja unakuwa ni mali ya familia, watu wako au jamii yako, urithi unaambatana na Heshima mfano Mgombe urais wa republican Donald Trump ambaye ni tajiri mkubwa sana duniani mwenye kuheshimika sana lakini inajulikana wazi kuwa utajiri wake na heshima yake inatokana na urithi wa utajiri wa Majumba kutokakwa Baba yake, na kwa mujibu wa maandiko katika torati Mungu alikataza kabisa kuuza urithi soma Hesabu 36:7 Biblia inasema haya:-

Hivyo hapana urithi wo wote wa wana wa Israeli utakaotoka kabila hii kwenda kabila hii; kwa kuwa wana wa Israeli watashikamana kila mtu na urithi wa kabila ya baba zake.”

Unaweza kuongezea na andiko kama Walawi 25:23Nayo nchi haitauzwa kabisa kabisa; kwani nchi ni yangu mimi; maana ninyi ni wageni na wasafiri wangu

Unaweza kuona Mungu alikataza kabisa kuuzwa kwa urithi lakini alikataza pia kuuza nchi, mtu aliyeuza alihesabiwa kama mtu asiyemcha Mungu au mwesharati, mtu anayefanya ukahaba ni tofauti na mtu anayefanya uasherati, makahaba huuza miili yao ili kupata kipato, wanatoa miili yao kwa mapatano ya kupata faida, anayefanya uasherati anatoa mwili wake bure, anautoa akitarajia kuwa hatimaye ataolewa mwisho wa siku anajikuta amechezewa lakini haolewi, anakuwa amepoteza tumaini, amepoteza muda na huku amesha chezewa vya kutosha na hakuna alichoambulia, mtu anayechezea urithi anachezea maisha yake ya baadaye naya jamii yake, shetani wakati wote ataangalia mbele katika mfumo wa maisha yako na kuanza kupambana na mafanikio yako ya baadaye, kumbuka alipambana na Yusuphu kwa sababu ya ndoto zake akitumia wivu wa kaka zake,
Watanzania kamwe tusikubali kuuza ardhi, wala wanyama wetu, tusikubali kuwaachia wakawa mawindo wala kuwauza katika nchi zao kwani baadaye hawatasafiri kuja kwetu kuangalia urithi tuliopewa na Mungu, tusikubali madini na malighafi nyinginezo kuchukuliwa hovyo

Katika 1Wafalme 21:1-4 Tumeona Jinsi Naboth alivyokuwa na msimamo, Mfalme Ahabu alitamani sana kulinunua shamaba la mizabibu la Nabothi , Jambo hili lilikuwa kinyume na Torati, Kama tulivyosoma, Nabothi alielewa vizuri sana swala hilo, na alijitia nguvu kumjibu mfalme kwa ujasiri 

BWANA APISHIE MBALI NIKUPE WEWE URITHI WA BABA ZANGU?

Ingawa majibu ya Nabothi yaligharimu maisha yake na familia yake kwani wote waliuawa na mfalme ili kujipatia shamba hilo kupitia mkewe muovu Yezebeli , Hata hivyo Nabothi anabaki kuwa mtushujaa na jasiri na mwenye imani na mcha Mungu kwani alijua umuhimu wa kuutunza urithi wa Baba zake, Mungu akupe neema na ampe neema kila mmoja wetu kuhakikisha kuwa kwa gharama yoyote anatunza na kuutetea urithi wa taifa letu, jamii yetu, ndugu zetu na wazazi wetu.
Ukiyajua hayo heri wewe ukiyatenda!

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni