Jumatano, 26 Oktoba 2016

Kila amwaminiye Hatatahayarika!


Mstari wa msingi: 1Petro 2:6-8
 
6. Kwa kuwa imeandikwa katika maandiko Tazama, naweka katika Sayuni jiwe kuu la pembeni, teule, lenye heshima, Na kila amwaminiye hatatahayarika. 7. Basi, heshima hii ni kwenu ninyi mnaoamini. Bali kwao wasioamini, Jiwe walilolikataa waashi, Limekuwa jiwe kuu la pembeni.8. Tena, Jiwe la kujikwaza mguu, na mwamba wa kuangusha, Kwa maana hujikwaza kwa neno lile, wasiliamini, nao waliwekwa kusudi wapate hayo.”

 "Naye Kristo Yesu mwenyewe ni jiwe kuu la pembeni."

Tutajifunza somo hili kwa kuzingatia vipengele viwili muhimu vifuatavyo

·         Maana ya jiwe kuu la Pembeni
·         Kila amwaminiye Hatatahayarika

Utangulizi:

Leo katika Mistari hii kuna mambo ya msingi sana ya kujifunza ambayo tunayapata kutoka kwa Petro, kimsingi Petro mahali hapa alinukuu maandiko kwa kusudi la kuwatia moyo wote waliomuamini Yesu Kristo, na kulikubali neno lake, Petro anatuhakikishia kuwa hatutaaibika katika wakati huu wa sasa na hata wakati wa kuja kwake Bwana na wakati wa hukumu. Kila amwaminiye Hatatahayarika!

Jiwe kuu la Pembeni.

Nataka kwanza kuweka wazi maana ya Neno Jiwe kuu la Pembeni Yesu Kristo anaitwa jiwe kuu la Pembeni, katika taratibu za ujenzi za zamani jiwe hilo lilichongwa kwa umakini sana ili liwe limenyooka na lilitumika kutafuta unyoofu wa mawe au matofali mengine, jiwe hili kwa kawaida lilitumika kujengwa katika kona ya jingo na ndipo mawe au matofali mengine yangefuata, licha ya kuitwa jiwe kuu la Pembeni pia liliitwa Jiwe la Msingi jiwe hilo kwa mujibu wa masimulizi ya kale liliwekwa kwa vigelegele na shangwe na ndio ulikuwa msingi muhimu wa nyumba ulioshika jingo zima, Mara nyingi hasa jiwe hili la Msingi au la pembeni lilikuwa na Heshima zaidi lilipotumika kujenga Hekalu ambao kwa sasa unazungumzia kanisa au watu wa Mungu 

Waefeso 2:20-22 “20. Mmejengwa juu ya msingi wa mitume na manabii, naye Kristo Yesu mwenyewe ni jiwe kuu la pembeni. 21. Katika yeye jengo lote linaungamanishwa vema na kukua hata liwe hekalu takatifu katika Bwana. 22. Katika yeye ninyi nanyi mnajengwa pamoja kuwa maskani ya Mungu katika Roho.”

Maandiko yanamtaja Yesu Kristo kuwa ndio jiwe kuu la Pembeni au jiwe la msingi, maandiko yanaonyesha kuwa wale wanaomuamini na kumtegemea watakuwa na heshima kuu lakini wasiomuamini na wanaomkataa watakumbwa na mwakwazo ya ajabu sana katika maisha yao, wataainbika katika ulimwengu huu na ule ujao

Biblia inapomtaja Yesu kama Jiwe katika sayuni inatabiri pia kuweko kwa watu watakaomkataa 

Zaburi 118: 22  Jiwe walilolikataa waashi Limekuwa jiwe kuu la pembeni.” Waashi wanaotajwa hapo ni wajenzi, Mafundi ujenzi Mason hili ni kundi la Makuhani wakuu, wazee na waandishi (waalimu wa torati) hawa ndio walikuwa na nafasi ya kwanza kulijenga Hekalu na kanisa kuanzia na jamii ya Wayahudi, lakini kupitia mafundisho yao hawakuwaelekeza watu kwa Yesu na walipinga kabisa mfumo mpya na msingi mpya wa Ujenzi wa Kanisa ambalo ni Yesu, Yesu kristo ni jiwe la kweli la Msingi wote wanaomkataa wataaibika, itakuwa bahati mbaya sana kwao kwani ni kama wameumbwa wapatwe na mabaya, Makunani wazee na waandishi ambao walitarajiwa kuwajenga watu na kuwaunga na Kristo na wamekataa itakuwa ni kama wale waangukao juu ya jiwe hilo ama wale ambao jiwe litawaangukia Mapema Mzee Simon alitambua unabii huu wa Isaya na Zaburi kuwa Yesu ndio jiwe lile na aliwaelekeza watu kwa kutoa habari zake

 Luka 2:34  Simeoni akawabariki, akamwambia Mariamu mama yake, Tazama, huyu amewekwa kwa kuanguka na kuinuka wengi walio katika Israeli, na kuwa ishara itakayonenewa.”

Simeon alikuwa ameelewa kuwa Yesu angekataliwa Israel nzima sawa na unabii wa Isaya na wenyeji wa Yerusalem wangemkataa masihi na kujiletea hukumu kubwa sana

Isaya 8:14-15 “14. Naye atakuwa ni mahali patakatifu; bali ni jiwe la kujikwaza na mwamba wa kujikwaa kwa nyumba za Israeli zote mbili, na mtego na tanzi kwa wenyeji wa Yerusalemu. 15. Na wengi watajikwaa juu yake, na kuanguka na kuvunjika, na kunaswa na kukamatwa.”

Mungu ampe neema kila mmoja wetu kutokuwa miongoni mwa wajenzi, waashi waliomkataa Yesu au watakao mkataa Yesu na kujiletea hukumu kubwa nay a aibu

Kila amwaminiye Hatatahayarika!

1Petro 2:6 “Kwa kuwa imeandikwa katika maandiko Tazama, naweka katika Sayuni jiwe kuu la pembeni, teule, lenye heshima, Na kila amwaminiye hatatahayarika.”

ni muhimu kufahamu kuwa Petro anaponukuu neno Kila amwaminiye hatatahayarika!, Neno hilo limetokana na na unabii wa Isaya katika kitabu cha nabii Isaya 28:16 Mstari huo unasomeka 

“16. kwa ajili ya hayo Bwana, MUNGU, asema hivi, Tazama, naweka jiwe katika Sayuni, liwe msingi, jiwe lililojaribiwa, jiwe la pembeni lenye thamani, msingi ulio imara; yeye aaminiye hatafanya haraka.”

Kuna lugha mbili hapo zinatumika  

1.       Na kila amwaminiye hatatahayarika - Petro
2.       yeye aaminiye hatafanya haraka – Isaya

Biblia zote zimetumia neno katika Isaya “He who believe shall not make HASTE” Neno la asili la kiebrania HASTE ni “NADAD” ambalo maana yake ni kutoupigwa vitani, kutokuchanganyikiwa, kutokimbia mbele ya adui zako, kutowapa kisogo adui zako, kutokuwaogopa, kutokuwa mkimbizi, kutokufutiliwa mbali, kutokuhukumiwa na kutokuaibika ndio kutokutahayarika

Petro anamthibitishia kila amwaminiye Yesu ambaye ni jiwe kuu la Pembeni hatakatiliwa mbali, hatapata aibu, hatakimbia vitani, atahishimika, kuna ushindi mkubwa kwa kila aliyemwamini na kumtegemea Yesu, kila mtu na amfanye Yesu kuwa tumaini lake aweze kuyafaidi mema ya nchi.

Na Rev. Innocent Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima

Maoni 1 :