Jumatatu, 24 Oktoba 2016

Sisi tutalitaja jina la Bwana Mungu wetu!


Andiko Zaburi 20:7 “ Hawa wanataja magari na hawa farasi, Bali sisi tutalitaja BWANA, Mungu wetu


 Hawa wanataja magari na hawa farasi, Bali sisi tutalitaja BWANA, Mungu wetu

Utangulizi.

Ni muhimu kufahamu kuwa Zaburi hii chimbuko lake ni Mfalme Daudi, kiongozi wa nyimbo au kwaya wa Daudi aliimba wimbo huu, au Daudi alitunga na kuwapa watu wa sifa waimbe hivyo Zaburi hii inahesabika kama moja ya zaburi ya Daudi, Hata hivyo kihistoria Zaburi hii ilitumiwa sana na wafalme waliofuata baada ya Daudi kama njia ya maombi walipokuwa wanakwenda kupigana vita, Mfalme aliomba na kutoa sadaka kisha watu walisindikiza maombi na dua za mfalme wao kwa Zaburi hii, hivyo ni zaburi maarufu kama maombi kwaajili ya kukabiliana na mambo ya kutisha! Ilitumika wakati wa shida na wakati wa kuhitaji msaada.

Kuna mambo mengi sana yaliyomo katika zaburi hii, lakini kubwa likiwa ni Dua ya kumuombea Mfalme, kwa nini mfalme aliomewa sana kwa sababu yeye alitangulia mbele wakati wa vita, alikuwa ndio mpambanaji mkuu na hivyo waimbaji na waombaji walimuombea angalia Mstari wa 1-4 Biblia inasema

1. Bwana akujibu siku ya dhiki, Jina la Mungu wa Yakobo likuinue. 2. Akupelekee msaada toka patakatifu pake, Na kukutegemeza toka Sayuni. 3. Azikumbuke sadaka zako zote, Na kuzitakabali dhabihu zako. 4. Akujalie kwa kadiri ya haja ya moyo wako, Na kuyatimiza mashauri yako yote.”

Baada ya dua na maombi ya kumuombea Mfalme waliweka matumaini yao kuwa Mungu anakwenda kuwapa ushindi hivyo walianza kushangilia ushindi, walilitumia jina la bwana na waliweka bendera tayari kwa imani  na pia walimkumbusha Mungu kwa imani kuwa atamwokoa masihi wake na kumjibu Maombi yake walikuwa na ujasiri kuwa watajibiwa Mstari wa 5-6 na kuwa ni lazima Mungu atafanya mambo makubwa kwa mkono wake 

“5. Na tuushangilie wokovu wako, Kwa jina la Mungu wetu tuzitweke bendera zetu. Bwana akutimizie matakwa yako yote. 6. Sasa najua kuwa Bwana amwokoa masihi wake;Atamjibu kutoka mbingu zake takatifu.”

Katika mstari wa 7 na wa 8 waimbaji hawa walionyesha tofauti iliyoko kati ya wanaoamini na wasioamini lakini pia walionyesha kwamba ndipo mahali pa kuzingatiwa sana katika utendaji wa Mungu, “Hao (wasiamini) au wenye kiburi wanataja Magari na hawa wasiomtegemea Mungu wa kweli wanataja Farasi, Bali sisi tunaoliamini Jina la Mungu tutalitaja jina la bwana Mungu wetu! Ni muhimu kupaangalia mahali hapa kwa makini sana

Mungu alikuwa amewafundisha Isarael siku nyingi sana kumtegemea yeye na kumwangalia kwaajili ya ushindi na dhiki ya aina yoyote, na katika nyakati za vita moja ya vitu vilivyokuwa vinaogopewa sana katika nyakati za vita za zamani ni magari ya vita na magari ya wapiganaji walikuwa wakipigana juu ya farasi, watu hao walikuwa hodari hata kufukuzia na hivyo katika nyakati za biblia watu au mataifa yaliyokuwa na magari ya vita na wapanda farsi hodari waliogopwa zaidi kwani ndio waliokuwa hatari na wenye kutisha sana katika nyakati za leo Magari haya tungeweza kufananisha na tanks au vifaru wakati wa vita wote tunajua namna vinavyotisha sana

Mungu aliwaonya mapema Israel kutokuogopa Kumbukumbu la taorati 20: 1Utokapo kwenda vitani kupigana na adui zako na kuona farasi na magari na watu wengi sana kuliko wewe usiwaogope, kwa kuwa Bwana Mungu wako yu pamoja nawe aliyekukweza kutoka nchi ya Misri” pia Yoshua 17:16

Nchi ya Misri na Syria ndio zilikuwa hatari zaidi kwa aina hii ya vita katika nyakati hizo na makabila mengine pia Israel hawakuwa na aina hiyo ya silaha wakati huo, wala hawakuwa na jeshi kubwa sana, hivyo wale wasiomuamini Mungu waliweka tumainilao katika hayo magari ya chuma nay a farasi na wapanda farasi, Israel walikuwa wamekwisha kupata somo kubwa kwamba Misri ilifanywa nini pamoja na kuwa na Magari ya farasi na wapanda farasi Kutoka 15:1-4, Mungu alikwisha kuwafundisha kutokuyategemea magari na wapanda farasi, Mungu aliwajulisha kuwa hufanya mambo kwaajili ya jina lake na kwaajili ya utukufu wake, Mungu hatakuinamisha bali Mungu atakusimamisha mungu hatakuaibisha bali Mungu atakuokoa Mstari 8-9 waimbaji wanaonyesha kuwa hawataaibika na kuwa adui zao watainama

Ndugu yangu haijalishi ni hila kiasi gani adui anazo,

Haijalishi watakuwa na nguvu kiasi gani

Haijalishi magonjwa yamekutesa kiasi gani, yamekuandama na kukukandamiza kwa kiwango gani mtegemee Mungu tu

Haijalishi watakuwa na mbinu  za kibinadamu kiasi gani, wana silaha na magari ya chuma kiasi gani, wana watetezi kiasi gani, wana uzoefu kiasi gani, wana akili kiasi gani, wana mitego kiasi gani, wana nguvu kiasi gani tunachokiangalia wanatumainia nini, je wanatumainia fedha, majeshi, nguvu waimbaji wakasema wao wanataja Farasi namagari sisi tutalitaja jina la Bwana Mungu wetu, wapendwa na tuchangamke, tunaye Mungu, tunaye shujaa, anauwezo, ana nguvu, ni hodari wa vita atatupigania anakwenda kutupa ushindi anza kuufurahia ushidni wako leo yuko Mungu wa Yakobo atatuokoa na ataisikia sauti yetu,

Bwana Mungu nimekutegemea wewe, tumaini langu si kwa wanadamu Bali ni katika jina lako
Sasa najua kuwa Bwana amwokoa masihi wake*

Na. Rev. Innocent Kamote
Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni