Andiko la Msingi: Matendo 1:8 “Lakini mtapokea nguvu, akiisha kuwajilia
juu yenu Roho Mtakatifu; nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, na
katika Uyahudi wote, na Samaria, na hata mwisho wa nchi.”
Hii hapo juu ni picha (symbol) ya Roho Mtakatifu na sio Roho Mtakatifu
Utangulizi.
Hali ya kanisa la leo imekuwa
dhaifu kuliko Nyakati za kanisa la Kwanza, Kanisa lilikusudiwa na Mungu kuwa
Chombo kikuuu cha ukombozi wa wanadamu Baada ya kazi njema iliyofanywa na Yesu
Msalabani, Mungu analitegemea kanisa kuwa kama Waamuzi, watetezi, wakombozi,
makuhani, wafalme na askari wa mstari wa mbele katika kuwatetea wanyonge,
walioonewa na waliosetwa katika vifungo vya Ibilisi, na kukemea uovu, kuikosoa
serikali na kuonyesha njia kwa ulimwengu!
Luka 4: 18-19 “Roho wa Bwana yu juu yangu, Kwa maana amenitia mafuta
kuwahubiri maskini habari njema. Amenituma kuwatangazia wafungwa kufunguliwa
kwao, Na vipofu kupata kuona tena, Kuwaacha huru waliosetwa, Na kutangaza mwaka
wa Bwana uliokubaliwa.”
Kanisa lilipaswa kufanya kazi
hizo alkizozitaja Yesu na kuzitabiri Isaya hapo Juu, ikiwa Roho wa Mungu yuko
juu yetu, ikiwa ametupaka Mafuta, lakini jiulize leo hii je kazi zinazofanywa
na kanisa ndizo hizo hapo juu? Leo kanisa limejaa watu wengi wenye Stresses
yaani migandamizo, lina watu wengi wasio waaminifu bila kujali kuwa wako ngazi
gani za kiroho, yale ambayo zamani tulikuwa tunayaona na kuyashuhudia
yakifanywa na watu tuliowaita Mataifa watu wasiomjua Mungu, tuliokuwa
tukiwalilia waokolewe, wamjue Mungu wamgeukie Mungu sasa ndio yanafanywa na Kanisa,
Je ni mara ngapi kanisa limekaa kimya watu wanapoonewa, Mauaji yanapotokea
Duniani, vita vinavyoendelea, matishio ya umwagikaji wa damu na dhuluma za kila
aina je leo ni nani anaifanya kazi hii? Nani anasimamia haki za binadamu
zinazoendana sawa na Neno la Mungu? Kwa nini tumefikia hapa tulipofikia? Kuna
na mambo mengi sana sitaki kuyazungumza hapa lakini wewe unayajua kuhusu hali
ya kanisa la leo! Ni ya kushangaza, ni kweli ziko huduma za kinabii na mitume
na miujiza ambayo inatendeka na najua inatendeka kwa nguvu za Roho Mtakatifu,
lakini je uadilifu? Uko? Je Hakuna ulevi, uongo, picha za ngono, chuki, uadui,
uchawi, ushirikina, masengenyo, uasherati na zinaa, je hatutoi muda mwingi kwa
simu zetu, tablets, na laptop, zaidi kuliko kwa Mungu na familia zetu, hali ni
mbaya mno sasa, Turudi kukazia kazi za Roho Mtakatifu ndani ya kanisa,
tutajifunza somo hili kwa kuzingatia vipengele viwili vifuatavyo:-
1. Roho
Mtakatifu ni Nani?
2. Kazi
za Roho Mtakatifu Katika ya Kanisa
Roho Mtakatifu Ni nani?
Katika Maandiko Roho Mtakatifu
anaelezewa vema kama Nafsi kamili inayojitegemea
yeye ni BWANA yaani ni Mungu 2Wakoritho
3:17-18 17. Basi 'Bwana' ndiye Roho; walakini alipo Roho wa Bwana, hapo
ndipo penye uhuru. Lakini sisi sote, kwa uso usiotiwa utaji, tukiurudisha utukufu
wa Bwana, kama vile katika kioo, tunabadilishwa tufanane na mfano uo huo, toka
utukufu hata utukufu, Waebrania 9:14 Roho Mtakatifu ni wa Milele
tunaelezwa katika maandiko “basi si zaidi damu yake Kristo, ambaye kwamba kwa
Roho wa milele alijitoa nafsi yake kwa Mungu kuwa sadaka isiyo na mawaa,
itawasafisha dhamiri zenu na matendo mafu, mpate kumwabudu Mungu aliye hai?”
kuwepo milele ni sifa ya uungu, 1Petro
1:2, Roho Mtakatifu ni Mungu kama ilivyo kwa Baba na Mwana kwa msingi huo
hatupaswi kumfikiri Roho mtakatifu kama nguvu tu au hamasa Fulani, ana sifa za
nafsi anafikiri, Warumi 8:27 ana hisia Warumi
15:30 ana maamuzi 1Wakoritho 12:11
na ana uwezowa kupenda na kufurahia ushirika , alitumwa na Mungu Baba kuleta
uwepo wa kiungu kwa washirika ili tufurahie ushirika wetu na Kristo Yohana 14:16-18,26, kwaajili ya hayo
Kanisa linapaswa kukumbuka kuwa Roho ni Mungu na ni nafsi na nilazima
tuhakikisha anaunganishwa mioyoni mwetu, na kuwa anastahili kuabudiwa kupendwa
na kusikilizwa Marko 1:11.
Kazi za Roho Mtakatifu katika Kanisa.
1. Yeye
ndio njia ya wokovu anayetushawishi kwa habari ya haki dhambi na hukumu Yohana 16:7-8 Sasa basi ni vigumu kwa
kanisa kujisikia hukumu na kufa kwa dhamiri kama Roho Mtakatifu hapewi nafasi
ya kutosha katika kuifanya kazi ya kutuhukumu kwa habari ya dhambi, kutuonyesha
kuna hukumu kubwa ijayo endapo hatutatubu na kutushuhudia namna ya kutenda
haki.
2. Anafunua
kweli kuhusu Kristo Yohana 14:16,26,
3. Anatuzaa
kwa upya Yohana 3:3-6
4. Anatufanya
washirika wa mwili wa Kristo 1Wakoritho
12:13
5. Anatutakasa Warumi
8:9, IWakoritho 6:19
6. Anatuthibitishia
kuwa sisi ni wana wa Mungu Warumi 8:16
7. Anatusaidia
katika kuabudu Matendo 8:26-27
8. Anatufanya
tumtukuze Yesu Kristo Wagalatia
5:22-23,1Petro
9. Anazalisha
neema ya Kristo inayotufanya tuwe na sifa zinazomtukuza Kristo Wagalatia 5:22-23, 1Petro 1:2
10. Ni
Mwalimu na hutuongoza katika kweli yote Yohana
16: 13, 14:26, 1Wakoritho 2:9-16
11. Aanamfunua
Yesu kwetu na kutuongoza katika kuwa na ushirika na Yeye Yohana 14:16-18,16:14
12. Anapanda
upendo wa Mungu siku zote ndani yetu Warumi 5:5
13. Anatupa
Furaha faraja na msaada Yohana 14:16,
1Thesalonike 1:6
14. Ni
njia ya huduma na hututia nguvu kwaajili ya huduma, shuhuda na utangazaji wa
Neno la Mungu Matendo 1:8, 4:31 na
hutenda miujiza Matendo 2:43;3:2-8,
5:15, 6:8, 10:38
15. Anatoa
Karama za Roho kwa kusudi la kulijenga Kanisa 1Wakoritho 12-14
16. Analijenga
Kanisa Waefeso 2:22, anatia moyo
kuabudu Wafilipi 3:3
17. Anaongoza
katika Umisheni Matendo 13:2,
anateua waamini Matendo 20:28
18. Anapaka
Mafuta watumishi Matendo 2:4 1Wakoritho
2:4
Hitimisho!
Kama ikiwa Roho wa Mungu hufanya
kazi hizo zote kanisa halipaswi kumdharau, upungufu mkubwa unaolikumba kanisa
la leo unatokana na sababu tu za kumzimisha Roho Mtakatifu, Ni lazima kanisa
limpe Roho Mtakatifu kipaumbele kama linataka kuwa hai nnapozungumza kanisa
namaanisha kila mtu aliyeokolewa anayemwamini Yesu anapaswa kuzingatia haya ili
Kazi za Mungu ziweze kufanyikakatika kiwango ambacho Mungu amekikusudia na sio
chini ya kiwango.
Mkuu wa Wajenzi mwenye Hekima
Rev. Innocent Kamote. 0718990796
Barikiwa Sana
JibuFutaAmina endelea kuelimisha jamii
JibuFuta