Jumatatu, 3 Aprili 2017

Mwamba wenye Imara.

Andiko: 1Wakoritho 10:4 Biblia inasema “wote wakanywa kinywaji kile kile cha roho; kwa maana waliunywea mwamba wa roho uliowafuata; na mwamba ule ulikuwa ni Kristo.”

 Mji uliochongwa katika Mwamba huko Jordan unajulikana kama mji wa Petra yaani Mwamba

Utangulizi:

Ilikuwa mwaka wa 1763 wakati Mchungaji Rev.Augustus  Montague Toplady, Muhubiri wa Injili kutoka kijiji cha Blagdon Huko Mendip Hill Uingereza, alipokuwa akisafiri kwa shughuli za injili, alikumbwa na dhoruba kali sana njiani alijaribu kutafuta hifadhi katika moja ya miamba na kufanikiwa kuwa salama na ndipo baadaye alitunga wimbo MWAMBA WENYE IMARA au MWAMBA ULIOPASUKA ambao ni moja ya nyimbo kuu na za Muhimu sana kwa waanglikan na umekuwa maarufu katika tenzi za rohoni namba 58 na nyimbo za injili 30, wimbo huu ulichapishwa kwa mara ya kwanza mwaka 1775 na gazeti moja la injili lililojulikana kama The gospel Magazine. Wimbo ulipendwa sana na Prince Albert ambaye aliagiza wimbo huo upigwe siku atakapokufa na ndipo ukawa maarufu sana wakati wa misiba hata ingawaje wimbo huu unamzunguzia Yesu kama Mwamba.
Mwamba wenye imara,
Kwako nitajificha,
Maji hayo na damu,
Yaliyotoka humu,
Hunisafi na dhambi,
Hunifanya mshindi.

Kwa kazi zote pia,
Sitimizi sheria,
Nijapofanya bidii,
Nikilia na kudhii,
Hayaishi makosa,
Ndiwe wa kuokoa. 

Sina cha mkononi,
Naja msalabani,
nili tupu, Nivike,
Ni mnyonge, nishike,
Nili mchafu naja,
Nioshe nisijafa.

Nikungojapo chini,
Na kwenda kaburini,
Nipaapo mbinguni,
Na kukwona enzini,
Roho yangu na iwe,
Rahani mwako wewe.


Mtunzi wa wimbo huu aliokoa maisha yake katika mwamba! Na kwa vile alikuwa muhubiri alielewa wazi kuwa Mwamba ulimwakilisha Yesu Kristo, Katika majira haya ya Pasaka ni muhimu kwetu kurudi katika maandiko na kutafakari kwa kina kwa nini Yesu anaitwa Mwamba? Watakatifu waliotutangulia walimfananisha Mungu na mwamba.

Biblia inamtaja wazi Mungu wetu kuwa ni Mwamba wa wokovu wetu

1.       Zaburi ya 18:2 Bwana ni jabali langu, na boma langu, na mwokozi wangu, Mungu wangu, mwamba wangu ninayemkimbilia, Ngao yangu, na pembe ya wokovu wangu, na ngome yangu.

2.       Zaburi ya 62:1-2 Nafsi yangu yamngoja Mungu peke yake kwa kimya, Wokovu wangu hutoka kwake.  Yeye tu ndiye mwamba wangu na wokovu wangu, Ngome yangu, sitatikisika sana

3.       Zaburi ya 95: 1 Njoni, tumwimbie Bwana, Tumfanyie shangwe mwamba wa wokovu wetu.

Neno mwamba katika Biblia ya Kiebrania linatajwa kwa maneno makuu mawili yaani TSUR ambalo maana yake ni gema au pande kubwa la jiwe, na neno lingine ni SELA ambalo maana yake ni mlima au Jabali au ngome ya Jiwe, Kiyunani ni Peter na Petra
 
Kwa hivyo Biblia inapomtaja Kristo kama Mwamba inamaanisha SELA au PETRA Kila mmoja wetu anaweza kujua ujasiri anaojisikia akiwa juu ya mwamba unapokuwa juu ya mwamba au juu ya jabali unaweza kukaa kwa ujasiri, unaweza kurukaruka na hakuna wa kukubabaisha, mwamba huwa hautikisiki, haung’oki, hauogopi dhoruba na kama mtu atashindana na mwamba atavunjika vunjika na kama mtu ataangukiwa na mwamba atasagwasagwa!

Hakuna njia nyingine yoyote ambayo kwa hiyo tunaweza kuwa salama isipokuwa kumtegemea Yesu tu mtuni wa wimbo alionyesha kuwa ni kwa Damu yake yesu tu tunaweza kuwa salama, kwake tunaweza kujificha na kuutegemea ushidni, kazi njema , na matendo mema hayawezi kutuokoa ni zawadi ya Yesu Kristo pekee aliyekufa msalabani kwaajili yetu ndio inayoweza kututhibitishia usalama wetu, kwa jambo lolote lile ni lazima tuweke tegemeo letu kwa Bwana Yesu

Tunaweza kukutana na dhuruba za aina mbalimbali zenye kuhuzunisha Magonjwa na mateso, Matatizo ya kifedha na kiuchumi, Matatizo ya kifamilia, Huzuni na kukata tamaa jambo kubwa na la msingi la kufanya ni kumwangalia Yesu ni kumtegemea ni kujificha kwake yeye ndio nguvu yetu, na kimbilio letu ndiye mwamba imara 

Yeye aliahidi kuwa atalijenga kanisa lake juu ya mwamba na wala malango ya kuzimu hayatalishinda, ushindi ni wetu kama tu tutajificha na kuutegemea Mwamba.  

Mathayo 16: 13-18Basi Yesu akaenda pande za Kaisaria-Filipi, akawauliza wanafunzi wake akasema, Watu hunena Mwana wa Adamu kuwa ni nani? Wakasema, Wengine hunena u Yohana Mbatizaji, wengine Eliya, wengine Yeremia au mmojawapo wa manabii.  Akawaambia, Nanyi mwaninena mimi kuwa ni nani?  Simoni Petro akajibu akasema, Wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai. Yesu akajibu, akamwambia, Heri wewe Simoni Bar-yona; kwa kuwa mwili na damu havikukufunulia hili, bali Baba yangu aliye mbinguni. Nami nakuambia, Wewe ndiwe Petro, na juu ya mwamba huu nitalijenga kanisa langu; wala milango ya kuzimu haitalishinda.”

Rev. Innocent Kamote
Mkuu wa Wajenzi mwenye Hekima.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni