Jumapili, 15 Oktoba 2017

Bwana Mungu wako Ndiye atakayevuka mbele yako!


Kumbukumbu 31:3-6 
 
Bwana Mungu wako, ndiye atakayevuka mbele yako, atawaangamiza mataifa haya mbele yako, nawe utawamiliki; na Yoshua atavuka mbele yako, kama Bwana alivyonena. Na Bwana atawatenda hao kama vile alivyowatenda Sihoni na Ogu, wafalme wa Waamori, na nchi yao, ambao aliwaharibu.  Naye Bwana atawatia mikononi mwenu, nanyi mtawatenda kadiri ya amri ile niliyowaamuru. Iweni hodari na moyo wa ushujaa, msiogope wala msiwahofu; kwa maana Bwana, Mungu wako, yeye ndiye anayekwenda pamoja nawe, hatakupungukia wala kukuacha.”



Utangulizi.

Hivi karibuni sasa tunaelekea ukingoni au mwishoni kabisa mwa mwaka 2017, kila mara unapofika wakati kama huu unakuwa ni wakati wa wanafunzi kukabiliwa na mitihani yao ya mwisho, mitihani hii ni moja wapo ya changamoto kwa wanafunzi wote, kwa kidato cha pilina cha nne watakuwa na mitihani yao ya mwisho, hali kadhalika na mitihani ya kitaifa, na madarasa mengine watakuwa na mitihani ya aina mbalimbali ya mwisho kwaajili ya kuwapima ili wavukekuingia darasa lingine, katika wakati kama huu wanafunzi wengi hata wale wenye uwezo huanza kuinhgia hofu kwa vile hawajui mtihani utaamua nini katika maisha yao.

Wakati huu ni wakati wa muhimu sana kwao na kwetu pia sisi walimu na shule kwa ujumla hivyo katika majira kama haya ni muhimu kila mmoja akiutafuta uso wa Mungu na kujisomea kwa bidii sana lakini hali kadhalika kuwa na neno la ushindi litakaloongoza maisha yetu wakati huu unapokaribia.

Kumbukumbu 31:3-6 Mungu anataka kututia moyo kupitia torati ya Musa kwa wana wa Israel, kuna maswala kadhaa ambayo Musa alikuwa akiwaambia Israel kama siri ya ushindi wao

1.      Bwana Mungu wako ndiye atakayevuka mbele yako, 

Kuna uwezekano wa kuwa umesoma kwa bidii, umekuwa na ratiba yako ya kujisomea na umetumia akili yako yote na hekima yako yote kujiandaa ilivyo jambo hjilo ni jema lakini inawezekana pamoja na maandalizi hayo ukawa unaogopa Biblia inatupa njia ya ushindi kwamba ni lazima tumuombe Mungu aweze kwenda pamoja nasi na kututangulia Kutoka 33:14-15 “Akasema, Uso wangu utakwenda pamoja nawe, nami nitakupa raha. Naye akamwambia, Uso wako usipokwenda pamoja nami, usituchukue kutoka hapa.” Musa alimweleza Mungu kuwa hawezi kwenda bila uso wa Mungu neno uso wa Mungu maana yake ni uwepo wa Mungu maana yake ni Kumpa Roho wa Mungu nafasi ya kukuongoza katika masomo yako na maandalizi ya mitihani yako Yohana 16:13 “Lakini yeye atakapokuja, huyo Roho wa kweli, atawaongoza awatie kwenye kweli yote; kwa maana hatanena kwa shauri lake mwenyewe, lakini yote atakayoyasikia atayanena, na mambo yajayo atawapasha habari yake.”

2.      Iweni hodari na moyo wa ushujaa, msiogope wala msiwahofu,

Neno la Mungu hapa linatutaka tusiogope linatutaka tuendelee kuwa na imani na kuweka hofu mbali Israel waliahidiwa inchi ya kanaani ambayo ndani yake ilikuwa ikikaliwa na majitu hodari, lakini Israel walipaswa kutokuwaogopa na kuwakabili na kuwashinda, wanafunzi mnaokabiliwa na mitihani, huu ni wakatoi muhimu sana kwenu, mitihani Inasimama kama majitu inasimama kama tishio la kufanikiwa katika masomo yako, Lakini unapaswa kuishinda na kufanikiwa kabisa kwaajili ya Maendeleo yako mbeleni 

Joshua 1:5-9 “Hapatakuwa mtu ye yote atakayeweza kusimama mbele yako siku zote za maisha yako; kama nilivyokuwa pamoja na Musa, ndivyo nitakavyokuwa pamoja na wewe; sitakupungukia wala sitakuacha. Uwe hodari na moyo wa ushujaa, maana ni wewe utakayewarithisha watu hawa nchi hii niliyowaapia baba zao ya kwamba nitawapa. Uwe hodari tu na ushujaa mwingi, uangalie kutenda sawasawa na sheria yote aliyokuamuru Musa mtumishi wangu; usiiache, kwenda mkono wa kuume, au wa kushoto, upate kufanikiwa sana kila uendako.Kitabu hiki cha torati kisiondoke kinywani mwako, bali yatafakari maneno yake mchana na usiku, upate kuangalia kutenda sawasawa na maneno yote yaliyoandikwa humo; maana ndipo utakapoifanikisha njia yako, kisha ndipo utakapositawi sana. Je! Si mimi niliyekuamuru? Uwe hodari na moyo wa ushujaa; usiogope wala usifadhaike; kwa kuwa Bwana, Mungu wako, yu pamoja nawe kila uendako.” 

3.      Tamka Neno la Mungu.

Tamka neno la Mungu kwa kuliamini na kwa ujasiri Yohana 6:63Roho ndiyo itiayo uzima, mwili haufai kitu; maneno hayo niliyowaambia ni roho, tena ni uzima” kumbuka kuwa hofu ni roho hivyo ili kuishinda unapaswa kuwa na ujasiri na hivyo ni muhimu kwako kuliangalia neno na kulitamka hata ndani ya moyo wako kwa ujasiri  Matendo 4:29 “Basi sasa, Bwana, yaangalie matisho yao; ukawajalie watumwa wako kunena neno lako kwa ujasiri wote,”

4.      Uwe na Moyo wa Ushujaa (Imani).

Tendo lolote lile lisilotokana na imani ni dhambi, Warumi 14:23 “Lakini aliye na shaka, kama akila, amehukumiwa kuwa ana hatia, kwa maana hakula kwa imani. Na kila tendo lisilotoka katika imani ni dhambimara tunaporuhusu mashaka katika maisha yetu ndipo ytunapoanza kuzama Mathayo 14:30-31 “Lakini alipouona upepo, akaogopa; akaanza kuzama, akapiga yowe, akisema, Bwana, niokoe. Mara Yesu akanyosha mkono wake, akamshika, akamwambia, Ewe mwenye imani haba, mbona uliona shaka?” Ni muhimu kwetu tukimuamini Mungu kwa yasiyowezekana, Luka 1:37 “kwa kuwa hakuna neno lisilowezekana kwa Mungu.” 

Kila mwanafunzi anayetarajia kufanya Mitihani hivi karibuni tafadhali omba Maombi haya pamoja na Mkuuwa wajenzi.

Mungu wa Rehema ni wewe utakayevuka mbele yangu katika nyakati hizi za mitihani, ni wewe utakayetengeneza future yangu kupitia ushindi wakati wa mitihani yangu nya mwisho na mitihani ya kitaifa najiweka katika mikono yako nikikutegemea wewe, niweke mbali na hofu zote maana wewe hukutupa roho ya woga, Nisaidie kwa Roho wako Mtakatifu na uwepo wako ukawe pamoja name katika mitihani yangu sawasawa na Mapenzi yako Katika jina la Yesu amen!  

Nakutabiria ushindi, nakutabiria mafanikio makubwa katika mitihani yako, natabiri ufaulu wa kupita kawaida katika mitihani yako ya mwaka huu katika jina la Yesu amen!

Na mkuu wa wajenzi mwenye Hekima

Rev. Innocent Kamote.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni