Jumamosi, 21 Oktoba 2017

Daudi ni Nani? Na Mwana wa Yese ni nani?


Mstari wa Msingi 1Samuel 25:10-11 “Naye Nabali akawajibu wale watumishi wa Daudi, akasema, Huyu Daudi ni nani? Na mwana wa Yese ni nani? Siku hizi kuna watumwa wengi wanaomtoroka kila mtu bwana wake! Basi mimi je! Nitwae mkate wangu, na maji yangu, na machinjo yangu niliyowachinjia hao watu wangu wakatao manyoya kondoo zangu, na kuwapa watu ambao siwajui wametoka wapi?”


Utangulizi.

Katika kifungu cha maandiko hapo juu tunajifunza habari za Daudi na Nabal ambazo kwa ujumla zimeshehemi mambo mengi sana ya kujifunza kulingana na mtazamo wa msomaji, lakini leo mmi kama mkuu wa wajenzi katika kisa hiki najifunza mfano wa watu wasio na shukurani tulio nao duniani, watu ambao wanasahau fadhili, watu ambao wanaweza kuwa na kiburi na kusahau kuwa uwepo wao umechangiwa na watu wengine pia.

Wote tunafahamu jinsi ambavyo Daudi, alivyo mtu muhimu sana na wote tunatambua jinsi alivyo maarufu sana, Daudi ndiye aliyewaokoa Israel nzima wasiwe watumwa wa wafilisti, 1Samuel 17 :8-9. Naye akasimama, akawapigia kelele majeshi ya Israeli akawaambia, Mbona mmetoka kupanga vita? Je! Mimi si Mfilisti, na ninyi si watumishi wa Sauli? Jichagulieni mtu, akanishukie mimi. Kama akiweza kupigana nami na kuniua, sisi tutakuwa watumwa wenu; nami nikimshinda yeye na kumwua, ninyi mtakuwa watumwa wetu, na kututumikia.” Kwa msingi huo Hakuna mtu aliyekuwa hatambui kuwa Daudi ni nani na nini alikifanya katika taifa la Israel nzima kwani aliwaokoa watu wote wasiwe watumwa wa Israel, na kama haitoshi Maalumu sana kwa mtu anayeitwa Nabali Daudi alimtendea mema binafsi kwa kulinda mifugo yake na wachungaji wake.

Wakati Daudi aliposikia kuwa Nabali mtu aliyekuwa mkubwa sana na tajiri anakata manyoya kondoo aliomba chakula, huku akimkumbusha namna na jinsi alivyomtendea mema lakini kwa jeuri kubwa  Nabali alimpuuza Daudi na nyumba ya Baba yake, Daudi ni nani na Mwana wa Yese ni nani?, lugha hii ilikuwa lugha ya zarau kubwa yenye matusi makubwa lakini kama aitoshi Nabali alimtukana Daudi kuwa ni mkimbizi tu, amemkimbia Bwana wake, aliwakuza watumwa wake na kuwaona ni wa muhimu sana kuliko Daudi aliyeokoa taifa zima Jambo hili lilimuudhi sana Daudi na Mungu pia, Hivyo daudi alikusudia kumuua Nabali na ukoo wake wote kutokana na Kauli mbaya na maneno yasiyofaa kwa Daudi.

1Samuel 25:2-17 “Na huko Maoni kulikuwa na mtu mmoja, ambaye alikuwa na mali yake katika Karmeli; naye yule mtu alikuwa mkuu sana, mwenye kondoo elfu tatu na mbuzi elfu; naye alikuwa akiwakata manyoya kondoo zake huko Karmeli. Na jina la mtu huyo aliitwa Nabali; na jina la mkewe aliitwa Abigaili, na huyo mwanamke alikuwa mwenye akili njema, mzuri wa uso; bali yule mwanamume alikuwa hana adabu, tena mwovu katika matendo yake; naye alikuwa wa mbari ya Kalebu. Basi Daudi akasikia huko nyikani ya kuwa Nabali alikuwa katika kuwakata manyoya kondoo zake. Daudi akatuma vijana kumi, Daudi naye akawaambia hao vijana, Kweeni mwende Karmeli, na kumwendea huyu Nabali ili mnisalimie; na hivi ndivyo mtakavyomwambia huyu aishiye salama, Amani na iwe kwako, na amani nyumbani mwako, na amani kwao wote ulio nao. Nami sasa nimesikia ya kuwa una watu wanaokata manyoya kondoo zako; haya! Wachungaji wako wamekuwa pamoja nasi, wala hatukuwadhuru, wala hawakukosa kitu wakati wote walipokuwako huko Karmeli. Waulize vijana wako, nao watakuambia; basi na wakubaliwe vijana hawa machoni pako; maana tumekujia katika siku ya heri; uwape, nakusihi, cho chote kitakachokujia mkononi, uwape watumwa wako na mwanao Daudi. Basi walipofika vijana wake Daudi, wakamwambia Nabali sawasawa na maneno hayo yote kwa jina la Daudi, kisha wakanyamaza. Naye Nabali akawajibu wale watumishi wa Daudi, akasema, Huyu Daudi ni nani? Na mwana wa Yese ni nani? Siku hizi kuna watumwa wengi wanaomtoroka kila mtu bwana wake! Basi mimi je! Nitwae mkate wangu, na maji yangu, na machinjo yangu niliyowachinjia hao watu wangu wakatao manyoya kondoo zangu, na kuwapa watu ambao siwajui wametoka wapi? Basi vijana wake Daudi wakageuka, wakaenda zao, wakarudi, nao wakaja wakamwambia sawasawa na maneno hayo yote. Kisha Daudi akawaambia watu wake, Haya! Jifungeni kila mtu upanga wake. Nao wakajifunga kila mtu upanga wake; Daudi naye akajifunga upanga wake; nao wakapanda nyuma yake Daudi, wapata kama watu mia nne; na watu mia mbili wakakaa na vyombo vyao. Lakini kijana mmojawapo alimpasha habari Abigaili, mkewe Nabali, kasema, Tazama, Daudi alituma wajumbe kutoka nyikani waje ili kumsalimu bwana wetu, naye akawatukana. Walakini watu hawa walitutendea mema sana, wala hatukupata dhara, wala sisi hatukupotewa na kitu cho chote, wakati wote tulipofuatana nao, tulipokuwako mavueni; watu hao walikuwa boma kwetu usiku na mchana, wakati wote tulipokuwa nao tukiwachunga kondoo. Basi sasa ujue na kufikiri utakayotenda; kwa sababu yamekusudiwa mabaya juu ya bwana wetu, na juu ya nyumba yake yote; kwa kuwa yeye ni mtu asiyefaa kabisa, hata mtu hawezi kusema naye.”

Unaweza kuona jinsi Nabali alivyoweza kupuuzia mambo yote mema aliyokuwa ametendewa na Daudi kitaifa na kwa binafsi na badala yake alilipa mabaya na kumtukana Daudi. Hivi ndivyo ilivyo kwa watu wengi sana ambao tunaweza kuwatendea mema lakini wao wakatulipa maovu.

Mfano

Mtu mmoja wa makamo alipata bahati mbaya akapotea njia walipokuwa msituni na rafiki zake, Yeye na rafiki zake walikuwa katika safari  ya kuvunjari msituni, baada ya chakula cha mchana aliamua kutembea kidogo, Rafiki zake walimuonya kwammba asiende ndani sana msituni asije akapotelea nyikani, ingawa hakujali ushauri wa rafiki zake.

Msitu ulikuwa mzuri na wenye kuvutia, licha ya kuonywa kuwa asiende mbali alipotelea msituni, alijaribu kurudi lakini hakuona njia wala pa kutokea  na alianza kuogopa, Mara alianza kusikia sauti ya Simba akiunguruma na sauti hiyo ilimuogopesha sana, alitambua kuwa ni sauti ya simba, lakini wakati huo hakumuona simba,

Aliamua kutimua mbio ili kuokoa maisha yake na hatimaye alimuoina simba akimkaribia, kwa haraka na kwa hofu alikimbia na kupanda juu ya mti na kujibanza katika tawi mojawapo la mti ule na kutulia vema,alijishangaa hata namna alivyoupanda ule mti, alipoangalia pembeni ya mti ule aliona sokwe mkubwa akiwa amelala kwenye tawi lingine.

Simba alifika na kuona mti, sokwe na binadamu, simba alimwambia sokwe msukume chini huyu mwanadamu nimle mana nina njaa mbaya!,  Sokwe kwa upole alijibu kwa unyenyekevu mti huu ni wangu na  mtu huyu amekimbilia hapa kuokoa maisha yake hivyo siwezi, kumuacha afe wala aanguke na aliposikia maneno hayo mwanadamu yule alijisikia furaha sana.

Simba alinyamaza kimya kwa muda kisha alimwambia mwanadamu tafadhali msukume sokwe chini nam nitakuacha wewe, Jamaa bila kufikiri hata kwa dakika moja alimsukuma sokwe chini, ingawa kwa uhodari mkubwa sokwe alirukia tawi lingine la juu zaidi na kuokoa maisha yake.

Simba alicheka sana na kisha akaondoka zake.

Mtu yule aliona aibu kwani ukweli ni kuwa sokwe alikuwa ameokoa maisha yake kutoka katika mikono ya simaba hatari, lakini yeye alijaribu kumsukuma chini, ni muhimu kuwa kama sokwe kwa kuwasaidia wengine na kamwe tusiwe kama mtu yule mbaya.

Hivi ndivyo ilivyo kwa watu wengi, Hawana shukurani, unawakaribisha, unawapokea wewe mwenyewe lakini kesho wakifanikiwa wewe unahesabika kuwa sio kitu, nimara nyingi sana hata walimu wamewasaidia sana wanafunzi wametunza maisha yao miaka miwili, mitatu au minne lakini unaweza kushangaa wanafunzi wakilipa dharau kwa walimu, wakiwavunjia heshima, wengine wamewapuuzia hata wazazi wao waliowalea na kadhalika.

Tabia ya mwanadamu huyu na tabia ya Nabali hazitofautiani sana Mungu hakupendezwa na Nabali kwani baada ya siku kumi tu Nabali alifariki, ingawa daudi hakumuua, lakini Mungu alimtetea Daudi na kumlipa Nabali sawasawa na matusi yake

1Samuel 25:36-39 “Kisha Abigaili alimjia Nabali; na tazama, alikuwa amefanya karamu nyumbani mwake, kama karamu ya kifalme; na moyo wake huyo Nabali ukafurahiwa ndani yake, kwa maana amelewa kabisa. Kwa sababu hiyo hakumwambia neno, dogo wala kubwa, hata kulipopambazuka. Ikawa asubuhi, divai ilipokuwa imemtoka Nabali, mkewe alimwambia mambo hayo, na moyo wake ukafa ndani yake, akawa kama jiwe. Tena ikawa, yapata siku kumi baadaye, Bwana alimpiga huyo Nabali, hata akafa. Naye aliposikia ya kwamba Nabali amekufa, Daudi alisema, Na ahimidiwe Bwana ambaye amenitetea teto la shutumu langu mkononi mwa Nabali, na kumzuia mtumwa wake asitende maovu; tena uovu wake Nabali Bwana amemrudishia juu ya kichwa chake mwenyewe. Kisha Daudi akatuma watu, akamposa Abigaili ili amwoe

Bwana na ampe neema kila mmoja wetu kuwa na moyo wa shukurani na kutokuwalipa mabaya wale wanaotutendea mema, iweni watu wa shukurani na kuwalipa mema wanaotutendea wema” 
          
Na mkuu wa wajenzi mwenye Hekima.

Rev. Innocent Kamote.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni