Ijumaa, 19 Aprili 2019

Mwondoshe huyu, utufungulie Baraba.!


Luka 23:18-25Wakapiga kelele wote pamoja, wakisema, Mwondoe huyu, utufungulie Baraba.  Naye ni mtu aliyetupwa gerezani kwa ajili ya fitina iliyotokea mjini, na kwa uuaji Basi Pilato alisema nao mara ya pili, kwa vile alivyotaka kumfungua Yesu.  Lakini wakapiga kelele, wakisema, Msulibishe. Msulibishe. Akawaambia mara ya tatu, Kwa sababu gani? Huyu ametenda uovu gani? Sikuona kwake hata neno lipasalo kufa. Basi nikiisha kumrudi nitamfungua. Lakini wakatoa sauti zao kwa nguvu sana, wakitaka asulibiwe. Sauti zao zikashinda. Pilato akahukumu kwamba haja yao ifanyike. Akamfungua yule aliyetupwa gerezani kwa ajili ya fitina na uuaji, yule waliyemtaka, akamtoa Yesu wamfanyie watakavyo”.


Utangulizi:
Moja ya mambo ya kuyatafakari na kujiuliza kwa kina hususani katika wakati huu wa Pasaka ni pamoja na tabia ya wanadamu ambayo ni tabia ya kushangaza sana, tabia hii ngumu kuelezeka kwamba inatokana na woga, kutokujiamini, saikolojia ya mkumbo, kushindwa kusimama katika kweli, unafiki, au namna gani, hii ni ile tabia yetu ya kung’angania vitu vibaya, viovu na vyenye kuleta shida katika maisha yetu na kupoteza vitu vyema vizuri na vyenye thamani au vyenye kuleta ukombozi kutoka katika changamoto tulizonazo, Mwondoshe huyu, utufungulie Baraba! Haya yalikuwa maneno ya watu wote siku Mwokozi wa ulimwengu huu alipohukumiwa kusulubiwa kwa kura za wanadamu ambao kwa nia moja walitaka asulubiwe na mtu mhalifu zaidi aweze kuachwa huru!

Nani maarufu kati ya Yesu na Baraba?

Wote tunaweza kukubaliana wazi kuwa kifo cha Yesu Msalabani kilikuwa kina kusudi la Mungu nyuma yake, ilikuwa ni lazima Yesu asulubiwe ili mimi na wewe tuokolewe kutoka katika adhabu ya dhambi zetu sio mimi na wewe tu bali na hata watu waovu labda huenda kuliko mimi na wewe kama ilivyokuwa kwa Baraba

Kinachonishangaza hapa na amabachoi nataka kukijadili kwa kina ni sababu gani inapelekea watu wampuuzie Yesu kwa kiwango hata cha kutokutaja jina lake, na wakati huo huo wamchague mtu mhaini na muuaji Baraba kwamba awe huru huku akitajwa kwa jina lakini Yesu akitajwa kama huyu? Je wadhani Yesu na baraba ni nani alikuwa maarufu zaidi?

Biblia au neno la Mungu linatueleza wazi kuwa Yesu Kristo ndiye alikuwa mtu maarufu zaidi katika karne yake kuliko mtu awaye yote, Yeye aliandamwa na maelfu ya watu kila alikokwenda ili waponywe magonjwa yao na kusikiliza hekima yake na mafundisho yake na wengine wakitaka tu kumuona, nataka nikuwekee wazi kabisa kuwa haikuwa jambo rahisi kuweza kumfikia Yesu hata kwa karibu, Bibliainaeleza kuwa watu walipanda hata juu ya miti ili angalau waweze kumuona

Luka 19:2-4Na tazama, palikuwa na mtu, jina lake Zakayo, mkubwa mmoja katika watoza ushuru, naye ni tajiri. Huyu alikuwa akitafuta kumwona Yesu ni mtu wa namna gani, asiweze kwa sababu ya umati wa watu, maana ni mfupi wa kimo.  Akatangulia mbio, akapanda juu ya mkuyu apate kumwona, kwa kuwa atakuja kuipitia njia ile” unaweza kuona Biblia inaeleza kuwa huyu alikuwa mtu mkubwa, tena alikuwa tajiri nyakati za leo tungeweza kumfananisha mtu huyu kama alikuwa waziri wa fedha hivi, alitamani kumuona Yesu lakini ilikuwa ni ngumu sana, maelfu ya watu walikuwa wakimzingira Yesu pande zote alikuwa maarufu Yesu kuliko mtu yeyote,


Luka 5:19Hata walipokosa nafasi ya kumpeleka ndani kwa ajili ya lile kundi la watu, walipanda juu ya dari wakampisha katika matofali ya juu, wakamshusha yeye na kitanda chake katikati mbele ya Yesu.” Wako watu walikosa nafasi ya kumuona Yesu kiasi ambacho walitoboa dari ya nyumba ili angalau waweze kufikisha mgonjwa wao kutokana na Yesu kuzungukwa na umati mkubwa wa watu, Yesu alikuwamaarufu kuliko mtu awaye yote, wewena mimi hata tukipanda daladala hakuna hata mtu mmoja anashituka au kugeuka kukuangalia, kondakta anaweza hata kukuamboa brother adjust tuikae watano watano hapo kati, Hii haikuwa hivyo kwa Yesu alijulikana mno, Biblia imejaa mifano mingi na habari nyingi kuhusu Yesu kuzingirwa na umati wa watu wakihitaji huduma kutoka kwake.

Watu walimzunguka Yesu kiasi ambacho yeye na wanafunzi wake walikosa hata nafasi ya kula Marko 3:20Mkutano wakakusanyika tena, hata wao wenyewe wasiweze hata kula mkate.”
Yesu alizungukwa na watu pande zote wakati mwingine alilazimika kukaa katika chombo cha majini ili kila mmoja aweze kumuona alipokuwa akifundisha Marko 4:1Akaanza kufundisha tena kando ya bahari. Wakamkusanyikia mkutano mkubwa mno, hata yeye akapanda chomboni, akakaa baharini, mkutano wote ulikuwako juu ya nchi kavu kando ya bahari.
Yesu hata aliposafiri aliandamwa sio tu na wanafunzi wake lakini biblia inasema umati mkubwa wa watu walifuatana pamoja naye Luka 7:11 “Baadaye kidogo alikwenda mpaka mji mmoja uitwao Naini, na wanafunzi wake walifuatana naye pamoja na mkutano mkubwa”.
Yesu ndiye mtu pekee ambaye hata Mama yake na ndugu zake walipotaka kumuona walipata taabu saba kufikia kutokana na kuzongwazongwa na watu Luka 8:19 “Wakamwendea mama yake na ndugu zake, wasiweze kumkaribia kwa sababu ya mkutano.”
Yesu ndiye kiongozi pekee ambaye maelfu ya watu walikusanyika pamoja ili kumuona, alikuwa na mvuto mkubwa kiasi ambacho watu waliweza kukanyagana Luka 12:1a. “Wakati huo, makutano walipokutanika elfu elfu, hata wakakanyagana,aidha maandiko yanaeleza wazi kuwa umati mkubwa wa watu ulimfuata kila mahali alikokwenda watu walitoka uyahudi, Yerusalem, Idumeya, Yordani, Tiro na hata Sidoni yaani sehemu za Lebanon ya leo, wengine wakimfuata kutoka Galilaya

Marko 3:7-10 “Naye Yesu akajitenga, yeye na wanafunzi wake, akaenda baharini. Mkutano mkuu ukamfuata, kutoka Galilaya, na Uyahudi, na Yerusalemu, na Idumaya, na ng'ambo ya Yordani, na pande za Tiro na Sidoni, mkutano mkuu, waliposikia habari za mambo yote aliyokuwa akiyatenda, wakamwendea. Akawaambia wanafunzi wake ya kwamba chombo kidogo kikae karibu naye, kwa sababu ya mkutano, wasije wakamsonga. Maana aliponya wengi, hata wote waliokuwa na misiba wakamrukia wapate kumgusa.”
Luka 9:12 “Na jua likaanza kushuka; wakamwendea wale Thenashara, wakamwambia, Uage mkutano, ili waende katika vijiji na mashamba ya kandokando wapate mahali pa kulala na vyakula, maana hapa tulipo ni nyika tupu”.  Yesu aliandamwa na umati mkubwa wa watu ambao walikuwa hawataki kumuachia kundi hili kubwa sana la watu walishuhudia miujiza ya ajabu ya kihistoria walishuhudia pia wakilishwa mikate na Yesu kiasi cha kushibisha biblia inataka kuwa wanaume 5000 walilishwa bila kuhesabu wanawake na watoto, vilema waliponywa, vipofu walifunguliwa, pepo walitolewa, wafu walifufuliwa na miujiza mingine mingi ya kuwahudumia watu      Biblia inaeleza kuwa Nafasi isingeliweza kutosha kuelezea kila alilolifanya Yesu Yohana 21:25 “Kuna na mambo mengi aliyoyafanya Yesu; ambayo yakiandikwa moja moja, nadhani hata ulimwengu usingetosha kwa vile vitabu vitakavyoandikwa.”
Yesu aliwaponya wote walikuwa wanaumwa Mathayo 12:15, Alipowaona umati mkubwa wa watu waliokuwa kama kondoo wasio na Mchungaji aliwahurumia Mathayo 14:14 na umati mkubwa wa watu walimfuata kwa sababu waliona miujiza na ishara na jinsi alivyoponya wagonjwa Luka 19:37 lakini kama haiztoshi umati mkubwa sana ulikuwa pamoja naye alipomfufua lazaro Yohana 12:17  
Unaweza kupata picha na ushahidi wa kimaandiko namna na jinsi Yesu alivyokuwa mtu muhimu sana katika jamii, yeye hakuwa muhalifu, alizunguka huko na huko akiwahudumia watu na kuwahurumia na kuwaponya yeye alikuwa mwema sana katika maisha yao.

Kwa nini makutano walimchagua Baraba?

Swali linakuja sasa kwa nini Pilato alipowataka watu wayahudi hadharani kuchagua Mfungwa mmojawapo kati ya Yesu  mtenda miujiza na Baraba  muuaji watu walichagua tusichikidhani? Mbona ni kama jibu lilikuwa wazi sana lakini eti watu walijibu tena bila ya kumtaja jina Bwana Yesu kana kwamba hakuwa na faida yoyote kwao? Muondoshe huyu, tufungulie Baraba,
Uchaguzi huu wa watu unatuthibitishia wazi kuwa wakati huu Yesu hakuhesabika kuwa ni wa thamani kabisa, na alidharaulika na kutokuonekana kuwa kitu kwamkiwango ambacho baraba alionekana kuwa wa muhimu, umuhimu wa Yesu na Baraba kwa jamii ulikuwa na tofauti kubwa sana, wayahudi na jamii ya watu waliokuwepo sio tu kuwa walipiga kelele kuwa waachiwe Baraba lakini pia walionyesha wazi kuwa wanchukizwa na hawampendi kabisa Yesu Luka 23:23 inasema wazi kabisa kuwa walipiga kelele kwa nia moja wakisema Msulubishee msulubishee, hii inaonyesha wazi kuwa watu hawakuwa wamevutiwa na Yesu wala kazi zake
Hali halisi iliyokuwepo inaweza kukutoa Machozi kama tungekuwepo na sisi pale, tukiacha ujuzi kuwa Mungu alikuwa kazini kuwaokoa wanadamu na kuwafia wenye dhambi baraba akiwa mmoja wao, Lakini tujiulize je walikuwa wapi wale ambao kwa dhati kabisa walitemntewa mema na Yesu live? Liko wapi lile kundi lililokuwa likimfuata? Wako wapi wale waliokula mikate wakashiba na kutaka kumfanya kuwa mfalme?, je walishindwa kusema muachie Yesu kwa sababu mimi nilikuwa kipofu na sasa kwaajili yake ninaona? Wako wapi walemavu walioponywa? Wako wapi waliotolewa Pepo?, wako wapi walioponywa magonjwa yao? Wako wapi maakida ambao Yesu aliwaponya watumwa wao, yuko wapi mwanamke aliyekuwa akitokwa na damu na Yesu akamponya, yuko wapi Zakayo aliyetembelewa na Yesu Nyumbani kwake, yuko wapi Lazaro angeweza kusema mimi nilikuwa maiti siku nne huyu jamaa akanifufua, wako wapi wale waliomshangilia siku ya mitende na kutandaza nguo zao njiani na kuimba Hosana mwana wa Daudi?, yuko wapi yule aliyetolewa Jeshi kubwa la mapepo, wako wapi watu kutoka Galilaya, Yerusalemu, Dekapoli, Yudea, Tiro na Sidoni, Kama Yesu alikuwa akizxungukwa na watu mpaka anakosa nafasi ya kula ilikuwaje siku hii?
Hakuna mtu aliyemfikiri Yesu kuwa ni wa muhimu kwa wakati huu, Muimbaji mmoja wa kitanzania aliyeitwa Patric Balisidya aliimba akisema “ni mashaka ya hangaiko wema hawana maisha” akiwataja watu wema ambao walikuwa wema kwa watu wao lakini hata hivyo waliuawa dunia imejawa na chuki na wivu na ndiyo yaliyoipamba dunia, wema wamepakwa majivu wala hawaonekani, je itakuwaje kizazimkile wakifufuka na kuona leo Majengo makubwa yakiwa yamejengwa na watu wakimuabudu Yesu, au wakiona watu waliokuwa waovu kuliko baraba wakiwa wamebadilishwa kabisa kitabia wangesemaje? Wangesema wao walikuwepo na kuwa sisi leo tumechagua vibaya?

Mwondoshe huyu, utufungulie Baraba.!

Swali bado linabaki kwa nini umati huu haukumtetea Yesu, ukiachilia zile sababu za kiroho kuwa ni ili mapenzi ya Mungu ya kuwaokoa wenye dhambi yaweze kutimizwa? Kuna ukweli ulio wazi kibiblia kwamba chuki hii ilipandwa, chuki hii ilikuwa ni mbegu iliyopandwa kutoka kwa viongozi wa dini, chuki ni mbegu mbaya, mbegu mbaya kwa kawaida hustawi haraka na kwa nguvu zaidi kiasi cha kuweza kuharibu jamii, ilichukua muda mfupi sana wanyarwanda kuuana kwa mamia na maelfu kwa sababu tu mbegu ya chuki ilipandwa, mbeguu hii ya chuki ilipandwa na adui ilipandwa na shetani kupitia viongozi wa kidini  biblia inaweka wazi kuwa wao ndio waliowashawishi makutano  wamchague baraba Mathayo 27:20 biblia inasema “ Nao wakuu wa makuhani na wazee WAKAWASHAWISHI makutano ili wamtake Baraba, na kumwangamiza Yesu.”  Unaweza kuona pia katika Marko 15:11Lakini wakuu wa makuhani WAKAWATAHARAKISHA makutano, kwamba afadhali awafungulie Baraba.
Maandiko yanaonyesha kuwa chuki dhidi ya Yesu ilipandwa tu, ilikuwa ni mbegu kutoka kwa shetani, ilipandikizwa dhidi ya Yesu viongozi hawa wa dini walikuwa ni maadui wa Yesu, walipinga kila alichokuwa akikifanya, walipanga mipango ya kumuua, walitafuta makosa hata ya kutunga kwaajili yake, walitaharakisha na kuwachochea makutano wachague lililo ovu, wakati wote tunapoona watu wakitenda maovu ni lazima uelewe kuwa kuna mchochezi, alisema Sulemani kuwa moto hauwezi kuwaka pasipo kuchochewa kwa kuni, Mungu alikuwa amewapiga upofu kuchagua uovu na kukataa wema Yesu alikuwa amekwisha kuwaonya mbeleni kuwa ikiwa wameutendea vile mti mbichi itakuwaje kwa mti mbichi?
Inasikitisha kuwa watu waliacha kumuamini Yesu na waamini uongo, waliacha kumuamini mtenda miujiza wakaamini viogozi vipofu wa kidini, Mbegu ya chuki inapoingia katika eneo lolote lile hata kutaja jina lako inakuwa shida Yesu sasa anatajwa kama “huyu” mwondoshe huyu! Tufungulie Baraba
Ni wazi kabisa hata katika jamii leo watu wanaamua kuchagua njia mbovu na kuacha kuacha njia njema, leo ukisimama kupinga uovu na kuwashauri watu wema unaonakana kama adui,watu wenye akili leo na walioendelea wanapiga kura kuchagua uovu na kupitisha uovu huku wakiwa na majina yanayoashiria kuwa wao ni wa upande wa Mungu?  Katika wakati huu wa pasaka ni muhimu kila moja kujiuliza nani aondoshwe na nani afunguliwe! Nakushauri muondoshe Baraba katika maisha yako na mfungulie Yesu kristo mlango katika moyo wako
Yeye aliahidi kuwa anagonja na mtu akifungua ataingia kwake na kukaa naye Pasaka hii mkaribishe Yesu na mfukuze baraba katika maisha yako, usikubali kuangalia umati wa watu wanasemaje na wana maoni gani wewe simama umtetee Yesu hadharani.
Rev. Innocent Kamote
Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni