Jumatano, 10 Julai 2019

Walioalikwa Harusini wawezaje kuomboleza



Mathayo 9:14-15Wakati ule wanafunzi wake Yohana wakamwendea, wakasema, Kwa nini sisi na Mafarisayo twafunga, bali wanafunzi wako hawafungi? Yesu akawaambia, Walioalikwa arusini wawezaje kuomboleza, muda bwana arusi akiwapo pamoja nao? Lakini siku zitakuja watakapoondolewa bwana arusi; ndipo watakapofunga.

  

Utangulizi:

Wanafunzi wa Yohana Mbatizaji walikuwa miongoni mwa watu waliopendezwa sana na kuvutiwa na utendaji  na mafundisho ya Yesu Kristo, Licha ya Yohana Mbatizaji kuwa nabii mwenye nguvu na kuheshimika sana,ambaye kazi yake kubwa ilikuwa ni kuandaa njia kwaajili ya Masihi, wanafunzi wake vile vile walivutiwa kumsikiliza Yesu, huenda nao pia walitaka kulinganisha kweli kadhaa kuhusu mafundisho ya Yesu na yale ya mwalimu wao wa kwanza Yohana Mbatizaji.

Yohana mbatizaji alikuwa amewafundisha watu wake kufunga, hili ni moja ya somo muhimu sana la wakati wote tuwapo Duniani, Yesu hajawahi kulikataaa somo kuhusu kufunga hata na yeye alisisitiza sana watu wafunge, Yesu mwenyewe kabla ya huduma alifunga siku 40, kufunga ni muhimu sana, Katika hutuba yake ya Mlimani Yesu alikazia sana juu ya kufunga na tena alitaka kufunga kwa wanafunzi wake kuwe ni zaidi ya kufunga kwa Mafarisayo akithibitisha kuwa baba anaona sirini na kujalia kile ambacho mfungaji amekikusudia, Mungu atatupa thawabu tufungapo sawa na maelekezo ya Yesu


Mathayo 6:16-18
Tena mfungapo, msiwe kama wanafiki wenye uso wa kukunjamana; maana hujiumbua nyuso zao, ili waonekane na watu kuwa wanafunga. Amin, nawaambia, wamekwisha kupata thawabu yao. Bali wewe ufungapo, jipake mafuta kichwani, unawe uso; ili usionekane na watu kuwa unafunga, ila na Baba yako aliye sirini; na Baba yako aonaye sirini atakujazi” Swali kubwa la wanafunzi wa Yohana Mbatizaji ilikuwa mbona sisi na Mafarisayo tunafunza lakini wanafunzi wako hawafungi? Jibu la Yesu ndilo linalotupa somo kuu katika siku ya leo;-

Yesu alijibu walioalikwa Harusini wawezaje Kuomboleza?

Kwa mujibu wa tamaduni za kiyahudi mtu alipooa, waliooana walitakiwa kukaa nyumbani kwa mapumziko, walitakiwa kuwa kama Mfalme na Malkia, walihudumiwa na watu maalumu, waliokuwa na majina maalumu, walioitwa wana wa chumba cha harusi, walihudumia watu kwa furaha wiki nzima watu wakifurahi na kula na kunywa vyakula vya aina mbalimbali, ulikuwa ni wakati wa furaha kwa tamaduni za Israel.

Katika desturi za kinabii manabii wengi walitabiri kuja kwa Masihi, ujio wake ulifananishwa na ujiio wa bwana harusi kila mmoja alijua kuwa siku za faraja na furaha zinakuja na Masihi mkuu atakapokuja

Isaya 54:4-6
Usiogope; maana hutatahayarika; wala usifadhaike; maana hutaaibishwa; kwa kuwa utaisahau aibu ya ujana wako, pia mashutumu ya ujane wako hutayakumbuka tena. Kwa sababu Muumba wako ni mume wako; Bwana wa majeshi ndilo jina lake; na Mtakatifu wa Israeli ndiye Mkombozi wako; Yeye ataitwa Mungu wa dunia yote. Maana Bwana amekuita kama mke aliyeachwa na kuhuzunishwa rohoni, kama mke wakati wa ujana, atupwapo, asema Mungu wako”. Unaweza pia kuona katika

Isaya 62:4-5Hutaitwa tena Aliyeachwa, wala nchi yako haitaitwa tena, Ukiwa; bali utaitwa Hefsiba; na nchi yako Beula;kwa kuwa Bwana anakufurahia ,na nchi yako itaolewa.Maana kama vile kijana amwoavyo mwanamwali, ndivyo wana wako watakavyokuoa wewe; na kama vile bwana arusi amfurahiavyo bibi arusi, ndivyo Mungu wako atakavyokufurahia wewe”.

       
Kwa hiyo wataalamu wa maandiko wa Kiyahudi walikuwa wanajua wazi kuwa Bwana harusi anayetajwa na kutabiriwa katika maandiko hayo ni Masihi, hivyo walikuwa wakimsubiri, Majibu ya Yesu kwa wanafunzi wa Yohana Mbatizaji yalitaka mioyo yao ifunguliwe waelewe kuwa Yeye ndio Masihi, na kwa sababu hiyo anapokuwepo Masihi yaani kwanini watu wasifurahi, kimsingi Yesu hakukataza watu wasifunge, Lakini funga yetu haiwezi kuwa funga ya maombolezo kama watu wasio na matumaini, haipaswi kuwa ya kujivika magunia na kujipaka Majivu, na kulia kama watu waliokata tamaa, hii ilikuwa funga yenye mtazamo wa agano la kale, sisi kwetu kufunga ni ibada

Matendo 13:1-21
. “Na huko Antiokia katika kanisa lililokuwako palikuwa na manabii na waalimu, nao ni Barnaba, na Simeoni aitwaye Nigeri, na Lukio Mkirene, na Manaeni aliyekuwa ndugu wa kunyonya wa mfalme Herode, na Sauli. Basi hawa walipokuwa wakimfanyia Bwana ibada na kufunga, Roho Mtakatifu akasema, Nitengeeni Barnaba na Sauli kwa kazi ile niliyowaitia

Yesu anataka watu wake wamfanyie ibada sii maombolezo unafunga huku uko smart unatabasamu, unaoga unajipaka mafuta na kupendeza na kwa siri wala si kwa namna ya mafarisayo walikuwa wanafanya, Kimsingi Yesu ni ukamilifu wa Furaha.

Alipo Yesu maana yake Mungu yupo, ukiwa naye maana yake uwepo wa Mungu upo, Yaani inakuwaje mtu awe katika uwepo wa Mungu kisha awe anaomboleza? Popote Yesu alipo haiwezekani kuwe na matanga, Haiwezekani mtu aalikwe Harusini au aje kwenye Karamu amefunga uwepo wa Mungu katika maisha yetu ni wa muhimu sana, Hakuna jambo tamu duniani akama kukaa katika uwepo wa Mungu, Ni furaha kuwa katika uwepo wa Mungu, Kufunga katika agano la kale kulimaanisha kupoteza matumaini, kukumbwa na huzuni, kuomboleza, kuwa na huzuni kwa sababu ya dhambi na kuharibika kwa dunia, kwa sababu ya kutengwa mbali na Mungu, kwa sababu ya majanga, kwa sababu ya kupoteza matumaini hivyo waliofunga katika agano la kale walikuwa katika mtazamo wa kuhuzunika wakihitaji msaada wa Munhgu aweze kuingilia kati, kuwa na Yesu kuwa na uwepo wa Mungu kutakufanya usiwe na huzuni, Alipo Yesu ni Harusi na sio matanga.

Mahali alipo Bwana Yesu ni furaha na amani, Hakuna huzuni ambayo Yesu anashindwa kushughulika nayo, naweza kusema kuwa tafuteni kwa bidii kuwa na uwepo wa Mungu na mengine yote yatashughulikiwa, Masihi alitarajiwa katika Israel kama Bwana harusi ambaye angeondoa huzuni za watu waliokata tamaa, angeweza kujibu kila aina ya changamoto ambazo watu wangekutana nazo, kama kuna jambo kubwa tunapaswa kulifurahia ni kuwa na huyu Bwana mkubwa na kutunza uwepo wake, Yeye ni tabibu kwa wasio na afya,ni mfariji kwa wenye huzuni, ni kicheko kwa wanaolia, ni majibu kwa wenye maswali, ni furaha kwa wenye huzuni, ni harusi kwa wanaoomboleza, anaweza kubadili msiba kuwa harusi, anaweza kubadili matarajio ya ya adui zako wanaofikiri umekwisha wanashangaa unainuliwa.

Watu wa ulimwengu wakikusumbua usihuzunike wewe umealikwa harusini wawezaje kuomboleza? Tembea kifua mbele, acha unyonge ni wakati wa kuinjoy, ni wakati wa kufurahia; furahi pamoja na bwana harusi, achana na mambo yaliyokwisha kupita alika na wengine harusini , watu wale na kunywa. Wewe unaye Yesu unaye Bwana harusi maombolezo ni ya nini, yeye ana majibu yote ya misiba yako, jiving nguo za harusi, ukiwa na Yesu acha kulia changamka, ahaaa haiwezekani uomboleze ili hali umealikwa harusini, haiwezekani ujipake majivu, haiwezekani uvae nguo za maombolezo ili hali mwana wa seremala anaoa, na wewe ni mgeni wa Bwana harusi, Nasema hivi changamka huzuni yako lazima ibadilike kuwa furaha , msiba wako lazima ugeuke kuwa harusi, huzuni yako lazima igeuke kuwa kicheko kwa sababu Mwana wa seremala amenituma nikukumbushe kuwa uwepo wake ni wa thamani kubwa sana kaa uweponi mwake hapa ndipo penye kilele cha furaha, ukiondoka uweponi mwake umerejea kwenye maombolezo, ndio maana mimi nimekusudia nitaandamana na Yesu, nitamfuata Yesu, nitamshika Yesu, nitamuhubiri Yesu, sitajali watru wananena nini juu yangu, ama wanahistoria gani kunihusu mimi najua neno moja tu niko uweponi mwake wala sitaondoshwa, nina kadi nimealikwa rasmi na Bwana Yesu nikionyesha kadi yangu hakuna wa kunizuia mlangoni nina kibali chake naungana naye kusheherekea, ni wakati wa kufurahi huwezi kunichinganisha na Bwana harusi,best mana wake ni Yihana mbatizaji ahaaaaaa Yeye alithibitisha wazi kuwa Yesu ndiye Bwana harusi mwenyewe

Yohana 3:27-30 “Yohana akajibu, akasema, Hawezi mtu kupokea neno lo lote isipokuwa amepewa kutoka mbinguni. Ninyi wenyewe mwanishuhudia ya kwamba nalisema, Mimi siye Kristo, bali nimetumwa mbele yake. Aliye naye bibi arusi ndiye bwana arusi; lakini rafiki yake bwana arusi, yeye anayesimama na kumsikia, aifurahia sana sauti yake bwana arusi. Basi hii furaha yangu imetimia. Yeye hana budi kuzidi, bali mimi kupungua

Alipo Yesu ni Harusi na sio Matanga!
Na mkuu wa wajenzi mwenye Hekima
Rev. Innocent Kamote.

Endapo umebarikiwa na Ujumbe huu tafadhali uisiste kunijulisha kwa ujumbe au Kwa whatsApp kwa namba 0718990796

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni