Jumamosi, 18 Aprili 2020

Wenye haki ni wajasiri kama simba !

Mithali 28:1 "Waovu hukimbia wasipofuatiwa na mtu; Bali wenye haki ni wajasiri kama simba."

Ufunuo 5:1-5Kisha nikaona katika mkono wa kuume wake yeye aliyeketi juu ya kile kiti cha enzi kitabu kilichoandikwa ndani na nyuma, kimetiwa muhuri saba. Nikaona malaika mwenye nguvu akihubiri kwa sauti kuu, N'nani astahiliye kukifungua kitabu, na kuzivunja muhuri zake? Wala hapakuwa na mtu mbinguni, wala juu ya nchi, wala chini ya nchi, aliyeweza kukifungua hicho kitabu, wala kukitazama. Nami nikalia sana kwa kuwa hapakuonekana mtu astahiliye kukifungua hicho kitabu, wala kukitazama. Na mmojawapo wa wale wazee akaniambia, Usilie; tazama, SIMBA ALIYE WA KABILA YA YUDA, SHINA LA DAUDI, yeye ameshinda apate kukifungua kile kitabu, na zile muhuri zake saba.”





Utangulizi:


Je ni Jambo gani hukujia kwanza kwenye akili zako mara unapomuona simba? Au unaposikia habari zake, Je nguvu zake, au kutisha kwake?, au ushujaa wake, au uzuri wake, uwezo wake, na muonekano wake, vyovyote vile itakavyokujua ni lazima tukubaliane kuwa simba ni mnyama maalumu sana, na umaalumu wqake utakufanya ukubali kuwa ni mfalme wa nyika, Japo wanapenda sana kukaa katika nyasi, Simba kama mnyama ana tabia ambazo kila mtu shujaa anapaswa kuwa nazo hapa duniani, leo tutachukua muda kujifunza tabia kadhaa za simba na kisha tutaziangalia namna tunavyoweza kuzitumia katika maisha yetu.
1.       Simba ana mtazamo tofauti na wanyama wengine.





Moja ya sifa inayomfanya simba kuwa mwindaji mzuri sana ni uwezo wake wa kuona, yaani mtazamo wake Jicho au macho ya samba katika mwanga wa kawaida yana uwezo wa kuona mara sita zaidi ya macho ya mwanadamu, na ndio maana samba wanauwezo mkubwa wa kuwinda usiku, uwezo wake wa kuona unampa uhakika wa kupata mawindo wakati wowote anapotaka mawindo, ana uwezo wa kukimbia kilomita 80 kwa saa na uwezo wa kuruka juu futi thelathini na sita wakati akikimbia, uwezo wake wa kutazama mambo unamfanya awe bora zaidi kuliko wanyama wengine japokuwa yeye
a.       Yeye sio mrefu kuliko wanyama wote (twiga ni mrefu kuliko yeye)
b.      Yeye sio mkubwa kuliko wengine (Tembo na faru na kiboko ni wakubwa kuliko yeye)
c.       Yeye sii mzito kuliko wengine ( Kiboko ni mzito zaidi na tembo pia)
d.      Yeye sio mzuri kuliko wengine (punda Milia ni mnyama mzuri zaidi)
e.      Yeye hatishi sana kuliko wengine ( Nyati anatisha mno kuliko yeye)
f.        Lakini simba ni mfalme na mtawala wa nyika
Simba anatufundisha kuwa uwezo wa mtu kuongoza hautokani na ukubwa alionao, uzito alionao, akili aliyo nayo, elimu aliyonayo, vitishio alivyonavyo, uzuri alionao utisho ulionao, Lakini namna unavyofikiri au namna unavyoona mambo, uwezo wa kiongozi uko katika mtazamo, tembo ni mkubwa sana lakini ndani hujiona kuwa yeye ni chakula cha simba, Simba huwaona wote hao kuwa ni chakula kwake, Hatuwaongozi watu kwa kuwatisha au kuwaogopesha bali watu wakituona tu watatuheshimu kwa muonekano wetu na mtazamo wetu, Simba hueshimika mara moja watu wanapomuona na kukubali kuwa yeye ndiye, kweli mfalme wa nyika

Isaya 11:1-4
Basi litatoka chipukizi katika shina la Yese, na tawi litakalotoka katika mizizi yake litazaa matunda.  Na roho ya Bwana atakaa juu yake, roho ya hekima na ufahamu, roho ya shauri na uweza, roho ya maarifa na ya kumcha Bwana; na furaha yake itakuwa katika kumcha Bwana; WALA HATAHUKUMU KWA KUYAFUATA AYAONAYO KWA MACHO YAKE, WALA HATAONYA KWA KUYAFUATA AYASIKIAYO KWA MASIKIO YAKE; bali kwa haki atawahukumu maskini, naye atawaonya wanyenyekevu wa dunia kwa adili; naye ataipiga dunia kwa fimbo ya kinywa chake, na kwa pumzi ya midomo yake atawaua wabaya.”
2.       Simba ana Sauti yenye kusikiika kuliko wengine.






Kuna wanyama wakubwa sana kumzidi Simba nyikani, wana nguvu kumzidi Simba na warefu kumzidi Simba lakini moja ya jambo linalomfanya Simba kuwa tofauti na wao ni sauti, Simba wana sauti kubwa na inayosikika inaemekana kuwa Simba anapounguruma uwezo wa sauti husikika kama miles 5 yaani sawa na kilomita 8, Sauti yake ni kama onyo kwa kila kiumbe kwamba Mfalme wa pori ameunguruma, unaweza kuwa na mawazo mazuri lakini kama hujui kujieleza huwezi kueleweka , unaweza kuwa na nguo za kiaskari lakini kama huna mamlaka huwezi kutiisha wala kutawala, unaweza kuwa na sifa zote njema lakini bila uadilifu huwezi kuogopwa, ukikosa uadilifu huwezi kuheshimiwa, unaweza kuwa na mawazo mazuri lakini usipofungua kinywa kuyasema hakuna atakayejua ni namna gani una hekima, Kuna wanyama wakubwa mno kuliko, Simba kuna wenye nguvu kuliko yeye, kuna wepesi kuliko yeye na wawindaji wazuri kuliko yeye lakini nini ninamfanya samba aogopwe ni sauti yake ni mamlaka yake ni haki yake, wengi wetu hatujawahi kumjua plato lakini tuna maneno yake na hekima yake kwa sababu alisema, tunawajua watu wengi sana ambao hatujawahi kuwaona kutiokana na kile walichiokisema, watu hodari ni wanenaji hodari  Yesu likuwa na uwezo katika kunena na kutenda

Luka 24:19
Akawauliza, Mambo gani? Wakamwambia, Mambo ya Yesu wa Nazareti, aliyekuwa mtu nabii, mwenye uwezo katika kutenda na kunena mbele za Mungu na watu wote;

Matendo 7:22
Musa akafundishwa hekima yote ya Wamisri, akawa hodari wa maneno na matendo.

Matendo 18:24 -26
Basi Myahudi mmoja, jina lake Apolo, mzalia wa Iskanderia, mtu wa elimu, akafika Efeso; naye alikuwa hodari katika maandiko. Mtu huyo alikuwa amefundishwa njia ya Bwana; na kwa kuwa roho yake ilikuwa ikimwaka, alianza kunena na kufundisha kwa usahihi habari za Yesu; naye alijua ubatizo wa Yohana tu. Akaanza kunena kwa ujasiri katika sinagogi; hata Prisila na Akila walipomsikia wakamchukua kwao, wakamweleza njia ya Bwana kwa usahihi zaidi.
Muungurumo wa simba porini uwezo wake na nguvu ya sauti yake hudhihirisha na kuwajulisha kuwa simba yupo, na hata kama yuko mbali unaweza kufikiri yuko karibu na utisho wake hufika kila mahali, ni muhimu kufahamu kuwa sio kila tunachokisema tu ndio kinaweza kutufanya kuwa viongozi wazuri bali pia  yale tunayoyatenda, viongozi wote wazuri katika biblia walikuwa hodari katika kunena na kutenda, kwa maneno yetu na matendo yetu sifa zetu huenea kila mahali, Simba anakuwa na ujasiri sio tu kwa sauti yake bali pia na kutenda kwake sauti yake inatisha na matendo yake pia sauti yake inaonyesha ujasiri na matendo yake pia , Sauti yake simba humtangulia kila anakokwenda, hivyo ni muhimu maneno yetu na matendo yetu yakawa sambamba, tumia uwezo wako wote kuhakikisha kuwa unatimiza kusudi la Mungu.

3.       Simba huishi kijamaa.






Simba ni mnyama anayeishi kwa ajili ya jamii pamoja na ujasiri na uwezo wake mkubwa alionao wao huishi kijamii kwa kiingereza huitwa “PRIDES” ambayo maana yake - the achievements of those with whom one is closely associated, yaani mafanikio ya mmoja ni mafanikio yao wote kwa lugha nzuri tungeweza kusema kuwa Simba anaishi kijamaa, inasemekana kuwa simba hata kama utamuona peke yake wao huishi kwa makundi na kundi la simba katika familia yaio huwa ni kuanzia simba 15-40 kundi hili laweza kujumuisha masimba dume wakubwa na majike mengi na vitoto vya simba vingi, kadiri kundi linavyokuwa kubwa na  ndio nguvu yao inavyokuwa kubwa zaidi. Majike wengi pia hutegemea madume kwaajili ya ulinzi wa watoto wao. Usipende kubeba mzigo peke yako ulinzi na usalama wako hata kama wewe ni shujaa kiasi gani unategemea watu wote wakubwa kwa wadogo, wana wake kwa wanaume unapokumbana na changamoto mbalimbali ni muhimu kukumbuka kuwa hauko peke yako uko unawatu wanaokuzunguka Familia, tuna marafiki, watenda kazi wenzetu katika bwana, team work tunahitajiana,

Daniel 2:1-17
Hata katika mwaka wa pili wa kumiliki kwake Nebukadreza, Nebukadreza aliota ndoto; na roho yake ikafadhaika, usingizi wake ukamwacha. Ndipo mfalme akatoa amri kuwaita waganga, na wachawi, na wasihiri, na Wakaldayo, wapate kumweleza mfalme ndoto zake. Basi wakaingia, wakasimama mbele ya mfalme. Mfalme akawaambia, Nimeota ndoto, na roho yangu imefadhaika hata niijue tafsiri yake. Ndipo hao Wakaldayo wakamwambia mfalme, kwa lugha ya Kiaramu, Ee Mfalme, uishi milele; tuambie sisi watumishi wako ile ndoto, nasi tutakuonyesha tafsiri yake. Mfalme akajibu, akawaambia Wakaldayo, Neno lenyewe limeniondoka; msiponijulisha ile ndoto na tafsiri yake, mtakatwa vipande vipande, na nyumba zenu zitafanywa jaa. Bali kama mkinionyesha ile ndoto na tafsiri yake, nitawapa zawadi na thawabu na heshima nyingi; basi nionyesheni ile ndoto na tafsiri yake. Wakajibu mara ya pili, wakasema, Mfalme na atuambie sisi watumishi wake ile ndoto, nasi tutamwonyesha tafsiri yake. Mfalme akajibu, akasema, Najua hakika ya kuwa mnataka kupata nafasi, kwa sababu mmeona ya kuwa lile neno lenyewe limeniondoka. Lakini msiponijulisha ile ndoto, iko amri moja tu iwapasayo; maana mmepatana kusema maneno ya uongo, na maneno maovu, mbele yangu, hata zamani zitakapobadilika; basi niambieni ile ndoto, nami nitajua ya kuwa mwaweza kunionyesha tafsiri yake. Wakaldayo wakajibu mbele ya mfalme, wakasema, Hapana mtu duniani awezaye kulionyesha neno hili la mfalme; kwa maana hapana mfalme, wala bwana, wala liwali, aliyetaka neno kama hili kwa mganga, wala kwa mchawi, wala kwa Mkaldayo. Ni neno la ajabu, hili analolitaka mfalme, wala hapana mwingine awezaye kumwonyesha mfalme neno hilo, ila miungu, wasio na kikao pamoja na wenye mwili. Basi kwa hiyo mfalme akaghadhibika sana, akaona hasira nyingi, akatoa amri kuwaangamiza wenye hekima wote wa Babeli. Basi ile amri ikatangazwa, na hao wenye hekima walikuwa karibu na kuuawa; watu wakamtafuta Danieli na wenzake ili wauawe. Ndipo Danieli kwa busara na hadhari akamjibu Arioko, akida wa walinzi wa mfalme, aliyekuwa ametoka ili kuwaua wenye hekima wa Babeli; alijibu, akamwambia Arioko, akida wa walinzi wa mfalme, Mbona amri hii ya mfalme ina ukali namna hii? Ndipo Arioko akamwarifu Danieli habari ile. Basi Danieli akaingia, akamwomba mfalme ampe muda, kisha yeye atamwonyesha mfalme tafsiri ile. Ndipo Danieli akaenda nyumbani kwake, akawapasha habari kina Hanania, na Mishaeli, na Azaria wenzake; ili waombe rehema kwa Mungu wa mbinguni kwa habari ya siri hiyo, ili kwamba Danieli na wenzake wasiangamizwe pamoja na wenye hekima wa Babeli. Ndipo Danieli alipofunuliwa siri hiyo katika njozi ya usiku. Basi Danieli akamhimidi Mungu wa mbinguni.”

Daniel, Shadrack, Meshak na Aberdhego walikuwa mashujaa lakini walishirikiana pamoja katika kumuomba Mungu kwaajili ya changamoto walizokuwa wakikutana nazo wawapo, kazini na katika utumishi wao kwa jamii waliishi katika kundi ambalo kwa pamoja walijihisi salama wakiwa na imani moja.

Nyakati za kanisa la Kwanza tunafahamu kuwa mitume walikuwa na ushujaa mwingi ujasiri na kujiamini lakini hata hivyo wakati walipokutana na changamoto hawakuwa wakizibeba peke yao bali waliwashirikisha na kanisa na kumuomba Mungu pamoja na wote wakatiwa nguvu na Roho Mtakatifu ona Matendo ya

Mitume 4:18-31 “
Wakawaita, wakawaamuru wasiseme kabisa wala kufundisha kwa jina la Yesu. Petro na Yohana wakawajibu wakawaambia, Kwamba ni haki mbele za Mungu kuwasikiliza ninyi kuliko Mungu, hukumuni ninyi wenyewe; maana sisi hatuwezi kuacha kuyanena mambo tuliyoyaona na kuyasikia. Nao walipokwisha kuwatisha tena wakawafungua, wasione njia ya kuwaadhibu, kwa sababu ya watu; kwa kuwa watu wote walikuwa wakimtukuza Mungu kwa hayo yaliyotendeka; maana umri wake yule mtu aliyefanyiwa ishara hii ya kuponya ulipita miaka arobaini. Hata walipofunguliwa, wakaenda kwa watu wao, wakawapasha habari ya mambo yote waliyoambiwa na wakuu wa makuhani na wazee. Nao waliposikia, wakampazia Mungu sauti zao kwa moyo mmoja, wakisema, Mola, wewe ndiwe Mungu, ndiwe uliyefanya mbingu na nchi na bahari na vitu vyote vilivyomo; nawe ulinena kwa Roho Mtakatifu kwa kinywa cha babaetu Daudi, mtumishi wako, Mbona mataifa wamefanya ghasia, Na makabila wametafakari ubatili? Wafalme wa dunia wamejipanga, Na wakuu wamefanya shauri pamoja Juu ya Bwana na juu ya Kristo wake. Maana ni kweli, Herode na Pontio Pilato pamoja na Mataifa na watu wa Israeli, walikusanyika katika mji huu juu ya Mtumishi wako mtakatifu Yesu, uliyemtia mafuta, ili wafanye yote ambayo mkono wako na mashauri yako yamekusudia tangu zamani yatokee. Basi sasa, Bwana, yaangalie matisho yao; ukawajalie watumwa wako kunena neno lako kwa ujasiri wote, ukinyosha mkono wako kuponya; ishara na maajabu vifanyike kwa jina la Mtumishi wako mtakatifu Yesu. Hata walipokwisha kumwomba Mungu, mahali pale walipokusanyika pakatikiswa, wote wakajaa Roho Mtakatifu, wakanena neno la Mungu kwa ujasiri.”


Kila mtu ata awe shujaa kiasi gani anahitaji wengine katika mafanikio yake na katika kutimiza malengo ya kiuongozi na kiutawala huwezi kufanikiwa ukiwa mwenyewe hata kama una nguvu na sauti kiasi gani.

4.       Simba wana muda mrefu wa Kupumzika.



Simba wana tabia ya kupumzika kwa muda mrefu sana inasemekana simba hutumia msaa karibu 20 wakiwa wamepumzika  kisayansi simba hawana mate mengi sana hivyo hupumika vya kutosha ili waweze kuwa na nguvu mpya zaidi, kuna tofauti kubwa sana kati ya mfalme na mtumwa, Mfalme anapaswa kuwa na muda wa kupumzika, lakini mtumwa anapaswa kufanya kazi kwa kiwango kikubwa sana mpaka kuwa mtumwa wa kazi, Mungu hubariki kazi za mikono yetu, na neno lake limesisitiza kuwa asiyefanya kazi na asile hivyo kufanya kazi ni mpango wa Mungu, lakini liko jaribu kwa wanadamu la kutaka kufanya kazi kupita kiasi hiii ni dhambi, Mungu ametufundisha katika neno lake kuwa na muda wa mapumziko na kutokuogopa maisha wala kuwaza itakuwaje kesho,

Mwanzo 2:1-3
Basi mbingu na nchi zikamalizika, na jeshi lake lote. Na siku ya saba Mungu alimaliza kazi yake yote aliyoifanya; akastarehe siku ya saba, akaacha kufanya kazi yake yote aliyoifanya. Mungu akaibarikia siku ya saba, akaitakasa kwa sababu katika siku hiyo Mungu alistarehe, akaacha kufanya kazi yake yote aliyoiumba na kuifanya.

kila siku tunaamka tukiwa na malengo au nkusudi fulani la kulitimiza na hatutaki kuacha nkitu kwaajili ya hayo tunajaribiwa kutokupumzika na tunajikuta tumekuwa watumwa wa kazi, Mungu anataka tufanye kazi lakini Mungu hatai tuwe watumwa wa kazi, tunajitoa kirahisi sana kwa watu na kazi, tukijichosha na kujiumiza sana na hivyo tunayafanyua maisha yetu kuwa ya kitumwa kabisa duniani na wala hatufurahii matunda ya kazi zetu, Simba hawako hivyotunapaswa kujifunza kutoka kwao, wana wanajua kuwa wanapaswa kula kila siku, lakini wanajua pia umuhimu wa mapumziko, simba halali na njaaa, ana uhakika wa kula, lakini wanapumzika kwa muda wa kutosha, kama mtu anataka kuyafurahia maisha ni lazima ajifunze kuwa hatupaswi kuacha hofu nza maisha zikatutawala kwa hiyo ni muhimu kuwa na muda wa kuyafurahia maisha na kujipumzisha relax

Mathayo 6:25-34
Kwa sababu hiyo nawaambieni, Msisumbukie maisha yenu, mle nini au mnywe nini; wala miili yenu, mvae nini. Maisha je! Si zaidi ya chakula, na mwili zaidi ya mavazi? Waangalieni ndege wa angani, ya kwamba hawapandi, wala hawavuni, wala hawakusanyi ghalani; na Baba yenu wa mbinguni huwalisha hao. Ninyi je! Si bora kupita hao? Ni yupi kwenu ambaye akijisumbua aweza kujiongeza kimo chake hata mkono mmoja? Na mavazi, ya nini kuyasumbukia? Fikirini maua ya mashamba, jinsi yameavyo; hayafanyi kazi, wala hayasokoti nami nawaambia, ya kwamba hata Sulemani katika fahari yake yote hakuvikwa vizuri kama mojawapo la hayo. Basi, ikiwa Mungu huyavika hivi majani ya kondeni, yaliyopo leo, na kesho hutupwa kalibuni, je! Hatazidi sana kuwavika ninyi, enyi wa imani haba? Msisumbuke, basi, mkisema, Tule nini? Au Tunywe nini? Au Tuvae nini? Kwa maana hayo yote Mataifa huyatafuta; kwa sababu Baba yenu wa mbinguni anajua ya kuwa mnahitaji hayo yote. Bali utafuteni kwanza ufalme wake, na haki yake; na hayo yote mtazidishiwa. Basi msisumbukie ya kesho; kwa kuwa kesho itajisumbukia yenyewe. Yatosha kwa siku maovu yake.
Simba wanapumzika wakijuankuwa wana uhakika watapata wanachikitaka na maisha yataendelea hawalali na njaa na hawaogopi njaa, wanajua watatumia muda mfupi na watapata wakitakacho.

5.       Simba hawana choyo




Simba hawana tabia ya choyo kwa kawaida samba wakiwa katika familia Jike ndiye anayefanya kazi ya kutafuta chakula na dume hubaki na familia na kulinda watoto, samba wanatabia ya kuwinda chakula cha kutosha kwaajili ya familia nzima na wanakula na kushiba na kusaza kasha samba huwaachia chakula fisi na tai mla mizoga aitwaye vulture ili nao waponee kwenye mawindo yake, hivyo simba huwinda kwaajili yake na wengine, Uwezo wa kuhsirikisha wengine Baraka za Mungu ni moja ya alama ya kiongozi na mtu aliyekomaa kiroho, Yesu alitufundisha kwamba ni muhimu kujilinda na choyo, uhai wa mtu hauko katika wingi wa vitu alivyonavyo ona

Luka 12:15-21
Akawaambia, Angalieni, jilindeni na choyo, maana uzima wa mtu haumo katika wingi wa vitu vyake alivyo navyo. Akawaambia mithali, akisema, Shamba la mtu mmoja tajiri lilikuwa limezaa sana; akaanza kuwaza moyoni mwake, akisema, Nifanyeje? Maana sina pa kuyaweka akiba mavuno yangu. Akasema, Nitafanya hivi; nitazivunja ghala zangu, nijenge nyingine kubwa zaidi, na humo nitaweka nafaka yangu yote na vitu vyangu. Kisha, nitajiambia, Ee nafsi yangu, una vitu vyema vingi ulivyojiwekea akiba kwa miaka mingi; pumzika basi, ule, unywe, ufurahi. Lakini Mungu akamwambia, Mpumbavu wewe, usiku huu wa leo wanataka roho yako! Na vitu ulivyojiwekea tayari vitakuwa vya nani?  Ndivyo alivyo mtu ajiwekeaye nafsi yake akiba, asijitajirishe kwa Mungu.”

Mungu anapokuwa amekufanikisha kwa Baraka zozote zile Baraka hizo sio kwaajili yetu wenyewe bali ni kwaajili yatu na wengine Simba huwa hasemi kwamba hii ni nguvu yangu mimi, nimetafuta mwenyewe, kwaajili ya nafsi yangu tu, hapana Simba hutafuta vya kutosha kwaajili ya jamii yaka na kwaajili ya wale wasio wa jamii yake samba wakishiba wanabakiza chakula cha kutosha nkisha fisi na ndege wa mwituni hujipatiamo humo, watu walio bora na viongozi walio bora hawana kitu chao wenyewe hufanya mambo kwa manufaa ya jamii na kwa manufaa ya watu wote, ni muhimu nkukumbuka kuwa wajibu wetu sio kutoa amritu na kuwatisha wengine au kuwafanya wengine wafanye kazi tu, tunao wajibu wa kuwatia moyo wengine na kuwaachia na wengine Baraka , Simba wakishiba baada ya kuwinda mawindo huwaachia wengine mabaki, ili nao wale waishi kwa nguvu za Simba, watu wenye choyo huzoa kila kitu hawaachi akiba hata kwa wanyonge hawajali yatima wala wajane wanakula kila kitu huo sio mpango wa Mungu

Kumbukumbu la Torati 24:18-22 “
bali kumbuka ya kuwa ulikuwa mtumwa katika Misri, Bwana, Mungu wako, akakukomboa huko; kwa hiyo nakuamuru kutenda neno hili. Uvunapo mavuno yako katika shamba lako, ukasahau mganda shambani, usirudi kuuchukua; na uwe wa mgeni, au yatima, au mjane; ili Bwana, Mungu wako, akubariki katika kazi yote ya mikono yako. Utakapochuma matunda ya mizeituni yako, usirudi kuchuma mara ya pili; yaliyobaki apewe mgeni, na yatima, na mjane. Uchumapo zabibu katika shamba lako la mizabibu, usichume mara ya pili; zilizobaki apewe mgeni, na yatima, na mjane. Nawe kumbuka ya kuwa ulikuwa mtumwa katika nchi ya Misri; kwa hiyo nakuamuru kutenda neno hili.Mungu anataka watu wake wajifunze ukarimu wawe watoaji kuna Baraka nyingi sana katika kutoa imeandikwa kuwa ni heri kutoa kuliko kupokea samba ni watoaji

Matendo 20:34-35 “Ninyi wenyewe mnajua ya kuwa mikono yangu hii imetumika kwa mahitaji yangu na ya wale waliokuwa pamoja nami. Katika mambo yote nimewaonyesha ya kuwa kwa kushika kazi hivi imewapasa kuwasaidia wanyonge, na kuyakumbuka maneno ya Bwana Yesu, jinsi alivyosema mwenyewe, Ni heri kutoa kuliko kupokea.


Kama unataka kuheshimiwa na watu hakikisha kuwa unatoa, hakuna kiwango cha maisha ambayo unapaswa kutokutoa kama hujayafikia waingereza wana usemi unaosema kumpa mbwa mfupa sio ukarimu ukarimu ni kushiriki mfupa na mbwa wakati wote mkiwa na njaa” Simba anapokula fisi huja kushiriki kula mwindo yake na hata hivyo akishiba huwaachia, ni mfalme gani anayekula vyote asiwaachie wale walio wanyonge wapate chochote.6.       Simba hugawana majukumu.

Simba wana mgawanyo wa majukumu hawafanyi kila kitu wenyewe, Mwandishi mmoja alisema hivi anaamini kuwa iko sababu kubwa sana kwa nini tumepewa mikono miwili na miguu miwili, na iko sababu ya kwa nini mwanadamu ana nguvu za kibinadamu na sio nguvu za farasi, hii maana yaka ni nini hatuwezi kufanya kila kitu wenyewe kwa sababu huwezi kuwa mahali kote kwa wakati mmoja hata kama utakuwa unatumia mafuta, hakuna muda wa kutosha kwa siku kwa mtu mmoja kufanya kila kitu, kwa msingi huo ni lazima tuwape majukumu watu wengine pia kuna usemi unaosema “ kama unataka kila kitu kifanyike kwa ukamilifu, basi fanya mwenyewe”  kwa bahatimbaya ukitaka kufanyia kazi  msemo huu utakufa haraka, ndio maana samba hugawana majukumu, wakati jike likienda kutafuta mawindo na kuleta chakula dume hubaki na familia na kuwalinda watoto, ni lazima tujifunze kuwa kumpa mtu mamlaka haimaanishi kuwa mtu huyo atakudharau, au atakuwa na mamlaka kuliko wewe, lakini badala yake ni utambuzi ya kuwa unatambua uweza na ufundi wa wenmgine katika kukamilisha mambo, na kuwa wao pia ni muhimu, kwa hiyo kiongozi mzuri haogopi kuwaamini wengine, Simba anapoacha jike likawinde yeye hubaki na majukumu mengine ya kuilinda familia kwa hiyo samba sio mvivu, lakini anatambua umuhimu wa kila mmoja katika familia na jamii na umuhimu wa majukumu ya kila mmoja  wagogo wanausemi kuwa ukikimbiza panya wawili kwa wakati mmoja mmoja atakuponyoka kwa hiyo ni muhimu kumuamini kila mmoja sawa na kipawa na karama aliyo nayo.

1Wakoriho 12:3-4
Basi pana tofauti za karama; bali Roho ni yeye yule. Tena pana tofauti za huduma, na Bwana ni yeye yule.  Kisha pana tofauti za kutenda kazi, bali Mungu ni yeye yule azitendaye kazi zote katika wote. Lakini kila mmoja hupewa ufunuo wa Roho kwa kufaidiana.


Warumi 12:6-8 “Basi kwa kuwa tuna karama zilizo mbalimbali, kwa kadiri ya neema mliyopewa; ikiwa unabii, tutoe unabii kwa kadiri ya imani; ikiwa huduma, tuwemo katika huduma yetu; mwenye kufundisha, katika kufundisha kwake; mwenye kuonya, katika kuonya kwake; mwenye kukirimu, kwa moyo mweupe; mwenye kusimamia kwa bidii mwenye kurehemu, kwa furaha.


Waefeso 4:11-13 “Naye alitoa wengine kuwa mitume, na wengine kuwa manabii; na wengine kuwa wainjilisti na wengine kuwa wachungaji na waalimu; kwa kusudi la kuwakamilisha watakatifu, hata kazi ya huduma itendeke, hata mwili wa Kristo ujengwe; hata na sisi sote tutakapoufikia umoja wa imani na kumfahamu sana Mwana wa Mungu, hata kuwa mtu mkamilifu, hata kufika kwenye cheo cha kimo cha utimilifu wa Kristo;”   
          
7.       Simba hulinda jamii yao na hatari






Kama tulivyoona kuwa simba jike mara kadhaa ndiye anayehusika na kuwinda kwa asilimia 85-90% wakati asilimia chache zinazosalia za uwindaji ndizo hufanywa na Simba Dume, katika mgawano wao wa kazi na majukumu wakati simba jike anawinda simba dume hufanya kazi ya kulinda jamii yake, Simba hulinda kundi lake lote lakini pia hulinda mipaka ya kundi lake kwa kiwango cha mile 100, yaani sawa na kilomita za mraba 160, katika eneo hilo lote chochote kitakachoaribia, kitaweza kufyekelewa mbali, Simba hatakubali adui akaribie jamii yake atapambana kuhakikisha jamii yake iko salama na wanaishi kwa amani, ni mpiganaji wa amani, wanautulivu hekima na busara na hutumia akili sana katika uwindaji wake lakini ni wapambanaji kwaajili ya jamii huyatoa maisha yao kwaajili ya wengine hawakubali kuona uonevu, hulinda simba wadogo na kundi zima


Yuda - Mwanzo 44:1-34,Akamwamuru yule msimamizi wa nyumba yake akisema, Jaza magunia ya watu hawa chakula kwa kadiri wawezavyo kuchukua, utie na fedha ya kila mtu kinywani mwa gunia lake. Na kikombe changu, kikombe kile cha fedha, ukitie kinywani mwa gunia la yule mdogo pamoja na fedha ya nafaka yake. Akafanya kama vile alivyomwambia Yusufu. Asubuhi kulipopambazuka, hao watu wakapewa ruhusa, wao na punda zao. Na walipotoka mjini, wala hawajaendelea sana, Yusufu akamwambia yule msimamizi wa nyumba yake, Ondoka, uwafuate watu hawa, nawe utakapowapata, waambie, Kwa nini mmelipa mabaya kwa mema? Je! Kikombe hiki, sicho anyweacho bwana wangu? Naye hufanya uaguzi kwa hicho. Mmefanya vibaya kwa kufanya hivi. Akawafuata, akawapata, na kuwaambia maneno hayo. Wakamwambia, Kwa nini bwana wangu anasema maneno kama haya? Hasha! Watumwa wako wasifanye hivi; tazama, hizo fedha mlizoziona kinywani mwa magunia yetu, tumekuletea tena kutoka nchi ya Kanaani. Tuwezeje sisi kuiba nyumbani mwa bwana wako fedha au dhahabu?  Atakayeonekana kuwa nacho miongoni mwa watumwa wako, na afe, na sisi nasi tutakuwa watumwa wa bwana wangu. Akasema, Basi na iwe hivyo kama mlivyosema, Mtu atakayeonekana kuwa nacho atakuwa mtumwa wangu, na ninyi mtakuwa hamna hatia. Wakafanya haraka, wakashusha kila mtu gunia lake, na kufungua kila mtu gunia lake.Naye akatafuta, akaanza kwa mkubwa na kuisha kwa mdogo. Kikombe kikaonekana katika gunia la Benyamini. Wakararua nguo zao, wakaweka kila mtu mzigo wake juu ya punda wake, wakarudi mjini. Akaja Yuda na ndugu zake nyumbani kwa Yusufu, naye mwenyewe alikuwamo, nao wakamwangukia kifudifudi. Yusufu akawaambia, Ni tendo gani hili mlilolitenda? Hamkujua ya kwamba mtu kama mimi naweza kufanya uaguzi? Yuda akasema, Tumwambie nini bwana wangu? Tusemeje! Tujivutieje haki? Mungu ameona uovu wa watumwa wako. Tazama, sisi ni watumwa wa bwana wangu, sisi na yeye ambaye kikombe kilionekana mkononi mwake. Akasema, Hasha! Nisifanye hivi; mtu ambaye kikombe kilionekana mkononi mwake, ndiye atakayekuwa mtumwa wangu. Nanyi enendeni zenu kwa amani kwa baba yenu. Ndipo Yuda akamkaribia, akasema, Tafadhali, bwana wangu, mtumwa wako na aseme neno moja masikioni mwa bwana wangu, wala hasira yako isimwakie mtumwa wako, maana wewe u kama Farao. Wewe, bwana wangu, ulituuliza watumwa wako, ukisema, Je! Mnaye baba, au ndugu? Tukakuambia wewe, bwana wangu, Tunaye baba, naye ni mzee, na mwana wa uzee wake ni mdogo, na nduguye amekufa; amebaki yeye peke yake wa katika tumbo la mamaye, na baba yake anampenda.Ukatuambia watumwa wako, Mleteni kwangu, ili macho yangu yamwangalie. Tukakuambia, bwana wangu, Kijana hawezi kumwacha babaye, maana akimwacha babaye, babaye atakufa.Ukatuambia watumwa wako, Asiposhuka ndugu yenu mdogo pamoja nanyi, hamtaniona uso wangu tena Ikawa tulipokwenda kwa mtumwa wako, baba yangu, tukamwarifu maneno yako, bwana wangu. Kisha baba yetu akanena, Rudini huko, mkatununulie chakula kidogo. Tukasema, Hatuwezi kwenda; ndugu yetu mdogo akiwapo pamoja nasi, tutashuka, maana hatutaweza kuuona uso wa mtu huyo, ndugu yetu mdogo asipokuwa pamoja nasi. Mtumwa wako, baba yangu, akatuambia, Mnajua ya kuwa mke wangu alinizalia wana wawili; mmoja alitoka kwangu, nikasema, Bila shaka ameraruliwa, wala sikumwona tangu hapo. Na mkiniondolea huyu naye, na madhara yakimpata, mtashusha mvi zangu na msiba kaburini. Basi, nikienda kwa mtumwa wako, baba yangu, na huyu kijana hayupo pamoja nasi, iwapo roho yake imeshikamana na roho ya kijana; itakuwa atakapoona ya kwamba huyu kijana hayuko, atakufa; na watumwa wako watashusha mvi za mtumwa wako, baba yetu, kwa huzuni kaburini Kwa maana mtumwa wako alijifanya mdhamini wa huyu kijana kwa baba yangu, nikisema, Nisipomrudisha kwako, nitakuwa na hatia kwa baba yangu sikuzote. Basi, sasa nakusihi, uniache mimi mtumwa wako nikae badala ya huyu kijana kuwa mtumwa wa bwana wangu; na huyu kijana umwache aende pamoja na nduguze. Kwa maana nitawezaje kumwendea baba yangu, na huyu kijana hayuko pamoja nami? Nisije nikayaona mabaya yatakayompata baba yangu.”

       
 Kutokana na kujitoa kwake na upendo wake mkuu aliokuwa nao Yuda Yakobo alipombariki alimtaja kuwa kama mwana Simba

Mwanzo 49:8-10 “Yuda, ndugu zako watakusifu, Mkono wako utakuwa shingoni mwa adui zako. Wana wa baba yako watakuinamia.Yuda ni mwana-simba, Kutoka katika mawindo, mwanangu, umepanda; Aliinama akajilaza kama simba, Na kama simba mke; ni nani atakayemwamsha? Fimbo ya enzi haitaondoka katika Yuda, Wala mfanya sheria kati ya miguu yake, Hata atakapokuja Yeye, mwenye milki, Ambaye mataifa watamtii.


Hiki ndio alichokifanya Bwana Yesu kwaajili yetu pamoja na waamuzi hawakukubali uonevu dhidi ya watu wao walipambana kuhakikisha nusalama wa watu wao hivyo ndivyo samba walivyo
Isaya 53:1-5Ni nani aliyesadiki habari tuliyoileta? Na mkono wa Bwana amefunuliwa nani? Maana alikua mbele zake kama mche mwororo, Na kama mzizi katika nchi kavu; Yeye hana umbo wala uzuri; Na tumwonapo hana uzuri hata tumtamani. Alidharauliwa na kukataliwa na watu; Mtu wa huzuni nyingi, ajuaye sikitiko; Na kama mtu ambaye watu humficha nyuso zao, Alidharauliwa wala hatukumhesabu kuwa kitu. Hakika ameyachukua masikitiko yetu, Amejitwika huzuni zetu; Lakini tulimdhania ya kuwa amepigwa, Amepigwa na Mungu, na kuteswa. Bali alijeruhiwa kwa makosa yetu, Alichubuliwa kwa maovu yetu; Adhabu ya amani yetu ilikuwa juu yake, Na kwa kupigwa kwake sisi tumepona.” Huu ni upendo mkubwa sana Yesu alikufa kwaajili yetu, Hatuna budi kuhakikisha kuwa tunasimama upande wake siku zote za maisha yetu, tusihesabu damu yake ya thamani kuwa kitu cha hovyo tudumu katika wokovu na kuwa wavumilivu kwaajili ya Mungu wetu.”
Ujumbe na Rev. Innocent Kamote
Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima
0718990796

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni