Ijumaa, 12 Februari 2021

Ni Afadhali kukaa katika pembe ya darini!

Mithali 25:24, “Ni afadhali kukaa katika pembe ya darini, Kuliko katika nyumba pana pamoja na mwanamke mgomvi.” Mithali 21:9 “Ni afadhali kukaa katika pembe ya darini, Kuliko katika nyumba pana pamoja na mwanamke mgomvi.”


Utangulizi:

Mithali ni mojawapo ya kitabu muhimu katika vitabu vya mashairi ya kiebrania, kama wengi wetu tunavyofahamu kuwa katika tamaduni nyingi kwenye misemo na mashairi au nyimbo, watunzi wengi huifadhi maneno ya maana na yenye uadilifu fulani kwa kusudi la kupeleka mafunzo fulani katika jamii, kama Jinsi ambavyo tumeona hapa katika kitabu cha Mithali, hapo juu, Katika kifungu au vifungu hivyo, Walengwa wa kifungu hiki hasa wanaweza kuwa wanaume na wanawake pia! Na hasa vifungu vinaweza kuwa na kusudi la kutoa ushauri au kuwafundisha wanaume ni mwanamke wa aina gani anaweza kumuoa na wanawake jinsi gani na namna wanaweza kutumia ndimi zao na kutunza hisia zao “TEMPER” zinazoweza kuondoa amani na utulivu katika nyumba na sehemu nyinginezo, Tunapoendelea kujifunza somo hili AFADHALI KAUKAA KATIKA PEMBE YA DARINI, Utagundua kuwa kuna umuhimu mkubwa sana wa kila mwanamke kuchunga kauli zake katika mahusiano ya aina yoyote ile! Lakini zaidi sana uhusiano wake katika ndoa. Lakini vilevile kuna maonyo makubwa sana kwa wanaume kuwa kama kuna kitu ukikikosea wakati unakusudia kuoa kuna jambo utakutana nalo. Kwa ufupi matumizi ya ulimi na udhbiti wa hisia zetu una faida na ama hasara kubwa sana katika swala zima la mahusiano. tutajifunza somo hili kwa kuzngatia vipengele kadhaa vifuatacyo:- 

·         Maana ya Pembe ya darini

·         Afadhali kukaa katika Pembe ya darini

·         Mwanamke mgomvi!

·         Umuhimu wa kutunza amani ya moyo!


Maana ya pembe ya darini

Katika tamaduni za ujenzi wa kale hasa katika jamii ya waarabu na wayahudi, walijenga nyumba za ghorofa ambazo juu zilikuwa na dari au sehemu maalumu za kupumzikia, ambayo ilijengwa kwa kusawazishwa juu, Pwani ya Afrika mashariki watakuwa na ufahamu kuhusu aina hii ya ujenzi kwa sababu waarabu walipokuja mapema sana katika miji ya Kilwa, Malindi, Mombasa, Zanzibar, Mafia na Sofala waliacha urithi wa aina hizo za majengo na ambazo wenyeji pia waliigiza, Katika ujenzi huo juu waliweka dari na dari iliweza kuwekwa aina fulani ya lami  na hivyo kupata eneo zuri na salama la kupumzikia, hata hivyo wakati muafaka wa kukaa katika Pembe ya dari ulikuwa ni wakati wa hari yaani wakati wa joto, wakati wa tufani, pepo kali na mvua na radi eneo hilo halingeweza kufaa kwa kupumzikia.

Afadhali kukaa katika Pembe ya Darini

Mwandishi wa kitabu hiki cha Hekima anaona ni heri kukaa katika Pembe ya dari kuliko kukaa na mwanamke mwenye kelele, Yeye mtazamo wake ni kuwa pale kwenye pembe ya darini pana afadhali kukaa wakati wote ikiwa ni pamoja na wakati wa tufani na joto kali na hata wakati wa mvua na radi kuliko kukaa katika nyumba pana na mwanamke mwenye kelele, Nyumba pana  inayozungumzwa hapa ni zile ambazo ni kubwa na zina vyumba vingi na familia kubwa  nyumba ya jamii, nyumba ambayo familia kubwa wanaweza kukaa na kushirikiana nyumba ambayo ina mume mke na watoto yeye anaiona nyumba hiyo kuwa ni nyumba isiyofaa kabisa kama atakuwepo mwanamke mwenye kelele, yaani mwanamke mtawala, mkaidi, kimbelembele asiye na uvumilivu mdadisi, mchunguzi mwenye kushuku, mchoyo, asiye na ushirikiano katika tendo la ndoa mgomvi, mwenye luigha mbaya mwenye matumizi mabaya ya ulimi, kwa mwandishi wa kitabu cha Mithali Mfalme solomoni anaona ni Kheri kukaa katika pemba ya dari kuliko kukaa na aina hii ya mwanamke katika jumba la kifahari  au wakati mwingine ni afhadhali uende nyikani au jangwani kuliko kukaa na mwanamke huyo mgomvui ona

Mithali 21:19 “Ni afadhali kukaa katika nchi ya nyika; Kuliko na mwanamke mgomvi, mchokozi.
Mwandishi pia anaona afadhali kula ukoko wa wali au ukoko wa mkate kuliko kwenye nyumba yenye karamu nyingi lakini haina amani ona

Mithali 17:1 “Afadhali mego kavu pamoja na utulivu, Kuliko nyumba yenye karamu nyingi pamoja na magomvi.” aidha katiika

Mithali 19: 13 Biblia inasema hivi “Mwana mpumbavu ni msiba kwa babaye; Na ugomvi wa mke kama kutona-tona daima.”

Mwandishi anazungumzia hapo ugomvi wa mke yaani mwanamke mwenye kelele ni kama kutona tona neno hilo kutona tona katika biblia ya kiingereza ya The Amplified Bible  linatumika neno “continual dripping” hali hii ni ngumu kuielezea kwa kizazi cha leo ambao wanaishi kwenye nyumba nzuri zilizosakafiwa vema kila mahali lakini wale wenye umri wa miaka kadhaa na waliowahi kuishi vijijini wanafahamu taabu ya nyumba inayovuja hasa zile za nyasi au za makuti, unafahamu karaha ya kuishi katika nyumba ambayo hapa panavuja na pale panavuja na kadhalika ile taabu ya kuishi kwenye nyumba inayovuja daima ndio inaitwa kutona tona kwa hiyo kimsingi Sulemani anaonyesha yale maudhi ya kukaa katika nyumba inayovuja ile hali ya kuishi kwa mashaka na wasiwasi katika nyumba inayovuja inalingana kabisa na kuishi na mwanamke mgomvi

Mwanamke mgomvi ni wa namna gani?

Mithali hii ina maswala ya msingi ya kuzingatia sana ona mwanamume aliyeoa hapa anatamani kukaa katika Pembe ya darini au anaona ni afhadhali kukaa katika pembe ya darini juu npeke yake  kuliko kukaa na mwanamke mwenye kelele au mgomvi Mithali inaonekana kuwa yenye kutaka kuchukua ufahamu wetu wote uelekee kwenye kitu kigeni na cha muhimu kwetu kujifunza yaani iweje jamaa aone kuwa kwenye kona ya darini peke yake ni pazuri kuliko kukaa na mwanamke mwenye kelele mgomvi, kuna tatizo kukaa katika kona ya darini ni maisha gani je ni kweli panaweza kuwa na faraja? Bila shaka ni lugha ya kukuza jambo ili kutoa umuhimu kwenye kitu mwandishi anataka kukiwasilisha na hiki si kingine ni mwanamke mgomvi ni mwanamke mwenye kelelel huyu ni mwanamke wa namna gani? Biblia ya kiebrania inatumia neno “MADON” inamaanisha mtu aliyejawa na uchungu Biblia ya kiingereza inatumia neno strife dissension yaani muasi, mwenye uchungu na asiyekubaliana au mwenye mijadala na mpinzani unaweza kuona  kwa hiyo unapokuwa naye  wakati wote kunakuwa na mafuriko ya ugomvi

Mithali 17:14 “Mwanzo wa ugomvi ni kama kutoboa penye maji; Basi acheni ugomvi kabla haujafurika.
au kunapotokea ugomvi na kutokuelewana yeye hamalizi kwa haraka haachilii hawezi kuacha kubwatuka na kusema na kusengenya  yuko kwaajili ya mashindano yuko kwaajili ya kulipiza kisasi ona

Mithali 18:19 “Ndugu aliyechukizwa ni mgumu kuliko mji wa nguvu; Na mashindano ni kama mapingo ya ngome.”
yaani ni aina ya mwanamke ambaye wakati wote anakwaza au anakuwekea vikwazo na hii inaambatana na ubovu wa moyo alionao na hisia mbaya, acha ya kuwa atakukwaza kiasi ambacho hutakuwa na hamu ya kushirikiana naye hata tendo la ndoa, atajificha katika silaha ya kulia na kujibanza kwenye kuamua kufungasha au kukuletea aibu miongoni mwa watu wanaokuheshimu, atataka akuweke vikao akupeleke kwa wachungaji au wazee wa kanisa au kwa wakwe kule ukasutwe mpaka aonekane yeye ndio mshindi,  ni aina ya mwanamke mwenye wivu mkali sana akikuona umesimama na mwanamke tu hata bila kujali ni wa rika gani na wa aina gani na mnazungumza nini mtajikuta mnaingia katika ugomvi mkubwa , huyu kila kitu ni ugomvi hii ni dhambi mbaya sana ni katika aina hii ya mwanamke ndio inaonekana kuwa ni afadhali kukaa katika pembe ya darini na kuvumilia dhuruba na upepo na upweke kuliko jumba kubwa la karamu na sherehe lakini na aina ya mwanamke kama huyu, aina hii ya mwanamke kwa mujibu wa Sulemani ni msiba ukikaa naye, badala ya kuwa mpole na mwenye kujinyenyekeza na mtii kwa mumewe kama maandiko yanavyoelekeza huyu ni mwanamke mtawala, mwenye hasiram asiye na utulivu hawezi kuzuia hisia zake  amejaa chuki na wakati wowote roho yake iko tayari kwa majibu ya hovyo na kupambana na mumewe, ukiwa na aina hiyo ya mwanamke ni heri kukaa katika pembe ya dari, eneo ambalo utatulia kimyaa na utajisikilizia moyo wako kuliko kuwa na misiba kila wakati na majanga kila wakati!

Mungu alimkusudia mwanamke awe msaada mkubwa wa mumewe MSAIDIZI Neno Msaidizi limetumika pia kuelezea ukaribu wetu na msaada tunaoupata kutoka kwa Mungu ROHO MTAKATIFU  yeye hutusaidia, hujaziliza madhaifu yetu, hutushauri hutuombea na kuleta msaada mwingi, kututeteta na kututia nguvu,  kwa maana nyingine Mwanamke anatakiwa kuwa msaada Mkubwa kama alivyo Roho Mtakatifu katika maisha yetu, kama umeokoka unapojazwa Roho Mtakatifu unakuwa na ujasiri na unapokea nguvu ya ajabu na mambo mengi yanaonekana kurahisishwa hata ukipitia magumu kwa uwepo wa Roho Mtakatifu,  wanaume hawapaswi kufikia hatua ya kuamua kushinda ofisini, au kwenda kunywa kahawa na tangawizi mbali kama watakuwa na mwanamke mwenye kuvutia,  Mithali hii inatufunza kwamba Lugha na matumizi ya ulimi na udhibiti wa hisia kwa mwanamke ni jambo la maana sana mwanamke aliyepewa mume ni muhimu sana kwa mumewe, kwamba mumeo atakuelewa au hata kuelewa maneno yako ni ya muhimu sana na matendo yako pia wakati wote unapomkwaza mumeo na kuzungumza maneno ya kejeli na kumkatisha tamaa unamuharibu mumeo kabisa kabisa na kumbomoa mara 1000 kuliko mtu yeyote yule , sababu ya mtu yule kuona umuhimu wa kutulia katika pembe ya dari ni kwa sababu anajisikia kuumizwa, anajisikia vibaya anajisikia kuvnjika moyo, anakosa faraja ya kweli anaumizwa badala ya kupata faraja kutoka kwa mwanamke, kusema kweli amani katika nyumba na ndoa yoyote ile inaweza kupokea mabadiliko kama wanawake watajua nafasi zao, inawezekana ukawa unasoma hapa halafu ukasema mkuu wa wajenzi anasema tu huyu hajui aina ya mwanaume niliye naye! Angejua ! inawezekana kweli anakuudhi kweli ni kama hakufai lakini alikufaa mpaka mkaoana na kuchumbiana  najua kuwa kuna weza kuwa na maudhi ya hapa na pale lakini hapa Biblia inamtaka mwanamke  awe mtulivu, amtiii amtie moyo na awe na lugyha nzuri hii itamuondoa mumeo katika pembe ya dari, wengi waume zenu wako katika pembe ya dari, hawataki hata kuwasikiliza, wako tayari kusikiliza mpira na kuzungumza na wengine katika magroup ya mitandao ya kijamii wako tayari kuzungumza na wengine kwa lugha ya upole na ubembelezi lakini kwako wanasubiri kufyaua maneno kama risasi ili kujeruhiana, mimi nilikuwa nagombana sana na mke wangu mapaka wakati mwingine nikawa nimezoea maisha ya ugomvi, mpaka nikawa mchokozi nasubiri arushe neno moja tu nimtapikie mpaka anyauke ndio alinizoesha mwenyewe!, Lakini nataka nikuhakikishie mwanamke akibadilika akawa katika nafasi yake ya ulaini wa moyo, ulaini wa lugha ulaini wa ngozi ulaini wa sauti ulaini wa mapishi ulaini wa kujali ulaini wa kukupmkea ulaini wa kila kitu mwanamke akikaa katika uanawake kwelikweli Mwanaume atatoka gerezani, atatoka fgereji atatoka pangoni atatoka kazini atatoka kwenye mpira atatoka kanisani, atatioka kwenye jumuia atatoka kwenye simu na redio na television  ataondoka kwenye pembe ya dari na kuja kutulia na mkewe, haiwezekani nyumba iwe kama ina wanaume wawili ndani haiwezi kuwa nyumba yenye kufaa tafadhali wanawake kuweni wanawake kweli na sisi tutashuka darini na kuwasogelea!

Umuhimu wa kutunza amani ya moyo!

Mithali hii pia inatumika kama mafunzo kwa vijana hasa wale ambao hawajaoa inawakumbusha kuwa ni jambo baya sana kuwa peke yako, Upweke na kuwa mwenyewe ni jambo baya kimaandiko Biblia inasema si vema huyo mtu awe peke yake ona

Mwanzo 2;18 “BWANA Mungu akasema, Si vema huyo mtu awe peke yake, nitamfanyia msaidizi wa kufanana naye.”
ingawa sio vema mtu kuwa mpweke lakini ni mbaya zaidia kama utaona mwanamke mgomvi mwenye kelele, anayetajwa katika mithali hii, kwa hiyo mithali hii inakutaka ujiokoe mwenyewe kuoa mwanamke mgumu kunaweza kuleta huzuni kubwa zaidi kuliko unavyoweza kuwaza, usimkaribie kabisa mwanamke jeuri mwenye mijadala na asiyeweza kuzuia hisia zake, Kuna namna ambayo Mungu ameumba wanakwake na kuna namna neno la Mungu linavyomtarajia mwanamke awe Sulaimani ambaye amewahi kuwa na wanawake wengi aliowaoa anaandika mithali hiii akiwaonya wanaume kujihadhari na mwanamke wa aina hii, wanawake wengi wameharibu huduma za waume zao, maisha ya waume zao, kazi za waume zao heshima za waume zao kwa sababu ya tabia mbaya isiyokuwa ya kimaandiko

Mithali 12:4  Mwanamke mwema ni taji ya mumewe; Bali aaibishaye ni kama kuoza mifupani mwake.“

Mithali 14:1 “Kila mwanamke aliye na hekima hujenga nyumba yake; Bali aliye mpumbavu huibomoa kwa mikono yake mwenyewe”

Mithali 27:15-16  Kutona-tona daima siku ya mvua nyingi, Na mwanamke mgomvi ni sawasawa; Atakaye kumzuia huyo huuzuia upepo; Na mkono wake wa kuume hukuta mafuta.”

Mithali 30:21-23 “Kwa ajili ya mambo matatu nchi hutetemeka, Naam, kwa ajili ya manne haiwezi kuvumilia. Mtumwa apatapo kuwa mfalme; Mpumbavu ashibapo chakula;Mwanamke mwenye kuchukiza aolewapo; Na mjakazi aliye mrithi wa bibi yake.”
~
Mithali 31:10-12 “Mke mwema, ni nani awezaye kumwona? Maana kima chake chapita kima cha marijani. Moyo wa mumewe humwamini, Wala hatakosa kupata mapato.”

Mfalme Sulemani anaelewa anachokiandika alikuwa na wake 700 na masuria 300,  anajua namna mwanamke mkorofi anavyokua anaonya vijana kuwa makini unapofika wakati wa kufabnya maamuzi ya kuoa siku moja ya majuto na hasira za mwanamke inaweza kukuokoa wewe unayetaka kuoa, Ndoa inaweza kuwa kaburi  na ukajuta na kutamani kutoka na kuwa single tena kuwa na mwanamke mkorofi ni msalaba mkubwa sana  mwanamke mgomvi, mwanamke mwenye kukosoa kila kitu hana jema, mwanamke anayependa kugombana anayependa kukupinga anayependa kushindana nawewe, asiyeridhika na kitu chochote, mwenye maswali ya kila aina, mwenye kukukumbusha makosa ya nyuma, mwenye kisasi asiyesamehe, mwanamke mwenye kumlaani mumewe, asiyetia moyo asiye na adabu, mwenye kiburi mtawala Biblia inatoa maonyo kwamba ni afadhali kukaa kwenye pembe ya dari, mwanamke yeyote utakayeoa na ukagundua kuwa hali yako ya kiroho inaharibika baada ya kumpata, hali yako ya kuomba na kuabudu na upendo unaondoka na kuanza kuwa katili mwanamke anayekufabnya ujute kwanini umeaoa ? huyo ndio mwanamke ambaye biblia inasema hafai, huyu ni mwanamke asiyeweza kuitawala roho yake  anayependa kugombana na kusema leo na mimi nimemkomesha ukizungumza naye anazungumza ukimweleza anakuja juu, sauti yake inapanda kwa kiasi ambacho hata walio nje wanasikia mnavyozozana au anaweza kuwa na kiburi mpaka ukatamani umpige , mwanmake asiyetosheka aliyekinyume na kila kitu, na kila tukio na kuzungumzia vibaya kila kitu, mgumu, hawapendi hata ndugu zako, wakati wote yeye ni kulaumu kila kitu Mwanamke wa namna hiyo Biblia inasema hakufai na kwa vyovyote vila atakupeleka kwenye pembe ya dari,  hawa ni wanawake watawala kama utakuwa umeoa mwanamke wa aina hii utakuwa umechelewa kujiokoa na kifo na hasara vinakuhusu na ndio maana Sulemani anaonya kuwa wanaweza kuionekana kuwa nadhifu na wazuri wakati wa uchumba lakini utakapoingia kwenye agano naye umekwisha hawa kutokana na utawala wao wanaweza kukufanya ukashindwa hata kumudu tendo la ndoa, Maisha yako ni ya muhimu sana jifunze kutokana na maonyo, mke gani anashinda kwenye TV daima , mke gani anashinda anachati tu, simu jmemnunulia wewe, vocha unaweka wewe na simu hiyohiyo na vocha hiyo hiyo inatumika kukutukana jiokoe na maumivu, jiokoe na viumbe wa aina hiyo, ogopa maumivu ya maisha, mwanagalie mama yake ni mwanamke wa namna gani, waulize waliooa , kuwaa mwangalifu na kwanini uishi miaka karibu 50 na mtu atakayeshinda anakuumiza tu tunza amani ya moyo wako!

Mwanamke wa Kikristo anapaswa kujifunza na kuishi kwa upendo, na anapaswa kujua namna ya kujinyenyekeza kwa mumewe anajua nafasi yake kimaandiko

1Wakoritho 11:8-9 “Maana mwanamume hakutoka katika mwanamke, bali mwanamke katika mwanamume.Wala mwanamume hakuumbwa kwa ajili ya mwanamke, bali mwanamke kwa ajili ya mwanamume.
” Mwanaume hakuumbwa kwaajili ya mwanamke bali mwanamke kwaajili ya mwanaume hivyo mwanamke wa Kikristo anapaswa kujua wajibu wake anapaswa kuishi maisha ya kumpendeza mumewe ona

1Timotheo 2:13 “Kwa maana Adamu ndiye aliyeumbwa kwanza, na Hawa baadaye
” Mungu alimuumba mwanaume kwaajili yake na wala sio kwaajili ya mwanamke hivyo mwanamke wa kikristo anapaswa kuwa anayejipendekeza nakazia tena anayejipendekeza kwa mumewe, ni lazima wakati wote ahakikishe anajiweka vizuri anajaa neema ili aweze kuwa mwenye mvuto na mwenye kumpendeza mumewe

Mithali 11:16 “ Mwanamke wa adabu huheshimiwa daima; Na watu wakali hushika mali siku zote.
“ mwanamke ni adabu bwana ! mwanamke unyenyekevu jifunze kutoka kwa Abigaili  anajua kubembeleza mpaka mwanaume shujaa mwenye hasira anayetaka kuua anakuwa mpole huu ndio uzuri ambao wanaume wa kweli wanautafuta

1Samuel 25:21-35
Basi Daudi alikuwa amesema, Hakika ni bure nilivyokuwa nikilinda nyikani yote aliyo nayo mtu huyu, asipotewe na kitu cho chote cha mali yake yote; naye amenilipa mabaya badala ya mema. Mungu naye awafanyie hivyo adui za Daudi, na kuzidi, nikimwachia katika wote walio wake hata mtoto mume mmoja, kutakapopambazuka asubuhi. Ndipo hapo Abigaili alipomwona Daudi, alifanya haraka kushuka juu ya punda wake, akamwangukia Daudi kifulifuli, akainama mpaka nchi. Akamwangukia miguuni pake, akasema, Juu yangu, bwana wangu, juu yangu mimi na uwe uovu; tafadhali mjakazi wako na anene masikioni mwako, nawe uyasikilize maneno ya mjakazi wako. Nakusihi, bwana wangu, wewe usimwangalie huyu mtu asiyefaa, yaani, Nabali; kwa maana kama lilivyo jina lake ndivyo alivyo yeye; jina lake ndilo Nabali, na upumbavu anao; lakini mimi, mjakazi wako, sikuwaona hao vijana wa bwana wangu aliowatuma. Basi sasa, bwana wangu, aishivyo Bwana, na iishivyo nafsi yako, kwa kuwa Bwana amekuzuia usimwage damu, tena usijilipize kisasi mkono wako mwenyewe, basi sasa adui zako, na hao wamtakiao bwana wangu mabaya, wawe kama Nabali. Na sasa zawadi hii, mjakazi wako aliyomletea bwana wangu, na wapewe vijana wamfuatao bwana wangu. Nakuomba ulisamehe kosa lake mjakazi wako, kwa kuwa hakika Bwana atamfanyia bwana wangu nyumba iliyo imara, kwa sababu bwana wangu anavipiga vita vya Bwana; tena uovu hautaonekana ndani yako siku zako zote. Na hata ijapokuwa binadamu angeinuka akuwinde, na kuitafuta nafsi yako, hiyo nafsi ya bwana wangu itafungwa katika furushi ya uhai pamoja na Bwana, Mungu wako; na nafsi za adui zako ndizo atakazozitupa nje, kama kutoka kati ya teo.Tena itakuwa, hapo Bwana atakapokuwa amemtendea bwana wangu sawasawa na mema yote aliyoyanena juu yako, na kukutawaza juu ya Israeli; hili halitakuwa kwazo, wala chukizo la moyoni kwa bwana wangu, ama ya kuwa umemwaga damu bure, ama ya kuwa bwana wangu amejilipiza kisasi mwenyewe; tena hapo Bwana atakapokuwa amemtendea bwana wangu mema, ndipo umkumbuke mjakazi wako. Naye Daudi akamwambia Abigaili, Na ahimidiwe Bwana, Mungu wa Israeli, ambaye amekuleta hivi leo kunilaki; na ibarikiwe busara yako, na ubarikiwe wewe, uliyenizuia hivi leo nisimwage damu, wala kujilipiza kisasi kwa mkono wangu mwenyewe. Kwa kuwa ni kweli, aishivyo Bwana, Mungu wa Israeli, aliyenizuia nisikudhuru, kwamba hungefanya haraka kuja kunilaki, hakika huyu Nabali asingaliachiwa hata mtoto mume mmoja, kutakapopambazuka asubuhi. Basi Daudi akapokea mkononi mwake vitu vile alivyomletea; akamwambia, Haya! Kwea kwa amani kwenda nyumbani kwako; tazama, nimeisikiliza sauti yako, nami nimeukubali uso wako”. Wanawake wacha Mungu sio kuwa wanapendezwa na kufurahishwa na kila kitu kuhusu waume zao hapana wanawatii, wanawanyenyekea, wanawaheshimu wanatumia busara kuishi nao, hawashindani nao ndio biblia inavyoagiza

Waefeso5:22-24
Enyi wake, watiini waume zenu kama kumtii Bwana wetu.Kwa maana mume ni kichwa cha mkewe, kama Kristo naye ni kichwa cha Kanisa; naye ni mwokozi wa mwili.Lakini kama vile Kanisa limtiivyo Kristo vivyo hivyo wake nao wawatii waume zao katika kila jambo 

Tito 2:3-5  Vivyo hivyo na wazee wa kike wawe na mwenendo wa utakatifu; wasiwe wasingiziaji, wasiwe wenye kutumia mvinyo nyingi, bali wafundishao mema; ili wawatie wanawake vijana akili, wawapende waume zao, na kuwapenda watoto wao; na kuwa wenye kiasi, kuwa safi, kufanya kazi nyumbani mwao, kuwa wema, kuwatii waume zao wenyewe; ili neno la Mungu lisitukanwe.
” Wanawake wacha Mungu sio wagomvi wala jeuri  wanajua kuutumia ulimi wao ona

Mithali 31:26 “Hufumbua kinywa chake kwa hekima, Na sheria ya wema i katika ulimi wake.” 1Petro 3:1-4 “Kadhalika ninyi wake, watiini waume zenu; kusudi, ikiwa wako wasioliamini Neno, wavutwe kwa mwenendo wa wake zao, pasipo lile Neno; wakiutazama mwenendo wenu safi, na wa hofu.Kujipamba kwenu, kusiwe kujipamba kwa nje, yaani, kusuka nywele; na kujitia dhahabu, na kuvalia mavazi; bali kuwe utu wa moyoni usioonekana, katika mapambo yasiyoharibika; yaani, roho ya upole na utulivu, iliyo ya thamani kuu mbele za Mungu
.

Ni wajibu wa kila mzazi wa kikristo na mwenye kupenda uadilifu kumfunza mtoto wake wa kike nawa kiume namna anavyotakiwa kuwa kupitia Mithali za Suleimani kwenye mithali kuna hekina na maarifa na ujuzi utakaosaidia jamii katika maisha ya kawaida na ya kiroho, kila kijana ajifunze kuhusu mke mwema na kujua anapaswa kuoa mwanamke wa namna gani na kila mwanamke anapaswa kujivunza na kujikosoa au kumuiomba Mungu ambadilishe ili asimpeleke mumewe kwenye pembe ya dari kuna faida kubwa sana za kujifunza kupitia mithali za solomon

Rev. Innocent Kamote

Mkuu wa wajenzi Mwenye Hekima!

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni