Alhamisi, 25 Machi 2021

Kifo Katika Mpango wa Mungu!

Ayubu 14:5 “Kwa kuwa siku zake zimeamriwa, hesabu ya miezi yake unayo wewe, Nawe umemwekea mipaka yake asiyoweza kuipita;”


Utangulizi:

Kumekuwepo na mijadala mbalimbali, mitazamo na falsafa kuhusu kifo!, Baadhi wakiamini kuwa kila kifo ni mapenzi ya Mungu, wengine wanaamini kama Mungu akiamua usife huwezi kufa na akiamua ufe unakufa, na wengine wakiamini kuwa kila mwanadamu ana siku zake zilizoamriwa kuishi duniani na zikikamilika anaondoka, wengine wanaamini kuwa Mungu huwa anahuzunika sana mtu anapokufa kama sisi  nasi tunapohuzunika matukio ya kifo yanapotokea, lakini kwa sababu tunaishi katika ulimwengu wa dhambi Mungu huruhusu kifo kutokea Ni muhimu kufahamu kuwa ni neno la Mungu pekee yaani Biblia inayoweza kutupa majibu ya maswali yetu kuhusu kifo na maana halisi ya kifo kinapotokea! Lakini ni lazima kwanza tufahamu kuwa Mungu hapendi kuwatesa wanadamu wala kuwahuzunisha ona

 

Maombolezo 3:31-33 “Kwa kuwa Bwana hatamtupa mtu Hata milele. Maana ajapomhuzunisha atamrehemu, Kwa kadiri ya wingi wa huruma zake. Maana moyo wake hapendi kuwatesa wanadamu. Wala kuwahuzunisha.”

Kifo katika mpango wa Mungu!

Ni muhimu kufahamu kuwa Mungu katika mpango wake hakuwa amekusudia kifo kiwepo katika maisha ya mwanadamu, na ndio maana kwa asili hakuna mwanadamu anayekubali au kukipenda kifo kwa sababu kimsingi sio maumbile ya asili yetu Mungu alimuumba mwanadamu ili aishi milele na ndio maana kifo kimekuwa kinampa taabu sana mwanadamu kwa maana haukuwa mpango wala mapenzi kamili ya Mungu



Muhubiri 3:10-11 “Nimeiona taabu ambayo Mungu amewapa wanadamu, ili kutaabika ndani yake. Kila kitu amekifanya kizuri kwa wakati wake; tena ameiweka hiyo milele ndani ya mioyo yao; ila kwa jinsi mwanadamu asivyoweza kuivumbua kazi ya Mungu anayoifanya, tangu mwanzo hata mwisho.” 


Kifo na taabu zake kimekuja kama matokeo ya kuasi kwa mwanadamu, kwa hiyo Mungu alimuwekea mwanadamu uchaguzi kuchagua uzima au mauti kupitia kutii au kuasi na kwa bahati mbaya mwanadamu akaasi na hapo ndipo ilipokuja adhabu ya kifo ambayo Mungu alikuwa amemuonya nayo Adamu ona


Mwanzo 2:15-17 “BWANA Mungu akamtwaa huyo mtu, akamweka katika bustani ya Edeni, ailime na kuitunza. BWANA Mungu akamwagiza huyo mtu, akisema, Matunda ya kila mti wa bustani waweza kula, walakini matunda ya mti wa ujuzi wa mema na mabaya usile, kwa maana siku utakapokula matunda ya mti huo utakufa hakika.”


Kwa msingi huo kifo kipo Duniani leo kwa sababu ya kuasi kwa mwanadamu mmoja baba yetu Adamu na mama yetu Eva kwa sababu sisi tulikuwa viunoni mwao wakati wana wanaasi na kwa sababu hiyo wanadamu wote wanaonja mauti ona


Warumi 5:12 “Kwa hiyo, kama kwa mtu mmoja dhambi iliingia ulimwenguni, na kwa dhambi hiyo mauti; na hivyo mauti ikawafikia watu wote kwa sababu wote wamefanya dhambi;”


kwa hiyo kifo kiliingia ulimwenguni kwa sababu ya dhambi na kikawafikia watu wote kwa nini kwa sababu wote tulikuwa katika viuno vya wazazi hao kwa msingi huo tuwe wema au tuwe waovu ni lazima tutaionja mauti, Kama mwanadamu hangelifanya dhambi, muda wetu wa kutimiza makusudi ya Mungu Duniani ungekuwa kama umekamilika Mungu angetutwaa kwenda mbinguni kukaa naye bila kuonja mauti ona

Mwanzo 5:24 “Henoko akaenda pamoja na Mungu, naye akatoweka, maana Mungu alimtwaa


.” Huu ndio ulikuwa mpango kamili wa Mungu (Perfect will of God), kwa msingi huo kifo sio mpango kamili wa Mungu bali ni matokeo ya dhambi ambayo yameruhusiwa na Mungu (permissive will of God).sasa kifo kimekuwepo na Mungu aliandaa mpango mwingine wa kukikomesha wakati wa utimilifu wa dahari utakapowadia.

Je kila kifo kinachotokea ni mpango wa Mungu?

Swali hili linaweza kuwa na majibu NDIO na HAPANA kulingana na mazingira ya kifo chenyewe kwa mujibu wa neno la Mungu sio kila kifo kinachotokea ni mpango wa Mungu wala sio mapenzi yake kamili, Maandiko ynashuhudia wazi kuwa Mungu hapendi wala hafurahii kufa kwake mtu mwenye dhambi! Ona

Ezekiel 33:11 “Waambie, Kama mimi niishivyo, asema Bwana MUNGU, SIKUFURAHII kufa kwake mtu mwovu; bali aghairi mtu mwovu, na kuiacha njia yake mbaya, akaishi. Ghairini, ghairini, mkaache njia zenu mbaya; mbona mnataka kufa, Enyi nyumba ya Israeli?


kwa hiyo kumbe linapokuja swala la Mtu kufa Mungu hapendi afe mtu mwenye dhambi, Mungu hafurahii kufa kwake mtu muovu, Mungu anatamani mtu awe ametubu, awe amegeuka na kuacha njia mbaya kabla ya kifo ili waweze kuungana naye, haya ndio mapenzi kamili kwa kila mwanadamu na ndio maana wakati mwingine Mungu huwaacha waovu kwa kitambo na kuwavumilia ili yamkini ikiwezekana wafikie wakati wa kutubu ona


2Petro 3:9 “. Bwana hakawii kuitimiza ahadi yake, Kama wengine wanavyokudhani kukawia, bali huvumilia kwenu, maana HAPENDI mtu ye yote apotee, bali wote wafikilie toba”.


kwa hiyo Mungu hapendi, na hafurahii na hivyo kuna nyakati huwacheklewesha waovu wasife kwa haraka au wasife kabla hawajafikia toba, kwa hiyo kuna mazingira ambayo kwayo Mungu hatafurahia au hafurahii kufa kwa mtu hususani mtu mwenye dhambi. Kwa hiyo Mungu husubiri mtu aifikie toba mtu ageuke na kuiacha njia yake mbaya

Hata hivyo kifo ni kanuni, ni kanuni ya adhabu kwa kitokumtii Mungu, kifo kama kanuni ya adhabu ya kutokumtii Mungu ni hitimisho la hatua kadhaa zisizochukuliwa katika hatua ya dhambi, angalia andiko hili kwa mfano


Yakobo 1:14-15 “Lakini kila mmoja hujaribiwa na tamaa yake mwenyewe huku akivutwa na kudanganywa. Halafu ile tamaa ikiisha kuchukua mimba huzaa dhambi, na ile dhambi ikiisha kukomaa huzaa mauti.”


Kanuni ya kifo ni dhambi kuna namna ambavyo Mungu katika hekima yake anakiruhusu kifo kwa nafi yenye dhambi, japo kifo sio mapenzi yake kamili lakini ni mshahara wa dhambi kwa hiyo kama nafsi itajaribiwa dhambini na kukawia kufanya toba na kwa bahati mbaya hatuwezi kujua muda ambao Mungu anatupa wa toba kanini ya kifo ambayo ni dhambi ikikomaa inaleta mauti kwa hiyio Mungu pia huruhusu mtu kufa endapo nafsi ya mtu huyo itatenda dhambi ona mfano


Ezekiel 18:20-23 “Roho itendayo dhambi, ndiyo itakayokufa; mwana hatauchukua uovu wa baba yake, wala baba hatauchukua uovu wa mwanawe, haki yake mwenye haki itakuwa juu yake, na uovu wake mwenye uovu utakuwa juu yake. Lakini mtu mbaya akighairi, na kuacha dhambi zake zote alizozitenda, na kuzishika amri zangu zote, na kutenda yaliyo halali na haki, hakika ataishi, hatakufa. Dhambi zake zote alizozitenda hazitakumbukwa juu yake hata mojawapo; katika haki yake aliyoitenda ataishi. Je! Mimi ninafurahia kufa kwake mtu mwovu? Asema Bwana MUNGU; si afadhali kwamba aghairi, na kuiacha njia yake, akaishi?” 


Unaona hivyo basi kutokana na kanuni Fulani za dhambi zinapoendelea kutendwa na nafsi basi Mungu huweza kuruhusu Dhambi hiyo kusababisha kifo na kukatiza uhai wa nafsi husika kwa ain azote za uzima huu na ule ujao 


Kutoka 21:14,-16 “Lakini, mtu akimwendea mwenziwe kwa kujikinai, kusudi apate kumwua kwa hila; huyo utamwondoa hata madhabahuni pangu, auawe. Ampigaye baba yake au mama yake, sharti atauawa.Yeye amwibaye mtu, na kumwuza, au akipatikana mkononi mwake, sharti atauawa huyoKatika mazingira kama kifo kinachotokea hapa ni mpango wa Mungu katika mantiki kwamba uovu umepelekea kufa, tama imepelekea nafsi itendayo dhambi kufa, kwa hiyo sio mapenzi ya Mungu mtu kufia katika dhambi, lakini ni mwanadamu anapokuwa na ukaidi Fulani kinyume na amri za Mungu mungu huruhusu mtu huyo kufa. Kwa hiyo yako mazingira jibu linaweza kuwa ndio na yako mazingira jibu linaweza kuwa sio!

Kwa mfano sio mapenzi ya Mungu kwa watoto wasiowahehimu wazazi wao kufa kabla ya wakati ona Waefeso 6:1-3 “Enyi watoto, watiini wazazi wenu katika Bwana, maana hii ndiyo haki. Waheshimu baba yako na mama yako; amri hii ndiyo amri ya kwanza yenye ahadi, Upate heri, ukae siku nyingi katika dunia.” Kumbe ni mapenzi ya Mungu kwamba watoto wawaheshimu wazazi wao ili siku zao zipate kuwa nyingi tena na za heri duniani, Lakini mtoto ambaye atamlaani baba yake au mama yake Mungu ameamuru apigwe kwa mawe mpaka kufa, kwa lugha nyingine maisha ya mtoto asiyewaheshimu wazazi yatafupishwa 


Kutoka 21:15, 17 “Ampigaye baba yake au mama yake, sharti atauawa. Yeye amwapizaye baba yake au mama yake, sharti atauawa.” kwa hiyo ni wazi kuna mazingira ya aina fulani Mungu hataki mtu afe kwa dhambi na kuna mazingira fulani Mungu huruhusu mtu afe kwa sababu ya dhambi.

Je Mungu hujisikiaje wanapokufa watu wengi?

Swala lingine nyeti ni je Mungu hujisikiaje wanapokufa watu kwa wingi? Kimaandiko bado Mungu huuzunishwa sana wanapokufa watu wengi wakiwa dhambini, Mungu huuzunishwa dhambi inapozidi na hivyo huweza kuruhusu maangamizi mfano 


Mwanzo 6:5-7 “BWANA akaona ya kuwa maovu ya mwanadamu ni makubwa duniani na kwamba kila kusudi analowaza moyoni mwake ni baya tu sikuzote. BWANA akaghairi kwa kuwa amemfanya mwanadamu duniani, akahuzunika moyo. BWANA akasema, Nitamfutilia mbali mwanadamu niliyemwumba usoni pa nchi; mwanadamu na mnyama, na kitambaacho na ndege wa angani; kwa maana naghairi ya kwamba nimewafanya.” 


Wakati wa Nuhu Mungu aliufutilia ulimwengu kwa gharika kwa sababu ya kuongezeka kwa maasi, kimsingi Mungu hafurahii udhalimu na uovu unaofanywa na watu, hapendi watu wafe lakini dhambi hupelekea Mungu kuruhusu vifo.


Dunia inaweza kukabiliwa na majanga kama watu hawatatubu, mji au nchi au taifa kama halitamjali Mungu Mungu anaweza kuachilia roho ya mauti ikafanya kazi yake na kuleta madhara kwa watu wema na wabaya wote wakaathirika kutokana na ule ukaidi wa kibinadamu wa kufa kwa dhamiri na kutaka kuendelea kuishi katika maisha ya dhambi ona 


Mwanzo 18:20 “BWANA akasema, Kwa kuwa kilio cha Sodoma na Gomora kimezidi, na dhambi zao zimeongezeka sana,” 

Dhuluma na uharibifu wa dhambi uliofanywa na watu wa Sodoma na Gomora ulimsukuma Mungu kuruhusu miji hiyo kuangamizwa kwa wingi wao, Kimsingi watu wengi wa mji au taifa wanapomgeukia Mungu na kuomba rehema zake kwa toba na kuacha njia yao mbaya Mungu huwarehemu watu hao ona 

Yona 3:11-10 “Neno la Bwana likamjia Yona mara ya pili, kusema, Ondoka, uende Ninawi, mji ule mkubwa; ukaihubiri habari nitakayokuamuru. Basi Yona akaondoka, akaenda Ninawi, kama Bwana alivyonena. Basi Ninawi ulikuwa mji mkubwa mno, ukubwa wake mwendo wa siku tatu. Yona akaanza kuuingia mji mwendo wa siku moja, akapaza sauti yake, akasema, Baada ya siku arobaini Ninawi utaangamizwa. Basi watu wa Ninawi wakamsadiki Mungu; wakatangaza kufunga, wakajivika nguo za magunia, tangu yeye aliye mkubwa hata aliye mdogo. Habari ikamfikia mfalme wa Ninawi, naye akaondoka katika kiti chake cha enzi, akavua vazi lake, akajivika nguo za magunia, na kuketi katika majivu. Naye akapiga mbiu, akatangaza habari katika mji wa Ninawi, kwa amri ya mfalme na wakuu wake; kusema, Mwanadamu asionje kitu, wala mnyama wala makundi ya ng'ombe, wala makundi ya kondoo; wasile, wala wasinywe maji; bali na wafunikwe nguo za magunia, mwanadamu na mnyama pia, nao wakamlilie Mungu kwa nguvu, naam, na wageuke, kila mtu akaache njia yake mbaya, na udhalimu ulio mikononi mwake. Ni nani ajuaye kwamba Mungu hatageuka na kughairi, na kuiacha hasira yake kali, ili msiangamizwe? Mungu akaona matendo yao, ya kuwa wameiacha njia yao mbaya. Basi Mungu akalighairi neno lile baya, ambalo alisema atawatenda; asilitende.” 


 Ni wazi kuwa Ninawi ulikuwa mji mkubwa yaani wenye watu wengi na waliishi maisha ya dhambi na dhambi hiyo ilifikia mstari wa kuwaletea mauti lakini walipogeuka na kutubu Mungu aliwasamehe na kifo kikaahirishwa kwao, hii ni ahadi ya Mungu kwa miji yoye, nchi zote na mataifa yote ya kuwa watu wafikilie toba na kuwa watu wakigeuka kuacha njia zao mbaya Rehema za Mungu zitakuwa juu ya watu hao ona 


2Nyakati 7:13-14 “Nikizifunga mbingu isiwe mvua, tena nikiamuru nzige kula nchi, au nikiwapelekea watu wangu tauni; ikiwa watu wangu, walioitwa kwa jina langu, watajinyenyekesha, na kuomba, na kunitafuta uso, na kuziacha njia zao mbaya; basi, nitasikia toka mbinguni, na kuwasamehe dhambi yao, na kuiponya nchi yao.” Kumbe basi yanapotokea majanga ya aina mbalimbali, na matukio yenye kuua watu wengi na matukio mengone ya asili yanayodhuru wanadamu na kuumiza wengi haimaanishi tu kuwa watu wale wanaweza kuwa waovu kuliko wale wanaobaki salama lakini kwa Mungu wakati wote matukio hayo yanakuwa ni wito wa toba kwa watu wote wapate kumgeukia Mungu ona 


Luka 13:1-5 “Na wakati uo huo walikuwapo watu waliompasha habari ya Wagalilaya wale ambao Pilato alichanganya damu yao na dhabihu zao. Akawajibu akawaambia, Je! Mwadhani ya kwamba Wagalilaya hao walikuwa wenye dhambi kuliko Wagalilaya wote, hata wakapatwa na mambo hayo? Nawaambia, Sivyo; lakini msipotubu, ninyi nyote mtaangamia vivyo hivyo. Au wale kumi na wanane, walioangukiwa na mnara huko Siloamu, ukawaua, mwadhani ya kwamba wao walikuwa wakosaji kuliko watu wote waliokaa Yerusalemu? Nawaambia, Sivyo; lakini msipotubu, ninyi nyote mtaangamia vivyo hivyo.” 


Kwahiyo hata yanapotokea majanga katika upande wa Mungu inabaki vilevile Mungu hafurahii kufa kwa wenye dhambi na angepeda wafikie toba lakini ni wazi kwetu kuwa yanapotokea majanga na kuchukua watu wengi, sisi tunaosalia hatuna budi kukaa katika toba na kuacha njia mbaya tukikumbuka kuwa wale walioangamia sio kuwa walikuwa wabaya kuliko sisi.                            

Heri wafu wafao katika Bwana !

Ufunuo 14:13 “Nikasikia sauti kutoka mbinguni ikisema, Andika, Heri wafu wafao katika Bwana tangu sasa. Naam, asema Roho, wapate kupumzika baada ya taabu zao; kwa kuwa matendo yao yafuatana nao.”

Kifo ni jambo la kuhuzunisha sana lakini ni tamko la Mungu, kwa hiyo Mungu hawezi kuwa kinyume na neno lake kwa sababu hiyo kifo kitamchukua mtu awaye yote mwema au muovu, kwa wakati wake ambao Mungu ameukusudia chini ya Mbingu, Yesu alipokuwa duniani alidhihirisha kuwa anahuzunishwa na kufa mtu tena hata wale waliokuwa rafiki zake ona Yohana 11:35 “Yesu akalia machozi.” Yesu alilia kwa sababu alihuzunishwa na kifo cha mtu wa karibu na rafiki yake yaani maana yake anahuzunishwa na kila mtu anayemuamini na anayeishi maisha ya haki bila kujali mtu huyo amekufa katika umri wa namna gani. Lakini Maandiko yanaeleza kuwa Heri wafu wafao katika Bwana yaani bila kujali umri au miaka lakini kama mtu huyo amekufa akiwa na imani katima Mungu akiamini kuwa yesu ni Bwana mtu huyo ana Baraka kubwa sana na maandiko yanaonyesha kuwa anapata pumziko baada ya taabu

Kwa sili andiko hilo ni matokeo ya maonyo kwa watu waovu ambao maandiko yanaonyesha kuwa wao wanapokufa hawatakuwa na nafasi ya kupumzika na badala yake watapata taabu sana Ufunuo 14:11 “Na moshi wa maumivu yao hupanda juu hata milele na milele, wala hawana raha mchana wala usiku, hao wamsujuduo huyo mnyama na sanamu yake, na kila aipokeaye chapa ya jina lake.”


Maandiko hayo yanaonyesha kwa asili wale watakaokufa wakati wa dhiki kuu, na tofauti yake kati ya wale watakaokufa kwa imani na wale watakaokuwa wamemuabudu mpinga kristo, Lakini maandiko hayo kuwa katika muktadha wa nyakati za dhiki kuu, hayaachi uole ukweli ulio wazi wa hata sasa kwamba wale wanaomuamini Yesu watapata raha na wale wasiomuamini watapata taabu sana kwani hayo ni matokeo yanayotokea haraka sana mara mtu anapokufa na aina ya maisha aliyoishi huamua hatima ya maisha yake ya umilele mara moja baada ya kufa ona Waebrania 9:27 “Na kama vile watu wanavyowekewa kufa mara moja, na baada ya kufa hukumu;” Maandiko ynaonyesha wazi kuwa mara baada ya kufa hukumu hujitokeza pale pale kwa aidha kwenda katika raha au kwenda katika mateso mtu aliyemuamini Bwana Yesu anasamehewa na kuwanywa kuwa kiumbe kipya 2Wakoritho 5:17 “Hata imekuwa, mtu akiwa ndani ya Kristo amekuwa kiumbe kipya; ya kale yamepita tazama! Yamekuwa mapya.” Watu hawa ambao neema ya Mungu imefunuliwa kwao watapata raha nafsini mwao kama maandiko yasemavyo Mathayo 11:28-29. Kwa hiyo anapokufa mtu mcha Mungu Mungu hufurahia anahuzunika anapoona wale walioko duniani wanalia na wanahuzunika na huhuzunika pamoja nao lakini mtu wa Mungu anapokufa kuna faidha kubwa sana na Mungu hufurahia mauti yake maandiko yanatuambia ina thamani kama nini mauti ya wacha Mungu wake ona Zaburi 116:15 “Ina thamani machoni pa Bwana Mauti ya wacha Mungu wake.” Haijalishi mtu wa Mungu atakufa katika mazingira ya aijna gani vyovyote vile kama Mungu ameruhusu mauti hiyo ina thamani kubwa sana mbele za Mungu aliyekuwa Askofu wa Antiokia aliuawa wakati wa mateso ya Decian askofu huyu ambaye katika historia ya kanisa aliitwa Babylas alikufa akiwa anaimba zaburi hii ina thamani machoni pa Bwana Mauti ya wacha Mungu wake!, Mtume Paulo aliungana na wazo kama hili kuhusu mauti ya mtu wa Mungu yeye alihesabu hivi kwake yaani kwa mtu kama yeye kuishi ni Kristo na kufa ni faida ona 


Wafilipi 1:21-24 21.Kwa maana kwangu mimi kuishi ni Kristo, na kufa ni faida. Ila ikiwa kuishi katika mwili, kwangu mimi ni matunda ya kazi; basi nitakalolichagua silitambui. Ninasongwa katikati ya mambo mawili; ninatamani kwenda zangu nikae na Kristo maana ni vizuri zaidi sana; bali kudumu katika mwili kwahitajiwa zaidi kwa ajili yenu” kumbe basi kufa katika imani kwa mtu wa Mungu na kwa watu wema ni busara ya Mungu ambaye anakwenda kuwapumzisha na kukaa pamoja na wao, bila kujali ni mazingira gani anakuchukua nani katika umri gani anakuchukua kwa msingi huo kwa uelewa mwembamba kifo ni kupoteza katika akili za kibinadamu na hasa anapokufa mtu mwema lakini kwa uelewa mpana kifo cha mtu mwema kina thamani kubwa sana kwa Mungu, Mara kadhaa wakati mwingine nimeshangazwa na Kocha wa mpira wa miguu anaweza kumtoa mtu ambaye amefunga magoli mengi siku hiyo au mwenye uchu wa kufunga zaidi, na ukatamani aendelee kucheza kwa vile unakuwa na matumaini naye lakini unashangaa kocha anamtoa! Unaweza kumtukana au kumlaumu lakini kwa nini anatolewa kocha ndiye anayejua Katika Biblia kama kuna mtu binafsi nisingelipenda Mungu amchukue Mapema ni Stefano mimi nahizi kuwa angakuwa muhubiri mkubwa na alikuwa ni mtu muhimu, mitume walimtegemea sana na alikuwa na uwezo wa juu sana kulitetea kanisa lakini Mungu kama Mungu aliruhusu Stefano auawe kwa kupigwa mawe na kuwa mtu wa kwanza kuifia Imani, hivyo wakati mwingine Mungu hufanya mambo kama apendavyo yeye na hata hivyo wanatheolojia wanajua faida ya kifo cha Stefano lakini pia tunaijua Furaha ya Yesu aliyesimama kumpokea Stefano!

Je mtu akifa ni kweli kuwa siku yake imefika?

Tumewasikia watu mara kadhaa wakisema mara baada ya mtu kufa kuwa siku yake imefika, au amemaliza kazi iliyokusudiwa au siku yako ikifika bwana hakuna cha kuzia na kadhalika na kadhalika je Mungu amekusudia mwanadamu awe na wakati Fulani muafaka wa kuishi? Je kuna uwezekano wa siku kufupizwa au kuongezwa na nini faida zake na makusudi yake? Maandiko yanatufundisha wazi kuwa kwaajili ya dhambi umri wa kuishi mwanadamu umefupizwa ona Mwanzo 6:1-3 “Ikawa wanadamu walipoanza kuzidi usoni pa nchi na wana wa kike walizaliwa kwao, wana wa Mungu waliwaona hao binti za wanadamu ya kuwa ni wazuri; wakajitwalia wake wo wote waliowachagua. BWANA akasema, Roho yangu haitashindana na mwanadamu milele, kwa kuwa yeye naye ni nyama; basi siku zake zitakuwa miaka mia na ishirini.              


Mwanzoni wanadamu waliweza kuishi hata karne 9 yaani miaka mia tisa na kitu na mwanadamu aliyepata kuishi miaka mingi zaidi aliitwa Methusela yeye aliishi miaka 969 katika rekodi za Biblia ona Mwanzo 5:27 “Siku zote za Methusela ni miaka mia kenda na sitini na kenda, akafa.” Kutokana na kuongezeka kwa maasi duniani Mungu aliipunguza miaka ya kuishi mwanadamu na kuwa 120 kama tuonavyo katika maandiko, hivyo 120 ndio kiwango cha wastani wa juu zaidi ambao mwanadamu anaweza kuishi, Wakati wana wa Israel wakiwa Jangwani kutokana na kuasi kwao mara kwa mara Mungu aliwapunguzia wao wana wa Israel Miaka ya kuishi hususani wale walikuwa jangwani wakati wa Musa na miaka yao ikakadiriwa kuwa kati ya 70-80 ona Zaburi 90:10 “Siku za miaka yetu ni miaka sabini, Na ikiwa tuna nguvu miaka themanini; Na kiburi chake ni taabu na ubatili, Maana chapita upesi tukatokomea mara.” Musa aliyasema maneno hayo wakati wa hukumu ya wana wa Israel ambao walikuwa wanakufa jangwani kwa sababu ya kutokumuamini Mungu, lakini kibiblia swala la msingi linabakia kuwa wastani wa mwanadamu kuishi ni kati ya miaka “70-120” hata hivyo hii haimaanishi kuwa ni lazima mwanadamu afiikishe miaka hiyo au kwamba anayekufa chini ya umri huo ni muovu hapana hata kidogo bado maisha ya mwanadamu yanabaki kuwa katika mipaka aliyoiweka Mungu! Kama itafikiriwa kuwa mtu akifa chini ya umri huo amekufa kijana basin i vema kuyafikiri maisha ya Yesu ambaye alipokuwa duniani aliishi miaka 33 tu, au kufikiri maisha ya Nabii Yohana mbatizaji ambaye aliishi miaka 30 tu na akauaawa! Ni Mungu tu ndiye anayejua kwanini na lini kifo kitokee kwa mtu kwa sababu zake mwenyewe, siku za mwanadamu za kuishi kwa ujumla sio nyingi kama hata kama mtu ataishi 120 bado ni siku zenye kupita haraka mno. Kwa mujibu wa maandiko 

Ayubu 14:1-2 “Mwanadamu aliyezaliwa na mwanamke Siku zake za kuishi si nyingi, naye hujaa taabu. Yeye huchanua kama vile ua, kisha hukatwa; Hukimbia kama kivuli, wala hakai kamwe” mwandishi mwingine wa Biblia anayafananisha maisha ya mwanadamu kama vile maua, maua na majani ndio mfano wa vitu vyenye muda mfuoi sana wa kuishi, ni kama wanasema muda tuliopewa ni mdogo sana ona 

Zaburi 103:15 “Mwanadamu siku zake zi kama majani; Kama ua la kondeni ndivyo asitawivyo.” Pia maisha ya mwanadamu yanafananishwa na kivuli yaani kitu kinachopita na kutoweka kwa haraka sana Zaburi 144:4 “Binadamu amefanana na ubatili, Siku zake ni kama kivuli kipitacho.” 

Katika namna ya kibinadamu wengi tunaweza kufikiri kuwa maisha ya duniani ni matamu sana lakini kwa Mungu katika uwepo wake ndio kuzuri zaidi, Mungu amepangilia na kuweka mipaka katika maisha ya mwanadamu kwamba ukifika wakati huo aliouweka mwanadamu ataondoka tu kwa sababu siku zake zimeamriwa zimeratibiwa ziko programed kwamba huyu zitakuwa hizi tu 


Ayubu 14:5 “Kwa kuwa siku zake zimeamriwa, hesabu ya miezi yake unayo wewe, Nawe umemwekea mipaka yake asiyoweza kuipita;kwa hiyo iko wazi kuwa Mungu ameweka mpaka katika maisha yetu ambao huo hatuwezi kuuvuka iwe tuna pesa kiasi gani, wema kiasi gani na kadhalika aidha pia Mungu huweza kuitimiza ile iliyokusudiwa au kuipunguza maika iliyokusudiwa kwa wanadamu kwa sababu zake na kanuni zake mfano 


Kutoka 23:25-26 “Nanyi mtamtumikia BWANA, Mungu wenu, naye atakibarikia chakula chako, na maji yako; nami nitakuondolea ugonjwa kati yako. Hapatakuwa na mwenye kuharibu mimba, wala aliye tasa, katika nchi yako; na hesabu ya siku zako nitaitimiza.” Aidha Mungu anaweza kuhakikisha kuwa miaka iliyokusudiwa kwa mtu inatimizwa au anaweza kuiongeza lakini pia anaweza kuipunguza kutokana na kanuni mbalimbali za maisha na neno lake mfano Mithali 10:27 “Kumcha Bwana kwaongeza siku za mtu; Bali miaka yao wasio haki itapunguzwa.         


Kila mwanadamu anatamani sana kuishi muda mrefu sana lakini wakati mwingine Mungu hutuepusha na mambo kadhaa na dhiki au mambo mabaya ambayo yeye hangependa ukumbane nayo Hezekia alikuwa moja ya wafalme wazuri ambaye Mungu alitaka kumchukua mapema lakini aliomba Mungu amuongezee muda wa kuishi na Mungu alimuongezea muda wa miaka 15 2Wafalme 20:1-6 “Siku hizo Hezekia akaugua, akawa katika hatari ya kufa. Isaya, nabii, mwana wa Amozi, akamjia akamwambia, Bwana asema hivi, Tengeza mambo ya nyumba yako; maana utakufa, wala hutapona. Basi Hezekia akajigeuza, akaelekeza uso wake ukutani, akamwomba Bwana akasema,Nakusihi, Bwana, ukumbuke sasa, jinsi nilivyokwenda mbele zako katika kweli na kwa moyo mkamilifu, na kutenda yaliyo mema machoni pako. Hezekia akalia sana sana. Ikawa, kabla Isaya hajatoka katika mji wa kati, neno la Bwana likamjia, kusema, Rudi, ukamwambie Hezekia, mkuu wa watu wangu, Bwana, Mungu wa Daudi baba yako asema hivi, Nimeyasikia maombi yako, na kuyaona machozi yako; tazama, nitakuponya; siku ya tatu utapanda nyumbani kwa Bwana. Tena, nitazizidisha siku zako, kiasi cha miaka kumi na mitano, nami nitakuokoa wewe, na mji huu, na mkono wa mfalme wa Ashuru, nami nitaulinda mji huu kwa ajili yangu, na kwa ajili ya Daudi, mtumishi wangu.” 


Hata hivyo jambo la kushangaza ni kuwa baada ya miaka hiyo ya nyongeza Hezekia alipata mtoto na ambaye aliwaongoza watu kufanya mambo mabaya sana na kufanya machukizo mabaya zaidi ambayo hata baba yake angalikuwa hai asingeliweza kuyavumilia mauozo hayo ona 2Wafalme 21:9 “Walakini hawakusikia; naye Manase akawakosesha wafanye mabaya, kuliko mataifa Bwana aliowaharibu mbele za wana wa Israeli.” 

Ni kama kusema afadhali Hezekia angelikubali kwenda kwa bwana wakati wake ulipofika kuliko miaka aliyoongezwa. Wakati mwingine Mungu katika hekima yake hufanya mambo kwa manufaa makubwa sana anayoyajua mwenyewe kwaajili ya hayo ni vigumu kumuuliza Mungu kwanini, kwanini hili litokee, lakini tunapaswa kumshukuru Mungu kwa kila jambo na kutokumkufuru Mungu linapofanyika tukio lenmye kushangaza tuendelee kumuamini yeye katika njia zake zote na tusizitegemee akili zetu wenyewe 

Mithali 3:5-6 “Mtumaini Bwana kwa moyo wako wote, Wala usizitegemee akili zako mwenyewe; Katika njia zako zote mkiri yeye, Naye atayanyosha mapito yako.” Wakati mwingine Mungu anaweza kumchukua mtu mwema akapumzike nyumbani kwa kusudi la kumuepusha na machukizo ya aina Fulani bila kujali njia itakayotumika kwa kuondoka kwake, 


Isaya 57:1 “Mwenye haki hupotea, wala hakuna atiaye hayo moyoni; na watu watauwa huondolewa, wala hakuna afikiriye ya kuwa mwenye haki ameondolewa asipatikane na mabaya.” Mungu anaweza kumchukua mtu ili kumuepusha na mabaya au maumivu makali au ulemavu, au kupooza na maswala mengine mengi,Jambo kubwa la msingi ni kila mmoja kuwa tayari kwa kifo wakati wowote tangu siku unapozaliwa Hata hivyo Yesu Ndiye mwenye funguo yaani mamlaka na kifo na hivyo hutaweza kuondoka mpaka Mungu ameruhusu Shetania anaweza kutujaribu kwa kiwangochochote kile lakini hana ruhusa kuondoa uhai wetu mpaka Mungu mwenyewe afanye hivyo 


Ayubu 2:6 “Bwana akamwambia Shetani, Tazama, yeye yumo mkononi mwako; lakini tunza tu uhai wake” Ufunuo 1:17-18 “Nami nilipomwona, nalianguka miguuni pake kama mtu aliyekufa. Akaweka mkono wake wa kuume juu yangu, akisema, Usiogope, Mimi ni wa kwanza na wa mwisho, na aliye hai; nami nalikuwa nimekufa, na tazama, ni hai hata milele na milele. Nami ninazo funguo za mauti, na za kuzimu.”        

Adui wa mwishio atakayeangamizwa ni kifo:

1Wakoritho 15:26  Adui wa mwisho atakayebatilishwa ni mautiHatimaye Yesu Kristo ambaye ana mamlaka dhidi ya kifo na mauti na ambaye alionja mauti ya msalabani na kuishinda kwa kufufuka siku ya tatu mwisho wa dahari atambatilisha adui huyu ambaye amekuwa akisumbua kili zetu na kutuchukulia wapendwa wetu na kutuondolea tumaini duniani na kutufanya tuione dunia kuwa haina maana na ni batili na kutukatisha tamaa na kutufanya tuishi kwa hofu,  habari njema ni kuwa Mungu ataibatilisha mauti yaani kifo na hakitakuwepo tena mjadala wake utafungwa na Mungu mwenyewe kwa kutupa uzima wa milele na kujibu maswali yote ya msingi kuhusu Kifo, kwa sasa kifo ni siri ya ajabu, na Mungu ndiye aijuaye.

Rev. Innocent Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni