Jumatatu, 26 Julai 2021

Ilikuwa vile ili iwe hivi!

Mwanzo 50:19-20 “Yusufu akawaambia, Msiogope, je! Mimi ni badala ya Mungu? Nanyi kweli mlinikusudia mabaya, bali Mungu aliyakusudia kuwa mema, ili itokee kuokoa taifa kubwa, kama ilivyo leo.”


Utangulizi:

Je umewahi kutokewa na jambo gani baya duniani ambalo hutaweza kulisahau katika maisha yako? Ukiulizwa swali hili unaweza kutokwa na machozi na kujibu ni habari ndefu sana ndugu yangu, na unaweza kuvuta Pumzi na kuwa tayari sasa kusimulia yaliyokusibu!

Leo nataka kukuambia wazi kuwa hakuna jambo linoalotutokea Duniani liwe jema au baya ambalo linaweza kuzuia kusudi la Mungu ndani yako, Kusudi la Mungu ndani yako haliwezi kuzuilika.  Ayubu 42:2 “Najua ya kuwa waweza kufanya mambo yote, Na ya kuwa makusudi yako hayawezi kuzuilika.” Mungu huweza kuitumia njia yoyote ile hata nia mbaya za watu kwa kusudi la kutuleta katika jambo jema, Hilo tunalijua! Tunajua kuwa njia za Mungu ziko juu sana kuliko mawazo ya kibinadamu, tunafahamu kuwa upumbavu wa Mungu una hekima kuliko uweza, ujuzi, ufahamu na maarifa ya kibinadamu

Warumi 8:28-30 “Nasi twajua ya kuwa katika mambo yote Mungu hufanya kazi pamoja na wale wampendao katika kuwapatia mema, yaani, wale walioitwa kwa kusudi lake. Maana wale aliowajua tangu asili, aliwachagua tangu asili wafananishwe na mfano wa Mwana wake, ili yeye awe mzaliwa wa kwanza miongoni mwa ndugu wengi. Na wale aliowachagua tangu asili, hao akawaita; na wale aliowaita, hao akawahesabia haki; na wale aliowahesabia haki, hao akawatukuza.”

Kila linalokutokea duniani hata kama linaonekana kuwa baya kwa wakati huo, ila ukakumbuka kuwa uko katika kusudi la Kiungu, basi ni vema ukafahamu kuwa Mungu yuko pamoja nawe hata katika hayo magumu unayoyapitia ili hatimaye aweze kuleta jambo jema, aweze kutokeza jambo zuri kwa utukufu wake  hata kama hujui kwa sasa, baadaye utakubaliana nami kuwa ilikuwa vile ili iwe hivi!

Ilikuwa vile ili iwe hivi!               

Mfalme mmoja alikuwa na punda wake amba0 aliwapenda sana, ikawa siku moja punda hao walidumbukia kwenye shimo kubwa sana ambalo ilikuwa ni vugumu kuwatoa, basi alijaribu kila njia lakini njia zote zilishindikana, hatimaye kwa masikitiko makubwa na kwa hasira aliamua kwamba atawazika punda wale katika shimo lile, hivyo aliagiza watumwa wake walete udongo na kuwafukia punda wale katika shimo lile wakiwa hai!

Kazi ya kuwazika Punda wakiwa hai ilianza watumwa walichimba udongo na kuusombelea kwa kusudi la kuwafukia punda wale, na kazi hiyo ikaaanza na kuendelea, hata hivyo bila watumwa wale kuelewa Punda wale kila walivyokuwa wakimwagiwa udongo wao walikuwa wakijikung’uta madongo yale  na hali hiyo iliendela mpaka shimo lile likajaaa na kumbe katika hali ya kushangaza punda wale walijikuta wanakuwa juu ya udogo uliokuwa umekusudiwa wazikwe na waliokuwa wakijikung’uta hivyo walijikuta juu ya shimo lililokuwa limejaa udongo na wao wakiwa wanajikung’uta na hivyo waliweza kutoka kwa urahisi sana !  na maisha yakaendelea! Unajua nini ilikuwa vile ili iwe hivi!

Wote tunajua habari za Yusufu, kwamba Ndugu zake walikuwa wamekusudia kumuua, lakini vilevile walimuuza Misri,  wakati huu haukuwa wakati mzuri kwa Yusufu kwa vyovyote vile, Ndugu zake ambao pia kwa wivu waligeuka kuwa adui zake walikusudia kumuangamiza na kuua kabisa ndoto zake ambazo zilikuwa zinawakera japo ndoto zile zilikuwa zimebeba kusudi la Mungu kwa manufaa ya wote! Wao walikuwa kweli wamemkusudia mabaya lakini ni ukweli ulio wazi kuwa  Mungu aliyakusudia mapito yake kuwa  mambo mema.  Mwishoni walitahayari, walimuinamia wote walimuomba radhi walifikiri atalipiza kisasi Lakini Yusufu Alikuwa amewasamehe kabisa, Mambo mema yalikuwa hitimisho la chuki zao

Mwanzo 50:19-20 “Yusufu akawaambia, Msiogope, je! Mimi ni badala ya Mungu? Nanyi kweli mlinikusudia mabaya, bali Mungu aliyakusudia kuwa mema, ili itokee kuokoa taifa kubwa, kama ilivyo leo.” Yusufu ni ka ma alikuwa anawaambia ilikuwa vile ili iwe hivi, Ndugu msomaji wangu mimi binafsi siyajutii mapito yangu, niliumia wakati napita lakini najua ilikuwa vile ili iwe hivi, vyovyote vile, waltu walifanya hila, watu walitaka kua huduma, watu walitaka tusihubiri tena, watu walipigwa upofu, watu walijawa na wivu au chuki au uchungu au walikuwa wanaogopa nafasi zao vyovyote vile najua ilikuwa vile ili iwe hivi, hata kama sasa kuna unayoyapitia na inawezekana hujui kwanini unayapitia kumbuka tu iko hivyo ili iwe vile ahaaaa Mungu ana kusudi jema na maisha yako

Wako watu wanatamani utoweke, wanatamani wasikuone tena, wanateseka kwa wivu, wamejaa wivu wenye uchungu,  hwafurahii chochote chema kinachoendelea katika maisha yako, wanataka uteseke, wanataka ukione cha mtemakuni, wanataka upate taabu, na wakati mwingine kwa ujinga na upofu wanafikiri mawazo yao ya kijinga yanatoka kwa Bwana! No Mungu ni mwema wakati wote, Mungu anawachungulia na kuwacheka, waoa wamejaa chuki sana basi tu kwaajili ya uchungu mioyoni mwao, wanataka kukuzika ilihali uko hai, utasikiwa wanesema jamaa kwishinei, Jamaa ndio basi, waene vile waangalie kwanza nisikilize nataka nikutie Moyo kuwa hata kama hila zao zinaonekana kuwa zinafanikiwa kinyme na maisha yako  nataka nikuambie ni kwa kitambo tu, madamu jambo lako, maisha yako tumaini lako liko kwa Mungu, Mungu hajaishiwa mbinu za wokovu  wakati wao wanatufukia kumbe bila kujijua wanatuleta juu, wanatupeleka mahali ambapo tutalitimiza kusudi la Bwana Mungu wetu Haleluya! Usihuzunike wala kufadhaike katika hali yoyote unayoipitia kwa sasa unapopita unaweza usielewe ni kwa nini unapitia unachokipitia lakini baadaye utaelewa kuwa ILIKUWA VILE ILI IWE HIVI!

Isaya 55:8-9Maana mawazo yangu si mawazo yenu, wala njia zenu si njia zangu; asema Bwana. Kwa maana kama vile mbingu zilivyo juu sana kuliko nchi, kadhalika njia zangu zi juu sana kuliko njia zenu, na mawazo yangu kuliko mawazo yenu. 

Tumanini Letu ni kwa Bwana Mungu wetu kwa maana ana uwezo wa Milele!

Rev. Innocent Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni