Alhamisi, 16 Septemba 2021

Bwana hatamtupa mtu hata milele!


Maombolezo 3:31-33 “Kwa kuwa Bwana hatamtupa mtu Hata milele. Maana ajapomhuzunisha atamrehemu, Kwa kadiri ya wingi wa huruma zake. Maana moyo wake hapendi kuwatesa wanadamu. Wala kuwahuzunisha.


Utangulizi:

Ni muhimu kufahamu kuwa Mungu kama baba yetu, ana njia zake za anazozitumia katika kutujenga, kutufunza, kutubadilisha na kutuonya, katika wakati huo Mungu hutumia njia mbalimbali hata mateso, vita na hata matishio ya hapa na pale, ili Hatimaye aweze kutuleta katika toba tumgeukie yeye na kushikamana naye na kumfanya yeye kuwa tegemeo letu

2Petro 3:9 “Bwana hakawii kuitimiza ahadi yake, kama wengine wanavyokudhani kukawia, bali huvumilia kwenu, maana hapendi mtu ye yote apotee, bali wote wafikilie toba.”

Kusudi kubwa la Mungu ni kutuleta katika toba, toba maana yake ni mabadiliko, Neno toba katika lugha ya kiyunani (Greek) ni METANOIA Ambalo maana yake ni badiliko kubwa la moyo, au kugeuka na kuacha njia isiyofaa na kuendea njia inayofaa, kwa hivyi Mungu hutumia huzuni kama baba wa kiroho kutuleta katika makusudi yale yaliyo mema ona

 Waebrania 12:5-11 “tena mmeyasahau yale maonyo, yasemayo nanyi kama kusema na wana, Mwanangu, usiyadharau marudia ya Bwana, Wala usizimie moyo ukikemewa naye; Maana yeye ambaye Bwana ampenda, humrudi, Naye humpiga kila mwana amkubaliye. Ni kwa ajili ya kurudiwa mwastahimili; Mungu awatendea kama wana; maana ni mwana yupi asiyerudiwa na babaye? Basi kama mkiwa hamna kurudiwa, ambako ni fungu la wote, ndipo mmekuwa wana wa haramu ninyi, wala si wana wa halali. Na pamoja na hayo tulikuwa na baba zetu wa mwili walioturudi, nasi tukawastahi; basi si afadhali sana kujitia chini ya Baba wa roho zetu na kuishi? Maana ni hakika, hao kwa siku chache waliturudi kama walivyoona vema wenyewe; bali yeye kwa faida yetu, ili tuushiriki utakatifu wake. Kila adhabu wakati wake haionekani kuwa kitu cha furaha, bali cha huzuni; lakini baadaye huwaletea wao waliozoezwa nayo matunda ya haki yenye amani.”

Mungu katika hekima yake anapotaka kutonya, kuturekebisha, kutufundisha anaruhusu mateso, lakini sio kwa kusudi la kututesa bali kwa kusudi la kutuleta katika toba yaani mabadiliko makubwa ili hatimaye, tuweze kujenga uhusiano imara na yeye na hatimaye tuweze kuwa na ukomavu wa kiroho na kumuua yeye na njia zake jambo ambalo litaleta furaha milele katika maisha yetu, sawa na baba anavyomuonya mwanae kwa makusudi yale yale ya kumzoeza mtoto kuzaa matunda ya haki na amani.

Bwana hatamtupa mtu hata milele!

Ni ukweli usiopingika kuwa Mungu hakutufanya sisi kuwa kama mashetani, ambao walipoasi aliwakataa milele, sisi ametupa nafasi ambayo kwayo tunaweza kurejesha uhusiano wetu na yeye, Wana wa Israel katika ufalme wa Yuda walikuwa wameacha kumtegemea Mungu na wakawa wakitegema mafanikio yao, akili zao na mambo mengine Mungu akiwaonya kwa vinywa vya manabii huwa angeakatilia mbali kutoka katika nchi njema aliyokuwa amewapa, na anageruhusu waende utumwani

Yeremia 27:6 -8 “Na sasa nimetia nchi hizi zote katika mkono wa Nebukadreza, mfalme wa Babeli, mtumishi wangu; na wanyama wa mwituni pia nimempa wamtumikie. Na mataifa yote watamtumikia yeye, na mwanawe, na mwana wa mwanawe, hata utakapowadia wakati wa nchi yake mwenyewe, ndipo mataifa mengi na wafalme wakuu watamtumikisha yeye. Na itakuwa, taifa lile na mfalme yule asiyetaka kumtumikia Nebukadreza, huyo mfalme wa Babeli, na kutia shingo zao katika nira ya mfalme wa Babeli, mimi nitaliadhibu taifa lile kwa upanga, na kwa njaa, na kwa tauni, asema Bwana, hata nitakapokuwa nimewaangamiza kwa mkono wake.”

Kwa msingi huo Yeremia alitumiwa na Mungu mara kadhaa kuwaonya wana wa Israel na kuwataka wakubali kumtumiakia mfalme huyu wa Babeli kama adhabu  kwao ili baadaye akawabadilishe, Hata hivyo wana wa Yuda hawakutubu wala kuamini kile alichokionya Nebukadreza, hivyo walichukuliwa utumwani na hekalu lao lilibomeolewa na kuchomwa moto kila kitu cha kifahari kiliharibiwa vibaya watu walipitia mateso na walilia na kusaga meno huku Yeremia nabii akiona kila kilichokuwa kinaendelea  jambo lililomfanya ateseke mno kwani aliona mateso ambayo hajawahi kuyaona japo yeye akuuawa lakini ndugu zake na jamaa zake walipata taabu sana  ndipo Yeremuia anaeleza katika maombolezo yake 

Maombolezo 3:1-18 “Mimi ni mtu aliyeona mateso Kwa fimbo ya ghadhabu yake. Ameniongoza na kuniendesha katika giza Wala si katika nuru. Hakika juu yangu augeuza mkono wake Mara kwa mara mchana wote. Amechakaza nyama yangu na ngozi yangu; Ameivunja mifupa yangu.  Amejenga boma juu yangu, Na kunizungusha uchungu na uchovu.  Amenikalisha penye giza, Kama watu waliokufa zamani. Amenizinga pande zote hata siwezi kutoka; Ameufanya mnyororo wangu mzito. Naam, nikilia na kuomba msaada, Huyapinga maombi yangu. Ameziziba njia zangu kwa mawe yaliyochongwa; Ameyapotosha mapito yangu. Alivyo kwangu ni kama dubu aoteaye, Kama simba aliye mafichoni. Amezigeuza njia zangu, na kunirarua-rarua; Amenifanya ukiwa. Ameupinda upinde wake, Na kunifanya niwe shabaha kwa mshale. Amenichoma viuno Kwa mishale ya podo lake. Nimekuwa dhihaka kwa watu wangu wote; Wimbo wao mchana kutwa.  Amenijaza uchungu, Amenikinaisha kwa pakanga. Amenivunja meno kwa changarawe; Amenifunika majivu. Umeniweka nafsi yangu mbali na amani; Nikasahau kufanikiwa. Nikasema, Nguvu zangu zimepotea, Na tumaini langu kwa Bwana.”

Mfalme huyu katili alifanya unyama wa ajabu sana ona mukhtasari wa unyama wake:-

1.       Aliuzingira Yerusalem kwa muda wa miaka miwili na kuhakikisha kuwa wanateseka kwa njaaa

2.       Aliwavamia na kuwapiga na kuwachukua mateka vijana wenye nguvu

3.       Alilibiomoa hekalu na kulichoma moto kwa kuliteketeza

4.       Aliwaongoza njiani wayahudi huku akiwaachia wengine waliwe na simba

5.       Alihakikisha kuwa wanapelekwa utumwani Babeli moja kwa moja bila kupumzika ili kuwanyima wayahudi nafasi ya toba, na maombi ili Mungu wao asije akawaokoa

6.       Akiwaasi vijana wenye hekima na wazuri wasizae tena, na kuwageuza matowashi katika nyumba yake

Katika historia ya Israel wanamkumbuka Mfalme huyu kama mfalme katili zaidi kupata kutokea katika ulimwengu, dikteta asiye na huruma ambaye ataendelea kukumbukwa kwa miaka Mingi kama anavyokumbukwa “Adolf Hitler” aliyeua wayahudi wapatao milioni sita, watu wale walioona mateso haya walihuzunishwa sana na hiki kilichotokea, ilikuwa ni taabu mno na wengi wakasema Mungu ametutupa, ni ukweli uliokuwa wazi kwamba hata adui za Israel waliita Sayuni mji uliotupwa, Na ndipo Yeremia alipotoa unabii kuwa Mungu ataujenga tena Sayuni 

Yeremia 30:17-19 “Maana nitakurudishia afya, nami nitakuponya jeraha zako, asema Bwana, kwa sababu wamekuita, mwenye kutupwa, wakisema, Ni Sayuni, ambao hapana mtu autakaye. Bwana asema hivi, Tazama, nitarudisha tena hema za Yakobo zilizohamishwa, na kuyahurumia makao yake; nao mji huo utajengwa juu ya magofu yake wenyewe, nalo jumba litakaliwa, kama ilivyokuwa desturi yake. Tena kwao itasikiwa shukrani, na sauti yao wachangamkao; nami nitawazidisha, wala hawatakuwa wachache; tena nitawatukuza, wala hawatakuwa wanyonge.”

Mungu ametuahidi kuwa hatatutupa kamwe !

Ni ahadi ya Mungu kuwa hatatutupa milele, Yesu alisema kila ajae kwangu sitamtupa nje kamwe Yohana 6:37-39 “Wote anipao Baba watakuja kwangu; wala ye yote ajaye kwangu sitamtupa nje kamwe. Kwa kuwa mimi sikushuka kutoka mbinguni ili niyafanye mapenzi yangu, bali mapenzi yake aliyenipeleka. Na mapenzi yake aliyenipeleka ni haya, ya kwamba katika wote alionipa nisimpoteze hata mmoja, bali nimfufue siku ya mwisho.”

  Ni wajibu wetu kufahamu kuwa tunaweza kupita katika giza, tunaweza kupitia mateso na huzuni nzito, mashaka na woga, mashutumu na masengenyo, giza na kutokufanikiwa, mashambulizi ya adui pande zote, kizibiwa niia, kama milango imefunga kila mahali lakini hatuna budi kukumbuka neno la Mungu na Bwana wetu Yesu ametuahidi kuwa hatatuacha milele, wala hatatutupa kamwe, wanadamu wanaweza kututupa, wanaweza kutudharau, wanaweza kutuweka pembeni, wanaweza kutozomea lakini Mungu hawezi kamwe kuwatupa watu wake, tunapohisi kuwa tunapita katiika huzuni na mateso kumbuka kuwa hatujaweka tumaini letu kwa mwanadamu wala kwa miungu tutaendelea kuliitia jina la bwana Mungu wetu mpaka kielelweke

a.       Endelea kuliitia jina la Bwana na kumpazia sauti  Zaburi 77:7 – 1-2, “Nimpazie Mungu sauti yangu, Naam, nimpazie Mungu, naye atanisikia. Siku ya taabu yangu nalimtafuta Bwana; Mkono wangu ulinyoshwa usiku, haukulegea; Nafsi yangu ilikataa kufarijika.” 7-9 “Je! Bwana atatupa milele na milele? Hatatenda fadhili tena kabisa? Rehema zake zimekoma hata milele? Ahadi yake imekwisha hata vizazi vyote? Mungu amesahau fadhili zake? Amezuia kwa hasira rehema zake?

               

b.      Kumbuka wewe ndio urithi wa Bwana na hakuna mwingine  Zaburi 94:14 “Kwa kuwa Bwana hatawatupa watu wake, Wala hutauacha urithi wake,”

 

c.       Kumbuka tunalibeba jina lake kuu na Bwana amekusudia kutufanya kuwa watu wake 1Samuel 12:20-22 “Samweli akawaambia, Msiogope; ni kweli mmeutenda uovu huu wote; lakini msigeuke na kuacha kumfuata Bwana, bali mtumikieni Bwana kwa mioyo yenu yote. Wala msigeuke upande, maana, kufuata vitu vya ubatili, visivyoweza kusaidia wala kuokoa, kwa kuwa havifai kitu. Maana Bwana hatawaacha watu wake kwa ajili ya jina lake kuu; kwa kuwa imempendeza Bwana kuwafanya ninyi kuwa watu wake mwenyewe.”

 

d.      Kumbuka kuwa mapito yako ni ya kitambo tu na kuwa Bwana hatamtupa mtu hata milele! Maombolezo 3:31-33 “Kwa kuwa Bwana hatamtupa mtu Hata milele. Maana ajapomhuzunisha atamrehemu, Kwa kadiri ya wingi wa huruma zake. Maana moyo wake hapendi kuwatesa wanadamu. Wala kuwahuzunisha.


Wewe ni Mungu mpasua bahari, haufananishwi na kitu kingine, haulinganishwi. na kitu kingine unafanya mambo ambayo mwanadamu hawezi kufanya, unatoa faraja ambayo mwanadamu hawezi kutoa haulinganishi na kitu kingine.

Na Rev. Innocent Samuel Jumaa Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye hekima!

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni