Jumatatu, 18 Oktoba 2021

Msiba katika bonde la kukata maneno!


Yoeli 3:12-14Mataifa na wajihimize, wakapande juu katika bonde la Yehoshafau; maana huko ndiko nitakakoketi niwahukumu mataifa yote yaliyo pande zote. Haya! Utieni mundu, maana mavuno yameiva; njoni, kanyageni; kwa maana shinikizo limejaa, mapipa nayo yanafurika; kwani uovu wao ni mwingi sana. Makutano makubwa, makutano makubwa, wamo katika bonde la kukata maneno! Kwa maana siku ya Bwana i karibu, katika bonde la kukata maneno.”


Utangulizi:

Maandiko matakatifu yanatufundisha kuwa kila mtu na aitii mamlaka iliyokuu, kwa sababu hakuna mamlaka isiyotoka kwa Mungu na kuwa ile iliyoko imeamriwa na Mungu au imeruhusiwa na Mungu, na kwa sababu hiyo kuiasi mamlaka ni kumuasi Mungu mwenyewe ona

Warumi 13:1-4 “Kila mtu na aitii mamlaka iliyo kuu; kwa maana hakuna mamlaka isiyotoka kwa Mungu; na ile iliyopo umeamriwa na Mungu. Hivyo amwasiye mwenye mamlaka hushindana na agizo la Mungu; nao washindanao watajipatia hukumu. Kwa maana watawalao hawatishi watu kwa sababu ya matendo mema, bali kwa sababu ya matendo mabaya. Basi, wataka usimwogope mwenye mamlaka? Fanya mema, nawe utapata sifa kwake; kwa kuwa yeye ni mtumishi wa Mungu kwako kwa ajili ya mema. Lakini ufanyapo mabaya, ogopa; kwa maana hauchukui upanga bure; kwa kuwa ni mtumishi wa Mungu, amlipizaye kisasi mtenda mabaya kwa ajili ya ghadhabu.”

Maandiko yanathibitisha wazi kuwa kama mtu atashindana na mwenye mamlaka ni wazi kuwa anashinda ana agizo la Mungu na sio hivyo tu washindanao na Mungu watajipatia hukumu! Kanuni ya Mungu siku zote hasimami na muasi, Mungu husimama na mtu wake au mtumishi wake aliyemuweka, Mungu hajipingi mwenyewe wala hawezi kushindana kinyume na kusudi lake hivyo atasimama na Mtumishi wake, aliyemuweka kwa kusudi lake

1Samuel 2:9-10 “Yeye atailinda miguu ya watakatifu wake; Bali waovu watanyamazishwa gizani, Maana kwa nguvu hakuna atakayeshinda; Washindanao na Bwana watapondwa kabisa; Toka mbinguni yeye atawapigia radi; Bwana ataihukumu miisho ya dunia; Naye atampa mfalme wake nguvu, Na kuitukuza pembe ya masihi wake.”

Nyakati za agano la kale Mungu katika Hekima yake, alipokuwa amekusudia kuamua lipi ni lipi au watu walipokuwa wanataka kuamua jambo au kutafuta suluhu ya kivita mara nyingi maamuzi yao yalifanyika katika bonde, pande zinazoshindanda zingekaa upande huu wa mlima na upande huu wa mlima na kisha baada ya uamuzi kufanyika pale bondeni ndipo mahali ambapo watu wangeweza kufanya maamuzi yao na hapo palijulikana sana kama Bonde la kukata maneno. Vita ingapiganwa hapo na damu ingemwagika hapo bila kuinajisi nchi, na Mungu angetoa ushindi kwa mtu husika.


Maana ya Bonde la kukata maneno!

Kama nilivyogusia katika utangulizi neno Bonde la kukata maneno, limetumika katika maandiko kumaanisha eneo la kufanya uamuzi, au bonde la kumaliza maneno hususani wakati kuna jambo linahitaji kufanyiwa uamuzi ikiwemo kumaliza vita, au bonde la kumaliza migogoro kati ya watu wa Mungu na adui wa watu wa Mungu, Nyakati za biblia watu walipokuwa na vita kati ya taifa moja na taifa jingine au ufalme mmoja na ufalme mwingine walikuwa na tabia ya kukaa upande mmoja wa mlima na upande wa pili wa mlima na kutupiana maneno ya kujigamba, kila mmoja angeweza kusema kile anachoweza kukisema lakini hatimaye wangeshuka katika Bonde na kumaliza mgogoro au maneno kwa kuonyeshana umwamba  bonde la kukata maneno lilikuwa kama Mahakama ya usuluhishi au kumaliza ubishi wa kila mmoja kwa namna yake mfano

1Samuel 17:1-11 “Wakati huo Wafilisti walikusanya majeshi yao kwa vita, nao wakakusanyika huko Soko, ulio mji wa Yuda, wakatua kati ya Soko na Azeka, katika Efes-damimu. Naye Sauli na watu wa Israeli wakakusanyika, wakatua katika bonde la Ela, nao wakapanga vita juu ya hao Wafilisti. Wafilisti wakasimama juu ya mlima upande huu, na Waisraeli wakasimama juu ya mlima upande huu, napo palikuwa na hilo bonde katikati. Ndipo akatoka shujaa katika kambi ya Wafilisti, aliyeitwa Goliathi, wa Gathi, ambaye urefu wake ulikuwa mikono sita na shibiri moja. Alikuwa na chapeo ya shaba kichwani, tena amevaa darii ya shaba; na uzani wake ile darii ya shaba ulikuwa shekeli elfu tano za shaba. Tena amevaa mabamba ya shaba miguuni mwake, naye alikuwa na mkuki wa shaba kati ya mabega; yake. Na mti wa fumo lake ulikuwa kama mti wa mfumaji; na kichwa cha mkuki wake kilikuwa shekeli mia sita za chuma uzito wake; na mtu aliyemchukulia ngao yake akamtangulia. Naye akasimama, akawapigia kelele majeshi ya Israeli akawaambia, Mbona mmetoka kupanga vita? Je! Mimi si Mfilisti, na ninyi si watumishi wa Sauli? Jichagulieni mtu, akanishukie mimi. Kama akiweza kupigana nami na kuniua, sisi tutakuwa watumwa wenu; nami nikimshinda yeye na kumwua, ninyi mtakuwa watumwa wetu, na kututumikia. Yule Mfilisti akasema, Nayatukana leo majeshi ya Israeli; nipeni mtu tupigane. Basi Sauli na Israeli wote waliposikia maneno hayo ya Mfilisti, wakafadhaika na kuogopa sana.”

Kwa hiyo utaweza kuona kuwa katikati walipokuwa wakitupiana maneno walikaa upande huu wa mlima na upande huu wa mlima na walitupiana maneno, lakini hapa katikati ya bonde ndio mahali sasa paliitwa bonde la kukata maneno, kwamba sema utakavyosema na tukana utakavyotukana tamba utakavyotamba na kunya utakavyo kunya na harisha uatakavyoharisha toa shombo za kila namna lakini tutakutana katika bonde la kukata maneno na hapo ndio Mungu ataonyesha kuwa nani ni mbabe? Nani yuko pamoja naye na ni nani aliyechaguliwa na Mungu, nani anapigana vita vya kishetani na ni nani anapigana vita vya Bwana!, Bonde la kukata maneno kwa msingi huo liliitwa bonde la maamuzi, kibiblia pia liliitwa bonde la Yehoshafau kwa mujibu wa nabii Yoeli, hii ni kwa sababu katika bonde hili Mungu aliwadhalilisha maadui wa Israel mara kadhaa hususani wakati wa Yehoshafati  mara mbili, lakini pia jina Yehoshafati maana yake Yehova ndiye muamuzi wangu,  kinabii mahali hapa ndipo Mungu atakapokuja kuuhukumu Mataifa yote yatakayosimama kinyume na Israel na Mungu atawaangamiza watu wengi sana katika eneo hili  hivyo patakuwa na mauti ya kutisha na kushangaza patakuwa ni mahali pa msiba kwa wale wote wasiomcha Mungu ona

Ezekiel 39:13-16Naam, watu wote wa nchi hiyo watawazika; itakuwa ni sifa kwao katika siku ile nitakapotukuzwa, asema Bwana MUNGU. Nao watawachagua watu wa kufanya kazi ya daima, watakaopita kati ya nchi, ili kuwazika waliosalia juu ya uso wa nchi, ili kuisafisha; miezi saba itakapokwisha kupita watatafuta. Na hao wapitao kati ya nchi watatafuta; na mtu ye yote aonapo mfupa wa mtu, ndipo atakapoweka alama karibu nao, hata wazishi watakapouzika katika bonde la Hamon-Gogu. Tena, Hamona litakuwa jina la mji. Hivyo ndivyo watakavyosafisha nchi.

Ezekiel analiona bonde hilo pia kuwa ni mahali watakapozikwa watu wengi sana walio kinyume na mapenzi ya Mungu, maiti zao zitazikwa mahali hapo na kumbukumbu lao litapotelea mahali hapo, Kijiografia eneo hilo linasemekana liko Israel karibu na bonde la Kidron Mashariki ya Yerusalem, eneo hili kinabii pia ndio litakuja kuwa eneo ambalo Yesu atabagua Kondoo na Mbuzi na kutoa hukumu kwa mataifa yatakayokuwa kinyume na Israel

Mathayo 25:31-46 “Hapo atakapokuja Mwana wa Adamu katika utukufu wake, na malaika watakatifu wote pamoja naye, ndipo atakapoketi katika kiti cha utukufu wake; na mataifa yote watakusanyika mbele zake; naye atawabagua kama vile mchungaji abaguavyo kondoo na mbuzi;atawaweka kondoo mkono wake wa kuume, na mbuzi mkono wake wa kushoto. Kisha Mfalme atawaambia wale walioko mkono wake wa kuume, Njoni, mliobarikiwa na Baba yangu, urithini ufalme mliowekewa tayari tangu kuumbwa ulimwengu; kwa maana nalikuwa na njaa, mkanipa chakula; nalikuwa na kiu, mkaninywesha; nalikuwa mgeni, mkanikaribisha; nalikuwa uchi, mkanivika nalikuwa mgonjwa, mkaja kunitazama; nalikuwa kifungoni, mkanijia. Ndipo wenye haki watakapomjibu, wakisema, Bwana, ni lini tulipokuona una njaa, tukakulisha, au una kiu tukakunywesha? Tena ni lini tulipokuona u mgeni, tukakukaribisha, au u uchi, tukakuvika? Ni lini tena tulipokuona u mgonjwa, au kifungoni, tukakujia? Na Mfalme atajibu, akiwaambia, Amin, nawaambia, kadiri mlivyomtendea mmojawapo wa hao ndugu zangu walio wadogo, mlinitendea mimi. Kisha atawaambia na wale walioko mkono wake wa kushoto, Ondokeni kwangu, mliolaaniwa, mwende katika moto wa milele, aliowekewa tayari Ibilisi na malaika zake; kwa maana nalikuwa na njaa, msinipe chakula; nalikuwa na kiu, msininyweshe; nalikuwa mgeni, msinikaribishe; nalikuwa uchi, msinivike; nalikuwa mgonjwa, na kifungoni, msije kunitazama. Ndipo hao pia watajibu, wakisema, Bwana, ni lini tulipokuona wewe una njaa, au una kiu, au u mgeni, au u uchi, au u mgonjwa, au u kifungoni, tusikuhudumie? Naye atawajibu, akisema, Amin, nawaambia, Kadiri msivyomtendea mmojawapo wa hao walio wadogo, hamkunitendea mimi. Na hao watakwenda zao kuingia katika adhabu ya milele; bali wenye haki watakwenda katika uzima wa milele.” Watu wasiotaka kutawaliwa na Yesu aidha watachinjwa katika eneo hili Luka 19: 27 “Tena, wale adui zangu, wasiotaka niwatawale, waleteni hapa mwachinje mbele yangu.”

Msiba katika Bonde la kukata maneno!

Kama tulivyoona maana ya bonde la kukata maneno kwa kawaida Hapa ndio mwisho wa mabishano yote na mashindano yote, Mungu anapokuja katika bonde la kukata maneno huwa anaonyesha wazi wazi nani ni mshindi na ni nani yuko upande wake na kwa kawaida katika Bonde la kukata maneno huwa ndio mwisho wa maamuzi ya Mungu, kwa kawaida hata kama mahali hapo hapana bonde Mungu huweza kuifunua ardhi na kufanya bonde popote na kupoteza watu waliomuasi,

Hesabu 16:1-34 “Basi Kora, mwana wa Ishari, mwana wa Kohathi, mwana wa Lawi, akatwaa watu, pamoja na Dathani na Abiramu, wana wa Eliabu, na Oni, mwana wa Pelethi, waliokuwa wana wa Reubeni; nao, pamoja na watu kadha wa kadha wa wana wa Israeli, watu mia mbili na hamsini, Wakuu wa mkutano, waliokuwa wateule wa mkutano, watu wenye sifa, wakainuka mbele ya Musa; nao wakakusanyika kinyume cha Musa na Haruni, na kuwaambia, Ninyi inawatosha, kwa kuwa mkutano wote ni mtakatifu, kila mmoja miongoni mwao, Bwana naye yu kati yao; n'nini basi kujitukuza juu ya mkutano wa Bwana? Musa aliposikia maneno haya, akapomoka kifudifudi;  kisha akanena na Kora na mkutano wake wote, akawaambia, Asubuhi Bwana ataonyesha ni kina nani walio wake, kisha ni nani aliye mtakatifu, tena ni nani atakayemkaribisha kwake; maana, yeye atakayemchagua ndiye atakayemsongeza kwake. Fanyeni neno hili; twaeni vyetezo, ninyi Kora na mkutano wake wote; vitieni na moto, mkaweke na uvumba juu yake mbele za Bwana kesho; kisha itakuwa ya kwamba mtu Bwana atakayemchagua, yeye atakuwa mtakatifu; inawatosha ninyi, enyi wana wa Lawi. Musa akamwambia Kora, Sikizeni basi, enyi Wana wa Lawi; Je! Mwaona kuwa ni jambo dogo kwenu, kuwa Mungu wa Israeli amewatenga ninyi na mkutano wa Israeli, ili apate kuwakaribisha kwake; ili mfanye utumishi wa maskani ya Bwana, na kusimama mbele ya mkutano ili kuwatumikia; tena ya kuwa amekuleta uwe karibu, na ndugu zako wote wana wa Lawi pamoja nawe? Nanyi, je! Mwataka na ukuhani pia? Kwa sababu hii wewe na mkutano wako wote mmekusanyika kinyume cha Bwana; na Haruni, je! Yeye ni nani hata mkamnung'unikia? Kisha Musa akatuma kuwaita Dathani na Abiramu, wana wa Eliabu; nao wakasema, Hatuji sisi; je! Ni jambo dogo, wewe kutuleta kutoka nchi iliyojawa na maziwa na asali, ili kutuua jangwani, lakini pamoja na haya wajikuza mwenyewe uwe mkuu juu yetu kabisa? Kisha, hukutuleta katika nchi iliyojawa na maziwa na asali, wala hukutupa urithi wa mashamba, na mashamba ya mizabibu; je! Unataka kuwatoboa macho watu hawa? Hatuji. Musa akakasirika sana, akamwambia Bwana. Usiikubali sadaka yao; mimi sikutwaa hata punda mmoja kwao, wala sikumwumiza hata mtu mmoja miongoni mwao. Kisha Musa akamwambia Kora, Wewe na mkutano wako wote iweni hapa mbele ya Bwana kesho, wewe, na wao, na Haruni; mkatwae kila mtu chetezo chake, na kutia uvumba juu yake, mkavilete mbele za Bwana, vyetezo mia mbili na hamsini; wewe pia, na Haruni, kila mtu na awe na chetezo chake. Basi wakavitwaa kila mtu chetezo chake, wakatia na moto ndani yake, wakatia na uvumba juu ya moto, na kusimama pale mlangoni pa hema ya kukutania, pamoja na Musa na Haruni. Kisha Kora akakutanisha mkutano wote kinyume chao mlangoni pa hema ya kukutania; na utukufu wa Bwana ukatokea mbele ya mkutano wote. Kisha Bwana akanena na Musa na Haruni, na kuwaambia,Jitengeni ninyi mkaondoke kati ya mkutano huu, ili nipate kuwaangamiza mara moja. Nao wakapomoka kifudifudi, wakasema, Ee Mungu, Mungu wa roho za wenye mwili wote, je! Mtu mmoja atafanya dhambi, nawe utaukasirikia mkutano wote? Bwana akasema na Musa, na kumwambia, Nena na mkutano, na kuwaambia, Ondokeni ninyi hapo karibu na maskani ya Kora, na Dathani, na Abiramu. Basi Musa akainuka na kuwaendea Dathani na Abiramu; na wazee wa Israeli wakaandamana naye.  Akasema na mkutano, na kuwaambia, Nawasihi, ondokeni penye hema za hawa watu waovu, wala msiguse kitu chao cho chote, msiangamizwe katika dhambi zao zote. Basi wakaondoka hapo karibu na maskani ya Kora, na Dathani na Abiramu, pande zote; nao kina Dathani na Abiramu wakatoka nje wakasimama mlangoni mwa hema zao, pamoja na wake zao, na wana wao na watoto wao wadogo. Musa akasema, Kwa jambo hili mtajua ya kwamba Bwana amenituma, ili nifanye kazi hizi zote; kwa kuwa mimi sikuzifanya kwa akili zangu mwenyewe. Kama watu hawa wakifa kifo cha sikuzote, kama watu wote wafavyo, au kama wakipatilizwa kwa mapatilizo ya watu wote; hapo basi Bwana hakunituma mimi. Lakini Bwana akiumba kitu kipya, na hiyo nchi ikifunua kinywa chake na kuwameza, pamoja na wote walio nao, nao washukia shimoni wali hai; ndipo mtatambua ya kwamba watu hawa wamemdharau Bwana Basi ilikuwa, hapo alipokwisha kusema maneno haya yote, nchi iliyokuwa chini yao ikapasuka; nchi ikafunua kinywa chake, na kuwameza, na watu wa nyumba zao na wote walioshikamana na Kora, na vyombo vyao vyote. Basi wao, na wote waliokuwa nao, wakashukia shimoni wali hai; nayo nchi ikawafunika wakaangamia kutoka mle mkutanoni. Nao Israeli wote waliokuwa kando-kando yao wakakimbia kwa ajili ya kilio chao; kwa kuwa walisema, Nchi isije kutumeza na sisi.”

Haijalishi kuwa wapinzani wako wana maneno kiasi gani, wana nguvu kiasi gani, wana tisha kiasi gani, lakini mwisho wa siku wataingia katika bonde la kukata maneno na hapa Mungu ataingilia kati na kutenda mambo ya ajabu, atamsambaratisha adui na kumfutilia mbali, heri leo kuwa upande wa Bwana, fungua macho yako uelewe kuwa Mungu yuko upande gani simama kule aliko Mungu na ushindi utakuwa dhahiri, usipokuwa upande wa Bwana na usipotaka Bwana akutawale utachinjwa

Goliati alijitamba kwa siku 40 kila siku akiwatisha watu wa Israel lakini alipotokea mtu aliyepakwa mafuta katika bonde la kukata maneno Daudi mwana wa Yese. Goliathi alizimia na kukatwa kichwa

1Samuel 17:44-51 “Mfilisti akamwambia Daudi, Njoo huku kwangu; nyama yako nitawapa ndege wa angani na wanyama wa mwituni. Ndipo Daudi akamwambia yule Mfilisti, Wewe unanijia mimi na upanga, na fumo, na mkuki, bali mimi ninakujia wewe kwa jina la Bwana wa majeshi, Mungu wa majeshi ya Israeli uliowatukana. Siku hii ya leo Bwana atakuua mkononi mwangu, nami nitakupiga, na kuku ondolea kichwa chako, nami leo nitawapa ndege wa angani na wanyama wa nchi mizoga ya majeshi ya Wafilisti, ili kwamba dunia nzima wajue ya kuwa yuko Mungu katika Israeli. Nao jamii ya watu wote pia wajue ya kwamba Bwana haokoi kwa upanga wala kwa mkuki; maana vita ni vya Bwana, naye atawatia ninyi mikononi mwetu. Ikawa, hapo Mfilisti alipojiinua, akaenda akamkaribia Daudi, ndipo Daudi naye akapiga mbio, akalikimbilia jeshi ili akutane na yule Mfilisti. Daudi akatia mkono wake mfukoni, akatwaa humo jiwe moja, akalitupa kwa kombeo lake, akampiga Mfilisti katika kipaji cha uso; jiwe hilo likamwingilia kipajini, akaanguka chini kifudifudi. Hivyo Daudi akamshinda yule Mfilisti kwa kombeo na jiwe, akampiga Mfilisti, akamwua; walakini Daudi hakuwa na upanga mkononi mwake. Ndipo Daudi akapiga mbio, akasimama juu ya Mfilisti, akautwaa upanga wake, akaufuta alani mwake, akamwua, akamkata kichwa kwa upanga huo. Nao Wafilisti walipoona ya kuwa shujaa wao amekufa, wakakimbia.”   

Kama wako watu wanakushambulia katika maisha yako wanatangaza vita na wewe usiogope uko mwisho wao katika Bonde la kukata maneno Mungu ataingilia kati na bonde lako la vita litageuka kuwa Bonde la Baraka kwako lakini litakuwa bonde la msiba kwa maadui zako

2Nyakati 20:17-27 “Hamtahitaji kupigana vita, jipangeni, simameni, mkauone wokovu wa Bwana ulio pamoja nanyi, enyi Yuda na Yerusalemu; msiogope, wala msifadhaike; kesho tokeni juu yao; kwa kuwa Bwana yu pamoja nanyi. Yehoshafati akainama kichwa, kifulifuli; wakaanguka mbele za Bwana Yuda wote na wakaao Yerusalemu, wakimsujudia Bwana.Na Walawi, wa wana wa Wakohathi na wa wana wa Wakorahi, wakasimama ili wamsifu Bwana, Mungu wa Israeli, kwa sauti kuu sana. Wakaamka asubuhi na mapema, wakaenda nje katika jangwa la Tekoa; nao walipokuwa wakitoka, Yehoshafati akasimama, akasema, Nisikieni, enyi Yuda nanyi wenyeji wa Yerusalemu; mwaminini Bwana, Mungu wenu, ndivyo mtakavyothibitika; waaminini manabii wake, ndivyo mtakavyofanikiwa. Naye alipokwisha kufanya shauri na watu, akawaweka wale watakaomwimbia Bwana, na kumsifu katika uzuri wa utakatifu, wakitoka mbele ya jeshi, na kusema, Mshukuruni Bwana; kwa maana fadhili zake ni za milele. Nao walipoanza kuimba na kusifu, Bwana akaweka waviziao juu ya wana wa Amoni, na Moabu, na wa mlima Seiri, waliokuja juu ya Yuda; nao wakapigwa. Kwani wana wa Amoni na wa Moabu waliwaondokea wenyeji wa mlima Seiri kuwaulia mbali na kuwaharibu; nao walipokwisha kuwakomesha hao wakaao Seiri, wakajitia kuharibu kila mtu mwenziwe. Hata Yuda walipofika mnara wa kulindia wa jangwani, wakalitazama hilo jeshi; nao, angalia, walikuwa maiti walioanguka nchi, wala hapana aliyeokoka. Nao Yehoshafati na watu wake walipokuja kuchukua nyara zao, wakaona kati yao wingi wa mali, na mavazi, na johari za thamani, walivyojivulia, zaidi kuliko wawezavyo kuchukua; wakawa siku tatu katika kuteka nyara, maana zilikuwa nyingi sana. Hata siku ya nne wakakusanyika katika bonde la Baraka; maana ndipo walipombarikia Bwana; kwa hiyo jina lake mahali pale pakaitwa Bonde la Baraka hata leo. Kisha wakarudi, kila mtu wa Yuda na Yerusalemu, na Yehoshafati mbele yao, ili kuurudia Yerusalemu kwa furaha; kwa kuwa Bwana amewafurahisha juu ya adui zao.”

Bonde lilikuwa ni kama ulingo wa mabondia waliotambiana kwa muda mrefu, afile munu asigale munu, acholile kachola, show show na kadhalika, Bonde la kukatya maneno ni ikama kiwanja cha mpira wa soka watu wataingia kati dakika 90 utachezwa na mwamba ataonekana, watu wataingia ulingoni zitapigwa na mwamba ataonekama

Siku ya leo haijalishi una vita na nani, haijalishi nani ametangaza vita na wewe kumbuka liko Bonde la kukata maneno, liko bonde ambalo kwalo Mungu atamaliza migogoro yote atamaliza kesi zote atafanya maamuzi na mwisho wa siku wale ambao Bwana amewachagua atawaleta kwake naye ataligeuza Bonde lako kuwa sio la vita tena bali la ushindi na bonde la Baraka  na bonde la kuteka mateka na bonde la kukusanya nyara na wapinzani wako na maadui zako itakuwa ni msiba katika bonde la kukata maneno!, Ukiwa na Yesu hutaogopa kama mfalme Yehoshafati, watu walio na Mungu hawapigani tu vita vya maneno, kama Goliathi sisi tunalitaja jina la Bwana Mungu wetu yeye ndio tegemeo letu na tumaini letu hakuna mtu aliyemtumainia akatahayari, hatutatahayarika kamwe, Mungu atamaliza ngebe za adui zako, Penina alikuwa na maneno sana kuliko Hanna kwa sababu hana alionekana kuwa tasa na hazai, lakini siku moja mwenye nguvu akaingilia kati na hana akasema maneno ya ushindi, ona

1Samuel 2:2-9 “Hakuna aliye mtakatifu kama Bwana; Kwa maana hakuna ye yote ila wewe, Wala hakuna mwamba kama Mungu wetu. Msizidi kunena kwa kutakabari hivyo; Majivuno yasitoke vinywani mwenu; Kwa kuwa Bwana ni Mungu wa maarifa, Na matendo hupimwa na yeye kwa mizani.Pinde zao mashujaa zimevunjika, Na hao waliojikwaa wamefungiwa nguvu. Walioshiba wamejikodisha ili kupata chakula, Na hao waliokuwa na njaa wamepata raha. Naam, huyo aliyekua tasa amezaa watoto saba, Na yeye aliye na wana wengi amedhoofika. Bwana huua, naye hufanya kuwa hai; Hushusha hata kuzimu, tena huleta juu. Bwana hufukarisha mtu, naye hutajirisha; Hushusha chini, tena huinua juu. Humwinua mnyonge kutoka mavumbini, Humpandisha mhitaji kutoka jaani, Ili awaketishe pamoja na wakuu, Wakakirithi kiti cha enzi cha utukufu; Kwa maana nguzo za dunia zina Bwana, Naye ameuweka ulimwengu juu yake. Yeye atailinda miguu ya watakatifu wake; Bali waovu watanyamazishwa gizani, Maana kwa nguvu hakuna atakayeshinda;”
 

Bwana ampe neema kila mmoja wetu na maisha ya ushindi kwa kila anayemtegemea Bwana na asiyezitegemea akili zake mwenyewe na tukutane katika bonde la kukata maneno!

Rev. Innocent Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni