Jumatatu, 1 Novemba 2021

Maisha ya viwango!


Warumi 12:1-2 “Basi, ndugu zangu, nawasihi, kwa huruma zake Mungu, itoeni miili yenu iwe dhabihu iliyo hai, takatifu, ya kumpendeza Mungu, ndiyo ibada yenu yenye maana. Wala msiifuatishe namna ya dunia hii; bali mgeuzwe kwa kufanywa upya nia zenu, mpate kujua hakika mapenzi ya Mungu yaliyo mema, ya kumpendeza, na ukamilifu.”

 


 Utangulizi:

 

Wote tunafahamu wazi ya kuwa tunaishi katika ulimwengu, unaoendeshwa kwa viwango, na kwa namna Fulani hatuwezi kamwe kukwepa kuishi kwa viwango, Dunia ina viwango vyake, na vingine tunavitumia katika maisha yetu ya kila siku, Lakini neno la Mungu vilevile linatuelekeza kuishi kwa  kiwango kinachokusudiwa, katika maandiko yaani neno la Mungu,  tunasoma hivi katika Warumi 12:1-2 “Basi, ndugu zangu, nawasihi, kwa huruma zake Mungu, itoeni miili yenu iwe dhabihu iliyo hai, takatifu, ya kumpendeza Mungu, ndiyo ibada yenu yenye maana. Wala msiifuatishe namna ya dunia hii; bali mgeuzwe kwa kufanywa upya nia zenu, mpate kujua hakika mapenzi ya Mungu yaliyo mema, ya kumpendeza, na ukamilifu.”Kuna neno muhimu ambalo hatuna budi kuliangalia kwa undani ili tuweze kupata maana iliyokusudiwa hususani neno MSIIFUATISHE NAMNA, na tutajifunza somo hili kwa kuzingatia maeneo matatui yafuatayo:-

 

·         Maana ya Viwango

·         Umuhimu wa Viwango

·         Jinsi ya kuishi kwa Viwango

 

Maana ya viwango:-

 

Warumi 12:2 “Wala msiifuatishe namna ya dunia hii; bali mgeuzwe kwa kufanywa upya nia zenu, mpate kujua hakika mapenzi ya Mungu yaliyo mema, ya kumpendeza, na ukamilifu.” Hebu tuliangalie andiko hilo vilevile katika tafasiri za kiingereza  ya New International Version (NIV) andiko hilo linasiomeka hiviDo not conform to the pattern of this world, but be transformed by the renewing of your mind, then you will be able to test and approve what God’s will is –his good, pleasing and perfect will.” Unapoangalia sasa tafasiri ya Biblia yetu ya Kiswahili na kiingereza utaweza kuona neno “MSIIFUATISHE NAMNA” Na Katika kiingereza cha NIV “DO NOT CONFORM TO THE PATTERN” maneno hayo sasa katika biblia ya kiyunani yanasomeka kama “PROTYPO” ambalo sasa maana yake halisi kwa kiingereza ni Standard, au Pattern, au Norm, au Exemplar, au Archetype, au Measure, au meter, au Gauge, au measurement, au values. Kwa hiyo utaweza kuona kwa mfano Biblia ya tafasiri ya kiingereza ya Good News inatumia maneno hayaDo not Conform yourselves to the STANDARDS of this world, but let God transform you inwardly by a comlete change of your mind. Then you will be able to know the will of God- what is good and is pleasing to him and is perfect. Kwa msingi huo ni kama neno la Mungu linawataka watu waliookolewa au wanaomcha Mungu kutokuishi sawa na viwango vya ulimwengu huu, Maana yake ni kuwa kuna aina ya kiwango cha maisha ambacho Mungu anakikusudia kwetu! Na maandiko yanataka tuishi zawa na viwango hivyo. Kwa hiyo neno Standard sasa tafasiri yake ni a level of quality or attainment, au Something used as a measure, norm or model in comparative evaluations, something used or accepted as normal or average, ni kipimo kinachohusika kupimia ubora wa mambo, wastani wa mambo, kwa kulinganisha na mengine

 

Umuhimu wa viwango:-

 

Katika ulimwengu tulio nao, viwango vina umuhimu mkubwa sana, na dunia ina vipimo vingi sana vya kupima ubora wa mambo kwa kina, mapana, na marefu, tunaishi katika ulimwengu ambao unajua kupima, na thamani ya kitu hupimwa kutokana na kiwango kinachokusudiwa, wakati mwingine fahari ya kitu Fulani duniani hata kama hakina maana inaangaliwa sana na ubora wa kiwango chake, sio hivyo tu watu wanaotumia kitu chenye ubora wa hali ya juu, huweza kujisikia kuwa wao ni maalumu sana na wakati mwingine hata kujivunia kitu hicho na kuwa na furaha kwa sababu kina ubora! Kwa hiyo dunia ni dunia ya viwango! Kila kitu duniani kinapimwa kutokana na kiwango chake!, Mataifa mengi yana mashirika yanayohusika na kupima au kuangalia viwango vya bidhaa, hapa Tanzania bidhaa huthibitishwa ubora wake kupitia shirika la (TBS) yaani Tanzania Bureau Standard , wao wakisha thibitisha kuwa kitu hiki kina ubora huweka neno yao, yako mashirika mengine pia ya kidini kama ya kislamu, huweka neno Halal au Haram kwa manufaa ya bidhaa hiyo kutumiwa na imani ya watu hao, Mashirika haya pia hufanya kazi ya kudhibiti bidhaa fake au zisizo na ubora, kwa hiyo dunia ina utaratibu wake wa kuweka kitu katika viwango mfano;-

 

·         Mataifa kwa mfano yako mataifa yanayoitwa yaliyoendelea na yanayoendelea, Developed and underdevelopment country (nchi zenye uchumi wa juu, wa wastani wa kati na wa chini)

·         Taaluma kwa mfano kuna Elimu ya juu na Elimu ya chini, Graduates and undergraduates

·         Matokeo ya mitihani secondary yanapimwa kwa migawanyo ijulikanayo kama Division I,II,III,IV na 0

·         Matokeo ya vyuoni zile degree ziko za aina saba kwa waingereza zinapimwa kutokana na viwango vya GPA yaani Grade Point Average, Marekani wao degree ni degree tu Lakini Waingereza Degree zao wanazigawanya kwenye maeneo saba mfano:-

 

*      Ukipata 70-100 utatunukiwa  degree First Class with honours ambayo ina GPA 4.0

*      Ukipata 65-69   utatunukiwa degree Upper second Class honours ambayo ina GPA  3.7

*      Ukipata 60-64   utatunukiwa degree Upper second class honours ambayo ina GPA 3.3

*      Ukipata 55-59   utatunukiwa degree lower Second class honours ambayo ina GPA 3.0

*      Ukipata 50-54   unatunukiwa degree lower second class honours ambayo ina GPA 2.7

*      Ukipata 45-49   unatunukiwa degree Third Class honours ambayo ina GPA 2.3

*      Ukipata 40-44   unatunukiwa degree Third Class honours ambayo ina GPA 2.0

 

·         Sio hivyo wote tunafahamu kuwa kuwa aina za simu tunazomiliki pia zina namna watu wanaziweka katika ubora, i-phone, sumsung, Nokia, Siemens, Motorola infinix, techno na kadhalika lakini sio hivyo tu zinatengenezwa wapi

 

·         Kumbuka hata aina za magari ambazo wazazi wetu wanamiliki yana ubora, wake, mabati, cement, unga na kila kitu duniani kinapimwa kutokana na ubora wake

 

·         Ni katika hali kama hiyo vilevile Mungu atazipima kazi ya kila mmoja na maisha ya kila mmoja duniani kwa msingi huo basi namna tunavyomtumikia Mungu duniani katika Nyanja yoyote ile mwisho wa siku Mungu atazipima kazi zetu kuwa zina thamani ya kiwango gani ona

 

1Wakoritho 3:12-15 “Lakini kama mtu akijenga juu ya msingi huo, dhahabu au fedha au mawe ya thamani, au miti au majani au manyasi, kazi ya kila mtu itakuwa dhahiri. Maana siku ile itaidhihirisha, kwa kuwa yafunuliwa katika moto; na ule moto wenyewe utaijaribu kazi ya kila mtu, ni ya namna gani. Kazi ya mtu aliyoijenga juu yake ikikaa, atapata thawabu. Kazi ya mtu ikiteketea, atapata hasara; ila yeye mwenyewe ataokolewa; lakini ni kama kwa moto.”

 

Viwango ni Muhimu kwa sababu ndivyo vinavyotofautisha katia ya ubora wa jambo Fulani na lingine katika maisha yetu Mungu namekusudia sisi tuwe na viwango vya juu sana vya maisha tukiishi kwa viwango vya juu kabisa vya ubora Mungu atajivunia maisha yetu, Mungu hujivunia watu wake wanaoishi kwa ubora alioukusudia hapa Duniani lakini Mungu pia huuzunishwa tunapoishi chini ya kiwango ona 

 

Ayubu 1:1-8 “Palikuwa na mtu katika nchi ya Usi, jina lake alikuwa akiitwa Ayubu; mtu huyo alikuwa mkamilifu na mwelekevu, ni mmoja aliyemcha Mungu, na kuepukana na uovu. Kisha walizaliwa kwake wana saba, na binti watatu. Mali yake nayo yalikuwa ni kondoo elfu saba, na ngamia elfu tatu, na jozi za ng'ombe mia tano, na punda wake mia tano, na watu wa nyumbani wengi sana; basi hivi mtu huyo alikuwa ni mkuu sana kuliko watu wote wa upande wa mashariki. Nao wanawe huenda na kufanya karamu katika nyumba ya kila mmoja wao kwa siku yake; nao wakatuma na kuwaita maumbu yao watatu ili waje kula na kunywa pamoja nao. Basi ilikuwa, hapo hizo siku za karamu zao zilipokuwa zimetimia, Ayubu hutuma kwao akawatakasa, kisha akaamka asubuhi na mapema, na kusongeza sadaka za kuteketezwa kama hesabu yao wote ilivyokuwa; kwani Ayubu alisema, Yumkini kwamba hawa wanangu wamefanya dhambi, na kumkufuru Mungu mioyoni mwao. Ndivyo alivyofanya Ayubu sikuzote. Ilikuwa, siku moja ambayo hao wana wa Mungu walikwenda kujihudhurisha mbele za Bwana, Shetani naye akaenda kati yao.  Bwana akamwuliza Shetani, Umetoka wapi wewe? Ndipo Shetani akamjibu Bwana, na kusema, Natoka katika kuzunguka-zunguka duniani, na katika kutembea huku na huku humo. Kisha Bwana akamwuliza Shetani, Je! Umemwangalia huyo mtumishi wangu Ayubu? Kwa kuwa hapana mmoja aliye kama yeye duniani, mtu mkamilifu na mwelekevu, mwenye kumcha Mungu na kuepukana na uovu.”

 

Tunapoishi kwa kiwango Mungu hujivunia sana lakini tukiishi chini ya kiwango tutadharaulika, Paulo Mtume alimtaka Askofu kijana Timotheo kuzingatia kutunza ubora wake  katika Nyanja zote za usemi, mwenendo, imani, upendo na usafi, ili asije akadharaulika  ona

 

 1Timotheo 4:12-14 “Mtu awaye yote asiudharau ujana wako, bali uwe kielelezo kwao waaminio, katika usemi na mwenendo, na katika upendo na imani na usafi. Hata nitakapokuja, ufanye bidii katika kusoma na kuonya na kufundisha. Usiache kuitumia karama ile iliyomo ndani yako, uliyopewa kwa unabii na kwa kuwekewa mikono ya wazee.”

 

Jinsi ya kuishi kwa viwango:      

 

Warumi 12:1-2 “Basi, ndugu zangu, nawasihi, kwa huruma zake Mungu, itoeni miili yenu iwe dhabihu iliyo hai, takatifu, ya kumpendeza Mungu, ndiyo ibada yenu yenye maana. Wala msiifuatishe namna ya dunia hii; bali mgeuzwe kwa kufanywa upya nia zenu, mpate kujua hakika mapenzi ya Mungu yaliyo mema, ya kumpendeza, na ukamilifu.”

 

Mungu anamtarajia kila mmoja wetu kuishi kwa viwango vya juu ambavyo sio vya ulimwengu huu jambo hili linawezekana na ndio maana maandiko yanamtia moyo kila mmoja kuishi katika viwango vya juu, ushindi wetu dhidi ya adui yetu shetani na mafanikio kadhaa ya ahadi za Mungu kwetu yamewekwa katika kiwango, kila siku kuna kiwango ambacho Mungu amekusudia ukiishi  na ukifikie, kiwango cha juu cha kuishi maishanyanayompendeza Mungu ni kuishi maisha ya utakatifu, na kufikia kwenye cheo cha kimo cha utimilifu wa Kristo, hilo ndio lengo letu kuu.

 

1Petro 1:14-16 “Kama watoto wa kutii msijifananishe na tamaa zenu za kwanza za ujinga wenu; bali kama yeye aliyewaita alivyo mtakatifu, ninyi nanyi iweni watakatifu katika mwenendo wenu wote; kwa maana imeandikwa, Mtakuwa watakatifu kwa kuwa mimi ni mtakatifu.”

 

Tukiishi maisha matakatifu tutaweza kufurahia kwa kiwango cha juu yale ambayo Mungu ameyakusudia kwetu katika ahadi zake na katika neno lake ili tuweze kufikia kiwango ambacho Mungu anakitaka hatuna budi kufanya yafuatayo.

 

1.       Amua kuishi kwaajili ya Mungu, Mungu ametupa kuchagua uzima au mauti laana au Baraka  Kumbukumbu 30:19-20 “Nazishuhudiza mbingu na nchi juu yenu hivi leo, kuwa nimekuwekea mbele yako uzima na mauti, baraka na laana; basi chagua uzima, ili uwe hai, wewe na uzao wako; kumpenda Bwana, Mungu wako, kuitii sauti yake, na kushikamana naye; kwani hiyo ndiyo uzima wako, na wingi wa siku zako; upate kukaa katika nchi Bwana aliyowaapia baba zako, Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo, kuwa atawapa.”

               

2.       Vunja uhusiano na watu wasiomcha Mungu 2Wakoritho 6:14-18 “Msifungiwe nira pamoja na wasioamini, kwa jinsi isivyo sawasawa; kwa maana pana urafiki gani kati ya haki na uasi? Tena pana shirika gani kati ya nuru na giza? Tena pana ulinganifu gani kati ya Kristo na Beliari? Au yeye aaminiye ana sehemu gani pamoja na yeye asiyeamini? Tena pana mapatano gani kati ya hekalu la Mungu na sanamu? Kwa maana sisi tu hekalu la Mungu aliye hai; kama Mungu alivyosema, ya kwamba, Nitakaa ndani yao, na kati yao nitatembea, nami nitakuwa Mungu wao, nao watakuwa watu wangu. Kwa hiyo, Tokeni kati yao, Mkatengwe nao, asema Bwana, Msiguse kitu kilicho kichafu, Nami nitawakaribisha. Nitakuwa Baba kwenu, Nanyi mtakuwa kwangu wanangu wa kiume na wa kike

 

3.       Acha tabia mabaya zisizofaa na ufanye mwili wako kuwa Hekalu la Mungu Roho Mtakatifu  1Wakoritho 6:19-20 “Au hamjui ya kuwa mwili wenu ni hekalu la Roho Mtakatifu aliye ndani yenu, mliyepewa na Mungu? Wala ninyi si mali yenu wenyewe; maana mlinunuliwa kwa thamani. Sasa basi, mtukuzeni Mungu katika miili yenu.”

 

4.       Tubu dhambi zako kwa kumaanisha kuziacha na Mungu atakupa rehema na neema ya kuishi maisha ya viwango Mithali 28:13 “Afichaye dhambi zake hatafanikiwa; Bali yeye aziungamaye na kuziacha atapata rehema.”

 

5.       Soma neno la Mungu kila siku na kuliishi Yoshua 1:8 “Kitabu hiki cha torati kisiondoke kinywani mwako, bali yatafakari maneno yake mchana na usiku, upate kuangalia kutenda sawasawa na maneno yote yaliyoandikwa humo; maana ndipo utakapoifanikisha njia yako, kisha ndipo utakapositawi sana.”

 

6.       Chukia anachochukia Mungu na penda anachokipenda, usifanye maovu na Mungu atakutumia sana  Mungu Daniel 11:32 “Na wao wafanyao maovu juu ya hilo agano atawapotosha kwa maneno ya kujipendekeza; lakini watu wamjuao Mungu wao watakuwa hodari, na kutenda mambo makuu.”

 

Kumbuka kuwa bidhaa nyingi zisizokidhi viwango huchomwa moto na kuteketezwa, kabisa, Mungu hataruhusu chochote kilicho kinyonge yaani kilicho chini ya ubora wake kingie mbinguni ona Ufunuo 21:27 “Na ndani yake hakitaingia kamwe cho chote kilicho kinyonge, wala yeye afanyaye machukizo na uongo, bali wale walioandikwa katika kitabu cha uzima cha Mwana-Kondoo.” Hatuna budi kumuomba Mungu atuongezee viwango, atpeleke katika kiwango cha juu, na atupe neema ili kwamba tusiishi sawa na viwango vya watu wa dunia hii, bali sisi tukapate kuishi kwa kiwango cha juu, tukamtumikie Mungu kwa kiwango cha juu, kila tunachokifanya tuhakikishe tunakifanya kwa kiwango cha juu, Mungu ni Mungu wa viwango pia.

 

Na. Rev. Innocent Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!     

       

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni