Jumatatu, 20 Desemba 2021

Nayahesabu mambo yote kuwa hasara kwaajili ya Kristo!


Wafilipi 3:4-11 “Walakini mimi ningeweza kuutumainia mwili. Mtu ye yote akijiona kuwa anayo sababu ya kuutumainia mwili, mimi zaidi. Nalitahiriwa siku ya nane, ni mtu wa taifa la Israeli, wa kabila ya Benyamini, Mwebrania wa Waebrania, kwa habari ya kuishika torati, ni Farisayo, kwa habari ya juhudi, mwenye kuliudhi Kanisa, kwa habari ya haki ipatikanayo kwa sheria sikuwa na hatia. Lakini mambo yale yaliyokuwa faida kwangu, naliyahesabu kuwa hasara kwa ajili ya Kristo. Naam, zaidi ya hayo, nayahesabu mambo yote kuwa hasara kwa ajili ya uzuri usio na kiasi wa kumjua Kristo Yesu, Bwana wangu; ambaye kwa ajili yake nimepata hasara ya mambo yote nikiyahesabu kuwa kama mavi ili nipate Kristo; tena nionekane katika yeye, nisiwe na haki yangu mwenyewe ipatikanayo kwa sheria, bali ile ipatikanayo kwa imani iliyo katika Kristo, haki ile itokayo kwa Mungu, kwa imani; ili nimjue yeye, na uweza wa kufufuka kwake, na ushirika wa mateso yake, nikifananishwa na kufa kwake; ili nipate kwa njia yo yote kuifikia kiyama ya wafu



Utangulizi:

Kwa watu au kampuni zinazofanya biashara neno hasara na faida ni maneno ya karibu sana katika misamiati ya kila siku ya maisha ya biashara, Kila wakati wanajua mwenendo wa biashara zao endapo wanapata faida au wanapata hasara, kusimama au kuendelea kwa Biashara yoyote ile kunategemeana na faida inayopatikana au hasara inayopatikana, kuendelea kwa biashara Fulani kunategemeana sana na jinsi biashara hiyo inavyoingiza faida, Marabi wa kiyahudi wengi walikuwa wanafahamu swala hili  la kibiashara nao wakalitumia katika kuainisha jambo lililo na umuhimu na lisilo na umuhimu  mfano utaweza kuona Mathayo 16:26 “Kwani atafaidiwa nini mtu akiupata ulimwengu wote, na kupata hasara ya nafsi yake? Au mtu atatoa nini badala ya nafsi yake?”

Katika somo letu la msingi Paulo mtume anatumia mtindo huo huo kuonyesha maswala ya msingi kwake na maswala yasiyo ya msingi, Wafilipi 3:7-8 “Lakini mambo yale yaliyokuwa faida kwangu, naliyahesabu kuwa hasara kwa ajili ya Kristo. Naam, zaidi ya hayo, nayahesabu mambo yote kuwa hasara kwa ajili ya uzuri usio na kiasi wa kumjua Kristo Yesu, Bwana wangu; ambaye kwa ajili yake nimepata hasara ya mambo yote nikiyahesabu kuwa kama mavi ili nipate Kristo;Unapofanya uchunguzi wa kimaandiko utaweza kuona kuwa hasara na faida inayozungumziwa hapa ni mambo ambayo ni ya msingi na mambo ambayo sio ya msingi, na hii inatusaidia sisi nasi leo kujihoji na kutafakari kuwa ni mambo gani tunayapa kipaumbele kama mambo ya msingi na mambo yapi hatuyapi kipaumbele yaani mambo yasiyo ya msingi katika maisha!. Kwaajili ya hayo hapo tutaweza kugundua mambo yaliyo na faida kwetu na mambo yasiyo na faida kwetu, Paulo mtume aliyahesabu mambo yote yasiyo na faida kama hasara na kuyahesabu kuwa kama mavi kutokana na faida ya kumpata Yesu. Ni mambo gani hayo ya msingi ambayo aliyazingatia kisha baadaye akayaacha na kuona ni afadhali kupata hasara iwa mambo ambayo mwanzoni alifikikuwa yana faida kwake:-

1.       Dini za wazazi wetu.

 

Kama kuna jambo litawapa hasara kubwa sana watu wengi ni pamoja na kung’ang’ania dini za wazazi wao, hizi ni zile imani ambazo tumezirithi kutoka kwa wazazi wetu, imani hizi zitatuleta katika hasara kubwa badala ya faida, Paulo Mtume alikuwa akipambana vikali na watu waliokuwa wakihubiri dini ya kiyahudi na kufikiri kuwa ni dini bora zaidi kuliko kumpata Yesu, ni ukweli ulio wazi na dhahiri kuwa hakuna urithi wa kiroho, hali ya kiroho ya kila mtu inategemeana na yeye anavyokutana na Mungu kwa binafsi na sio kwa sababu ya wazazi, wake nyakati za namna hiyo kwa sasa haziko tena, watu wengi leo hii wako katika madhehebu au dini Fulani kwa sababu tu eti babu yake baba yake na ndugu zake wote walizaliwaga humo, kwa hiyo mtu yuko tayari kwenda Motoni na kutokumkubali Kristo kwa sababu tu anaiona dini ya baba zake kuwa ina faida, Wayahudi wengi sana walidhani kuwa Mungu atawahesabia haki kwa sababu wao ni watoto wa Ibrahimu, Yesu aliwajibu wazi kuwa huwezi kuwa mtoto wa Ibrahimu kisha ukawa muuaji, kwa vyovyote vile wayahudi hawakujua kuwa tayari wamekuwa na baba mwingine

 

Yohana 8:39-44 “Wakajibu, wakamwambia, Baba yetu ndiye Ibrahimu! Yesu akawaambia, Kama mngekuwa watoto wa Ibrahimu, mngezitenda kazi zake Ibrahimu. Lakini sasa mnatafuta kuniua mimi, mtu ambaye nimewaambia iliyo kweli, niliyoisikia kwa Mungu. Ibrahimu hakufanya hivyo. Ninyi mnazitenda kazi za baba yenu. Ndipo walipomwambia, Sisi hatukuzaliwa kwa zinaa; sisi tunaye Baba mmoja, yaani, Mungu. Yesu akawaambia, Kama Mungu angekuwa baba yenu, mngenipenda mimi; kwa maana nalitoka kwa Mungu, nami nimekuja; wala sikuja kwa nafsi yangu, bali yeye ndiye aliyenituma. Mbona hamyafahamu hayo niyasemayo? Ni kwa sababu ninyi hamwezi kulisikia neno langu. Ninyi ni wa baba yenu, Ibilisi, na tamaa za baba yenu ndizo mpendazo kuzitenda. Yeye alikuwa mwuaji tangu mwanzo; wala hakusimama katika kweli, kwa kuwa hamna hiyo kweli ndani yake. Asemapo uongo, husema yaliyo yake mwenyewe; kwa sababu yeye ni mwongo, na baba wa huo.”   

 

Wayahudi wengi walijifikiri wako sahihi kwa sababu baba yao ni Ibrahimu, walidhani hali ya kiroho inaweza kurithiwa kwa jinsi ya mwili na kwa kushika mapokeo ya baba zao, Lakini Yesu alikuwa akiwajulisha kuwa huwezi kurithi hali ya kiroho bila kuamua kufuata mambo ya rohoni wewe mwenyewe, Paulo mtume anaonyesha hali kama hiyo kuwa kabla hajamjua Yesu alifikiri kuwa ana haki zote vilevile kama wayahudi wengine naye alikuwa mwenye bidii sana katika maswala ya imani akijua kuwa yatampa faida kubwa sana kwa kumpendeza Mungu kupitia taratibu za baba zake na mila za kwao na madhehebu ya kwao na kupitia vyuo vyao, lakini alipomfahamu Yesu alifahamu kuwa yale mambo ya kwanza aliyokuwa akiyashikilia na kufikiri kuwa na faida sasa anaachana nayo na kuyaiona kuwa ni hasara ukilinganisha na uzuri wa kumpokea Kristo:-

 

Wafilipi 3:3-7 “Maana sisi tu tohara, tumwabuduo Mungu kwa Roho, na kuona fahari juu ya Kristo Yesu, wala hatuutumainii mwili. Walakini mimi ningeweza kuutumainia mwili. Mtu ye yote akijiona kuwa anayo sababu ya kuutumainia mwili, mimi zaidi.Nalitahiriwa siku ya nane, ni mtu wa taifa la Israeli, wa kabila ya Benyamini, Mwebrania wa Waebrania, kwa habari ya kuishika torati, ni Farisayo, kwa habari ya juhudi, mwenye kuliudhi Kanisa, kwa habari ya haki ipatikanayo kwa sheria sikuwa na hatia. Lakini mambo yale yaliyokuwa faida kwangu, naliyahesabu kuwa hasara kwa ajili ya Kristo.”

 

Paulo anaonyesha kuwa yeye kama ni kuitumainia Dini aliitumainia sana, alitahiriwa siku ya nane kama dini yao ilivyoagiza,  alikuwa ni muisraeli yaani ni myahudi kama walivyo wayahudi wengine, alizaliwa katika kabila la Benjamin, alikuwa mwebrania halisi, na alikuwa wa madhehebu ya mafarisayo na aliishika torati, na aliliudhi kanisa na kuwatesa wakristo akifikiri kuwa ni sawa kwa mujibu wa dini yao, na aliishika torati hasa na kuwa kwa habari ya kuishika torati hakuwa na dhambi yoyote, Paulo anaonyesha jinsi alivyokuwa jemadari wa kuishi maisha ya haki kwa niaba ya dini yake  na aliipigania.

 

·         Aliishika torati tangu utoto, yeye alipitia mafunzo ya sharia chini ya mkufunzi aliyeheshimika sana na wayahudi aliyeitwa Gamaliel ona

 

Matendo 22:3 “Mimi ni mtu wa Kiyahudi, nalizaliwa Tarso, mji wa Kilikia, ila nililelewa katika mji huu, miguuni pa Gamalieli, nikafundishwa sheria ya baba zetu kwa usahihi, nikawa mtu wa jitihadi kwa Mungu kama ninyi nyote mlivyo leo hivi;”

 

Matendo 5:34 “Lakini mtu mmoja, Farisayo, jina lake Gamalieli, mwalimu wa torati, mwenye kuheshimiwa na watu wote, akasimama katika baraza, akaamuru mitume wawekwe nje kitambo kidogo,”

 

Gamaliel alikuwa ni Rabbi aliyeheshimika sana, kusoma kwake ni kama kusoma chuo kikuu kilichoheshimika sana kwa wakati huo kwa kuwa alikuwa ni Mwalimu wa sharia aliyebobea sana katika madhehebu ya mafarisayo, na Paulo mtume alikuwa mwanafunzi wa mkufunzi huyu wa kiyahudi. Lakini hata hivyo alipompata Yesu degree zake za dini ya kiyahudi alizihesabu kuwa si kitu au ni hasara ukilinganisha na kumpata Yesu Kristo!

 

·         Alikuwa Farisayo yaani moja ya madhehebu yaliyokuwa yakiheshimika sana kwa mitazamo mikali sana na iliyohesabika kama dini sahihi zaidi  Matendo 26:5 “wakinijua sana tangu mwanzo, kama wakipenda kushuhudia, ya kwamba nalikuwa Farisayo kwa kuifuata madhehebu ya dini yetu iliyo sahihi kabisa.”

 

·         Kwa habari ya wivu zeal yaani imani kali Paulo alikuwa na imani kali kiasi cha kutumika kuliudhi kanisa ona

 

Wafilipi 3:6 “kwa habari ya juhudi, mwenye kuliudhi Kanisa, kwa habari ya haki ipatikanayo kwa sheria sikuwa na hatia”. 

 

Matendo 8:3 “Sauli akaliharibu kanisa, akiingia kila nyumba, na kuwaburuta wanaume na wanawake na kuwatupa gerezani.”

 

Matendo 9:1-2 “Lakini Sauli, akizidi kutisha na kuwaza kuwaua wanafunzi wa Bwana, akamwendea Kuhani Mkuu, akataka ampe barua za kuenda Dameski zilizoandikwa kwa masinagogi, ili akiona watu wa Njia hii, waume kwa wake, awafunge na kuwaleta Yerusalemu

                               

·         Kwa asili alikuwa myahudi ni wa uzao wa Ibrahimu

·         Kwa asili alikuwa mbenjamin kabila mojawapo halisi la kiyahudi

·         Kwa asili alikuwa mwebrania wa waebrania, yaani alizaliwa akiwa mwebrania kweli kweli na kiutamaduni yeye ni mwebrania kwelikweli ambapo napo hakuwa na sababu ya kubagulika  Palulo mtume anaonyesha kuwa alikuwa amekamilika idara zote kwa habari ya dini, yeye sio tu alimcha Mungu bali pia alikuwa tayari kuuwa  na kuwatesa na kuwafunga wale wote aliodhani kuwa  hawamchi Mungu kwa mujibu wa dini yake, Paulo mtume alikuwa mtu aliyejitoa katika dini yake kuliko kawaida huu ulikuwa ni wakati ambapo hakuwa amemjua Yesu,  maisha yake ya awali katika dini yake yalikuwa ya muhimu na ya faida kwa wakati huo akijua ya kuwa anaingiza kwake na kwa Mungu wake, Lakini sasa alipobaini ya kuwa kwa Yesu kunalipa zaidi akabadili kibao na kuhesabu yale ya zamani kuwa hayana faida kama kumpata Yesu

 

Wafilipi 3:7 “Lakini mambo yale yaliyokuwa faida kwangu, naliyahesabu kuwa hasara kwa ajili ya Kristo. Naam, zaidi ya hayo, nayahesabu mambo yote kuwa hasara kwa ajili ya uzuri usio na kiasi wa kumjua Kristo Yesu, Bwana wangu; ambaye kwa ajili yake nimepata hasara ya mambo yote nikiyahesabu kuwa kama mavi ili nipate Kristo;”     

 

Unaweza kuona wako watu ambao wanadhani imani walizozirithi zina faida kubwa sana kwao na hawataki kuachana nazo kwa sababu ni mila, kwa sababu ndugu zao wote ni wa aina hiyo, hawataki kuziachia wakidhani kuwa yana faida kwao, wako wenye kuabudu mizimu, wako wenye kushika dini Fulani na desturi za aina Fulani, au imani zao zimewafikisha mahali Fulani, labda wamesomea maswala kadhaa katika imani zao, wana degree, wana phd, wana diploma za aina mbalimbali, wana heshima, wana wivu kwaajili ya miungu yao, wanaheshimika katika dini zao, wamepewa vyeo ni wazee wa kanisa, wamehiji maeneo matakatifu wako karibu na viongozi wakubwa wa kidini  wanaamini kuwa wamewekeza kwa faida na kiwango kikubwa sana katika dini zao, vyovyote vile iwavyo Paulo mtume alipobaini kuwa Yesu, analipa aliachana na kila kitu na kuyahesabu yote kuwa ni hasara  na kuwa faida kubwa ni kumpata Yesu!

Paulo mtume alikuwa amejifunza ya kuwa hakuna mtu anaweza kuokolewa kwa matendo yake mema au sifa zake za zamani, Mungu hatuhesabii haki kwa sababu ya wema na matendo mazuri tuliyoyafanya katika dini zetu

Warumi 3:20-24 “kwa sababu hakuna mwenye mwili atakayehesabiwa haki mbele zake kwa matendo ya sheria; kwa maana kutambua dhambi huja kwa njia ya sheria. Lakini sasa, haki ya Mungu imedhihirika pasipo sheria; inashuhudiwa na torati na manabii; ni haki ya Mungu iliyo kwa njia ya imani katika Yesu Kristo kwa wote waaminio. Maana hakuna tofauti; kwa sababu wote wamefanya dhambi, na kupungukiwa na utukufu wa Mungu; wanahesabiwa haki bure kwa neema yake, kwa njia ya ukombozi ulio katika Kristo Yesu;”

Tunaishi katika ulimwengu wa pongezi, na wengi wanadhani kwa kufanya vizuri wanaweza kukubalika kwa Mungu na wanadamu pia lakini ukweli unabaki palepale kwamba mafanikio ya kiroho yanapatikana kwa kumuamini Yesu tu, tunapofanya mema tukumbuke maelekezo ya Yesu ya kuwa tumefanya tu yatupasayo kufanywa, Luka 17:10 “Vivyo hivyo nanyi, mtakapokwisha kuyafanya yote mliyoagizwa, semeni, Sisi tu watumwa wasio na faida; tumefanya tu yaliyotupasa kufanya.” Kutumainia lolote nje ya Yesu Kristo ni kutumainia hasara.

2.       Mila na desturi za baba zetu.

Jambo linguine kubwa litakalowatesa wengi na kuwapeleka Motoni ni kushika mila na desturi za baba zao au babu zao, Jambo hili vilevile liliwaathiri wayahudi, walidhani ya kuwa wanaweza kuokolewa kupitia mila zao na hivyo walishika sana mila zao na desturi kiasi cha kusahahu kujua Mungu anataka nini kwao kuna watu wengi sana leo wanayashika mapokeo ya madhehebu yao, mila na desturi za wazee wao na kuacha kuliangalia neno la Mungu kwa undani hii ilikuwa shida kubwa kwa wayahudi wa kawaida na kwa Paulo Mtume pia Mathayo 15:1-3 “Ndipo Mafarisayo na waandishi toka Yerusalemu walipomwendea Yesu wakisema, Mbona wanafunzi wako huyahalifu mapokeo ya wazee, kwa maana hawanawi mikono walapo chakula. Akajibu, akawaambia, Mbona ninyi nanyi huihalifu amri ya Mungu kwa ajili ya mapokeo yenu?Yesu alikemea vikali sana na kuiita tabia hii kuwa ni ya kinafiki alionya vikali kutokuhubiri neno la Mungu na kuhubiri mila na desturi ambayo kwa lugha nyingine aliyaita maagizo ya wanadamu au mapokeo ya wanadamu ona Mathayo 15:7-9 “Enyi wanafiki, ni vema alivyotabiri Isaya kwa habari zenu, akisema, Watu hawa huniheshimu kwa midomo; Ila mioyo yao iko mbali nami. Nao waniabudu bure, Wakifundisha mafundisho Yaliyo maagizo ya wanadamuNabii Yohana aliwaonya vikali na mapema wayahudi kuwa kujifikiri ya kuwa wanaye baba ndiye Ibrahimu bila kufungua mioyo yao na kumpokea masihi kwa imani ona Mathayo 3:7-10 “Hata alipoona wengi miongoni mwa Mafarisayo na Masadukayo wakiujia ubatizo wake, aliwaambia, Enyi wazao wa nyoka, ni nani aliyewaonya ninyi kuikimbia hasira itakayokuja? Basi zaeni matunda yapasayo toba; wala msiwaze mioyoni mwenu kwamba, Tunaye baba, ndiye Ibrahimu; kwa maana nawaambia ya kwamba Mungu aweza katika mawe haya kumwinulia Ibrahimu watoto. Na shoka limekwisha kuwekwa penye mashina ya miti; basi kila mti usiozaa matunda mazuri hukatwa na kutupwa motoni.” Swala la mila na desturi lilisumbua mno nyakati za kanisa la kwanza na linasumbua hata leo, watu wengi wameacha kweli ya neno la Mungu na wanasumbuliwa na mafundisho na mapokeo ya wanadamu na hivyo wanaweza kujikuta kuwa wanapata hasara kwa kufuata desturi za kidhehebu, kimila na taratibu zilizowekwa na wanadamu, Paulo aliyashika sana mapokeo ya baba zake ona Wagalatia 1:14 “Nami naliendelea katika dini ya Kiyahudi kuliko wengi walio hirimu zangu katika kabila yangu, nikajitahidi sana katika kuyashika mapokeo ya baba zangu.” Hata hivyo baada ya kumjua Kristo aliliasa kanisa kuachana na aina hii ya Elimu yenye kupotosha ambayo kismingi sio neno la Kristo Wakolosai 2:8 “Angalieni mtu asiwafanye mateka kwa elimu yake ya bure na madanganyo matupu, kwa jinsi ya mapokeo ya wanadamu, kwa jinsi ya mafundisho ya awali ya ulimwengu, wala si kwa jinsi ya Kristo.” Ukristo utakuwa na nguvu kubwa sana kama watu wataacha mapokeo ya kujifunza kulishika neno la Mungu ambalo kimsingi ni kumjua Yesu Kristo jambo hili ndio lenye faida kubwa sana kuliko tunavyoweza kufikiri.          

Faida kubwa iko katika kumjua Yesu Kristo

Tangu nyakati za nabii Yeremia maandiko yalionyesha kuwa jambo lanye faida kubwa na la kujivunia ni kumjua Yesu, Mungu anataka tujivunie kumjua yeye zaidi ya kitu kingine chochote!

Yeremia 9:23-24 “Bwana asema hivi, Mwenye hekima asijisifu kwa sababu ya hekima yake, wala mwenye nguvu asijisifu kwa sababu ya nguvu zake, wala tajiri asijisifu kwa sababu ya utajiri wake; bali ajisifuye na ajisifu kwa sababu hii, ya kwamba ananifahamu mimi, na kunijua, ya kuwa mimi ni Bwana, nitendaye wema, na hukumu, na haki, katika nchi; maana mimi napendezwa na mambo hayo, asema Bwana,”       

Paulo anaiona faida kwa kumjua Yesu Kristo Wafilipi 3:8 “Naam, zaidi ya hayo, nayahesabu mambo yote kuwa hasara kwa ajili ya uzuri usio na kiasi wa kumjua Kristo Yesu, Bwana wangu; ambaye kwa ajili yake nimepata hasara ya mambo yote nikiyahesabu kuwa kama mavi ili nipate Kristo;”

Hili ndio jambo lenye faida kubwa mno, kumjua Yesu, kuwa na uhusiano naye na zaidi sana hata kutamani kwenda kukaa naye milele na milele Wafilipi 3:9-10 “tena nionekane katika yeye, nisiwe na haki yangu mwenyewe ipatikanayo kwa sheria, bali ile ipatikanayo kwa imani iliyo katika Kristo, haki ile itokayo kwa Mungu, kwa imani; ili nimjue yeye, na uweza wa kufufuka kwake, na ushirika wa mateso yake, nikifananishwa na kufa kwake;Kumjua Yesu kristo kuna faida kubwa sana, kumjua yeye kunaaanza na kusoma habari zake, ili tuziamini na kwa kumuamini yeye tunakuwa na uzima tena uzima wa milele ona Yohana 20:30-31 “Basi kuna ishara nyingine nyingi alizozifanya Yesu mbele ya wanafunzi wake, zisizoandikwa katika kitabu hiki. Lakini hizi zimeandikwa ili mpate kuamini ya kwamba Yesu ndiye Kristo, Mwana wa Mungu; na kwa kuamini mwe na uzima kwa jina lake

Muhimu

Wafilipi 3:10-11 “ili nimjue yeye, na uweza wa kufufuka kwake, na ushirika wa mateso yake, nikifananishwa na kufa kwake; ili nipate kwa njia yo yote kuifikia kiyama ya wafu.”

Kuna mambo mengi ambayo tungependa kuyajua duniani kwa sababu tunataka kuitawala dunia,na kuyajua mazingira yetu ya sasa na kukabiliana na changamoto za ulimwengi huu kila mmoja ana mengi ambayo kwayo anaweza kuyaona kuwa yana faida nyingisana, hata katika maisha tunatoa kipaumbele kwa mambo tunayodhani na kufikiri kuwa ni ya Muhimu na yana faida kubwa sana kama ilivyiokuwa kwa Paulo mtume hata hivyo tunapaswa kumuelewa kuwa kwa nini alitamani sana kumuona Kristo Paulo alikuwa na uelelewa kuwa kumjua Yesu Kristo lilikuwa jambo lenye faida pan asana na hivyo aliyahesabu mabo mengine yote kuwa ni hasara na kuyafafnanisha na mavi, ili kumpata Kristo

Rev. Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!      

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni