Jumatatu, 4 Julai 2022

Msiwape Mbwa kilicho kitakatifu, wala msitupe lulu zenu mbele ya nguruw

Matthayo 7:6 “Msiwape mbwa kilicho kitakatifu, wala msitupe lulu zenu mbele ya nguruwe, wasije wakazikanyaga chini ya miguu yao, wakageuka na kuwararua.”                  


Utangulizi:

Ni muhimu kufahamu kuwa hapa Yesu anatumia lugha ya mfano (mficho) iitwayo Metaphor ambapo neno au maneno yanayotumika katika hali ya kawaida yanaweza kumaanisha matumizi,  ya kitu au jambo lingine au linalofanana na hilo, Yesu anawatumia umbwa na nguruwe hapa akiwaonya wanafunzi wake kuwa na ufahamu na kuelewa unyeti wa kuwapa vitu vya thamani watu wasio na shukrani, Wanyama kama mbwa na nguruwe hawawezi kufurahia uadilifu, wala kushukuru kwa sababu hawajui thamani ya kile wanachofanyiwa

2Petro 2:20-22 “Kwa maana wale waliokwisha kuyakimbia machafu ya dunia kwa kumjua Bwana na Mwokozi Yesu Kristo, kama wakinaswa tena na kushindwa, hali yao ya mwisho imekuwa mbaya kuliko ile ya kwanza. Maana ingekuwa heri kwao kama wasingaliijua njia ya haki, kuliko kuijua, kisha kuiacha ile amri takatifu waliyopewa. Lakini imetukia kwao sawasawa na ile mithali ya kweli, Mbwa ameyarudia matapiko yake mwenyewe, na nguruwe aliyeoshwa amerudi kugaa-gaa matopeni.”

Hali kadhalika wako wanadamu, ambao kwa namna moja ama nyingine, sio waadilifu, hawana moyo safi, wenye nia ovu, waliokataa kuwa na Mungu nafsini mwao hawawezi kwa namna yoyote ile  kukubaliana na maelekezo mema yanayotolewa kuhusu injili aidha pia mwisho wa kila kitu wanaweza kuwadhuru hata wale wanaoihubiri injili,  kwa ujumla ujumbe unahusu wale ambao hawawezi kukubali habari njema lakini sio tu kuikubali hatimaye kuwakataa wanaoihubiri. Au hata anayehubiriwa !

Kwa muda Mrefu sana wayahudi walikuwa wakimsubiri Masihi aliyeahidiwa kama mkombozi wao, na zaidi ya yote walikuwa wamechoshwa na hali ya kuwa watumwa wa mataifa mengine na walikuwa wkiutazamia uhuru wa kweli chini ya serikali ya kweli ambayo ingeongozwa na Masihi yaani ufalme wa Mung, Yesu alikuja akiwa anahubiri habari hizo na kuwathibitia shia kuwa ufalme wa Mungu umekaribia ona Mathayo 4:17 “Tokea wakati huo Yesu alianza kuhubiri, na kusema, Tubuni; kwa maana ufalme wa mbinguni umekaribia.” Wale waliomuamini na kumkubali walikuwa tayari kuwashirikisha na wengine habari hii njema, lakini hata hivyo wengi hawakuiamini, badala yake walimuona kuwa mzushi na mtu ambaye anakufuru

Mark 14:61-65 “Lakini akanyamaza, wala hakujibu neno. Kuhani Mkuu akamwuliza tena, akamwambia, Wewe ndiwe Kristo, Mwana wake Mtukufu? Yesu akasema, Mimi ndiye, nanyi mtamwona Mwana wa Adamu ameketi mkono wa kuume wa nguvu, akija na mawingu ya mbinguni. Kuhani Mkuu akararua nguo zake, akisema, Tuna haja gani tena ya mashahidi? Mmesikia kufuru yake; mwaonaje ninyi? Wote wakamhukumu kuwa imempasa kuuawa. Wengine wakaanza kumtemea mate, wakamfunika uso, na kumpiga makonde, na kumwambia, tabiri. Hata watumishi nao wakampiga makofi.”

Yesu aliyasema haya mapema akiwa anaelewa kuwa ni watu wa namna gani wanamzunguka nan i mambo gani yatawatokea, watu wanaolihubiri neno la Mungu hawapendwi, ni vigumu kuwakubali watu wanaosema kweli, wanaoongoza wengi katika njia ya haki, hivyo japokuwa wanaifanya kazi iliyo njema lakini matokeo yake ni kuwa watalipwa mabaya

Yohana 16:1-4 “Maneno hayo nimewaambia, msije mkachukizwa. Watawatenga na masinagogi; naam, saa yaja atakapodhania kila mtu awauaye ya kuwa anamtolea Mungu ibada. Na hayo watawatenda kwa sababu hawakumjua Baba wala mimi. Lakini nimewaambia hayo, ili makusudi saa ile itakapokuja myakumbuke ya kuwa mimi naliwaambia. Sikuwaambia hayo tangu mwanzo, kwa sababu nalikuwapo pamoja nanyi.”

Kazi kubwa ya injili pamoja na mafanikio yake yote ni kuwapa watu uzima wa milele Yohana 10:28 Nami nawapa uzima wa milele; wala hawatapotea kamwe; wala hakuna mtu atakayewapokonya katika mkono wangu. Zawadi hii inatolewa kwa kuitangaza injili, lakini ni katika namna ya kushangaza sana wahubiri wa injili mara kadhaa wameonekana kama kitu cha kukataliwa kutupwa na kufanywa kuwa takataka za dunia, kusema vibaya kama watu waliotolewa wahukumiwe kuuawa ona

1Wakorintho 4:9-13 “Maana nadhani ya kuwa Mungu ametutoa sisi mitume mwisho, kama watu waliohukumiwa wauawe; kwa sababu tumekuwa tamasha kwa dunia; kwa malaika na wanadamu. Sisi tu wapumbavu kwa ajili ya Kristo, lakini ninyi ni wenye akili katika Kristo; sisi tu dhaifu, lakini ninyi mna nguvu; ninyi mna utukufu, lakini sisi hatupati heshima. Hata saa hii ya sasa, tuna njaa na kiu, tu uchi, twapigwa ngumi, tena hatuna makao; kisha twataabika tukifanya kazi kwa mikono yetu wenyewe. Tukitukanwa twabariki, tukiudhiwa twastahimili; tukisingiziwa twasihi; tumefanywa kama takataka za dunia, na tama ya vitu vyote hata sasa.”

Katika tamaduni za kiyahudi Umbwa na Nguruwe ni alama ya wanyama wachafu na Najisi sawa na wanavyotamkwa katika maandiko Walawi 11:7-8 “Na nguruwe, kwa sababu yeye anazo kwato, ni mwenye miguu iliyopasuka kati, lakini hacheui, yeye ni najisi kwenu. Msiile nyama yao, wala msiiguse mizoga yao; hao ni najisi kwenuwanyama hawa wanakula chochote kile na ni wakali hasa wanapojisikia njaa, wanapotumika kama mfano katika mithali kuwawakilisha wanadamu, au watu wachafu, baradhuli, wasio na uadilifu, na wapuuzi, ni ukweli ulio wazi kuwa ni udhalilishaji wa hali ya juu sana mtu akikutukana au kukuita Mbwa au nguruwe! Hususani katika jamii ya kiyahudi, lakini hata hivyo Yesu hasiti kufananisha mtu, umbwa na Nguruwe, akiwalinganisha na watu waliomkataa masihi, kusudi lake sio kuwadhalilisha, lakini mkazo wake sio watu wengine lakini wale wanaodhaniwa kuwa watu wa Mungu na kisha wanakataa karama za Mungu, na mwito wake, Hivyo Yesu anaonya kuwa usipoteze Muda na watu wanaojiita Ndugu lakini hawayahsiki mafundisho nan i wakristo wa uongo

1Wakoritho 5:11-12 “Lakini, mambo yalivyo, naliwaandikia kwamba msichangamane na mtu aitwaye ndugu, akiwa ni mzinzi au mwenye kutamani au mwenye kuabudu sanamu au mtukanaji au mlevi au mnyang'anyi; mtu wa namna hii msikubali hata kula naye.Maana yanihusu nini kuwahukumu wale walio nje? Ninyi hamwahukumu hao walio ndani?

Neno la Mungu limeagiza kuendelea kuihubiri injili na hivyo lazima tutakutana na watu mbalimbali katika kuihubiri injili 1Petro 3:15 “Mwe tayari siku zote kumjibu kila mtu awaulizaye habari za tumaini lililo ndani yenu; lakini kwa upole na kwa hofu.” Kwa hiyo hatupaswi kuogopa kuwahubiria watu habari njema, lakini wakati mwingine hatuna budi kuwa makini kwamba wako mbwa na nguruwe ambao kile unachokitoa kwao, hakitazaa matunda yanayokusudiwa na badala yake watakurarua kwa sababu hawaijui thamani ya neno la Mungu, wala hawajui thamani ya Yesu unayemuhubiri na hivyo hawawezi kukukubali wewe unayebeba mambo yale ya thamani, hii haimaanishi tuwachukie wasioamini au wale wanaoipinga injili lakini kuwa makini na kutambua kuwa tutakataliwa, na tusipoteze muda na watu wasioona umuhimu wa injili, zawadi za Mungu na kuwekeza muda wetu kwa wapinzani wa injili ambao wanaelekea shimoni na wakiishikia injili au mafundisho wanachukizwa

Mathayo 15:12-14 “Ndipo wanafunzi wake walipomwendea, wakamwambia, Wajua ya kuwa Mafarisayo walipolisikia neno lile walichukizwa? Akajibu, akasema, Kila pando asilolipanda Baba yangu wa mbinguni litang'olewa. Waacheni; hao ni viongozi vipofu wa vipofu. Na kipofu akimwongoza kipofu mwenzake, watatumbukia shimoni wote wawili.”            

Wale ambao wataipinga injili na mafundisho yetu simple rahisi tu Yesu aliagiza kuwa sio tu tuwache lakini vilevile tukung’ute mavumbi ya miguuni mwetu

Mathayo 10:14-15 “Na mtu asipowakaribisha wala kuyasikiliza maneno yenu, mtokapo katika nyumba ile, au mji ule, kung'uteni mavumbi ya miguuni mwenu. Amin, nawaambia, itakuwa rahisi nchi ya Sodoma na Gomora kustahimili adhabu ya siku ya hukumu, kuliko mji ule.”

Hata hivyo wahubiri wa injili hawapaswi kukata tamaa, na wanapaswa kuendelea kuihubiri injili, kwani sio watu wote wataipinga injili wako wale wanaomcha Mungu ambao Bwana atafungua mioyo yao ili wayatunze yale tunayoyahubiri;-

Matendo 16:13-15 “Hata siku ya sabato tukatoka nje ya lango, tukaenda kando ya mto, ambapo tukadhani ya kuwa pana mahali pa kusali; tukaketi, tukasema na wanawake waliokutana pale. Mwanamke mmoja, jina lake Lidia, mwenye kuuza rangi ya zambarau, mwenyeji wa Thiatira, mcha Mungu, akatusikiliza, ambaye moyo wake ulifunguliwa na Bwana, ayatunze maneno yaliyonenwa na Paulo.Hata alipokwisha kubatizwa, yeye na nyumba yake, akatusihi, akisema, Kama mmeniona kuwa mwaminifu kwa Bwana, ingieni nyumbani mwangu mkakae. Akatushurutisha.”

Aidha ikumbukwe kuwa wakati wote mlango mmoja wa kuihubiri injli ukifungwa Mungu atafungua mlango mwingine, kwani wako watu wenye kiu ya neno la Mungu ambao Mungu amewaandaa kuipokea injili na habari njema za Yesu Kristo bila kikwazo japo changamoto zitaendelea kuwepo ona Matendo 16:6-10 “Wakapita katika nchi ya Frigia na Galatia, wakikatazwa na Roho Mtakatifu, wasilihubiri lile neno katika Asia. Walipofika kukabili Misia wakajaribu kuenda Bithinia, lakini Roho wa Yesu hakuwapa ruhusa, wakapita Misia wakatelemkia Troa. Paulo akatokewa na maono usiku; alimwona mtu wa Makedonia amesimama, akimsihi, na kumwambia, Vuka, uje Makedonia utusaidie.Basi alipokwisha kuyaona yale maono, mara tukataka kutoka kwenda Makedonia, kwa kuwa tuliona hakika ya kwamba Mungu ametuita tuwahubiri Habari Njema.”

Aidha wahudumu wa injili wanapaswa kutambua kuwa sio kila wakati watakutana na changamoto kwani iko miji Mingine ambako Mungu ana wau wake na usalama kwaajili yetu upo Matendo 18:9-10 “Bwana akamwambia Paulo kwa maono usiku, Usiogope, bali nena, wala usinyamaze, kwa kuwa mimi ni pamoja nawe, wala hapana mtu atakayekushambulia ili kukudhuru; kwa maana mimi nina watu wengi katika mji huu.”               

Ni maombi yangu kuwa Mungu anipe watu, watakaofunguliwa na Bwana wayatunze ninayoyahubiri na kuyafundisha badala ya kuturarua, Aidha Roho Mtakatifu aendelee kufungua milango ya injili kwa wale wenye uhitaji wa kusaidiwa na Mungu atupe kukaa kwa amani pale ambako ana watu wengi na utisho wake utufunike ili maadui wa injili na ndugu za uongo wasigeuka na kutusumbua, tuendelee kulinena neno la Mungu kwa ujasiri tukijua wazi kuwa Yesu yuko Pamoja nasi, lakini tusiache kuwang’utia mavumbi wale wanaoikataa injili ili Mungu awaletee hukumu kwa haraka, kama yanenavyo maandiko! Awaye yote atakayejaribu kukupinga kwa sababu yu waihubiri injili Mungu akakutane naye, Bwana akulinde na Mbwa na Nguruwe wasioelewa utathamani wa kile ulichikibeba katika jina la Yesu!

Na. Rev. Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni