Jumanne, 8 Novemba 2022

Heri wenye Upole !


Mathayo 5:1-5 “Naye alipowaona makutano, alipanda mlimani; na alipokwisha kuketi, wanafunzi wake walimjia; akafumbua kinywa chake, akawafundisha, akisema, Heri walio maskini wa roho; Maana ufalme wa mbinguni ni wao. Heri wenye huzuni; Maana hao watafarijika. Heri wenye upole; Maana hao watairithi nchi.”


Utangulizi.

Nimekuwa kiongozi na Mchunjaji kwa Muda mrefu sana nimemtumikia Mungu kwa karibu robo tatu ya maisha yangu yote sasa, nimekutana na changamoto nyingi na za aijna mbalimbali, Pia nimewahi kupigana vita za aina mbalimbali za kiroho na naweza kukiri wazi kuwa hakuna vita nimewahi kushindwa kwa sababu wakati wote nilipopigana nalimtafuta Bwana ili awe upande wangu kwanza kwa hiyo ushindi wangu umetokana na Bwana mwenyewe kunipigania!, Moja ya changamoto kubwa kutoka kwa watu wanaonipiga vita katika uongozi wangu ni pamoja na kunishutumu kuwa mimi sifai kwa sababu ni MPOLE sikuhuzunika lakini hili lilinipa kutafakari kwani Upole ni sifa mbaya kwa mwanadamu? Au ni sifa Njema? Hili lilinifanya nianze kurejea katika maandiko na kuanza kujifunza kwa kina na mapana na marefu ili nipate kujua kuhusiana na UPOLE. Viongozi wakubwa sana katika maandiko wanaelezwa kuwa walikuwa wapole akiwemo Musa ona katika Hesabu 12:3 “Basi huyo mtu, huyo Musa, alikuwa mpole sana zaidi ya wanadamu wote waliokuwa juu ya uso wa nchi.” Unaona lakini sio hivyo tu Yesu akitoa mwaliko wa watu wenye kuelemewa na changamoto mbalimbali anajitaja mwenyewe kuwa ni mpole na mnyenyekevu wa Moyo unaweza kuona katika Mathayo 11:28-29 “Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha. Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata raha nafsini mwenu; Upole ni nini hasa je ni sababu ya kulaumiwa? Ni sifa mbaya? Ama ni sifa njema? Hili swala litupa nafasi ya kutafakari kwa kina na mapana na marefu katika somo hili katika jina la Yesu Kristo amen!

Maana ya Upole!

Katika hutuba maarufu sana ya Yesu Kristo inayojulikana kama Hutuba ya Mlimani, Yesu alifundisha pamoja na mafundisho mengine mafundisho ya HERI kama nane hivi ambazo kwa kiingereza zinaitwa Beatitudes ambalo maana yake ni “Supreme Blessedness” yaani mtu aliyebarikiwa sana sasa katika moja ya sifa hizo za watu waliobarikiwa sana mojawapo ni UPOLE kwa hiyo Mathayo 5:5 “Heri wenye upole; Maana hao watairithi nchi.” Maana yake wamebarikiwa sana wenye upole maana hao watairithi nchi kwa hiyo UPOLE ni Baraka UPOLE ni neema ya Mungu ya ngazi ya juu sana, lakini ni lazima nan i muhimu kuelewa maana na neno hilo UPOLE

Neno upole linalotumika katika Kiswahili kwenye Biblia ya kiingereza linasomeka kama MEEK ambalo kwa ujumla linabeba maana tajiri sana ambazo kimsingi zinaweza kukomba matunda yote ya roho yanayotajwa katika maandiko MEEK - MILD, SUBMISSIVE, MODERATE, QUITE, GENTLE, LONG-SUFFERING, PATIENT. Maneno hayo yote yanayozingumzia upole kama MEEK katika unyambulisho wake yanatupa picha pana sana kuwa mtu mwenye upole kwa vyovyote vile ni mtu mkamilivu na momavu na katika maswala ya kiroho ni mtu wa ngazi ya juu sana kwani ameweza kubeba matunda mengi ya rohoni ona maana hizo kwanza 

MILD – MTARATIBU, SUBMISSIVE – MTIIFU, MNYENYEKEVU, MODERATE – MTU WA WASTANI (KIASI), ULINGANIFU USAWA, QUITE MKAMILIFU, GENTLE – MUUNGWANA, LONG-SUFFERING – MVUMILIFU, ASIYEKASIRIKA KWA HARAKA, PATIENCE – ALIYE NA SUBIRA.

Unaona kwa hiyo tunaposoma katika kitabu cha Wagalatia 5:22-23 “Lakini tunda la Roho ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, upole, kiasi; juu ya mambo kama hayo hakuna sheria.

Aina hii ya upole Yakobo aliita Upole wa hekima Yakobo 3: 13 “N'nani aliye na hekima na ufahamu kwenu? Na aonyeshe kazi zake kwa mwenendo wake mzuri, katika upole wa hekima”.

Aidha neno hili katika Biblia ya kiyunani linatumika kama neno PRAUS au PRAEIS ambalo tafasiri yake ni MILD  ikimaanisha mtu mwenye uwezo wa kujishusha kwa Mungu na wanadamu, au mtu mwenye uwezo wa kutumia nguvu na mamlaka lakini akawa na subira kwa faida ya wengine, Kimsingi hii ilikuwa sifa kubwa sana ya viongozi wa kibiblia na hata mfalme Daudi alikuwa miongoni mwa watu wa namna  hata alipotafuta kuuawa na Sauli aliyekuwa anamchukia sana yeye hakufanya haraka kumdhuru waola kujitakia kisasi hata pale ambapo Mungu alimwambia kufanya hivyo yeye alisubiri wakati muafaka wa Mungu hii ona

Zaburi 37:10-13 “Maana bado kitambo kidogo asiye haki hatakuwapo, Utapaangalia mahali pake wala hatakuwapo. Bali wenye upole watairithi nchi, Watajifurahisha kwa wingi wa amani. Asiye haki hunuia mabaya juu ya mwenye haki, Na kumsagia meno yake. Bwana atamcheka, Maana ameona kwamba siku yake inakuja.”

Unaona kwa msingi huo ni vema ikaeleweka wazi kuwa Upole sio udhaifu bali Nguvu za Mtu mwenye uwezo  chini ya udhibiti wa Nguvu za Mungu, kwa hiyo mtu Mpole ni mtu anayeachia mambo chini ya udhibiti wa Mungu, ili Mungu mwenyewe achukue hatua za haki, ni mtu ambaye hajifikiri kuwa bora nje ya neema ya Mungu, upole ni hali ya kufikiri kuwa nguvu zetu na mamlaka yetu ina mipaka ya kufikiri katika Mungu kwa nia njema kuliko kuitikia haraka kwa hasira za kibinadamu Yakobo 1:20 “kwa maana hasira ya mwanadamu haiitendi haki ya Mungu.” Mtu mwenye upole hutembea katika neema ya Mungu na hanaga mpango wa kunia makuu kuliko impasavyo kunia.

Warumi 12:3 “Kwa maana kwa neema niliyopewa namwambia kila mtu aliyeko kwenu asinie makuu kupita ilivyompasa kunia; bali awe na nia ya kiasi, kama Mungu alivyomgawia kila mtu kiasi cha imani.”

Heri wenye upole!

Maana yake kuna amebarikiwa sana Mtu mwenye upole hii maana yake ni kuwa kuna faida kubwa sana za upole kama ifuata vyo:-

ü  Watu wenye upole ni watu waliobarikiwa kwa kiwango kikubwa Mathayo 5:5 “Heri wenye upole; Maana hao watairithi nchi.” Hii maana yake ni nini maana yake ni kuwa na uhusiano na Muumba wa mbingu na Nchi, urithi mtu huupata kutokwa kwa yule eliyemzaa au aliyekuandikisha uupate kwa sababu ya wema wake mtu akiwa mpole maana yake anafanana na Mungu ni mwana wa Mungu hivyo anastahili urithi, Ni Mungu ndiye aliyeumba mbingu nan chi na hivyo kuwa mwanae kwa sababu ya upole kwa msingi huo lazima tutarajie Baraka za Mungu hata pale atakapoiumba mbingu mpya nan chi mpya Mungu atawarithisha watoto wake

 

ü  Watu wenye upole hutetewa na Mungu Hesabu 12:1-9 “Kisha Miriamu na Haruni wakamnenea Musa kwa sababu ya mwanamke Mkushi aliyekuwa amemwoa; maana, alikuwa amemwoa mwanamke Mkushi. Wakasema, Je! Ni kweli Bwana amenena na Musa tu? Hakunena na sisi pia? Bwana akasikia maneno yao. Basi huyo mtu, huyo Musa, alikuwa mpole sana zaidi ya wanadamu wote waliokuwa juu ya uso wa nchi. Bwana akanena ghafula na Musa, na Haruni na Miriamu, na kuwaambia, Tokeni nje ninyi watatu, mwende hemani mwa kukutania. Basi hao watatu wakatoka nje. Bwana akashuka katika nguzo ya wingu akasimama pale mlangoni pa Hema, akawaita Haruni na Miriamu, nao wakatoka nje wote wawili. Kisha akawaambia, Sikizeni basi maneno yangu; Akiwapo nabii kati yenu, Mimi, Bwana, nitajifunua kwake katika maono, Nitasema naye katika ndoto. Sivyo ilivyo kwa mtumishi wangu, Musa; Yeye ni mwaminifu katika nyumba yangu yote; Kwake nitanena mdomo kwa mdomo, Maana, waziwazi wala si kwa mafumbo; Na umbo la Bwana yeye ataliona. Mbona basi ninyi hamkuogopa Kumnenea mtumishi wangu, huyo Musa? Hasira za Bwana zikawaka juu yao; naye akaenda zake.”

 

ü  Watu wenye upole hudumu muda mrefu katika nafasi zao na katika maisha Zaburi 37:10-13 “Maana bado kitambo kidogo asiye haki hatakuwapo, Utapaangalia mahali pake wala hatakuwapo. Bali wenye upole watairithi nchi, Watajifurahisha kwa wingi wa amani. Asiye haki hunuia mabaya juu ya mwenye haki, Na kumsagia meno yake. Bwana atamcheka, Maana ameona kwamba siku yake inakuja.” Unaona kama unataka kudumu Muda mrefu uwe mwenye haki, kama watu wapole kuna stori moja ya kuchekesha kuhusu Meno na Ulimi, siku moja ulimi ulimwambia Mungu kuwa tafadhali umeniweka mimi katika wito wangu pamoja na meno na meno ni mgumu kuliko mimi kwa hiyo mara kwa mara katika kutimiza wajibu wetu meno amekuwa akinumiza na kuniacha na majeraha nikipona tena baada ya Muda meno hufanya hivyo hivyo ndipo Mungu akamjibu meno kazi yenu ni ya muda tu lakini wewe ulimi ni wa muda mrefu zaidi kuliko meno hivyo ni lazima ujifunze kuvumilia, baada ya miaka 70 au 80 hivi ya maisha yenu uje unipe majibu, baada ya muda huo kupita kumbe meno mengi yalioza na kung’oka lakini ulimi ulibaki, ni wazi kabisa kama maandiko yasemavyo aggressive people shall not live longer but Mild people will live more than normal ,  watu wakali hawadumu lakini watu wapole hudumu, in the workplace the arrogant and powerful seems to win but in the end they  lose alisema mtu mmoja kazini watu jeusi na wanaojiinua huonekana kama washindi lakini mwishoni wanyenyekevu ndio wanaoshinda, Ni changamoto kubwa sana kuachia mamlaka zetu na nguvu zetu katika mikono ya Mungu na kujinyenyekesha, tunaweza kuona raja kwa kitambo kutumia mamlaka zetu, kufukuza watu, kumarisha watu lakini ni ukweli ulio wazi kuwa hatima yake ni huzuni, hawafanikiwi katika lolote watu jeuri hawana marafiki wala hata wakipata fedha hawatosheki, wanaweza kudhani kuwa wanaumiliki ulimwengu lakini ni ukweli kuwa ulimwengu unawamiliki, Mwanamke na mwanaume wanaojikweza na kutaka kuonyesha nguvu zao huishia katika aibu na upweke hakuna mtu anaweza kuwa na urafiki na mtu jeuri!, wanawake huvutiwa sana na mwanaume mpole. Mwaname mkali hawezi kufaidi lolote hata katika ndoa yake! Mithali 22:24-25 “Usifanye urafiki na mtu mwenye hasira nyingi; Wala usiende na mtu wa ghadhabu nyingi; Usije ukajifunza njia zake; Na kujipatia nafsi yako mtego.”

 

ü  Upole unakaribisha uwepo wa Mungu Isaya 66:1-2 “Bwana asema hivi, Mbingu ni kiti changu cha enzi, na dunia ni mahali pa kuweka miguu yangu; mtanijengea nyumba ya namna gani? Na mahali pangu pa kupumzikia ni mahali gani? Maana mkono wangu ndio uliofanya hivi vyote, vitu hivi vyote vikapata kutokea, asema Bwana; lakini mtu huyu ndiye nitakayemwangalia, mtu aliye mnyonge, mwenye roho iliyopondeka, atetemekaye asikiapo neno langu.” Uwepo wa Mungu unakaa na watu wanyenyekevu wanyonge na wapole bila upole nafsi ya mwanadamu inakuwa katika mgogoro wa ndani, inasababisha hasira, kuchanganyikiwa, uchungu, na kukosa utulivu,  Upole unaweka mambo sawa na kupunguza mawimbi, unaleta utaratibu wakati wa machafuko unaponya nafsi na kutiisha mawimbi, Lazima mwanadamu akumbuke kuwa yeye ni mavumbi, ukikumbuka kuwa wewe ni udongo itakusaidia, Upole unaleta furaha na amani ya kweli, kama Mungu akiwa na ghadhabu na hasira kama tulizonazo sisi kwa wengine tungekuwa wapi leo? Watu wengine hata wakisikia masengenyo tu  mahali wanakurupuka na kufanya maamuzi hata bila kufanya uchunguzi wa kina na wa kutosha  je Mungu anekuwa mwepesi wa hasira kama wewe na mimi ingekuwaje ?

 

ü  Upole ni alama ya ukomavu wa kiroho Wagalatia 5:22-23 “Lakini tunda la Roho ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, upole, kiasi; juu ya mambo kama hayo hakuna sheria.” Hakuna jambo linachosha duniani kama kuchunga wakristo wa Mwilini yaani wakristo ambao hawajakomaa kiroho au waliodumaa, Paulo mtume alisikitishwa sana na Kanisa lililodumaa na la wakristo wa mwilini kwani jamii hii ya wakristo wana taabu sana kuliko hata wapagani kutokana na kufarakana na kugombana na kufanya mambo ya ajabu yanayotukanisha ukristo 1Wakorintho 3:1-3 “Lakini, ndugu zangu, mimi sikuweza kusema nanyi kama na watu wenye tabia ya rohoni, bali kama na watu wenye tabia ya mwilini, kama na watoto wachanga katika Kristo. Naliwanywesha maziwa sikuwalisha chakula; kwa kuwa mlikuwa hamjakiweza. Naam, hata sasa hamkiwezi, kwa maana hata sasa ninyi ni watu wa tabia ya mwilini. Maana, ikiwa kwenu kuna husuda na fitina, je! Si watu wa tabia ya mwilini ninyi; tena mnaenenda kwa jinsi ya kibinadamu?  unaona watu waliokomaa kiroho hawana muda wa majungu, fitina na husuda na maswala mengine, UPOLE ni alama muhimu sana kwa mtu aliyekomaa kiroho, lakini mtu wa tabia ya mwilini asiyekomaa kiroho hawezi kuwa na utulivu, kwa sababu hana matunda ya rohoni!

 

Hitimisho:

Ni mmuhimu kuelewa kuwa tunaweza kumuomba Mungu atupe upole kama jinsi ambavyo tunaomba Mambo mengine Yakobo 1:5 “Lakini mtu wa kwenu akipungukiwa na hekima, na aombe dua kwa Mungu, awapaye wote, kwa ukarimu, wala hakemei; naye atapewa.” Ingawa Yakobo hapo  anaelezea swala la kuomba Hekima ni muhimu pia kujua kuwa Upole ni Hekima kwa hiyo tunapoomba Hekima tunaweza kupokea na upokle ndani yake hekima ya kiungu ikoje? Yakobo 3:17-18 “Lakini hekima itokayo juu, kwanza ni safi, tena ni ya amani, ya upole, tayari kusikiliza maneno ya watu, imejaa rehema na matunda mema, haina fitina, haina unafiki. Na tunda la haki hupandwa katika amani na wale wafanyao amani.” Kumbe tunaweza kuiomba Hekima hii iliyojaaa amani, rehema, matendo mema na iko tayari kusikiliza kwa hiyo ni lazima tumuombe Mungu atupe upole. Martin Luther King Alipingana na ubaguzi uliokuwepo Marekani, alitaka watu wote wahesabike kuwa sana alifanya maandamano ya amani hakuwahi kufanya vurugu wala kuruhusu wafuasi wake kufanya fujo akitumia falsafa ya Mahatma Ghandi ya non-violence resistance, kupinga maswala yasiyo haki bila kumwaga Damu, hii maana yake ni kuwa alikuwa Mpole Bwana na ampe neema kila mmoja wetu kuwa mpole katika jina la Yesu Kristo, kwa hiyo ieleweke wazi kuwa Upole sio udhaifu upole ni sifa kubwa na ya kipekee sana katika uhusiano wetu na Mungu, hivyo wale wanaonishutumu kuwa mimi ni Mpole sasa nimewaelewa vema asanteni!

 

Na Rev. Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima     

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni