Jumatatu, 7 Novemba 2022

Jina la Bwana ni Ngome imara !


Mithali 18:10-14 “Jina la Bwana ni ngome imara; Mwenye haki huikimbilia, akawa salama. Mali ya mtu tajiri ni mji wake wa nguvu; Ni kama ukuta mrefu katika mawazo yake. Kabla ya uharibifu moyo wa mwanadamu hujivuna; Na kabla ya heshima hutangulia unyenyekevu. Yeye ajibuye kabla hajasikia, Ni upumbavu na aibu kwake. Roho ya mtu itastahimili udhaifu wake; Bali roho iliyovunjika nani awezaye kuistahimili?


Utangulizi:

Kifungu cha mistari ya msingi kwa ujumla kinazungumzia ulinzi unaopatikana kwa Mungu jinsi ulivyo Muhimu kuliko ulinzi wa matajiri, au moyo  wa mwanadamu ulioharibika au wenye kiburi na majivuno,  Mwenye Hekima hapa anataka kufafanua jambo la muhimu na la msingi kwamba usalama na ulinzi unaopatikana kwa Mungu ni wa msingi sana kuliko ule tunaoufikiria kibinadamu na moyoni mwetu! Na kwa sababu hiyo kulitumainia Jina la Mungu ni kwa Muhimu zaidi ya marafiki, mioyo yetu na kiburi cha kibinadamu! Lakini hakuna mtu anayemtegemea Mungu au jina lake kisha Mungu akamuacha aaibike ona

Yeremia 17:5-9 “Bwana asema hivi, Amelaaniwa mtu yule amtegemeaye mwanadamu, Amfanyaye mwanadamu kuwa kinga yake Na moyoni mwake amemwacha Bwana. Maana atakuwa kama fukara nyikani, Hataona yatakapotokea mema; Bali atakaa jangwani palipo ukame, Katika nchi ya chumvi isiyokaliwa na watu. Amebarikiwa mtu yule anayemtegemea Bwana, Ambaye Bwana ni tumaini lake. Maana atakuwa kama mti uliopandwa kando ya maji, Uenezao mizizi yake karibu na mto; Hautaona hofu wakati wa hari ujapo, Bali jani lake litakuwa bichi; Wala hautahangaika mwaka wa uchache wa mvua, Wala hautaacha kuzaa matunda. Moyo huwa mdanganyifu kuliko vitu vyote, una ugonjwa wa kufisha; nani awezaye kuujua?

Kwa msingi huo ni wazi kuwa maandiko yanatuasa kuwa kumtumainia Mungu na jina lake ni jambo la msingi na la muhimu sana kuliko kuitegemea Hekima ya kibinadamu au kujivunia mitazamo ya kibinadamu na utajiri wa Dunia hii.

Maana ya Neno Ngome!

Nyakati za Biblia watu walipokuwa wanajenga miji, walihakikisha kuwa miji yao vilevile inazungukwa na kuta kubwa ngumu na imara kwa kusudi la kuhakikisha ulinzi na usalama wa watu wote pamoja na mfalme wa mji ule ili ustawi wa watu uweze kuendelea kuwepo, aidha juu ya kuta hizo askari walikuwa wakizunguka zunguka kufanya matembezi ya kiulinzi na pia kulikuwa na minara mirefu ambayo pia ilikuwa na walinzi waliokaa kwa zamu kwaajili ya kuangalia usalama wa mji na wakati mwingine kutoa taarifa kwa wananchi na serikali kuhusiana na usalama wao, kwa msingi huo uimara wa mji ulitegemea sana na Ngome za miji hiyo zikoje Miji mingi katika nchi ya Kanaani ilikuwa imejengwa kwa ngome imara zisizopenyeka kwa ulaini ambazo pia ziliitwa boma kwa jina lingine  ona

Yoshua 19:35-39 “Na miji yenye boma ilikuwa ni hii, Sidimu, na Seri, na Hamathi, na Rakathi, na Kinerethi; na Adama, na Rama, na Hazori; na Kedeshi, na Edrei, na Enhasori; na Ironi, na Migdal-eli, na Horemu, na Bethanathi, na Bethshemeshi; miji kumi na kenda, pamoja na vijiji vyake. Huu ndio urithi wa kabila ya wana wa Naftali kwa kuandama jamaa zao; miji hiyo pamoja na vijiji vyake.”

Ngome au boma katika miji ilikuwa ni alama kubwa sana ya kuonyesha ulinzi na nguvu kwaajili ya miili, akili, uwezo, utajiri, ushawishi, ulinzi, uadilifu, nguvu, uthabiti, afya, uwezo wa kutokuvamiwa na kuonewa, uhakika, uimara, na uwezo wa kutoa mahitaji ya watu, na usalama,  kwa hiyo kila kitu ambacho kilikuwa kinahifadhiwa na wenye miji yenye boma ndio katika Jina la Mungu navyo vinapatikana endapo kila mwanadamu atalitumainia na kulikimbilia. 

Jina la Bwana ni ngome Imara.

Mfalme Sulemani anaposema Jina la Bwana Ni ngome imara mwenye haki hukimbulia akawa salama ana maanisha nini?  Nyakati za Biblia jina lilikuwa lina maana pana sana kuliko tunavyoweza kufikiri katika siku za leo, jina lilikuwa linatambulisha uwezo na mamlaka ya kila kitu alichokuwa nacho Mtu, au mwenye jina, Jina la bwana ni Ngome imara neno Bwana hapo lilikuwa linasomeka kama YAHWEH na hii ilikuwa inafunua uhalisia na ukweli wote kuhusu sifa zake zote alizokuwa nazo Mungu, kwa hiyo jina lilifunua tabia na sifa alizokuwa nazo, kwa hiyo jila la Mtu lilikuwa linauwezo wa kukupa picha nzima ya anayetajwa katika jina hilo, kwa mfano Mungu alipojifunua kwa Musa kuhusu jina lake alikuwa anamaanisha maswala kadhaa yafuatayo:-

Kutoka 34:5-7 “BWANA akashuka ndani ya lile wingu, akasimama pamoja naye huko, akalitangaza jina la BWANA. BWANA akapita mbele yake, akatangaza, BWANA, BWANA, Mungu mwingi wa huruma, mwenye fadhili, si mwepesi wa hasira, mwingi wa rehema na kweli; mwenye kuwaonea huruma watu elfu elfu, mwenye kusamehe uovu na makosa na dhambi; wala si mwenye kumhesabia mtu mwovu kuwa hana hatia kamwe; mwenye kuwapatiliza watoto uovu wa baba zao, na wana wa wana wao pia, hata kizazi cha tatu na cha nne.”

Jina la Mungu wetu linafunua uwezo wake na mamlaka yake na yale yote ambayo Mungu wetu anaweza kutufadhili kwayo, kwa msingi huo kama Mungu ana uwezo wote ni wazi kuwa jina lake linapita vyote ni jina ambalo liko juu mno kwa uweza na mamlaka na kwa msaada wowote ule

1.       Jina hili lilo juu mno Zaburi 148:11-13 “Wafalme wa dunia, na watu wote, Wakuu, na makadhi wote wa dunia. Vijana waume, na wanawali, Wazee, na watoto; Na walisifu jina la Bwana, Maana jina lake peke yake limetukuka; Adhama yake i juu ya nchi na mbingu.”

 

2.       Jina hili linafunua ya kuwa yeye anamiliki na kuwa hakuna mfalme wala taifa linaloweza kusimama mbele yake kila anayesikia matendo yake anatetetmeka Yoshua 2:9-11 “akawaambia wale wanaume, Mimi najua ya kuwa Bwana amewapa ninyi nchi hii, na ya kuwa hofu imetuangukia mbele yenu, na ya kuwa wenyeji wote wa nchi wanayeyuka mbele yenu. Maana tumesikia jinsi Bwana alivyoyakausha maji ya bahari ya Shamu mbele yenu, hapo mlipotoka Misri, tena mambo hayo mliyowatendea wafalme wawili wa Waamori waliokuwa huko ng'ambo ya Yordani, yaani, Sihoni na Ogu, mliowaangamiza kabisa. Na mara tuliposikia hayo mioyo yetu iliyeyuka, wala haukusalia ujasiri wo wote katika mtu awaye yote, kwa sababu yenu; kwa kuwa Bwana, Mungu wenu, yeye ndiye Mungu, katika mbingu juu na katika nchi chini.”

 

3.       Ni jina ambalo kwalo linaokoa Yoeli 2:32Na itakuwa ya kwamba mtu awaye yote atakayeliita jina la Bwana ataponywa; kwa kuwa katika mlima Sayuni na katika Yerusalemu watakuwako watu watakaookoka, kama Bwana alivyosema; na katika mabaki, hao awaitao Bwana.”       Warumi 10:13 “kwa kuwa, Kila atakayeliitia Jina la Bwana ataokoka.” Matendo 2:21 “Na itakuwa kila atakayeliitia jina la Bwana ataokolewa.”

 

4.       Ni jina ambalo ukilitumia kwenye maombi kuomba lolote utajibiwa ona Yohana 14:12-14 “Amin, amin, nawaambieni, Yeye aniaminiye mimi, kazi nizifanyazo mimi, yeye naye atazifanya; naam, na kubwa kuliko hizo atafanya, kwa kuwa mimi naenda kwa Baba. Nanyi mkiomba lo lote kwa jina langu, hilo nitalifanya, ili Baba atukuzwe ndani ya Mwana. Mkiniomba neno lo lote kwa jina langu, nitalifanya.

                 

5.       Ni jina lenye uwezo wa kutiisha kila kitu chini yake Wafilipi 2:9-11 “Kwa hiyo tena Mungu alimwadhimisha mno, akamkirimia Jina lile lipitalo kila jina; ili kwa jina la Yesu kila goti lipigwe, la vitu vya mbinguni, na vya duniani, na vya chini ya nchi; na kila ulimi ukiri ya kuwa YESU KRISTO NI BWANA, kwa utukufu wa Mungu Baba.” 

 

6.       Jina hili ni ngome ya kumfanya adui asikupate Zaburi 61:2-3 “Ee Mungu, ukisikie kilio changu, Uyasikilize maombi yangu. Toka mwisho wa nchi nitakulilia nikizimia moyo, Uniongoze juu ya mwamba nisioweza kuupanda. Kwa maana ulikuwa kimbilio langu, Ngome yenye nguvu adui asinipate.”

 

Hitimisho

Kwa msingi huo sasa iwapo unakabiliwa na hali yoyote ya hatari, iwe ya kimwili au kiroho, kiakili au kisaikolojia  na hatari nyingine za aina yoyote maandiko yanatushauri kuwa ni hekima kulikimbilia jina la Bwana kwani jina hilo linatoa usalama, usalama maana yake ni kuwa katika ulinzi, kulindwa na madhara, au kuawa, au kujeruhiwa, au kupotea, na nhatari nyingine yoyote, Jina  la Mungu wetu liko juu ya kila jina maana yake liko juu ya mamlaka zote, ni salama kwa ulinzi, ni salama kwa kulikimbilia ni salama kwa kulitegemea, ni nguvu yetu, ni katika jina hili ndiko kuliko na usalama wa kweli na ulinzi wa uhakika, jina la Bwana ni ngome imara maana yake hatupaswi kuogopa kama tunaumwa, hatupaswi kuchanganyikiwa kama tuna huzuni, hatupaswi kuogopa wakitutisha, hatupaswi kuhofia tuwapo, dhaifu, tunapolemewa na au tunapokuwa na uchumi dhaifu, tunapopatwa na matisho ya aina yoyote ukweli ni kwamba wakati wowote hatuna budi kukumbuka ya kuwa ni jina la Yesu ndilo ngome imara hapo ndipo tunapoweza kukimbilia na kuliitia jina lake kwa msaada tunaouhitaji, Jina lake linawakilisha kila tunachokihitaji, iwe, Upendo, Rehema, Neema, Nguvu, Haki, na zaidi, Watakatifu waliotutangulia walilitegemea na kuliitia wakati wote na Mungu akawasaidia ni hekima kubwa kumkimbilia Mungu, ni ujinga kutegemea wanadamu, na tujiachie katika mikono yake ili tuwe salama kwani hakuna sababu ya kuogopa

Mithali 29:25 “Kuwaogopa wanadamu huleta mtego; Bali amtumainiye Bwana atakuwa salama.”

Na Rev. Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima !



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni