Mathayo 2:12-16 “Nao wakiisha kuonywa na
Mungu katika ndoto wasimrudie Herode, wakaenda zao kwao kwa njia nyingine. Na
hao walipokwisha kwenda zao, tazama, malaika wa Bwana alimtokea Yusufu katika
ndoto, akasema, Ondoka, umchukue mtoto na mama yake, ukimbilie Misri, ukae huko
hata nikuambie; kwa maana Herode anataka kumtafuta mtoto amwangamize. Akaondoka akamchukua mtoto na mama yake
usiku, akaenda zake Misri; akakaa huko hata alipokufa Herode; ili litimie neno
lililonenwa na Bwana kwa ujumbe wa nabii, akisema, Kutoka Misri nalimwita
mwanangu. Ndipo Herode, alipoona ya kuwa amedhihakiwa na wale mamajusi,
alighadhabika sana, akatuma watu akawaua watoto wote wanaume waliokuwako huko
Bethlehemu na viungani mwake mwote, tangu wenye miaka miwili na waliopungua,
kwa muda ule aliouhakikisha kwa wale mamajusi.”
Utangulizi.
Moja ya wafalme aliyekuwa katili sana na mroho,
mwenye tamaa na mbinafsi na muongo alikuwa ni mfalme Herode mkuu, kwa ujumla
alikuwa ni mfalme mwenye kutisha sana, ni katili na muuaji aidha ni mwenye
dhuluma, Huyu alikuwa tofauti sana na mfalme wetu Yesu Kristo, ambaye alikuja
kwaajili ya ukombozi wa wanadamu, wakati Herode alikuwa na mpango wa kuangamiza
na kuua, Mfalme Yesu alikuja na mpango wa wokovu, Herode alikuwa na mpango wa
mateso, Yesu alikuja akileta matumaini na upendo, Herode alikuwa ni mkatili
mwenye chuki na mwenye mpango wa kuangamiza, Kristo alikuja kutafuta na kuokoa kile
kilichopotea tena alikuja ili watu wawe na uzima tena wawe nao tele, Katika
wakati huu wa kuadhimisha kuzaliwa kwa Yesu Kristo hatuna budi vilevile katika
wakati huu kujikumbusha Mambo ya msingi na ya muhimu yanayoyakabili maisha yetu
na kisha kupata hekima ya kiungu namna ya kuokolewa katika mikon ya adui zetu.
Yesu alizaliwa wakati ambapo
mfalme muovu na adui wa maisha yake alikuwa anatawala na mfalme huyu aliposikia
habari kuwa Yesu Kristo amezaliwa ni ukweli ulio wazi kuwa badala ya kufurahi
alifadhaika sana ona
Mathayo 2:1-3 “Yesu alipozaliwa katika
Bethlehemu ya Uyahudi zamani za mfalme Herode, tazama, mamajusi wa mashariki walifika
Yerusalemu, wakisema, Yuko wapi yeye aliyezaliwa mfalme wa Wayahudi? Kwa maana
tuliiona nyota yake mashariki, nasi tumekuja kumsujudia. Basi mfalme Herode
aliposikia hayo, alifadhaika, na Yerusalemu pia pamoja naye.”
Mfalme Herode aliita baraza la
wazee wa kiyahudi na wakuu wa makuhani na kufanya uchunguzi wa kina, na sio
hivyo tu aliwahoji mamajusi na kutaka kujua kuwa ni kwa muda gani na wakati
gani sahihi mtoto huyo atakuwa amezaliwa kufuatia mwenendo ya nyota waliyoiona nani
wapi, na zaidi ya yote alitaka aletewe habari kamili kuhusu huyo mtoto kwa
kusudi la kutaka kumuangamiza ona
Mathayo 2:4-8 “Akakusanya wakuu wa makuhani
wote na waandishi wa watu, akatafuta habari kwao, Kristo azaliwa wapi? Nao
wakamwambia, Katika Bethlehemu ya Uyahudi; kwa maana ndivyo ilivyoandikwa na
nabii, Nawe Bethlehemu, katika nchi ya Yuda, Hu mdogo kamwe katika majumbe wa
Yuda; Kwa kuwa kwako atatoka mtawala Atakayewachunga watu wangu Israeli. Kisha
Herode akawaita wale mamajusi faraghani, akapata kwao hakika ya muda tangu
ilipoonekana ile nyota. Akawapeleka Bethlehemu, akasema, Shikeni njia, mkaulize
sana mambo ya mtoto; na mkiisha kumwona, nileteeni habari, ili mimi nami niende
nimsujudie.”
Ni muhimu kufahamu kuwa roho ya
Herode inatenda kazi hata leo, katika ulimwengu wa kisiasa, makazini, duniani
na hata makanisani, katika nyakati hizi za mwisho hatuna budi kuhakikisha kuwa
wakati wote tunaendenda kwa hekima sana kwani hali halisi ya kiroho ya watu
wengi imebadilika sana, wauaji wakubwa kabisa, wenye chuki, waharibifu,
wabambikiaji, wasingiziaji, wenye siasa chafu, wachawi na watu wenye wivu wenye
uchungu nyakati za leo hawako nje ya kanisa bali sasa wako ndani ya kanisa na
hata madhabahuni, tunazungukwa na mbwa mwitu wakali huku wewe na mimi tukiwa
kama kondoo tu, Bila kuweka tumaini letu kwa Mungu ni rahisi sana kujeruhiwa,
kuumizwa na kutendewa kila aina ya ubaya na hata kuuawa kwa njia za ajabu au
kuwekewa sumu, na watu ambao wala hatukuwahi kudhani kuwa wanaweza kuwa wasaliti
na wenye kupingana na mpango wa Mungu katika maisha yetu, hali inatisha sana
kwa sasa, watu wanatuma mpaka watu watushambulie, wako watumishi wa Mungu ambao
sasa wamekuwa wachawi hata wokovu sijui waliuacha lini, wako washirikina pia
hali inatisha hata hivyo Mungu aliye hai yuko macho na bila shaka atakuokoa na
kila mpango mbaya wa ibilisi na maajenti wake katika maisha yako na yangu!
Herode alikuwa ni mtu wa namna gani?
Herode ambaye pia alijulikana
kama Herode mkuu alikuwa ni mtawala wa Israel iliyokuwa chini ya utawala wa
Warumi, Kimsingi yeye alizaliwa mwaka wa 72 kabla ya Kristo na kwa asili
alitokea maeneo ya Idumeya yaani Eneo la Edomu wana wa Esau, Yeye na ukoo wake
waliwekwa kuwa watawala vibaraka kwa niaba ya utawala wa warumi, Mwanzoni yeye
alitawala Galilaya na uyahudi kabla ya utawala wa watoto wake watatu ambao
waligawana majimbo baada ya kifo chake na Herode Akleo akatawala Idumeya, Uyahudi
na Samaria na Herode Antipas alitawala Galilaya na Philip alitawaka huko Jordan,
Kwa mujibu wa mwanahistoria maarufu wa kiyahudi wa karne ya Kwanza Josephus, Herode mkuu alikuwa
ni mwanasiasa mwenye ushawishi mkubwa sana ambaye ili kuongeza ushawishi wake
alimuoa binti wa kuhani mkuu wa kiyahudi Kayafa na pia wakati wa utawala wake alilikarabati
Hekalu la pili la Yerusalem na kuliongezea eneo mlima wa Hekalu kwa upande wa
kaskazini, Jambo lililopelekea yeye kukubalika na Wayahudi wengi. Hata hivyo pamoja na umaarufu wake mkubwa
hivyo ni jambo la kushangaza ya kuwa alipozaliwa Yesu Kristo Mfalme huyu
alifadhaika na kugadhibika na ili aweze kujihakikishia usalama wake
alihakikisha kuwa anawaua watoto wote wapatao miaka miwili kule Bethelehemu ili
yamkini aweze kumuua Yesu Kristo ona
Mathayo 2:16 “Ndipo Herode, alipoona ya
kuwa amedhihakiwa na wale mamajusi, alighadhabika sana, akatuma watu akawaua
watoto wote wanaume waliokuwako huko Bethlehemu na viungani mwake mwote, tangu
wenye miaka miwili na waliopungua, kwa muda ule aliouhakikisha kwa wale mamajusi.”
Unaweza kuona Herode alikuwa ni
mtu mwenye ghadhabu, mbinafsi na aliyekuwa hataki upinzani, alitamani kuwa yeye
katika madaraka wakati wote, alitamani kuwa yeye abaki kuwa maarufu wakati
wote, alikuwa mtu katili aliweza kuua watoto wote ili kujihakikishia usalama
wake ni jambo la kusikitisha kuwa hii roho ya Herode ni roho inayotenda kazi
katika nyakati zetu na katika kanisa la leo, Mara ngapi tumesikia viongozi
wakubwa na maarufu wakiwaua wengine kisiasa na kuwachafua wengine kwa skendo za
kutengeneza ili yamkini waweze kubakia wao tu madarakani, au wao tu waonekane
kuwa ni safi na wenguine waonekane kuwa hawafai, au kuharibu umaarufu wa
wengine na wao tu waweze kuwa maarufu,
hujawaona watu wenye kila kitu na wenye nguvu zote lakini wakifukuzana na watu
masikini wasio na kitu wala nguvu yoyote wakitaka kuwazima ili yamkini wabakie
wao tu hii ni roho chafu na mikono mibaya ya Herode, roho ya Herode ni roho ya
watu wenye uchungu, hasira na tama mbaya wakiwa wamejawa na ubinafsi wa kila
aina ni roho ya watu ambao hawawezi kufurahi nyota za wengine kung’aa lakini
pamoja na hayo Bwana ana ujumbe muhimu leo Usiogope Bwana amenituma nikupe
ujumbe huu kama nabii wake na kama malaika wake leo nakuletea habari njema ya
kuwa wakati Herode anataka kusababisha misiba katika jamii, Mungu atakunusuru
wewe na atakulinda na kukupa mlango wa kutokea mpaka atakapokufa Herode, Bwana
atakuficha katika mikono yake nawe utakuwa salama hutaogopa madamu Mungu
anakukubali, leo ziko habari njema kwaajili yako ona Yesu amezaliwa kwaajili
yako na yeye ni mwokozi sio wa mtu mmoja tu wa ulimwengu mzima na hivyo amani
inapaswa kutawala duniani kwa kila mtu ambaye Bwana ana mridhia najua wewe na
mimi Bwana anaturidhia
Luka 2:8-17 “Na katika nchi ile ile
walikuwako wachungaji wakikaa makondeni na kulinda kundi lao kwa zamu usiku. Malaika
wa Bwana akawatokea ghafula, utukufu wa Bwana ukawang'aria pande zote,
wakaingiwa na hofu kuu. Malaika akawaambia, Msiogope; kwa kuwa mimi ninawaletea
habari njema ya furaha kuu itakayokuwa kwa watu wote; maana leo katika mji wa
Daudi amezaliwa, kwa ajili yenu, Mwokozi, ndiye Kristo Bwana. Na hii ndiyo
ishara kwenu; mtamkuta mtoto mchanga amevikwa nguo za kitoto, amelala katika
hori ya kulia ng'ombe. Mara walikuwapo pamoja na huyo malaika, wingi wa jeshi
la mbinguni, wakimsifu Mungu, na kusema, Atukuzwe Mungu juu mbinguni, Na
duniani iwe amani kwa watu aliowaridhia. Ikawa, malaika hao walipoondoka kwenda
zao mbinguni, wale wachungaji waliambiana, Haya, na twendeni mpaka Bethlehemu,
tukalione hilo lililofanyika, alilotujulisha Bwana. Wakaenda kwa haraka
wakamkuta Mariamu na Yusufu, na yule mtoto mchanga amelala horini. Walipomwona
wakatoa habari waliyoambiwa juu ya huyo mtoto.”
Kwaajili ya hayo ni imani yangu nani
mpango wa Mungu ya kuwa pamoja na changamoto unazozipitia katika huduma, kazini
ndoa na maeneo mengine Mungu hatimaye atatuokoa na mipango mikakakati ya
heriode katika maisha yetu
Kuokolewa katika mikono ya Herode !
Mathayo 2:12-15 “Nao wakiisha kuonywa na
Mungu katika ndoto wasimrudie Herode, wakaenda zao kwao kwa njia nyingine. Na
hao walipokwisha kwenda zao, tazama, malaika wa Bwana alimtokea Yusufu katika
ndoto, akasema, Ondoka, umchukue mtoto na mama yake, ukimbilie Misri, ukae huko
hata nikuambie; kwa maana Herode anataka kumtafuta mtoto amwangamize. Akaondoka akamchukua mtoto na mama yake usiku,
akaenda zake Misri; akakaa huko hata alipokufa Herode; ili litimie neno
lililonenwa na Bwana kwa ujumbe wa nabii, akisema, Kutoka Misri nalimwita
mwanangu.”
Kila mtu mwenye mapenzi mema
Mungu ana mpango mkakati ulio mwema na maisha yako na kwa jinsi Mungu
alivyomwema anatuwazima mem, Mungu hana mpango wa kusababisha maombolezo katika
maisha yetu wala hana malipizi anayotulipiza kwaajili ya maovu yetu, Mungu ni
mwema mno yeye anatuwazia mema hana kisasi juu yetu yeye sio mwanadamu ana mpango
mwema na mahususi kuliko mpango alionao Herode wako na wangu ona ;-
Yeremia 29:11-13 “Maana nayajua mawazo
ninayowawazia ninyi, asema Bwana, ni mawazo ya amani wala si ya mabaya, kuwapa
ninyi tumaini siku zenu za mwisho. Nanyi mtaniita, mtakwenda na kuniomba, nami
nitawasikiliza. Nanyi mtanitafuta na kuniona, mtakaponitafuta kwa moyo wenu
wote..”
Vile adui zako na zangu
wanavyotuwazia sivyo Mungu anavyotuwazia nataka kuanzia Christmas hii uweze
kuelewa kuwa hakuna adui anayeweza kusimama mbele yako na kupingana au kushindana na mapenzi ya Mungu
yaliyowekwa ndani yako, kila baya linalokusudiwa na adui dhidi yako Mungu
ataligeuza kuwa Baraka, kila adui anayekutafuta akuangamize ataangamiza wengine
na wewe utajikuta umefichwa; msomaji wangu nataka nikuhakikishie yakuwa ujumbe
huu ni halisi katika maisha yako hakuna wa kukupata, hakuna atakayeweza
kusimama mbele yako siku zote za maisha yako sio kwa Herode huyu tu lakini kwa
kila mkono wa Herode yeyote atakayeinuka juu yako Mungu atakuokoa na mikono yake,
wakati wa Petro alikuweko herode mwingine aliyaangamiza maisha ya Yakobo mtume
na akataka kumuangamiza na Petro, lakini Mungu akawa mwaminifu akamfungua Petro
kutoka katika mikono ya Herode Mungu huyu huyu atakufungua na wewe atakuweka huru na Herode wako atatokwa na roho
Hakuna herode aliyewafuatilia watu wa Mungu na kuwatesa na kuwaua ambaye alibaki salama, Herode aliyetaka kumuua Yesu
alikufa Yesu akiwa amefichwa Misri na herode aliyemuua Yakobo alipotaka kumuua
Petro Mungu aklituma malaika wake ona
Matendo 12:1-23 “Panapo majira yale yale
Herode mfalme akanyosha mikono yake kuwatenda mabaya baadhi ya watu wa kanisa. Akamwua
Yakobo, ndugu yake Yohana, kwa upanga. Na akiona ya kuwa imewapendeza Wayahudi
akaendelea akamshika na Petro. Siku hizo zilikuwa siku za mikate isiyochachwa. Alipokwisha
kumkamata, akamweka gerezani akamtia mikononi mwa vikosi vinne vya askari wanne
wanne, wamlinde, akitaka baada ya Pasaka kumtoa na kumweka mbele ya watu. Basi
Petro akalindwa gerezani, nalo kanisa likamwomba Mungu kwa juhudi kwa ajili
yake. Hata wakati Herode alipotaka kumtoa, usiku ule ule Petro alikuwa analala
katikati ya askari wawili, amefungwa minyororo miwili; walinzi mbele ya mlango
wakailinda gereza. Mara malaika wa Bwana akasimama karibu naye, nuru ikamulika
mle chumbani, akampiga Petro ubavuni, akamwamsha, akisema, Ondoka upesi.
Minyororo yake ikamwanguka mikononi. Malaika akamwambia, Jifunge, kavae viatu
vyako. Akafanya hivyo. Kisha akamwambia, Jivike nguo yako, ukanifuate. Akatoka
nje, akamfuata; wala hakujua ya kuwa ni kweli yaliyofanywa na malaika; bali alidhani
kwamba anaona maono. Na walipopita lindo la kwanza na la pili, wakaja hata
mlango wa chuma wa kuingilia mjini, ukawafungukia wenyewe. Wakatoka nje,
wakapita katika njia moja; mara malaika akamwacha. Hata Petro alipopata fahamu
akasema, Sasa nimejua yakini ya kuwa Bwana amempeleka malaika wake na kunitoa
katika mkono wa Herode na katika kutazamia kote kwa taifa la Wayahudi. Na
alipokuwa akifikiri haya akafika nyumbani kwa Mariamu, mamaye Yohana, ambaye
jina lake la pili ni Marko; na watu wengi walikuwa wamekutana humo wakiomba. Naye
alipobisha kilango cha lango, kijakazi, jina lake Roda, akaja kusikiliza. Alipoitambua sauti ya Petro, hakukifungua
lango, kwa ajili ya furaha, bali alipiga mbio, akaingia ndani akawaambia kwamba
Petro anasimama mbele ya lango. Wakamwambia, Una wazimu. Lakini yeye akakaza
sana, akasema ya kwamba ndivyo hivyo. Wakanena, Ni malaika wake. Petro
akafuliza kugonga, hata walipokwisha kumfungulia wakamwona, wakastaajabu. Naye
akawapungia mkono wanyamaze, akawaeleza jinsi Bwana alivyomtoa katika gereza.
Akasema, Kampasheni Yakobo na wale ndugu habari hizi. Akaondoka, akaenda mahali
pengine. Hata kulipopambauka askari wakaingiwa na fadhaa nyingi, amekuwaje
Petro. Na Herode alipomtafuta, asimwone, aliwauliza-uliza wale walinzi,
akaamuru wauawe. Kisha akatelemkia kutoka Uyahudi kwenda Kaisaria, akakaa huko.
Naye Herode alikuwa amewakasirikia sana watu wa Tiro na Sidoni; wakamwendea kwa
nia moja, na wakiisha kufanya urafiki na Blasto, mwenye kukitunza chumba cha
mfalme cha kulalia, wakataka amani; kwa maana nchi yao ilipata riziki kwa nchi
ya mfalme. Basi siku moja iliyoazimiwa, Herode akajivika mavazi ya kifalme, akaketi
katika kiti cha enzi, akatoa hotuba mbele yao. Watu wakapiga kelele, wakisema,
Ni sauti ya Mungu, si sauti ya mwanadamu. Mara malaika wa Bwana akampiga, kwa
sababu hakumpa Mungu utukufu; akaliwa na chango, akatokwa na roho.”
Hitimisho.
Ujumbe wangu wa Chrismas hii ni
unabii, ni ujumbe ambao sio tu wa sikukuu hii lakini ni ujumbe wa maisha ya
siku zote wote wanaoonewa na watu wenye nyadhifa zilizokubwa kupita wao
wasiogope ni ujumbe wa matumaini na kukutia moyo ya kuwa Mungu yuko na
anaifuatilia mipango ya Herode na ata shughulika naye ni ujumbe wa maonyo pia
kama una roho ye herode lazima utubu na kubadilika Mungu hawezi kufurahia
udhalimu, kusudi lake ni pana mno na yuko tayari kulilinda kusudi lake kwa
gharama yeyote wewe sio wa Muhimu kuliko wanaochipukia uwe na roho ya malezi
walee wengine na kuwainua na kuwaunga mkono usijidhanie ya kuwa uko mwenyewe au
kuwa wewe ndiwe maalumu sana kwa Mungu, kujenga hekalu hakutakusaidia, kuoa
mtoto wa kuhani mkuu hakutakusaidia, kuwa na wapelelezi hakutakusaidia, kuwa na
jeshi hakukusaidiaa kitu Mungu wetu ni mwenye Nguvu na hekima yake ni kubwa
kuliko hekima ya kibinadamu, hii ni Chrismas ya wokovu nani ya habari njema kwa
wote wanaoonewa na maonyo makali kwa
waonevu! Kamwe asitokee mtu akashindana na kusudi la Mungu lililoko ndani yako
kwani atapotea kama walivyopotea wakina herode na kusudi la Mungu ndilo
litakalosimama.
Na Rev. Innocent Samuel Kamote
Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!
Ukurasa huu umewekwa wakfu kwaajili ya Kuwaelekeza watu kwa Mungu ambaye ndiye msaada wetu mkuu, Maandiko yanasema Mungu kwetu sisi Ni kimbilio na Ngu vu msaada uonekanao tele wakati wa Mateso, hivyo kama yuko mwanadamu anatumia ukurasa huu, kujitangaza kuwa anaweza kuwasaidia wanadamu basi Mwanadamu huyo anamkufuru Mungu na ukurasa huu hautawajibika kwa mtu anayetegemea ushirikina badala ya kumtegemea Mungu, Maandiko yanasema amelaaniwa Mtu yule amtegemeaye mwanadamu na kumfanya kuwa kinga yake
JibuFuta