Jumatatu, 20 Februari 2023

Ikawa Mwanzo wa Mwaka Mpya!


2Samuel 11:1-4 “Hata ikawa, mwanzo wa mwaka mpya, wakati watokapo wafalme kwenda vitani, Daudi akampeleka Yoabu, na watumishi wake pamoja naye, na Israeli wote; wakawaangamiza wana wa Amoni, wakauhusuru Raba. Lakini Daudi mwenyewe akakaa Yerusalemu. Ikawa wakati wa jioni, Daudi akaondoka kitandani, akatembea juu ya dari ya jumba la mfalme; na alipokuwa juu ya dari aliona mwanamke anaoga; naye huyo mwanamke alikuwa mzuri sana, wa kupendeza macho. Naye Daudi akapeleka, akauliza habari za yule mwanamke. Mtu mmoja akasema, Je! Huyu siye Bath-sheba, binti Eliamu, mkewe Uria, Mhiti? Basi Daudi akapeleka wajumbe, akamtwaa; naye akaingia kwake; naye akalala naye; (maana yule mwanamke amekwisha kutakasika unajisi wake); kisha akarudi nyumbani kwake.



Utangulizi:

Ni muhimu kufahamu kuwa kifungu hiki cha maandiko kina jambo kubwa la msingi la kutufundisha ambalo mwandishi wa kifungu hiki alikuwa anakusudia kukileta kwetu! Wengi wetu tunafahamu sana habari ya anguko la Daudi katika zinaa, na tunafahamu madhara makubwa yaliyompata kutokana na dhambi hii, lakini vilevile tunaweza kukubaliana wazi kuwa Daudi alikuwa na udhaifu sawa na ule walionao wanaume wengine, kwamba aliona mwanamke mzuri anaoga akamtamani, na kuzini naye na wengi wameweza kumalumu Daudi kwa sababu mbalimbali hata ikiwa ni pamoja na kujenga Ghorofa lenye dari ya kutembelea na kusababisha kuona mke wa jirani yake ambaye alikuwa anaoga, tunaweza kuwa na sababu lukuki kuhusu anguko la Mfalme Daudi na sababu hizo zikawa na mashiko kadhaa, Lakini mwandishi wa kifungu hiki ana sababu mojawapo ya muhimu zaidi ambayo kimsingi ndio nataka tuiangalie kwa kina katika siku kama hii ya leo!

Ikawa Mwanzo wa Mwaka mpya!

Mwandishi anaanza kwa kueleza Habari ya anguko la Daudi akiwa na sababu nyingine tofauti mno Ikawa Mwanzo wa Mwaka Mpya! Wakati watokapo wafalme kwenda vitani!  Majira ya nchi katika mashariki ya kati yanafanana sana kwa kiwango kikubwa na majira ya Afrika ya mashariki, Mwezi wa Januari na February Mpaka March ndio miezi ambayo tunaweza kuyaita majira ya Mwanzo wa mwaka kunakuwa na Joto kali na ukavu wa aina Fulani, katika majira haya kwa wana wa Israel huangukia kati ya mwezi wa Abibu au mwezi (Nisani) katika majira haya ardhi huwa kame na kavu, na hivyo ndio majira ambayo wafalme wengi waliyatumia kuingia vitani kwa kusudi la kupanua mipaka ya mataifa yao, kuteka nyara, kulipisha kodi wale utakaowashinda au kulinda mipaka yako, wakati huu ulikuwa ni wakati muafaka kwa vita kwa sababu ardhi ilikuwa kavu, na hivyo iliweza kurahisisha vita vya miguu, magari ya kukokotwa na farasi lakini pia kusafirisha silaha na wanajeshi kwa urahisi zaidi kuliko wakati wa baridi na wakati wa mvua ambapo ardhi huwa na matope na vita vinakuwa ni ngumu,  wakati huu pia ilikuwa ni rahisi kuteka nyara vitu na kuvibeba kwa hiyo ilikuwa ni desturi ya Wafalme kutoka kwenda kupigana vita mwanzoni mwa mwaka mpya, Hata Mungu aliwaokoa wana wa Israel kutoka Misri katika majira kama haya.

Kutoka 12;1-2”BWANA akanena na Musa na Haruni katika nchi ya Misri, akawaambia, Mwezi huu utakuwa mwanzo wa miezi kwenu; utakuwa ni mwezi wa kwanza wa mwaka kwenu”.

Kwa hiyo wataalamu wa nyakati waliweza kuuelewa vema kuwa ulikuwa ni wakati gani na wanapaswa kufanya nini, Mwandishi anataka kutuonyesha kuwa Sababu zilizopelekea Daudi kufanya dhambi au kuanguka dhambini ilikuwa ni  pamoja na:-

1.       Aliudharau wakati – kumbe ilikuwa wazi kabisa na ilikuwa inajulikana kabisa kwamba Mwanzo wa mwaka mpya ni lazima wafalme watoke kwenda kupigana vita, Lakini yeye aliupuuzia wakati  Moja ya tatizo kubwa linaloweza kumleta mwanadamu katika anguko la maisha yake ni kutokujua kuutumia wakati, kuna madhara mengi na majuti makubwa sana kwa kila mwanadamu ambaye hakujua kuutumia wakati, wakati tuliopewa duniani ni mfupi sana na unaenda haraka mno, wastaafu wengi wanajua leo kwa sababu hawakujua kuutumia wakati, vijana wengi wanafikiri wataendelea kuwa vijana tu, wasichana wengi wanadhani wataendelea kuwa wasichana tu, wanafunzi wengi sana wanadhani iko siku watakaa ajipange na kusoma kwa bidii na sasa wengi wanalala na kupoteza muda wakifikiri uko wakati, Hakuna jambo linaumiza sana kama kuja kugundua baadaye kuwa sikuutumia wakati, nilikuwa wapi mimi? Hakuna jambo linaumiza kama kupotezewa wakati!  Kila mmoja wetu anapaswa kufahamu kuwa wakati usipoutumia vema anguko lake ni kubwa  na lenye kuleta madhara makubwa sana duniani, kwa hiyo ni vema kuutumia wakati na kutokuupuuza Yesu alilalamika kwa njia ya kinabii kwa mji wa Yerusalem kwamba utabomolewa na kuharibiwa vibaya sana na Majeshi ya warumi tukio ambalo lilitimizwa mwaka wa 70 baada ya Kristo lakini malalamiko ya Yesu kwa Yerusalem ni kwa sababu tu ya kutokuujua majira na wakati hususani Mwokozi wa ulimwengu alipowatembelea.

 

Luka 19:41-44 “Alipofika karibu aliuona mji, akaulilia, akisema, Laiti ungalijua, hata wewe katika siku hii, yapasayo amani! Lakini sasa yamefichwa machoni pako. Kwa kuwa siku zitakuja, adui zako watakapokujengea boma, likuzunguke; watakuzingira na kukuhusuru pande zote; watakuangusha chini wewe na watoto wako ndani yako, wasikuachie jiwe juu ya jiwe, kwa sababu hukutambua majira ya kujiliwa kwako.”

 

Daudi alifahamu wazi kuwa ulikuwa ni wakati wa wafalme kwenda vitani lakini yeye hakwenda vitani, alibaki anarandaranda mjini tu na hiki ndio moja ya sababu ambayo mwandishi anaiona kuwa Daud alikosea!

 

2.       Aliudharau wajibu -  Kupigania watu ulikuwa ni moja ya wajibu wa waamuzi na wafalme Daudi alikuwa anawajibika kabisa kwenda vitani, huu ulikuwa ni wajibu wake na wajibu wa wafalme wa mataifa yote, ndio kuna wakati unaweza kumtuma mtu aende, Lakini mwandishi anaonyesha kuwa tatizo hapa lililopelekea habari kuwa nyingine kwa Mfalme Daudi ni kutokwenda vitani yeye alimtuma Yoabu aende, wakati mwingine ili Mungu aweze kuleta ukombozi kwa jamii ni lazima waweko watu watakaokubali kubeba wajibu, kama kila mmoja wetu akibeba wajibu wake kwa ufanisi tutaweza kuona mwanga

 

Luka 1:38 “Mariamu akasema, Tazama, mimi ni mjakazi wa Bwana; na iwe kwangu kama ulivyosema. Kisha malaika akaondoka akaenda zake.”

 

Mariam alikubali kuubeba wajibu wa kumzaa Yesu na akaleta faida Kubwa sana Duniani, walimu wakifanya wajibu wao, wanafunzi wakifanya wajibu wao, wanasiasa wakifanya wajibu wao na  wananchi wakifanya wajibu wao hakuna kitakachoshindikana, mke naye afanye wajibu wake na mume naye afanya wajibu wake kila mmoja atimize wajibu, wake kila mmoja akitimiza wajibu wake hakuna changamoto itakayojitokeza popote, Daudi alikwepa wajibu, na kudharau muda na majira aliyotakiwa kwenda vitani na matokeo yake alipatwa na anguko la kihistoria, hatuwezi kumlaumu yeye kwa sababu zozote zile kwani kuna kitu cha kujifunza kutoka kwake lakini mwandishi anatuonyesha kuwa moja ya sababu ya anguko lake ni kudharau wajibu, inapotokea kuwa shetani akatutia katika kishawishi cha kutokuzingatia kutimiza wajibu tunaweza kujikuta tunajutia maisha yetu yote na kusema laiti ningelijua kwa msingi huo ni muhimu kwetu tukatimiza wajibu, najua ziko ndoa nyingi sana zinapitia kwenye changamoto ambazo kimsingi ni kwa sababu tu watu hawataki kutimiza wajibu wao, kila mmoja akimfanyia mwenziwake kile ambacho maandiko yameagiza basi, katika jamii yetu kama kila mmoja wetu atatimiza wajibu kamwe haitakuja tuone madhara na majuto baadaye timiza wajibu.

 

3.       Kupenda rahisi/au uvivu – kupenda rahisi au uvivu kuna madhara makubwa sana katika maisha yetu tunaambiwa kuwa Daudi alikaa tu onaLakini Daudi mwenyewe akakaa Yerusalemu.”Maana yake alikaa tu hakufanya kazi, Daudi aliingiwa na uvivu, mtu akikaa tu bila jambo la Muhimu la kufanya, kinachofuata sasa ni kumpa ibilisi nafasi, “Idlenes gives great adavantage to the temper  Neno la Mungu linapingana vikali sana na swala zima la la uvivu, na wakati wote neno la Mungu linatutaka kupingana na tatizo la uvuvi na linawataka watu wafanye kazi likiwa na mifano mingi sana na maelekezo mengi sana mfano

 

Mithali 6:6-11 “Ewe mvivu, mwendee chungu, Zitafakari njia zake ukapate hekima. Kwa maana yeye hana akida, Wala msimamizi, wala mkuu, Lakini hujiwekea akiba ya chakula wakati wa jua; Hukusanya chakula chake wakati wa mavuno. Ewe mvivu, utalala hata lini? Utaondoka lini katika usingizi wako? Bado kulala kidogo, kusinzia kidogo, Bado kukunja mikono upate usingizi! Hivyo umaskini wako huja kama mnyang'anyi, Na uhitaji wako kama mtu mwenye silaha.”

 

Biblia ina la kusema kuhusu uvivu. Kitabu cha Mithali imejawa na hekima kuhusu uvivu na onyo kwa mtu mvivu. Mithali inatuambia kwamba mtu mvivu anachukia kazi:

 

Mithali 21:25 "Matakwa yake mtu mvivu humfisha, kwa maana mikono yake hukataa kufanya kazi."

 

Mithali 26:13-14 “Mtu mvivu husema, Simba yuko njiani, Simba yuko katika njia kuu. Kama vile mlango ugeukavyo katika bawaba zake; Kadhalika mtu mvivu katika kitanda chake.“

 

Mithali 18:9 Yeye naye aliye mvivu katika kazi yake, Ni ndugu yake aliye mharabu. Newton's first law states that, “if a body is at rest or moving at a constant speed in a straight line, it will remain at rest or keep moving in a straight line at constant speed unless it is acted upon by a force”. Mwandishi anaonyesha kuwa taabu nyingine ambayo Daudi ilimpelekea kuingia katika hali hii nzito ya anguko ni kukaa tu bila kufanya shughuli 2 Wathesalonike 3:10 “Kwa kuwa hata wakati ule tulipokuwapo kwenu tuliwaagiza neno hili, kwamba ikiwa mtu hataki kufanya kazi, basi, asile chakula”. Kila mmoja wetu anapaswa kuhakikisha kuwa hatumpi ibilisi nafasi, kila mmoja ahakikishe kuwa anaukomboa wakati na hapotezi muda, muda sio wa kuchezea muda ni mali, lakini wakati huo huo kila mmoja atimize wajibu wake na mwisho tuhakikishe kuwa tunapiga vita uvizu, maswala haya yalipodharauliwa na daudi yalileta anguko kwake ashukuriwe Mungu yeye alianguka katika zinaa lakini anguko baya kuliko yote ni kushindwa maisha hili linaleta majuto makubwa na machungu sana Duniani kuliko naguko la iana nyinguine lolote tunaweza kujiokoa kwa kujituma kwa bidii kwa kutumia nafasi na vipawa tulivyopewa na Mungu na kukamilisha kusudi la Mungu alilolikusudia kwetu Duniani, Neema ya Mungu na ikufunike ikiwa unataka kuishi kama Mfalme katika wakati ujao ni vema ukiyazingatia hayo!

Rev. Innocent Samuel Kamote.

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni