Jumanne, 28 Machi 2023

Mungu Katikati ya shida zako !


Zaburi 138:6-8 “Ingawa Bwana yuko juu, amwona mnyenyekevu, Naye amjua mwenye kujivuna tokea mbali. Nijapokwenda kati ya shida utanihuisha, Utanyosha mkono juu ya hasira ya adui zangu, Na mkono wako wa kuume utaniokoa. Bwana atanitimilizia mambo yangu; Ee Bwana, fadhili zako ni za milele; Usiziache kazi za mikono yako.”



Utangulizi:

Duniani ni mahali ambapo pana changamoto za aina mbalimbali ambazo kila mwanadamu aliyezaliwa na mwanamke atakutana nazo, wakati mwingine tutakutana na hali ngumu sana ama upinzani mzito sana, au magonjwa makubwa ya kusumbua au kuwa na ndoto kubwa  ambazo tunatafuta namna ya kuzitimiza, na changamoto nyinginezo nyingi, na wakati mwingine hali Fulani za kukatisha tamaa na kuvunja moyo na ama wakati mwingine ukiwa katika vita kali sana, katika ndoa, katika kazi, katika masomo, katika biashara, katika mashamba, katika mifugo na katika mahusiano taabu hizi zote Yesu Kristo anazifahamu na anajua ya kuwa tunazipitia na alitutaka tujipe moyo kwa sababu yeye amezishinda kwaajili yetu. 

Yohana 16:33 “Hayo nimewaambieni mpate kuwa na amani ndani yangu. Ulimwenguni mnayo dhiki; lakini jipeni moyo; mimi nimeushinda ulimwengu.” 

Yesu anazungumza maneno haya kwa sababu anatambua wazi kuwa wakati mwingine tunaweza kujiona kama tuna mapungufu Fulani nani kama hatutoshi wala hatustahili hata kufanyiwa muujiza, lakini ni muhimu sana kukumbuka ya kuwa Mungu yuko pamoja nasi yeye anaitwa Emmanuel yaani Mungu pamoja nasi na wakati tunapopitia kila aina ya changamoto na mambo yoyote yanayotukabili yeye yuko pamoja nasi, alikuwa pamoja na Yesu Kristo katika mateso yake na alihakikisha anamfufua, na hakumuacha kaburini, wakati Daudi anakabiliana na jitu kubwa kuliko uwezo wake Mungu alikuwa pamoja naye, wakati Paulo na Sila wakiwa gerezani ni yeye aliyafungua milango ya gereza, wakati Danieli anatupwa katika tundu la Simba ni yeye aliyekuweko kufunga makanwa ya simba, na wakati Shadrak, Meshak na Abednego wakitupwa kwenye tanuri la moto mkali ni yeye ndiye aliyejiunga nao wasiunguzwe jambo kubwa la msingi ni kukumbuka tu ya kuwa Mungu yuko kati kati ya shida zako. 

Zaburi 138:6-8 “Ingawa Bwana yuko juu, amwona mnyenyekevu, Naye amjua mwenye kujivuna tokea mbali. Nijapokwenda kati ya shida utanihuisha, Utanyosha mkono juu ya hasira ya adui zangu, Na mkono wako wa kuume utaniokoa. Bwana atanitimilizia mambo yangu; Ee Bwana, fadhili zako ni za milele; Usiziache kazi za mikono yako.” 

Katika mistari hii ya msingi hususani mstari ule wa saba yaani Zaburi ya 138:7 “Nijapokwenda kati ya shida utanihuisha, Utanyosha mkono juu ya hasira ya adui zangu, Na mkono wako wa kuume utaniokoa.  Mungu nanatufundisha kupitia mtumishi wakeMwandishi wa zaburi hii ya kuwa yeye huwa katikakati ya shida zetu mstari huu katika lugha ya kiingereza Biblia ya NIV husomeka hiviThough I walk in the midst of trouble, you preserve my life you stretch out your hand against the anger of my foes with your hand you save meambapo katika tafasiri yangu naweza kusema Mstari huu unasema hivi NINAPOPITA KATIKATI YA TAABU/SHIDA UNANYOOSHA MKONO WAKO KUNIOKOA NA HASIRA ZA ADUI ZANGU, Yaani maana yake katikati ya shida Mungu anakuwepo, na anatoa msaada kwaajili ya utukufu wake hii maana yake ni nini ? sio kila wakati Mungu atakutoa nje ya shida lakini wakati mwingine atakuacha uingie katika shida na changamoto mbalimbali kisha ataweka mkono wake kwaajili ya utukufu wake, kwa sababu hiyo jambo kubwa la Msingi na la kukumbuka ni kuwa Bwana yuko pamoja nawe bila kujali hali unayoipitia, kuokolewa katika shida sio jambo la Msingi sana kama Mungu kuwa pamoja nawe, Mungu kuwa pamoja nawe hilo ndio jambo kubwa na la msingi, 

Isaya 43:1-2 “Lakini sasa, Bwana aliyekuhuluku, Ee Yakobo, yeye aliyekuumba, Ee Israeli, asema hivi, Usiogope, maana nimekukomboa; nimekuita kwa jina lako, wewe u wangu. Upitapo katika maji mengi nitakuwa pamoja nawe; na katika mito, haitakugharikisha; uendapo katika moto, hutateketea; wala mwali wa moto hautakuunguza.” 

Unaona haijalishi kuna dhuruba kiasi gani kama Mungu yuko pamoja nawe hakuna kitakachoshindikana kwaajili ya utukufu wake, Mungu atatokeza muujiza kwa sababu yumo katikati ya shida yako pamoja nawe 

Kumbuka kuwa 

1.       Wakati Suleiman anaanza kutawala alikuwa na hofu kuwa anawezaje kuongoza taifa kubwa na watu wengi kama wale, baba yake alikuwa mtu wa vita na mtu aliyemtegemea Mungu, hivyo Mungu alimsaidia Suleimani kuwa na hekima ya namna ya kuingia na kutoka na mambo yakawa shwari 

2.       Mungu hakumuwacha Yesu asisulubiwe lakini alimfufua siku ya tatu, hakumwacha mtakatifu wake aonje uharibifu

3.       Mungu hakumwacha Nyangumi asimmeze Yona na badala yake alimsababisha nyangumi amtapike Yona siku ya tatu

4.       Mungu hakumuacha Daniel asiingizwe kwenye tundu la Simba badala yake aliyafunga makanwa ya simba

5.       Mungu hakuwaacha Shadrak na Meshak na Abednego wasitupwe katika tanuru la Moto lakini badala yake alijiunga nao katikati ya Moto ili usiwateteze

6.       Mungu hakuwaacha Paulo na Silas wasipigwe na kutupwa gerezani lakini badala yake aliwaacha wakafungwa gerezani na baadaye akayafungua malango ya magereza na vifungo vyake   

Changamoto kubwa katika maisha yetu sio kutokupitia changamoto bali ni kumuomba Mungu awe pamoja nasi hili ndilo jambo la Msingi Yesu aliahidi ya kuwa atakuwa pamoja nasi hata ukamilifu wa dahari, na alihahidi kuwa tunapokutanika wawili au watatu kwa ajili ya jina lake atakuwa pamoja nasi, Hakuna jambo la msingi duniani kama kuwa na Mungu, Muulize jirani yako una Mungu ukiwa na Mungu una kila kitu!, Changamoto yako sio kubwa kuliko Mungu tunayemtumikia na kumuabudu, Bwana ampoe neema kila mmoja wetu kuwa na Mungu wakati tunapopita katika siku za kujaribiwa kwetu katika jina la Yesu Kristo amen! 

Na Rev. Innocent Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni