Jumanne, 11 Aprili 2023

Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha?

 

Mathayo 27:46 - 49. “Na kama saa tisa, Yesu akapaza sauti yake kwa nguvu akisema, Eloi, Eloi, lama sabakthani? Yaani, Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha? Na baadhi yao waliohudhuria, waliposikia, walisema, Huyu anamwita Eliya. Mara mmoja wao akaenda mbio, akatwaa sifongo, akaijaza siki, akaitia juu ya mwanzi, akamnywesha. Wale wengine wakasema, Acha; na tuone kama Eliya anakuja kumwokoa.”


Utangulizi:

Leo tutachukua Muda kujifunza kwa undani mojawapo ya maneno Muhimu katika maneno yaliyosemwa na Yesu Kristo wakati wa Mateso yake pale msalabani MUNGU WANGU MUNGU WANGU MBONA UMENIACHA, tunataka kujifunza maana ya maneno haya kwa kina na kuangalia uhalisia wa ubinadamu hususani wakati wanadamu wanapopitia mateso, Pamoja na menono haya muhimu, tutakayoangalia leo maneno mengine kwa mfululizo katika maneno saba aliyozungumza Kristo pale msalabani kwa mujibu wa injili zote nne ni pamoja na :-

·         Baba uwasamehe kwa maana hawajui walitendalo Luka 23:34

·         Amin nakuambia leo hii utakuwa pamoja nani peponi Luka 23:43

·         Mama tazama mwanao, mwana tazama mama yako Yohana 19:26-27

·         Mungu wangu Mungu wangu mbona umeniacha Mathayo 27:46

·         Nina kiu Yohana 19:28

·         Imekwisha Yohana 19:30

·         Baba mikononi mwako naiweka roho yangu Luka 23:46

Maana ya Maneno Mungu wangu Mungu wangu mbona umeniacha?

Mathayo 27:46 “Na kama saa tisa, Yesu akapaza sauti yake kwa nguvu akisema, Eloi, Eloi, lama sabakthani? Yaani, Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha?”

Ni muhimu kufahamu kuwa Mwandishi wa kitabu cha Mathayo anajaribu tu kufupisha kile ambacho Yesu Kristo alikisema na pia anajaribu kutafasiri lugha kiaramu ambayo Yesu aliitumia wakati anazungumza maneno hayo. Maneno hayo Eloi, Eloi, Lamasabakthan, katika lugha ya asili yanasomeka kama Eli, Eli, Lama Sabachthan ni sehemu ya maneno kamili ambayo Yesu aliyazungumza ka lugha ya kiaramu, maneno hayo yanatafasirika hivi Eli, (Adonai) Eli (Adonai) Lama (Why?) kwanini ?, mbona? Sabachthani (You have left, Abandoned) me) Umeniacha.  Kimsingi ni kuwa katika kini cha mateso yake Yesu Kristo alikuwa anatimiza na kumuomba Mungu sawa na Zaburi ya 22:1-22 ambapo katika Zaburi hii Daudi ambaye alipendwa sana na Mungu alikuwa akimuomba Mungu kutokana na Mapito aliyokuwa akiyapitia ambayo kimsingi pia yalikuwa ni mapito ya kinabii yaliyohusiana na Yesu Kristo Mwenyewe Mwana wa Daudi, Kumbuka kuwa Yesu alikuja kutimiza maandiko ambayo torati na manabii na maandiko yote yaliweka bayana kuwa Masihi hana budi kuteseka 

Luka 23:13- 27 “Na tazama, siku ile ile watu wawili miongoni mwao walikuwa wakienda kijiji kimoja, jina lake Emau, kilichokuwa mbali na Yerusalemu kama mwendo wa saa mbili. Nao walikuwa wakizungumza wao kwa wao habari za mambo hayo yote yaliyotukia. Ikawa katika kuzungumza na kuulizana kwao, Yesu mwenyewe alikaribia, akaandamana nao. Macho yao yakafumbwa wasimtambue. Akawaambia, Ni maneno gani haya mnayosemezana hivi mnapotembea? Wakasimama wamekunja nyuso zao. Akajibu mmoja wao, jina lake Kleopa, akamwambia, Je! Wewe peke yako u mgeni katika Yerusalemu, hata huyajui yaliyotukia humo siku hizi? Akawauliza, Mambo gani? Wakamwambia, Mambo ya Yesu wa Nazareti, aliyekuwa mtu nabii, mwenye uwezo katika kutenda na kunena mbele za Mungu na watu wote; tena jinsi wakuu wa makuhani na wakubwa wetu walivyomtia katika hukumu ya kufa, wakamsulibisha. Nasi tulikuwa tukitumaini ya kuwa yeye ndiye atakayewakomboa Israeli. Zaidi ya hayo yote, leo ni siku ya tatu tangu yalipotendeka mambo hayo; tena, wanawake kadha wa kadha wa kwetu walitushitusha, waliokwenda kaburini asubuhi na mapema, wasiuone mwili wake; wakaja wakasema ya kwamba wametokewa na malaika waliosema kwamba yu hai. Na wengine waliokuwa pamoja nasi walikwenda kaburini wakaona vivyo hivyo kama wale wanawake walivyosema, ila yeye hawakumwona. Akawaambia, Enyi msiofahamu, wenye mioyo mizito ya kuamini yote waliyoyasema manabii! Je! Haikumpasa Kristo kupata mateso haya na kuingia katika utukufu wake? Akaanza kutoka Musa na manabii wote, akawaeleza katika maandiko yote mambo yaliyomhusu yeye mwenyewe.”

Unaona kimsingi Yesu alikuwa ameandikiwa kila atakalokuja kulitenda na kulinena katika Torati, Manabii na Zaburi au maandiko hivyo Neno Mungu wangu Mungu wangu ilikuwa ni nukuu ya Zaburi ya 22 ambayo ina mukhtasari wa Mateso ya Bwana Yesu yaliyotabiriwa na Daudi katika zaburi hiyo hebu tuyaangalie tuweze kuona 

Zaburi 22:1-20 “Mungu wangu, Mungu wangu, Mbona umeniacha? Mbona U mbali na wokovu wangu, Na maneno ya kuugua kwangu? Ee Mungu wangu, nalia mchana lakini hujibu Na wakati wa usiku lakini sipati raha. Na Wewe U Mtakatifu, Uketiye juu ya sifa za Israeli. Baba zetu walikutumaini Wewe, Walitumaini, na Wewe ukawaokoa. Walikulilia Wewe wakaokoka, Walikutumaini wasiaibike. Lakini mimi ni mdudu wala si mtu, Laumu ya wanadamu na mzaha wa watu. Wote wanionao hunicheka sana, Hunifyonya, wakitikisa vichwa vyao; Husema, Umtegemee Bwana; na amponye; Na amwokoe sasa, maana apendezwa naye. Naam, Wewe ndiwe uliyenitoa tumboni, Ulinitumainisha matitini mwa mama yangu.  Kwako nalitupwa tangu tumboni, Toka tumboni mwa mamangu ndiwe Mungu wangu. Usiwe mbali nami maana taabu i karibu, Kwa maana hakuna msaidizi. Mafahali wengi wamenizunguka, Walio hodari wa Bashani wamenisonga; Wananifumbulia vinywa vyao, Kama simba apapuraye na kunguruma. Nimemwagika kama maji, Mifupa yangu yote imeteguka, Moyo wangu umekuwa kama nta, Na kuyeyuka ndani ya mtima wangu. Nguvu zangu zimekauka kama gae, Ulimi wangu waambatana na taya zangu; Unaniweka katika mavumbi ya mauti Kwa maana mbwa wamenizunguka; Kusanyiko la waovu wamenisonga; Wamenizua mikono na miguu. Naweza kuihesabu mifupa yangu yote; Wao wananitazama na kunikodolea macho. Wanagawanya nguo zangu, Na vazi langu wanalipigia kura. Nawe, Bwana, usiwe mbali, Ee Nguvu zangu, fanya haraka kunisaidia. Uniponye nafsi yangu na upanga, Mpenzi wangu na nguvu za mbwa.”

Kimsingi maombi ya Daudi na Maombi ya Yesu Kristo yanafanana na hatujawahi kuona wakati wowote Mungu akimuacha Daudi au akimuacha Yesu Kristo lakini kwanini walilia maneno hayo na kuomba dua hizo wakati wa mateso yao ilihali wote tunajua kuwa maandiko yanamsifia Daudi kama mtu aliyeupendeza Moyo wa Mungu ona

Matendo 13:22 “Na alipokwisha kumwondoa huyo, akamwinua Daudi awe mfalme wao ambaye alimshuhudia, akisema, Nimemwona Daudi, mwana wa Yese, mtu anayeupendeza moyo wangu, atakayefanya mapenzi yangu yote.”

Aidha katika namna kama hiyo Mungu katika neno lake vilevile anajivunia Kristo Yesu mwanae kama mtu aliyeupendeza moyo wake ona

Mathayo 3:16-17 “Naye Yesu alipokwisha kubatizwa mara akapanda kutoka majini; na tazama, mbingu zikamfunukia, akamwona Roho wa Mungu akishuka kama hua, akija juu yake; na tazama, sauti kutoka mbinguni ikisema, Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, ninayependezwa naye.”

Inawezekanaje Mungu kuwaacha awapendao? Mungu anatujali sana katika kiwango ambacho hata mama anaweza kumsahau mtoto wake lakini sio Mungu wetu ona

Isaya 49:15-16 15. “Je! Mwanamke aweza kumsahau mtoto wake anyonyaye, hata asimhurumie mwana wa tumbo lake? Naam, hawa waweza kusahau, lakini mimi sitakusahau wewe. Tazama, nimekuchora katika vitanga vya mikono yangu; kuta zako ziko mbele zangu daima. Kimsingi kila mwanadamu anapokuwa na mafanikio watu”               

Mungu wetu anatujali mmno lakini katika hali ya kawaida kila mwanadmu anapopitia mateso na changamoto za aina mbalimbali kwa kawaida wanadamu wana tabia ya kuwa mbali nawe wanatabia ya kukuacha ubaki peke yako na wakati huu Mungu hukaa kimya ili mateso yale yaweze kuleta somo linalokusudiwa kwako hivuo kibinadamu zinakuweko fikra ya kuwa huenda Mungu amekuacha, Ayubu alipokuwa na mafanikio makubwa sana tunaambiwa watu wengi sana walimwendea na nyumba yake ilijaa watu wa kila aina maandiko yanasema na watu wa nyumbani wengi sana ona

Ayubu 1:3 “Mali yake nayo yalikuwa ni kondoo elfu saba, na ngamia elfu tatu, na jozi za ng'ombe mia tano, na punda wake mia tano, NA WATU WA NYUMBANI WENGI SANA; basi hivi mtu huyo alikuwa ni mkuu sana kuliko watu wote wa upande wa mashariki.”

Tunaambiwa kuwa wakati wa mateso yake Ayubu watu wote waliokuwa nyumbani mwake walimkimbia mpaka pale Ayubu alipobarikiwa tena ndio tunaelezwa kuwa watu wote wakamwendea ona

Ayubu 42:10-12 “Kisha Bwana akaugeuza uteka wa Ayubu, hapo alipowaombea rafiki zake; Bwana naye akampa Ayubu mara mbili kuliko hayo aliyokuwa nayo kwanza. Ndipo wakamwendea nduguze wote, waume kwa wake, nao wote waliojuana naye hapo zamani, wakala chakula pamoja naye katika nyumba yake; nao wakamlilia na kumtuza moyo katika habari za huo uovu wote Bwana aliouleta juu yake; kila mtu akampa kipande cha fedha, na pete ya dhahabu kila mmoja. Basi hivyo Bwana akaubarikia huo mwisho wa Ayubu zaidi ya mwanzo wake; naye alikuwa na kondoo kumi na nne elfu, na ngamia elfu sita, na jozi za ng'ombe elfu, na punda wake elfu.”

Ni swala la kawaida kwamba wakati wa mateso watu wanakukimbia na mara kadhaa inadhaniwa kuwa Mungu amekuacha nani kilio cha kawaida Pale mtu anapopita katika magumu kufikiri mkuwa ni Mungu ndiye aliyemtendea hayo, Ndio maana Daudi alilia katika Zaburi ya 22 japo ilikuwa pia ni unabii kw Mwanaye Yesu Masihi ambaye naye alilia akijua ya kuwa anaitimiza Zaburi ya 22 yote alitioandikiwa humo yalitokea siku ya mateso yake maneno mabaya , kugawanywa kwa nguo zake kwa kuzipigia kura, kugomelewa mikono yake na miguu yake msalabani, kudharauliwa na kuwekwa katika mikono ya watu wabaya wapate kumdhihaki, na kumdhalilisha, Kifo cha Msalabani hakikuwa kifo cha kawaida kilikuwa ni kifo cha maumivu ya kila aina kisaikolojia na nafsi na mwili Yesu ni kama alikuwa amabaki pake yake msalabani, saa ya kujaribiwa huwa ni kama tunabaki peke yetu, kundi kubwa la watu waliofaidika na huduma yake hakuna hata mmoja aliyeweza kusogea na kufanya utetezi wakati Masihi alipokuwa anateseka Msalabani na ndio maana akaisema zaburi ya 22 ambayo hutambulika zaidi kwa Mstari wake wa kwanza Mungu wangu Mungu wangu mbiona umeniacha!

Msalabani Yesu hakuwa ametundikwa kwa sababu nya dhambi yake ilikuwa ni kwaajili ya dhambi zetu mimi na wewe, nani mimi na wewe ndio ambao tulipaswa kuyabeba maumivu yale, lakini Mwokozi alibeba kwa niaba yetu na kilio kilikuwa kwa ajili yetu na ubinadamu wetu, alilia kuonyesha kuwa wanadamu wakati wote tunahitaji msaada wa Mungu na kuwa peke yetu hatuwezi, adui yetu yu aweza kufanya jambo lolote la kutuumiza sana kama tutabaki bila msaada wa Mungu, Mtu mmoja aliimba wimbo unasema nafikiria ukiniacha roho yangu itakuwaje Bwana ? itakuwa ni mawindo ya adui kwa wepesi sana… wakati wote tunapokuwa na maisha yetu bila ya Mungu tunajiweka katima hatari ya kushambuliwa na kuumizwa na ibilisi, magonjwa matesi na dhiki za dunia hii, lakini ashukuriwe Mungu kuwa pale msalabani Yesu Kristo alikuwa anateseka kwaajili yatu na kwaajili ya ukombozi wetu ili kuukaribisha uwepo wa Mungu katika maisha yetu

Isaya 53:4-5 “Hakika ameyachukua masikitiko yetu, Amejitwika huzuni zetu; Lakini tulimdhania ya kuwa amepigwa, Amepigwa na Mungu, na kuteswa. Bali alijeruhiwa kwa makosa yetu, Alichubuliwa kwa maovu yetu; Adhabu ya amani yetu ilikuwa juu yake, Na kwa kupigwa kwake sisi tumepona.”

Na Rev. Innocent Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni