Jumapili, 28 Mei 2023

Usiende bila uwezo utokao juu!


Luka 24:46-49 “Akawaambia, Ndivyo ilivyoandikwa, kwamba Kristo atateswa na kufufuka siku ya tatu; na kwamba mataifa yote watahubiriwa kwa jina lake habari ya toba na ondoleo la dhambi, kuanza tangu Yerusalemu. Nanyi ndinyi mashahidi wa mambo haya. Na tazama, nawaletea juu yenu ahadi ya Baba yangu; lakini kaeni humu mjini, hata mvikwe uwezo utokao juu.”



Utangulizi:

Ni muhimu kwa kila mmoja kuwa na ufahamu, ya kwamba uhai wa kanisa unategemeana sana na jinsi au namna Kanisa linavyompa nafasi Roho Mtakatifu kufanya kazi pamoja nasi, Endapo kanisa litaendelea na kazi zake za kutimiza agizo kuu bila kutoa nafasi kwa mwenye kanisa yaani Roho Mtakatifu, itakuwa ni rahisi sana kanisa kupoteza nguvu zake na kubaki na hekima ya kibinadamu, jambo ambalo linaweza kutuletea aibu na kushindwa vibaya, ni kwa kuzingatia hilo leo katika siku ya Pentekoste ni muhimu kwa kila mmoja wetu kujikumbusha tena umuhimu wa kumpa nafasi Roho Mtakatifu kufanya kazi pamoja nasi vinginevyo au kinyume chake usiende bila Roho Mtakatifu au uwezo utokao juu!.

Mathayo 28:18-20 “Yesu akaja kwao, akasema nao, akawaambia, Nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani. Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu; na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi; na tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku zote, hata ukamilifu wa dahari.”

Tutajifunza somo hili kwa kuzingatia vipengele viwili muhimu vifuatavyo:-

*      Agizo la kwenda kuihubiri injili

*      Agizo la kutokwenda bila uwezo utokao juu      

Agizo la kwenda kuihubiri injili.

Moja ya agizo muhimu sana na ambalo ndio msingi wa uwepo wa Kanisa duniani ni kuihubiri injili, Yesu Kristo aliwandaa wanafunzi wake kwa muda wa kutosha ili hatimaye aweze kuwatuma kwenda kuihubiri injili

Marko 3:13-15 “Akapanda mlimani, akawaita aliowataka mwenyewe; wakamwendea.  Akaweka watu kumi na wawili, wapate kuwa pamoja naye, na kwamba awatume kuhubiri, tena wawe na amri ya kutoa pepo.”

Unaona kusudi kubwa na Yesu Kristo kuwaita mitume au wanafunzi wake ni ili awafundishe waweze kuwa pamoja naye wakae katika uwepo wake kisha baada ya hayo aweze kuwatuma kwenda kuihubiri injili, haya ndio makusudi makubwa zaidi ya uwepo wa kanisa, kila kanisa linawajibu wa kuihubiri injili, kuhubiri injili ya Bwana wetu Yesu Kristo kwa watu wote ndio mapenzi ya Mungu, kanisa lisilo hubiri injili ni kanisa lisilo na utii kwa kazi ya Kristo ni kanisa linalozimika katika moto wa injili, nachelea kusema ni kanisa lililokufa; lakini ni wazi kuwa litakuwa ni kanisa lililopoteza mwelekeo, ni lazima tuihubiri injili, ni lazima tuwafikie watu wa mataifa yote na vile vile na kuwafungua kutoka katika nguvu za giza yaani vifungo vya shetani na kutoa pepo wachafu kwa wanaoonewa nao,

Marko 16:15-18 “Akawaambia, Enendeni ulimwenguni mwote, mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe. Aaminiye na kubatizwa ataokoka; asiyeamini, atahukumiwa. Na ishara hizi zitafuatana na hao waaminio; kwa jina langu watatoa pepo; watasema kwa lugha mpya; watashika nyoka; hata wakinywa kitu cha kufisha, hakitawadhuru kabisa; wataweka mikono yao juu ya wagonjwa, nao watapata afya.”

Agizo hili kubwa ni la muhimu sana watu waokolewe na kufunguliwa kutoka katika nguvu za giza ili wahamishiwe kwenye ufalme wa mwana wa pendo lake, kila kanisa na kila mtu anayetambua umuhimu wa agizo hili kuu anapaswa kulitii na kuhakikisha kuwa linafanyiwa kazi na hayo ndio mapenzi ya Mungu. Kuna changamoto kiasi Fulani katika kanisa la leo, ya kuwa watu wengine wamejikita sana katika kuwafungua watu bila kuhakikisha kuwa watu hao wanatubu dhambi zao na kumwamini Bwana Yesu, mambo haya yanahitaji uwiano, lakini kubwa zaidi tunapolitimiza agizo kuu Bwana mwenyewe atakuwepo kulithibitisha neno kwa ishara na miujiza, hivyo miujiza iwe ni sehemu tu ya kuthibitishwa kwa neno na sio biashara ya kuponywa tu kwa miili ya watu hao ili hali nafsi na roho zao zingali kifungoni, ni muhimu sana kuihubiri injili sawa na agizo la Bwana wetu Yesu Kristo na hayo ndio mapenzi ya Mungu      

Agizo la kutokwenda bila uwezo utokao juu.

Pamoja na umuhimu mkubwa wa agizo hili kuu na msisitizo wake ni muhimu sana tukatilia maanani kuwa ndani ya agizo kuu Yesu mwenyewe vilevile alisisitiza wanafunzi wake wasiende bila kuvikwa uwezo utokao juu! Ona

Luka 24:46-49  Akawaambia, Ndivyo ilivyoandikwa, kwamba Kristo atateswa na kufufuka siku ya tatu; na kwamba mataifa yote watahubiriwa kwa jina lake habari ya toba na ondoleo la dhambi, kuanza tangu Yerusalemu. Nanyi ndinyi mashahidi wa mambo haya. Na tazama, nawaletea juu yenu ahadi ya Baba yangu; lakini kaeni humu mjini, hata mvikwe uwezo utokao juu.”

Uwezo huo utokao juu ni nini na unapatikanaje? uwezo huu utokao juu ni matokeo ya nguvu za Mungu kuwa juu ya wale waliomuamini Bwana Yesu na waliotayari kulitimiza agizo kuu, uwezo huu unapatikana baada ya Roho Mtakatifu kuja juu yetu ona

Matendo 1:8 “Lakini mtapokea nguvu, akiisha kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu; nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, na katika Uyahudi wote, na Samaria, na hata mwisho wa nchi.”

Kwa nini Yesu Kristo alisisitiza kwamba wanafunzi wake wasiende bila uwezo huo kutoka juu yaani Bila kupokea nguvu kutoka kwa Mungu Roho Mtakatifu? Sababu kubwa mojawapo ni kuwa kazi ya kuihubiri injili ina upinzani, ina upinzani wa aina mbalimbali, kutoka kwa watu, dini zao, tamaduni zao, serikali zao na miungu yao na nguvu za giza, hivyo kuna nguvu za upinzani ambazo ni ngumu kuzikabili katika hali ya kawaida ya kibinadamu bila neema na msaada wa Mungu, kujaribu kufanya kazi za injili na hata kukemea pepo bila kuwa na nguvu za kukabiliana na mapepo hayo na upinzani huo ni hatari sana na rahisi kujikuta unakata tamaa na kuingia katika kuabishwa na upinzani wa kishetani, hatuwezi kuigiza kwa kuwa shetani anaogopa wazi nguvu ya Mungu na anajua watu wanaotumiwa na Mungu na wale wanaoigiza!

Matendo 19:11-20 “Baadhi ya Wayahudi wenye kutanga-tanga, nao ni wapunga pepo, wakajaribu kutaja jina la Bwana Yesu juu yao waliopagawa na pepo wachafu, wakisema, Nawaapisha kwa Yesu, yule anayehubiriwa na Paulo. Walikuwako wana saba wa mtu mmoja Skewa, Myahudi, kuhani mkuu, waliofanya hivyo. Yule pepo mchafu akawajibu, akawaambia, Yesu namjua na Paulo namfahamu, lakini ninyi ni nani? Na yule mtu aliyepagawa na pepo mchafu akawarukia wawili, akawaweza, akawashinda, hata wakatoka mbio katika nyumba ile hali wa uchi na kujeruhiwa. Habari hii ikajulikana na Wayahudi wote na Wayunani waliokaa Efeso, hofu ikawaingia wote, na jina la Bwana Yesu likatukuzwa. Na wengi wa wale walioamini wakaja wakaungama, wakidhihirisha matendo yao. Na watu wengi katika wale waliotumia mambo ya uganga wakakusanya vitabu vyao, wakavichoma moto mbele ya watu wote; wakafanya hesabu ya thamani yake, wakaona ya kwamba yapata fedha hamsini elfu. Hivyo ndivyo neno la Bwana lilivyozidi na kushinda kwa nguvu.”

Unaona kutoka katika kifungu hiki cha maandiko tunaona mambo makubwa mawili, watu waliojaribu kukemea mapepo kwa jina la Yesu huku wakiwa hawajavikwa uwezo ule utokao juu, wala hata kuokoka!  na matokeo yake walipigwa na kujeruhiwa vibaya kwa sababu hawakuwa na nguvu wala mamlaka ya kutoa Pepo, lakini Paulo mtume alitumiwa na Mungu kwa miujiza Mingi na zaidi sana hata watu waliotumia uganga walibadilika na kuchoma moto vitabu vyao vya uchawi vyenye gharama kubwa sana, Paulo mtume hakufanya haya kwa nguvu zake, alijaa Roho Mtakatifu alitumiwa na Mungu, ikiwa kanisa linataka kuona nguvu za Mungu ni lazima tutii agizo kuu lakini wakati huo huo tusiende bila uwezo utokao juu, yaani bila nguvu za Mungu Roho Mtakatifu ndani yetu!

Mungu hajawahi kumtuma mtu katika kazi fulani bila nguvu zake, nguvu za Roho wake Mtakatifu zinamuwezesha mtu huyo kukabiliana na upinzani kutoka kwa maadui wa injili, alipomtuma Musa dhidi ya Farao, kwa kusudi la kuwaokoa wana wa Israel katika nchi ya Misri, alimpa nguvu za kupambana na serikali ile iliyokuwa ikitumainia miungu na nguvu za giza zilizoongozwa na wachawi maarufu walioitwa Yane na Yambre ambao kimsingi walishindana na Musa na Haruni kwa kufanya kiujiza ya kuigiza ona 

2Timotheo 3:8 “Na kama vile Yane na Yambre walivyopingana na Musa, vivyo hivyo na hawa wanapingana na ile kweli; ni watu walioharibika akili zao, wamekataliwa kwa mambo ya imani.”

Unaona hawa walikuwa wachawi wakuu wa serikali pinzani ya Farao ambayo ilijawa na kuabudu miungu na kutegemea uganga na uchawi, Musa na Haruni na wazee wa Israel wangewezaje kudai uhuru katika serikali ya aina ile bila Nguvu za Mungu?  Hatuwezi kuwasaidia watu bila nguvu ya Mungu izidiyo nguvu zote!

Kutoka 7:20-22 “Musa na Haruni wakafanya hivyo, kama BWANA alivyowaambia; naye akaiinua ile fimbo, na kuyapiga maji yaliyokuwa mtoni, mbele ya Farao, mbele ya watumishi wake; na hayo maji yote yaliyokuwa katika mto yakageuzwa kuwa damu. Hao samaki waliokuwa mtoni nao wakafa; na ule mto ukatoa uvundo, Wamisri wasipate kunywa maji ya mtoni; na ile damu ilikuwa katika nchi yote na Misri. Lakini waganga wa Misri wakafanya mfano wa hayo kwa uganga wao; na moyo wake Farao ukawa mgumu, wala hakuwasikiza, kama BWANA alivyonena.”

Mwinjilisti Filipo alipokwenda kuihubiri injili katika eneo la Samaria alikutana na mtu aliyekuwa mchawi na aliyekuwa na nguvu za giza ambazo watu wengi waliamini ni uweza wa Mungu, mtu huyu aliiamini injili na kubatizwa lakini bado alikuwa na moyo wa kichawi mpaka alipokuja kushughulikiwa na Roho Mtakatifu wakati Petro na Yohana walipokwenda kutoa msaada wa kihuduma kule Samaria, ni hatari sana kama kanisa litafanya kazi chini ya kiwango cha nguvu za Mungu zinazohitajika na ndio maana leo kuna shuhuda za kuwepo kwa wachawi makanisani wakiingia na kutoka na kujifanyia uchawi wao na kanisa linaogopa tunawezaje kukabiliana na haya usiende bila uwezo utokao juu, lazima tujae ngvu za Roho Mtakatifu katika kiwango cha kufurika ona :-

Matendo 8:5-21 “Filipo akatelemka akaingia mji wa Samaria, akawahubiri Kristo. Na makutano kwa nia moja wakasikiliza maneno yale yaliyosemwa na Filipo walipoyasikia na kuziona ishara alizokuwa akizifanya. Kwa maana pepo wachafu wakawatoka wengi waliopagawa nao, wakilia kwa sauti kuu; na watu wengi waliopooza, na viwete, wakaponywa. Ikawa furaha kubwa katika mji ule. Na mtu mmoja, jina lake Simoni, hapo kwanza alikuwa akifanya uchawi katika mji ule, akiwashangaza watu wa taifa la Wasamaria, akisema ya kuwa yeye ni mtu mkubwa. Wote wakamsikiliza tangu mdogo hata mkubwa, wakisema, Mtu huyu ni uweza wa Mungu, ule Mkuu. Wakamsikiliza, kwa maana amewashangaza muda mwingi kwa uchawi wake. Lakini walipomwamini Filipo, akizihubiri habari njema za ufalme wa Mungu, na jina lake Yesu Kristo, wakabatizwa, wanaume na wanawake. Na yeye Simoni mwenyewe aliamini akabatizwa, akashikamana na Filipo; akashangaa alipoziona ishara na miujiza mikubwa inayotendeka. Na mitume waliokuwako Yerusalemu, waliposikia ya kwamba Samaria imelikubali neno la Mungu, wakawapelekea Petro na Yohana; ambao waliposhuka, wakawaombea wampokee Roho Mtakatifu; kwa maana bado hajawashukia hata mmoja wao, ila wamebatizwa tu kwa jina lake Bwana Yesu. Ndipo wakaweka mikono yao juu yao, nao wakampokea Roho Mtakatifu. Hata Simoni alipoona ya kuwa watu wanapewa Roho Mtakatifu kwa kuwekewa mikono ya mitume, akataka kuwapa fedha akisema, Nipeni na mimi uwezo huu, ili kila mtu nitakayemweka mikono yangu, apokee Roho Mtakatifu. Lakini Petro akamwambia, Fedha yako na ipotelee mbali pamoja nawe, kwa kuwa umedhania ya kuwa karama ya Mungu yapatikana kwa mali.”

Nadhani sasa unaweza kumuelewa Bwana Yesu kwanini alisisitiza usiende bila kuvikwa uwezo utokao juu, upinzani wowote katika injili unaweza kuzimwa endapo tu tutamruhusu Roho Mtakatifu Mungu kuwa pamoja nasi katika kazi hii, sio tu katika nguvu za giza pekee bali hata kuitetea imani na kukubali kuwa mashahidi na kufa kwaajili ya Kristo bila nguvu hizo ni vigumu kustahimili hata majaribu na upinzani dhidi ya injili na watumishi wa kweli ona

Matendo 6: 8-10 “Na Stefano, akijaa neema na uwezo, alikuwa akifanya maajabu na ishara kubwa katika watu. Lakini baadhi ya watu wa sinagogi lililoitwa sinagogi la Mahuru, na la Wakirene, na la Waiskanderia, na la wale wa Kilikia na Asia, wakaondoka na kujadiliana na Stefano; lakini hawakuweza kushindana na hiyo hekima na huyo Roho aliyesema naye.”

Katika kila kazi ambayo Mungu anampa mtu na au kumtuma mtu anampa nguvu hizo za Roho Mtakatifu ili kukabiliana na upinzani wake Samsoni aliitwa kuwa mwamuzi dhidi ya wafilisti waliokuwa wakiwaonea Waisraeli wakati huo hakuenda Samsoni bila uwezo huo utokao juu  Nguvu za Mungu zlimfanya samsoni kuwa wa kipekee ona

 Waamuzi 15:14-16 “Alipofika Lehi, Wafilisti wakapiga kelele walipokutana naye; ndipo roho ya Bwana ikamjia kwa nguvu, na zile kamba zilizokuwa juu ya mikono yake zikawa kama kitani iliyoteketezwa kwa moto, na vile vifungo vyake vikaanguka mikononi mwake. Naye akaona mfupa mbichi wa taya ya punda, akautwaa, akapiga watu elfu kwa mfupa huo; Samsoni akasema, Kwa taya ya punda chungu juu ya chungu, Kwa taya ya punda nimepiga watu elfu.”

Vilevile Mungu alipomuinua Eliya dhidi ya manabii wa baali Mungu alimpa Eliya uwezo utokao juu ulioweza kudhihirisha nguvu za Mungu aliye hai na kuwafanya watu waliokuwa wanasita sita kumgeukia Mungu na kurejea kwake 1Wafalme 18:21-40, Pia Paulo mtume alikutana na Elima yule mchawi kule Cyprus Matendo 13:6-12 na Daniel aliweza kuonekana kuwa mwenye majibu katika serikali ya Nebukadreza na Belshaza kuliko wanajimu na wachawi kwa sababu Roho Mtakatifu alikuwa juu yake

Kwa hiyo unaweza kuona ni hatari na aibu kubwa kwenda bila uwezo utokao juu, kanisa tunapaswa kumuomba Mungu wakati wote na kuhakikisha kuwa wakati wote tunajaa nguvu za Mungu, kwaajili ya usalama wetu, na kwaajili ya kuthibitisha uwepo wa Mungu na kukabiliana na nguvu za kipinzani, Roho Mtakatifu ni ahadi ya Mungu, ahahdi za Mungu zimehakikishwa, na Mungu ni mwaminifu katika ahadi zake, yeye huliangalia neno lake ili aweze kulitimiza ni muhimu kwetu kuhakikisha kuwa kama kuna jambo la Muhimu la kuliombea ni kujaa Roho Mtakatifu, Nguvu hizi ndio silaha yetu ya ushindi wakati wa upinzani, kazi ya Mungu ina vita katika ulimwengu wa roho, ziko protoko za kipepo zinazoshindana na injili na watenda kazi wote kwa hiyo ni muhimu kukumbuka  na kumkumbusha Mungu atupe neema hii tusiende bila uwezo utokao juu, nguvu hii ni moja ya silaha muhimu katika vita zetu za rohoni!

2Wakorintho 10:3-4 “Maana ingawa tunaenenda katika mwili, hatufanyi vita kwa jinsi ya mwili; (maana silaha za vita vyetu si za mwili, bali zina uwezo katika Mungu hata kuangusha ngome;)

Unaona iko vita katika ulimwengu wa roho, haionekani katika macho ya kawaida lakini wakati mwingine hujitokeza katika ulimwengu wa mwili asili ya kila kitu ni rohoni, hivyo lazima tuwe hodari katika Bwana na katika uwezo wa nguvu zake kwa kuvaa silaha zote mojawapo ikiwa nimkusali katika Roho, tunawezaje kufanya hivyo lazima tuwe pia tumevikwa uwezo kutoka juu ona

Waefeso 6:10-18 “Hatimaye, mzidi kuwa hodari katika Bwana na katika uweza wa nguvu zake. Vaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kuzipinga hila za Shetani. Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho.  Kwa sababu hiyo twaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kushindana siku ya uovu, na mkiisha kuyatimiza yote, kusimama. Basi simameni, hali mmejifunga kweli viunoni, na kuvaa dirii ya haki kifuani, na kufungiwa miguu utayari tupatao kwa Injili ya amani; zaidi ya yote mkiitwaa ngao ya imani, ambayo kwa hiyo mtaweza kuizima mishale yote yenye moto ya yule mwovu.  Tena ipokeeni chapeo ya wokovu, na upanga wa Roho ambao ni neno la Mungu; kwa sala zote na maombi mkisali kila wakati katika Roho, mkikesha kwa jambo hilo na kudumu katika kuwaombea watakatifu wote;”

Usiende bila uwezo utokao juu, wanafunzi wa Yesu walimuelewa Bwana na walikaa katika maombi katika chumba cha juu pale Yerusalem wakafunga na kuomba kwa siku kumi, siku ya 50 Pentekoste Roho Mtakatifu alikuja juu yao na kuwafanya kuwa na ujasiri, watu ambao awali walikuwa wakijifungia kwa hofu ya wayahudi, sasa walikuwa tayari kukabiliana na kila aina ya upinzani wakivikwa ujasiri na wakaipeleka injili kwa ujasiri bila kujali mazingira magumu waliyokutana nayo. Injili hiiambayo kanisa limeipokea duniani kote hata leo, ilitokana na kanisa la kwanza kuzingatia sana swala zima kuhusu ujazo wa Roho Mtakatifu, endapo tutafuata nyao zao kanisa halitakuwa na kitu cha kupoteza! Injili itawafikiwa watu, maisha ya watu yatabadilishwa na hakutakuwa na utata kwa miujiza inayofanywa chini ya utendaji wa Mungu mwenyewe, ukomavu wa wakristo na watumishi wa Mungu utaonekana na matunda ya Roho Mtakatifu yataonekana katika maisha yetu ya kila siku! Asante kwa kufuatilia mafundisho yangu uongezewe neema kumbuka usiende bila uwezo utokao juu!

Na Rev. Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni