2Nyakati 13:5 “je!
Haikuwapasa kujua ya kwamba Bwana, Mungu wa Israeli, alimpa Daudi ufalme juu ya
Israeli milele, yeye na wanawe kwa agano la chumvi?”
Utangulizi:
Ni
muhimu kufahamu kuwa Chumvi ni moja ya madini muhimu sana duniani, na kuwa chumvi
ina matumizi mengi na makubwa zaidi ya kunogesha ladha ya chakula, Chumvi
imekuwa ikitumika katika jamii na tamaduni mbalimbali duniani kwa matumizi
mengi tofauti tofauti, Neno Mshahara kwa kiingereza ni “SALARY” inasemekana
neno hili chimbuko lake ni neno “Salt – Money” likimaanisha
fedha inayostahili hela ya chumvi kwa askari wa kirumi, yaani malipo ya
mshahara yalikuwa ni kwaajili ya kununulia chumvi, Kutokana na umuhimu wa
chumvi katika nyakati hizo!
Chumvi
ilitumika nyakati za zamani kumaanisha urafiki wa kudumu, au kutimiza ahadi
miongoni mwa watu na kwa wayunani (Greeks)
waliihesabu chumvi kuwa ina asili ya uungu, Katika tamaduni za kiarabu hata
sasa endapo watu wawili walipatana jambo walijiapiza na kulamba chumvi
wakimaanisha ni patano la kulindana milele, ni ishara ya uaminifu wa kudumu na
hata kama ikitokea kuwa wamekuwa maadui au walikuwa maadui walipaswa kuheshimu
kulindana huko endapo walifanya patano au agano la chumvi.
Nyakati
za agano la kale walipofanya agano la patano katika ya mtu na mtu mapatano hayo
yaliweza kuthibitishwa na kulamba chumvi mbele ya mashahidi na tendo hili
lingemaanisha kuwa ni patano la kudumu, Ahadi ya kudumu milele, ahadi isiyoweza
kuvunjika na kama mtu ataivunja aharibikiwe vibaya na kupata madhara makubwa
sana.
Kwa
msingi huo unapoona katika maandiko 2Nyakati 13:5 “je!
Haikuwapasa kujua ya kwamba Bwana, Mungu wa Israeli, alimpa Daudi ufalme juu ya
Israeli milele, yeye na wanawe kwa agano la chumvi?” Mfalme Abiya Hapa alikuwa akizungumza na Israel na Yeroboamu
kuwaonya wasipigane naye na kuwajulisha kuwa Mungu yuko Pamoja na ufalme wa
agano na Daudi kwa sababu lilikuwa ni agano la chumvi, Abiya aliwathibitishia
Israel kuwa watapigwa Na kamwe hawataweza kushindana na ufalme wa ukoo wa Daudi
kwa vile ana agano la chumvi na Mungu, akimaanisha agano thabiti, lisiloweza
kubatilika la ahadi ya Mungu aliyoiweka kwa Daudi na uzao wake milele na kwamba
hakuna mtu anaweza kuiharibu.
Nyakati
za agano la kale maandiko yaliamuru kila aina ya sadaka za mbegu na nafaka
ziambatanishwe na chumvi ili kufanya “agano la chumvi”
kila aina ya sadaka ya nafaka iliambatanishwa na chumvi angalia
Mambo ya walawi 2:13 “Tena,
kila toleo la sadaka yako ya unga utalitia chumvi; wala usiiache sadaka yako ya
unga kupungukiwa na chumvi ya agano la Mungu wako; utatoa chumvi pamoja na
matoleo yako yote.”
Aidha
Mungu alipowachagua wana wa walawi kuwa makuhani wake kwa vile hawakuwa na
urithi Mungu aliwapatia chakula kupitia sadaka zilizoletwa na watu wake na
jambo hili Mungu aliliita “Agano la Chumvi”
Hesabu 18:19 “Sadaka
zote za kuinuliwa za vitu vitakatifu, wana wa Israeli wavisongezavyo kwa Bwana,
nimekupa wewe na wanao na binti zako pamoja nawe, ni haki yenu ya milele; ni
agano la chumvi la milele mbele za Bwana kwa ajili yako, na kizazi chako pamoja
nawe.”
Hapa
Mungu alikuwa anamaanisha kuwa patano hilo au agizo hilo ni la kudumu na
halitaweza kubatilishwa ni agano la chumvi! Vilevile ukuhani wake na kabila ya
lawi ni wa milele. Kwa msingi huo utaweza kuona kuwa wzo kuhusu chumvi lilipewa
umuhimu mkubwa sana katika maandiko, Leo chumvi inapatikana kwa urahisi katika
tamaduni nyingi ikiwa na umuhimu uleule japo inaweza isihitajike sana katika
uhifadhi kutokana na teknolojia ya kuwepo kwa mafriji majumbani, lakini nyakati
za Biblia chumvi ilikuwa na umuhimu mkubwa sana kwaajili ya kutunzia vitu
visiharibike kama tu ilivyokwa mafriji leo, na ndio maana utaweza kuona katika
mifano ya Yesu aliwataja wanafunzi wake au kanisa kuwa ni chumvi ya ulimwengu
akimaanisha vilevile kuwa usalama wa ulimwengu unategemea sana uwepo wa kanisa
ili kuutunza usiharibiwe na uovu
Mathayo 5:13 “Ninyi
ni chumvi ya dunia; lakini chumvi ikiwa imeharibika itatiwa nini hata ikolee?
Haifai tena kabisa, ila kutupwa nje na kukanyagwa na watu.” Kwa
msingi huo neno la Mungu linapozungumzia kuhusu agano la chumvi linazungumzia
katika uelewa kuwa ni uaminifu wa Mungu katika kutunza ahadi zake kwa mwanadamu
bila kuvunjia, ni tabia ya Mungu kuendelea kuwa mwema hata katika mazingira ya
udhaifu wa kibinadamu yeye anabaki kuwa mwaminifu.
Chumvi inahusishwa na umilele
Chumvi
imekuwa ikijulikana tangu zamani kuwa inauwezo wa kutunza vitu visiharibike,
ina uwezo wa kulinda, na inawezekana Mungu aliamuru matumizi ya chumvi katika
kutunza nyama ili isiharibike idumu lakini iwe na ladha na hivyo chumvi ilikuwa
kitu cha thamani kwa makuhani ambao waliishi kwa kuitegemea sadaka za kila siku.
Wazo la agano la
Chumvi linabeba uthamani mkubwa kutokana na uwezo wake wa kutunza kitu kwa muda
mrefu na wa kudumu bila kuharibika, Nyakati za Biblia na mpaka wakati wa Kristo
Chumvi ilikuwa ni bidhaa ya thamani kubwa sana, Na kwa msingi huo ndio maana
utaweza kuona Yesu akiwaambia wanafunzi wake kuwa ninyi ni “Chumvi ya ulimwengu” akimaanisha kuwa
watu waliomuamini Yeye wanathamani kubwa sana Duniani kwaajili ya kuitunza na
kuishawishi dunia kuishi katika haki sawa na injili yake aidha Yesu alitaka
kuonyesha kuwa wanafunzi wake wanapaswa kuwa watu watakaodumu na ambao ni
vigumu kuharibiwa!
Mathayo 5:13 “Ninyi ni
chumvi ya dunia; lakini chumvi ikiwa imeharibika itatiwa nini hata ikolee?
Haifai tena kabisa, ila kutupwa nje na kukanyagwa na watu.”
Yesu hatarajii
awaye yote ambaye amemuamini aharibike na kufikia hatua ya kushindwa kabisa
kuwa ladha kwa ulimwengu, Chumvi yenyewe ni ngumu sana kuharibika lakini
vilevile hufanya vitu vingine visiharibike, chumvi inadumu, chumvi inazuia
uharibifu, chumvi inaleta ladha, chumvi ni tiba inaleta uponyaji, chumvi
inadumisha, ingawa tuna namna nyingine nyingi leo za kuzuia vitu visiharibike
lakini bado chumvi imekuwa ni njia bora na ya kale zaidi ya kuhifadhi vitu
visiharibike. Kwa msingi huo unapozungumza chimvi unazungumzia kudumu milele na
kutokuharibiwa!
Chumvi pia
katika mafundisho ya Yesu Kristo ilihusika kumaanisha agano la amani na watu
wote, kwamba tuwe na moyo wa chumvi ndani yetu kwa kuwa na amani sisi kwa sisi,
kuwa na uhusiano usioharibika, Kristo anatarajia kuwa wanafunzi wake watakuwa
watu wenye amani ya kudumu na isiyoweza kuharibika kwa namna yoyote, kwa msingi
huo kwa Mungu anashangaza sana pale wanafunzi wake wanapoharibu mahusiano,
wanapokuwa na bifu la kudumu, wanaposhindwa kusameheana wanaposhindwa kupatana
na wanaposhindwa kuwa na amani wao kwa wao na hata ndoa ya kikristo kuvunjika
pia ni sawa na chumvi kuharibika ni jambo baya ambalo kimsingi ni jambo
lisilotarajiwa litokee!
Marko 9: 50 “Chumvi ni
njema; lakini chumvi ikiwa si chumvi tena, mtaitia nini ikolee? Mwe na chumvi
ndani yenu, mkakae kwa amani ninyi kwa ninyi”
Hivyo chumvi ni
agano la Amani chumzvi haitarajiwi kuharibika hcumvi haitarajiwinkutikufaa tena
chumvi haitarajiwi kuruhusu uharibifu.
AGANO LA CHUMVI.
Neno agano la
chumvi limejitokeza mara tatu katika maandiko, huenda inamaanisha kuhusu utatu,
kwa maana nyingine linamuhusisha Mungu, Ukiacha andiko la Msingi sehemu
nyingine ni
Hesabu 18:19 “Sadaka zote za
kuinuliwa za vitu vitakatifu, wana wa Israeli wavisongezavyo kwa Bwana,
nimekupa wewe na wanao na binti zako pamoja nawe, ni haki yenu ya milele; ni
AGANO LA CHUMVI LA MILELE mbele za Bwana kwa ajili yako, na kizazi chako pamoja
nawe.”
Na
utaweza kuona tena katika Walawi 2:13 “Tena,
kila toleo la sadaka yako ya unga utalitia chumvi; wala usiiache sadaka yako ya
unga kupungukiwa na chumvi ya agano la Mungu wako; utatoa chumvi pamoja na
matoleo yako yote.”
Mungu
alifanya maagano kadhaa na watu wake mbalimbali akitumia alama mbalimbali
muhimu za kupita kawaida.
·
Agano la Mungu na Nuhu lilihusisha upinde wa
Mvua.
Mwanzo 9:15-17 “nami
nitalikumbuka agano langu, lililoko kati yangu na ninyi, na kila kiumbe hai
katika wote wenye mwili, wala maji hayatakuwa gharika tena kuwaharibu wote
wenye mwili. Basi huo upinde utakuwa winguni; nami nitauangalia nipate
kulikumbuka agano la milele lililoko kati ya Mungu na kila kiumbe hai katika
wote wenye mwili kilichoko katika nchi. Mungu akamwambia Nuhu, Hii ndiyo ishara
ya agano nililoliweka kati yangu na wote wenye mwili walioko katika nchi”.
·
Agano la Mungu na Ibrahimu lilihusisha Nyota na
tohara ya govi
Mwanzo 15:5, 18 “Akamleta
nje, akasema, Tazama sasa mbinguni, kazihesabu nyota, kama ukiweza kuzihesabu.
Akamwambia, Ndivyo utakavyokuwa uzao wako.”, Siku ile BWANA akafanya agano na
Abramu, akasema, Uzao wako nimewapa nchi hii, kutoka mto wa Misri mpaka huo mto
mkubwa, mto Frati,”
Matendo 7:8 “Akampa
agano la tohara; basi Ibrahimu akamzaa Isaka, akamtahiri siku ya nane. Isaka
akamzaa Yakobo. Yakobo akawazaa wale kumi na wawili, wazee wetu.”
·
Agano la Mungu
na wana wa Israel kupitia Musa lilihusisha amri kumi katika Mawe.
Kutoka 34:28 “Naye alikuwa huko pamoja na BWANA
siku arobaini na masiku yake; hakula chakula, wala hakunywa maji. Naye
akaandika katika hizo mbao, hayo maneno ya maagano, hizo amri kumi.”
·
Agano la Mungu na Mfalme Daudi lilihusisha
Chumvi.
2Nyakati 13:5 “je!
Haikuwapasa kujua ya kwamba Bwana, Mungu wa Israeli, alimpa Daudi ufalme juu ya
Israeli milele, yeye na wanawe kwa agano la chumvi?”
Makusudi makubwa ya somo
hili ni kuzungumzia agano hili la chumvi na matumizi ya chumvi katika maeneo
mbalimbali ya kiibada kama tunavyoweza kuona katika siku za karibuni kukiwa na
matumizi makubwa sana ya chumvi maarufu kama chumvi ya upako!
Matumizi ya Chumvi.
Kwaajili ya kuleta ladha – Chumvi inatumika
katika kuleta ladha na utamu katika chakula au kinywaji au kitu kingine kwa
kuchanganya na chumvi na kuleta ladha
Kwaajili ya Kutunza – Chumvi inatumika
kuhifadhi na kutunza nyama na samaki na kadhalika visioze
Kwaajili ya tiba – Chumvi hutumika
kukausha, kuandaa kwaajili ya kutunza kitu kisiharibike, kwa kusafishia na
kutakasa.
Kwaajili ya uwiano – ukiizidisha
hainogi, ukiipunguza hainogi ni mpaka iwekwe kwa kiwango chenye kuwiana
Umuhimu wa chumvi katika maisha ya Ukristo.
Mathayo 5:13a “Ninyi ni chumvi ya ulimwengu”
hii ina maana gani, Biblia inatufundisha sisi tuliomuamini Kristo kwamba
tunapaswa kuwa chumvi ya ulimwengu, tupo hapa duniani kwa wakati kuhakikisha
kuwa tunautunza ulimwengu uliooza kwa dhambi
na kuuponya kutoka katika chuki dhidi ya Mungu na mambo ya Mungu.
Sifa halisi za Chumvi na maana zake
za kiroho.
Huwezi kuila Chumvi peke yake!
Jaribu
kuchukua kijiko kimoja cha chumvi kisha dumbukiza mdomoni kwako, hutaweza
kuimeza, Chumvi haiko kwaajili ya kuliwa yenyewe ni lazima uiweke katika kitu
kingine ili uweze kuitumia pamoja na kitu hicho, Ni lazima uitumie chumvi kwa
kiwango sahihi yaani kinachotosha kulingana na kitu unachokula na hapo ndipo
unapoweza kukifurahia, ukiweka kidogo hutaweza kufurahia na ukizidisha
utapoteza ladha lazima itumiwe vizuri kwa uwiano sahihi. Biblia inasema katika
Wakolosai 4:6 “Maneno yenu yawe na neema siku zote,
yakikolea munyu, mpate kujua jinsi iwapasavyo kumjibu kila mtu.”
Maneno
yetu kukolea munyu yaani chumvi maana yake kujawa na kiasi, kuzungumza kwa
upendo, Kufanya mambo yote tukiongozwa na upendo Maisha ya Ukristo yasipojawa
na upendo yanakuwa hayana maana hata kama tumeajaliwa kila kitu 1Wakoritho 13:1 “Nijaposema kwa lugha za wanadamu na za malaika,
kama sina upendo, nimekuwa shaba iliayo na upatu uvumao.”
Kama
watu tuliookolewa kwa damu ya Yesu tunapaswa kuwa na ushuhuda, kwa hivyo maneno
yetu ni mojawapo ya maneneo ambayo watu wasiookolewa hutafuta kutushambulia,
wanasema kuwa tunapowazungumzia kuhusu neno la Mungu, tunawahukumu, Hatupaswi
wakati wote tu kuhukumu mambo, kwani wakati tunapoonekana kuihukumu dhambi, ni
lazima tuonyeshe kuwa tunawapenda na kwa sababu hiyo tutaweza kufanikiwa
kuwaleta kwa Yesu kwa upendo na uvumilivu wala tusijinyeshe kuwa sisi ni wema
zaidi kuliko wanadamu wa kawaida au kwa sababu ya wiokovu wetu kuwa labada sisi
hatuwezi kukosea, kimsingi duniani tunajifunza sana kwa kukosea kwa hiyo wote
tunakosea kama asemavyo Yakobo ndugu yake bwana ona
Yakobo 3:1-2 “Ndugu zangu, msiwe waalimu wengi, mkijua ya kuwa mtapata
hukumu kubwa zaidi. Maana twajikwaa sisi sote pia katika mambo mengi. Mtu
asiyejikwaa katika kunena, huyo ni mtu mkamilifu, awezaye kuuzuia na mwili wake
wote kama kwa lijamu.”
Aidha
hatuna budi kuvumiliana sisi kwa sisi, kutokana na uwezo wa chumvi kustahimili
muda mrefu duniani bila kupoteza ladha chumvi inatufundisha uwezo wa kuvumilia
na kuchukuliana
2Timothy 4:2“lihubiri neno, uwe tayari, wakati ukufaao
na wakati usiokufaa, karipia, kemea, na kuonya kwa uvumilivu wote na
mafundisho.”
Ni
muhimu kushughulika na wengine kwa busara biblia inatoa muongozo kwa mfano
namna na jinsi ya kushughulika na kiongozi katika kanisa 1Timotheo 5:1-3 “Mzee usimkemee, bali umwonye kama baba; na vijana kama
ndugu; wanawake wazee kama mama; wanawake vijana kama ndugu wa kike; katika
usafi wote. Uwaheshimu wajane walio wajane kweli kweli” unaweza
kuona kuwa kuwa chumvi kunatupasa kuhakikisha kuwa tunawaheshimu wengine,
tunakemea kwa uvumilivu, hatuwakemei wazee, tunawaheshimu wajane na kuzungumza
na wengine kama dada na kaka zetu
Aidha
wanawake pia wanapaswa kuwa makini na namna wanavyozungumza na waume zao 1Petro 3:1-2 “Kadhalika ninyi wake, watiini waume zenu;
kusudi, ikiwa wako wasioliamini Neno, wavutwe kwa mwenendo wa wake zao, pasipo
lile Neno; wakiutazama mwenendo wenu safi, na wa hofu.” Hakuna jambo
linatia maudhi kama kumsikia mwanamke akizungumza kama baharia. Biblia
inapozungumia maneno kukolea munyu au chimvi ina maanisha pia namna bora ya
uzungumzaji wa wanawake katika kutii kwao waume zao kimsingi Mungu hapendezwi
na kelele na mafarakano katika ndoa ambayo yanaweza yakasababishwa na wanawake,
ni matarajio ya kibiblia kuwa wanawake walioolewa watakuwa chumvi katika ndoa
zao
Biblia
pia inatuonya juu ya matumizi bora ya Meneno kwa maana kuwa sio vema kwetu
kuapa, kulaani au kukufuru Yakobo 5:12 “Lakini zaidi ya
yote, ndugu zangu, msiape, wala kwa mbingu wala kwa nchi; wala kwa kiapo
kinginecho chote; bali ndiyo yenu na iwe ndiyo, na siyo yenu iwe siyo, msije
mkaangukia hukumu.” Kumbe
Mungu anachukizwa sana kumsikia Mkristo akitumia maneno yasiyojaa munyu.
Maneno
yetu pia hayapaswi kuleta aibu na kuharibu ushuhuda wa Bwana wetu Yesu Tito
2:7-8 “katika mambo yote ukijionyesha wewe mwenyewe
kuwa kielelezo cha matendo mema, na katika mafundisho yako ukionyesha usahihi
na ustahivu, na maneno yenye uzima yasiyoweza kuhukumiwa makosa, ili yule
mwenye kupinga atahayarike, kwa kuwa hana neno baya la kunena juu yetu.”
Chumvi ni fundisho kwetu sisi wahubiri wa injili katika kuhakikisha kuwa
maisha yanakuwa kielelezo ambapo tutaweza kusababisha watu washindwe kutuhukumu
na kupata sababu za kupinga hawa wale ambao wako kinyume na injili.
Chumvi inaweka ladha
Wote
tunafahamu kuwa ni vigumu sana kufurahia chakula cha aina yoyote hususani mboga
kama chumvi ikikosekana kwa hiyo ili mboga ziwe tamu ni lazima chumvi iwekwe
katika uwiano husika ona Ayubu 6:6a “Je! Kitu kisicho na ladha yumkini kulika pasipo chumvi?”
ni rahisi watu kukubali ujumbe wetu wa injili ya wokovu kama ujumbe huo
utatolewa katika roho sahihi, watu wamuelewe mwokozi na mpango na makusudi ya
Mungu kabla ya kushawishika kumpokea Yesu kama Bwana na mwokozi wa maisha yao! Mahubiri
yetu, maneno yetu na matendo yetu na mafundisho yetu yajawe na ladha ya hekima
yenye kuwavutia watu kwa kuwaonjesha ile ladha ya wokovu na utamu tulio nao
katika Kristo
Chumvi hutumika kuyeyusha barafu.
Katika
nchi ambazo wakati wa baridi kunakuwa na umende ujulikanao kama snow na barafu
ambazo wakati mwingine hujikusanya hata kufikia futi sita na kadhalika mara
nyingi wamekuwa wakitumia chumvi pia katika kuyeyusha barafu ili iwe rahisi kwa
watu kupita na kuendelea na shughuli zao, kwa hivyo tunajifunza pia kuwa chumvi
ina ngubu ya kutekebisha hali joto na kuhakikisha kuwa mambo yanakuwa sawa Neno
la Mungu lina uwezo wa kuweka sawa mioyo ya watu kuliko kitu kingine chochote
Zaburi 147:16-18 “Ndiye atoaye theluji kama sufu, Huimwaga barafu yake kama
majivu, Hutupa mvua ya mawe kama makombo, Mbele ya baridi yake ni nani awezaye
kusimama? Hulituma neno lake na kuviyeyusha, Huuvumisha upepo wake, maji
yakatiririka.”
Matumizi
mazuri ya maneno yetu tunayoyatumia katika kuwajibu watu na kuzungumza nao
yanatusaidia katika kuyeyusha mioyo ya watu kwa neno la Mungu ambalo lina nguvu
ya kushughulika na watu wa kila aina na wenye mioyo migumu na wanaojihami
tunapowahubiri Mithali 15:1 “Jawabu la upole hugeuza hasira; Bali neno liumizalo
huchochea ghadhabu.”
Chumvi hutumika kama tiba.
Chumvi
pia hutumika kama sehemu ya matibabu, watu wanaitumia chumvi kuiweka kwenye
eneo la kidonda kilichotokana na kujikata, Wamisri pia waliitumia chumvi kama
tiba na pia kwenye utunzaji wa maiti ili isharibike kazi kubwa ya chumvi katika
tiba hufanya kazi ya kukausha majimaji yote na kuleta ukavu, Neno la Mungu
linauwezo wa kukausha dhambi katika maisha ya watu, Roho Mtakatifu anaweza
kuondoa mambo yasiyofaa katika maisha yetu
na kumfanya mtu kuwa kiumbe kipya
2Wakorintho 5:17 “Hata imekuwa, mtu akiwa ndani ya Kristo amekuwa kiumbe
kipya; ya kale yamepita tazama! Yamekuwa mapya.”
Endapo
kuna eneo katika maisha yako linakupa changamoto na unapambana kubadilika
ushindi wako unathibitishwa kupatiana kwa neno la Mungu, kila kitu uvutaji wa
sigara, masengenyo, wivu, uchungu, kiburi, na kadhalika Mungu yuko tayari kutoa
msaada na amini ya kuwa atakusaidia.
Maisha ya Mwanadamu ni chumvi.
Unapojaribu
kuonja kila aina ya majimaji yanayotoka kwenye mwili wa mwanadamu yana ladha ya
chumvi chumvi, chumvi inatufundisha kuwa Mungu Roho Mtakatifu anapokuwa ndani
ya mtu humwezesha mtu huyo kuwa na ladha nzuri katika maeneo yake yote kila
ulifanyalo katika maisha linatukuwa na ubora wenye kuleta radha kwaajili ya
utukufu wa Mungu Luka 6:45 “Mtu mwema katika hazina njema ya moyo wake hutoa yaliyo
mema, na mtu mwovu katika hazina mbovu ya moyo wake hutoa yaliyo maovu; kwa
kuwa mtu, kinywa chake hunena yale yaujazayo moyo wake.”
Maneno
yako yatakuwa yanampa Mungu utukufu, japo wako wanaoweza kuchukizwa na jambo
hili na kwao itakuwa ni kama chumvi inawekwa kwenye majeraha yao lakini neno la
Mungu ndio lilivyo
Chumvi inatufundisha kuishi maisha
ya kiasi.
Wote
tunajua pale chumvi inapozidi na tunajua vilevile chumvi inapopungua, wakristo
wameitwa kuishi maisha ya kiasi ili kila kit duniani kiwe kitamu ona
Tito 2:11-12 “Maana neema ya Mungu iwaokoayo wanadamu wote imefunuliwa;
nayo yatufundisha kukataa ubaya na tamaa za kidunia; tupate kuishi kwa kiasi,
na haki, na utauwa, katika ulimwengu huu wa sasa;”
Maisha
ya kiasi yana umuhimu mkubwa katika maeneo mengi, hata ya kiafya chumvi
ikizidishwa sana inaweza hata kusababisha magonjwa kama shinikizo la juu la
damu na kadhalika , kama maisha yetu hayana kiasi ni ngumu pia kwetu kuihubiri
injili, Maisha ya kiasi ya na umuhimu mkubwa katika afya ya kimwili na kiroho,
chumvi inatukumbusha kuishi maisha ya kiasi.
Agano la Chumvi.
2Nyakati 13:5 “je!
Haikuwapasa kujua ya kwamba Bwana, Mungu wa Israeli, alimpa Daudi ufalme juu ya
Israeli milele, yeye na wanawe kwa agano la chumvi?”
Agano ni patano
linalofanywa baina ya watu wawili, huku kila upande ukiahidi kuwa mwaminifu kwa
mwingine, agano ni tofauti na mapatano, ni tofauti na kiapo, ni tofauti na
nadhiri, kwa vile agano huwa linamuhushisha Mungu mwenyewe, Hata upande wa
kibinadamu unapokuwa sio mwaminifu upande unaobaki wa Mungu unapaswa kuwa
mwaminifu katika kulitimiza agano au patano, hata pale Daudi alipokesea pamoja
na watoto wake wote ambao walishindwa kukaa katika njia yake kiasi kwamba ilikuwa Mungu awaangamize lakini
kwaajili ya agano lake na Daudi ilimpasa Mungu kuwa mwaminifu katika upande
wake ili ahadi ile isianguke,
1Wafalme
9:3-5 “Bwana akamwambia, Nimeyasikia maombi yako na
dua zako, ulizotoa mbele zangu. Nimeitakasa nyumba hii uliyoijenga ili niweke
jina langu humo milele; tena macho yangu na moyo wangu utakuwapo hapo siku
zote; na wewe, ukienda mbele zangu kama alivyokwenda Daudi, baba yako, kwa
ukamilifu wa moyo, na kwa adili, kufanya hayo yote niliyokuamuru, na kuzishika
sheria zangu na hukumu zangu, ndipo nitakapokifanya imara kiti cha ufalme wako
juu ya Israeli milele; kama nilivyomwahidia Daudi, baba yako, nikisema,
Hutakosa kuwa na mtu wa kukaa katika kiti cha enzi cha Israeli.”
Unaona Mungu
alikuwa amemuahidi Daudi akimwambia ya kuwa “HUTAKOSA MTU WA KUKAA KATIKA KITI CHA ENZI CHA ISRAEL MILELE” Agano
hili ndio linaitwa agano la chumvi, namna agano hili lilivyofanyika Nabii
Nathan au Gadi mmojawapo aliyetumwa kuleta ujumbe huu ndiye aliyemfanyia Daudi
na watoto wake wote agano la chumvi.
Jinsi
ya kufanya agano la chumvi
Wakati
wa kufanya agano la chumvi.
- Mizimu,
mapepo, shetani na wachawi na waganga au makuhani wa kichawi huwaathiri
watu katika maisha yao na kusababisha msongo wa mawazo, kwa kutumia nguvu
za giza, kwa kutumia nguvu hizo za giza na za kichawi wanawasababishia
watu kupoteza mwelekeom kuwa na bumbuwazi, kuteseka, kuelemewa, kuwa na
uzito na kupata changamoto za kifedha na kiuchumi na changamoto nyinginezo
nyingi.
Uchawi ni silaha ya giza inayotumiwa na wachawi kwa kusudi
la kuharibu maisha ya watu wanaofanikiwa na kufanikiwa katika mazingira mbalimbali, silaha hiyo ya
giza ni silaha ya kiroho lakini matokoe yake hutokea katika hali
halisi.kuteseka kwa watu waliorogwa au kuchawiwa kunategemeana na nguvu
iliyotumika katika kunuiziwa nguvu za mashambulizi
Pepo watatafasiri uchawi na manuizo na kuyawasilisha kwa
watu waliolengwa na kuwashambulia na matokeo yanaweza kutokea katika ulimwengu
wa miili yao, mambo magumu na matukio ya ajabu huanza kutiokea katika maisha
yao na njia pakee ya kuimarisha na kuleta ukombozi ni agano la chumvi
Ukombozi kupitia gano la chumvi ni rahisi sana kwa muonekano
lakini una nguvu kubwa za ajabu sana, ukombozi huu una nguvu ya kuondoa kabisa
maedhara ya nguvu zisizoonekana za kichawi na kuukausha au kuuondoa kabisa na
kuondoa hali ya kushindwa kwa sababu zozote zile, kwa kufanya hivyo haimaanishi
oia mkuwa tutaacha kabisa kuschughulikia nguvu za giza kwa namna za kawaida,
lakini tutaendelea ili kuhakikisha kuwa tunaendelea kukua kiroho.
- Unafanya gano la Chumvi wakati
gani?
Tunafanya agano la chumvi wakati tunapohisi kuwa kuna
matukio ya vita za kiroho zilizohusisha nguvu za giza, ni kweli kwamba mtu
aliyeokoka hawezi kushambuliwa na nguvu za giza kwa sababu imeandikwa hakuna
ugaga wala uchawi juu ya Yakobo Hesabu
23:23 “Hakika
hapana uchawi juu ya Yakobo, Wala hapana uganga juu ya Israeli. Sasa habari za
Yakobo na Israeli zitasemwa, Ni mambo gani aliyoyatenda Mungu!”
Lakini kumbuka tuna mashambulizi kutoka kwa mamadui, tuko
vitani, majeshi ya pepo yanatumwa kwetu kwa mauizo na sadaka za iana mbalimbali
na kwa maelekezo ya aina mbalimbali kwa hiyi kuna kiwango cha mashambulizi
ambayo tunakutana nayo wakati mwingine kwa asilimia 30 au 60 au 90 kwa hiyo
wote kwa kiwango Fulani tunashambuliwa na nguvu za giza kulingana na kiwango za
kuzaa kwetu matunda kumbuka mfano wa zile mbegu zilizoangukia kwenye udongo
mzuri Marko 4:8 “Nyingine zikaanguka penye udongo ulio mzuri, zikazaa matunda, zikimea
na kukua, na kuzaa, moja thelathini, moja sitini, na moja mia.” Kama
ukuaji wetu wa kiroho unaweza kuzaa matunda kwa asilimia hizo zilizotajwa ni
dhahiri na mashambulizia yanaweza kuwepo kutokana na kiwango kwa hiyo niia
nyepesi ya kuondoa kiwango hicho cha mashambulizi ya nguvu za giza ni kwa
kutumia ganano la chumvi na ukifanya
mara kwa mara unaziondoa kabisa katika mwili wako tunaweza kujitibu kwa agano
la chumvi mara unapohisi au kusikia changamoto hizi:-
-
Uchovu wa kimwili na kiroho
-
Kupoteza hamasa
-
Kupoteza uwezo wa kufikiri
-
Kuelemewa na mawazo
-
Hasira za kupita kawaida
-
Mgandamizo wa mawazo stresses
-
Aina yoyote ya ugonjwa na wakati wowote
unapokuwa unahisi kuwa kuna uvamizi na hali isiyo ya kawaida katika mwili wako,
uchumi wako, kazi yako, huduma yako na roho yako.
-
Lakini pia udhaifu wowowte wa kimwili,
kiroho na kihisia ujue kuna mashambulizi ya mizimu, mapepo, wachawi na
kadhalika basi unahitaji tiba ya agano la chumvi.
- Mambo unayohitaji kwaajili ya
kutekeleza agano la chumvi
-
Utahitaji ndoo au beiseni
-
Utalijaza maji safi kwa asilimia 50%
yaani nusu
-
Utahitaji chumvi yam awe kwa kiwango
chochote kana huna ya mawe unaweza kutumia ya mezani lakini ya mezani uwezo
wake utapungua kwa asilimia 30% ukilinganisha na ile ya mawe
-
Taulo la kujikaushia
-
Na sehemu ya kukanyajia
-
- Jinsi ya kufanya ibada ya agano la
chumvi.
1.
Weka maji kwenye ndoo yajae kwa
asilimia 50% yaani nusu yake kwa kiwango tu cha kufunika enka za miguu
2.
Weka vijiko vidogo viwili vya chumvi ya
mawe
3.
Omba kwa kumaanisha na kwa imani kwamba
Mungu akuondolee nguvu zote za giza, pia omba maalumu kwaajili ya kuziharibu
kabisa na kuzibomboa nguvu zote za mizimu, pepo, waganga na wachawi na kila
manuizo yaliyofanywa kinyume nawe na kukuletea athari, omba maombi ni muhimu
sana na yana uwezo mkubwa sana yanapofanyika sambaba na ibada hii ya ukombozi.
4.
Hakikisha umekaa sawa sawa na miguu
yako hususani enka ziwe zimezama katika maji, miguu yako isigusane bali iwe
mbalimbali kati ya sentimita 2-3 hii inasaidia kuodoa uchawi wote uliorogwa kwa
nguvu za giza, kama miguu yako itagusana itakuwa kikwazo kwa ibada hii,
5.
Hakikisha miguu inakaa kati ya dakika
10-15 na usizidishe zaidi ya dakika 15, ukizidisha nguvu za giza zinazotoka kwa
njia ya miguu zinaweza kuingia mwilini mwako
6.
Wakati miguu yako inapokuwa katika maji
yenye chumvi anza kuomba au kunuiza kwa jina la Yesu Mungu au kuimba maombi
7.
Wote wenye pumzi wote waishio duniani
wote wampendao (Wamchao) Mungu na waseme
fadhili zake ni za milele
8.
Wote wanaoeneza habari zake watangazao
habari njema duniani kote na waseme fadhili zake ni za milele.
Kwa
ufupi utaimba zaburi 118:1-14
1.
Haleluya. Mshukuruni Bwana kwa kuwa ni mwema, Kwa maana fadhili zake ni za
milele.
2.
Israeli na aseme sasa, Ya kwamba fadhili zake ni za milele.
3. Mlango
wa Haruni na waseme sasa, Ya kwamba fadhili zake ni za milele.
4.
Wamchao Bwana na waseme sasa, Ya kwamba fadhili zake ni za milele.
5. Katika
shida yangu nalimwita Bwana; Bwana akanijibu akaniweka panapo nafasi.
6. Bwana
yuko upande wangu, sitaogopa; Mwanadamu atanitenda nini?
7. Bwana
yuko upande wangu, msaidizi wangu, Kwa hiyo nitawaona wanaonichukia
wameshindwa.
8. Ni
heri kumkimbilia Bwana Kuliko kuwatumainia wanadamu.
9. Ni
heri kumkimbilia Bwana. Kuliko kuwatumainia wakuu.
10.
Mataifa yote walinizunguka; Kwa jina la Bwana naliwakatilia mbali.
11.
Walinizunguka, naam, walinizunguka; Kwa jina la Bwana naliwakatilia mbali.
12.
Walinizunguka kama nyuki, Walizimika kama moto wa miibani; Kwa jina la Bwana
naliwakatilia mbali.
13.
Ulinisukuma sana ili nianguke; Lakini Bwana akanisaidia.
14. Bwana
ni nguvu zangu na wimbo wangu, Naye amekuwa wokovu wangu.
Hitimisho:
Baada ya
kumaliza maombi haya ya ukombozi kulinga nan a mahitaji yako unaweza kuanza
kumshukuru Mungu kwa ulinzi wake anaokupa na namna anavyokuzunguka
Utayamwaga
maji yake chooni na kisha utasafisha ndoo na maji safi. Utakausha miguu yako
vema kwa taulo na kisha utajipaka mafuta ya mzeituni na kuomba Mungu akupeleke
kwenye kiwango kingine cha maswala mbalimbali uyatakayo. Ibada inaweza
kufanyika pia kwa makusudi mbalimbali ambayo mengine hayajaainishwa katika somo
hili mfano kuweka wakfu, kiongozi, kujilinda na cheo chako na kadhalika
Mwisho
wa ibada hii.
Matokeo:
- Athari
zote za nguvu za Giza na mashambulizi ya wachwi, waganga na mapepo na
shetani zinaondoka
- Maji
ya agano la chumvi yana nguvu kubwa sana yenyewe tu kunyonya nguvu zote za
giza
- Nguvu
za giza na magonjwa yote yanayoambatana na nguvu hizo yanaondoka na wakati
mwingine maji yanaweza kuwa na rangi nyeusi kama ishara ya kuondoka kwa
nguvu hizo, au yanaweza kuwa na uvuguvugu au yakawa na harufu mbaya hii ni
shara ya vitu vibaya kuondoka mwilini mwako
KUMBUKA.
Mafundisho haya ya katika shule za kinabii na kama imani yako inakinzana
usitilie maanani wala usifundishe kanisani kwako!
Na
Rev. Innocent Samuel Kamote
Mkuu
wa wajenzi mwenye hekima
ubarikiwe sana mwalimu na chumvi iliyondani yako ikazidi kugusa na kutia ladha katika maisha ya wengi zaidi katika jina la bwana na kuzaa matunda ili mtukufu zaaidi azidi kutukuka.
JibuFutaAmen Nakushukuru sana Matavika 95 kwa kunitia moyo mbarikiwe sana
JibuFuta