Ijumaa, 11 Agosti 2023

Kumwamini Mungu tokea Pangoni!


Zaburi 57:1-3. “Unirehemu, Ee Mungu, unirehemu mimi, Maana nafsi yangu imekukimbilia Wewe. Nitaukimbilia uvuli wa mbawa zako, Hata misiba hii itakapopita.  Nitamwita MUNGU Aliye juu, Mungu anitimiziaye mambo yangu. Atapeleka toka mbinguni na kuniokoa, Atukanapo yule atakaye kunimeza. Mungu atazipeleka Fadhili zake na kweli yake




Utangulizi:

Moja ya zaburi zenye utajiri wa kutufundisha kumuamini Mungu katika mazingira magumu na ya aina yoyote ile ni Pamoja na Zaburi hii ya 57, Kihistoria Zaburi hii iliandikwa au kutungwa katika mazingira ya wakati Daudi anamkimbia Mfalme Sauli ambaye alikuwa amekusudia kumuua kwa vile ni kijana aliyeonyesha kuwa anaweza kuwa mfalme baada ya Sauli, Daudi alikimbia katika Pango liitwalo Pango la Adulamu na watu kadhaa wakamfuata huko pamoja na ndugu zake kwaajili ya usalama wao na kulitumia pango hili kama ngome ya kujificha dhidi ya Adui zake ona

1Samuel 22:1-2 “Basi Daudi akaondoka huko, akakimbilia pango la Adulamu; na ndugu zake na watu wote wa mbari ya baba yake waliposikia habari hiyo, wakamwendea huko. Na kila mtu aliyekuwa katika hali ya dhiki, na kila mtu aliyekuwa na deni, na watu wote wenye uchungu mioyoni mwao, wakakusanyika kwake; naye akawa jemadari wao; nao waliokuwa pamoja naye walipata kama watu mia nne.”     

Unaweza kuona kwa nini maandiko yanasema Daudi akaondoka huko akakimbilia Pango la Adulamu? Sababu kubwa ni kuwa Daudi alikuwa ametiwa Mafuta ili awe mfalme baada ya Sauli kwa mapenzi ya Mungu ona

1Samuel 16:1-3 “Bwana akamwambia Samweli, Hata lini utamlilia Sauli, ikiwa mimi nimemkataa asiwamiliki Israeli? Ijaze pembe yako mafuta, uende, nami nitakupeleka kwa Yese, Mbethlehemi; maana nimejipatia mfalme katika wanawe. Samweli akasema, Nawezaje kwenda? Sauli akipata habari, ataniua. Basi Bwana akasema, Chukua ndama pamoja nawe, ukaseme, Nimekuja ili kumtolea Bwana dhabihu. Ukamwite Yese aje kwenye dhabihu, nami nitakuonyesha utakayotenda; nawe utamtia mafuta yule nitakayemtaja kwako.”

Baada ya Daudi kutiwa Mafuta ili aje kuwa mfalme baadaye uweza wa Mungu ulikuwa juu yake, Roho Mtakatifu alikuja juu ya Daudi kwa nguvu na kuanza kumtumia katika kazi zake kwa uhodari Mkubwa ona

1Samuel 16:11-13 “Kisha Samweli akamwambia Yese, Watoto wako wote wapo hapa? Naye akasema, Amesalia mdogo wao, na tazama, anawachunga kondoo. Basi Samweli akamwambia Yese, Tuma watu, wamlete; kwa sababu hatutaketi hata atakapokuja huku. Basi akatuma mtu, naye akamleta kwao. Naye alikuwa mwekundu, mwenye macho mazuri, na umbo lake lilikuwa la kupendeza. Bwana akasema, Ondoka, umtie mafuta; maana huyu ndiye. Ndipo Samweli akaitwaa pembe yenye mafuta, akamtia mafuta kati ya ndugu zake; na roho ya Bwana ikamjilia Daudi kwa nguvu tangu siku ile. Basi Samweli akaondoka, akaenda zake Rama.”

Maandiko yanatuonyesha kuwa Daudi alianza kuwa Mtu shujaa kutokana na uweza wa Mungu uliokuwa juu yake kupitia Roho Mtakatifu, aliweza kuwalinda kondoo wa Baba yake walipokuwa wakihatarishiwa maisha na Simba na dubu pamoja na wanyama wakali sana bila kujulikana ushujaa wake lakini Zaidi sana alikuja kujitiokeza kama shujaa wa kitaifa pale alipokabiliana na adui wa kutisha wa Israel aliyeitwa Goliati na kujipatia umaarufu mkubwa hata kuliko Sauli jambo lilopelekea kuanza kuwepo kwa wivu na visa vya kutaka kuuawa na Mfalme Sauli:-

1Samuel 17:49-51Daudi akatia mkono wake mfukoni, akatwaa humo jiwe moja, akalitupa kwa kombeo lake, akampiga Mfilisti katika kipaji cha uso; jiwe hilo likamwingilia kipajini, akaanguka chini kifudifudi. Hivyo Daudi akamshinda yule Mfilisti kwa kombeo na jiwe, akampiga Mfilisti, akamwua; walakini Daudi hakuwa na upanga mkononi mwake. Ndipo Daudi akapiga mbio, akasimama juu ya Mfilisti, akautwaa upanga wake, akaufuta alani mwake, akamwua, akamkata kichwa kwa upanga huo. Nao Wafilisti walipoona ya kuwa shujaa wao amekufa, wakakimbia.”

1Samuel 18:6-9 “Hata ikawa, walipokuwa wakienda, hapo Daudi aliporudi baada ya kumwua yule Mfilisti, wanawake wakatoka katika miji yote ya Israeli, kwa kuimba na kucheza, ili kumlaki mfalme Sauli; wakatoka na matari, na shangwe, na vinanda. Nao wale wanawake wakaitikiana wakicheza, wakasema, Sauli amewaua elfu zake, Na Daudi makumi elfu yake. Basi Sauli akaghadhibika sana, na maneno haya yakamchukiza; akasema, Wamempa Daudi makumi elfu, na mimi wamenipa elfu tu; kuna nini tena awezayo kupata, isipokuwa ni ufalme? Sauli akamwonea Daudi wivu tangu siku ile.”               

Ni katika mazingira kama haya sasa ndipo tangu wakati huo Daudi alianza kuwindwa na Sauli ili yamkini akipata nafasi aweze kumuua, na kwa kweli mara kadhaa Daudi alikoswa koswa kuuawa kwa mkuki kupitia  na njia nyinginezo, Sauli ambaye alikusudia kumtenda vibaya  kwa ujumla Sauli alikusudia kumuu a Daudi mara saba

1Samuel 19:10-12 “Ikawa siku ya pili yake, roho mbaya kutoka kwa Mungu ikamjilia Sauli kwa nguvu, naye akatabiri ndani ya nyumba. Basi Daudi alikuwa akipiga kinubi kwa mkono wake kama siku zote; naye Sauli alikuwa na mkuki mkononi mwake. Mara Sauli akautupa ule mkuki; maana alisema, Nitampiga Daudi hata ukutani. Daudi akaepa, akatoka mbele yake, mara mbili. Sauli akamwogopa Daudi, kwa sababu Bwana alikuwa pamoja naye, ila amemwacha Sauli.” 

Ni katika mazingira kama hayo ya kuwindwa kila wakati na kutaka kuuawa ndipo Daudi alipoanza kuishi maisha ya kuhama hama huku na kule akijificha kwaajili ya kuokoa uhai wake ndipo sa tunamuona Daudi pamoja na kundi kubwa la watu wanyonge wakimkimbilia na kumfuata naye akawa kamanda wao hii ndio sababu ya Daudi kukimbilia katika Pango la Adulamu.

Tutajifunza somo hili sasa kumwamini Mungu tokea Pangoni kwa kuzingatia vipengele vitatu vifuatavyo:-


·         Kumkimbilia Mungu wakati wa shida zetu  

·         Kumsifu Mungu wakati wa shida zetu

·         Kumwamini Mungu tokea Pangoni


Kumkimbilia Mungu wakati wa shida zetu.

Baada ya kuwa tumeona changamoto aliyokuwa akikutana nayo Daudi akitafutwa kuuawa na huku akiwa amekoswa koswa kuuawa mara saba kutoka kwa sauli, tunamuona Daudi akikimbia sasa kutoka kwa Sauli na kwenda kujificha katika Pango la Adulamu, tunaweza kujiuliza kuwa ni kwanini Daudi alifanya jambo hili? Ni ukweli ulio wazi kuwa Daudi alikuwa anatafutwa na Mfalme Sauli na Sauli hakuwa peke yake alikuwa na Jeshi kubwa la wateule yaani watu waliochaguliwa kuwa wanajeshi  wenye uzoefu mkubwa na ni hodari katika vita kwa hiyo unaweza kuona wazi kabisa kwamba Daudi alikuwa hatarini kweli kweli kwa ujumla Jeshi alilokuwa nalo Sauli lilikuwa na watu hodari wa vita wapatao elfu tatu (3000) ona  

1Samuel 24:1-2 “Ikawa, Sauli aliporudi baada ya kuwafuatia Wafilisti, aliambiwa ya kwamba, Daudi yuko katika nyika ya Engedi. Ndipo Sauli akatwaa watu elfu waliochaguliwa katika Israeli wote, akaenda kumtafuta Daudi na watu wake juu ya majabali ya mbuzi-mwitu.”

Kwa bahati mbaya Biblia ya Kiswahili ya (SUV) iliacha neno tatu kwa hiyo inasomeka kama watu hao walikuwa Elfu lakini matoleo mengine ya kiingereza likiwepo toleo la kiingereza cha KJV ambapo ndipo tafasiri ya Biblia ya Kiswahili inakotokea yanaonyesha kuwa lilikuwa jeshi la watu 3000 unaweza kuona mfano:-

NIV inaonyesha 3000 1Samuel 24:1-2 “After Saul returned from pursuing the Philistines, He was told, “David is in the Desert of Engedi. So Saul took three thousand able young men from all Israel and set out to look for David and his men near the Crags of the wild goats

KJV inaonyesha pia 3000 1Samuel 24:1-2 “And it came to pass, when Saul was returned from following the Philistines, that it was told him, saying, Behold David is in the wilderness of Engedi, then Saul took three thousand chosen men out of all Israel and went to seek David and his men upon the rocks of the wild goats

Kwa hiyo utaweza kuona mtu aliyekoswa koswa kuuawa zaidi ya mara saba na sasa anafuatiliwa na Jeshi kubwa la wanajeshi Hodari yaani makomandoo walio na mafunzo ya kivita katika Nyanja mbalimbali za kijeshi wanamtafuta Daudi ambaye alikuwa na kundi la watu wasio na mafunzo kama mia nne tu  wastani kila askari wa Daudi alikuwa na askari wa upinzani saba hivi wa kupigana nao, kwa hiyo kukimbilia Pangoni pekee kulikuwa hakutoshi wala hakukuwa salama kwa sababu wapelelezi walimueleza Sauli kila alikokimbilia Daudi na sasa Daudi anajua kuwa anapaswa kumkimbilia nani katika msiba wake Daudi alijiona kama kwamba anazungukwa na simba wakali na msaada wake ulikuwa ni Mungu tu:-

Zaburi 57:1-3 “Unirehemu, Ee Mungu, unirehemu mimi, Maana nafsi yangu imekukimbilia Wewe. Nitaukimbilia uvuli wa mbawa zako, Hata misiba hii itakapopita. Nitamwita MUNGU Aliye juu, Mungu anitimiziaye mambo yangu. Atapeleka toka mbinguni na kuniokoa, Atukanapo yule atakaye kunimeza. Mungu atazipeleka Fadhili zake na kweli yake

Daudi anatufundisha ya kuwa wakati wote tunapokutana na changamoto mbali mbali katika maisha yetu hatuna budi kumkimbilia Mungu, yeye ndiye anayeweza kuturehemu na kusaidia katika shida zetu, kukimbilia Pangoni ni sawa tu na mtu akiwa anaumwa anaweza kwenda Hospitali kwaajili ya msaada wa kawaida wa kibinadamu lakini changamoto nyingine haziwezi kutatuliwa hospitali wala haziwezi kutatuliwa na ujuzi wetu na ushujaa wetu na utaalamu wetu na elimu zetu na vyeti na kadhalika lakini neno la Mungu linatueleza wazi ya kuwa tunaweza kumkimbilia Mungu na tunaweza kulitumainia jina lake na tukawa salama, Daudi alikuwa na uelewa huo kuwa Usalama wake utatoka kwa Mungu tu na hivyo ingawa amekimbilia katika Pango la Adulamu bado anatufundisha kuwa pango pekee halitoshi kwani yuko Mungu anayeweza kutupa uvuli, anayeweza kututimizia mambo yetu anayeweza kutuokoa kwa msaada kutoka mbinguni anayeweza kupeleka fadhili zake kwa watumishi wake huyo tukimtumaini na kumkimbilia tunajihakikishia usalama wa kutosha !.

Mithali 18:10 “Jina la Bwana ni ngome imara; Mwenye haki huikimbilia, akawa salama.” Daudi anakimbilia katika lile Pango akiwa katika hali ya kuvunjika moyo amenusurika kuuawa mara saba na sasa anamkimbia Sauli, anajiona nafsi yake kuwa sasa kwa msala huu anaweza kuuawa anachukiwa mno anapingwa mno, hakuna wa kuweza kumsaidia isipokuwa Mungu peke yake, Kaka zangu na dada zangu tunapopita katika changamoto mbalimbali za maisha haya hakikisha ya kuwa unamkimbilia Mungu, mfanye yeye kuwa kimbilio lako!. Mkimbilie yeye na fungua kinywa chako kuomba mwambie nakuhitaji hakuna wa kunisaidia ila wewe Mungu katika hali yangu naye atakufanikisha.

Kumsifu Mungu wakati wa shida zetu.

Kuna nguvu kubwa sana katika kumsifu Mungu, Daudi alikuwa na ufahamu mkubwa sana wote tunajua kuwa katika maisha yake Daudi hakuwahi kushindwa vita, moja ya siri yake kubwa ya ushindi ukiacha kupakwa mafuta, ukiacha kumkimbilia Mungu, ukiacha kutafuta uso wa Mungu ili aweze kujua mapenzi ya Mungu katika kila alilokuwa anataka kulifanya  yeye alitangulia kumsifu Mungu kwa Imani akitarajia ushindi mkubwa ya kuwa Mungu atafanya kitu, hii inatufundisha kumsifu Mungu wakati wa shida zetu.

Zaburi 57:5-11 “Ee Mungu, utukuzwe juu ya mbingu, Na juu ya nchi yote uwe utukufu wako. Wameweka wavu ili kuninasa miguu; Nafsi yangu imeinama; Wamechimba shimo mbele yangu; Wametumbukia ndani yake! Ee Mungu, moyo wangu u thabiti, Moyo wangu u thabiti. Nitaimba, nitaimba zaburi, Amka, utukufu wangu. Amka, kinanda na kinubi, Nitaamka alfajiri. Ee Bwana, nitakushukuru kati ya watu, Nitakuimbia zaburi kati ya mataifa. Maana fadhili zako ni kubwa hata mbinguni, Na uaminifu wako hata mawinguni. Ee Mungu, utukuzwe juu ya mbingu, Na juu ya nchi yote uwe utukufu wako.”

Wako watu wengi sana katika maandiko ambao walipokuwa wakikabiliwa na mambo magumu walimsifu Mungu wakiwa katika shida zao na Mungu akawakomboa mfano mmojawapo ni Paulo na Sila waliomsifu Mungu wakiwa gerezani.

Matendo 16:25-28 “Lakini panapo usiku wa manane Paulo na Sila walikuwa wakimwomba Mungu na kumwimbia nyimbo za kumsifu, na wafungwa wengine walikuwa wakiwasikiliza. Ghafula pakawa tetemeko kuu la nchi, hata misingi ya gereza ikatikisika, na mara hiyo milango ikafunguka, vifungo vya wote vikalegezwa. Yule mlinzi wa gereza akaamka, naye alipoona ya kuwa milango ya gereza imefunguka, alifuta upanga, akataka kujiua, akidhani ya kuwa wafungwa wamekimbia. Ila Paulo akapaza sauti yake kwa nguvu, akisema, Usijidhuru, kwa maana sisi sote tupo hapa.”

Kumwamini Mungu tokea Pangoni.

Daudi kama tulivyojifunza ya kuwa alikuwa anakabiliwa na jeshi kubwa na zaidi ya yote alijiona kama yuko katikati ya simba kwa ujumla ukiitazama hali halisi utaweza kujua kuwa Daudi alikuwa anawindwa na kuzungukwa na hatari kubwa adui yake alikuwa Sirius sana, alikuwa amemaanisha kumua kama Sauli alijaribu kumuua Daudi mara saba na sasa anamfuatia kwa silaha kali, na Jeshi la watu 3000 ni Dhahiri kuwa alikuwa na msako mkubwa sana wa kumfanya Daudi kuwa kitu kibaya sana 

Zaburi 57:4 “Nafsi yangu i kati ya simba, Nitastarehe kati yao waliowaka moto. Wanadamu meno yao ni mikuki na mishale, Na ndimi zao ni upanga mkali.”

Daudi anakubaliana wazi kuwa adui zake walikuwa na nguvu kuliko yeye walikuwa wengi na wenye uzoefu wa vita, walikuwa na umri mkubwa kumzidi, anakumbuka alivyokuwa akikabiliana na simba huko nyikani na anakumbuka alivyoweza kupata usingizi  kati ya simba lakini kwetu sisi kama kanisa tunafahamu Simba huyu ni adui  yetu mkubwa yaani shetani.

 1Petro 5:8 “Mwe na kiasi na kukesha; kwa kuwa mshitaki wenu Ibilisi, kama simba angurumaye, huzunguka-zunguka, akitafuta mtu ammeze.”

Licha ya kuwa maadui hawa walikuwa na nguvu kama simba lakini pia ndimi zao na meno yao yaani nguvu yao ni mikuki na mishale lakini pia walikuwa wakinena maneno mabaya sana dhidi ya Daudi, kwa ujumla walikuwa ni wenye nguvu, hodari wenye silaha kali na maneno yao makali ya kutisha sana lakini pia walimtukana Daudi; Daudi alimuamini Mungu, aliamini kuwa atastarehe kati yao waliowaka moto yaani ni kama adui zake watageuka majivu tu Mungu atawafanya kuwa sio kitu, Mungu atawageuza kuwa kitu kilichoteketea na watakuwa kama mavumbi ya majivu watatoweka wote na hawatakuwako tena!, tunajifunza ya kuwa ni lazima kumwamini Mungu bila kujali unapitia hali gani, hata kama hali hiyo inatisha kiasi gani, hata kama gonjwa hilo linatisha kupita kawaida, hata kama, hata kama  afya yako haijatengemaaa mwamini Mungu ya kuwa anaweza kukusaidia na utakuwa salama atawafutilia mbali adui zako, kikla kinachosumbua katika maisha yako kitafanywa kuwa majivu katika jina la Yesu Kristo.

Hitimisho:

Zaburi hii imeandikwa wakati Daudi akiwa katika mateso ya kumkimbia mfalme Sauli na Daudi alikuwa amekimbilia huko Adulamu, na ni katika kumbukizi hii zaburi ikaandikwa, ni wakati alipokoswa koswa kuuawa mara saba. Zaburi imegawanyika katika makundi makuu mawili aya ya 1-6 anakimbilia rehema za Mungu, na kumuomba na kumlilia ili aweze kumpa msaada aya ya 7-11 Anaonyesha Imani na ujasiri na kumsifu Mungu na kumtukuza kutoka Pangoni kwa Imani akijua kuwa fadhili za Mungu ni kuu na Mungu hatampungukia, tunaweza kumsifu Mungu hata kama tumepungukiwa, hata kama ndoto zetu zinaonekana kupotea au kufifia, Daudi alikuwa amepakwa mafuta kuwa mfalme na sasa anakimbia mbali na kiti cha ufalme anaishi Pangoni mbali na nyumba ya Mungu hakutumia muda huo kulalamika lakini aliamini kuwa Mungu aliye mwema bila kujalisha yuko Mazingira gani atamtoa na kumuokoa na mwaswaibu yanayomkuta Yeye alimuamini Mungu tokea pangoni wewe unamwamini Mungu ukiwa wapi? Kwa wale wenye vita za kiroho na watu wenye wivu siku zote kumbuka kwamba kiwango cha watu wanaokupiga vita kinaonyesha ni kiwango gani cha utukufu Mungu anakupa, kama unapigwa vita na mfalme ujue wewe ni mfalme ajaye.

Na. Rev Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye hekima!

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni