Jumanne, 31 Oktoba 2023

Unapokuwa katika wakati Mgumu!


Wafilipi 4:4-7 “Furahini katika Bwana sikuzote; tena nasema, Furahini.  Upole wenu na ujulikane na watu wote. Bwana yu karibu. Msijisumbue kwa neno lo lote; bali katika kila neno kwa kusali na kuomba, pamoja na kushukuru, haja zenu na zijulikane na Mungu. Na amani ya Mungu, ipitayo akili zote, itawahifadhi mioyo yenu na nia zenu katika Kristo Yesu.”



Utangulizi:

Yesu Kristo alisema Ulimwenguni mnayo dhiki lakini jipeni moyo Mimi nimeushinda ulimwengu Yohana 16:33 “Hayo nimewaambieni mpate kuwa na amani ndani yangu. Ulimwenguni mnayo dhiki; lakini jipeni moyo; mimi nimeushinda ulimwengu.”,

Kwa kawaida tunapokuwa taabuni, yaani tunapokutana na changamoto mbalimbali katika maisha yaani ile hali ya changamoto zenye kuumiza au kukosesha Amani, au kuogopa au kuhisi kuwa umeharibu, umeshuka moyo, umeumizwa, umepotezewa Amani una msongo wa Mawazo, hasira na mashaka hali zote hizi zinatuweka katika taabu, na kwa mujibu wa Biblia tunajifunza ya kuwa tuna uwezo wa kutawala na kuchukuliana na hali hizo zote endapo tutaamua kufurahi na kujiendeleza katika tabia kujenga afya ya kukabiliana na hali zote hizi ambazo ni kikwazo cha maendeleo yetu kimwili, kiroho na kisaikolojia, maandiko yanasema tunaweza kuzitawala hali hizo. Ni katika mazingira ya wakati mgumu kama huo Mungu anatufundisha namna tunavyoweza sasa kujitawala wakati wa taabu, tutajifunza somo hili kwa kuzingatia vipengele vitatu vifuatavyo:- 

·         Agizo la kufurahi katika Bwana.

·         Mfano wa Paulo mtume kwa Wafilipi.

·         Unapokuwa katika wakati Mgumu. 

Agizo la kufurahi katika Bwana.

Wafilipi 4:4-7 “Furahini katika Bwana sikuzote; tena nasema, Furahini.  Upole wenu na ujulikane na watu wote. Bwana yu karibu. Msijisumbue kwa neno lo lote; bali katika kila neno kwa kusali na kuomba, pamoja na kushukuru, haja zenu na zijulikane na Mungu. Na amani ya Mungu, ipitayo akili zote, itawahifadhi mioyo yenu na nia zenu katika Kristo Yesu.”

Kwa kawaida ni vigumu sana kumwambia mtu afurahi hususani anapokuwa katika changamoto mbalimbali nilizoziainisha hapo juu, unawezaje kufurahi, ukiwa unapitia taabu? Nawezaje kufurahi ilihali ukweli niko taabuni sio swala jepesi, na Paulo mtume anawaagi za Wafilipi wafurahi tena kwa msisitizo, Ni muhimu kufahamu kuwa Agizo la Kufurahi kimsingi sio la Paulo Mtume, ni Agizo la kibiblia ni Agizo la Yesu Kristo Mwenyewe Paulo mtume alirejea tu kile ambacho Kristo alikuwa amekiagiza katika  injili ya Yohana 16:33  kwa kawaida unaposoma andiko hilo kidogo hususani katika lugha yetu ya Kiswahili iliyotumika kutafasiri mstari huo badala ya kujipa moyo unaweza kukata tamaa zaidi kwanini Kwa sababu Yesu au Mungu hawezi kutuambia TUJIPE MOYO Lugha hiyo ni lugha ya kibinadamu kwenda kwa mwanadamu mwenzake, Mungu hana neno JIPE MOYO hana  utakubaliana name tunapoangalia Mstari huu tena na kuungalia kwa kina ona

Yohana 16:33 “Hayo nimewaambieni mpate kuwa na amani ndani yangu. Ulimwenguni mnayo dhiki; lakini JIPENI MOYO; mimi nimeushinda ulimwengu.”,

John 16:33 “These things I have spoken unto you that in me ye might have peace. In the world ye shall have tribulation but BE OF A GOOD CHEER Ihave overcome the world

Unapoyaangalia maandiko haya katika tafasiri nyingine za kimaandiko huzusani Biblia ya kiyunani ambayo ndio Lugha ya asili iliyotafasiri agano jipya katika Kiingereza na kisha Kiswahili neno JIPE MOYO linasomeka kama  THARSEO ambalo tafasiri yake katika kiingereza ni BE OF A GOOD CHEER  yaani FURAHINI AU CHANGAMKENI  na hiki ndicho ambacho Paulo anakisema sasa kwa wafilipi katika njia ambayo sasa iko wazi zaidi kwa msingi huo sasa tafasiri halisi ya andiko hili la Yohana 16:33 ilitakiwa kuwa hivi “Hayo nimewaambieni mpate kuwa na amani ndani yangu. Ulimwenguni mnayo dhiki; lakini FURAHINI (CHANGAMKENI) (MSIOGOPE); mimi nimeushinda ulimwengu.”,

Unaona hii inakubaliana kabisa na tafasiri ya kiingreza ya Amplified Bible ambapo mstari huo unasomekaI have told you these things that in me you may have peace. In the world you have trouble; but CHEER UP! I have overcome the worldkwa msingi huo maandiko yanaagiza wakati wote kwamba tuchangamke, tusiogope tufurahi tunapioangukia katika changamoto za aina mbalimbali hili lilikuwa agizo la Bwana mwenyewe na mitume walifanya tu rejea ya mafundhisho ya Bwana, Kumbuka atakapokuja roho mtakatifu atawakumbusha yote atatwaa katika yaliyo yangu na kuwafundisha kwa hiyo agizo la kibiblia linatutaka tufurahi tunapokuwa katika taabu na majaribu ya aina mbalimbali

Yakobo 1:2-4 “Ndugu zangu, hesabuni ya kuwa ni furaha tupu, mkiangukia katika majaribu mbalimbali; mkifahamu ya kuwa kujaribiwa kwa imani yenu huleta saburi. Saburi na iwe na kazi kamilifu, mpate kuwa wakamilifu na watimilifu bila kupungukiwa na neno.”

Marko 6:46-50 “Hata alipokwisha kuagana nao akaenda zake mlimani kuomba. Na kulipokuwa jioni mashua ilikuwa katikati ya bahari, na yeye yu peke yake katika nchi kavu. Akawaona wakitaabika kwa kuvuta makasia, kwa maana upepo ulikuwa wa mbisho; hata ilipopata kama zamu ya nne ya usiku akawaendea, akitembea juu ya bahari; akataka kuwapita. Nao walipomwona anatembea juu ya bahari, walidhani ya kuwa ni kivuli, wakapiga yowe, kwa kuwa wote walimwona, wakafadhaika. Mara akasema nao, akawaambia, Changamkeni; ni mimi, msiogope.”

Kwa hiyo katika lugha halisi ya kimaandiko Neno la Mungu halijawahi kuagiza tujipe moyo na badala yake tuchangamke tusiogope na tufurahi na katika namna kama hiyo Paulo mtume anawambia Wafilipi wafurahi tena nsema furahini hivyo tunapokuwa taabuni agizo la kibiblia linatutaka tufurahi na kuchangamka, Bwana ampe neema kila mmoja wetu kuwa na uwezo wa kuchangamka anapopita katika magumu sawa na mapenzi ya Mungu katika jina la Yesu amen.

Mfano wa Paulo Mtume kwa Wafilipi.

Paulo mtume ni mfani hai unaoweza kuigwa wa jinsi na namna ya kuwa wakati unapokuwa katika wakati mgumu, yeye sio tu anawaagiza wafilipi wafurahi wakati wa changamoto, lakini yeye mwenyewe ni mfano wa kuigwa wa kushangaza wakati kanisa hilo lilipokuwa linafunguliwa, Paulo Mtume na rafiki yake Sila walipotembelea Filipi kwa mara ya Kwanza kwaajili ya kuihubiri injili, walikamatwa na kupigwa mijeledi na kuvuliwa ngyo zao mbele ya umati wa watu na kupigwa kinyama ona

Matendo 16:20-24 “wakawachukua kwa makadhi, wakasema, Watu hawa wanachafua sana mji wetu, nao ni Wayahudi; tena wanatangaza habari ya desturi zisizokuwa halali kwetu kuzipokea wala kuzifuata, kwa kuwa sisi tu Warumi. Makutano wote wakaondoka wakawaendea, makadhi wakawavua nguo zao kwa nguvu, wakatoa amri wapigwe kwa bakora. Na walipokwisha kuwapiga mapigo mengi, wakawatupa gerezani, wakamwamuru mlinzi wa gereza awalinde sana. Naye akiisha kupata amri hii akawatupa katika chumba cha ndani, akawafunga miguu kwa mkatale.”

Unapoangalia kifungu hicho unaweza kupata picha ya kuwa walikuwa katika wakati mgumu sana, wameaibishwa na wamefedheheshwa na kupigwa bakora na kufungwa kama wahalifu, wakiwa na madonda na wamewekwa gerezani katika gereza chafu, lililokuwa limechongwa juu ya kilima pale Filipi,  na kufungwa kwa mikatale maana yake bado walikuwa katika wakati mgumu, lakini mwitikio wa matukio hayo kwao na katika mioyo yao iilikuwaje? Na baada ya haya yote eti wao Paulo na sila waliokuwa katika wakati Mgumu walianza kuomba na kisha kumsifu Mungu huku wakisikilizwa na wafungwa wengine ona

Matendo 16:25-31 “Lakini panapo usiku wa manane Paulo na Sila walikuwa wakimwomba Mungu na kumwimbia nyimbo za kumsifu, na wafungwa wengine walikuwa wakiwasikiliza. Ghafula pakawa tetemeko kuu la nchi, hata misingi ya gereza ikatikisika, na mara hiyo milango ikafunguka, vifungo vya wote vikalegezwa. Yule mlinzi wa gereza akaamka, naye alipoona ya kuwa milango ya gereza imefunguka, alifuta upanga, akataka kujiua, akidhani ya kuwa wafungwa wamekimbia. Ila Paulo akapaza sauti yake kwa nguvu, akisema, Usijidhuru, kwa maana sisi sote tupo hapa. Akataka taa ziletwe, akarukia ndani, akitetemeka kwa hofu, akawaangukia Paulo na Sila; kisha akawaleta nje akasema, Bwana zangu, yanipasa nifanye nini nipate kuokoka? Wakamwambia, Mwamini Bwana Yesu, nawe utaokoka pamoja na nyumba yako.”

Kama haya yangekuwa yamenipata mimi au wewe Mungu angekuwa mahakamani, na angekula maswala makali sana tungewezaje kumsifu Mungu katika hali kama ile?  Unakumbuka wana wa Israel walipochukuliwa utumwani kule Babeli kisha waliowachukua mateka wakataka waimbe je waliweza?

Zaburi 137:1-4 “Kando ya mito ya Babeli ndiko tulikoketi, Tukalia tulipoikumbuka Sayuni. Katika miti iliyo katikati yake Tulivitundika vinubi vyetu. Maana huko waliotuchukua mateka Walitaka tuwaimbie; Na waliotuonea walitaka furaha; Tuimbieni baadhi ya nyimbo za Sayuni.  Tuuimbeje wimbo wa Bwana Katika nchi ya ugeni?

Sio rahisi kama tunavyoweza kudhani kile ambacho Mtume Paulo alikifanya na Sila wakiwa gerezani katika hali kama ile sio rahisi, wana wa Israel walishindwa walipochukuliwa mateka, na ugomzi mkubwa kweli ungekuwa kati yetu na Mungu, kwamba Mungu ee cha unafiki? Unawezaje kuacha tumevuliwa nguo, unawezaje kuacha tunacharazwa bakora, unawezaje kuacha tunapigwa na kuhukumiwa kwenda jela bila hatia? Unawezaje kuwaacha wacheza disko huko nje afu sisi wamisionari unatuacha tunateseka hivi? Alafu baadaye ndio unakuja kutikisha magereza kwa tetemeko kubwa na kuzifanya pingu ziachie zenyewe?  Lakini siri ya hekima ya Mungu ni kubwa mno unaweza kuyatukuza matendo makuu ya Mungu kama ukielewa njia zake angalia kwamba Mungu alikuwa na mpango wa kuokoa na kuliongeza kanisa la filipi kwa kumuokoa mkuu wa gereza wafungwa na familia yake

Maana yake kila linapokuja swala gumu katika maisha yetu, maswala hayo magumu yanakuja na majibu mazuri kutoka kwa Mungu, kwa msingi huo ni muhimu kuyapokea majaribu yetu kwa furaha na Amani ya Kristo, hivyo baadaye Paulo alipokuwa akiwaandikia waraka huu aliwaamuru wafilipi wafurahi katika Bwana tena wafurahi.

Unapokuwa na magumu katika maisha yako, msongo wa mawazo, kukata tamaa, kuchanganyikiwa, hofu za maisha, kazi, ndoa, watoto na kila aina ya changamoto inayokukabili katika maisha yako huipaswi kuogopa wala kukata tamaa na badala yake mtukuze Mungu, mshukur, mwambie Mungu namna unavyompenda bado chagua kufurahi wakati wa changamoto zako kwani kuchagua kufurahi maana yake ni kuchakua kumuamini Mungu na hapo Amani ya Mungu itakuwa pamoja nasi.

Unapokuwa katika wakati mgumu!

Kwa hiyo tayari tuna majibu kwamba wakati mambo magumu yanatupata tunapaswa kufurahi, lakini kwa nini tufurahi hili ni jambo muhimu sana kulijibu, kwa sababu wote tunafahamu madhara yanayosababishwa na huzuni, Huzuni ni kinyume cha furaha ni upande wa pili wa maisha kama jinsi ambavyo kuna uzima na mauti, kuchagua huzuni ni kuchagua mauti, kuchagua huzuni ni kuchagua kushindwa, kuchagua furaha ni kuchagua ushindi, kuchagua huzuni ni kurudi nyuma kuchagua furaha ni kusonga mbele, tunaweza kuutafasiri ulimwengu au maisha katima mitazamo tofauti kama tukiwa na huzuni tunaweza kufikiri kuwa hatustahili tena, tumekataliwa, hatuna bahati, mamb hayawezi kuwa, hatuwezi kusonga mbele, hatuwezi kuwa na Imani, hatuwezi kuwa na matumaini tunakuwa na hisia za kupoteza lakini kuna athari nyingi za kisaokolojia na kupoteza baadhi ya homoni katika wili wetu kama tukichagua huzuni, ndio maana maandiko yanatutaka tufurahi unaona kwa hiyo unapohhisi mambo sio mazuri

1.       Ingia katika toba, usijali kuwa umemkosea Mtu au hujamkosea mtu, umemkosea Mungu au hujamkosea Mungu lakini omba msamaha kwa Mungu.

 

2.       Omba msamaha watu wote ambao u nadhani kuwa umehitilafiana nao hakikisha kuwa uko vizuri na Mungu na wanadamu  lakini pia kama moyoni mwako kuna watu hujawasamehe samehe na au waweke mbali kabisa na maisha yako kama watu waliopoteza thamani katika maisha yako, sio kila mtu anakufaa katika maisha yako, wengine hawakufai na hivyo hupaswi kuwa nao hususani kama kuwaacha hakuleti madhara katika maisha yako

 

Waebrania 12:14 “Tafuteni kwa bidii kuwa na amani na watu wote, na huo utakatifu, ambao hapana mtu atakayemwona Bwana asipokuwa nao;”

 

 

3.       Fanya matengenezo, wakati wa mambo magumu kama tulizidiwa na maswala mbalimbali tunaweza kujikuta tuliumiza watu wengine au tulichukua mali zao au kuharibu vitu vyao au kutokuwalipa fedha zao hebu walipe

 

Luka 19:8Zakayo akasimama, akamwambia Bwana, Tazama, Bwana, nusu ya mali yangu nawapa maskini, na ikiwa nimenyang'anya mtu kitu kwa hila namrudishia mara nne”.

 

4.       Furahia siku zote na uwe mwenye mawazo chanya, Mwamini Mungu ukijua kuwa katika kila jambo Mungu hufanya mambo yote yaani mema na hata mabaya kuwapatia mema wale wampendao

 

Warumi 8:28 “Nasi twajua ya kuwa katika mambo yote Mungu hufanya kazi pamoja na wale wampendao katika kuwapatia mema, yaani, wale walioitwa kwa kusudi lake.”       

Na. Rev. Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni