Jumatatu, 16 Oktoba 2023

Unirehemu mimi, maana nafsi yangu imekukimbilia wewe!


Zaburi 57:1-3 “Unirehemu, Ee Mungu, unirehemu mimi, Maana nafsi yangu imekukimbilia Wewe. Nitaukimbilia uvuli wa mbawa zako, Hata misiba hii itakapopita. Nitamwita MUNGU Aliye juu, Mungu anitimiziaye mambo yangu.  Atapeleka toka mbinguni na kuniokoa, Atukanapo yule atakaye kunimeza. Mungu atazipeleka Fadhili zake na kweli yake” 



Utangulizi:

Hakuna jambo lililozuri kulipokea duniani kama Rehema, Kila mwanadamu anapenda kurehemiwa na ndio maana katika zaburi hii ya 57 tunamuona Daudi, akiomba rehema kwa Mungu, kwa mujibu wa historia ya kimaandiko zaburi hii ilitokana na Maisha ya Daudi nyikani wakati alipokuwa katika miaka ya kumkimbia Sauli, ambaye alikuwa anataka kumuua kwa sababu ya wivu, Daudi alikuwa akikimbia kuyaokoa maisha yake na kujificha katika mapango huko Engedi magharibi mwa pwani ya bahari iliyokufa. Ni katika mazingira ya aina hiyo yaliyokuwa magumu katika maisha ya Daudi ndio tunaona akimuomba Mungu katika zaburi hii akihitaji rehema za Mungu kwake!

1Samuel 24:1-3 “Ikawa, Sauli aliporudi baada ya kuwafuatia Wafilisti, aliambiwa ya kwamba, Daudi yuko katika nyika ya Engedi. Ndipo Sauli akatwaa watu elfu (tatu) waliochaguliwa katika Israeli wote, akaenda kumtafuta Daudi na watu wake juu ya majabali ya mbuzi-mwitu. Akafika penye mazizi ya kondoo kando ya njia, na huko kulikuwa na pango; Sauli akaingia ndani ili kuifunika miguu. Na Daudi na watu wake walikuwa wakikaa mle pangoni ndani sana.”            

Kuomba rehema za Mungu hakuhitajiki tu wakati ambapo tumetenda dhambi na tuko katika toba na basi kwaajili hiyo tunaomba Rehema Hapana hapa Daudi kuna kitu kingine cha tofauti anatufundisha kuhusu utajiri wa rehema, tunaweza kumuomba Mungu rehema hata wakati wa mapito yetu na mahitaji yetu, wote tunakumbuka ombi la Batrimayo kwa Yesu Kristo Mwana wa Daudi aliomba arehemiwe lakini kwaajili ya nini kwaajili ya ukarabati wa macho yake ili aweze kuona ona 

Luka 18:35-43 “Ikawa alipokaribia Yeriko, mtu mmoja kipofu alikuwa ameketi kando ya njia, akiomba sadaka; na alipowasikia makutano wakipita, aliuliza, Kuna nini? Wakamwambia, Yesu wa Nazareti anapita. Akapiga kelele, akisema, Yesu, Mwana wa Daudi, unirehemu. Basi wale waliotangulia wakamkemea ili anyamaze; lakini yeye alizidi sana kupaza sauti, Ee Mwana wa Daudi, unirehemu. Yesu akasimama, akaamuru aletwe kwake; na alipomkaribia, alimwuliza, Wataka nikufanyie nini? Akasema, Bwana, nipate kuona. Yesu akamwambia, Upewe kuona; imani yako imekuponya. Mara hiyo akapata kuona, akamfuata, huku akimtukuza Mungu. Na watu wote walipoona hayo walimsifu Mungu.”

Kwa hiyo tunaweza kuinua macho yetu katika mtazamo mwingine na kujifunza umuhimu wa rehema za Mungu katika maisha yetu na utaweza kufurahia mpango wa Mungu katika maisha yetu na kujua kuwa kila wakati katika changamoto yoyote tunayokutana nayo tunahitaji rehema za Mungu na zitatupa upenyo tunaouhitaji siku zote katika maisha yetu. Tutajifunza somo hili kwa kuzingatia maswala matatu muhimu yafuatayo:-

1.       Umuhimu wa rehema za Mungu

2.       Madhara  ya kukosekana kwa rehema

3.       Unirehemu maana nafsi yangu imekukimbilia wewe

Umuhimu wa rehema za Mungu.

Ni muhimu kufahamu kuwa hakuna jambo muhimu duniani Kama rehema! Rehema inapokosekana katika dunia kila kitu kinaweza kuharibika na picha la kutisha likajitokeza Duniani, kwa kuelewa umuhimu wa rehema Daudi anaomba rehema wakati akiwa anapita katika mateso na majaribu makali sana

Rehema ni nini? Neno rehema alilolitumia Daudi katika zaburi ya 57 katika biblia ya kiebrania linasomeka kama CHANAN kimatamshi Khaw-nan ambalo maana yake ni kuomba kuhurumiwa katika wakati wa mgandamizo wa mawazo, hususani wakati unapitia hali ngumu au mateso, au kuomba kuhurumiwa kutoka kwa mtu mwenye uwezo na mamlaka na nguvu ya kukuadhibu au kukudhuru, Neno hilo kwa kilatini ni Merced au merces kwa kiingereza Mercy

Daudi alihitaji rehema za Mungu wakati alipokuwa amekimbilia katika nyika ya Engedi ambayo ilikuwa na mapango mengi yeye alikuwa na watu wapatao mia sita tu wakati Sauli alikuwa akimtafuta na askari wapatao 3000 tena hawa walikuwa ni wateule yaani watu hodari na wataalamu wa vita kama ungekuwepo katika uwanja wa vita ungeweza kuona mapango kila mahali na upelelezi ulikuwa umeonyesha wazi kuwa Daudi yuko huko na hivyo Sauli alikuwa na uhakika wa kumpata na kumla nyama au kumfanya akitakacho!

Daudi alisali sala hii katika zaburi 57 Yeye alihitaji rehema alijua kuwa Mungu atatuma rehema zake na kuwa rehema hiyo hiyo ndiyo itakayomuokoa na majanga yanayomkabili, Mungu alijibu vipi Mungu alimpiga Sauli upofu yeye na majeshi yake walifanya mapumziko katika pango lilelile ambalo Daudi na watu wake walikuwa kwa ndani zaidi ona kilichojitokeza

1Samuel 24:3-6 “Akafika penye mazizi ya kondoo kando ya njia, na huko kulikuwa na pango; Sauli akaingia ndani ili kuifunika miguu. Na Daudi na watu wake walikuwa wakikaa mle pangoni ndani sana. Nao watu wa Daudi wakamwambia, Tazama, hii ndiyo siku ile aliyokuambia Bwana, Angalia, nitamtia adui yako mikononi mwako, nawe utamtenda yo yote utakayoona kuwa mema. Basi Daudi akainuka, akaukata upindo wa vazi lake Sauli kwa siri. Lakini halafu, moyo wake Daudi ukamchoma, kwa sababu amekata upindo wa vazi lake Sauli. Akawaambia watu wake, Hasha! Nisimtendee bwana wangu, masihi wa BWANA,neno hili,kuunyosha mkono wangu juu yake,kwa maana yeye ni masihi wa BWANA.”          

Unaona matokeo ya kuomba rehema yalisababisha majibu ya kushangaza Mungu alimleta Sauli katika pango lilelile alilokuwepo Daudi na tayari kulikuwa na neno la unabii ya kuwa siku moja bwana angentia Sauli mikononi mwa Daudi angalia sentensi hii - hii ndiyo siku ile aliyokuambia Bwana, Angalia, nitamtia adui yako mikononi mwako Ilikuwa wazi kabisa kuwa Mungu alikuwa ameshasema wazi kuwa Daudi afanye anachoweza kukifanya na washirika wa Daudi walimkumbusha lakini yeye aliwakataza, Daudi alikumbuka rehema, yeye alikuwa amemuomba Mungu rehema na hivyo aliziamini rehema za Mungu na fadhili za Mungu kuwa zinaweza kumlipia. Rehema ni tabia ya uungu, Daudi alionyesha ukomavu na alikuwa na ujuzi kuwa Mungu wa Ibrahimu Isaka na Yakobo ni Mungu wa rehema Biblia inasema katika Maombolezo 3:22 “Ni huruma za Bwana kwamba hatuangamii, Kwa kuwa rehema zake hazikomi.” Unaona hatuwezi kukwepa huruma na rehema za Mungu kabisa hata wakati wa majanga maana hii ndio tabia ya Mungu ndio rehema ndio jina lake kwa kweli na

Kutoka 34:5-7 “BWANA akashuka ndani ya lile wingu, akasimama pamoja naye huko, akalitangaza jina la BWANA. BWANA akapita mbele yake, akatangaza, BWANA, BWANA, Mungu mwingi wa huruma, mwenye fadhili, si mwepesi wa hasira, mwingi wa rehema na kweli; mwenye kuwaonea huruma watu elfu elfu, mwenye kusamehe uovu na makosa na dhambi; wala si mwenye kumhesabia mtu mwovu kuwa hana hatia kamwe; mwenye kuwapatiliza watoto uovu wa baba zao, na wana wa wana wao pia, hata kizazi cha tatu na cha nne.”

Bila rehema za Mungu hakuna mwanadamu angestahili kuwepo, Bila rehema za Mungu hakuna mwanadamu angeweza kuhesabiwa haki, Bila rehema za  Mungu tungeweza kuangamia, kila mmoja wetu anapaswa kukumbuka rehema, rehema zinabeba, reheema zinafungua njia, rehema za Mungu zinatutunza rehema ni uhai wetu!

Madhara ya kukosekana kwa rehema

Ni ukweli uio wazi kuwa hakuna mtu anaweza kumfikia Mungu na hata kuomba kama hakuna rehema, rehema za Mungu zingekosekana hali ya kila mtu na kila mwanadamu ingekuwa mbaya sana duniani, tunaweza kuona wakati wa agano a kale Mungu alipotaka kukaa kati kati ya wanadamu kupitia hema ya kukutania alitoa maelekezo kwa Musa kutengeneza Sanduku la agano ili ipatikane njia ya rehema za Mungu kuwafikia wana wa Israel Mungu alielekeza kuwa ni lazima kiwepo kiti cha rehema, maelekezo haya ni muhimu sana kwa sababu yanaonyesha wazi kuwa Mungu anakaa juu ya kiti cha rehema, niseme hivi ofisini kwa Mungu anapokuwa kazini na kufanya kazi zake zote kiti alichokikalia ni Rehema, bila rehema huwezi kufanikiwa kuwa na mawasiliano yoyote na Mungu.  

Kutoka 25:17-22 “Nawe fanya kiti cha rehema cha dhahabu safi; urefu wake utakuwa dhiraa mbili na nusu, na upana wake dhiraa moja na nusu. Nawe fanya makerubi mawili ya dhahabu; uyafanye ya kazi ya kufua, katika hiyo miisho ya kiti cha rehema, huku na huku. Weka kerubi moja mwisho mmoja, na kerubi la pili mwisho wa pili; fanya hayo makerubi ya kitu kimoja na kiti cha rehema, mwisho huku na mwisho huku. Na hayo makerubi yatainua mabawa yao juu, na kukifunika hicho kiti cha rehema kwa mabawa yao, na nyuso zao zitaelekeana hili na hili; nyuso za hayo makerubi zitaelekea kiti cha rehema. Weka kiti cha rehema juu ya hilo sanduku, kisha utie huo ushuhuda nitakaokupa ndani ya sanduku. Nami nitaonana nawe hapo, na kuzungumza nawe pale nilipo juu ya kiti cha rehema, katikati ya hayo makerubi mawili yaliyo juu ya sanduku la ushuhuda, katika mambo yote nitakayokuagiza kwa ajili ya wana wa Israeli.”               

Watu wa agano la kale waliweza kumfikia Mungu kupitia kiti cha rehema, Mungu ni mtakatifu mno, usafi wake na utakatifu wake unamtenga kwa wazi na kutoa sababu sahihi ya yeye kuwa mbali na wanadamu na hata akitakiwa kutokujali, lakini watu wabaya wasiokombolewa na damu ya Yesu waliweza kumfikia Mungu kwa damu za mafahari ya mbuzi na kondoo na sadaka za kuteketezwa na damu ya kunyunyizwa iliyomwaga juu ya kiti cha rehema, hii ilikuwa ni picha ya agano la kale yenye kutusaidia kufahamu umuhimu wa rehema sisi watu wa agano jipya, kuvunjwa kwa amri kumi za Mungu kukosekana kwa uadilifu kungepelekea kifo cha kila mtu lakini kabla Mungu hajaziangalia amri zake tulizozivunja anaangalia  anatuangalia sisi kupitia kiti chake cha rehema ambacho unajua wazi kuwa kwa damu ya Yesu Kristo iliyomwagiza pale msalabani tunawezeshwa kuwa na haki ya kupata rehema

Waebrania 4:14-16 “Basi, iwapo tunaye kuhani mkuu aliyeingia katika mbingu, Yesu, Mwana wa Mungu, na tuyashike sana maungamo yetu. Kwa kuwa hamna kuhani mkuu asiyeweza kuchukuana nasi katika mambo yetu ya udhaifu; bali yeye alijaribiwa sawasawa na sisi katika mambo yote, bila kufanya dhambi. Basi na tukikaribie kiti cha neema kwa ujasiri, ili tupewe rehema, na kupata neema ya kutusaidia wakati wa mahitaji.”

Unaona maandiko yako wazi kuwa sisi katika agano jipya sasa tunaweza kukaribia kiti cha rehema na kupewa rehema na neema ya kutusaidia wakati wa mahitaji yetu, kwa hiyo utakubaliana nami kuwa hatuhitaji rehema tu wakati tumefanya dhambi, lakini pia tunahitaji rehema ya Mungu wakati wa mahitaji yetu, na tunaweza kuwasiliana na Mungu pia kwa kupitia rehema,  na hivyo usishangazwe na Daudi kuomba rehema wakati akiwa anawindwa na adui au kuomba rehema akiwa vitani, zaburi yake inatufunulia wazi umuhimu mkubwa wa rehema ya Mungu na madhara makubwa ambayo yangetupata endapo Mungu angekuwa sio mwingi wa rehema! Kama sio rehema za Mungu hali ya kila mmoja wetu ingekuwa mbaya. Mungu alipokaa juu ya kiti cha rehema damu ilifunika madhaifu ya kibinadamu na kusababisha Mungu asijali wala kuruhusu hasira yake kuwaka dhidi ya wanadamu, unakumbuka ni alama ya damu katika miimo ya milango iliyowaokoa wanadamu wote waliokuwa ndani ya nyumba zilizowekwa alama ya damu bila kujali ni jinsia gani iko ndani, ni kabila gani iko ndani na nyumba zote misiri ambazo hawakuwa na alama ya damu waliangamizwa, ni alama ya damu ndio iliyomuokoa kahaba Rahabu na familia yake yote, wote waliokuwamo katika nyumba yake walisalimika kwa sababu ya alama ya damu, asante sana Yesu kuhani mkuu kama sio damu yake aliyoimwaga msalabani leo tungekuwa pabaya Yesu ndio kiti cha rehema damu yake ina nguvu, ina uwezo wa kututetea kama sio damu yake leo hii tunapoigwa kwa hukumu, kwa magonjwa, kwa laana, kwa hasira ya Mungu, kwa majini, kwa mapepo kwa wachawi kwa nguvu za giza na changamoto nyingi sio hivyo tu hata tusingeweza kusamehewa dhambi zetu pia

Waebrania 9:22-28 “Na katika Torati karibu vitu vyote husafishwa kwa damu, na pasipo kumwaga damu hakuna ondoleo. Basi ilikuwa sharti nakala za mambo yaliyo mbinguni zisafishwe kwa hizo, lakini mambo ya mbinguni yenyewe yasafishwe kwa dhabihu zilizo bora kuliko hizo. Kwa sababu Kristo hakuingia katika patakatifu palipofanyika kwa mikono, ndio mfano wa patakatifu halisi; bali aliingia mbinguni hasa, aonekane sasa usoni pa Mungu kwa ajili yetu; wala si kwamba ajitoe mara nyingi, kama vile kuhani mkuu aingiavyo katika patakatifu kila mwaka kwa damu isiyo yake; kama ni hivyo, ingalimpasa kuteswa mara nyingi tangu kuwekwa msingi wa ulimwengu; lakini sasa, mara moja tu, katika utimilifu wa nyakati, amefunuliwa, azitangue dhambi kwa dhabihu ya nafsi yake. Na kama vile watu wanavyowekewa kufa mara moja, na baada ya kufa hukumu; kadhalika Kristo naye, akiisha kutolewa sadaka mara moja azichukue dhambi za watu wengi; atatokea mara ya pili, pasipo dhambi, kwa hao wamtazamiao kwa wokovu.”

Ni damu ya Yesu pekee inayoweza na ambayo inalia kwake ili tupate rehema ndio yenye nguvu, inatupa kibali, inatupa mamlaka dhidi ya uovu inatuthibitishia usalama, inavunja vifungo vya kila aina inasafisha, inatupa uhakika wa kusamehewa na kuondolewa hatia zetu za mambo yaliyopita yaliyopo na yajayo inavunja minyororo yote na misiba na huzuni, inaondoa utumwa wa aina yoyote katika maisha yetu inawafanya majini na mapepo kutuogopa ni damu ya Yesu ndio kiti cha rehema                

Ikikosekana rehema maisha huwa na majuto  na uchungu mkubwa sana, visasi na mikasa na maisha ya uadui kati ya wanadamu kwa wanadamu yanaweza kutokea pale rehema inapokosekana, kama shetani anataka kuangamiza maisha yako moja ya njia atakayoifanya ni kuhakikisha ya kuwa unakosa Rehema, anapoitwa mshitaki wetu na kazi anayoifanya ya kushitaki ni kuhakikisha kuwa tunakosa rehema kwa Mungu alafu tunaangamizwa au kupitia machungu na hali ngumu,  ni jambo baya sana Mungu anapokubali kuacha kutuangalia kupitia rehema zake

Zekaria 11:6 “Maana mimi sitawahurumia tena wenyeji wa nchi hii, asema Bwana; bali, tazama, nitawatia, kila mmoja wao, mikononi mwa mwenzake, na mikononi mwa mfalme; nao wataipiga hiyo nchi, wala mimi sitawaokoa mikononi mwao.”

Ezekiel 7:8-9 “Basi hivi karibu nitamwaga ghadhabu yangu juu yako, nitazitimiza hasira zangu juu yako, nami nitakuhukumu sawasawa na njia zako; nami nitakupatiliza machukizo yako yote. Jicho langu halitaachilia, wala sitaona huruma; nitakupatiliza njia zako na machukizo yako yote yatakuwa katikati yako; nanyi mtajua ya kuwa mimi, BWANA, napiga.”

Unaweza kuona ulinzi wetu na usalama wetu uko katika rehema za Mungu, Rehema zikikosekana utaweza kuona tukipatilizwa, tukishughuikiwa, tukinyooshwa, ghadhabu ya Mungu itakuwa juu yetu hasira zake zitawaka, tutahukumiwa, kila njia yetu itanyooshwa, tutalipia kila dhambi, tutakosa msaaada tutakutana na machukizo, tutapigwa, tutaonewa, tutakuwa hatarini, tutatiwa mikononi mwa adui zetu, tutadhalilishwa, na kutendewa mabaya na uonevu wa kila aina kwa hiyo utakubaliana nami kuwa kuna madhara makubwa sana ikikosekana rehema! Kanisani kukikosekana rehema, waliookoka wakikosa rehema, taasisi zikikosa rehema, hospitali kukikosa rehema, shuleni na nyumbani katika ndoa ikikosekana rehema hakuna kitu kinaweza kusimama Daudi alielewa umuhimu wa Rehema akasema unirehemu ee bwana unirehemu maana nafsi yangu imekukimbilia wewe!

Unirehemu maana nafsi yangu imekukimbilia wewe

Zaburi 57:1-3 “Unirehemu, Ee Mungu, unirehemu mimi, Maana nafsi yangu imekukimbilia Wewe. Nitaukimbilia uvuli wa mbawa zako, Hata misiba hii itakapopita. Nitamwita MUNGU Aliye juu, Mungu anitimiziaye mambo yangu.  Atapeleka toka mbinguni na kuniokoa, Atukanapo yule atakaye kunimeza. Mungu atazipeleka Fadhili zake na kweli yake

Daudi alikuwa anajua anachokiomba na sio tu alikuwa akiomba rehema kwa Mungu yeye mwenyewe alikuwa mstari wa mbele kuishi kile anachokiomba, kama hujawahi kuishi maisha ya kuwa na maadui nataka nikuambie hakuna jambo baya sana duniani kama kuwa na maadui, vilevile kama hujawahi kuchukiwa nataka nikuambie hakuna jambo baya duniani kama kuchukiwa, na pia kama hujawai kuona madhara ya kisasi nataka nikujulishe kuwa hakuna jambo baya kama kulipa kisasi, Daudi alichagua rehema alijua kuwa rehema inalipa Mwanaye mkuu baadaye Yesu Kristo mwana wa Daudi alikazia wazi kuwa rehema kwa wengine inatuzalishia rehema kwa Mungu ona Mathayo 5:7Heri wenye rehema; Maana hao watapata rehema.”  Rehema inatusaidia kutokulipa mabaya kwa mabaya rehema ndio inayoongoza kusamehe, kuachilia maumivu yote, uwezo wetu wa kutokuinua mkono wetu juu ya adui zetu ndio unaoonyesha ukomavu wetu wa kiroho ni rehema, Daudi alimua kumuachia Mungu, kuhusu Sauli, alikuwa na uzoefu kuwa hata Nabali aliyemtukana matusi pamoja na kuwa alimtendea wema alitaka kumuua kwa mikono yake Mwenyewe lakini alipotulizwa na Abigaili Mungu alinyoosha mkono wake juu ya Nabali yeye mwenyewe kwa niaba ya Daudi, chochote ambacho tunataka Mungu atufanyie Yesu alionyesha kuwa Mungu anaweza kutupa kama pia tunawafanyia wengine Mathayo 6:14-15 “Kwa maana mkiwasamehe watu makosa yao, na Baba yenu wa mbinguni atawasamehe ninyi. Bali msipowasamehe watu makosa yao, wala Baba yenu hatawasamehe ninyi makosa yenu.”

Kwa lugha nyingine ili tupate rehema kwa Mungu hatuna budi kuwa na rehema kwa wanadamu wenzetu, Daudi aliifahamu siri hii, angeweza kumuua Sauli, angeweza kumdhuru kwa sababu alipewa pia neno la unabii kuwa nitamtia adui yako mikononi mwako nawe utamfanya vyovyote upendavyo hata hivyo aliamua kuchagua njia iliyobora zaidi ambayo ni Kumuachia Mungu, anapoomba rehema yeye mwenyewe alielewa kuwa anahitaji sana rehema , ndugu mpenzi msomaji wangu tunahitaji rehema sana, rehema kila mahali, katika ndoa katika malezi katika maongozi ni rehema za Mungu tu ndio maana hatuangamii kila mmoja wetu anahitaji rehema na rehema inalipa.

Mithali 11:17-18 “Mwenye rehema huitendea mema nafsi yake; Aliye mkali hujisumbua mwili wake. Mtu mwovu hupata mshahara wa udanganyifu; Apandaye haki ana thawabu ya hakika.”

Kuwa na Rehema kwa Daudi dhidi ya Sauli kulisababisha apate rehema pale alipokuja kufanya makosa makubwa, kuna benki ya rehema mbinguni, na hivyo kila mmoja wetu ajifunze kutoka kwa Daudi na kuachia rehema au kutunza rehema katika maisha yake hifadhi rehema ili baadaye uje upate faida ya rehema kutoka benki ya mbinguni, rehema ni ufunguo wa kila aina ya muujiza, tukikosa rehema tunajifungia Baraka zetu, liko gereza na taabu ya kulipia katika ulimwengu wa roho kama tumekosa rehema  ona mfano wa mtumishi asiye na rehema kuna vitu vya kujifunza

Mathayo 18:21-35 “Kisha Petro akamwendea akamwambia, Bwana, ndugu yangu anikose mara ngapi nami nimsamehe? Hata mara saba? Yesu akamwambia, Sikuambii hata mara saba, bali hata saba mara sabini. Kwa sababu hii ufalme wa mbinguni umefanana na mfalme mmoja aliyetaka kufanya hesabu na watumwa wake.  Alipoanza kuifanya, aliletewa mtu mmoja awiwaye talanta elfu kumi. Naye alipokosa cha kulipa, bwana wake akaamuru auzwe, yeye na mkewe na watoto wake, na vitu vyote alivyo navyo, ikalipwe ile deni. Basi yule mtumwa akaanguka, akamsujudia akisema, Bwana, nivumilie, nami nitakulipa yote pia. Bwana wa mtumwa yule akamhurumia, akamfungua, akamsamehe ile deni. Mtumwa yule akatoka, akamwona mmoja wa wajoli wake, aliyemwia dinari mia akamkamata, akamshika koo, akisema Nilipe uwiwacho. Basi mjoli wake akaanguka miguuni pake, akamsihi, akisema, Nivumilie, nami nitakulipa yote pia. Lakini hakutaka, akaenda, akamtupa kifungoni, hata atakapoilipa ile deni. Basi wajoli wake walipoyaona yaliyotendeka, walisikitika sana, wakaenda wakamweleza bwana wao yote yaliyotendeka. Ndipo bwana wake akamwita, akamwambia, Ewe mtumwa mwovu, nalikusamehe wewe deni ile yote, uliponisihi; nawe, je! Haikukupasa kumrehemu mjoli wako, kama mimi nilivyokurehemu wewe? Bwana wake akaghadhibika, akampeleka kwa watesaji, hata atakapoilipa deni ile yote. Ndivyo na Baba yangu wa mbinguni atakavyowatenda ninyi, msiposamehe kwa mioyo yenu kila mtu ndugu yake.”

Daudi anatufunza jambo kubwa sana kuhusu rehema, hatuna budi kumuomba Mungu na kumshihi aturehemu, kila eneo la maisha yetu lijawe na rehema na maisha yetu na kila tulifanyalo tukumbuke umuhimu wa kujawa na rehema weka rehema katika maisha ya watu ili Mungu naye akutunzie katika akaunti yako ya akiba za rehema maana ni rehema ya Mungu inayohitajika kila wakati na zaidi sana wakati wa mahitaji yetu, Bwana ampe neema kila mmoja wetu kuwa mtu aliyejaa rehema ili tuweze kupata rehema katika jina la Yesu Kristo, Amen

Rev. Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye hekima!

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni