Ijumaa, 17 Novemba 2023

Baba yangu na mama yangu wameniacha


Zaburi 27:9-11 “Usinifiche uso wako, Usijiepushe na mtumishi wako kwa hasira. Umekuwa msaada wangu, usinitupe, Wala usiniache, Ee Mungu wa wokovu wangu. Baba yangu na mama yangu wameniacha, Bali Bwana atanikaribisha kwake. Ee Bwana, unifundishe njia yako, Na kuniongoza katika njia iliyonyoka; Kwa sababu yao wanaoniotea;”




Utangulizi:

Watu wote tunaweza kuwa na ufahamu wa kutosha kuhusiana na swala zima la Umuhimu wa Baba na Mama yaani wazazi wetu na walezi wetu, kwa jinsi walivyo wa Muhimu sana Duniani, Wazazi wetu na walezi wetu wana mchango mkubwa sana na wa muhimu sana katika kutuleta Duniani na uangalifu wao mkubwa wa kuhakikisha tunapata malezi na kukua tukiwa na furaha na Amani, wao pia hujitahidi sana katika kuhakikisha wanatutimizia mahitaji yetu, wanatunza afya zetu wanaonyesha kujali na nafikiri hata kabla ya kumjua Mungu kwa kawaida tunaanza kuwajua wao, wao ni wa Muhimu sana kama hujui umuhimu wa wazazi baba na mama na walezi Hebu wapoteze siku moja ndipo utakapoingia katika wimbi la kujua uchungu wa dunia, mimi nilipoteza mama yangu nikiwa mdogo sana mpaka leo moyo wangu umejawa na majonzi makubwa mno siwezi kumkufuru Mungu kwa kutokuwepo kwake lakini wakati mwingine hata katika utu uzima huu huwa nasema laiti mama yangu angelikuwepo nadhani unaelewa! Nataka tu kuonyesha umuhimu wa watu hawa, na ndio maana Mungu katika Hekima yake anataka watu hawa wapewe heshima maalumu na ya tofauti katika maandiko na kuwa kupitia wao kunakuwa na Baraka kubwa sana katika maisha yetu ona

Waefeso 6:1-3 “Enyi watoto, watiini wazazi wenu katika Bwana, maana hii ndiyo haki. Waheshimu baba yako na mama yako; amri hii ndiyo amri ya kwanza yenye ahadi,Upate heri, ukae siku nyingi katika dunia.”

Unaona tuwapo Duniani wazazi ni nguzo ya ulinzi na usalama wa maisha yetu duniani, kama utakuwa umeishi katika nyumba ambayo baba na mama wameachana au kuna mafarakano yaliyopelekea mmoja akaondoka au ukibaki yatima unaweza kujua umuhimu wa uwepo wa wazazi ndipo sa Maandiko yanatuasa tuwaheshimu sana kwani kwa kufanya hivyo tunapata Baraka na mafanikio na kupewa uwezo wa kuishi siku nyingi duniani, Hata hivyo katika mazingira Fulani wazazi wetu wanaweza kutuacha na tukajikuta tumebaki wenyewe na ni mmoja tu anayeweza kubaki na uaminifu wake mpaka dakika ya mwisho yaani Mungu wetu wa Mbinguni, hilo ndilo ambalo Mwandishi wa zaburi anataka kutuonyesha leo:-

·         Maana  ya neno kuachwa

·         Baba yangu na mama yangu wameniacha!

·         Bali Bwana atanikaribisha kwake !

Maana ya neno Kuachwa!

Zaburi 27:9-11 “Usinifiche uso wako, Usijiepushe na mtumishi wako kwa hasira. Umekuwa msaada wangu, usinitupe, Wala usiniache, Ee Mungu wa wokovu wangu. Baba yangu na mama yangu wameniacha, Bali Bwana atanikaribisha kwake. Ee Bwana, unifundishe njia yako, Na kuniongoza katika njia iliyonyoka; Kwa sababu yao wanaoniotea;”

Ni Muhimu kufahamu kuwa neno kuachwa linalotumika hapo katika maandiko ya Kiebrania linasomeka kama  AZAB ambalo kwa kiingereza wanatumia neno FORSAKEN  Lakini kimsingi neno linalopaswa kutumika hapo ili kuleta maana inayokusudiwa ni neno ABANDONED ambalo ufafanuzi wake ni cease to support or look after someone kwa Kiswahili ni KUTELEKEZA wakati neno Forsaken ni kuacha, kwa hiyo kimsingi neno ambalo Daudi analimaanisha hapo ni KUTELEKEZWA  kwa hiyo kuachwa ni jambo lingine na kutelekezwa ni swala lingine na ni zaidi ya kuachwa!, Kama mtu aliyekuwa amejenga nyumba ya thamani sana kisha akaacha kuihudumia na kuiacha ikawa ka ma gofu au mahame!

Neno kutelekeza linatumika katika Kiswahili kumaanisha Mtu anayetegemewa kutoa msaada wa matumizi, malezi, chakula mavazi na matibabu, makazi ulinzi pamoja na mahitaji yote ya msingi anapopotea au kuacha kutoa huduma hizo au kuacha kujihusisha na wale wanaomtegemea na kuwaacha wakiwa hawana msaada. Wzazi wetu wa kiroho pia wanaweza kufanya hivyo yaani kututelekeza!

Baba yangu na mama yangu wameniacha!

Zaburi 27:9-11 “Usinifiche uso wako, Usijiepushe na mtumishi wako kwa hasira. Umekuwa msaada wangu, usinitupe, Wala usiniache, Ee Mungu wa wokovu wangu. Baba yangu na mama yangu wameniacha, Bali Bwana atanikaribisha kwake. Ee Bwana, unifundishe njia yako, Na kuniongoza katika njia iliyonyoka; Kwa sababu yao wanaoniotea;”

Kimsingi hatuna uhakika kama kuna mahali ambapo Daudi aliwahi kutelekezwa na baba yake na mama yake, Japo tunaweza tu kukumbuka tukio la Daudi kuachwa akiwachunga kondoo wa babaye wakati Samuel alipokuja kutawadha mtu atakayekuwa mfalme kutoka katika familia ya Yese ona

1Samuel 16:11-13 “Kisha Samweli akamwambia Yese, Watoto wako wote wapo hapa? Naye akasema, Amesalia mdogo wao, na tazama, anawachunga kondoo. Basi Samweli akamwambia Yese, Tuma watu, wamlete; kwa sababu hatutaketi hata atakapokuja huku. Basi akatuma mtu, naye akamleta kwao. Naye alikuwa mwekundu, mwenye macho mazuri, na umbo lake lilikuwa la kupendeza. Bwana akasema, Ondoka, umtie mafuta; maana huyu ndiye. Ndipo Samweli akaitwaa pembe yenye mafuta, akamtia mafuta kati ya ndugu zake; na roho ya Bwana ikamjilia Daudi kwa nguvu tangu siku ile. Basi Samweli akaondoka, akaenda zake Rama.”  

Hapa tunaweza tu kupata mwanga kwamba Daudi alipuuziwa ukilinganisha na ndugu zake wengine japo ukweli ni kuwa Mungu alikuja kumchagua yeye, hatuwezi kusema kuwa Daudi alitelekezwa, aidha wakati wa taabu zake alikimbia pamoja na wazazi wake na baadaye aliona ni vema akawahifadhi kwa Mfalme wa Moabu yaani kwa ndugu wa bibi yake RUTHU ambako aliwahifadhi wazazi wake kwa muda ili wasikutane na misukosuko ya kukimbia huku na huko

 1Samuel 22:3-4 “Kutoka huko Daudi akaenda Mispa ya Moabu; akamwambia mfalme wa Moabu, Tafadhali ukubali baba yangu na mama yangu watoke huko waliko, wakakae kwenu, hata nitakapojua Mungu atakalotenda kwa ajili yangu. Akawaleta mbele ya mfalme wa Moabu, nao wakakaa pamoja naye wakati wote Daudi alipokuwa ngomeni.”

Hapa pia hatuoni ushahidi wa Daudi kuachwa au kutelekezwa na Familia yake kwanini Daudi anazungumza katika zaburi hii kuwa baba yangu na mama yangu wameniacha Lakini Bwana atanikaribisha kwake ? hii ilikuwa ni lugha ya kimashairi ambayo Daudi aliitumia kutufundisha jambo kuhusu utendaji wa Mungu, Daudi anataka kuonyesha wasikilizaji wake kuwa hata pamoja na ukaribu mkubwa walio nao wazazi wetu na walezi wetu na uwezo wao na uchungu wao mkubwa wa kutuhudumia, bado Mungu anabaki kuwa msaada ulio karibu zaidi kuliko msaada wa wazazi, anataka kuonyesha kuwa utendaji wa Mungu katika maisha yetu unazidi ule  wa wazazi, kwani  wao pamoja na kujitoa kwao na kujidhabihu kwao kuna wakati wanaweza kuacha kuwa na huruma dhidi yetu lakini sivyo alivyo Bwana Mungu wetu, wale wote wanaodhani ya kuwa Mungu amewatelekeza wanapaswa kujua kuwa wazazi baba na mama wanaweza kufanya tukio hilo lakini sio ilivyo kwa Bwana Mungu wetu ona

Isaya 49:14-16. “Bali Sayuni alisema, YEHOVA ameniacha, Bwana amenisahau.  Je! Mwanamke aweza kumsahau mtoto wake anyonyaye, hata asimhurumie mwana wa tumbo lake? Naam, hawa waweza kusahau, lakini mimi sitakusahau wewe. Tazama, nimekuchora katika vitanga vya mikono yangu; kuta zako ziko mbele zangu daima.”

Na ndio maana inapotokea Mtu amepoteza mume, au amepoteza wazazi na kuwa yatima Mungu mwenyewe huchukua nafasi hiyo na kuwa mume wa wajane na baba wa yatima ona

Zaburi 68:5-6 “Baba wa yatima na mwamuzi wa wajane, Mungu katika kao lake takatifu. Mungu huwakalisha wapweke nyumbani; Huwatoa wafungwa wakae hali ya kufanikiwa; Bali wakaidi hukaa katika nchi kavu.”

Wakati wote katika maisha yetu, tunapohisi kutelekezwa, au kuachwa au kuwa peke yetu hakuna sababu ya kuumia na kuteseka tukijuliza kuwa Msaada (wokovu) wetu utatokea wapi Mungu aliye baba wa wapweke baba wa Yatima mwamuzi wa wajane atatuletea wokovu mkuu

Hosea 14:3 “Ashuru hatatuokoa; hatutapanda farasi; wala hatutaiambia tena kazi ya mikono yetu, Ninyi ndinyi miungu yetu; maana kwako wewe wasio na baba hupata rehema.”

Mungu atachukua jukumu la baba na mama au walezi kwa kila anayemuamini, ataonyesha upendo wake usiokoma  na ataonyesha kujali  katika namna ambayo mwanadamu hawezi kuifanya, kimsingi katika lugha hii kwa sababu ni ya kimashairi Daudi katika lugha ya kawaida anazungumza kuwa HATA KAMA  baba yangu na mama yangu wataniacha Mungu atachukua nafasi  na ni mwenye nafasi ya kuonyesha anajali zaidi ya ukaribu walio nao wazazi wetu  yeye hatakuja kutuacha wala kutupungukia na tunaweza kuliitia jina lake katika mazingira magumu kama hayo!, na sio baba na mama peke yao awaye yote tunayemtegemea katika maisha haya akitutelekeza Mungu aliyetuumba na aliye baba mwema anachukua jukumu kubwa la kutuweka mabegani mwake katika ulimwengu wa roho na kuonyesha kujali kuliko karibu zaidi ya mwanadamu wa kawaida

Bali Bwana atanikaribisha kwake !

Kwa kawaida Bwana hukaribisha kwake watu wa aina yoyote ile  hata wale ambao wamekataliwa kwa sababu zozote zile katika jamii, hakuna mtu mwema na mzuri sana kiasi cha kumshawishi Mungu kumkubali wala hakuna mtu mbaya sana kiasi cha kumshawishi Mungu kumkataa, yeye alisema katika neno lake kuwa yeyote ajaye kwake hatamtupa nje kamwe

Yohana 6:37 “Wote anipao Baba watakuja kwangu; wala ye yote ajaye kwangu sitamtupa nje kamwe.”

Kristo Yesu alipokuwa duniani aliwakaribisha watu wengi sana kwake hata wale waliokuwa wamekataliwa na jamii

Luka 15:1-2 “Basi watoza ushuru wote na wenye dhambi walikuwa wakimkaribia wamsikilize. Mafarisayo na waandishi wakanung'unika, wakisema, Mtu huyu huwakaribisha wenye dhambi, tena hula nao.”

Neno kukaribisha katika biblia ya kiyunani linasomeka kama neno PROSLAMBANO/PROSDECHOMAI  na kwa Kiebrania ni ASAPH  ambalo maana zake ni Kuhudumia, kukubali, kuwaangalia, kuwapokea, kuwatambua, kuwakusanya,  Wakati wote milango ya Mungu iko wazi kutukaribisha kwake na tukawa kwake watoto wake na wanae, Kuachwa kwa aina yoyote ile kutakakokupata Duniani kusikufanye wewe ukajisikia kuwa una bahati mbaya, kutelekezwa kwako kwa aina yoyote ile kusikufanye wewe ukajisikia kuwa huna thamani yuko Mungu mbinguni ambaye ndiye aliyekuumba yeye anakuthamini kuliko unavyoweza kufikiri alishatuahidi ya kuwa hatatuacha wala hatatupungukia

Yoshua 1:5 “Hapatakuwa mtu ye yote atakayeweza kusimama mbele yako siku zote za maisha yako; kama nilivyokuwa pamoja na Musa, ndivyo nitakavyokuwa pamoja na wewe; sitakupungukia wala sitakuacha.”

Zamani sana tulikuwa tunaimba Baba na mama wawezakuniacha, lakini Yesu hawezi kuniacha, Rafiki zangu waweza kuniacha lakini Yesu hawezi kuniacha!

 

Rev. Innocent Kamote.

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni