Wagalatia 4:4-5 “Hata ulipowadia utimilifu
wa wakati, Mungu alimtuma Mwanawe ambaye amezaliwa na mwanamke, amezaliwa chini
ya sheria, kusudi awakomboe hao waliokuwa chini ya sheria, ili sisi tupate
kupokea hali ya kuwa wana.”
Utangulizi:
Leo ni sikukuu ya Christmas,
wakristo wote Nchini wanaungana na wakristo wengine duniani kuadhimisha
kuzaliwa kwa Yesu Kristo kulikotokeza zaidi ya miaka 2000 iliyopita huko
Bathelehemu, Israel. Katika wakati huu ni muhimu kujikumbusha kuwa kuzaliwa kwa
Yesu Kristo hakukutokea kwa bahati mbaya kwani Kuzaliwa kwa Yesu Kristo
kulitokea kwa wakati mkamilifu, katika mpango wa Mungu, watu wengi wanaweza
wasielewe umuhimu wa Yesu kuzaliwa kwa wakati, na ikawa kwao kama watu ambao walikuwa na
shughuli nyingine wakati Yesu anazaliwa wasijue kuwa mwokozi amekuja kwaajili
yao, Kuzaliwa kwa Yesu Kristo huu
ulikuwa ni mpango kamili wa Mungu, na ulitekelezwa ulipowadia utimilifu wa
wakati, tutajifunza somo hili kwa kuzingatia vipengele vitatu vifuatavyo:-
·
Hata ulipowadia
utimilifu wa wakati!
·
Kukombolewa
kwa waliokuwa chini ya sheria
·
Kupokea
hali ya kuwa wana
Hata ulipowadia
utimilifu wa wakati.
Wagalatia 4:4-5 “Hata ulipowadia utimilifu
wa wakati, Mungu alimtuma Mwanawe ambaye amezaliwa na mwanamke, amezaliwa chini
ya sheria, kusudi awakomboe hao waliokuwa chini ya sheria, ili sisi tupate
kupokea hali ya kuwa wana.”
Neno Utimilifu wa wakati katika
Biblia ya kiyunani linasomeka kama “Pleroma - Chronos”. Pleroma ikiwa na
maana ya Kujaa kabisa, au kukamilika
completion or Filled, na Chronos ni Time
kwa hiyo utimilifu wa wakati kwa kiingereza Fullness of the time yaani
ni kama mtu aliyekuwa anakijaza chombo kwa muda maalumu, kisha kikajaa, au muda
uliokusudiwa kwa kitu Fulani kutimia, kwa hiyo Kiswahili kilichotumika hapo ni
sahihi na chepesi zaidi ya mafafanuzi sawa tu utimilifu wa wakati, Kwa hiyo
Kuzaliwa kwa Yesu Kristo hakukutokea tu kwa bahati mbaya, bali kulitoka kwa
wakati mtimilifu ambao Mungu alikuwa ameukusudia katika mpango wake!.
Huu ulikuwa ni wakati utawala wa
kiyunani ulikuwa umeisha na umeacha athari ya Lugha ya Kiyunani (Greek) na tamaduni kadhaa za kiyunani
(Hellenistic culture), Lugha hii kwa
wakati huo ilikuwa ni lugha ya kisomi na iliyotumiwa na wasomi wengi wa nyakati
zile jambo lilolopelekea Maandiko kutafasiriwa na hata kuandikwa katika
kiyunani kwani ulimwengu wa wakati huo ulikuwa ni ulimwengu wa kisomi sana na
athari zake zilikuwa zimeachwa na Wayunani.
Warumi walikuwa sasa ndio
wanaotawala ulimwengu wa wakati huo na walikuwa ni watu waliohakikisha Amani
inakuwepo kila mahali duniani, na pia waliunganisha ulimwengu wa wakati ule kwa
mifumo ya bara bara zilizorahishisha mawasiliano na ulinzi mkali uliohakikisha
Amani inatawala kila mahali duniani, utaratibu na ustawi mkubwa sana wa kijamii
(Pax Romana)
Wayahudi walikuwa na matazamio
Makali ya kutimizwa kwa unabii hususani wa Daniel kuhusu majuma sabini, na walikuwa tayari wamejiandaa kumpokea
Masihi, wakielewa wazi kuwa wakati wowote masihi atazaliwa, ili awakomboe na
kuleta faraja na kuondoa uchovu wa kukandamizwa na utumwa wa kigeni na utumwa
wa sheria
Pia ulikuwa wakati ambapo watu
wamechoshwa na kufilisika sana kiroho, wamefilisika kidini na kiimani, na
walikuwa wameshindwa kabisa kuishi sawa na sharia ya Musa ambayo kwa wakati huu
ilikuwa inaonekana kuwa ina viwango ambavyo wanadamu wa kawaida hawaviwezi,
dhambi ilikuwa imewaelemea na wanyama wa kutekeketzwa kwaajili ya dhambi
lilianza kuonekana kama jambo lisilowezekana tena
Ni katika wakati huu Ndipo Yesu
anazaliwa, anazaliwa katika wakati ambapo watu walikuwa wamefilisika kiimani,
kidini na kiuadilifu, uadui kati ya mwanadamu na Mungu ulikuwa umeongezeka
sana, kwa hiyo kuja kwa Yesu na kuzaliwa kwake kwa wakati hasa wakati ambapo
wanadamu wamechoka, ilikuwa ni kuleta auheni na unafuu mkubwa, kuleta neema na
kutangaza rehema ulikuwa ni wakati sahihi kwa wanadamu kutangaziwa wokovu ambao
wameusubiri kwa muda wakati wa kukombolewa kutoka katika laana zinazotokana na
wanadamu kushindwa kuzitii sheria za Mungu, kuelekea wazi katika adhabu ambazo
kwa ukweli hakuna mtu angeweza kulipa na
ndio katika wakati huu sasa Mungu anamleta Yesu Kristo kwaajili ya ukombozi.
Sio hivyo tu Paulo mtume
anazungumzia wakati ambapo mtoto wa kifalme ambaye alikuwa chini ya usimamizi
anapoanza kuhesabika kama mtoto wa kifalme ambaye ameiva na yuko tayari kwa
utawala na kuanza kujitegemea kutoka chini ya mwangalizi, kama ukiangalia
vizuri kwa kina katika kitabu cha Wagalatia Paulo anazungumza yafuatayo:-
Wagalatia 4:1-5 “Lakini nasema ya kuwa
mrithi, wakati wote awapo mtoto, hana tofauti na mtumwa, angawa ni bwana wa
yote; bali yu chini ya mawakili na watunzaji, hata wakati uliokwisha kuamriwa
na baba. Kadhalika na sisi, tulipokuwa watoto, tulikuwa tukitumikishwa na
kawaida za kwanza za dunia. Hata ulipowadia utimilifu wa wakati, Mungu alimtuma
Mwanawe ambaye amezaliwa na mwanamke, amezaliwa chini ya sheria, kusudi
awakomboe hao waliokuwa chini ya sheria, ili sisi tupate kupokea hali ya kuwa
wana.”
Paulo anachokizungumza hapo, ni
utaratibu uliokuwa unafuatwa katika nyumba za kifalme, ambapo mtoto wa kifalme
anapokuwa mdogo anakuwa chini ya uangalizi wa mtu maalumu anayeitwa kwa
kiyunani “EPITROPOS” yaani kwa kiingereza Domestic Manager or guardian yaani
Mwangalizi maalumu wa watoto wa kifalme nyumbani, ambaye kazi yake ni kutoa
maelekezo na kufundisha mtoto wa kifalme namna anavyotakiwa kuishi kama mfalme
maelekezo anayoyatoa yanaitwa “PEDAGOGY” yaani mafundisho na melekezo maalumu, kwa
hiyo watoto wote wa kifalme huwa chini ya watu hao wakipokea maelekezo na
mafundisho, wakielekezwa na kuamuliwa nini cha kufanya, wapi waende wapi
wasiende, wakati mwingine hufudishwa hata vita au kupelekwa jeshini na
kushiriki vita na wakati huu wanakuwa kama watumwa tu, mpaka unapofikia wakati uliokusudiwa na mfalme wawe wamefuzu Mfalme huwapangia majukumu ya
kiutawala au kuwapa majimbo ya kurithi kiutawala ili watawale pamoja naye
Kwa msingi huo basi
tunapozungumza kuhusu utimilifu wa wakati, ambao Paulo mtume anauzungumza ni
wakati ambapo Mungu alikusudia sasa wa kuwaweka watu huru kutoka katika vifungo
mbalimbali pamoja na kifungo cha sharia ya Musa (Torati), na kuwakomboa
wanadamu ambao walikuwa wanateswa na mateso ya aina mbalimbali na laana
zinazotokana na kuivunja torati sasa anazaliwa Kristo kwa wakati kwa kusuda la
kutukomboa kutoka katika hali ya utumwa.
Wagalatia 3:11-14 “Ni dhahiri ya kwamba
hakuna mtu ahesabiwaye haki mbele za Mungu katika sheria; kwa sababu Mwenye
haki ataishi kwa imani. Na torati haikuja kwa imani, bali, Ayatendaye hayo
ataishi katika hayo.Kristo alitukomboa katika laana ya torati, kwa kuwa
alifanywa laana kwa ajili yetu; maana imeandikwa, Amelaaniwa kila mtu
aangikwaye juu ya mti; ili kwamba baraka ya Ibrahimu iwafikilie Mataifa katika
Yesu Kristo, tupate kupokea ahadi ya Roho kwa njia ya imani.”
Kwa hiyo utimilifu wa wakati
unaozungumzwa hapo, kimsingi ni wakati wa kuwapa wote waliomuamini Yesu mamlaka
kamili, ya kuondoka kuwa chini ya sheria na kuwa wafanya sheria hii ni Baraka
kubwa sana kuliko zote, wakati Israel alipokuwa akiwabariki watoto wake na
kutoa unabii ya kuwa masihi yaani mtawala atatokea katika kabila la Yuda,
kabila hii ilibarikiwa pia kuwa haitakosa mfanya sheria katika miguu yake
Mwanzo 49:8-10 “Yuda, ndugu zako
watakusifu, Mkono wako utakuwa shingoni mwa adui zako. Wana wa baba yako
watakuinamia. Yuda ni mwana-simba, Kutoka katika mawindo, mwanangu, umepanda;
Aliinama akajilaza kama simba, Na kama simba mke; ni nani atakayemwamsha? Fimbo
ya enzi haitaondoka katika Yuda, Wala mfanya sheria kati ya miguu yake, Hata
atakapokuja Yeye, mwenye milki, Ambaye mataifa watamtii.”
Ni aina hii ya mamlaka,
kutumikiwa, kuwa na uweza dhidi ya adui zetu, kutumainiwa, kutokukosa mawindo,
kuogopwa, kuwa na mamlaka, kuwa wafanya sheria, hii inakuja kwa kila mtu
anayemuamini Bwana Yesu na huu ni wakati wa furaha sana kwani kristo amekuja
kutuondoa katika hali ya unyonge na kutuleta katika wakati wa kutawala na
kumiliki na kuwashinda maadui zetu, hata ulipowadia utimilifu wa wakati, Mungu
anamtangazia kila mmoja wetu kuwa umewadia utimilifu wa wakati sasa, ni wakati
wa ushindi, ni wakati wa kutawala, ni wakati wa kumiliki, ni wakati wa kuweka
huru, ni wakati wa kufurahia uhuru kutoka utumwani ni wakati wa kuondoka katika
uonevu ni wakati wa Amani na utulivu ni wakati wa ustawi, ni wakati wamkunena
kwa lugha mpya, ni wakati wa kutembea na uungu ndani yetu, wakati wa kupakwa
mafuta, wakati wa kuzungumza kwa mamlaka ya kifalme, wakati wa ushindi, wakati
wa upenyo, wakati wa kutoboa, wakati wa kuyataja yasiyokuwako kana kwamba
yamekuwako, Bwana ampe neema kila mmoja wetu kuufurahia wakati mtimilifu
uliokusudiwa kwa Baraka zake katika jina la Yesu Kristo Amen!
Kukombolewa kwa waliokuwa chini ya sharia.
Katika utimilifu huo wa wakati
Paulo mtume anaeleza kuwa moja ya sababu ya ujio wa Yesu Kristo ni kuwakomboa
wanadamu katika laana ya torati, yaani wale waliokuwa chini ya sheria, hapa
inamaanisha sharia ya Musa ambayo ki msingi inapatikana katika vitabu vitano
vya Musa, ambayo ina maelekezo yote ya namna ya kumuabudu Mungu na kumtumikia
jambo ambalo kwa ujumla halikuwa rahisi, kuivunja torati kuliambatana na
tangazo la laana kubwa na nyingi sana nzito na za kusikitisha mno angalia :-
Kumbukumbu la torati 28:15-56 “Lakini
itakuwa usipotaka kuisikiza sauti ya Bwana, Mungu wako, usiyaangalie kufanya
maagizo yake yote na amri zake, nikuagizazo hivi leo, ndipo zitakapokujia laana
hizi zote na kukupata. Utalaaniwa mjini, utalaaniwa na mashambani. Litalaaniwa
kapu lako na chombo chako cha kukandia. Utalaaniwa uzao wa tumbo lako, na uzao
wa nchi yako, maongeo ya ng'ombe wako, na wadogo wa kondoo zako. Utalaaniwa uingiapo,
utalaaniwa na utokapo, Bwana atakuletea laana na mashaka, na kukemewa, katika
yote utakayotia mkono wako kuyafanya, hata uangamie na kupotea kwa upesi; kwa
ule uovu wa matendo yako, uliyoniacha kwayo. Bwana atakuambatanisha na tauni,
hata atakapokwisha kukuondoa katika nchi uingiayo kwa kuimiliki. Bwana
atakupiga kwa kifua kikuu, na kwa homa, na kwa kuwashwa, na kwa hari ya moto,
na kwa upanga, na kwa ukaufu, na kwa koga; navyo vitakufukuza hata uangamie. Na
mbingu zako zilizo juu ya kichwa chako zitakuwa shaba, na nchi iliyo chini yako
itakuwa chuma. Bwana atafanya mvua ya nchi yako iwe vumbi na mchanga;
itakujilia juu yako kutoka mbinguni hata uangamie. Bwana atakufanya upigwe
mbele ya adui zako; utawatokea juu yao kwa njia moja, lakini utakimbia mbele
yao kwa njia saba; nawe utatupwa huko na huko katika falme zote za duniani. Na
mzoga wako utakuwa chakula cha ndege wote wa angani, na wanyama wote wa
duniani, pasiwe na mtu wa kuwafukuza. Bwana atakupiga kwa majipu ya Misri, na
kwa bawasiri, na kwa pele, na kwa kujikuna, ambayo hupati kupoa. Bwana
atakupiga kwa wazimu, na kwa upofu, na kwa bumbuazi la moyoni; utakwenda kwa
kupapasa-papasa mchana, kama apapasavyo kipofu gizani, wala hufanikiwi katika
njia zako; nawe sikuzote utaonewa na kutekwa nyara, wala hapatakuwa na mtu wa
kukuokoa. Utaposa mke na mume mwingine atalala naye; utajenga nyumba usiikae;
utapanda mizabibu usitumie matunda yake.Ng'ombe wako atachinjwa mbele ya macho
yako, usile nyama yake; utanyang'anywa punda wako mbele ya uso wako kwa jeuri,
usirudishiwe; kondoo zako watapewa adui zako, usipate mtu wa kukuokoa. Wanao na
binti zako litapewa taifa lingine, na macho yako yataangalia, na kuzimia kwa
kuwatamani mchana kutwa; wala hapatakuwa na kitu katika uwezo wa mkono wako. Matunda
ya nchi yako, na taabu yako yote, vitaliwa na taifa usilolijua; utaonewa tu, na
kupondwa chini daima; hata uwe mwenye wazimu kwa yaonwayo na macho yako,
utakayoyaona. Bwana atakupiga magoti na miguu kwa jipu lililo zito, usilopata
kupozwa, tokea wayo wa mguu mpaka utosi wa kichwa. Bwana atakupeleka wewe, na
mfalme wako utakayemweka juu yako, kwa taifa usilolijua wewe wala baba zako;
nawe huko utatumikia miungu mingine ya miti na mawe. Nawe utakuwa ushangao, na
mithali, na dharau, kati ya mataifa yote huko atakakokuongoza Bwana. Mbegu
nyingi utazichukua nje shambani, lakini utavuna haba, kwa kuwa nzige watazila. Utapanda
mizabibu na kuitengeza, wala hutakunywa katika divai yake, wala kuichuma kwani
italiwa na mabuu. Utakuwa na mizeituni katika mipaka yako yote usijipake mafuta
yake; kwa kuwa mzeituni wako utapukutika. Utazaa wana na binti, lakini
hawatakuwa wako wewe; kwa sababu watakwenda utumwani. Miti yako yote, na mazao
ya nchi yako, nzige watakuwa nayo.Mgeni aliye kati yako atazidi kupaa juu yako;
nawe utazidi kushuka chini.Yeye atakukopesha, wala wewe usimkopeshe; yeye
atakuwa ni kichwa, wewe utakuwa mkia.Na laana hizi zote zitakujilia juu yako,
zitakuandama na kukupata, hata uangamizwe, kwa kuwa hukuisikiza sauti ya Bwana,
Mungu wako, kushika maagizo yake na amri zake alizokuagiza; nazo zitakuwa juu
yako kwa ishara na ajabu, na juu ya uzao wako milele; kwa kuwa hukumtumikia
Bwana, Mungu wako, kwa furaha na moyo wa kushukuru, kwa ajili ya ule wingi wa
vitu vyote; kwa hiyo utawatumikia adui zako atakaowaleta Bwana juu yako, kwa
njaa, na kwa kiu, na kwa uchi, na kwa uhitaji wa vitu vyote; naye atakuvika
kongwa la chuma shingoni mwako, hata atakapokwisha kukuangamiza. Bwana
atakuletea taifa juu yako kutoka mbali, kutoka ncha ya dunia, kama arukavyo
tai; taifa usiloufahamu ulimi wake; taifa lenye uso mkali, ambalo haliangalii
uso wa mzee, wala halipendelei kijana; naye atakula uzao wa ng'ombe wako wa
mifugo, na uzao wa nchi yako mpaka utakapokwisha kuangamizwa; wala hatakuachia
nafaka, wala divai, wala mafuta, wala maongeo ya ng'ombe wako, wala wana-kondoo
wako, hata atakapokwisha kukuangamiza. Naye atakuhusuru katika malango yako
yote, hata kuta zako ndefu, zenye maboma, ulizokuwa ukiziamini, zishuke, katika
nchi yako yote kila upande; naye atakuhusuru katika malango yako yote kila
upande, katika nchi yako yote aliyokupa Bwana, Mungu wako. Nawe utakula uzao wa
tumbo lako mwenyewe, nyama ya wana wako na binti zako aliokupa Bwana, Mungu
wako; katika mazingirwa na katika mkazo utakaokazwa na adui zako. Mtu mume kati
yenu aliye mwororo na laini sana, jicho lake litakuwa ovu juu ya nduguye, na
juu ya mke wa kifuani mwake, na juu ya masalio ya wanawe waliosalia naye; hata
asitake wao mmojawapo apewe katika nyama ya wanawe atakaowala, kwa kuwa hana
kitu kilichomsalia kwake; katika mazingirwa na mkazo utakaokazwa na adui yako
katika malango yako yote. Mwanamke kati yenu aliye mwororo na laini, ambaye
hangehatirisha kuweka wayo wa mguu wake nchi kwa umalidadi na ulaini, jicho
lake huyu litakuwa ovu juu ya mume wa kifuani mwake, na juu ya mwanawe, na juu
ya binti yake,”
Kutii maagizo yote na amri zote
za Mungu kwa wanadamu halikuwa jambo rahisi, ilikuwa ni dhambi na ilileta laana
hii isingeliwezekana kwa wayahudi na hata wasio wayahudi, lilikuwa ni agizo
gumu sana ambalo kila wakati lingekufanya ujione mwenye dhambi, unayestahili
hukumu na hasira ya Mungu na kifo tu Petro mwenyewe alisema wazi kuwa sharia ya
Musa lilikuwa ni kongwa ambalo sisi wala baba zetu tusingeliweza kulimudu
angalia
Matendo 15:7-11 “Na baada ya hoja nyingi
Petro akasimama, akawaambia, Ndugu zangu, ninyi mnajua ya kuwa tangu siku za
kwanza Mungu alichagua miongoni mwenu ya kwamba Mataifa walisikie neno la
Injili kwa kinywa changu, na kuliamini. Na Mungu, ajuaye mioyo ya watu, akawashuhudia,
akiwapa Roho Mtakatifu vile vile kama alivyotupa sisi; wala hakufanya tofauti
kati yetu sisi na wao, akiwasafisha mioyo yao kwa imani. Basi sasa mbona
mnamjaribu Mungu na kuweka kongwa juu ya shingo za wanafunzi, ambalo baba zetu
wala sisi hatukuweza kulichukua. Bali twaamini kwamba tutaokoka kwa neema ya
Bwana Yesu vile vile kama wao.”
Unaona ni jambo la kushangaza ya
kuwa walimu kutoka uyahudi walisambaa ameneo mbalimbali na kuwafundisha
wakristo kuishika sharia ya Musa jambo ambalo lingewarudisha nyuma utumwani
mahali ambako Kristo alikuwa amekwisha kuwatoa na hivyo kuishika sharia ya Musa
tena kungeleta laana, kwa msingi huo Yesu alizaliwa kwa wakati ili pia aweze
kumkomboa mwanadamu kutoka katika laana ya Torati ujio wa Yesu Kristo duniani
ulikuwa ni kwa utimilifu wa wakati wakati wa kuwakomboa wanadamu kutoka katika
kongwa zito la Sheria hii ina maana gani? Neno ukombozi linalotumiwa na Paulo
katika Wagalatia kwa kiyunani ni EXAGORAZO ambalo lina maana ya
kununua, kwamba kama mtu ni mtumwa wa mtu na yuko chini ya sharia na unataka
kumkomboa kutoka katika sharia za mtu huyo unamnunulia uhuru wake na anakuwa huru mbali na sharia na adhabu za
mtu huyo kwa hiyo yeye aliyenunuliwa na kuwekwa huru katika utumwa wa sharia
maana yake hapaswi tena kuwa chini ya sharia na kanuni za Musa ambazo wana wa Israel walilazimika
kuzishika, sio hivyo tu hata laana za sharia hazituhusu, kwa namna yoyote ile
tusingeweza sisi kuishika sharia yote ya Musa kwa uwezo wetu wenyewe na ndio
maana Kristo alikuja kuitii kwa niaba yetu na kutulipia deni huko ndio
kuikamilisha torati na manabii.
Mathayo 5:17 “Msidhani ya kuwa nalikuja
kuitangua torati au manabii; la, sikuja kutangua, bali kutimiliza.”
Warumi 8:33-39 “Ni nani atakayewashitaki
wateule wa Mungu? Mungu ndiye mwenye kuwahesabia haki. Ni nani atakayewahukumia
adhabu? Kristo Yesu ndiye aliyekufa; naam, na zaidi ya hayo, amefufuka katika
wafu, naye yuko mkono wa kuume wa Mungu; tena ndiye anayetuombea. Ni nani
atakayetutenga na upendo wa Kristo? Je! Ni dhiki au shida, au adha, au njaa, au
uchi, au hatari, au upanga? Kama ilivyoandikwa, ya kwamba, Kwa ajili yako
tunauawa mchana kutwa, Tumehesabiwa kuwa kama kondoo wa kuchinjwa. Lakini
katika mambo hayo yote tunashinda, na zaidi ya kushinda, kwa yeye aliyetupenda.
Kwa maana nimekwisha kujua hakika ya kwamba, wala mauti, wala uzima, wala
malaika, wala wenye mamlaka, wala yaliyopo, wala yatakayokuwapo, wala wenye
uwezo,wala yaliyo juu, wala yaliyo chini, wala kiumbe kinginecho chote
hakitaweza kututenga na upendo wa Mungu ulio katika Kristo Yesu Bwana wetu.”
Yesu amekwishakufanya kila kitu
kwa niaba yetu, hatuwezi tena kuwa chini ya sharia ya kitumwa wala hatuwezi
kuadhibiwa na Mungu kwa kushindwa kuishi sawa na sharia, wala hatuhitaji tena
kuua au kuchinja wanyama kwaajili ya dhambi zetu na laana zetu kwani Kristo
amemaliza kila kitu hii sasa ina maana gani tunaweza kufanya lolote tulipendalo
hapana iko sharia ya kifalme tumeondolewa katika utumwa sharia ambayo ilikuwa
Mwalimu, wa watoto wa mfalme, sasa tumekuwa wafalme wafanya sharia na iko
sharia ya kifalme ambayo kwayo inatuongoza ni ipi hiyo hii hapa
Yakobo 2:8 “Lakini mkiitimiza ile sheria ya
kifalme kama ilivyoandikwa, Mpende jirani yako kama nafsi yako, mwatenda vema.”
Kwa hiyo kukombolewa katika laana
ya torati maana yake ni kuwekwa huru katika kushika na kufuata sharia na kanuni
ambazo zingeleta hasira ya Mungu juu yetu, kwa hiyo Yesu aliyahukumu hayo pale
Msalabani na sasa sisi tunaweza kuishi kwa njia iliyo rahisi kumpenda Mungu na kuwapenda
wanadamu wenzetu jambo ambalo litatupelekea kufikiri pale tunapotaka kuwafanyia
dhambi wengine
Mathayo 7:12 “Basi yo yote myatakayo
mtendewe na watu, nanyi watendeeni vivyo hivyo; maana hiyo ndiyo torati na
manabii.”
Kupokea hali ya kuwa wana.
Paulo anaeleza manufaa mengine ya
Yesu kuja katika utimilifu wa wakati, kwamba tunapokea hali ya kuwa wana au
watoto wa Mungu, hapa anamanisha kwa wale wanaompokea
Yohana 1:12 -13 “Bali wote waliompokea
aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake;
waliozaliwa, si kwa damu, wala si kwa mapenzi ya mwili, wala si kwa mapenzi ya
mtu, bali kwa Mungu.”
Ni mtoto yule yule aliyekuwa
chini ya Mwangalizi sasa anapatiwa nafasi ya kutawala pamoja na baba yake, neno
linalotumika katika maandiko kupokea kuwa mwana ni Adoption ambalo maana yake ni
KUMRITHI au KUMUASILI, ni kitendo cha mtu hususani mtoto kupewa haki kwa
baba mwingine na kuhesabiwa kuwa
amestahili kuwa mwanae wa kudumu aitwe kwa jina lake na kuwa na haki zote sawa
na watoto wa baba husika jambo hili linathibitishwa kwa kuvunjiliwa mbali kwa
hofu ya kuona Mungu kama Mtawala na kumuhisi Mungu kuwa ni baba na ndani yetu
tunapewa uhakika wa kumuita Mungu baba yetu kupitia muunganiko wa kazi za Roho
Mtakatifu, Baada ya kutununua na kutuweka huru mbali na sharia anatufanya kuwa
watoto wake na sio watumwa tena
Wagalatia 4:6-7 “Na kwa kuwa ninyi mmekuwa
wana, Mungu alimtuma Roho wa Mwanawe mioyoni mwetu, aliaye, Aba, yaani, Baba.
Kama ni hivyo, wewe si mtumwa tena bali u mwana; na kama u mwana, basi, u
mrithi kwa Mungu.”
Warumi 8:15 -16 “Kwa kuwa hamkupokea tena
roho wa utumwa iletayo hofu; bali mlipokea roho ya kufanywa wana, ambayo kwa
hiyo twalia, Aba, yaani, Baba. Roho mwenyewe hushuhudia pamoja na roho zetu, ya
kuwa sisi tu watoto wa Mungu;”
Ujio wa Yesu Kristo duniani kwa
wakati mtimilifu ulikusudiwa na Mungu kutukomboa kutoka katika hali ya utumwa
na kutupandisha kwa heshima katika ulimwengu wa roho ili awe baba yetu na
tuweze kutawala pamoja naye, hatupaswi kuogopa tena, tunapaswa kuwa na ujasiri,
dhambi sio tatizo tena, adhabu ya Mungu na hukumu zake hazina nguvu tena sharia
ya kifalme ndiyo dira yetu hakuna kitu cha kututenga na upendo wa kristo,
tunapoadhimisha siku kuu hii ya Christmas hatuna budi kufahamu kuwa Bwana wetu
Yesu amekuja kuyapandisha juu maisha yetu amekuja kutupa thamani, amekuja
kutubadilisha kutoka chombo cha hasira za Mungu na kuwa chombo cha upendo wa
Mungu, sisi sasa tuna mamlaka kamili
sisi ni kama yeye ni wafanya sharia tunayoyatamka yanakuwa, kwanini kwa
sababu sasa tunakuwa kama yeye alivyo
maana tu watoto wake na tamko la mfalme ni sharia ona
1Yoahan 4:16-18 “Nasi tumelifahamu pendo
alilo nalo Mungu kwetu sisi, na kuliamini. Mungu ni upendo, naye akaaye katika
pendo, hukaa ndani ya Mungu, na Mungu hukaa ndani yake. Katika hili pendo
limekamilishwa kwetu, ili tuwe na ujasiri katika siku ya hukumu; KWA KUWA, KAMA
YEYE ALIVYO, NDIVYO TULIVYO NA SISI ULIMWENGUNI humu. Katika pendo hamna hofu;
lakini pendo lililo kamili huitupa nje hofu, kwa maana hofu ina adhabu; na
mwenye hofu hakukamilishwa katika pendo.”
Hapa hapa ulimwenguni sisi sio wa
kawaida tena, maisha yetu yamebadilishwa kupitia kuja kwa Yesu Kristo kwa
utimilifu wa wakati, kila mmoja anaweza kuutumia wakati huu kumkubali Yesu na
kumkaribisha ili awe Bwana na mwokozi wa maisha yake, sisi tuliompokea
tuliutumia wakati vizuri wewe nawe hujachelewa leo unaposikia ujumbe huu na
unaposoma ujumbe huu anza kuchangamka ukijua kuwa Mungu anatupenda na
ulipowadia utimilifu wa wakati alimtuma Kristo atukomboe, Kuna watu hapa leo ni
wakati wao wa kuponywa, kuna watu ni wakati wao wa kutoka kwenye madeni, kuna
watu ni wakati wao wa kupokea heshima, kuna watu ni wakati wao wa kuolewa, kuna
watu ni wakati wao wa kutolewa katika vifungo vya utumwa, kuna watu ni wakati
wao wa kuponywa, kuna watu ni wakati wao wa ukombozi, Kuna watu ni wakati wao
wa kutoka katika adhabu, kuna watu ni wakati wao wa kufunguliwa, kuna watu ni
wakati wao wa kupandishwa cheo, kuna watu ni wakati wao wa kuinuliwa, kuna watu
ni wakati wao wa ushindi, kuna watu ni wakati wao wa kuongezeka, kuna watu ni
wakati wao wakuzaa sana, kuna watu ni wakati wao wa kutoka katika magereza za
aina mbalimbali, kuna watu ni wakati wao wa kuacha kudharaulika, kuna watu ni
wakati wao wa kufurahia maisha, kuna watu ni wakati wao wa kukomesha udhalilishaji,
kuna watu ni wakati wao wa kupata mpenyo, kuna watu ni wakati wao wa kuvikwa
vazi jipya, kuna watu wakati wao mtimilifu umewadia wa kufurahia Baraka za
Mungu wewe sio mtumwa tena, hofu imetupwa mbali, wewe ni mwana wa Mungu
haleluyaaaaaaa!, leo nafanya sharia mpya kwa kukutangazia kuwa wakati wako
mtimilifu umewadia Yesu Kristo yuko hapa leo kukuhudumia haleluyaaaaa!, wewe
sio wa chini tena wewe ni wajuu, wewe sio wa kuonewa tena, wewe sio wa kupokea
maagizo, wewe ni wa kutoa maagizo, Kuzaliwa kwa Yesu ulipowadia utimilifu wa
wakati kumemuinua mwanadamu na kumleta katika heshima ile kubwa ambayo malaika
wanaichungulia leo ni siku ya kusimikwa kwako kuwa mfalme na kutoka kifungoni,
kutoka gerezani, kutoka kwenye migandamizo na kuwa mtawala na lolote
utakalolitamka kwa jina la Yesu Kristo litageuka kuwa Baraka na kutimia na
lolote watakalokutamkia la kukutakia laana litawarudia juu yao Hakuna mtu
alimtukana mfalme akaishi, Happy Christimas !
Na Rev. Innocent Samuel Kamote.
Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima. !
Asante, mafundisho mazuri.
JibuFuta