Jumatatu, 11 Desemba 2023

Nyakati zangu katika mikono ya Bwana!


Zaburi 31:14-18 “Lakini mimi nakutumaini Wewe, Bwana, Nimesema, Wewe ndiwe Mungu wangu. Nyakati zangu zimo mikononi mwako; Uniponye na adui zangu, nao wanaonifuatia. Umwangaze mtumishi wako Kwa nuru ya uso wako; Uniokoe kwa ajili ya fadhili zako. Ee Bwana, nisiaibishwe, maana nimekuita; Waaibishwe wasio haki, wanyamaze kuzimuni. Midomo ya uongo iwe na ububu, Imneneayo mwenye haki maneno ya kiburi, Kwa majivuno na dharau.”




Utangulizi:

Ni muhimu kufahamu kuwa hapa Duniani hasa Afrika sio kila mtu anaweza kufurahia mafanikio yako, mazungumzo ya watu wengi kukuhusu wewe au mimi hufanyika zaidi pale tunapokuwa tumeharibu au kuharibikiwa hayo ndio watu huyazungumza na kuyapa kipaumbele na kuyafurahia zaidi, kuliko tunapokuwa na mafanikio, na kama wako watu katika nafasi ambayo wanaweza kuhakikisha kuwa wanaharibu mafanikio yako wako tayari kuhakikisha ya kuwa wanakuharibia hawa wanaitwa kwa kiingereza DESTINY KILLERS, yaani waua ndoto, au watu ambao hawafurahii kuona unafanikiwa hawa ni wengi sana duniani kuliko wale wanaotaka ufanikiwe, hii ni kawaida tu kwa sababu wanadamu wana tabia ya wivu na hawawezi kufurahia mafanikio yako!, wengi wanafurahia tuwe sawa au uwe chini lakini usiwazidi wala usifanikiwe kuliko wao, wako pia watu ambao hujipanga kwa namna mbalimbali ili kuhakikisha ya kuwa hutoboi hawa wanaweza kuwa ni watu wanaotumiwa na shetani aidha wakijijua au wakiwa hawajijui, lakini wanakuwepo tu katika jamii kuhakikisha kuwa wanaharibu, wanaua, wanasambaratisha au wanahakikisha  kuwa hufiki mbali au hufikii na katika nyakati ambazo Mungu ameziandaa kwaajili yako!, wao wanaandaliwa kuhakikisha ya kuwa wanakukwamisha, wanachelewesha, wanaharibu juhudi zako au wanadhoofisha Nyakati ambazo Mungu anakusudia kwako, na hawaoni lolote jema kwako, wanazungumza mabaya kukuhusu, wanakutakia kuharibikiwa, wanatamani wakukwamishe na hata kuidhoofisha Imani yako, wakati huo wakidhani kuwa nyakati zako ziko katika mikono yao na wanasahau kabisa kuwa ni Mungu ndiye anayeshika majira na nyakati  na mipango ya mtu ni Mungu peke yake mwenye nyakati zetu!

Wafilipi 1:6 “Nami niliaminilo ndilo hili, ya kwamba yeye aliyeanza kazi njema mioyoni mwenu ataimaliza hata siku ya Kristo Yesu;”

Kumbuka ni Mungu ndiye aliyeanza kazi njema na wewe, na ni yeye ndiye atakayeimaliza, hakuna mwanadamu anayeweza kudai, au kujidai au kujisifu kuwa anashikilia hatima yako, wote wanaosema ngoja tuone, hatoboi, ameisha, tumemaliza hakuna anayeweza kumaliza kile ambacho Mungu amekisimamisha, mambo ya Mungu hukamilishwa na Mungu mwenyewe na wanaoshindana nawe wanajiweka katika madhara kwani wanaweza kujikuta kuwa wanapingana na Mungu heri wajiepushe

Matendo 5: 38-39 “Basi sasa nawaambia, Jiepusheni na watu hawa, waacheni; kwa kuwa shauri hili au kazi hii ikiwa imetoka kwa binadamu, itavunjwa, lakini ikiwa imetoka kwa Mungu hamwezi kuivunja; msije mkaonekana kuwa mnapigana na Mungu.”

Akiyajua haya Daudi anasema Nyakati zangu ziko mikononi mwako Ee bwana na anamuomba Mungu amlinde na maadui zake, wala asimuache kuaibishwa, na wote wanaomfuatia wawe bubu, wanyamazishishwe kuzimu, leo tutachukua muda kujifunza somo hili NYAKATI ZANGU KATIKA MIKONO YA BWANA kwa kuzingatia vipengele vitatu vifuatavyo:-

1.       Maana ya zangu katika mikono ya Bwana

2.       Mifano ya uweza wa Mungu katika nyakati za watu mbalimbali

3.       Nyakati zangu katika mikono ya Bwana

Maana ya Nyakati zangu katika Mikono ya Bwana

Zaburi 31:14-18 “Lakini mimi nakutumaini Wewe, Bwana, Nimesema, Wewe ndiwe Mungu wangu. Nyakati zangu zimo mikononi mwako; Uniponye na adui zangu, nao wanaonifuatia. Umwangaze mtumishi wako Kwa nuru ya uso wako; Uniokoe kwa ajili ya fadhili zako. Ee Bwana, nisiaibishwe, maana nimekuita; Waaibishwe wasio haki, wanyamaze kuzimuni. Midomo ya uongo iwe na ububu, Imneneayo mwenye haki maneno ya kiburi, Kwa majivuno na dharau.”

Neno nyakati linalotumika hapo katika maandiko ya kiingereza linasomeka katika namna hii

Psalm 31:14-18 “But I trust in you, O Lord: I say You are my God” MY TIMES ARE IN YOUR HANDS Deliver me from my enemies and from those who pursue me. Let your face shiner on your servant; save me in your unfailing love. Let me noy be put to shame O Lord, for I have cried out to you, but let the wicked be put to shame and lie silent in the grave. Let their lying lips be silenced, for with pride and contempt they speak arrogantly against the righteous

Kifungu hiki cha maandiko ni mojawapo ya kifungu cha Muhimu sana katika zaburi hii, Mwandishi alikuwa akifanya maombi yanayoonyesha ya kuwa anamuamini Mungu na kuwa anamtegemea kwa Ulinzi wake na mafanikio ya maisha yake dhidi ya watu wote wale wanaiomtakia mabaya, Mwandishi sio tu kuwa alikuwa anatakiwa mabaya na adui zake lakini adui zake walikuwa wamekwishakuchukua hatua kadhaa kuhakikisha kuwa hafanikiwi, hatoboi hatoki na anamalizwa kwa namna yoyote ile, ni kama walikuwa wanafikiri kuwa wameshamuweza,  Lakini mwandishi anamwambia Mungu kwamba yeye anamwamini na kwamba alikuwa anafahamu wazi kuwa NYAKATI ZAKE ZIKO KATIKA MKONO WA MUNGU hivyo alipokuwa akikutana na vita na upinzani kutoka kwa maadui alikuwa anafahamu kuwa yeye anatakiwa tu Kumuomba Mungu, kwa sababu yeye alifahamu kuwa alizaliwa kwa kusudi la Mungu na kuwa yuko duniani kutimiza mpango wake katika wakati uliokusudiwa na Mungu!

Neno Nyakati zangu Katika mikono ya Bwana au kwa kiingereza My times in the hands of Lord  kwa kiebrania linasomeka kama ETH kimatamshi AYTH  ambalo maana yake ni Majira na Makusudi, katika biblia ya kiingereza ya KJV limetumika mara 257 kumaanisha muda, mara 16 kumaanisha majira, mara 7 kumaanisha kusudi na mara 10 kumaanisha Kazi maalumu, hii maana yake ni nini ? Mungu anapotupa muda wa kuishi ndani yake anatoa majira, muda kazi na majukumu ambayo kila mwanadamu anatakiwa ayatimize awapo duniani unaona!  Na ili uyatimize kuna HATIMA yaani kilele cha kutimizwa kwa majukumu hayo maalumu ambayo Mungu anayatoa kwa kila mtu kwa majira na nyakati zake!

Kwa hiyo Mwandishi anapojieleza kuwa Nyakati zangu zimo Mikononi mwake anamaanisha Hatima  yaani Destiny, kusudi, wajibu, muda na kazi maalumu aliyopewa na iliyokusudiwa kwake iko mikononi mwa Mungu, na kama ni hivyo basi ni wazi kuwa juhudi na jitihada za maadui na wapinzani, na wanena mabaya, na wanga, na wachawi, na majeshi,   na wazandiki na wafitini, na wapika majungu, na walozi, na wenye chuki, na wenye wivu na wenye husuda kamwe haziwezi kuharibu wala kukatisha kusudi la Mungu lililokusudiwa na Mungu kwa wakati wake na kuwa ni lazima litatimia, hafi mtu wala haaribikiwi mtu, kwa sababu hao woote hawana hatimiliki ya Nyakati zilizokuduiwa kwako

-          Habakuki 2:3 “Maana njozi hii bado ni kwa wakati ulioamriwa, inafanya haraka ili kuufikilia mwisho wake, wala haitasema uongo; ijapokawia, ingojee; kwa kuwa haina budi kuja, haitakawia.”

 

-          Isaya 46:9-10 “kumbukeni mambo ya zamani za kale; maana mimi ni Mungu, wala hapana mwingine; mimi ni Mungu, wala hapana aliye kama mimi; nitangazaye mwisho tangu mwanzo, na tangu zamani za kale mambo yasiyotendeka bado; nikisema, Shauri langu litasimama, nami nitatenda mapenzi yangu yote.”

 

-          Hesabu 23:19 “Mungu si mtu, aseme uongo; Wala si mwanadamu, ajute; Iwapo amesema, hatalitenda? Iwapo amenena, hatalifikiliza?

Kwa hiyo ni Mungu ndiye aliyekusudia uzaliwe hapo ulipozaliwa, ni Mungu aliyekusudia uzaliwe mwanamke au mwanaume, ni Mungu aliyekusudia uzaliwe katika familia uliyozaliwa, ni Mungu aliyekusudia ufanye kazi unayoifanya ni Mungu aliyekusudia ufanye huduma unayoifanya, ni Mungu aliyekusudia uwe na mume uliye naye na mke uliye naye ni Mungu aliyekusudia uwe na cheo ulicho nacho na mambo haya yote Mungu aliyakusudia tangu kuwekwa kwa misingi ya dunia, maana yake ni nini Hakuna mtu au pepo au malaika au jambo lolote lile linaloweza kuharibu mpango wa Mungu katika maisha yako kwa sababu hakuna adui anayeshikilia hatima yako, wala muda wako, wala kazi maalumu ambayo Mungu ameikusudia katika maisha yako kwa nini kwa sababu NYAKATI ZAKO ZIKO KATIKA MIKONO YA BWANA !

Waefeso 2:10 “Maana tu kazi yake, tuliumbwa katika Kristo Yesu, tutende matendo mema, ambayo tokea awali Mungu aliyatengeneza ili tuenende nayo.”

 

Mifano ya uweza wa Mungu katika nyakati za watu mbalimbali

Maandiko yamejaa mifano mingi sana ambayo Muda hauwezi kuruhusu kuipitia yote, lakini mifano michache nitakayoitumia hapa inatosha kabisa kuonyesha kuwa adui zako hawakuwezi, na hawana mamlaka ya kuharibu chochote na kama wakiharibu ujue tu Mungu alikusudia waharibu, kwa sababu maandiko yanaonyesha kuwa hatua zetu zote yaani njia za maisha yetu zote zinaratibiwa na Mungu ona

Mithali 20:24 “Mwenendo wa mtu watoka kwa Bwana; Basi, awezaje mtu kuelewa na njia yake?

Mungu anapokuwa amekusudia jambo kwa Mtu na kwa wakati wake kisha akatokea mtu kuingilia kati kwa makusudi ya kuharibu, awe anajua au awe hajui, awe amatumiwa na shetani au awe hajatumiwa, awe ni ajenti wa ibilisi au vyovyote vile ni aidha mipango yao ifeli, au kupitia hila zao Mungu akupeleke katika mpango wake mwingine anaoukusudia kwa wakati huo kwanini kwa sababu Nykati zetu zimo katika mikono yake, hapa iko mifano ya watu waliozaliwa kwa wakati maalumu kwa kusudi la kufanya kazi maalumu katika majukumu maalimu kwa nyakati alizokuwa amekusudia Mungu kisha watu wakajitokeza na mikakakati ya kuharibu au kuzuia na haya ndio waliyokutana nayo:- ona

1.       Herode dhidi ya Mwana wa Mungu Yesu Kristo

 

Moja ya watu waliojaribu kuharibu maisha ya mtu mwingie ni pamoja na Herode Mfalme yeye alikuwa amekusudia kuyaharibu kabisa maisha ya Mwana wa Mungu Yesu Kristo, baada ya kusikia habari za kuzaliwa kwake na unabii aliosomewa na matamko ya wanajibu yaani mamajusi kuhusu hatima ya Yesu Kristo kuwa ni Mfalme mkuu wa wayahudi anayestahili kusujudiwa yeye alifadhaika na aliadhimia kuwa na mkakati wa kuharibu maisha ya Mwana wa Mungu

 

Mathayo 2:1-3 “Yesu alipozaliwa katika Bethlehemu ya Uyahudi zamani za mfalme Herode, tazama, mamajusi wa mashariki walifika Yerusalemu, wakisema, Yuko wapi yeye aliyezaliwa mfalme wa Wayahudi? Kwa maana tuliiona nyota yake mashariki, nasi tumekuja kumsujudia. Basi mfalme Herode aliposikia hayo, alifadhaika, na Yerusalemu pia pamoja naye.”

 

Wako watu wanaotuzunguka wako kama Herode badala ya kufurahia mafanikio yako wao wanafadhaika wanaumwa na mafanikio yako, wanaumwa wanapoona ya kuwa unaenda kutoboa,  wanaumwa wanaposikia kuwa unaenda kuoa au kuolewa, au kupata kazi, au kupewa cheo au wanapogundua kuwa wewe ni tishio la mafanikio kwao wanatumia kila hila na ujanja ili yamkini ikiwezekana waharibu Mpango wa Mungu ndani yako lakini ashukuriwe Mungu kuwa hekima yake haichunguziki yeye anajua kuifanya kuwa upuuzi hekima ya dunia hii nay a shetani nay a wanadamu, wewe kama ni mwana wa Mungu kama ilibyokuwa kwa Yesu Kristo Mungu ataandaa mpango wa kukuokoa na kuchepusha njia za adui kile wanachokifikiri, sio kile ambacho Mungu atakifanya

 

Mathayo 2:8-14 “Akawapeleka Bethlehemu, akasema, Shikeni njia, mkaulize sana mambo ya mtoto; na mkiisha kumwona, nileteeni habari, ili mimi nami niende nimsujudie.Nao waliposikia maneno ya mfalme, walishika njia; na tazama, ile nyota waliyoiona mashariki ikawatangulia, hata ikaenda ikasimama juu ya mahali alipokuwapo mtoto. Nao walipoiona ile nyota, walifurahi furaha kubwa mno. Wakaingia nyumbani, wakamwona mtoto pamoja na Mariamu mamaye, wakaanguka wakamsujudia; nao walipokwisha kufungua hazina zao, wakamtolea tunu; dhahabu na uvumba na manemane. Nao wakiisha kuonywa na Mungu katika ndoto wasimrudie Herode, wakaenda zao kwao kwa njia nyingine. Na hao walipokwisha kwenda zao, tazama, malaika wa Bwana alimtokea Yusufu katika ndoto, akasema, Ondoka, umchukue mtoto na mama yake, ukimbilie Misri, ukae huko hata nikuambie; kwa maana Herode anataka kumtafuta mtoto amwangamize. Akaondoka akamchukua mtoto na mama yake usiku, akaenda zake Misri;”

 

Mungu alifanya njia kuhakikisha kusudia aliloliweka ndani ya Mwana wake linatimia na kuwa hakuna mpumbavu anaweza kuliharibu, kiburi cha Herode kilifanywa kuwa ujinga pale Mungu alipotokeza njia na kusema na mamajusi lakini vile vile alisema na Yusufu, nataka nikuhakikishie kile ambacho Adui zako wanadhani kuwa watafanikiwa hakitafanikiwa na Mungu ana njia na mpango mkakati wa kuhakikisha kuwa anajitokeza kwako, kwa njia nyingine kuhakikisha ya kuwa kazi ile njema aliyoianza anaikamilisha hakuna anayeweza kushindana na kusudi la Mungu na kubadili mpango na nyakati alizozikusudia Bwana !

 

2.       Farao dhidi ya wana wa Israel

 

Farao alikwishakuambiwa mara kadhaa kusudi la Mungu kuhusu Israel, alielezwa wazi kuwa israel ni mzaliwa wa kwanza wa Mungu wa Ibrahim Isaka na Yakobo, na kuwa kusudi la Mungu wa waebrania ni kuwapeleka Israel katika inchi ya mkanaani aliyowaapia baba zao Ibrahim na Isaka na Yakobo, lakini kwa makusudi kabisa farao alikuwa akipingana na kusudi hili na akapigwa kwa mapigo kumi, hata baada ya pigo la mwisho yeye bado alitaka kuwaendea Israel na kuwarejesha tena katika inchi ya utumwa

 

Kutoka 14:5-8 “Mfalme wa Misri aliambiwa ya kuwa wale watu wamekwisha kimbia; na moyo wa Farao, na mioyo ya watumishi wake, iligeuzwa iwe kinyume cha hao watu, nao wakasema, Ni nini jambo hili tulilotenda, kwa kuwaacha Waisraeli waende zao wasitutumikie tena? Akaandalia gari lake, akawachukua watu wake pamoja naye; tena akatwaa magari mia sita yaliyochaguliwa, na magari yote ya Wamisri, na maakida juu ya magari hayo yote.Na BWANA akaufanya moyo wake Farao mfalme wa Misri kuwa mgumu, naye akawafuata wana wa Israeli; kwa sababu wana wa Israeli walitoka kwa ujeuri.”         

 

Unaweza kuuona moyo wa farao,? Bado walifikiri yeye na watumishi wake kuwa wanaweza kuamua hatima ya watu wa Mungu, wanaweza kuwarejesha nyuma wanaweza kuzuia mpango wa Mungu na neno lake  na kiapo chake kuwa anawapeleka katika inchi ya mkanaani na hivyo hata Mungu alipoigawa bahari ya shamu kwa ujinga walitaka kupita mle mle kinyume na kusudi la Mungu na hiki ndicho kilichowakuta

 

Kutoka 14:22-28 “Wana wa Israeli wakaenda ndani kati ya bahari katika nchi kavu; nayo maji yalikuwa ukuta kwao mkono wa kuume, na mkono wa kushoto. Na wale Wamisri wakawafuatia, wakaingia ndani kati ya bahari, farasi zote za Farao, na magari yake, na wapanda farasi wake. Ikawa katika zamu ya alfajiri, BWANA akalichungulia jeshi la Wamisri katika ile nguzo ya moto na ya wingu, akalifadhaisha jeshi la Wamisri. Akayaondoa magurudumu ya magari yao, hata yakaenda kwa uzito; na Wamisri wakasema, Na tukimbie mbele ya Israeli; kwa kuwa BWANA anawapigania, kinyume cha Wamisri. BWANA akamwambia Musa, Nyosha mkono wako juu ya bahari, ili maji yarudi tena juu ya Wamisri, juu ya magari yao, na juu ya farasi zao. Musa akaunyosha mkono wake juu ya bahari, na kulipopambazuka, bahari ikarudi kwa nguvu zake; Wamisri wakakimbia mbele yake; na BWANA akawakukutia mbali hao Wamisri kati ya bahari. Yale maji yakarudi yakafunikiza magari na wapanda farasi, hata jeshi lote la Farao lililoingia katika bahari nyuma yao; hakusalia hata mtu mmoja.”

 

Unaona hatima ya farao na majesi yake yote yalizikwa katika bahari ya shamu kwa nini kwa sababu alikuwa akishindana na kusudi lililokuwa ndani ya watu wa Mungu, nimefurahi Musa anavyomalizia mstari huu HAKUSALIA HATA MTU MMOJA  Bwana akufanyie hivyo na kuzidi mtu wa Mungu wote ambao wanakufuatilia ili kuhakikisha kuwa unaharibikiwa Bwana asimwache hata mmoja asisalie hata wa kutoa taarifa ya kilichotokea, awaye yote ambaye anazani kuwa ana mamlaka ya kushika Nyakati zako ajue wazi kuwa nyakati zako ziko katika mikono ya Bwana !

 

3.       Mawaziri dhidi ya Daniel

 

Wakati mwingine watu wanaodhani wanaweza kuharibu Nyakati zako kwaajili ya  sifa zako hupatwa na wivu tu, na kutafuta kuwa maarufu, au kutafuta kukuchafua ili wao waonekane au wawe na cheo kama ulichonacho hawajui kuwa wewe una upako wa huduma tofauti au niseme una kitu cha ziada ndivyo aklivyokuwa Daniel alipendwa aliwazidi watu katika sifa na cheo na uaminifu na watu wakawa wanatafuta namna ya kumpaka matope ili achafuke ili tu wamuharibie

 

Daniel 6:1-5 “Ilimpendeza Dario kuweka juu ya ufalme maliwali mia na ishirini, wawe juu ya ufalme wote; na juu yao akaweka wakubwa watatu, na Danieli alikuwa mmoja wao; ili maliwali hawa watoe hesabu kwao, mfalme asipate hasara. Basi Danieli huyo alipata sifa kuliko wakubwa na maliwali, kwa kuwa roho bora ilikuwa ndani yake; naye mfalme akaazimu kumweka juu ya ufalme wote. Basi mawaziri na maamiri wakatafuta sana kupata sababu za kumshitaki Danieli kwa habari za mambo ya ufalme; lakini hawakuweza kuona sababu wala kosa; kwa maana alikuwa mwaminifu, wala halikuonekana kosa wala hatia ndani yake. Ndipo wale watu wakasema, Hatutapata sababu ya kumshitaki Danieli huyo, tusipoipata katika mambo ya sheria ya Mungu wake.”

 

Ukiona watu wanatafuta kuchafua jina lako au kuwafanya wengine waamini kuwa haufai ujue kuna kitu cha ziada umewazidi, katika maisha yangu nimekutana na watu wengi sana wenye wivu wenye uchungu ambao sio tu wanatamani uharibikiwe lakini wanatamani usambaratike, wanatamani hata ndoa yako ife, wanatamani kazi zako ziharibike, ufukuzwe, uumwe, ufe upatwe na majanga na sio hivyo tu watakuandama wakiwa na wivu wenye uchungu, watatumia hata uchawi na majungu wakifikiri ya kuwa wamekuweza hivi ndivyo ilivyokuwa kwa Daniel lakini mwisho wa siku Daniel aliyetupwa katika tundu la simba alipona na wao wakaliwa na simba na kutoweka duniani kwa nini kwa sababu nyakati za mtu wa Mungu ziko mikononi mwa Mungu

 

Daniel 6:20-24 “Naye alipolikaribia lile tundu, akamlilia Danieli kwa sauti ya huzuni; mfalme akanena; akamwambia Danieli, Ee Danieli, mtumishi wa Mungu aliye hai, je! Mungu wako, unayemtumikia daima, aweza kukuponya na simba hawa? Ndipo Danieli akamwambia mfalme, Ee mfalme, uishi milele. Mungu wangu amemtuma malaika wake, naye ameyafumba makanwa ya simba, nao hawakunidhuru; kwa kuwa mbele zake mimi nalionekana kuwa sina hatia; tena, mbele yako, Ee mfalme, sikukosa neno. Basi mfalme akafurahi sana, akaamuru wamtoe Danieli katika lile tundu. Ndipo Danieli akatolewa katika lile tundu, wala dhara lo lote halikuonekana mwilini mwake, kwa sababu alikuwa anamtumaini Mungu wake. Mfalme akaamuru, nao wakawaleta wale watu waliomshitaki Danieli, wakawatupa katika tundu la simba, wao, na watoto wao, na wake zao; na wale simba wakawashinda wakaivunja mifupa yao vipande vipande, kabla hawajafika chini ya tundu.”

 

Wwatu wote waliokuwa wakiwafuatia watu wenye kusudi la Mungu hatima ya maisha yao ilikuwa mbaya sana, Ndugu usiogope wote waliokuonea Mungu atawalipia maovu yao yatakuwa juu ya vichwa vyao, hawawezi kukuharibu, hawawezi kukufitini, hawawezi kukuzika na badala yake utawazika wewe, muda usingeweza kutosha kusema habari za Hamani na Esta na wayhaudi walokuwako shushani Ngomeni, wala muda wa balaamu dhidi ya waisraeli, wala musa wa Yusufu na kaka zake, wala Sanbalati na tobia dhidi ya Nehemia, na kadhalika wewe kama mwanafunzi wa biblia unajua yaliyowakuta Mungu hataacha uonelewe atawakemea wote na kuwachafulia usemi wao wote wanaoinuka kinyume nao na wote wanaojenga mnara wa babeli dhidi yako watachafuliwa usemi

               

Nyakati zangu katika Mikono ya Bwana

Zaburi 31:14-18 “Lakini mimi nakutumaini Wewe, Bwana, Nimesema, Wewe ndiwe Mungu wangu. Nyakati zangu zimo mikononi mwako; Uniponye na adui zangu, nao wanaonifuatia. Umwangaze mtumishi wako Kwa nuru ya uso wako; Uniokoe kwa ajili ya fadhili zako. Ee Bwana, nisiaibishwe, maana nimekuita; Waaibishwe wasio haki, wanyamaze kuzimuni. Midomo ya uongo iwe na ububu, Imneneayo mwenye haki maneno ya kiburi, Kwa majivuno na dharau.”

Kwa misingi hiyo utaweza kuona kuwa kadiri unavyokaribia au unapofikia kilele cha kusudi lile ambalo Mungu amelikusudia au hatima ile ya Muhimu ndio utaweza kuona vita kali sana inainuka, Mungu anapotaka kukuinua au anapokuwa amekuinua unakuta watu hawapendezwi, hawafurahii wanazungumza vibaya, wanakuchafua wanakuchukia, njia yako inatiwa tope inawekwa giza, upinzani unakuwa mkubwa dharau, masengenyo, majungu, mateso, au vita kali sana jua sasa kuwa unakaribia Baraka kubwa ambazo Mungu amezikusudia kwako, na nataka nikuhakikishie kuwa Mungu yule yule anayetupa neema kupenya atakupa neema izidiyo na kukusaidia wakati wa mahitaji yako  watu hawashindani na mtu mwenye nyota ndogo, watu wenye nyota ndogo siku zote hupiga vita watu wenye nyota kubwa kumbuka nyota ya Yesu na Herode!

Waebrania 4:16 “Basi na tukikaribie kiti cha neema kwa ujasiri, ili tupewe rehema, na kupata neema ya kutusaidia wakati wa mahitaji.”

Wakati huo mtegemee Mungu ukiwa na ufahamu kama aliokuwa nao Daudi mtumaini yeye, mfanye kuwa ndie Mungu wako jua kuwa nyakati zako ziko mikononi mwake kwa hiyo atakuponya na adui zako, atakupa kibali, atashughulika na wanaokufuatilia, atakuokoa kwa upendo wake, hatakuacha uaibike, wataaibishwa wao na kunyamazishwa katika kuzimu, na wanaosema mabaya watapigwa ububu!

Hatupaswi kuogopa lolote wala mtu yeyote wala manenmo yoyote ya wapuuzi na wajinga walio kinyume na mapenzi ya Mungu katika maisha yetu, hakuna mtu anayeshika hatima ya maisha yako isipokuwa Mungu mwenyewe

Kila mtu anaweza kupanga lolote analoweza kulipanga lakini shauri la bwana ndio litakalosimama Mithali 19:21 “Mna hila nyingi moyoni mwa mtu; Lakini shauri la Bwana ndilo litakalosimama.”

Haijalishi wanadamu wanajenga nini la msingi ni lile Mungu analolijenga  Zaburi 127:1 “Bwana asipoijenga nyumba Waijengao wafanya kazi bure. Bwana asipoulinda mji Yeye aulindaye akesha bure.”    

Fahamu ya kuwa unaweza kuwa na vita kubwa na nyingi lakini ukimwambia Bwana yeye ndiye atakayepigana kwa niaba yako, Mungu ndiye aliyekusudia hakuna anayeweza kutangua kusudi, kupigana nawe adui zako ni kama wameamua kupigana na Mungu mwenyewe,  kwa kila jaribu uko mlango wa kutokea, Mwana wa Mungu alikuwa na maadui wengi walioinuka pasipo sababu lakini Yesu hakupoteza muda kujibizana nao alikuwa busy na majukumu ambayo Mungu amempa, ninaposema nyakati zangu katika mikono ya Mungu nina maana pana  sana hakuna mtu anaweza kudhibiti, kuongeza au kupunguza lolote lile katika makusudi ambayo kwayo Mungu ameyakusudia katika maisha yangu na yako kwa hiyo usiogope, Hakuna aibu itatutawala, hakuna vita hatutashinda, hakuna kikwazo hatutavuka, hakuna aibu haitazimishwa, hakuna kivywa hakitazibwa, hakuna kifo, hakuna kurudi nyuma, sio kwa sababu mimi na wewe ni wakamlilifu bali kwa sababu yeye ni mkamilifu, mpango wa Mungu ndani yetu hauwezi kuzimishwa na wazushi, ni fimbo yake na gongo lake ndilo linalotuongoza, tumeumbwa na Mungu na sio na watu, mimi na wewe tu  wana wa Mungu wagomvi wetu wanagombana na baba yetu haupaswi kuogopa kwa sababu NYAKATI ZAKO ZIKO KATIKA MIKONO YA MUNGU.


Na. Rev Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni