Jumapili, 21 Aprili 2024

Umponyaye masikini na mtu aliye hodari!

 

Zaburi 35:9-10 “Na nafsi yangu itamfurahia Bwana, Na kuushangilia wokovu wake.Mifupa yangu yote itasema, Bwana, ni nani aliye kama Wewe? Umponyaye maskini na mtu aliye hodari kumshinda yeye, Naam, maskini na mhitaji na mtu amtekaye.”





Utangulizi:

Kwa kawaida katika ulimwengu huu limekuwa ni jambo la kawaida katika mazingira Fulani, wenye nguvu kuwaonea wale wasio na nguvu, au Matajiri, kuwaonea masikini, au mtu aliye hodari kumuonea aliye mnyonge, Hali hii inaweza kuwa imekutokea wewe au familia yako katika mazingira Fulani. Familia nyingi za kiafrika bado ziko katika kipindi cha mpito, kutoka katika hali duni kuelekea katika hali njema kwa hiyo watu wengi sana wamewahi kukutana na uonevu wa namna nyingi, kutoka kwa wenye nguvu, wenye mamlaka, au watu Fulani kulingana na nyadhifa zao, wanaweza kwa namna mmoja ama nyingine kuwa wamekutana na aina Fulani ya uonevu Daudi alikuwa mmoja ya watu waliokutana na hali kama hiyo na kupata maumivu nafsini mwake, Hali hii inamkuta mtu anapokuwa Katika namna au nafasi ambayo hakuna wa kuingilia kati isipokuwa Mungu mwenyewe.

Katika Zaburi ya 35 Daudi anajaribu kumuomba Mungu sasa ili Mungu aweze kuinglia kati kwa haraka na kumtoa katika mazingira magumu aliyokuwa anakabiliana nayo ambayo yalikuwa hayana mtetezi. Na anamuahidi Mungu kuwa endapo atamletea msaada basi yeye ata mfurahia Bwana na kuushangilia wokovu wake!  

Zaburi 35:9 “Na nafsi yangu itamfurahia Bwana, Na kuushangilia wokovu wake.” Kwa sababu hii sisi nasi leo tutachukua muda mfupi kujifunza na kutafakari kifungu hiki muhimu kwa kuzingatia vipengele viwili vifuatavyo:-

 

·         Bwana ni nani aliye kama wewe

·         Umponyaye masikini na mtu aliye hodari!

 

Bwana ni nani aliye kama wewe! 

Zaburi 35:10b “Mifupa yangu yote itasema, Bwana, ni nani aliye kama Wewe? Umponyaye maskini na mtu aliye hodari kumshinda yeye, Naam, maskini na mhitaji na mtu amtekaye.”

Daudi akitumia lugha ya kimashairi hapa anaanza kwa kuahidi kuwa atamtukuza Mungu, endapo BWANA ataingilia kati mahitaji yake na maombi yake na kwa kweli yalikuwa ni maombi ya mtu mwenye uchungu mwingi yanayodhihirisha kuwa alikuwa amechoshwa na hali inayomkabili,  Mifupa yangu yote itasema Bwana ni nani aliye kama wewe, Ni Muhimu kufahamu kuwa Waebrania walitumia neno Mifupa kumaanisha nafsi au mtu wa ndani, wao walikuwa wakifikiri kuwa mtu wa ndani kabisa anawakilishwa na mifupa, kwa hiyo hata mtu alipokuwa akimaanisha mtu wake wa karibu au wa ndani  sana au ndugu alitumia neno Mifupa

Mwanzo 2:23 “Adamu akasema, Sasa huyu ni mfupa katika mifupa yangu, na nyama katika nyama yangu, basi ataitwa mwanamke, kwa maana ametwaliwa katika mwanamume.” 

Zaburi 6:2-4 “Bwana, unifadhili, maana ninanyauka; Bwana, uniponye, mifupa yangu imefadhaika. Na nafsi yangu imefadhaika sana; Na Wewe, Bwana, hata lini? Bwana urudi, uniopoe nafsi yangu, Uniokoe kwa ajili ya fadhili zako.” 

Kwa hiyo Daudi alikuwa akimaanisha nafsi yake imeumizwa na kama Bwana ataingilia kati dhidi ya adui zake ambao kimsingi walikuwa na nguvu au mamlaka au wenye kutisha kuliko yeye au wenye uwezo kuliko yeye au wenye uchumi mzuri kuliko yeye, au wenye nguvu, au uwezo wa kumchukua mateka, na kumuokoa Basi nafsi yake yaani kwa kibrania mifupa yake ingempa Mungu utukufu na kumshukuru sana na atasema Bwana ni nani aliye kama wewe! Mifupa katika lugha ya kiibrania wanatumia neno ETSEM ambalo linazungumzia mtu wa ndani Selfsame yaani nafsi neno hili limejitiokeza katika maandiko mara 126 katika mistari karibu 108.

Usemi huu Bwana ni nani aliye kama wewe ulikuwa ukionekana mara kwa mara katika mashairi ya kiibrania likitumika kama swali la kimashairi  kuhoji kuwa  ni nani mwenye nguvu au anayeweza kuwa na kiburi na jeuri kiasi cha kujilinganisha au kusimama kinyume na Mungu aliye hai anapoamua kuingilia kati mambo yake, wakati Farao alipokuwa na nguvu za kijeshi kuliko taifa lolote duniani na kuamua kusimama kwa ujeuri kinyume na wana wa Israel na hata walipookolewa aliamua kuwafuata ili awarejeshi utumwani, Israel baada ya udhihirisho mkubwa wa Mungu na ukombozi ulio hodari wa Bwana wa majeshi waliimba na kusema Bwana ni nani aliye kama wewe! 

Kutoka 15:10-12 “Ulivuma kwa upepo wako, bahari ikawafunikiza; Wakazama kama risasi ndani ya maji makuu. Ee BWANA, katika miungu ni nani aliye kama wewe? Ni nani aliye kama wewe, mtukufu katika utakatifu, Mwenye kuogopwa katika sifa zako, mfanya maajabu? Ulinyosha mkono wako wa kuume, Nchi ikawameza” 

Israel Walimshangilia Bwana na kumuimbia kwa furaha huku wakihoji ee Bwana katika miungu Ni nani aliye kama wewe huu ulikuwa ni usemi wa kawaida katika Israel wenye kuonyesha ya kuwa Hakuna wa kulinganishwa na Mungu mwenye nguvu wa Israel

Zaburi 89:7-9 “Mungu huogopwa sana barazani pa watakatifu, Ni wa kuhofiwa kuliko wote wanaomzunguka. Bwana, Mungu wa majeshi, Ni nani aliye hodari kama Wewe, Ee YAHU? Na uaminifu wako unakuzunguka. Wewe ndiwe ukitawalaye kiburi cha bahari. Mawimbi yake yainukapo wayatuliza Wewe.”

Zaburi 71:17-19 “Ee Mungu, umenifundisha tokea ujana wangu; Nimekuwa nikitangaza miujiza yako hata leo. Na hata nikiwa ni mzee mwenye mvi, Ee Mungu, usiniache. Hata niwaeleze watu wa kizazi hiki nguvu zako, Na kila atakayekuja uweza wako. Na haki yako, Ee Mungu, Imefika juu sana. Wewe uliyefanya mambo makuu; Ee Mungu, ni nani aliye kama Wewe?

Zaburi 113: 4-5. “Bwana ni mkuu juu ya mataifa yote, Na utukufu wake ni juu ya mbingu. Ni nani aliye mfano wa Bwana, Mungu wetu aketiye juu;” 

Bwana ni nani aliye kama wewe ni usemi unaoonyesha Mungu ni mwenye nguvu na hakuna mfano wake,ana uwezo kuliko kitu chochote, ana nguvu kuliko nguvu za wachawi na waganga na washirikina, ana nguvu kuliko jeshi lolote duniani, ana mamlaka kuliko mtu yeyote duniani, ana uweza, ulio juu kuliko mungu yeyote duniani, ana utajiri kuliko yeyote duniani na ndiye mkombozi na mtetezi wa wanadamu hasa kwa sababu yeye hapendi uonevu, kwa hiyo wakati tunajiona duni na tumeachwa tukiwa hatuna mtetezi, tumeachwa tupate kudhalilika, tuko katika hali ya unyonge hatuna budi kujiandaa kwa shuhuda, Daudi alikuwa anajiandaa kwa shuhuda alipokuwa anaomba kwamba Mungu akingilia kati na kumsaidia alisema nafsi yangu itakushukuru, atashuhudia jinsi Mungu alivyo mtenda miujiza mikubwa na mwokozi na mtetezi na kimbilio la wanyonge,  na hivyo fadhili za Bwana zina nguvu kuliko majeshi yoyote, mamlaka yoyote na wapanda farasi wake!

Zaburi 33:16-18. “Hapana mfalme aokokaye kwa wingi wa uwezo, Wala shujaa haokoki kwa wingi wa nguvu. Farasi hafai kitu kwa wokovu, Wala hamponyi mtu kwa wingi wa nguvu zake. Tazama, jicho la Bwana li kwao wamchao, Wazingojeao fadhili zake.”

Kwa hiyo haijalishi ukubwa wa changamoto zinazokukabili, haijalishi nguvu ya yule unayepambana nawe kama ilivyokuwa kwa Daudi liitie jina la Bwana na Mungu atajifunua kwako kutoka katika pembe ya kile unachokabiliana nacho ukijua wazi ya kuwa hakuna aliye kama yeye  naye atatenda mambo makuu, Nani aliye kama Bwana?


Umponyaye masikini na mtu aliye hodari! 

Zaburi 35:10b “Mifupa yangu yote itasema, Bwana, ni nani aliye kama Wewe? Umponyaye maskini na mtu aliye hodari kumshinda yeye, Naam, maskini na mhitaji na mtu amtekaye.”

Neno Umponyaye  hapa linaweza pia kutumika sambamba ba Uokoaye, Kwamba mtu wa Mungu anaweza kupitia katika hali ngumu na mateso na usumbufu wa mwili, nasfi na roho lakini hatimaye Bwana anaweza kukuokoa nayo yote, na  anaweza kukuponya nayo yote,  Maandiko yanaonyesha wakati wote tunapokabilia na mambo magumu ya kuumiza nafsi zetu, iwe ni magonjwa, iwe ni migogoro ya ndoa, migogoro ya malezi, migogoro ya kazini, migogoro ya maisha, kesi mahakamani, kukosa ada za shule, umasikini, mateso magonjwa ya aina mbalimbali, njaa, madeni, uonevu wa mirathi, uonevu wa mipaka ya shamba, kusalitiwa, kuogombana, vita baridi na kurushiana maneno huku na kule  nataka nikuhakikishie ya kuwa tukimlilia Bwana kwa mapenzi yake akaamua kutujibu atatutoa katika hali zote zinazotukabili.

Zaburi 34: “Walilia, naye Bwana akasikia, Akawaponya na taabu zao zote. Bwana yu karibu nao waliovunjika moyo, Na waliopondeka roho huwaokoa. Mateso ya mwenye haki ni mengi, Lakini Bwana humponya nayo yote.”

Hakuna changamoto ambayo Bwana hawezi kuitatua yeye anayaweza yote yeye ni mponyaji wa nafsi zetu na ni mwokozi wa kila janga linalotukabili  hata kama tunaweza kupita katika hali ngumu kwa sababu ya kuweko Duniani na kuweko kwa shetani, ni Muhimu kufahamu kuwa tutaokolewa katika hayo yote yanayotukabili labda kama Mungu sio Muaminifu kwa neno lake! Jambo ambalo haliwezekani kwa sababu uaminifu wake unadumu kizazi hata kizazi

2Timotheo 3:10-11 Bali wewe umeyafuata mafundisho yangu, na mwenendo wangu, na makusudi yangu, na imani, na uvumilivu, na upendo, na saburi; tena na adha zangu na mateso, mambo yaliyonipata katika Antiokia, katika Ikonio, na katika Listra, kila namna ya adha niliyoistahimili, naye Bwana aliniokoa katika hayo yote.”

Jambo kubwa la msingi ni kumtumainia Bwana na kumuweka yeye mbele naye atafanya kitu, yeye ni mwenye nguvu,  na uwezo wa kutukinga na kila kilicho hodari duniani anao kwa msingi huo wakati wote tunapopita katika wakati mgumu tukimtumainia yeye tutasimama tena,  Umponyaye maskini na mtu aliye hodari kumshinda yeye, Naam, maskini na mhitaji na mtu amtekaye.” Masikini katika luga ya kiebrania hapo linatumika neno ANIY ambalo maana yake ni mtu awaye yote ambaye yuko katika hali ya kudhikika, kuanzia kwenye akili mpaka katika mazingira ya kawaida, mtu mnyonge, mwenye uhitaji, masikini, aliyeonelewa, mtumwa, aliyechukuliwa mateka, mtu wa hadhi ya chini, mgonjwa anayeonewa na kitu chenye nguvu kiasi cha kumuumiza Hali zote hizo bwana hawezi kukubali hata kidogo, yeye huingilia kati na kuokoa na kuponya. Jambo kubwa la ziada ni kumtumaini yeye kama asemavyo;

Mithali 3:5-6. “Mtumaini Bwana kwa moyo wako wote, Wala usizitegemee akili zako mwenyewe; Katika njia zako zote mkiri yeye, Naye atayanyosha mapito yako.”

Na Rev. Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima.
     



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni