Jumapili, 23 Juni 2024

Naye alikuwa hana budi kupita katikati ya Samaria.


Yohana 4:1-10 “Kwa hiyo Bwana, alipofahamu ya kuwa Mafarisayo wamesikia ya kwamba, Yesu anafanya wanafunzi wengi kuliko Yohana, na kuwabatiza, (lakini Yesu mwenyewe hakubatiza, bali wanafunzi wake,) aliacha Uyahudi, akaenda zake tena mpaka Galilaya.  Naye alikuwa hana budi kupita katikati ya Samaria. Basi akafika kunako mji wa Samaria, uitwao Sikari, karibu na lile shamba ambalo Yakobo alimpa Yusufu mwanawe. Na hapo palikuwa na kisima cha Yakobo. Basi Yesu, kwa sababu amechoka kwa safari yake, akaketi vivi hivi kisimani. Nayo ilikuwa yapata saa sita. Akaja mwanamke Msamaria kuteka maji. Yesu akamwambia, Nipe maji ninywe. Kwa maana wanafunzi wake wamekwenda mjini kununua chakula. Basi yule mwanamke Msamaria akamwambia, Imekuwaje wewe Myahudi kutaka maji kwangu, nami ni mwanamke Msamaria? (Maana Wayahudi hawachangamani na Wasamaria.) Yesu akajibu, akamwambia, Kama ungaliijua karama ya Mungu, naye ni nani akuambiaye, Nipe maji ninywe, ungalimwomba yeye, naye angalikupa maji yaliyo hai.”



Utangulizi:

Leo tutachukua muda kujifunza mojawapo ya masomo ya Msingi sana katika Maisha na mafundisho ya Bwana wetu Yesu Kristo ili kujifunza jambo moja la msingi sana tunapofanya kazi ya kuieneza injili, na jambo hili lina uhusiano na kuvunja mipaka ya kijamii, kiimani, kidini, kisiasa, kiitikadi, kiadui na rangi, na kuhakikisha kuwa tunasambaza upendo wa Mungu kwa watu wote sawasawa na agizo kuu la Bwana wetu la kuihubiri injili na kuwafanya mataifa yote kuwa wanafunzi wake na kuwabatiza.

Mathayo 28:18-20 “Yesu akaja kwao, akasema nao, akawaambia, Nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani. Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu; na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi; na tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku zote, hata ukamilifu wa dahari.”

Katika kujifunza somo hili muhimu lenye kichwa, Naye alikuwa hana budi kupita katikati ya Samaria, ambalo kimsingi litazungumzia mazingira mazima ya mazungumzo ya Yesu na mwanamke Msamaria katika Yohana 4:1-42 pamoja na matokeo ya mazungumzo hayo kwa ujumla, tutaligawa somo hili katika vipengele vitatu muhimu:-

 

·         Uhusiano wa Wayahudi na Wasamaria.

·         Naye alikuwa hana budi kupita katikati ya Samaria.

·         Matokeo ya kupita kwa Yesu pale Samaria

 

 

Uhusiano wa Wayahudi na Wasamaria.

Ni muhimu kuwa na ufahamu, kwamba moja ya safari Muhimu sana ambayo ina maswala mengi sana ya kutufunza ni pamoja na safari hii ya Yesu Kristo kupita katika jimbo la Samaria, Kimsingi katika wakati huu Yesu alikuwa amejipatia umaarufu mkubwa sana kuliko Yohana Mbatizaji, Na mafarisayo walianza kuchukizwa na Yesu kwa sababu walianza kupoteza umaarufu wao na mamlaka yao,  na hivyo hawakuwa na furaha sana na uwepo wa Yesu, kwa hivyo Yesu alilazimika kuondoka kwaajili ya kuepusha migogoro na mafarisayo ambao kimsingi walishaanza kutafuta namna na njama za kutaka kumuangamiza,kabla ya muda wake halisi wa kusulubiwa.

Yohana 4:1-3 “Kwa hiyo Bwana, alipofahamu ya kuwa Mafarisayo wamesikia ya kwamba, Yesu anafanya wanafunzi wengi kuliko Yohana, na kuwabatiza, (lakini Yesu mwenyewe hakubatiza, bali wanafunzi wake,) aliacha Uyahudi, akaenda zake tena mpaka Galilaya.”

Yesu alikuwa amekwishakuwa maarufu pande zote Uyahudi na Galilaya na jamii kubwa ya watu walikuwa wakimfuata kila aliko, kwa hiyo ili kupata nafasi ya kupumua aliazimia kupita Samaria (Alikuwa hana budi maana yake  ilikuwa lazima) Biblia ya kiingereza inatumia maneno “And he must needs go through Samaria”  neno Must needs katika kiyunani linatumika neno DEI  au DEON kwa kiingereza Necessary yaani ilikuwa ni muhimu, ilikuwa ni lazima, ilikuwa kuna jambo la msingi la kukutana nalo, kwa sababu maalumu, ikiwa ni pamoja na kupunguza kwa kiwango fulani mkakati wa mafarisayo kumuwinda na kutaka kumwangamiza, lakini kulikuwa na uhitaji wa kiungu.

Marko 3:6-10 “Mara wakatoka wale Mafarisayo, wakawa wakifanya shauri juu yake pamoja na Maherodi, jinsi ya kumwangamiza. Naye Yesu akajitenga, yeye na wanafunzi wake, akaenda baharini. Mkutano mkuu ukamfuata, kutoka Galilaya, na Uyahudi, na Yerusalemu, na Idumaya, na ng'ambo ya Yordani, na pande za Tiro na Sidoni, mkutano mkuu, waliposikia habari za mambo yote aliyokuwa akiyatenda, wakamwendea. Akawaambia wanafunzi wake ya kwamba chombo kidogo kikae karibu naye, kwa sababu ya mkutano, wasije wakamsonga. Maana aliponya wengi, hata wote waliokuwa na misiba wakamrukia wapate kumgusa.”

Kwaajili ya hayo Yesu anakusudia kupita katikati ya Samaria, Samaria lilikuwa mojawapo ya jimbo kati ya majimbo makubwa matatu katika taifa la Israel, kusini kulikuwa na jimbo la Uyahudi (Yudea) na Kaskazini kulikuwa na jimbo la Galilaya, na katikati lilikuwepo jimbo la Samaria, kwa kawaida wayahudi halisi waliishi Yudea na Galilaya na wale wenye kuishika Imani sana walipotaka kwenda Galilaya au kuja Uyahudi hawakuthubutu kupita katikati ya Samaria kwani kufanya hivyo ilikuwa ni sawa na kujitia unajisi, na sababu kubwa ni kuwa kulikuwa na uhasama wa kihistoria kati ya Wayahudi na Wasamaria, hivyo Wayahudi walipokuwa wakienda Galilaya walilazimika kupita njia ndeefu kuzunguka nje ya Samaria kuliko kupita kati kati yake yaani Samaria ambayo kimsingi ilikuwa ndio njia fupi.

Wayahudi na Wasamaria walichukiana sana na hawakuwa hata na muda wa kuzungumza wao kwa wao, Sababu kubwa ni kuwa Wasamaria walikuwa ni Wayahudi hapo zamani, Lakini Israel ya kaskazini ilipovamiwa na Waashuru na watu wengi kuchukuliwa utumwani mwaka wa 722 KK.  Mfalme wa Ashuru aliwaleta wageni wengi sana kuikalia nchi ya Samaria, na wageni hawa walizaliana na waisrael waliobaki na hivyo kukazaliwa machotara wa kiyahudi na wageni na kwa sababu hiyo jamii hii ilianza kuabudu miungu na kujihusisha na tabia za mataifa wasio wayahudi.

2Wafalme 17:23-33 “hata Bwana akawaondoa Waisraeli wasiwe mbele zake, kama vile alivyosema kwa kinywa cha watumishi wake wote, manabii. Basi Waisraeli walichukuliwa mateka kutoka nchi yao wenyewe, waende nchi ya Ashuru, hata leo. Naye mfalme wa Ashuru akaleta watu kutoka Babeli, na Kutha, na Ava, na Hamathi, na Sefarvaimu, akawaweka katika miji ya Samaria badala ya wana wa Israeli; wakaumiliki Samaria, wakakaa katika miji yake. Basi ikawa, wakati ule walipoanza kukaa huko, hawakumcha Bwana; kwa hiyo Bwana akapeleka simba kati yao, nao wakawaua baadhi yao. Kwa hiyo wakamwambia mfalme wa Ashuru, wakasema, Wale wa mataifa uliowahamisha, na kuwaweka katika miji ya Samaria, hawaijui kawaida ya Mungu wa nchi; kwa hiyo amepeleka simba kati yao, na tazama, wanawaua, kwa sababu hawaijui kawaida ya Mungu wa nchi. Ndipo mfalme wa Ashuru akatoa amri, akasema, Mpelekeni mmojawapo wa makuhani, mliowachukua kutoka huko; aende akakae huko, akawafundishe kawaida ya Mungu wa nchi. Basi mmoja wa makuhani waliochukuliwa kutoka Samaria akaenda akakaa katika Betheli, akawafundisha jinsi ilivyowapasa kumcha Bwana. Lakini pamoja na hayo watu wa kila taifa wakajifanyia miungu yao wenyewe, wakaiweka katika nyumba za mahali pa juu, walipopafanya Wasamaria, kila taifa katika miji yao walimokaa. Watu wa Babeli wakafanya Sukoth-benothi kuwa mungu wao, watu wa Kutha wakafanya Nergali, watu wa Hamathi wakafanya Ashima, Waavi wakafanya Nibhazi na Tartaki; nao Wasefarvi wakawaunguza wana wao katika moto kwa Adrameleki na Anameleki, miungu ya Sefarvaimu. Basi hivyo wakamcha Bwana, nao wakijifanyia wengine wao kuwa makuhani wa mahali pa juu, ambao waliwafanyia dhabihu katika nyumba za mahali pa juu. Wakamcha Bwana, na kuitumikia miungu yao wenyewe, sawasawa na kawaida za mataifa ambao wao walihamishwa kutoka kwao.”

Kitendo cha wasamaria hawa kumwacha bwana na kuanza kutumikia miungu mingine kilijenga chuki kubwa sana kati ya wayahudi na wasamaria, lakini hata hivyo mpaka wakati wa Yesu baadhi walikuwa wanamwabudu Mungu wa kweli, lakini hata hivyo waliabudu katika mlima Gerizimu na ambapo pia palijengwa hekalu hapo, lakini wayahudi walilibomoa kabisa na hivyo kuongeza uhasama mkubwa baina yao, kwa hiyo uadui  wao ukawa mkubwa, Wayahudi waliwadharau sana Wasamaria, waliwaona kama watu waliopoteza utakatifu wao kwa kujichanganya na mataifa mengine, ambao walikuwa washirikina na wachawi na kamwe hawakuwahi wayahudi kufikiri kuwa Wasamaria wako sahihi, Mlima Gerizimu ni moja kati ya milima miwili iliyoko nchini Israel katika mji uitwao Nablus leo, lakini zamani paliitwa Shekemu, Neno Gerizim ni neno la kiarabu kumaanisha Jabal kwa kiibrania ni Argarizem  na mlima mwingine uliitwa Ebal.  Na wasamaria wengi waliishi chini ya mlima Gerizim, mlima huo ulifikiriwa kuwa mtakatifu.

Yohana 4:20 -23 “Baba zetu waliabudu katika mlima huu, nanyi husema ya kwamba huko Yerusalemu ni mahali patupasapo kuabudia. Yesu akamwambia, Mama, unisadiki, saa inakuja ambayo hamtamwabudu Baba katika mlima huu, wala kule Yerusalemu. Ninyi mnaabudu msichokijua; sisi tunaabudu tukijuacho; kwa kuwa wokovu watoka kwa Wayahudi.Lakini saa inakuja, nayo sasa ipo, ambayo waabuduo halisi watamwabudu Baba katika roho na kweli. Kwa maana Baba awatafuta watu kama hao wamwabudu.”

Uhasama baina ya wayahudi na wasamaria ukageuka kuwa uhasama wa kiimani, uhasama wa kiitikadi, uhasama wa ki ubaguzi, uhasama wa kisiasa na hata kijiografia,  Wasamaria waliamini vitabu vitano tu vya Musa na hawakutaka kuamini katika vitabu vingine hivyo walimtambua Musa tu na yule aliyetabiriwa na Musa tu yaani Masihi na yeye ndiye waliyekuwa wakimsubiria.

Kumbukumbu 18:15 “Bwana, Mungu wako, atakuondokeshea nabii miongoni mwa ndugu zako kama nilivyo mimi; msikilizeni yeye.”          

Uhasama wao ulipelekea kuchukiana kiasi ambacho hata kijiografia ilikuwa ni ngumu sana kwa myahudi wa kawaida kupita katikati ya Samaria akielekea Galilaya na badala yake walilazimika kupita njia ndefu ya kuzunguka yaani kuizunguka Samaria badala ya kupita katikati ya Samaria, sasa basi kwa mara ya Kwanza baada ya miaka mingi sana ndio tunamuona sasa Yesu akilazimika kupita Samaria kwa sababu maalumu za kimkakati katika kuwahudumia watu

Naye alikuwa hana budi kupita katikati ya Samaria.

Yesu Kristo akiwa na moyo wa tofauti kabisa na wayahudi wengine Yeye aliona iko haja ya kupita katikati ya Samaria, sio tu kwa sababu, Mafarisayo walikuwa na mpango wa kumwangamiza, bali pia ziko sababu nyingi sana na mambo mengi sana ya kujifunza kutokana na ziara hii ya kijasiri ya Yesu Kristo! Ambayo ilikuwa ziara ya kimkakati katika kuifikisha huduma ya injili kwa watu waliokataliwa lakini pia kwaajili ya kutufunza maswala kadhaa muhimu sana

1.       Injili ni kwa watu wote – Yesu alikuwa amekuja ulimwenguni kwaajili ya watu wote na sio kwaajili ya Wayahudi peke yao, Kupita Samaria na kuzungumza na yule Mwanamke na hata matokeo yake kunadhihirisha wazi kuwa injili yake na habari njema zinamuhusu kila mmoja duniani, watu wenye ukomavu kiroho, na kisiasa, wanashinda kabisa mipaka ya kibaguzi na kuvuka mipaka ya kawaida ya kibinadamu  na kumuiita kila mmoja kushiriki neema ya Mungu bila kujali, itikadi, historia, ukoo, rangi, uchotara, siasa yake na kadhalika na zaidi ya yote kuufikia ulimwengu mzima hata kwa wale tunaofikiria kuwa ni maadui zetu.

 

Tito 2:11-13 “Maana neema ya Mungu iwaokoayo wanadamu wote imefunuliwa; nayo yatufundisha kukataa ubaya na tamaa za kidunia; tupate kuishi kwa kiasi, na haki, na utauwa, katika ulimwengu huu wa sasa; tukilitazamia tumaini lenye baraka na mafunuo ya utukufu wa Kristo Yesu, Mungu mkuu na Mwokozi wetu;”

 

Yohana 3:16 -17 “Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele. Maana Mungu hakumtuma Mwana ulimwenguni ili auhukumu ulimwengu, bali ulimwengu uokolewe katika yeye.”             

 

Kila mtu anayedai ya kuwa anamfuata Yesu hana budi kuhakikisha ya kuwa anawafikia watu wote bila ubaguzi, hubiri kila mahali, kuna watu wanadhani iko jamii ya watu Fulani tu ndio wanaohitaji injili Yesu aliivunja mipaka hiyo na anatufundisha kivitendo ya kuwa ni lazima injili imfikie kila mtu, awe Mwafrika, awe Mzungu, awe Muasia, awe Mwarabu, awe muislamu, awe mbudha, awe mhindu, awe Singasinga, awe Mjapani (Shintoism), awe Mchina (Taoism na Comfucianism) na kadhalika ni wajibu wetu kuhakikisha injili inapenya na kufika kila mahali hata kwa watu ambao tuna historia nao mbaya,  wanaotuchukia, hawatupendi, hawatukubali,  ni lazima tutafute njia ya kuwafikia kwa upendo. Ziara ya hii  ya Bwana iliweka Msingi kwa wanafunzi wa Yesu ambao baadaye walishuka Samaria  na kuhihubiri injili na Samaria ikaipokea injili na watu  wakatubu na wakajazwa Roho Mtakatifu na kukawa na uamsho mkubwa sana

 

2.       Kuleta Maridhiano – Pamoja na mafundisho kadhaa wa kadhaa Yesu kwa kupita kwake Samaria kama kiongozi mkubwa sana Duniani na mbinguni anatufundisha umuhimu wa Maridhiano, Yeye kwa kuonyesha mfano anaonyesha na kufunua ukweli mpya wa kiroho ya kuwa kupitia injili watu wake wanaweza kuonyesha upendo, yeye akiwa Myahudi wa mfano anaonyesha ya kuwa sio kuwa karanga moja ikioza ndio zote, anaonyesha ya kuwa Sasa yeye kama Myahudi halisi na wa kweli anavunja mipaka ya kibaguzi,  na kustawisha uhusiano na kuvunja ubinafsi na ubaguzi uliokuwepo kati ya Wayahudi na Wasamaria. Kila Mkristo aliyekomaa kiroho na mwenye ujuzi wa juu sana anaweza kuwa njia na daraja la kuwapatanisha watu kwa Mungu, hata bila ya kusubiri adui akunyenyekee, ni sisi ndio ambao tunaweza kuchukua hatua za kuvunja kuta za uadui na kuwafikia wengine, Kama Yesu asingelichukua hatua uadui kati ya wasamaria na wayahudi ungedumu, Lakini aliye na afya nzuri ya kiroho ndiye aliyekuwa wa kwanza kuuvunja uadui huo na jambo hili lilimshangaza mwanamke msamaria kwa sababu alijua sio kawaida Myahudi kuchukua hatua ngumu kama hii, na alijiuliza inakuwaje? Je wewe unasubiri adui yako ndio achukue hatua? Aje akunyenyekee na kukuomba? Yesu alikuwa wa kwanza kuchukua hatua na ikawashangaza sana wasamaria

 

Yoahana 4:9-10 “Basi yule mwanamke Msamaria akamwambia, Imekuwaje wewe Myahudi kutaka maji kwangu, nami ni mwanamke Msamaria? (Maana Wayahudi hawachangamani na Wasamaria.) Yesu akajibu, akamwambia, Kama ungaliijua karama ya Mungu, naye ni nani akuambiaye, Nipe maji ninywe, ungalimwomba yeye, naye angalikupa maji yaliyo hai.”

 

Mungu anataka tuwashangaze wakati wote wale wanaojifikiria kuwa ni maadui zetu kwa kuwatendea mema, linapokuja swala la injili hakuna adui, hakuna mtu asiyestahili kufikiwa na upendo wa Mungu kwa sababu zozote zile, Kanisa ni lazima lijipange kuhakikisha kuwa injili inawafikia watu wote hata wale ambao tunadhani kuwa hawastahili, Wayahudi walikuwa ndio watu wa kwanza kuteuliwa na Mungu ili waweze kuwa Baraka kwa ulimwengu mzima, ingekuwa ni hasara kubwa sana kama wayahudi wangesahau wajibu wa kuvunja mipaka na kupeleka Baraka hizo kwa mataifa mengine, Na ashukuriwe Mungu kwamba Yesu kiongozi mkuu wa wokovu wetu anakuwa wa kwanza kuonyesha mfano huo kwa kuvunja mipaka ya kiadui, kibaguzi, kikabila, kidini, kitamaduni na kijimbo kwa kuifikisha injili kila mahali wakiwemo Wasmaria.

 

3.        Kufunua Mpango wa Mungu – Katika mpango wa Mungu kulikuwa na umuhimu sana wa ziara ya Yesu kule Samaria, nawe utakubaliana nami kuwa kulikuwa na mpango mahususi wa kiungu kwa Yesu kukutana na mwanamke huyu mjadala wao unatupa mafunzo makubwa sana kuanzia na mafundisho ya kweli na mpaka namna ya kuabudu na mafundisho sahihi ambayo yangeifaa sana jamii ya leo, Mazungumzo ya Kristo na mwanamke Msamaria yanatufunulia kweli kadhaa za muhimu katika Imani yetu kama tunavyoweza kuona

 

a.       Mungu ni Roho – Katika mazungumzo ya Yesu na Mwanamke Msamaria kuna mafundisho mengi ya msingi na moja ya Fundisho hilo ni kuwa Mungu ni Roho, Wayahudi waliamini kuwa sehemu sahihi ya kuabudu ni Yerusalem, na Wasamaria waliamini ya kuwa Mungu anapatikana katika Mlima Gerizimu, Lakini Yesu anaonyesha kuwa wakati sahihi unakuja ambapo watu watamuabudu Mungu sio kule Yerusalem wala kule Gerizimu, Lazima ufikie wakati watu wajue ya kuwa Mungu hapatikani katika mahekalu yaliyojengwa kwa mikono, wala hapatikani milimani, Mungu ni ROHO, mkao wako wa kiroho bila kujali uko wapi utamfanya Mungu akutembelee sawa na kiu uliyo nayo moyoni mwako, huitaji leo kwenda mahali Fulani kumtafuta Mungu kwani Mungu anapatikana kila mahali popote ulipo endapo tu utafungua moyo wako, Mungu yuko mahali kote na anapatikana kwa kila mtu amtafutaye kwa Moyo

 

Matendo 7:48-50 “Ila Yeye aliye juu hakai katika nyumba zilizofanywa kwa mikono, kama vile asemavyo nabii, Mbingu ni kiti changu cha enzi, Na nchi ni pa kuwekea miguu yangu; Ni nyumba gani mtakayonijengea? Asema Bwana, Au ni mahali gani nitakapostarehe? Si mkono wangu uliofanya haya yote?

 

Matendo 17:24-27 “Mungu aliyeufanya ulimwengu na vitu vyote vilivyomo, yeye, kwa kuwa ni Bwana wa mbingu na nchi, hakai katika hekalu zilizojengwa kwa mikono; wala hatumikiwi kwa mikono ya wanadamu kana kwamba anahitaji kitu cho chote; kwa maana ndiye anayewapa wote uzima na pumzi na vitu vyote. Naye alifanya kila taifa la wanadamu kutoka katika mmoja, wakae juu ya uso wa nchi yote, akiisha kuwawekea nyakati alizoziamuru tangu zamani, na mipaka ya makazi yao; ili wamtafute Mungu, ingawa ni kwa kupapasa-papasa, wakamwone, ijapokuwa hawi mbali na kila mmoja wetu.”

 

Ibada ya kweli haitegemei mahali, inategemea mkao wa Moyo wako, Mungu hawi mbali na yeyote anayemtafuta kwa dhati, uende milimani usiende, Yesu alitufundisha kupitia mwanamke huyu na kutupa kuelewa namna na jinsi inavyopaswa kumuabudu Mungu, Sio kwa sababu Ibrahimu na Isaka na Yakobo waliabudu katika mlima huo, basi na Mungu angepatikana katika mlima huo, Mungu ni Roho maana yake Mungu hapatikani katika namna ya asili kama wanadamu ambao wao wanafungwa na mipaka ya kijiografia, Mungu hana mwili kama huu wa kibinadamu, Yeye kwa kuwa ni roho hana mipaka na hivyo huwezi kumfungia Mungu katika mahali Fulani maalumu, kwani yeye yuko mahali pote na anapatikana kila mahali, kwa hiyo kupitia roho yako, na kujitoa kwako kwa moyo  unaweza kumpata Mungu  zaidi ya yote Msaada wa Roho Mtakatifu ndani yetu, yeye anayeweza kuiinua dhamiri yetu na kutuvuvia kumtafuta kwa msaada wake tunaweza kujiungamanisha na Mungu popote tulipo, ikiwa tu tunakuwa na dhamira ya kweli ya kumtafuta sawasawa na neno lake na kupitia Yesu ambaye ndiye ufunuo wa kweli, na zaidi ya yote ndani ya mwili wetu ambao ni hekalu la Roho Mtakatifu, Mungu anaweza kuwasiliana nasi na tunaweza kumuabudu yeye popote tulipo tukiamua tu kuwa katika roho na kumsikiliza kiibada

 

Yohana 14:6 “Yesu akamwambia, Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi.” Yohana 17:17 “Uwatakase kwa ile kweli; neno lako ndiyo kweli.”

 

1Wakorintho 6:19-20 “Au hamjui ya kuwa mwili wenu ni hekalu la Roho Mtakatifu aliye ndani yenu, mliyepewa na Mungu? Wala ninyi si mali yenu wenyewe; maana mlinunuliwa kwa thamani. Sasa basi, mtukuzeni Mungu katika miili yenu.”

 

b.      Maji ya Uzima – Mazungumzo ya Kristo na mwanamke huyu yalianzia kisimani, na yalianza kwa Yesu kuomba maji, Yesu aliomba maji ya kawaida, Na mwanamke huyu alisita kutokana na ubaguzi uliokuwepo, na mshangao na ndipo Yesu akajibu, akamwambia, Kama ungaliijua karama ya Mungu, naye ni nani akuambiaye, Nipe maji ninywe, ungalimwomba yeye, naye angalikupa maji yaliyo hai.  Maji yaliyo hai kwa kimasai Engare Embuani, Katika lugha ya kiebrania linatumika neno “Mayim Chayim” yaani Mayim maana yake maji na Chayim maana yake uzima au uhai,  Hii ilikuwa na maana ya maji yasiyo na chumvi wala magadi, Maji masafi yanayotiririka  maji ya aina hiyo yaliaminiwa kuwa yalikuwa ni maji bora na safi na salama  na anayeweza kuwapa watu maji ya aina hiyo ilisadikiwa kuwa chanzo chake ni Mungu tu na ndio maana mwanamke Msamaria alimshangaa Yesu kuwa huenda ni mkuu kuliko Ibrahimu na Isaka na Yakobo waliowaachia kisima kile.

 

Yeremia 2:13 “Kwa maana watu wangu hawa wametenda maovu mawili; wameniacha mimi, niliye chemchemi ya maji ya uzima, wamejichimbia mabirika, mabirika yavujayo, yasiyoweza kuweka maji.”

 

Kwa hiyo Maji ya uzima yalikuwa yanawakilisha Mungu mwenyewe ambaye ndiye chanzo cha uhai na uzima wa wanadamu wote, Ni Mungu pekee ndiye anayeitwa kisima cha maji yaliyo hai au chemichemi ya maji ya uzima, Kwa hiyo kimsingi Yesu alikuwa anajitambulisha kuwa yeye ndiye chemichemi hiyo mya maji ya uzima. Na unapomuacha Mungu maana yake umeenda mbali na kisima cha maji yaliyo hai.

 

Yeremia 17:13 “Ee Bwana, tumaini la Israeli, wote wakuachao watatahayarika. Wao watakaojitenga nami wataandikwa katika mchanga, kwa sababu wamemwacha Bwana, kisima cha maji yaliyo hai.”

 

Katika lugha ya kiyunani (Greek) neno linalotumika kuelezea maji ya uzima ni “Hydor zōn” “Hydor” likiwa na maana ya maji na zōn ikiwa na maana ya Uzima Kwa hiyo Yesu alipozungumzia  maji yaliyo hai au maji ya uzima alikuwa anazungumzia kile chanzo cha uzima wa milele, Yesu alikuwa anamaanisha jambo kubwa sana zaidi ya kiu ya kawaida ya maji ya kimwili, Yesu alikuwa akizungumzia utoshelevu kwa kiu ya wale wanaomtafuta Mungu unatoka kwake na yeye ndiye chanzo hicho yeye ndiye anayetoa utoshelevu huo, kama mtu anahitaji utoshelevu wa kweli wa kiibada na kiimani basi Yesu ndiye halisi.

 

Yohana 4:13-14 “Yesu akajibu, akamwambia, Kila anywaye maji haya ataona kiu tena; walakini ye yote atakayekunywa maji yale nitakayompa mimi hataona kiu milele; bali yale maji nitakayompa yatakuwa ndani yake chemchemi ya maji, yakibubujikia uzima wa milele.”

 

Kwa hiyo hapa Yesu anatumia mfano wa maji kuzungumzia kitu Fulani au chanzo Fulani ambacho ndio chanzo halisi cha maisha ya kiroho na uzima wa milele. Na ule uzima wa milele unaitwa ZOE kwa kiyunani ambalo kwa kiingereza ni God-Kind of life maisha ya umilele kama Mungu au maisha ya milele yanayotokana na kuungwa na Mungu. Ni dhahiri kuwa mwanamke yule ingawa alikuwa mwenye dhambi, lakini ndani yake alikuwa na kiu ya kutaka kumjua Mungu, na kiu ya kumuabudu Mungu, hakuwa kichwa tupu tu, alikuwa anajua pia kuwa masihi angekuja na angeweza kuleta majibu ya namna na jinsi iwapasavyo kuabudu, kiu yake ilikuwa imejibiwa kwa kuwa yeye aliyekuwa akisema naye alikuwa ndiye Masihi mwenyewe, na ndiye chanzo cha uzima na maji ya uzima, Kwa hiyo unaweza kuona kuwa ufunuo huu tusingeliupata kama Yesu asingelipita Samaria. Sio hivyo tu wale watu tunaoweza kuwaweka katika kundi la wat wasiofaa na tukawahukumu kama makahaba, au Malaya usije ukafikiri ya kuwa kichwani mwao hakuna kitu kabisa, au usije ukawahukumu na kufikiri kuwa hawastahili habari njema kila mwanadamu duniani bila kujali shetani amemuharibu kwa kiwango gani ndani yake iko kiu ya kumuhitaji Mungu na ni wajibu wetu kama wanafunzi wa Yesu kuyafikia makundi yote bila dharau kama za kifarisayo, na kuwapelekea injili hii ya uzima bila ubaguzi, wala kuwahukumu paleka habari njema kwao

 

c.       Nenda kamuite mumeo - Kuna kitu cha Ziada cha kujifunza tena na tena katika mazungumzo ya Yesu na Mwanamke Msamaria, Yesu alikuwa anayajua maisha ya Mwanamke huyu mwanzo mwisho,  na alikuwa anajua mahitaji yake ya kiroho, mwanamke huyu alikuwa anaishi maisha ya zinaa/alikuwa anaishi katika dhambi, Lakini alikuwa anajua maswala kadhaa ya kiroho, na ndio maana Yesu Hakumdharau hata kidogo alikuwa anataka kumsaidia na kuwasaidia na wengine katika siku za leo, Somo kuhusu maji ya uzima lilikuwa bado halijaeleweka kwa mwanamke huyu na alikusudia kubadilisha mada, Yesu akiwa anaelewa anachokifanya alimueleza nenda kamuite mumeo!

 

Mwanamke huyu hakutaka kuzungumza kuhusu mumewe wa sasa wala aliyekuweko nyumbani kwa hiyo alidanganya kuwa hana mume! Ni Kama aliyekuwa anasema shiishi na mume, Lakini pamoja na kuwa mwanamke huyu alikuwa akijaribu kumdanganya Yesu, ni ukweli ulio wazi kuwa jibu lake lilikuwa ni kweli, kwanini? Mwanamke huyu alikuwa anaishi na mwanaume ambaye hakuwa mume wake kihalali, na kwa mujibu wa sheria za Kiyahudi kama mwanamke mume wake wa kwanza bado yuko hai, na mwanamke huyu akaishi na mwanaume mwingine maana yake mwanamke huyu anaishi katika uzinzi

 

Marko 10:11-12 “Akawaambia, Kila mtu atakayemwacha mkewe na kuoa mwingine azini juu yake; na mke, akimwacha mumewe na kuolewa na mtu mwingine, azini.”

 

Warumi 7:2-3 “Kwa maana mwanamke aliye na mume amefungwa na sheria kwa yule mume wakati anapokuwa yu hai; bali akifa yule mume, amefunguliwa ile sheria ya mume. Basi wakati awapo hai mumewe, kama akiwa na mume mwingine huitwa mzinzi. Ila mumewe akifa, amekuwa huru, hafungwi na sheria hiyo, hata yeye si mzinzi, ajapoolewa na mume mwingine.”        

 

Hatuwezi kumdanganya Mungu kwa sababu zozote zile kwa sababu Mungu anajua kila kitu, Yesu alikuwa anamjua mwanamke huyu na asingeliweza kujificha, katika nyakati zetu leo, Ndoa za kikristo zinachukuliwa poa sana, wako watu wanafanya zinaa, zile za kuibia, lakini ziko zinaa zimepitishwa kiofisi, wako watu wamefungishwa ndoa kwenye makanisa ya kiroho, na wengine ni watu wanaoheshimika sana katika imani, watumishi wa Mungu na kadhalika leo wanaweza kusema kuwa ninawahukumu, mimi simuhukumu yeyote yule lakini Neno la Mungu linasimama leo na kutukumbusha wajibu wetu ya kuwa mwanaume na mwanamke wakristo kama uko kwenye ndoa nyingine na mumeo au mkeo bado yuko hai wewe una kesi ya kujibu kimaandiko  na kwa sababu hiyo, unapaswa kurudi kwa mkeo au mume au ukae hivyo hivyo bila kuoa au kuolewa kama yalivyo mfundisho ya Bwana ona, yeye Bwana amekataa kuwa hakuna sababu za mtu aliye katika Kristo kumuacha mkewe, Mungu haamini ya kuwa iko sababu inayoweza kupelekea wewe kama mwamini ukaacha ndoa yako halisi, au mkeo au mumeo halisi na ukapuuza lile agano na kuishi kinyumba, kama tu vile unavyoamini kuwa hakuna dhambi Mungu hawezi kusamehe, Basi Mungu naye anaamini hakuna dhambi inayoweza kusababisha wewe uachane na ndoa.

 

Mathayo 19:3-9 “Basi Mafarisayo wakamwendea, wakamjaribu, wakimwambia, Je! Ni halali mtu kumwacha mkewe kwa kila sababu? Akajibu, akawaambia, Hamkusoma ya kwamba yeye aliyewaumba mwanzo, aliwaumba mtu mume na mtu mke, akasema, Kwa sababu hiyo, mtu atamwacha babaye na mamaye, ataambatana na mkewe; na hao wawili watakuwa mwili mmoja? Hata wamekuwa si wawili tena, bali mwili mmoja. Basi aliowaunganisha Mungu, mwanadamu asiwatenganishe. Wakamwambia, Jinsi gani basi Musa aliamuru kumpa hati ya talaka, na kumwacha? Akawaambia, Musa, kwa sababu ya ugumu wa mioyo yenu, aliwapa ruhusa kuwaacha wake zenu; lakini tangu mwanzo haikuwa hivi. Nami nawaambia ninyi, Kila mtu atakayemwacha mkewe, isipokuwa ni kwa sababu ya uasherati, akaoa mwingine, azini; naye amwoaye yule aliyeachwa azini.”

 

Safari ya Yesu katika mji wa Samaria pia ilijaa fundisho hili na inatukumbusha kuhakikisha ya kuwa tunaishi katika ndoa kwa usafi na mwenendo sawasawa na imani yetu katika Kristo na sio vinginevyo. Mungu ni Mungu wa utaratibu, inamshangaza Yesu Leo kuona watu wakiachana na wakati huo huo wakitaka kuoa tena au kuolewa tena ili hali wenzi wao wako hai, Katika eneo hili ni muhimu kujitafakari.

 

d.      Mavuno – Safari ya Bwana Yesu iliyo mlazimu kupita Samaria pia ilikuwa na faida kubwa kwa ufalme wa Mungu yaani kumvunia Bwana nasfi na roho za watu wengi sana, na hivyo kuzungumza na yule mwanamke ilikuwa ni chanzo tu cha kubadilisha moyo wake ili kisha aweze kuwaleta wasamaria wengi kwa Bwana

 

Yohana 4:27-38 “Mara hiyo wakaja wanafunzi wake, wakastaajabu kwa sababu alikuwa akisema na mwanamke; lakini hakuna aliyesema, Unatafuta nini? Au, Mbona unasema naye? Basi yule mwanamke akauacha mtungi wake, akaenda zake mjini, akawaambia watu, Njoni, mtazame mtu aliyeniambia mambo yote niliyoyatenda. Je! Haimkini huyu kuwa ndiye Kristo? Basi wakatoka mjini, wakamwendea.  Huko nyuma wanafunzi wakamsihi wakisema, Rabi, ule. Akawaambia, Mimi ninacho chakula msichokijua ninyi. Basi wanafunzi wake wakasemezana, Je! Mtu amemletea chakula? Yesu akawaambia, Chakula changu ndicho hiki, niyatende mapenzi yake aliyenipeleka, nikaimalize kazi yake. Hamsemi ninyi, Bado miezi minne, ndipo yaja mavuno? Tazama, mimi nawaambieni, Inueni macho yenu myatazame mashamba, ya kuwa yamekwisha kuwa meupe, tayari kwa mavuno.”

 

Yesu alikuwa na akili sana alifanya kazi ndogo kwa hekima iliyomletea matokeo makubwa sana, alimfundisha neno la Mungu mwanamke mmoja tu, lakini kupitia huyo alijikuta anazungumza na mji mzima, alikuwa akiwaza mavuno, na kwa kuvunja ukuta wa kiitikadi, kuvunja ukuta wa kiimani na kitamaduni na ubaguzi alifanikiwa kuwapata wengi nao wakamwamini hili lilikuwa ni jicho la Mavuno, Kristo anatukumbusha hapa kufanya kazi ya Mungu kwa akili sana na kuhakikisha ya kuwa tunamletea mavuno na katika kulitekeleza hili hatuna budi kufuata njia ya Mungu na kuacha kuwadharau watu, kwa sababu zozote zile, tuwaendee watu wa kila kabila na kila mila na tamaduni na kumzaliwa Bwana matunda, kwa kumletea mavuno hakuna mtu mbaya duniani ambaye hawezi kubadilishwa na neema  

 

Yohana 4:39-43 “Na katika mji ule Wasamaria wengi walimwamini kwa sababu ya neno la yule mwanamke, aliyeshuhudia kwamba, Aliniambia mambo yote niliyoyatenda. Basi wale Wasamaria walipomwendea, walimsihi akae kwao; naye akakaa huko siku mbili. Watu wengi zaidi wakaamini kwa sababu ya neno lake. Wakamwambia yule mwanamke, Sasa tunaamini, wala si kwa sababu ya maneno yako tu; maana sisi tumesikia wenyewe, tena twajua ya kuwa hakika huyu ndiye Mwokozi wa ulimwengu. Na baada ya siku mbili hizo akaondoka huko, akaenda Galilaya.”

       

Matokeo ya kupita kwa Yesu pale Samaria

Kupita kwa Bwana Yesu katika Samaria kulikuwa na ulazima sana kwa sababu ya mafunuo makubwa na ya muhimu ambayo tunayapata kupitia safari yake, Na zaidi ya yote kuokolewa kwa nafsi za watu wengi sana na kuhudumiwa kwa huruma za Mungu, Mungu ametufundisha maswala mengi sana na ya muhimu kupitia safari hii yenye mafanikio makubwa sana watu wa Samaria wengi zaidi walimuamini Yesu. Kanisa ni lazima tukumbuke Upendo wa Mungu na neema yake haina mipaka, tunaweza kuwafikia wengi bila kujali jamii zao, tamaduni zao, historia zao, ama tofauti zetu, Yesu alitufundisha namna ya kuvunja mipaka hiyo na kuwafikishia watu huduma inayowastahili

Wagalatia 3:28 “Hapana Myahudi wala Myunani. Hapana mtumwa wala huru. Hapana mtu mume wala mtu mke. Maana ninyi nyote mmekuwa mmoja katika Kristo Yesu

Matendo 10:34-35 “Petro akafumbua kinywa chake, akasema, Hakika natambua ya kuwa Mungu hana upendeleo; bali katika kila taifa mtu amchaye na kutenda haki hukubaliwa na yeye.”

Hitimisho

Nimuhimu kukumbuka kuwa injili ni kwa ulimwengu wote na kwa watu wote na kabila zote, Bwana anatufundisha kuhakikisha ya kuwa tunavunja vihunzi vyote  vya kijamii, kiutamaduni, kikabila, na kiimani au kidini na hata kidhehebu, na kuhakikisha ya kuwa tunahubiri upendo kivitendo, umoja na neema na msamaha wa Mungu kwa watu wote,  na kuwa inatupasa kuuiga mfano wake ili kuwafikia watu wote kwa upendo na huruma bila kujali tofauti zetu, Bwana ampe neema kila mmoja wetu kuvuka mipaka na vihunzi vya kibaguzi vinavyotufanya tusiwafikie watu au kuifikia jamii fulani kwa sababu zozote zile katika jina la Yesu ameen!, Aidha nakukumbusha kuwa Yesu aliongea na mwanamke huyu Kisimani yaani mahali ambapo hapawezi kuwa na maswala na wakati wowote mtu anaweza kuja, Yesu hakuongea na mwanamke huyu mafichoni, nalieleza hili mapema, mtu asione kuwa unaweza kuzungumza na mtu wa jinsi tofauti popote tu hapana, ili kujiepusha na kasfa na kusingiziwa kaa na ongea na mtu wa jinsi tofauti mahali pasipo na utata. Mungu akubariki sana kwa kufuatilia somo hili na kama umebarikiwa kumbuka kuwasiliana nami, uongezewe neema na Mungu akutunze!

 

Na. Rev. Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi Mwenye Hekima        

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni