Jumamosi, 17 Agosti 2024

Sipora: Mwanamke mpatanishi!


Kutoka 4:24-26 “Ilikuwa walipokuwa njiani mahali pa kulala, BWANA akakutana naye akataka kumwua. Ndipo Sipora akashika jiwe gumu na kuikata govi ya zunga la mwanawe, na kuibwaga miguuni pake akasema. Hakika wewe u bwana arusi wa damu kwangu mimi.Basi akamwacha. Ndipo huyo mkewe akanena, U bwana arusi wa damu wewe, kwa ajili ya kutahiri.”


Utangulizi

Mojawapo ya wanawake muhimu sana katika imani na ambaye ni kama umuhimu wake hauonekani ni Sipora aliyekuwa mke wa Musa ambaye aliozwa na Baba yake aliyekuwa kuhani mkuu wa Midian, Mwanamke huyu aliwahi kuyaokoa maisha ya Musa aliyetaka kuuawa na Mungu kutokana na kupuuzia maswala ya sheria ya tohara, na kwa namna ya haraka sana Sipora aliyefahamu sana mapenzi ya Mungu kwa kina na kwa huduma ya kikuhani yaani huduma ya upatanishi alimuokoa Musa na kutufundisha kuwa alikuwa mwanamke hodari, jasiri aliyejaa imani na aliyeyajua mapenzi ya Mungu, ni mwanamke aliyekuwa na huduma ya upatanisho alimpatanisha Musa kwa Mungu

2Wakorintho 5:18-19 “Lakini vyote pia vyatokana na Mungu, aliyetupatanisha sisi na nafsi yake kwa Kristo, naye alitupa huduma ya upatanisho; yaani, Mungu alikuwa ndani ya Kristo, akiupatanisha ulimwengu na nafsi yake, asiwahesabie makosa yao; naye ametia ndani yetu neno la upatanisho.”

Sipora ni mwanamke mwenye asili ya Afrika, Ethiopia ndiye ambaye leo Bwana anataka tujifunze kitu kupitia yeye na kuinua imani za wanawake wa Kikristo na kujifunza pia kupitia yeye katika maisha yetu ya imani, Tutajifunza somo hili Sipora mwanamke Mpatanishi kwa kuzingatia maswala kadhaa yafuatayo:-

·         Sipora ni nani?

·         Sipora mwanamke mpatanishi

·         Mambo ya kujifunza kutoka kwa Sipora  


Sipora ni nani?

Sipora alikuwa binti wa kuhani mkuu wa Midian aliyejulikana sana katika torati kama Yethro au (Reuel). Sipora aliolewa na Musa katika wakati mgumu wa maisha ya Musa, wakati Musa akiwa uhamishoni jangwani kufuatia kukimbia hasira ya Farao baada ya yeye kuua raia wa Misri, kwa hiyo ni katika wakati huo mgumu binti huyu alifanyika faraja kubwa sana kwa Musa

Kutoka 2:11-16 “Hata siku zile, Musa alipokuwa mtu mzima, akatoka kuwaendea ndugu zake, akatazama mizigo yao. Akamwona Mmisri anampiga Mwebrania, mmojawapo wa ndugu zake. Basi akatazama huko na huko, na alipoona ya kuwa hapana mtu, akampiga Mmisri yule, akamficha ndani ya mchanga. Akatoka siku ya pili, na tazama, watu wawili wa Waebrania walikuwa wakipigana. Akamwambia yule aliyemdhulumu mwenzake, Mbona unampiga mwenzako? Yule akasema, Ni nani aliyekuweka wewe kuwa mkuu wetu, na mwamuzi juu yetu? Je! Wataka kuniua mimi kama ulivyomwua yule Mmisri? Musa akaogopa, akasema, Kumbe! Jambo lile limejulikana.Basi Farao alipopata habari, akataka kumwua Musa; lakini Musa akakimbia mbele ya Farao, akakaa katika nchi ya Midiani; akaketi karibu na kisima. Basi kuhani wa Midiani alikuwa na binti saba, nao wakaja wakateka maji, wakazijaza birika maji, wapate kunywesha kundi la baba yao.”

Kutoka 2:17-22 “Wachungaji wakaja wakawafukuza; lakini Musa akasimama, akawasaidia, akalinywesha kundi lao.Walipofika kwa Reueli baba yao, akasema, Imekuwaje hata mkarejea mapema leo? Wakasema, Mmisri mmoja alituokoa katika mikono ya wachungaji, tena zaidi ya hayo, akatutekea maji, akalinywesha kundi. Akawaambia binti zake, Yuko wapi basi? Mbona mmemwacha mtu huyo? Mwiteni, ale chakula. Musa akawa radhi kukaa kwake mtu yule, naye akampa Musa binti yake, Sipora.Huyo akamzalia mwana, akamwita jina lake Gershomu, maana alisema, Nimekuwa mgeni katika nchi ya ugeni.”

Sipora anakuwa mfano wa wanawake wapatanishi aliyeokoa maisha ya Musa kupitia huduma yake ya kikuhani aliyoifanya kwa uamuzi wa kuokoa maisha ya Musa kwa haraka sana wakati Mungu alipotaka kumuua Musa kwa sababu za kutokuwatahiri watoto wake wa kiume ona

Kutoka 4:24-26 “Ilikuwa walipokuwa njiani mahali pa kulala, BWANA akakutana naye akataka kumwua. Ndipo Sipora akashika jiwe gumu na kuikata govi ya zunga la mwanawe, na kuibwaga miguuni pake akasema. Hakika wewe u bwana arusi wa damu kwangu mimi. Basi akamwacha. Ndipo huyo mkewe akanena, U bwana arusi wa damu wewe, kwa ajili ya kutahiri.”

Tukio hili ni moja ya tukio muhimu liinalomuingiza Sipora katika orodha ya wanawake jasiri, wastahivu, wenye imani na ujasiri na upendo halisi kwa mume wake na ambaye alikuwa na uelewa wa juu sana wa kiungu, Sipora ni kama anaonekana alikuwa anamjua Mungu wa Musa, ambaye kimsingi pia alikuwa Mungu wa Yethro baba yake, na desturi zake kwa sababu alijua Hasira za Mungu huyo na namna ya kumtuliza na alijua namna ya kumkinga mumewe na watoto wake, Sipora alitoa dhabihu ya damu ya govi ya mwanae na kuzuia ghadhabu ya Mungu kumshukia Musa, ushujaa na ujasiri mkubwa na ujuzi kuhusu Mungu aliokuwa nao Sipora unatufundisha kuwa hakuna jambo la maana duniani kama wanawake kumjua Mungu, Mwanamke akimjua Mungu na sheria zake sio tu atakuwa mwokozi wa familia yake bali atakuwa mwokozi wa taifa na ulimwengu kwa ujumla, Kama Musa angeuawa ukweli kuhusu Historia ya Musa ungekuwa kwa mtu mwingine, tunajua Mungu angewaokoa wana wa Israel kutoka Misri, lakini labda sio kupitia Musa kama Sipora hangemuokoa katika tukio hili. Dunia nzima leo inafuata taratibu nyingi za sheria zilizoandikwa na Musa, hata wanasheria wanaposoma asili ya sheria duniani hawaachi kumtaja Musa kama moja ya waanzilishi wa sheria ambayo ilitoka kwa Mungu, hata hivyo nyuma ya mgongo wa Musa alikuwepo Sipora mwanamke mweusi wa ukoo wa kikuhani wa Yethro Mmidiani. Hii ndiyo inayotupa shauku katika siku ya leo kujifunza kwa kina na mapana na marefu na kutaka kumjua yeye na familia yake.

Sipora ni nani hasa? Ni vigumu sana kumjua Sipora vizuri kwa sababu habari zake hazikupewa umuhimu mkubwa na waandishi wa torati, penginepo ni kwa sababu ya jamii ya kiyahudi kutokuwapa umuhimu mkubwa wanawake, ama pia kwa sababu ya familia za kikuhani ambazo mara kadhaa ziliwataka wanaume kujitenga na wanawake kama sehemu ya usafi na utakatifu pale wanapofanya huduma zao kwa Mungu kwa mujibu wa sheria au torati

Kutoka 19:10-15 “BWANA akamwambia Musa, Enenda kwa watu hawa, ukawatakase leo na kesho, wakazifue nguo zao,wawe tayari kwa siku ya tatu; maana siku ya tatu BWANA atashuka katika mlima wa Sinai machoni pa watu hawa wote.Nawe utawawekea mipaka watu hawa pande zote, ukisema, Jihadharini, msipande mlima huu, wala msiuguse, hata mapambizo yake; kila mtu atakayeugusa mlima huu, bila shaka atauawa. Mkono wa mtu awaye yote usimguse mtu huyo, ila hakika yake atapigwa kwa mawe, au kupigwa kwa mkuki; kwamba ni mnyama au kwamba ni mwanadamu, hataishi. Hapo panda itakapotoa sauti kwa kufuliza ndipo watakapoukaribia mlima. Musa akatelemka mlimani akawaendea watu akawatakasa, nao wakafua nguo zao. Akawaambia watu; Mwe tayari siku ya tatu; msimkaribie mwanamke.”

Sipora alikuwa Binti Mkubwa wa Yethro kuhani mkuu wa Midian ambaye anatajwa kuwa alikuwa na mabinti saba, Sipora alikuwa na uelewa mkubwa kuhusu Mungu kwa sababu alikuwa amejifunza sheria zote za ukuhani na kumjua Mungu wa baba yake, Baba wa Sipora alikuwani kuhani mkuu wa Midian kwa hiyo ni wa uzao wa Ibrahimu ni ndugu wa wayahudi pia, wote tunakumbuka kuwa Ibrahimu ukiacha ya kuwa alikuwa amemzaa Ishmael na Isaka pia alikuwa na watoto wengine wa kume sita aliowazaa kupitia Ketura na katika hao Midian ni mmoja wao ona:-

Mwanzo 25:1-6 “Ibrahimu alioa mke mwingine jina lake akiitwa Ketura. Akamzalia Zimrani, na Yokshani, na Medani, na Midiani, na Ishbaki, na Sua. Yokshani akamzaa Sheba, na Dedani; na wana wa Dedani walikuwa Waashuri na Waletushi, na Waleumi. Na wana wa Midiani walikuwa, Efa, na Eferi, na Hanoki, na Abida, na Eldaa. Hao wote walikuwa ni wana wa Ketura. Ibrahimu akampa Isaka yote aliyokuwa nayo. Lakini wana wa masuria aliokuwa nao Ibrahimu, Ibrahimu akawapa zawadi, naye akawaondoa katika mahali alipokaa Isaka mwanawe, wakati wa uhai wake, waende pande za mashariki, mpaka nchi ya Kedemu.”            

Kwa hiyo unaweza kuona kuwa katika hawa watoto wengine wa Ibrahimu wanaotajwa hapo juu Midiani ni wanne kati ya watoto sita aliozaa Ibrahimu kupitia Ketura unaona? Je watoto hawa wa Ibrahimu walimjua Mungu? Walijua kutenda haki? Waliyashika mafundisho yote ambayo Bwana alikuwa amemfundisha Ibrahimu? Jibu ni NDIO kwa herufi kubwa sana kwa nini kwa sababu Mungu alimchagua Ibrahimu kwa sababu alijua kuwa Ibrahimu atakuwa Mwalimu mzuri sana kwa watoto wake wote na wakazi wote wa nyumbani mwake na kuwa kupitia yeye wataishika njia ya Bwana na watafanya haki, na hukumu. Kwa hiyo watoto wote wa Ibrahimu walikuwa werevu na wajuzi wa sheria za Mungu na hukumu zake akiwepo Yethro kutoka ukoo wa Midian! Unaona?  

Mwanzo Mwanzo 18:17-19 “BWANA akanena, Je! Nimfiche Ibrahimu jambo nilifanyalo, akiwa Ibrahimu atakuwa taifa kuu, hodari, na katika yeye mataifa yote ya dunia watabarikiwa? Kwa maana nimemjua ya kwamba atawaamuru wanawe, na nyumba yake baada yake waishike njia ya BWANA, wafanye haki na hukumu, ili kwamba BWANA naye akamtimizie Ibrahimu ahadi zake.”

Kwa hiyo ni wazi kupitia Ibrahimu na uzao wake sasa kupitia Midiani na kuja kwa Yethro ni wazi kuwa Sipora na wadogo zake walimjua Mungu, na walifahamu utaratibu wote wa Mungu wa baba yao, Yethro alikuwa ni kuhani wa Mungu wa ngazi ya juu sana anapokuwepo Yethro sio rahisi Musa na Haruni kusongeza dhabuhi kwa Bwana kwa sababu Yethro alikuwa na ujuzi mkubwa zaidi na ni kuhani wa Mungu aliyejuu zaidi yao

Kutoka 18:8-12 “Musa akamwambia mkwewe mambo hayo yote BWANA aliyomtenda Farao na Wamisri kwa ajili ya Israeli, na mambo mazito yote yaliyowapata njiani, na jinsi BWANA alivyowaokoa.Yethro alifurahi kwa ajili ya wema wote BWANA aliowatendea Israeli, kwa alivyowaokoa mikononi mwa Wamisri. Kisha Yethro akasema, Na ahimidiwe BWANA aliyewaokoa na mikono ya Wamisri, na mkono wa Farao; aliyewaokoa watu hao watoke mikononi mwa Wamisri.Sasa najua ya kuwa BWANA ni mkuu kuliko miungu yote; naam, katika jambo hilo walilowatenda kwa unyeti.Yethro mkwewe Musa akamletea Mungu sadaka ya kuteketezwa na dhabihu; na Haruni akaja, na wazee wote wa Israeli, wale chakula pamoja na mkwewe Musa mbele za Mungu.”

Kwa msingi huo utaweza kukubaliana nami kuwa Israel ambao wameishi Misri katika nyumba ya upagani mzito kwa miaka 430 tangu baba yao aliposhuka Misri na kizazi cha kina Yusufu, uwezo wao wa kumjua Mungu ni lazima ulikuwa umeathirika sana kumbuka wakati huo hakukuwa na Sheria bado, na hata Musa mwenyewe hangekuwa na ujuzi mkubwa wa kutosha kuhusu kumjua Mungu kama asingelipata muda wa kujifunza kutoka kwa Yethro, ni wazi kuwa Yethro na familia yake walikuwa wanamjua Mungu aliye hai, na walihusika sana kumsaidia Musa kujua maswala ya Mungu, huku Sipora akiwa binti hodari mwenye uwezo mkubwa wa kumjua Mungu na taratibu zake hata japokuwa alikuwa mwanamke na hakuwa nabii lakini alikuwa mshauri mkubwa sana wa Musa, Sio hivyo tu Sipora na familia yake wamekulia jangwani hivyo walilijua jangwa vizuri sana na ndio maana utaweza kuona alipokuja Yethro na kumleta Mke wa Musa pamoja na watoto, Musa sasa alikuwa akimsikiliza mkewe zaidi kuliko Miriam na Haruni ndio sababu Miriam aliona wivu na wakaanza kumteta na kumshambulia kwa ubaguzi wa rangi yake kama mwanamke Mkushi yaani mwanamke mwenye ngozi nyeusi (Ethiopian). Ona:-

Kutoka 18:1-7 “Basi Yethro, kuhani wa Midiani, mkwewe Musa, alisikia habari ya mambo hayo yote Mungu aliyokuwa amemtendea Musa, na Waisraeli watu wake, jinsi BWANA alivyowaleta Israeli watoke Misri. Ndipo Yethro mkwewe Musa akamtwaa Sipora, mke wa Musa, baada ya yeye kumrudisha, pamoja na wanawe wawili; katika hao, jina la mmoja ni Gershomu, maana alisema, Mimi nimekuwa mgeni katika nchi ya ugenini; na jina la wa pili ni Eliezeri, kwa kuwa alisema, Yeye Mungu wa baba yangu alikuwa msaada wangu, akaniokoa na upanga wa Farao. Basi Yethro, mkwewe Musa, pamoja na mke wa Musa na wanawe wawili wakamwendea Musa huko nyikani, hapo alipokuwa amepanga, kwenye mlima wa Mungu; naye akamwambia Musa, Mimi Yethro mkweo nimekuja kwako, na mkeo, na wanawe wawili pamoja naye. Basi Musa akatoka nje ili amlaki mkwewe, akasujudia na kumbusu; nao wakaulizana habari; kisha wakaingia hemani.”

Ujio wa Sipora kutoka nyumbani kwa Yethro kuungana na Musa mumewe na Musa kumpa kipaumbele unapelekea Haruni na Miriam kuona kama wanapoteza nafasi yao kwake na wakaanza kumsema vibaya jambo lililopeleka Mungu kuingilia kati na kuchukua hatua kali sana kwa Miriamu

Hesabu 12:1-13 “Kisha Miriamu na Haruni wakamnenea Musa kwa sababu ya mwanamke Mkushi aliyekuwa amemwoa; maana, alikuwa amemwoa mwanamke Mkushi. Wakasema, Je! Ni kweli Bwana amenena na Musa tu? Hakunena na sisi pia? Bwana akasikia maneno yao. Basi huyo mtu, huyo Musa, alikuwa mpole sana zaidi ya wanadamu wote waliokuwa juu ya uso wa nchi. Bwana akanena ghafula na Musa, na Haruni na Miriamu, na kuwaambia, Tokeni nje ninyi watatu, mwende hemani mwa kukutania. Basi hao watatu wakatoka nje. Bwana akashuka katika nguzo ya wingu akasimama pale mlangoni pa Hema, akawaita Haruni na Miriamu, nao wakatoka nje wote wawili. Kisha akawaambia, Sikizeni basi maneno yangu; Akiwapo nabii kati yenu, Mimi, Bwana, nitajifunua kwake katika maono, Nitasema naye katika ndoto. Sivyo ilivyo kwa mtumishi wangu, Musa; Yeye ni mwaminifu katika nyumba yangu yote; Kwake nitanena mdomo kwa mdomo, Maana, waziwazi wala si kwa mafumbo; Na umbo la Bwana yeye ataliona. Mbona basi ninyi hamkuogopa Kumnenea mtumishi wangu, huyo Musa? Hasira za Bwana zikawaka juu yao; naye akaenda zake. Kisha hilo wingu likaondoka kutoka pale juu ya hema; na tazama, Miriamu akawa mwenye ukoma, mweupe kama theluji; Haruni akamwangalia Miriamu, na tazama, yu mwenye ukoma. Kisha Haruni akamwambia Musa, Ee bwana wangu nakusihi sana usituwekee dhambi juu yetu, kwa kuwa tumefanya ya upumbavu, na kufanya dhambi. Nakusihi, asiwe kama mmoja aliyekufa, ambaye nyama ya mwili wake nusu imelika hapo atokapo tumbo la mama yake. Musa akamlilia Bwana, akasema, Mpoze, Ee Mungu, nakusihi sana.”

Unaona nadhani sasa unapata Mwanga jinsi Sipora alivyokuwa wa muhimu, Sipora ni mwanamke Jasiri, mwanamke aliyejaa imani, mwanamke mwenye upendo, mwanamke kiongozi, mwanamke anayelijua jangwa vizuri, alikuwa na utulivu wa ajabu sana na ndio maana hata katika hali ngumu aliweza kufanya maamuzi sahihi na kutuliza hasira za Mungu dhidi ya mumewe, alikuwa mshauri mzuri wa Musa mpaka Miriam aliona wivu, alisengenywa lakini yeye na Musa walikaa kimya, unaweza kuchunguza kwa kina kuwa aliyekuwa anasemwa hapo sio Musa bali ni mwanamke huyu mwenye rangi nyeusi, hapa maandiko yanamtaja kama mwanamke mkushi neno kushi katika Biblia ni “Ethiopia” Ethiopia ni neno la kigiriki/kiyunani ambalo tafasiri yake ni “Of burned face” yaani watu weusi au walioungua uso na lilitumika kumaanisa watu wa Afrika hususani inchi iliyokuwa inafikika kwa bara bara kwa wakati huo ilikuwa ni Ethiopia kwa hiyo wakushi kimsingi walikuwa ni watu wenye ngozi nyeusi yaani mwafrika na walijulikana kwa ngozi yao nyeusi  katika maandiko ona

Yeremia 13:23 “Je! Mkushi aweza kuibadili ngozi yake, au chui madoa-doa yake? Kama aweza, ndipo na ninyi mwaweza kutenda mema, ninyi mliozoea kutenda mabaya.”

Kwa hiyo unaweza kupata picha kuwa Musa yeye alikuwa ameoa binti huyo Sipora aliyekuwa mweusi mtoto wa kuhani wa Midian. Lakini mwenye ujuzi mkubwa kuhusu Mungu, malezi mazuri, Jasiri, mwenye kujaa Imani, mwenye upendo na mpatanishi na mwenye kulijua jangwa ni mwanamke huyu ndiye tunajifunza habari zake leo.

Sipora mwanamke mpatanishi

Jinsi ambavyo Sipora alimuokoa Musa na kuwa mpatanishi kati ya Musa na Mungu ndio habari ya mjini katika siku hii ya leo, tukio hili lilikuwa ni tukio la namna gani, kwa sababu watu wengi wanashindwa kulibainisha lilivyokua lakini swala la msingi ni kuwa matendo na maneno ya Sipora yalimuokoa Musa katika tukio hilo hebu tulione tena katika maandiko

Kutoka 4:24-26 “Ilikuwa walipokuwa njiani mahali pa kulala, BWANA akakutana naye akataka kumwua. Ndipo Sipora akashika jiwe gumu na kuikata govi ya zunga la mwanawe, na kuibwaga miguuni pake akasema. Hakika wewe u bwana arusi wa damu kwangu mimi. Basi akamwacha. Ndipo huyo mkewe akanena, U bwana arusi wa damu wewe, kwa ajili ya kutahiri.”

Ni tukio linaingizwa ghafla katika maandiko, Musa alipokuwa njiani akiwa pamoja na familia yake alikutana na Bwana na Bwana alitaka kumuua! Inaonekana kuwa kosa kubwa hapa ni kuwa Musa alikuwa hajawatahiri watoto wake na au alikuwa amepuuzia hivyo Mungu alichukizwa na hilo, hapa ndio tunajua kuwa Sipora alikuwa anajua umuhimu wa tukio hilo, kwani Musa huenda alishikwa na tatizo la ghafla na kwa ujasiri mkubwa mwanamke huyu alishika kisu cha jiwe gumu na kumtahiri mtoto na kuibwaga miguuni pake na kusema hakika wewe u bwana harusi wa damu kwangu mimi, Biblia ya kiingereza ya NRSV inasema aliikata govi ya mwanae wa kiume na kuitupa katika miguu ya Mungu na kusema maneno kwa kiebrania  (Dậm Chậthận) Baba mkwe wa Damu! Kwa hiyo aliitupa govi ya kijana katika miguu ya Mungu au aliiweka miguuni pa Mungu, na kwa sababu hiyo Musa na yeye wakawa wazima, bila tukio hili Musa angepigwa na Mungu kwa sababu ya kupuuzia agizo hili ambalo Mungu alimuamuru Ibrahimu, lakini kwa ushujaa wa Sipora na uelewa wake kuhusu tabia ya Mungu Musa aliokolewa na kuendelea na majukumu ya kazi ya ukombozi.

Sipora ni mwanamke wa kipekee na jasiri historia yake inatukumbusha kuwa hata katika hali ngumu wanawake wanaweza kujivika ujasiri, kutoka kwa Mungu, na kuwa wanaweza kuwa na ujuzi kuhusu Mungu na kusababisha wokovu mkubwa kwa familia yao na taifa na kufanikisha njia za Mungu, wanawake wanaweza kusimama kwa ujasiri na kuwapatanisha watu kwa Mungu, wanawake ndio waliokuwa wa kwanza kufika kaburini wakati Yesu amefufuka, na mwanamke msamaria aliwaleta wasamaria wengi kwa Yesu, Mungu anaweza kuwatumia wanawake na Imani ya kweli hukaa na wanawake na ndio maana Mungu hajawahi kuwapuuzia na aliwataka waisrael kutokuoa wanawake mabaradhuli, na wasiomcha Mungu kwani wanawake wanauwezo wa kugeuza moyo wa mwanaume hata kama ana hekima kiasi gani, hivyo kila mtumishi wa Mungu anapaswa kuoa mwanamke mcha Mungu kama alivyo Sipora mwanamke anayemjua Mungu na njia za Mungu na sio wanawake mabaradhuli wasio mcha Mungu.

1Wafalme 11:1-6 “Mfalme Sulemani akawapenda wanawake wengi wageni, pamoja na binti yake Farao, wanawake wa Wamoabi, na wa Waamoni, na wa Waedomi, na wa Wasidoni, na wa Wahiti, na wa mataifa Bwana aliyowaambia wana wa Israeli, Msiingie kwao, wala wasiingie kwenu; kwa kuwa hakika wataigeuza mioyo yenu kuifuata miungu yao. Sulemani akaambatana nao kwa kuwapenda.Akawa na wake mia saba binti za kifalme, na masuria mia tatu; nao wakeze wakamgeuza moyo.Maana ikawa, Sulemani alipokuwa mzee, wake zake wakamgeuza moyo wake, afuate miungu mingine, wala moyo wake haukuwa mkamilifu kwa Bwana, Mungu wake, kama moyo wa Daudi baba yake.Kwa kuwa Sulemani akamfuata Ashtorethi, mungu mke wa Wasidoni na Milkomu, chukizo la Waamoni.Sulemani akafanya yaliyo mabaya machoni pa Bwana, wala hakumfuata Bwana kwa utimilifu, kama Daudi baba yake.”

Wanaume wanapaswa kuwa makini ni aina gani ya mwanamke wanamuoa, ni ukweli usiozuilika kuwa hata uwe na hekima kiasi gani kama utapata mwanamke asiyemjua Mungu wala kuheshimu mambo ya Mungu na wito wako wa kiungu huduma yako itasambaratika, Huduma ya Musa iliweza kusimama na hata maisha yake kuwa salama kwa sababu alikuwa na mwanamke muelewa, wakati Sulemani aliharibikiwa kwa sababu ya wanawake, ni hatari hata kuoa mwanamke mchanga kiroho asiyelijua vema neno la Mungu wala hamjui Mungu wake inaweza kuleta madhara makubwa na kuwakosesha watu Baraka ambazo Mungu alizikusudia kwa watu wake, kama Sipora angekuwa mwanamke wa hovyo leo historia ya Israel na ushujaa wa Musa usingeliweza kuonekana, jina la Bwana na libarikiwe pia kwaajili ya malezi mazuri ya Yethro na ushauri  na mafunzo yaliyomsaidia Musa na wana wa Israel kwa ujumla.

Mambo ya kujifunza kutoka kwa Sipora

Je umewahi kukutana na hali ngumu ambayo kwa jiyo ulihitaji mwanamke jasiri kama wa Sipora? Unawezaje kuimarisha imani yako ili kuweza kukabiliana na changamoto mbalimbali? Unawezaje kuonyesha upendo usio na mipaka kwa wale tunaowapenda?

Sipora ni mfano na majibu kwa kila mmoja kwa sababu alitatua changamoto katika njia za kiungu, ameonyesha kuna faida kubwa sana katika kumjua Mungu aliye hai na njia zake, na anawakumbusha wanawake kujiamini katika Mungu

Kila mwanamke akumbuke kuwa anaweza kuwa mwenye nguvu na uwezo mkubwa, usiruhusu chochote kukuzuia kufikia malengo yako jifunzeni kutoka kwa Sipora na amini katika Mungu na kujijengea ujasiri na imani, hata kama watu hawamzungumzii sana Sipora, kama wanawake leo wanavyopuuziwa katika jamii nyingi, Roho Mtakatifu leo ametaka ujifunze kitu na uwe mwenye kumcha Mungu na kumjua Mungu  na kusifiwa kwa uchaji wa Mungu na kwa kufanya tukio lililo jema tafadhali kuwa mwema mche Mungu kama Sipora, uiokoe jamii yako na taifa stay blessed !   

Mithali 31:29-30 “Binti za watu wengi wamefanya mema, Lakini wewe umewapita wote. Upendeleo hudanganya, na uzuri ni ubatili; Bali mwanamke amchaye Bwana, ndiye atakayesifiwa.”

Na Rev. Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye hekima         

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni