Jumamosi, 7 Septemba 2024

Umuhimu wa kunena kwa lugha


Marko 16:15-18 “Akawaambia, Enendeni ulimwenguni mwote, mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe. Aaminiye na kubatizwa ataokoka; asiyeamini, atahukumiwa. Na ishara hizi zitafuatana na hao waaminio; kwa jina langu watatoa pepo; watasema kwa lugha mpya; watashika nyoka; hata wakinywa kitu cha kufisha, hakitawadhuru kabisa; wataweka mikono yao juu ya wagonjwa, nao watapata afya.”



Utangulizi:

Kunena kwa lugha ni moja ya kipawa cha Roho Mtakatifu kinachotolewa kwa mtu aliyeokoka kumuwezesha mtu huyo, kuwa na uwezo wa kuzungumza lugha nyingine ya wanadamu au malaika kwa uwezo wa Roho Mtakatifu, kipawa hiki kinatajwa na kuelezewa mara kadhaa katika maandiko hususani ya Agano Jipya na kwa sababu hiyo ni muhimu kwetu, kuchukua muda na kujifunza kwa kina na mapana na marefu, ili tuweze kuelewa umuhimu wake, faida zake na uhalisia wake, hii ni kwa sababu kama ilivyo kwa fundisho la utatu, na uungu wa Yesu, na hata uwepo wa Roho Mtakatifu, kitheolojia yamekuwa na mijadala mikubwa sana ambayo inapelekea watu kutilia shaka kuhusu mafundisho hayo hali kadhalika swala la kunena kwa Lugha. Na hivyo kupelekea kuwepo na upungufu wa kuzingatia umuhimu na faida za karama hii ya kunena kwa lugha, Bwana ampe neema kila mmoja wetu kufuatilia na kuelewa kwa kina ili tuweze kufaidika na uwepo wa kipawa hiki kwa faida ya ufalme wa Mungu: Tutajifunza somo hili  Umuhimu kwa kunena kwa lugha kwa kuzingatia vipengele viwili vifuatavyo:-


·         Ukweli kuhusu kunena kwa lugha.

·         Umuhimu wa kunena kwa lugha.


Ukweli kuhusu kunena kwa lugha.

Ni muhimu kufahamu kuwa swala la kunena kwa lugha sio swala la mzaha na dhihaka kama watu wengine wanavyofikiri, kunena kwa lugha ni ishara kamili na ni kipawa kamili kutoka kwa Baba wa mianga kama jinsi ambavyo Yesu Kristo mwenyewe alivyoahidi na kusema kuhusu swala hilo, sio hivyo tu, maandiko yamelitaja swala la kunena kwa lugha katika mazingira toshelevu ya kuwa na uwezo wa kufanya fundisho kupitia swala hilo:-

Marko 16:15-18 “Akawaambia, Enendeni ulimwenguni mwote, mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe. Aaminiye na kubatizwa ataokoka; asiyeamini, atahukumiwa. Na ishara hizi zitafuatana na hao waaminio; kwa jina langu watatoa pepo; watasema kwa lugha mpya; watashika nyoka; hata wakinywa kitu cha kufisha, hakitawadhuru kabisa; wataweka mikono yao juu ya wagonjwa, nao watapata afya.”

Yakobo 1:16-17 “Ndugu zangu wapenzi, msidanganyike.Kila kutoa kuliko kwema, na kila kitolewacho kilicho kamili, hutoka juu, hushuka kwa Baba wa mianga; kwake hakuna kubadilika, wala kivuli cha kugeuka-geuka.”

Kunena kwa lugha kupo, na ni karama au kipawa kutoka kwa Mungu, maandiko hayo hayako kwa bahati mbaya, Yesu mwenyewe aliahidi ya kuwa wale wanaomuamini watafuatiwa na ishara mbalimbali, ikiwemo hii ya kunena kwa lugha mpya, hiki ni kipawa kamili kutoka kwa baba wa mianga ambaye kwake hakuna kivuli cha kugeuka geuka, kwa msingi huo ni ukweli usiopingika kuwa zawadi hii ya kunena kwa lugha ipo na imethibitishwa katika maandiko,  bahati mbaya Makanisa mengi na baadhi ya madhehebu wana maoni tofauti tofauti kuhusu kunena kwa lugha hata hivyo eneo pekee ambalo tunaweza kujifunza na kuelewa kwa kina kuhusu karama hii ni kwenye neno la Mungu tu.

-          Matendo 2:3-4 “Kukawatokea ndimi zilizogawanyikana, kama ndimi za moto uliowakalia kila mmoja wao.Wote wakajazwa Roho Mtakatifu, wakaanza kusema kwa lugha nyingine, kama Roho alivyowajalia kutamka.”

 

-          Matendo 10:44-46 “Petro alipokuwa akisema maneno hayo Roho Mtakatifu akawashukia wote waliolisikia lile neno.Na wale waliotahiriwa, walioamini, wakashangaa, watu wote waliokuja pamoja na Petro, kwa sababu Mataifa nao wamemwagiwa kipawa cha Roho Mtakatifu.Kwa maana waliwasikia wakisema kwa lugha, na kumwadhimisha Mungu. Ndipo Petro akajibu,”

 

-          Matendo 19:1-6 “Ikawa, Apolo alipokuwa Korintho, Paulo, akiisha kupita kati ya nchi za juu, akafika Efeso; akakutana na wanafunzi kadha wa kadha huko; akawauliza, Je! Mlipokea Roho Mtakatifu mlipoamini? Wakamjibu, La, hata kusikia kwamba kuna Roho Mtakatifu hatukusikia. Akawauliza, Basi mlibatizwa kwa ubatizo gani? Wakasema, Kwa ubatizo wa Yohana. Paulo akasema, Yohana alibatiza kwa ubatizo wa toba, akiwaambia watu wamwamini yeye atakayekuja nyuma yake, yaani, Yesu.Waliposikia haya wakabatizwa kwa jina la Bwana Yesu.Na Paulo, alipokwisha kuweka mikono yake juu yao, Roho Mtakatifu akaja juu yao; wakaanza kunena kwa lugha, na kutabiri.”

 

-          1Wakorintho 14:2 “Maana yeye anenaye kwa lugha, hasemi na watu, bali husema na Mungu; maana hakuna asikiaye; lakini anena mambo ya siri katika roho yake.”

                               

-          1Wakorintho 13:1 “Nijaposema kwa lugha za wanadamu na za malaika, kama sina upendo, nimekuwa shaba iliayo na upatu uvumao.”                       

Kwa ushahidi wa maandiko kadhaa hapo tunaweza kukubaliana ya kuwa maandiko yanatambua kuwa iko ishara ya kunena kwa lugha na nyakati za kanisa la kwanza ilikuwa ni jambo la kawaida kwa wakristo waliobatizwa kwa Roho Mtakatifu kunena kwa lugha, na maandiko yameweka wazi hilo, kwa hiyo hatuwezi kupingana na neno kuhusu hili.


Umuhimu wa kunena kwa lugha


Ni muhimu kufahamu kuwa katika makanisa mengi sana watu wengi wanapuuzia swala zima la kunena kwa lugha kwa sababu wanadhani au kufikiri kuwa neno la Mungu linasema kuwa kunena kwa lugha kutakoma, lakini hiyo haimaanishi tukiwa ulimwenguni, kunena kwa lugha kutakoma tutakapofika mbinguni, kwa sababu tukifika mbinguni kunena kwa lugha kutapoteza umuhimu wake kwa sababu kule kila kitu kitakuwa kamili au kitakamilika kwa Mungu


1Wakorintho 13:9-12 “Kwa maana tunafahamu kwa sehemu; na tunafanya unabii kwa sehemu; lakini ijapo ile iliyo kamili, iliyo kwa sehemu itabatilika.Nilipokuwa mtoto mchanga, nalisema kama mtoto mchanga, nalifahamu kama mtoto mchanga, nalifikiri kama mtoto mchanga; tokea hapo nilipokuwa mtu mzima, nimeyabatilisha mambo ya kitoto.Maana wakati wa sasa tunaona kwa kioo kwa jinsi ya fumbo; wakati ule tutaona uso kwa uso; wakati wa sasa nafahamu kwa sehemu; wakati ule nitajua sana kama mimi nami ninavyojuliwa sana.Basi, sasa inadumu imani, tumaini, upendo, haya matatu; na katika hayo lililo kuu ni upendo.”


Wako pia wale wanaoamini katika kunena kwa lugha lakini pia hawaoni umuhimu wa kuendelea kunena kwa lugha aidha kwa kufikiri kuwa kunena kwa lugha hakuna umuhimu, hapa sizungumzii karama ya aina za lugha, nazungumzia kunena kwa lugha ambako ni fungu la kila mtu aliyebatizwa kwa Roho Mtakatifu, Kunena kwa lugha hakutokei mara moja pale tu mtu anapokuwa amebatizwa kwa Roho Mtakatifu lakini linapaswa kuwa swala endelevu ambalo lina faida kubwa sana, hapa yako maswala kadhaa yanayosisitiza umuhimu wa kunena kwa lugha sawa na neno la Mungu.


1.       Kusema na Mungu. -  Kunena kwa lugha uwe unajua hiyo lugha au huitambui lakini kuna kupa neema ya kuzungumza na Mungu na sio wanadamu, kwa hiyo kunena kwa lugha ni mawasiliano ya siri kati ya mtu na Mungu ambayo mwanadamu hawezi kuyaelewa, kwa hiyo roho ya mtu aliyeokoka na kubatizwa kwa Roho Mtakatifu, inawasiliana na Mungu moja kwa moja japokuwa huwezi kupanga kuhusu kunena kwa lugha lakini hatuna budi kuchochea kwa kina swala zima la kunena kwa lugha kutokana na umuhimu wake.kwani Mtu anaponena kwa lugha anazungumza na Mungu moja kwa moja maswala yote ya siri katika roho yake.

 

1Wakorintho 14:2 “Maana yeye anenaye kwa lugha, hasemi na watu, bali husema na Mungu; maana hakuna asikiaye; lakini anena mambo ya siri katika roho yake.”

 

2.       Kujijenga kiroho  - Kunena kwa lugha pia kunamjenga kiroho, yeye anenaye kwa lugha, kujijenga kiroho kuna maanisha nini kunamaanisha kuwa unaponena kwa lugha unaimarisha imani yako na kuijimarisha kiroho wakati huo akili yako haina matunda yaani haijui kile unachokizungumza lakini roho yako ndani yako inaomba katika kiwango kilicho bora zaidi, ambacho kimsingi kinaimarisha hali yako ya kiroho unajijenga. Kumbuka pia kunena ka lugha pia kunaitwa kuomba kwa roho katika maandiko.

 

1Wakorintho 14:3-4 “Bali yeye ahutubuye, asema na watu maneno ya kuwajenga, na kuwafariji, na kuwatia moyo.Yeye anenaye kwa lugha hujijenga nafsi yake; bali ahutubuye hulijenga kanisa.”

 

Yuda 1:20 “Bali ninyi, wapenzi, mkijijenga juu ya imani yenu iliyo takatifu sana, na kuomba katika Roho Mtakatifu,”

 

1Wakorintho 14:14-15 “Maana nikiomba kwa lugha, roho yangu huomba, lakini akili zangu hazina matunda. Imekuwaje, basi? Nitaomba kwa roho, tena nitaomba kwa akili pia; mtaimba kwa roho, tena nitaimba kwa akili pia.”

 

3.       Kumwadhimisha Mungu – Kunena kwa lugha kunakufanya umwadhimishe Mungu yaani umuabudu Mungu katika namna ya ndani sana, Na kumshukuru, Roho Mtakatifu anatusaidia kumuabudu Mungu katika namna ambayo kibinadamu ni ngumu kuelezea naweza kusema ni kama mnenaji kwa lugha ni kama anazungumza akiwa mbinguni katika ulimwengu wa roho, na ndio maana tunaambiwa katika maandiko kuwa mara baada ya Kornelio na watu wa nyumbani mwake kubatizwa katika Roho Mtakatifu walianza kumwadhimisha Mungu yaani kuuabudu kwa ndani na kumshukuru Mungu, lugha inakusaidia kumuabudu Mungu kwa usahihi.

 

Matendo 10:44-47 “Petro alipokuwa akisema maneno hayo Roho Mtakatifu akawashukia wote waliolisikia lile neno. Na wale waliotahiriwa, walioamini, wakashangaa, watu wote waliokuja pamoja na Petro, kwa sababu Mataifa nao wamemwagiwa kipawa cha Roho Mtakatifu. Kwa maana waliwasikia wakisema kwa lugha, na kumwadhimisha Mungu. Ndipo Petro akajibu, Ni nani awezaye kuzuia maji, hawa wasibatizwe, watu waliopokea Roho Mtakatifu vile vile kama sisi?     

 

4.       Mlango wa maisha ya ushindi – Moja ya siri kubwa sana ya mafanikio ya kunena kwa lugha ni pamoja na kukupa maisha ya ushindi, na kukupandisha kiroho pamoja na kuchochewa kwa karama za Rohoni, Kama unataka kuona hayo katika maisha yako chochea zoezi hili la kunena kwa lugha na utakuja kukubaliana nami kuwa kadiri unavyonena kwa lugha sana utagundua kuwa unapanda juu sana kiroho na kuchochea karama nyingi sana za rohoni, na kadiri unavyoacha utaona upungufu, watu wa Korintho walikuwa wananena kwa lugha na walikuwa na karama nyingi sana za rohoni lakini Paulo Mtume aliwaambia watamani sana karama zilizo kuu, karama zilizokuu maana yake kadiri mtu anavyotumia lugha katika mawasiliano na Mungu anajiweka katika nafasi ya kuchochea uwepo wa Mungu na karama za Roho na kutumiwa na Mungu zaidi.

 

1Wakorintho 14:1 “Ufuateni upendo, na kutaka sana karama za rohoni, lakini zaidi kwamba mpate kuhutubu.”

 

1Wakorintho 12:31 “Takeni sana karama zilizo kuu. Hata hivyo nawaonyesha njia iliyo bora.”

 

Kunena kwa lugha ni njia ya kipekee sana ambayo Mungu ametupa kwaajili ya kujijenga binafsi, kujenga roho zetu, hii ni njia ya kujiimarisha kiroho na kuimarisha mahusiano yetu, na kumuabudu Mungu, tunapoomba kwa roho yaani kunena kwa lugha roho iliyoko ndani yetu na Roho wa Mungu yaani Roho Mtakatifu anatusaidia kutuombea na kujiweka katika nafasi nzuri kwaajili ya mambo yajayo kwani yeye anayajua

 

Yohana 16:13-14 “Lakini yeye atakapokuja, huyo Roho wa kweli, atawaongoza awatie kwenye kweli yote; kwa maana hatanena kwa shauri lake mwenyewe, lakini yote atakayoyasikia atayanena, na mambo yajayo atawapasha habari yake.Yeye atanitukuza mimi, kwa kuwa atatwaa katika yaliyo yangu na kuwapasha habari.”

 

1Wakorintho 2:19-15 “Lakini Mungu ametufunulia sisi kwa Roho. Maana Roho Huchunguza yote, hata mafumbo ya Mungu. Maana Ni nani katika binadamu ayajuaye mambo ya binadamu ila roho ya binadamu iliyo ndani yake? Vivyo hivyo na mambo ya Mungu hakuna ayafahamuye ila Roho wa Mungu. Lakini sisi hatukuipokea roho ya dunia, bali Roho atokaye kwa Mungu, makusudi tupate kuyajua tuliyokirimiwa na Mungu. Nayo twayanena, si kwa maneno yanayofundishwa kwa hekima ya kibinadamu, bali yanayofundishwa na Roho, tukiyafasiri mambo ya rohoni kwa maneno ya rohoni. Basi mwanadamu wa tabia ya asili hayapokei mambo ya Roho wa Mungu; maana kwake huyo ni upuzi, wala hawezi kuyafahamu, kwa kuwa yatambulikana kwa jinsi ya rohoni. Lakini mtu wa rohoni huyatambua yote, wala yeye hatambuliwi na mtu.”

 

5.       Kuomba kwa usahihi zaidi – Kunena kwa lugha kunamsaidia mnenaji kuomba kwa njia inayomlingana Mungu, na hasa kuomba sawa na mapenzi ya Mungu kwa sababu kwa akili zetu na nguvu zetu kibinadamu hatujui kuomba kama jinsi itupaswavyo kuomba, kwa hiyo tunapoomba katika Roho Mtakatifu yaani kwa kunena kwa lugha tunajiweka katika nafasi ya kuomba kwa usahihi na kuboresha maisha ya maombi, bila Roho Mtakatifu ni vugumu kuwa waombaji lakini ni Roho wa Mungu ndani yetu na kupitia kunena kwa lugha tunaweza kuboresha kwa kiwango kikubwa sana maisha ya maombi, na kuongezea neema ya kuwa waombaji wenye maombi yenye kutosheleza na yenye kutuletea majibu na utaratibu ulio sahihi zaidi.

 

Warumi 8:26-27 “Kadhalika Roho naye hutusaidia udhaifu wetu, kwa maana hatujui kuomba jinsi itupasavyo, lakini Roho mwenyewe hutuombea kwa kuugua kusikoweza kutamkwa. Na yeye aichunguzaye mioyo aijua nia ya Roho ilivyo, kwa kuwa huwaombea watakatifu kama apendavyo Mungu.”

 

Zecharia 12:10 -11 “Nami nitawamwagia watu wa nyumba ya Daudi, na wenyeji wa Yerusalemu, roho ya neema na kuomba; nao watamtazama yeye ambaye walimchoma; nao watamwombolezea, kama vile mtu amwombolezeavyo mwanawe wa pekee; nao wataona uchungu kwa ajili yake, kama vile mtu aonavyo uchungu kwa ajili ya mzaliwa wake wa kwanza.Siku hiyo kutakuwa na maombolezo makuu huko Yerusalemu, kama maombolezo ya Hadadrimoni katika bonde la Megido.”

 

6.       Kuimarisha uhusiano wetu na Mungu - Wote tunafahamu jinsi lugha yoyote duniani ilivyo ya muhimu, iwe ni ya kuzungumza, au ya alama, au ya kimatendo, wote tunafahamu kuwa ubora na uzuri mkubwa wa lugha ni katika kuwasiliana na kujenga uhusiano, lugha ndiyo inayoruhusu kujielezea, na kuelezea hisia zetu, mawazo yetu shauku yetu na matakwa yetu. Kama hatuna ujuzi wa mawasiliano ni vigumu kwetu kueleweka ipaswavyo, ndani ya lugha kuna msingi wa mawasiliano, uhusiano, utamaduni, ukaribu, silaha, usalama, na nafasi, na kuunganisha, hii ndicho kinachotokea kati ya mtu aliyeokoka na Mungu pale tunaponena kwa lugha tunaimarika kila kitu katika uhusiano wetu na Mungu, hii haimaanishi kuwa Mungu hasikii lugha nyingine hapana lakini kwa njia rahisi tunaweza kusema kunena kwa Lugha ni lugha ya rohoni au ni lugha ya Mungu, ni Lugha ya Roho Mtakatifu, wote tunafahamu pale inapotokea ukikutana na mtu wa ngozi yako, rangi yako na lugha yako katika eneo la ugenini, jinsi inavyoleta msisimko mkubwa sana na kutaka kujuana na kuwasiliana ndicho kinachotokea pale unapozungumza na Mungu kwa kunena kwa lugha.  

 

1Wakorintho 14:2 “Maana yeye anenaye kwa lugha, hasemi na watu, bali husema na Mungu; maana hakuna asikiaye; lakini anena mambo ya siri katika roho yake.”               

 

7.       Kukabiliana na changamoto za kiroho – Kunena kwa lugha kunazalisha nguvu na nguvu mpya na kunazalisha upako kutoka kwa Roho Mtakatifu unaotusaidia kukabiliana na changamoto zozote za kiroho, Paulo mtume alikabiliana na changamoto nyingi sana, alifanya kazi kuliko mitume wote, alitumiwa na Mungu kwa viwango vikubwa sana lakini moja ya sababu kubwa ya yeye kuwa imara sana ni kwa sababu alinena sana kwa lugha, kunena kwa lugha sana au kuliko wengine ni wazi kuwa pia alikuwa na maisha ya maombi sana kuliko wengine na unaweza kuona utajiri wa kila karama aliokuwa nao, na utendaji au kutumiwa na Mungu kwa viwango vikubwa zaidi.  

 

Yuda 1:20 “Bali ninyi, wapenzi, mkijijenga juu ya imani yenu iliyo takatifu sana, na kuomba katika Roho Mtakatifu,”

 

1Wakorintho 14:18-19 “Namshukuru Mungu ya kuwa nanena kwa lugha zaidi ya ninyi nyote; lakini katika kanisa napenda kunena maneno matano kwa akili zangu, nipate kuwafundisha wengine, zaidi ya kunena maneno kumi elfu kwa lugha.”

 

1Wakorintho 15:9-10 “Maana mimi ni mdogo katika mitume, nisiyestahili kuitwa mitume, kwa sababu naliliudhi Kanisa la Mungu. Lakini kwa neema ya Mungu nimekuwa hivi nilivyo; na neema yake iliyo kwangu ilikuwa si bure, bali nalizidi sana kufanya kazi kupita wao wote; wala si mimi, bali ni neema ya Mungu pamoja nami.”                

 

Matendo 19:11-12 “Mungu akafanya kwa mikono ya Paulo miujiza ya kupita kawaida; hata wagonjwa wakaletewa leso na nguo zilizotoka mwilini mwake, magonjwa yao yakawaondokea, pepo wachafu wakawatoka.”                

 

Unaweza kuona muunganiko ulioko kati ya kunena kwa lugha sana, kufanya kazi sana na kutumiwa na Mungu sana siri ya kutumiwa na Mungu katika neema yake na kumsaidia mtu kuishi maisha matakatifu ya kumpendeza Mungu, na kumtumikia Mungu sana na kutumiwa sana katika ishara na miujiza iko katika kunena kwa lugha sana.

 

 

8.       Kupokea maelekezo ya kiroho – kwa kuwa kunena kwa lugha kunaimarisha uhusiano wetu na Mungu ni wazi kuwa kila anayenena kwa lugha anazungumza na Mungu na kwa sababu hiyo ni rahisi kupokea maelekezo, mafunuo, Elimu na hata unabii na maelekezo ya kimafundisho, kwa hiyo kunena kwa lugha hutuletea ufunuo mkubwa sana na maelekezo kutoka kwa Mungu ambayo yatatusaidia katika maisha yetu na huduma na utumishi kwa Mungu.

 

1Wakorintho 14:5-6 “Nami nataka ninyi nyote mnene kwa lugha, lakini zaidi sana mpate kuhutubu, maana yeye ahutubuye ni mkuu kuliko yeye anenaye kwa lugha, isipokuwa afasiri, ili kusudi kanisa lipate kujengwa. Ila sasa, ndugu, nikija kwenu na kunena kwa lugha, nitawafaidia nini, isipokuwa nasema nanyi kwa njia ya ufunuo, au kwa njia ya elimu, au kwa njia ya hotuba, au kwa njia ya fundisho?

 

9.       Kwaajili ya kuyatimiza maandiko – Hakuna jambo la msingi na la muhimu kama kutii maandiko, wakati mwingine utii unaleta Baraka kubwa sana hata kama jambo tulifanyalo linaonekana kama la kipuuzi, tukumbuke tu kuwa upumbavu wa Mungu una hekima kuliko maarifa ya kibinadamu, maandiko yanapotutaka tujae Roho, tutembee kwa Roho, tuishi kwa Roho, tuabudu katika roho na kweli hayo yote hayawezi kukamilika kama tutaachia nje swala hili la msingi sana la kunena kwa lugha.

 

Yohana 4:23-24 “Lakini saa inakuja, nayo sasa ipo, ambayo waabuduo halisi watamwabudu Baba katika roho na kweli. Kwa maana Baba awatafuta watu kama hao wamwabudu. Mungu ni Roho, nao wamwabuduo yeye imewapasa kumwabudu katika roho na kweli.”

 

Warumi 8:11-16 “Lakini, ikiwa Roho yake yeye aliyemfufua Yesu katika wafu anakaa ndani yenu, yeye aliyemfufua Kristo Yesu katika wafu ataihuisha na miili yenu iliyo katika hali ya kufa, kwa Roho wake anayekaa ndani yenu. Basi, kama ni hivyo, ndugu, tu wadeni, si wa mwili tuishi kwa kufuata mambo ya mwili, kwa maana kama tukiishi kwa kufuata mambo ya mwili, mwataka kufa; bali kama mkiyafisha matendo ya mwili kwa Roho, mtaishi. Kwa kuwa wote wanaoongozwa na Roho wa Mungu, hao ndio wana wa Mungu. Kwa kuwa hamkupokea tena roho wa utumwa iletayo hofu; bali mlipokea roho ya kufanywa wana, ambayo kwa hiyo twalia, Aba, yaani, Baba.Roho mwenyewe hushuhudia pamoja na roho zetu, ya kuwa sisi tu watoto wa Mungu

 

Wagalatia 5:16-18 “Basi nasema, Enendeni kwa Roho, wala hamtazitimiza kamwe tamaa za mwili.Kwa sababu mwili hutamani ukishindana na Roho, na Roho kushindana na mwili; kwa maana hizi zimepingana, hata hamwezi kufanya mnayotaka.Lakini mkiongozwa na Roho, hampo chini ya sheria

 

Waefeso 5:18 “ .Tena msilewe kwa mvinyo, ambamo mna ufisadi; bali mjazwe Roho;”

 

10.   Kwaajili ya vita vya kiroho – Kunena kwa lugha ni silaha, tunawasiliana kwa siri na Mungu na kwa sababu hiyo roho zetu huelewana vizuri na Mungu, na kwa sababu hiyo kutusaidia kupigana vita vya kiroho tukisaidiwa na Mungu kwa namna ya ajabu sana, kuomba katika roho yaani kunena kwa lugha kumetajwa na Paulo mtume kama miongoni mwa silaha za Rohoni zinazotusaidia kupata ushindi katika vita vyetu dhidi ya giza

 

Waefeso 6:10-18 “Hatimaye, mzidi kuwa hodari katika Bwana na katika uweza wa nguvu zake.Vaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kuzipinga hila za Shetani.Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho. Kwa sababu hiyo twaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kushindana siku ya uovu, na mkiisha kuyatimiza yote, kusimama. Basi simameni, hali mmejifunga kweli viunoni, na kuvaa dirii ya haki kifuani, na kufungiwa miguu utayari tupatao kwa Injili ya amani; zaidi ya yote mkiitwaa ngao ya imani, ambayo kwa hiyo mtaweza kuizima mishale yote yenye moto ya yule mwovu. Tena ipokeeni chapeo ya wokovu, na upanga wa Roho ambao ni neno la Mungu; kwa sala zote na maombi mkisali kila wakati katika Roho, mkikesha kwa jambo hilo na kudumu katika kuwaombea watakatifu wote;

 

Aidha utafiti wa kisayansi uliofanyika mnamo mwaka 2006  na kuandikwa katika gazeti la The new York Times limethibitisha kuwa watu wanaonena kwa lugha ni mara chache sana kupatwa na tatizo la kiakili, kule uingereza katika utafiti uliofanywa kwa watu 1000 wanaonena kwa lugha ilibainika kuwa watu wanaonena kwa lugha wako sawa kihisia kuliko wale wasionena kwa lugha, na huku kundi linalofuata likiwa ni wale wanaokaa kimya na kufanya tafakari, kwa hiyo kunena kwa lugha licha ya kukupa ushindi dhidi ya nguvu za giza unakufanya uwe imara kihisia na kiakili, kisaikolojia na kukufanya uishi maisha yaliyo sahihi. Kwa hiyo ile hali ya kufikiriwa kuwa wanaonena kwa lugha labda hawako sawa kiakili imebainika kuwa sio dhana sahihi.

 

Kwa msingi huo wote tunakubaliana ya kuwa swala hili ni swala la Muhimu sana, kwamba kunena kwa lugha kuna faida kubwa sana za kiroho, kwa kila Mkristo aliyebatizwa kwa Roho Mtakatifu kwani kunatujenga kiroho, kunatufanya kuomba kwa usahihi, kunaimarisha ushirika wetu na Mungu, kunatupa mafunuo, kunajenga mahusiano na mawasiliano, na Ndio maana Paulo mtume aliitumia sana zawadi hii ya kunena kwa lugha wewe na mimi hatunabudi kuhakikisha ya kuwa tunauiga mfano wa Paulo mtume na kuliweka swala hili katika vitendo kwa kumuhitaji sana Roho Mtakatifu katika kunena kwa lugha na kuimarisha uhusiano wetu na Mungu na kupata faida zote zinazoambatana na kunena kwa lugha. Ni kawaida yangu tu kufundisha neno la Mungu bila kuweka shuhuda lakini nnazo shuhuda nyingi zinazoashiria kunena kwa lugha kunabadilisha mfumo wa maisha yetu jambo la msingi tu lifanyie kazi neno hili na utabaini kuwa nisemayo ni kweli.

Yakobo 1:22-24 “Lakini iweni watendaji wa neno, wala si wasikiaji tu, hali mkijidanganya nafsi zenu.Kwa sababu mtu akiwa ni msikiaji wa neno tu, wala si mtendaji, mtu huyo ni kama mtu anayejiangalia uso wake katika kioo. Maana hujiangalia, kisha huenda zake, mara akasahau jinsi alivyo.”  

Na. Rev. Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye hekima!

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni