Ijumaa, 11 Oktoba 2024

Je ninyi nanyi mwataka kuondoka?


Yohana 6:65-69 “Akasema, Kwa sababu hiyo nimewaambia ya kwamba hakuna mtu awezaye kuja kwangu isipokuwa amejaliwa na Baba yangu. Kwa ajili ya hayo wengi miongoni mwa wanafunzi wake wakarejea nyuma, wasiandamane naye tena. Basi Yesu akawaambia wale Thenashara, Je! Ninyi nanyi mwataka kuondoka? Basi Simoni Petro akamjibu, Bwana! Twende kwa nani? Wewe unayo maneno ya uzima wa milele. Nasi tumesadiki, tena tumejua, ya kuwa wewe ndiwe Mtakatifu wa Mungu.”




Utangulizi:

Je kuna watu wamewahi kukuacha na kuondoka katika maisha yako? Je kuna watu hawakupigii simu wala hawashughuliki tena na maisha yako? Je kuna watu mlikuwa karibu sana na siku hizi hawako karibu kama ilivyokuwa zamani? Je unahuzunika kwaajili yao? Je unalalamika kuwa hawakusalimii, hawatumi hata ujumbe na hawaulizi hata uko wapi na unafanya nini?, hawashughuliki hata kukusalimu?  kuna watu ulikuwa msaada mkubwa sana kwao, lakini sasa wako mbali na wewe? Je unahuzunika kwaajili yao? Kuna watu walikuwa faraja kubwa sana katika maisha yako, uliwapenda na wao wakakupenda, wakakufuata lakini sasa ni kama hawako na wewe, kuna wale mlisoma nao shule moja, darasa moja, kuna wale uliwasimamia harusi, kuna wale mlikuwa pamoja, mlicheza pamoja, kuna wale walikaa kwenu wakasomea kwenu, kuna wale ulisoma kwao ukakulia kwao, kuna wale ulikuwa msaada mkubwa kwao kiroho na kimwili na sasa ni kama hawataki kutambua mchango wako je unaumia kwaajili yao? Unalia kwaajili yao? Unasikitia kwaajili yao? Sikiliza wako watu ambao Mungu huwavuta kwetu na kuwaleta karibu nasi kwa makusudi maalumu, wako ambao Mungu amewaleta kwetu kama wenzi wetu, ndugu zetu, watoto wetu na ambao tunawafurahia hawa ni furaha yetu ni damu yetu ni watiifu kwetu hawawezi kutuacha kwa sababu Mungu alikusudia wawe nasi milele, kwa wakati mzuri na wakati mbaya, wako pamoja nasi hawana namna ya kujitoa kwetu, wao ni familia hawawezi kutuacha wala sisi hatuwezi kuwaacha. Lakini wako ambao Mungu huwaleta kwetu kwa sababu maalumu kama marafiki kwa kitambo, ni watu wema kwetu na wazuri kwetu lakini uko wakati ambao Mungu hufunga mlango na kuwaacha waende zao kwa sababu hawana shughuli kwetu tena, lile kusudi ambalo Mungu alikuwa amelikusudia kwa kuwaleta kwetu limeisha, Mlango umefungwa kwao kwaajili yetu, hawawezi tena kwenda unakoenda kwa hiyo Mungu hufunga mlango kwaajili yao, mchango wao wa kimwili na kiroho na kiushirika unakuwa umeishia hapo ambapo Mungu amekusudia uishie, huu ni ukweli ulio mchungu katika maisha, lakini hatuna budi kuukubali na kuujifunza na kujua kuwa ni mapenzi ya Mungu., Kama wana kazi nasi Mungu atawaleta tena Mara.

Muhubiri 3:1-8 “Kwa kila jambo kuna majira yake, Na wakati kwa kila kusudi chini ya mbingu. Wakati wa kuzaliwa, na wakati wa kufa; Wakati wa kupanda, na wakati wa kung'oa yaliyopandwa; Wakati wa kuua, na wakati wa kupoza; Wakati wa kubomoa, na wakati wa kujenga; Wakati wa kulia, na wakati wa kucheka; Wakati wa kuomboleza, na wakati wa kucheza; Wakati wa kutupa mawe, na wakati wa kukusanya mawe; Wakati wa kukumbatia, na wakati wa kutokumbatia; Wakati wa kutafuta, na wakati wa kupoteza; Wakati wa kuweka, na wakati wa kutupa; Wakati wa kurarua, na wakati wa kushona; Wakati wa kunyamaza, na wakati wa kunena; Wakati wa kupenda, na wakati wa kuchukia; Wakati wa vita, na wakati wa amani.”

Leo tutachukua muda kujifunza kwa kina na mapana na marefu kuhusiana na uhusiano uliofifia au uliokufa au ulioondoka na faida zake katika ufalme wa Mungu, tutajifunza namna unavyoweza kuelewa Mapenzi ya Mungu watu wanapokuacha na kuondoka zao katika maisha yako, Utajifunza namna na jinsi unavyopaswa kutokuhuzunika na kuwa na mashaka watu wanapokuacha na kukuona huna maana kwao, na kuona ya kuwa hawakuhitaji tena, hupaswi kulazimisha, wala hupaswi kujikomba komba, wewe umeumbwa kwa thamani kubwa sana  na; Ni Mungu tu aliyekuumba ndiye anayeijua thamani yako, kwa hiyo hatujifunzi kubomoa uhusiano hapa katika somo hili lakini tunajifunza kuwaachia watu wanaojiondoa katika maisha yetu wajiondoe, wataendelea kuwa rafiki zetu, na tutaendelea kuwapenda, lakini kama hawajihusishi na maisha yetu hatupaswi kuumia lazima ufikie wakati ukubali waende na ujue ya kuwa Mungu ameruhusu waende zao!, na kuna faida zake katika hilo, kwa hiyo hupaswi kulazimisha wakae, kwani unapojaribu kulazimisha kuwa na watu ambao wameshajiondoa katika maisha yako au Mungu amewaondoa katika maisha yako hii maana ni nini? Maana yake yake unajaribu kung’ang’ania, na kulazimisha kitu ambacho, Mungu ameshamalizana nacho katika maisha yako!, fahamu kuwa kila mtu ambaye Mungu alimleta kwako alimleta yeye kwa kusudi la kukujenga na kukupa changamoto na unapofika wakati mtu huyo au watu hao wanaondoka fahamu kuwa ni Mungu amewaondoa kwako kwa kusudi maalumu, kwa hiyo hupaswi kushangaa, kulalamika au kujifikiri kuwa una mapungufu na kulalamika na kuhuzunika na kulaani hapana!

Kifungu kile cha msingi tulichokisoma leo, ndicho ambacho kinabeba mafunuo yote ambayo Mungu amekusudia kutufundisha katika siku ya leo kwa mfumo wa kichambuzi (an Expository preachings) na tutakiangalia kupitia mstari kwa mstari tukizingatia vipengele husika katika somo hili hebu tukisome tena na kisha tutakifanyia uchambuzi wake

Yohana 6:65-69 “Akasema, Kwa sababu hiyo nimewaambia ya kwamba hakuna mtu awezaye kuja kwangu isipokuwa amejaliwa na Baba yangu. Kwa ajili ya hayo wengi miongoni mwa wanafunzi wake wakarejea nyuma, wasiandamane naye tena. Basi Yesu akawaambia wale Thenashara, Je! Ninyi nanyi mwataka kuondoka? Basi Simoni Petro akamjibu, Bwana! Twende kwa nani? Wewe unayo maneno ya uzima wa milele. Nasi tumesadiki, tena tumejua, ya kuwa wewe ndiwe Mtakatifu wa Mungu.”

Tutajifunza somo hili “Je ninyi nanyi mwataka kuondoka?” kwa kuzingatia vipengele vitatu vifuatavyo:-

 

·         Mungu ndiye mwanzilishi wa uhusiano.

·         Maumivu ya kuvunjika kwa uhusiano.

·         Je ninyi nanyi mwataka kuondoka?

 

Mungu ndiye mwanzilishi wa uhusiano

Yohana 6:65 “Akasema, Kwa sababu hiyo nimewaambia ya kwamba hakuna mtu awezaye kuja kwangu isipokuwa amejaliwa na Baba yangu.”

Katika kifungu hiki Yesu Kristo anatufunulia jambo ambalo sio tu linatokea katika maisha yake lakini vile vile linatokea katika maisha yetu kama watoto wa Mungu, Yesu alizungumza hili kuhusiana na wanafunzi wake akieleza kuwa hakuna mtu awezaye kuja kwake isipokuwa amejaliwa na baba yake wa Mbinguni, hili linatufunualia sisi nasi kuwa Ni Mungu ndiye anayeruhusu watu watukaribie na ni Mungu ndiye anayeruhusu watu waondoke,  Marafiki zetu wanaweza kuwa msaada mkubwa sana katika maisha yetu, wanaweza kutumiwa na Mungu kututia moyo, kutusaidia, kutujenga na kutupa ufahamu fulani katika safari zetu za kiroho na kimwili na kisaikolojia na kimakuzi, kwa hiyo marafiki ni neema ya Mungu, ni kupitia mahusiano ya kirafiki Mungu huwatumia marafiki kutuonyesha upendo, kutuonyesha namna na jinsi Mungu anavyojali, na hata kututia moyo na wakati mwingine huwatumia kutupa changamoto, kwa hiyo kila urafiki ni lazima utunzwe na kuchukuliwa kama zawadi ya Mungu katika maisha yetu na kuwa kupitia wao liko kusudi la Mungu, marafiki wengine huokoa maisha yetu kutoka katika maangamizi ya adui, wengine hutufundisha kuwa hata kama wako watu wanatuchukia bado wako ambao wanatuthamini sana na wanathamini mchango wetu na umuhimu wetu katika dunia hii, wengine hutusaidia kukua kiroho, na wengine tunawasaidia wao kukua kiroho na kadhalika kwa ujumla tunahitajiana na ndio maana tunahitaji ushirika.

1Samuel 18:1-5 “Ikawa Daudi alipokwisha kusema na Sauli, roho ya Yonathani, ikaambatana na roho ya Daudi, Yonathani akampenda kama roho yake mwenyewe. Sauli akamtwaa siku ile, wala hakumwacha arudi tena nyumbani kwa baba yake. Nao Yonathani na Daudi wakaahidiana, kwa kuwa alimpenda kama roho yake mwenyewe. Ndipo Yonathani akalivua joho alilokuwa amelivaa, akampa Daudi, na mavazi yake, hata na upanga wake pia, na upinde wake, na mshipi wake. Basi Daudi akatoka kwenda kila mahali alikotumwa na Sauli, akatenda kwa akili; Sauli akamweka juu ya watu wa vita; jambo hili likawa jema machoni pa watu wote, na machoni pa watumishi wa Sauli pia.”

Daudi hakukubalika sana kwa Sauli lakini hata hivyo mwana wa mfalme Yonathan alikuwa rafiki mwenye kufaa sana kwa Daudi, maandiko yanaeleza kuwa Yonathan alimkubali Daudi na na watu hawa walikuwa na agano la urafiki uliodumu sana hata baada ya maisha yao, ulikuwa ni urafiki wa kweli na wenye kufaa sana, ulikuwa ni urafiki wenye uhusiano wa kina kama uhusiano wa ndugu, Yonathan alikuwa mwelewa kwa rafiki yake Daudi, Yonathan aliyajua mapenzi ya Mungu yaliyokuwa juu ya Daudi, Yonathan hakuwa rafiki mwenye wivu wala hila, Yonathan alimtia moyo Daudi, alimpa mavazi ya kifalme aliyotumia mwenyewe, alimpa silaha, alimlinda alikuwa akimtakia mema, pamoja na kuwa baba wa Jonathan hakumpenda Daudi, alimchukia alimkusudia mabaya lakini haikuwa hivyo kwa Yonathan yeye alikuwa rafiki wa kweli. Na mtu ambaye aliangalia maslahi ya Mungu kwa upana. Hakuwahi kumponda wala kumchafulia sifa yake wala kutaka rafiki yake asipate kibali kwa mfalme, wakati wote Yonathan alikuwa faraja kubwa

1Samuel 19:4-6 “Naye Yonathani akamsifu Daudi kwa Sauli, babaye akamwambia, Mfalme asikose juu ya mtumishi wake, yaani, juu ya Daudi kwa maana yeye hakukosa juu yako, tena matendo yake kwako yamekuwa mema sana. Kwa kuwa alitia uhai wake mkononi mwake, na kumpiga yule Mfilisti, naye Bwana akawatendea Israeli wote wokovu mkuu. Wewe mwenyewe uliona jambo hilo, ukafurahi; basi kwa nini kukosa juu ya damu isiyo na hatia, umwue huyo Daudi bure?Sauli akaisikiliza sauti ya Yonathani; naye Sauli akaapa, Aishivyo Bwana, yeye hatauawa.”

Kwa ujumla Yonathan alikuwa rafiki wa kweli kwa Daudi, alikuwa ni zaidi ya ndugu, alilinda uhai wa Daudi, na hakukubali maisha ya Daudi yawe hatarini wakati wote alitengeneza mazigira mazuri, ili raiki yake akubalike kwa baba yake asionekane kuwa muhalifu, alimtetea na kumtia Moyo na alimjulisha kuhusu hatari ambazo zingeweza kumkabili, kama tunataka kujifunza watu waliokuwa na urafiki wa dhati basi Daudi na Yonathani ni mfano wa kuigwa, Yonathani alikuwa ni rafiki aliyeambatana na Daudi na mwenye kufaa sana kuliko ndugu.

Mithali 18:24 “Ajifanyiaye rafiki wengi ni kwa uangamivu wake mwenyewe; Lakini yuko rafiki aambatanaye na mtu kuliko ndugu.”              

Marafiki zetu hawaji wenyewe kwetu huwa tunaletewa na Mungu na Mungu ndiye anayewavuta watu kuja kwetu, kama vile tu alivyowavuta wanafunzi kuja kwa Yesu Kristo, hakuna mtu awezaye kuja kwangu, isipokuwa amejaliwa na Baba yangu, Neno hilo kujaaliwa katika kiyunani linatumika neno “Didōmi” kimatamshi ni Did-o-mee ambalo maana yake “with the palm of hand” yaani ni tendo la Mungu kuushika mkono na kumleta mtu moja kwa moja na kushikisha katika kiganja cha mkono wa mwingine kama tu vile mtu anayemkabidhi bibi harusi kwa mumewe siku ya harusi yake, kwa hiyo Ni Mungu Baba ndiye anayetushika mkono na kutupeleka katika mikono ya Yesu, hali kadhalika ni Mungu ndiye anayewashika mkono wale waliokusudiwa kuwa rafiki zetu na kuwaleta katika mikono yetu, Kwa hiyo ni muhimu sana kutomchukulia kwa dharau mtu awaye yote anayetamani kuwa na urafiki na wewe kwa sababu kila unayeletewa au anayekujia analetwa kwako na Mungu kwa kusudi maalumu katika maisha yako na kwa ufalme wa Mungu, wakati wote watu wanapokuwa marafiki mioyo yao inaunganishwa kuwa kitu kimoja kwaajili ya mafanikio ya yule ambaye Mungu amemkusudia au kwa kufaidiana, na kila wakati Mungu huhakikisha kuwa pande zote mbili zinanufaika na urafiki huo, kwa hiyo wote mnajengana na kufaidiana kwani chuma hunoa chuma Mithali 27:17 “Chuma hunoa chuma; Ndivyo mtu aunoavyo uso wa rafiki yake.” Marafiki zetu huletwa kwetu na Mungu kwa kusudi la kutusaidia na sisi kuwasaidia na wakati mwingine kwajili ya kufaidiana, kama Barnaba na Sauli au Paulo

Matendo 9:26-28 “Na Sauli alipofika Yerusalemu, alijaribu kujiunga na wanafunzi, nao walikuwa wakimwogopa wote, wasisadiki ya kuwa yeye ni mwanafunzi. Lakini Barnaba akamtwaa, akampeleka kwa mitume, akawaeleza jinsi alivyomwona Bwana njiani, na ya kwamba alisema naye, na jinsi alivyohubiri kwa ushujaa katika Dameski kwa jina la Yesu. Naye akawa pamoja nao katika Yerusalemu akiingia na kutoka.”

Maumivu ya kuvunjika kwa uhusiano.

Yohana 6:66 “Kwa ajili ya hayo wengi miongoni mwa wanafunzi wake wakarejea nyuma, wasiandamane naye tena.”

Hata hivyo Pamoja na kuwa Mungu huwaleta watu karibu nasi kama tulivyojifunza kutoka kwa Bwana Yesu ni jambo la kusikitisha kuwa, kuna wakati  mwingine wengine wataondoka kama ilivyokuwa tu kwa Yesu, watu au wanafunzi wengi siku hiyo waliamua kuondoka tena biblia inasema wasiambatane naye tena, hapa ni kwa sababu walishindwa kupokea mafundisho yake magumu katika akili zao, jambo hili linatufunza ya kuwa si kila mtu anayeanza safari pamoja nasi atakuwa pamoja nasi mpaka mwisho, na wakati huu ni wakati wa maumivu makali sana hakuna jambo linaumiza kama kuvunjika kwa mahusiano, yawe ya ndoa, yawe na ushirika, yawe ya kichungaji, kazini na kadhalika, lakini Mungu huruhusu watu hao waende na huo ndio unakuwa mwisho wa stori yao katika maisha yetu, inauma sana na inaumiza sana lakini hatuna budi kukubali, kama ilivyokuwa kwa Yesu Kristo ambapo wanafunzi wake walimuacha na hawakuambatana naye tena ndivyo ilivyo kwetu pia kuna kusudi kwa kila jambo katika maisha yetu,  wakati huo hakuna lolote tunaloweza kulifanya kuwafanya wabaki, Mungu tayari amekwisha kukusudia, wakuache wale wanaokupenda kwa dhati hawawezi kukuacha  watabaki na wewe iwe jua iwe mvua lakini wale ambao Mungu amekusudia waende wataenda tu hakua namna unaweza kulizuia hilo, hukuwaleta wewe kumbuka kwa hiyo  acha waende zao kwa amani, Kama Mungu ndiye aliyeamua waende hakuna unaloweza kulifanya wasiende?

Mungu ndiye mwenye funguo na mamlaka za kufunga na akifunga hakuna afunguaye, na akifungua hakuna anayeweza kufunga unaweza kujaribu kubembeleza na kujipendekeza kwa watu na ukajitahidi kuwapendeza na kufanya vizuri lakini kama Bwana hajaruhusu utakuwa unajisumbua bure, kile utakachokuwa unakitafuta ni kutafuta maumivu ya moyo tu, jaribu njia mpya na waache waende usiumie wala usikwazike ni Mungu ameruhusu, lazima tuamini kuwa Mungu ndiye anayedhibiti watu kuja na kuondoka katika maisha yetu na wengine huletwa kwetu kwa majira fulani tu kisha anawaondoa, unapoendelea kuwang’ang’ania watu ambao wamepoteza maana katika maisha yako maana yake unazuia kusonga kwako mbele au kukua katika kiwango kingine. Rafiki mimi ninajua uchungu wa kupoteza marafiki, ninapenda watu sana, sitaki kila ambaye amewahi kuwa rafiki yangu aniache, lakini uko wakati unalazimika kufanya hivyo, wako wapi uliosoma nao shule ya msingi, sekondari, vyuoni, na hata katika utumishi huu wako wapi? Wako wapi uliofanya nao kazi zamani,? Ulifika wakati waliondoka na Mungu aliwaficha na hukuweza kuwaona tena, kusudi la kuwepo kwao katika maisha yako lilikwisha kutimia na sasa Mungu anataka ufungue ukurasa mpya. Ona mfano wa maumivu yaliyomkuta Naomi:-

Ruthu 1:3-18 “Akafa Elimeleki, mumewe Naomi; na yule mwanamke akasalia na wanawe wawili. Nao wakaoa wake katika wanawake wa Moabu; na jina la mmoja aliitwa Orpa, na jina la wa pili Ruthu. Wakakaa huko yapata miaka kumi. Wakafa na Maloni na Kilioni wote wawili; na huyo mwanamke akawa amefiwa na wanawe wawili, na mumewe pia. Ndipo alipoondoka, yeye na wakweze, ili kurudi kutoka nchi ya Moabu; maana huko katika nchi ya Moabu amesikia ya kwamba Bwana amewajilia watu wake na kuwapa chakula. Basi akatoka pale alipokuwapo, na wakweze wawili pamoja naye; wakashika njia ili kurudi mpaka nchi ya Yuda. Kisha Naomi akawaambia wakweze wawili, Nendeni sasa mkarejee kila mmoja nyumbani kwa mamaye; Bwana na awatendee mema ninyi, kama ninyi mlivyowatendea mema hao waliofariki na mimi pia. Bwana na awajalie kuona raha kila mmoja nyumbani kwa mumewe. Kisha akawabusu; nao wakapaza sauti zao wakalia. Wakamwambia, La, sivyo; lakini tutarudi pamoja nawe kwa watu wako.Naye Naomi akasema, Enyi wanangu, mrejee; kwani kufuatana na mimi? Je! Mimi ninao watoto wa kiume tena tumboni mwangu, hata wawe waume zenu? Enyi wanangu, mrejee; nendeni zenu; kwa kuwa mimi ni mzee, siwezi kupata mume tena. Kama ningesema, Natumaini; kama ningepata mume hata usiku huu, na kuzaa watoto wa kiume; je! Mngesubiri hata watakapokuwa watu wazima? Mngejizuia msiwe na waume? La, sivyo, wanangu; maana ni vigumu kwangu kuliko kwenu, kwa sababu mkono wa Bwana umetoka juu yangu. Nao wakapaza sauti zao, wakalia tena, na Orpa akambusu mkwewe, lakini Ruthu akaambatana naye. Naye akasema, Tazama, shemeji yako amerejea kwa watu wake, na kwa mungu wake; basi urejee wewe umfuate shemeji yako. Naye Ruthu akasema, Usinisihi nikuache, Nirejee nisifuatane nawe; Maana wewe uendako nitakwenda, Na wewe ukaapo nitakaa. Watu wako watakuwa watu wangu, Na Mungu wako atakuwa Mungu wangu; Pale utakapokufa nitakufa nami, Na papo hapo nitazikwa; Bwana anitende vivyo na kuzidi, Ila kufa tu kutatutenga wewe nami. Basi alipomwona kuwa amekaza nia yake kufuatana naye, aliacha kusema naye.”

Tunasoma habari za Naomi, ambaye mumewe alifariki na kumuacha na watoto wawili ambao nao baadaye walioa, lakini vile vile walikufa katika nchi ya Moabu, kwa hiyo Naomi alibaki peke yake yeye na wakwe zake, Naomi aliamua kurudi kwao Yuda na aliwaeleza wakweze juu ya maamuzi yake mmoja aliitwa Orpa na mwingine Ruthu, Ruthu aliamua kubaki naye na Orpa aliamua kubaki katika inchi yake, wote walimpenda mkwe wao Naomi lakini Orpa aliamua kumbusu Naomi na kuondoka, Naomi hakuanza kulalamika kuwa Orpa anaondoka hata pamoja na wema wote aliomtendea na malezi yote aliyowapa Naomi alielewa kuwa huu ni msimu mpya ni msimu wa mabadiliko katika maisha kwa hiyo alikuwa na amani alipoachwa na Orpa alikubali kuwa Orpa aende na asiwe sehemu ya maisha yake tena, Mtu aliyekomaa kiroho/na kiufahamu huwaachia watu waende, unakubali Mungu awaondoe watu fulani katika maisha yako, Mungu ndiye anayefunga mlango au kufungua, lakini Ruthu aliamua kubaki na Naomi kwa gharama yoyote ile, hii ndio hali halisi, Yesu watu waliondoka na hakutikisika aliwauliza waliobaki naye je ninyi nanyi mwataka kuondoka? Aliendelea kuacha mlango wazi kwa kila anayetaka kumuacha, Naomi Orpa aliondoka ulikuwa wakati mgumu na wa maumivu makali sana, ulikuwa ni wakati mgumu ulikuwa ni wakati wa machozi lakini hakuna tunachoweza kufanya pale watu waliokuwa rafiki, waliokuwa ndugu waliokuwa jamaa zetu, waliokuwa wenzetu waliokuwa tunashinda nao, na kuzungumza nao wanapoamua kutuacha ni vema kukubali waende, Naomi alimbusu Orpa na kumuacha aende, kumbuka  hatuhitaji kufukuza mtu au kumaliza nao vibaya wala kuwa na uadui nao lakini sasa wanaondoka utafanya nini tuwaache waende zao kwa Amani huo ndio ukomavu wa kifikra na ukomavu kiroho na ujuzi, sio wewe tu utaacha wewe pia unaweza kuachwa na watu uliowapenda lakini wakawa hawakuhitaji tena huwezi kubadili pai isiwe 22/7  ni lazima ukubaliane na ukweli wa mambo hata kama ni mchungu kiasi gani waache waende! 

Yesu aliwahi kuwafundisha wanafunzi wake kuwa sio kila mahali watawakubali, ziko sehemu nyingine watu watakukataa hawatafungua mioyo yao kwako, watakukataa hawatakukaribisha unajua unachotakiwa kukifanya ni kukung’uta mavumbi ya miguu yako kisha enenda kule ambako watakukaribisha, hii sio kwa ugomvi ni sehemu ya kawaida kabisa katika maisha kwamba watu watakuja kwetu na kisha wataondoka na sisi halikadhalika.

Mathayo 10:13-14 “Na nyumba ile ikistahili, amani yenu na iifikilie; la, kwamba haistahili, amani yenu na iwarudie ninyi.Na mtu asipowakaribisha wala kuyasikiliza maneno yenu, mtokapo katika nyumba ile, au mji ule, kung'uteni mavumbi ya miguuni mwenu.”

Matendo 18:6-8 “Walipopingamana naye na kumtukana Mungu, akakung'uta mavazi yake, akawaambia, Damu yenu na iwe juu ya vichwa vyenu; mimi ni safi; tangu sasa nitakwenda kwa watu wa Mataifa. Akaondoka huko akaingia katika nyumba ya mtu mmoja jina lake Tito Yusto, mcha Mungu, ambaye nyumba yake ilikuwa mpaka mmoja na sinagogi. Na Krispo, mkuu wa sinagogi, akamwamini Bwana pamoja na nyumba yake yote. Wakorintho wengi waliposikia, waliamini, wakabatizwa.”

Usijisumbue na watu ambao hawakutaki, watu ambao hawaoni thamani yako, wala usijaribu kuwashawishi, endapo utafanya hivyo utajichelewesha na utajipatia fadhaa bure, Ni kweli Mungu anaweza kuwabadilisha  kama watatakiwa kukuunga mkono lakini kamwe usijaribu kujilazimisha kuungana na watu wasiotambua uthamani wako, damu ya kifalme ya Yesu Kristo inatitiririka katika mwili wako wewe sio wa kawaida wewe ni mali ya Mungu na ndio maana Mungu alikuokoa na amekuumba kwa sura na mfano wake kwa hiyo usiwashawishi watu wakukubali kama mioyo yao imefungwa, Mungu ameandaa watu tayari wanaotambua uthamani wako, inaweza kuwa inauma sana lakini ndio ukubwa achana nao waache waende, katika maisha yetu wako Orpa wengi lakini vile vile wako Ruthu wengi ambao wamepangiwa kutokutuacha watakaokaa nasi, na kuambatana nasi wanaoondoka ni kuwa Mungu amemalizana nao katika kusudi lao kwako na wanaobaki ni wale ambao Mungu anataka ushirikiane nao Baraka zako, wale walio kama Ruthu watabaki kuwa waaminifu kwako  na hawatakuacha daima, hatupaswi kumfukuza mtu wala kumpiga teke mtu lakini acha wao watupige teke na kutufukuza na hapo neema ya Mungu ya urafiki wetu kwao itakuwa imefikia ukingoni  inasikitisha inaumiza sana lakini huu ndio ukweli katika maisha.

Matendo 15:36-40 “Baada ya siku kadha wa kadha Paulo akamwambia Barnaba, Haya! Mrejee sasa tukawaangalie hao ndugu katika kila mji tulipolihubiri neno la Bwana, wa hali gani.Barnaba akaazimu kumchukua Yohana aliyeitwa Marko pamoja nao. Bali Paulo hakuona vema kumchukua huyo aliyewaacha huko Pamfilia, asiende nao kazini. Basi palitokea mashindano baina yao hata wakatengana. Barnaba akamchukua Marko akatweka kwenda Kipro.Lakini Paulo akamchagua Sila, akaondoka, akiombewa na wale ndugu apewe neema ya Bwana.”

Paulo na Barnaba walikuwa marafiki, waliitwa pamoja  na Roho Mtakatifu katika kazi ya huduma, waliihubiri injili kwa pamoja kimsingi Barnaba alikuwa ni kama Mchungaji wa Paulo mtume, ni yeye ndiye aliyemtambulisha kwa mitume na ni yeye aliye mpeleka Antiokia, walizoeana sana, waliitwa kwa pamoja na Roho Mtakatifu kwa kazi ya umisheni, lakini ulifika wakati wakaachana haikuwa kwa lengo baya wala kwa ugomvi, lakini ulifika wakati ambapo Mungu alikusudia kila mmoja awe na njia yake hili ni jambo la kawaida sana katika maisha wao tofauti yao ilikuwa ni Marko, nadhani inawezekana Marko alijisikia vibaya maana Paulo alimuona ni mtu dhaifu, Lakini Barnaba aliona Marko anahitaji malezi tu kwa hiyo kulitokea tofauti na kulitokea matengano, Lakini Mungu ni mmoja, miaka mingi baadaye, Paulo aliutambua umuhimu wa Marko na aliomba aungane naye maana anamfaa kwa huduma! Angalia:-

2Timotheo 4:10-11 “Maana Dema aliniacha, akiupenda ulimwengu huu wa sasa, akasafiri kwenda Thesalonike; Kreske amekwenda Galatia; Tito amekwenda Dalmatia. Luka peke yake yupo hapa pamoja nami. Umtwae Marko, umlete pamoja nawe, maana anifaa kwa utumishi.”

Paulo alimkumbuka Marko na kuagiza aletwe kwake kwa sababu ana faida nyingi sana kwa utumishi, kumbe kuna mtu anaweza asiwe na faida kwako leo, lakini akawa na faida kwako kesho, unaweza usimuhitaji mtu leo lakini ukamuhitaji mtu huyo kesho, Mungu ndiye anayehusika anaweza mtu asikufae kwa jua akakufaa kwa mfua na anaweza mtu asikufae kwa mvua akakufaa kwa jua hii ndio dunia ya Mola kwa hiyo tuheshimu mahuisiano sana  na kuyatunza isipokuwa pale to Mungu anapoamua huyu aende kule na huyu aje hapa kwa makusudi yake mema.

Wakati mwingine mafanikio yetu yanaweza kuwavuta watu wengi sana kwetu, na mapito yetu yanaweza kuwafanya wengi watukimbie, unapitia upweke? Wakati wa changamoto hakuna mtu wa kukutia moyo? Hii ilimpata Ayubu Maandiko yanasema watu wa nyumbani mwake walikuwa wengi sana ona

Ayubu 1:3 “Mali yake nayo yalikuwa ni kondoo elfu saba, na ngamia elfu tatu, na jozi za ng'ombe mia tano, na punda wake mia tano, NA WATU WA NYUMBANI WENGI SANA; basi hivi mtu huyo alikuwa ni mkuu sana kuliko watu wote wa upande wa mashariki.”

Unaona tunasoma kuwa watu wa nyumbani kwa Ayubu walikuwa wengi sana wakati wa mafanikio yake, lakini wakati wa dhiki yake watu wote walimuacha na kundoka zao, hata hivyo wakati wa mafanikio yake walirejea tena kwa wingi sana, hili nalo ni jambo la kawaida katika uanadamu kwa hiyo usivunjike moyo unapopitia upweke!  

Ayubu   42:10-12 “Kisha Bwana akaugeuza uteka wa Ayubu, hapo alipowaombea rafiki zake; Bwana naye akampa Ayubu mara mbili kuliko hayo aliyokuwa nayo kwanza. Ndipo wakamwendea nduguze wote, waume kwa wake, nao wote waliojuana naye hapo zamani, wakala chakula pamoja naye katika nyumba yake; nao wakamlilia na kumtuza moyo katika habari za huo uovu wote Bwana aliouleta juu yake; kila mtu akampa kipande cha fedha, na pete ya dhahabu kila mmoja. Basi hivyo Bwana akaubarikia huo mwisho wa Ayubu zaidi ya mwanzo wake; naye alikuwa na kondoo kumi na nne elfu, na ngamia elfu sita, na jozi za ng'ombe elfu, na punda wake elfu.”

Wakati mwingine watu, na marafiki zako watakuacha kwa sababu tu unapita katika hali ngumu, lakini wanaweza kukurudia tena hali inapokuwa nzuri hili nayo ni jambo la kawaida katika maisha na hatuna budi kulielewa na kukubaliana nalo. Jambo kubwa la msingi ni kwamba mahusiano yanapaswa kutunzwa na kuwa na Amani na watu woe ni swala la smingi sana tuwapo duniani. lakini watu wanapoondolewa kwetu, tumshukuru Mungu kwaajili yao                                  

Je ninyi nanyi mwataka kuondoka?

Yohana 6:67-69 “Basi Yesu akawaambia wale Thenashara, Je! Ninyi nanyi mwataka kuondoka? Basi Simoni Petro akamjibu, Bwana! Twende kwa nani? Wewe unayo maneno ya uzima wa milele Nasi tumesadiki, tena tumejua, ya kuwa wewe ndiwe Mtakatifu wa Mungu.”

Yesu anatufundisha kuwa yeye alikuwa tayari kuwaacha watu waende zao, Kama wamechagua kwenda hakuwalazimisha kubaki nao lakini aliwapa uhuru wa kuondoka ili wafanye maamuzi yao wenyewe, waache waende zao kwa Amani, kama wamejisikia raha kuwa mbali na wewe wamejisikia Amani kukuacha acha waende! Na kama wamejisikia kubaki acha wabaki na wewe usiwalazimishe, kulazimisha watu wawe nawe wakati hawana Amani ya kuwa na wewe kutasababisha uchungu katika maisha yako, kukosa utulivu na majuto, lakini kama utawaacha waende watapata nafasi mpya na kujiamulia mambo yao wenyewe, wape watu uhuru wa kuamua  na Amani ya Mungu itaamua. Na huu ndio ukomavu wa kiroho, kiufahamu na kihekima. Let them go !

Wafilipi 4:6-7 “Msijisumbue kwa neno lo lote; bali katika kila neno kwa kusali na kuomba, pamoja na kushukuru, haja zenu na zijulikane na Mungu. Na amani ya Mungu, ipitayo akili zote, itawahifadhi mioyo yenu na nia zenu katika Kristo Yesu.”

Amini katika kusudi la Mungu kwamba Mungu anaporuhusu watu waende zao na au wabaki na wewe ufahamu kuwa Mungu ana mpango mkubwa na mpya na kila mmoja, inaweza kuwa ngumu kuelewa lakini hatuna budi kuamini katika mpango wa Mungu kwa kuwa Mungu ni mwema, watu wanapoondoka katika maisha yako iwe kwa wema au kwa ubaya bado fahamu ya kuwa Mungu ana mpango mwema kwenu wote yeye huweza kuitumia njia yoyote ile katika kutokeza jambo lililo jema zaidi.

Warumi 8:28 “Nasi twajua ya kuwa katika mambo yote Mungu hufanya kazi pamoja na wale wampendao katika kuwapatia mema, yaani, wale walioitwa kwa kusudi lake.”              

Rafiki wa kweli ni yule atakayesimama na wewe hata katika hali ngumu, Petro na wale thenashara walichagua kubaki na Yesu, Petro alisema tuende wapi Bwana wewe una maneno ya uzima wa milele, wako marafiki watakaa na wewe kwa muda mfupi, au watajitokeza kwako katika wakati Fulani maalumu na kisha watakoma lakini marafiki kama Petro kwa Yesu Kristo watamaanisha kubaki na wewe, kwa hiyo ni Muhimu kutambua umuhimu wao na kumshukuru Mungu kwaajili yao. Wakati wote kumbuka kuwa uhusiano wowote ule uwe wa muda au ule wa kudumu una kitu cha kutufundisha katika maisha yetu, hatukutanishwi na watu kwa bahati mbaya, Mungu hakumuumba mwanadamu awe peke yake, tunahitajiana, Lakini Mungu huruhusu watu waje na kuondoka katika maisha yetu kwa kusudi maalumu,  jambo kubwa na la msingi ni sisi kuendelea kuwa waaminifu katika kila aina ya uhusiano ambao Mungu ametupa kumbuka mahusiano yanapovunjika inaleta maumivu makali sana lakini wale wanaoondoka waache waende na wale wanaobaki kaa nao kumbuka kuwa ni Mungu ndiye anayewashika mkono na kuwaleta kwetu kwa hiyo amini katika mchakato huo na utakubali ukweli huu mchungu katika maisha, wafurahie sana wale wote ambao Mungu anawaleta katika maisha yako ukijua kuwa ni sehemu ya mpango wa Mungu,  wakubali wale wote ambao Mungu ameruhusu waende zao mbali na wewe ukijua pia kuwa Mungu ana mpango mwema, thamini umuhimu na msingi wa marafiki  hususani wale wanaobaki kuwa waaminifu kwako hasa wakati wa majaribu na wakati wa mambo magumu, waheshimu wote wapende wakubali lakini usilazimishe mtu akupende au awe na wewe hii haimaanishi uwatendee watu kikatili hapana lakini jifunze kuwa kama Yesu, Yesu aliwahoji hata wale waliobaki je ninyi nanyi mwataka kuondoka?  

Hatima yako haiko mikononi mwa waliokuacha, wala Mungu haitaji lolote uliloliacha au chochote ulichopoteza kupitia marafiki walioondoka, jambo kubwa la msingi uwe na Amani lakini usilazimishe watu wakupende na kukubali au wakuamini, ukiona wamekuacha maana yake huwahitaji tena, wao sio sehemu ya mpango wa Mungu katika maisha yako tena na Mungu ana mpango mwema na wewe na hata wale wanaokusema vibaya waache waseme, mimi nimewahi kusikia habari za mtu anayenisema vibaya na nikaonyeshwa sijawahi kumkataza wala kumbeleza aniseme vizuri, ninajua tu kuwa Mungu ameruhusu wawepo watu watakaonisema vizuri na wawepo watu watakaonisema vibaya wote wana faida katika mapenzi ya Mungu, wanaonisema vibaya wananisaidia nisiwe na kiburi, nikumbuke kuwa mimi ni mwanadamu na nizidi kunyenyekea na wale wanaofaidika na huduma yangu watamshukuru Mungu kwaajili yangu, sina muda wa kumbembeleza mtu asiniseme vibaya, siumii tena na wanaosema vibaya wala siwezi kutukuka watu wakinisifu, ninanyenyekea kwa Mungu kwa sababu mimi ni udongo tu, sikuja duniani kusifiwa, nimekuja duniani kutimiza kile ambacho Mungu amekikusudia katika maisha yangu na hivyo kile nitapangiwa na Mungu kukifanya nitakifanya, Petro alitambua ya kuwa Yesu ana maneno ya uzima wa milele, na ya kuwa ni Mtakatifu wa Mungu yaani ni Masihi.

Bwana ampe neema kila moja wetu kuelewa makusudi ya somo hili kwa kina na mapana na marefu katika jina la Yesu Amen!

 

Na. Rev Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni