Zaburi 34:15-18 “Macho ya Bwana huwaelekea
wenye haki, Na masikio yake hukielekea kilio chao. Uso wa Bwana ni juu ya
watenda mabaya, Aliondoe kumbukumbu lao duniani. Walilia, naye Bwana akasikia,
Akawaponya na taabu zao zote. Bwana yu karibu nao waliovunjika moyo, Na
waliopondeka roho huwaokoa.”
Utangulizi:
Mojawapo ya sifa kubwa ya Mungu
aliye hai ni pamoja na kuokoa! Mungu wa kweli ni lazima awe na sifa ya kuokoa
na uwezo wa kufanya hivyo, Watu wengi wanafahamu kuwa Moja ya kazi ya Mungu ni
kumuokoa mwanadamu na dhambi zake pamoja na matokeo ya dhambi hizo, hata hivyo
sio tu kuwa Mungu hutuokoa na dhambi na matokeo yake yaani athari zake lakini
pia hutuokoa na hatari za namna mbalimbali kwa hiyo Mungu hutuokoa na hatari za
aina zote. Mungu ni mwokozi.
Zaburi 68:19-22 “Na ahimidiwe Bwana, Siku
kwa siku hutuchukulia mzigo wetu; Mungu ndiye wokovu wetu. Mungu kwetu sisi ni
Mungu wa kuokoa; Na njia za kutoka mautini zina YEHOVA Bwana. Naam, Mungu
atakipasua kichwa cha adui zake, Utosi wenye nywele wa mtu afulizaye kukosa.
Bwana alisema, Kutoka Bashani nitawarudisha, Nitawarudisha kutoka vilindi vya
bahari;”
Kimsingi kila mwanadamu anahitaji
wokovu, katika maeneo mbalimbali, Tangu anguko la Adamu katika bustani ya Edeni
mambo yetu wanadamu yamekuwa hayatuendei kwa ukamilifu kama ilivyokuwa mwanzo
na kwa sababu hiyo tunamuhitaji Mwokozi, maisha ya mwanadamu yamejawa na taabu
na safari yetu haijanyooka, maisha yetu yamekuwa ya milima na mabonde, mchanganyiko
wa huzuni na furaha, uchungu na utamu, hatuna utulivu wa kutosha hatuwezi
kufurahia maisha moja kwa moja, Amani ya kweli imeingia mushikeli, fadhaa
zimetuzunguka kila upande, kukikucha ni kama hatuifurahii asubuhi, hata wale
tunaowaona kwa macho kuwa ni kama wanaonekana wana mafanikio makubwa wengine
wana changamoto kubwa zaidi kiasi cha kuwahurumia, tunamuhitaji Mungu
atakayetuokoa, tunamuhitaji atakayetuokoa mikononi mwa adui zetu ili hatimaye
tumuabudu Mungu pasipo hofu!, Watu waliomcha Mungu tangu mwanzo walikuwa
wakitazamia wokovu wake, walikuwa wanajua ya kuwa Mungu ameahidi kumleta
kiongozi atakayekuwa na msaada Mkubwa kwa wanadamu kifurushi kamili cha wokovu
kingekuwa juu yake yani huyu ni Yesu!
Luka 1:69-75 “Ametusimamishia pembe ya
wokovu Katika mlango wa Daudi, mtumishi wake. Kama alivyosema tangu mwanzo Kwa
kinywa cha manabii wake watakatifu;Tuokolewe na adui zetu Na mikononi mwao wote
wanaotuchukia; Ili kuwatendea rehema baba zetu, Na kulikumbuka agano lake
takatifu; Uapo aliomwapia Ibrahimu, baba yetu, Ya kwamba atatujalia sisi, Tuokoke
mikononi mwa adui zetu, Na kumwabudu pasipo hofu, Kwa utakatifu na kwa haki
Mbele zake siku zetu zote.”
Luka 2:25-31 “Na tazama, pale Yerusalemu
palikuwa na mtu, jina lake Simeoni, naye ni mtu mwenye haki, mcha Mungu,
akiitarajia faraja ya Israeli; na Roho Mtakatifu alikuwa juu yake. Naye alikuwa
ameonywa na Roho Mtakatifu ya kwamba hataona mauti kabla ya kumwona Kristo wa
Bwana. Basi akaja hekaluni ameongozwa na Roho; na wale wazazi walipomleta mtoto
Yesu ndani, ili wamfanyie kama ilivyokuwa desturi ya sheria, yeye mwenyewe
alimpokea mikononi mwake, akamshukuru Mungu, akisema, Sasa, Bwana, wamruhusu
mtumishi wako, Kwa amani, kama ulivyosema; Kwa kuwa macho yangu yameuona wokovu
wako, Uliouweka tayari machoni pa watu wote;”
Baba zetu walikuwa wakiutumainia
wokovu, wokovu ambao kwa kiyunani ni “SOTERIA” ni kifurushi cha ukombozi
ambacho ndani yake kuna msamaha wa dhambi, kuna ushindi dhidi ya dhambi, kuna
kutokulipwa sawaswa na makosa yetu, kuna faraja na amani ya kweli, kuna
kuponywa magonjwa, kuna kushindiwa vita, kuna kuokolewa kutoka utumwani, kuna nguvu
ya kushinda umasikini, na kuharibiwa kwa laana zote ni nani asiye hitaji
wokovu? Kila mmoja anahitaji wokovu na kwa sababu hiyo kila mmoja anamuhitaji
mwokozi na ni Mungu pekee anayeweza kuokoa, wokovu ni kazi ya Mungu peke yake!
Leo basi tutachukua muda kidogo kujikumbusha juu ya somo hili muhimu lenye
swali Je Mungu wako aweza kukuokoa?
Na tutajifunza hivyo kwa kuzingatia vipengele vitatu vifuatavyo!
·
Je Mungu
wako aweza kukuokoa?
·
Mungu
awezaye kuokoa!
·
Je wewe
una Mungu anayeweza kuokoa?
Je Mungu wako aweza kuokoa?
Kwa kuwa wanadamu wanapitia
changamoto za aina mbalimbali katika maisha! Mara nyingi sana wanadamu wamekuwa
wakijiuliza swali Je Mungu anaweza kuokoa? Kwa maana ya kuwa katika kila
changamoto tunazokutana nazo tunaweza kujiuliza kuwa je Mungu anaweza kunitoa
katika hali hii? Je Mungu anaweza kukushindia katika hali hiyo unayoipitia? Unaweza
wakati mwingine kupita katika hali na mazingira magumu sana ya kusikitisha,
kutisha, kuhuzunisha, kuvunja moyo na kukatisha tamaa na ukadhani ya kuwa Mungu
hashughuliki na hali hiyo au hawezi kushughulika na hali unayoipitia Je Mungu
wako anaweza kukuokoa? Katika maandiko tunapewa mifano ya watu mbalimbali ambao
walikuwa wanakabiliwa na hali za kutisha na katika kutishiwa huko ilifikiriwa
kuwa hawataweza kabisa kupata wokovu, shetani vilevile kupitia maajenti wake
alitaka kujua kuwa watu hao wataokolewa namna gani katika kona ambayo walikuwa
wamekabwa? Na kutishiwa ikifikiriwa ya kuwa hakuna mungu anayeweza kuwaokoa!
Hezekia - 2Wafalme 19:10-14 “Mwambieni
Hezekia, mfalme wa Yuda, maneno haya, mkisema, Asikudanganye Mungu wako
unayemtumaini, akisema, Yerusalemu hautatiwa katika mikono ya mfalme wa Ashuru.
Tazama, umesikia ni mambo gani wafalme wa Ashuru waliyozitenda nchi zote, kwa
kuziangamiza kabisa; je! Utaokoka wewe? Je! Miungu ya mataifa wale, ambao baba
zangu waliwaangamiza, imewaokoa? Yaani, Gozani, na Harani, na Resefu, na wana
wa Adini waliokuwa katika Telasari? Yuko wapi mfalme wa Hamathi, na mfalme wa
Arpadi, na mfalme wa mji wa Sefarvaimu, na wa Hena, na wa Iva? Basi Hezekia akaupokea
waraka katika mikono ya wale wajumbe, akausoma; kisha Hezekia akapanda,
akaingia katika nyumba ya Bwana, akaukunjua mbele za Bwana.”
Shadraka, Meshaki na Abednego - Daniel 3:13-15 “Basi Nebukadreza akatoa amri kwa hasira na ghadhabu, waletwe hao Shadraka,
na Meshaki, na Abednego. Basi wakawaleta watu hao mbele ya mfalme. Nebukadreza
akajibu, akawaambia, Enyi Shadraka, na Meshaki, na Abednego, je! Ni kwa
makusudi hata hammtumikii mungu wangu wala kuisujudia sanamu ya dhahabu
niliyoisimamisha? Basi sasa, kama mkiwa tayari wakati mtakapoisikia sauti ya
panda, na filimbi, na kinubi, na zeze, na santuri, na zomari, na namna zote za
ngoma, kuanguka na kuisujudia sanamu niliyoisimamisha, ni vema; bali
msipoisujudia, mtatupwa saa iyo hiyo katika tanuru iwakayo moto; naye ni nani
Mungu yule atakayewaokoa ninyi na mikono yangu?”
Daniel - Daniel 6:19-20 “Asubuhi mfalme
akaondoka mapema, akaenda kwa haraka mpaka penye lile tundu la simba. Naye
alipolikaribia lile tundu, akamlilia Danieli kwa sauti ya huzuni; mfalme
akanena; akamwambia Danieli, Ee Danieli, mtumishi wa Mungu aliye hai, je! Mungu
wako, unayemtumikia daima, aweza kukuponya na simba hawa?”
Hezekia, Shadraki Meshaki na
Abednego pamoja na Daniel katika nyakati tofauti waliwahi kuwa na wakati Mgumu
ambao ulihitaji, wokovu na kila wakati walioupitia walipaswa kuonyesha kama
Mungu wanayemuamini anaweza kuwaokoa, zilikuwa ni nyakati ngumu kwani ni mpaka
uwe na imani katika Mungu wa kweli, anayeweza kuokoa ili uweze kupita katika
hali hiyo!, Wapinzani wako na wale wanaokupa changamoto za Mungu uliye naye
wanataka tu kujua kuwa katika hali uliyoko je Mungu wako anaweza kukuokoa?
Watataka kuona kama Mungu wako anaweza kukusaidia kama unamwamini Mungu wa
kweli Muumba wa mbingu na ardhi kwa hakika yeye anaweza kuokoa!
Yesu Kristo alipokuwa
ameshitakiwa kwa husuda na kuhukumiwa kuuawa msalabani adui zake walimsanifu
wakitaka ashuke msalabani ili yamkini ikiwezekana nao waweze kumuamini,
alipolia Mungu wangu Mungu wangu mbina umeniacha, walimdhihaki wakisema
anamuita Mungu aje kumuokoa walidhani kuwa Msalaba ni hatua ya mwisho na ya
kuwa kama wamemtundika msalabani hawezi kuchomoka tena, walisema amemtegemea
Mungu na amwokoe sasa!
Mathayo 27:39-43 “Nao waliokuwa wakipita
njiani wakamtukana, wakitikisa-tikisa vichwa vyao, wakisema, Ewe mwenye
kulivunja hekalu na kulijenga kwa siku tatu, jiokoe nafsi yako; ukiwa ndiwe Mwana
wa Mungu, shuka msalabani. Kadhalika na wale wakuu wa makuhani wakamdhihaki
pamoja na waandishi na wazee, wakisema, Aliokoa wengine, hawezi kujiokoa mwenyewe.Yeye
ni mfalme wa Israeli; na ashuke sasa msalabani, nasi tutamwamini. Amemtegemea
Mungu; na amwokoe sasa, kama anamtaka; kwa maana alisema, Mimi ni Mwana wa
Mungu.”
Wakati mwingine adui atakuweka mahali ambapo anadhani kwamba huwezi kuchomoka na ya kuwa hata Mungu unayemuamini hawezi kukuokoa na atakuchungulia na kukudhihaki akifikiri ya kuwa hakuna anayeweza kukuokoa, Lakini jambo moja la kufurahia ni kuwa kama unamwamini Mungu aliye hai tambua ya kuwa Mungu mwenyezi, Mungu wa baba zetu Mungu wa Ibrahimu, na Isaka na Yakobo ni mwokozi na hatashindwa kukuokoa hata kidogo, Imeandikwa hatamwacha mtakatifu wake aone uharibifu, Mungu hatatuacha katika uharibifu hata kidogo! Atakuokoa yeye ni mwokozi!
Mungu awezaye kuokoa!
Mungu anayeweza kuokoa ni yule
ambaye anaweza kumuokoa mtu au taifa au jamii katika shida zao zote, Ni Mungu
ambaye hawezi kuvumilia mateso na huzuni, Ni Mungu anayeweza kukuepusha na
majanga ya kila aina, majaribu ya kila aina na mateso ya kila aina, matisho ya
kila aina, mitego ya kila aina, Magonjwa ya kila aina, hatari za kila aina na
hata kifo, sio tu kuwa Mungu anaweza kuokoa lakini vile vile anauwezo wa
kulinda na hata kuingilia kati maswala mbalimbali yanayoonekana kuwa magumu
katika maisha yetu.Yeye anatujua vema wakati tunapohitaji msaada wake na
hujitokeza mara na kuuleta wokovu kwa wakati anajua muda na wakati sahihi wa
kukutetea na kufanya hivyo:-
Wakati Hezekia alipokuwa
akitishiwa kuhusu mji wa Yerusalem kuwa utapigwa na Ashuru na kupewa shuhuda
jinsi mfalme wa Ashuru alivyoangamiza miji mingine na miungu, hata kuandikiwa
barua ya vitisho yeye aliichukua barua hiyo na kuipeleka mbele za Mungu wake
hekaluni na kisha akaishitakia mbele za Bwana Mungu wake awezaye kuokoa, katika
namna ya kushangaza sana Mungu aliyajibu maombi yake na hali ya mambo ikawa
tofauti, Mungu alimuokoa Hezekia na watu wake na mji wa Yerusalem lakini pia
Senekarebu mfalme wa Ashuru aliuawa mbele ya mungu wake asiye na msaada.
2Wafalme 19:15-19 “Naye Hezekia akaomba
mbele za Bwana, akasema, Ee Bwana, Mungu wa Israeli, ukaaye juu ya makerubi,
wewe, naam, wewe peke yako, ndiwe Mungu wa falme zote za dunia; wewe ndiwe
uliyeziumba mbingu na nchi. Tega sikio lako, Ee Bwana, usikie; fumbua macho
yako, Ee Bwana, uone; uyasikie maneno ya Senakeribu, ambayo amemtuma mtu aje
nayo ili kumtukana Mungu aliye hai. Ni kweli, Bwana, wafalme wa Ashuru
wamewaharibu mataifa na nchi zao, na kuitupa miungu yao motoni; kwa maana
haikuwa miungu, bali ni kazi ya mikono ya wanadamu; ilikuwa miti na mawe tu,
ndiyo sababu wakaiharibu. Basi sasa, Ee Bwana, Mungu wetu, utuokoe na mkono
wake, nakusihi, ili kwamba falme zote za dunia zipate kujua ya kuwa wewe ndiwe
Bwana Mungu, wewe peke yako.”
2Wafalme 19:32-37 “Basi Bwana asema hivi
katika habari za mfalme wa Ashuru, Yeye hatauingia mji huu, wala hatapiga
mshale hapa, wala hatakuja mbele yake kwa ngao, wala hatajenga boma juu yake.
Njia ile ile aliyojia, kwa njia iyo hiyo atarudi zake, wala hataingia ndani ya
mji huu, asema Bwana. Maana nitaulinda mji huu, niuokoe, kwa ajili yangu
mwenyewe, na kwa ajili ya Daudi, mtumishi wangu. Ikawa usiku uo huo malaika wa
Bwana alitoka, akakiingia kituo cha Waashuri, akawapiga watu mia na themanini
na tano elfu. Na watu walipoondoka asubuhi na mapema, kumbe! Hao walikuwa maiti
wote pia. Basi Senakeribu mfalme wa Ashuru akaondoka, akaenda zake, akarudi
akakaa Ninawi. Ikawa, alipokuwa akiabudu nyumbani mwa Nisroki, mungu wake,
Adrameleki na Shareza wakampiga kwa upanga; wakaikimbilia nchi ya Ararati. Na
Esar-hadoni mwanawe akatawala mahali pake.”
Wakati Daniel alipofanyiwa fitina
na mawaziri wenye wivu kiasi cha Daniel kutupwa katika tundu la simba wenye
njaa, jambo la kushangaza ni kuwa wakati mfalme alipojaribisha kuwatupa wale
waliofanya fitina katika tundu la simba ni ukweli ulio wazi kuwa walitafunwa
juu juu hata kabla miili yao haijagusa chini na tangu wakati huo mfalme
aliamuru watu wote katika utawala wake wamuabudu na kumtumikia Mungu wa Daniel
kwa sababu ni Mungu aliye hai na mwenye uweza wa kuokoa!
Daniel 6:21-27 “Ndipo Danieli akamwambia
mfalme, Ee mfalme, uishi milele. Mungu wangu amemtuma malaika wake, naye
ameyafumba makanwa ya simba, nao hawakunidhuru; kwa kuwa mbele zake mimi
nalionekana kuwa sina hatia; tena, mbele yako, Ee mfalme, sikukosa neno. Basi
mfalme akafurahi sana, akaamuru wamtoe Danieli katika lile tundu. Ndipo Danieli
akatolewa katika lile tundu, wala dhara lo lote halikuonekana mwilini mwake, kwa
sababu alikuwa anamtumaini Mungu wake. Mfalme akaamuru, nao wakawaleta wale
watu waliomshitaki Danieli, wakawatupa katika tundu la simba, wao, na watoto
wao, na wake zao; na wale simba wakawashinda wakaivunja mifupa yao vipande
vipande, kabla hawajafika chini ya tundu. Ndipo mfalme Dario akawaandikia watu
wa kabila zote, na taifa zote, na lugha zote, waliokaa juu ya uso wa dunia;
Amani na iongezeke kwenu. Mimi naweka amri, ya kwamba katika mamlaka yote ya
ufalme wangu watu watetemeke na kuogopa mbele za Mungu wa Danieli; maana yeye
ndiye Mungu aliye hai, adumuye milele, na ufalme wake ni ufalme usioharibika,
na mamlaka yake itadumu hata mwisho. Yeye huponya na kuokoa, hutenda ishara na
maajabu mbinguni na duniani, ndiye aliyemponya Danieli na nguvu za simba.”
Wakati Shadraka na Meshaki na
Abednego walipotupwa katika tanuru la moto uliokolezwa sana huku mfalme
Nebukadreza akidhania ya kuwa hakuna Mungu anayeweza kuwaokoa ni ukweli uliowazi
kuwa vijana hao wa kiyahudi walimuamini Mungu aliye hai na hata walipotupwa
kwenye moto muujiza mkubwa ulitokea kwani walikuwa akipiga stori na malaika
kwenye moto wakiwa salama bila kuungua tukio na mujiza uliopelekea mfalme
kuamuru kuwa watu wote wamuabudu Mungu aliyeweza kuwaokoa watu wake katika
tanuru la Moto kwa sababu hakuonekana Mungu anayeweza kuokoa kwa namna kama ile.
Daniel 3:19-29 “Ndipo Nebukadreza akajaa
ghadhabu, na sura ya uso wake ikabadilika juu ya Shadraka, na Meshaki, na
Abednego, basi akatoa amri watie moto ile tanuru mara saba kuliko desturi yake
ya kutiwa moto. Kisha akawaamuru baadhi ya watu mashujaa wa jeshi lake
kuwafunga Shadraka, na Meshaki, na Abednego, na kuwatupa katika ile tanuru
iliyokuwa ikiwaka moto. Basi watu hao wakafungwa, hali wamevaa suruali zao, na
kanzu zao, na joho zao, na mavazi yao mengine, wakatupwa katikati ya ile tanuru
iliyokuwa ikiwaka moto. Basi kwa sababu amri ya mfalme ilikuwa ni kali, na ile
tanuru ilikuwa ina moto sana, mwako wa ule moto ukawaua wale watu waliowashika
Shadraka, na Meshaki, na Abednego. Na watu hao watatu, Shadraka, na Meshaki, na
Abednego, wakaanguka, hali wamefungwa, katikati ya ile tanuru iliyokuwa inawaka
moto. Ndipo Nebukadreza akastaajabu, akainuka kwa haraka; akanena, akawaambia
mawaziri wake, Je! Hatukutupa watu watatu, hali wamefungwa, katikati ya moto?
Wakajibu, wakamwambia mfalme, Kweli, Ee mfalme. Akajibu, akasema, Tazama, mimi
naona watu wanne, nao wamefunguliwa, wanatembea katikati ya moto hali hawana
dhara; na sura yake yule wa nne ni mfano wa mwana wa miungu. Kisha Nebukadreza
akaukaribia mdomo wa ile tanuru iliyokuwa inawaka moto. Akanena, akasema, Enyi
Shadraka, na Meshaki, na Abednego, watumishi wa Mungu Aliye juu, tokeni, mje
huku. Ndipo Shadraka, na Meshaki, na Abednego, wakatoka katika ule moto. Na
maamiri, na manaibu, na maliwali, na mawaziri, waliokuwa wamekusanyika pamoja,
wakawaona watu hao, ya kuwa ule moto ulikuwa hauna nguvu juu ya miili yao, wala
nywele za vichwa vyao hazikuteketea, wala suruali zao hazikubadilika, wala harufu
ya moto haikuwapata hata kidogo. Nebukadreza akanena, akasema, Na ahimidiwe
Mungu wa Shadraka, na Meshaki, na Abednego; aliyemtuma malaika wake, akawaokoa
watumishi wake waliomtumaini, wakaligeuza neno la mfalme, na kujitoa miili yao
ili wasimtumikie mungu mwingine, wala kumwabudu, ila Mungu wao wenyewe. Basi
mimi naweka amri ya kuwa kila kabila ya watu, na kila taifa, na kila lugha,
watakaonena neno lo lote lisilopasa juu ya huyo Mungu wa Shadraka, na Meshaki,
na Abednego, watakatwa vipande vipande, na nyumba zao zitafanywa jaa; kwa kuwa
hakuna Mungu mwingine awezaye kuokoa namna hii.”
Yesu Kristo ambaye alidhihakiwa
na kusulubiwa msalabani na kusanifiwa na adui zake na kupewa maneno ya kejeli
walidhani ya kuwa Mungu hawezi kumsaidia, Neno la Mungu linasema, Mungu alimsikiliza
na alimuokoa na mauti na hakumwacha Mtakatifu wake aone uharibifu kwani Kristo Yesu
huyo Mungu alimfufua
Matendo 2:32 “Basi kwa kuwa ni nabii,
akijua ya kuwa Mungu amemwapia kwa kiapo, ya kwamba katika uzao wa viuno vyake
atamketisha mmoja katika kiti chake cha enzi; yeye mwenyewe akitangulia kuyaona
haya, alitaja habari za kufufuka kwake Kristo, ya kwamba roho yake haikuachwa
kuzimu, wala mwili wake haukuona uharibifu. Yesu huyo Mungu alimfufua, na sisi
sote tu mashahidi wake.”
Matendo 4:9-12 “kama tukiulizwa leo habari ya jambo jema alilofanyiwa yule mtu dhaifu, jinsi alivyoponywa, jueni ninyi nyote na watu wote wa Israeli ya kuwa kwa jina la Yesu Kristo wa Nazareti, ambaye ninyi mlimsulibisha, na Mungu akamfufua katika wafu, kwa jina hilo mtu huyu anasimama ali mzima mbele yenu. Yeye ndiye jiwe lile lililodharauliwa na ninyi waashi, nalo limewekwa kuwa jiwe kuu la pembeni. Wala hakuna wokovu katika mwingine awaye yote, kwa maana hapana jina jingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo.”
Je wewe una Mungu anayeweza kuokoa?
Tumejifunza kutoka katika mifano
ya kibiblia ya wenzetu ambao walikuwa na Mungu anayeweza kuokoa na aliwaokoa
walipokuwa na changamoto za aina mbalimbali, ukiwa na Mungu mwenye nguvu na
anayeweza kuokoa unaweza kutembea katika hii dunia ukiwa na Amani na furaha na
kiburi ya kuwa una Mungu anayeweza kutumainiwa, Mungu anayeweza kutegemewa,
Mungu aliye hai, Mungu anayetetea, Mungu anayejali, Mungu anayelinda, Mungu
anayejishughulisha sana na Mambo yetu, ukiwa na Mungu wa aina hii ni raha
iliyoje duniani. Watakatifu waliotutangulia walikuwa na Mungu wa aina hii
anayeweza kuokoa na waliufurahia wokovu wao katika mazingira na maeneo
mbalimbali ni Mungu wa pekee anayeweza kutumainiwa ni yeye peke yake anayeokoa,
Mungu mwenyewe amejifunua kwetu na kutamba kuwa anaweza kuokoa na kuwa hakuna
Mungu mwingine
Isaya 43:11-15 “Mimi, naam, mimi, ni Bwana,
zaidi yangu mimi hapana mwokozi. Nimetangaza habari, nimeokoa, nimeonyesha, na
hapakuwa mungu wa kigeni kati yenu; kwa sababu hiyo ninyi ni mashahidi wangu,
asema Bwana, nami ni Mungu. Naam, tangu siku ya leo, mimi ndiye; wala hapana
awezaye kuokoa katika mkono wangu; mimi nitatenda kazi, naye ni nani awezaye
kuizuia? Bwana, Mkombozi wenu, Mtakatifu wa Israeli, asema hivi; Kwa ajili yenu
nimetuma ujumbe Babeli nami nitawashusha wote mfano wa wakimbizi, naam,
Wakaldayo, katika merikebu zao walizozifurahia. Mimi ni Bwana, Mtakatifu wenu,
Muumba wa Israeli, mfalme wenu.”
Sisi wakristo tunamuamini Mungu anayeweza
kutuokoa na hakuna mwingine duniani wala mbinguni awezaye kuokoa isipokuwa yeye
peke yake na kwa jina lake Yesu Kristo ukiliitia Mungu amekusudia kutupa wokovu
kwa yeye, kila mmoja anapaswa kujitathimini kama je kweli ana Mungu anayeweza
kuokoa? Mimi ninaye Mungu anayeweza kuokoa, sisi tunaye Mungu anayeweza kuokoa,
Maandiko yanamtaja Yesu, kuwa ni Yesu Peke yake mwenye uwezo huo! Nje ya Yesu
hakuna mwokozi
Matendo 4:10-12 “jueni ninyi nyote na watu
wote wa Israeli ya kuwa kwa jina la Yesu Kristo wa Nazareti, ambaye ninyi
mlimsulibisha, na Mungu akamfufua katika wafu, kwa jina hilo mtu huyu anasimama
ali mzima mbele yenu. Yeye ndiye jiwe lile lililodharauliwa na ninyi waashi,
nalo limewekwa kuwa jiwe kuu la pembeni. Wala hakuna wokovu katika mwingine
awaye yote, kwa maana hapana jina jingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu
litupasalo sisi kuokolewa kwalo.”
Waebrania 7:25-27 “Naye, kwa sababu hii,
aweza kuwaokoa kabisa wao wamjiao Mungu kwa yeye; maana yu hai sikuzote ili
awaombee. Maana ilitupasa sisi tuwe na kuhani mkuu wa namna hii aliye
mtakatifu, asiyekuwa na uovu, asiyekuwa na waa lo lote, aliyetengwa na
wakosaji, aliyekuwa juu kuliko mbingu; ambaye hana haja kila siku, mfano wa
wale makuhani wakuu wengine, kwanza kutoa dhabihu kwa ajili ya dhambi zake
mwenyewe, kisha kwa ajili ya dhambi za hao watu; maana yeye alifanya hivi mara
moja, alipojitoa nafsi yake.”
Je wewe unaye Mungu anayeweza
kukuokoa? Shida na changamaoto zako hazikomi wala haziondoki kwa sababu huna Mungu
anayeweza kuokoa, huna Mungu anayeweza kukusikia wala huna Mungu
anayeshughulika na mambo yako, Mungu asiye na msaada ni wa nini? je wewe una
Mungu wa aina gani? Sisi Mungu wetu yuko hai, yuko mbinguni na uwezo anao
alitakalo hulitenda.Na ni kimbilio letu
Zaburi 115:3-9 “Lakini Mungu wetu yuko
mbinguni, Alitakalo lote amelitenda. Sanamu zao ni fedha na dhahabu, Kazi ya
mikono ya wanadamu. Zina vinywa lakini hazisemi, Zina macho lakini hazioni, Zina
masikio lakini hazisikii, Zina pua lakini hazisikii harufu, Mikono lakini hazishiki,
miguu lakini haziendi, Wala hazitoi sauti kwa koo zake. Wazifanyao watafanana
nazo, Kila mmoja anayezitumainia. Enyi Israeli, mtumainini Bwana; Yeye ni
msaada wao na ngao yao.”
Zaburi 46:1-5 “Mungu kwetu sisi ni kimbilio
na nguvu, Msaada utakaoonekana tele wakati wa mateso. Kwa hiyo hatutaogopa
ijapobadilika nchi, Ijapotetemeka milima moyoni mwa bahari. Maji yake
yajapovuma na kuumuka, Ijapopepesuka milima kwa kiburi chake. Kuna mto, vijito
vyake vyaufurahisha mji wa Mungu, Patakatifu pa maskani zake Aliye juu. Mungu
yu katikati yake hautatetemeshwa; Mungu atausaidia asubuhi na mapema.”
Nakutangazia ya kuwa mimi nina
Mungu aliye hai, nina shuhudua nyingi za ajabu na za kutisha jinsi na namna
Mungu aliye hai aliyonishindia na kunipigania, Ikiwa unataka kuona uhai wa
Mungu wangu wewe jaribu kushughulika nami na ujichanganye unikorofishe katika
habari za Mungu wangu, I tell you the truth you will be eliminated! Do tot mess
up with me or my God! Kama unataka kupotea chezea mimi cheza na Mungu wangu ni
Mungu ambaye anaokoa na kubariki na ameahidi sio tu kunibariki lakini pia yeye
ni ngao yangu na thawabu yangu kubwa sana ninakusihi msomaji wangu na
msikilizaji wangu hakikisha ya kuwa una uhusiano na Mungu aliye hai Mungu wa
kweli na hutakuja kujuta. Yeyote atakaye jaribu kushindana nawe
atasambaratishwa vibaya, ni Mungu ambaye haruhusu uonevu hata kidogo, haogopi
wafalme wala mtu mwonevu wote anawakemea kwa sababu ya aina ya mafuta aliyokupaka
onja habari za Bwana Mungu wangu utembee kifua mbele Mwamini Bwana Yesu
utetewe, Mwamini mfanye kuwa Bwana na mwokozi wa maisha yako na utaokolewa onja
uone ya kuwa Bwana ni mwema! Yesu Kristo hana mzaha na mali yake ikiwa
unamuamini na kumtegemea jua ya kuwa kwa jina lake Mungu ameruhusu watu wote
waokolewe kila atakayeliitia jina la Bwana yaani Yesu Kristo ataokoka, Ni vema
kumtegemea Mungu ambaye ni mwokozi, acha kutegemea miungu mingine isiyokuwa na
msaada, sisi tunaye Mungu anayeokoa leo hii kama utamuamini na kumsadiki na
kutegemea kwa hakika hutatahayarika, kama ilivyoandikwa ya kuwa kila amuaminiye
yeye hatatatahayarika kamwe, Mungu na akuokoe katika kila changamoto
unayoipitia katika jina la Yesu Kristo mwana wa Mungu aliye hai amen!
Na Rev. Innocent Samuel Kamote
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni