Jumapili, 14 Juni 2026

Huyu ndiye Mwanangu, mpendwa, msikieni yeye!


Mathayo 17:1-5 “Na baada ya siku sita Yesu akawatwaa Petro, na Yakobo, na Yohana nduguye, akawaleta juu ya mlima mrefu faraghani; akageuka sura yake mbele yao; uso wake ukang'aa kama jua, mavazi yake yakawa meupe kama nuru. Na tazama, wakatokewa na Musa na Eliya, wakizungumza naye. Petro akajibu akamwambia Yesu, Bwana, ni vizuri sisi kuwapo hapa; ukitaka, nitafanya hapa vibanda vitatu, kimoja chako wewe, na kimoja cha Musa, na kimoja cha Eliya. Alipokuwa katika kusema, tazama, wingu jeupe likawatia uvuli; na tazama, sauti ikatoka katika lile wingu, ikasema, Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, ninayependezwa naye; msikieni yeye.”


 

Utangulizi.

Moja ya maneno ya msingi ambayo dunia inapaswa kuyazingatia ni haya yaliyowahi kutamkwa na Mungu Baba mwenyewe katika mlima wa ugeuko (transfiguration) mbele ya Petro Yakobo na Yohana. Kauli hii ni moja ya kauli nzito sana katika Agano jipya kwa sababu ni kauli yenye mamlaka kubwa nayomtambulisha Bwana wetu Yesu Kristo kwa mamlaka kubwa ili kwamba wanadamu wote wamsikilize kumtii na kumfuata Kauli hii imerejewa kwa msisitizo katika njili zile tatu zifananazo, Mathayo, Marko na Luka.

Marko 9:2-7 “Hata baada ya siku sita Yesu akawatwaa Petro, na Yakobo, na Yohana, akawaleta juu ya mlima mrefu faraghani, peke yao; akageuka sura yake mbele yao; mavazi yake yakimeta-meta, meupe mno, jinsi asivyoweza dobi duniani kuyafanya meupe. Wakatokewa na Eliya pamoja na Musa, nao walikuwa wakizungumza na Yesu.Petro akajibu, akamwambia Yesu, Rabi, ni vizuri sisi kuwapo hapa; na tufanye vibanda vitatu, kimoja chako wewe, kimoja cha Musa, na kimoja cha Eliya. Maana, hakujua la kunena, kwa kuwa waliingiwa na hofu nyingi. Kisha likatokea wingu, likawatia uvuli; sauti ikatoka katika lile wingu, Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, msikieni yeye.”

Luka 9:28-35 “Baada ya maneno hayo yapata siku nane, aliwatwaa Petro na Yohana na Yakobo, akapanda mlimani ili kuomba. Ikawa katika kusali kwake sura ya uso wake ikageuka, mavazi yake yakawa meupe, yakimeta-meta. Na tazama, watu wawili walikuwa wakizungumza naye, nao ni Musa na Eliya; walioonekana katika utukufu, wakanena habari za kufariki kwake atakakotimiza Yerusalemu.Petro na wale waliokuwa pamoja naye walikuwa wamelemewa na usingizi; lakini walipokwisha amka waliuona utukufu wake, na wale wawili waliosimama pamoja naye. Ikawa hao walipokuwa wakijitenga naye, Petro alimwambia Yesu, Bwana mkubwa, ni vizuri sisi kuwapo hapa; na tufanye vibanda vitatu; kimoja chako wewe, na kimoja cha Musa, na kimoja cha Eliya; hali hajui asemalo. Alipokuwa akisema hayo, lilitokea wingu likawatia uvuli, wakaogopa walipoingia katika wingu hilo. Sauti ikatoka katika wingu, ikisema, Huyu ni Mwanangu, mteule wangu, msikieni yeye.”

Injili zote tatu zifananazo (Synoptic Gospel) zimerekodi tukio hili muhimu, lililoshuhudiwa na Petro, Yakobo na Yohana kwa sababu ya umuhimu wake mkubwa ambao leo tutachukua muda kuutafakari na kuusisitiza kwa jamii ili kila mtu duniani apate kusadiki ya kuwa Yesu ni mwana wa Mungu na kwamba yeye ndiye njia na kweli na uzima na hakuna mwingine kabla yake na baada yake, umuhimu wa tukio hili kwa mtazamo wangu hauko katika kubadilika sura kwa Yesu Kristo, wala katika kutokewa na Musa na Eliya lakini uzito mkubwa wa tukio hili uko katika sauti ile “Huyu ndiye Mwanangu, mpendwa, msikieni yeye!”, tutajifunza somo hili HUYU NDIYE MWANANGU MPENDWA MSIKIENI YEYE kwa kuzingatia vipengele muhimu vitatu vifuatavyo:-

·         Maana ya neno Msikieni yeye!

·         Umuhimu wa Yesu Kristo kwa wanadamu.

·         Huyu ndiye Mwanangu mpendwa msikieni yeye.

Maana ya neno Msikieni yeye

Wote tutakuwa tunafahamu kuwa neno la Kiebrania kuhusu kusikia linajulikana kama neno “SHEMA” maana yake katika kiingereza “hear” or “Listen” “understand” “Obey” or “take action”neno hili lina uzito mkubwa sana katika maandiko ya Kiebrania sio kwaajili ya kusikia sauti pekee bali kusikia, kutii na kutekeleza, neno hilo likifanyiwa kazi kimsingi lina Baraka kubwa sana na lisipofanyiwa kazi linasababisha laana mikosi na balaa, kwa hiyo kila Myahudi alisisitizwa kuwa na bidii katika kusikia, utaisikiliza sauti ya Bwana Mungu wako, huu ulikuwa ni msisitizo wa kitorati

Kumbukumbu 6:3-5 “SIKIZA BASI, EE ISRAELI, ukaangalie kuzitenda; upate kufanikiwa, mpate kuongezeka sana, kama Bwana, Mungu wa baba zako, alivyokuahidi, katika nchi ijaayo maziwa na asali. Sikiza, Ee Israeli; Bwana, Mungu wetu, Bwana ndiye mmoja. Nawe mpende Bwana, Mungu wako, kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa nguvu zako zote.”

Kutoka 19:5-6 “Sasa basi IKIWA MTAITII SAUTI YANGU kweli kweli, na kulishika agano langu, hapo ndipo mtakapokuwa tunu kwangu kuliko makabila yote ya watu; maana dunia yote pia ni mali yangu, nanyi mtakuwa kwangu ufalme wa makuhani, na taifa takatifu. Hayo ndiyo maneno utakayowaambia wana wa Israeli.”

Kumbukumbu 28:1-2 “Itakuwa UTAKAPOSIKIA SAUTI YA BWANA, Mungu wako, kwa bidii, kutunza kuyafanya maagizo yake yote nikuagizayo leo, ndipo Bwana, Mungu wako, atakapokutukuza juu ya mataifa yote ya duniani;na baraka hizi zote zitakujilia na kukupata usikiapo sauti ya Bwana, Mungu wako.”

Kutoka 23:20-26 “Tazama, mimi namtuma malaika aende mbele yako, ili akulinde njiani na kukupeleka mpaka mahali pale nilipokutengezea. Jitunzeni mbele yake, mwisikize sauti yake; wala msimtie kasirani; maana, hatawasamehe makosa yenu; kwa kuwa jina langu limo ndani yake. Lakini UKIISIKIZA SAUTI yake kweli, na KUYATENDA YOTE ninenayo mimi; ndipo mimi nitakuwa ni adui wa adui zako, na mtesi wa hao wakutesao. Kwa kuwa malaika wangu atatangulia mbele yako, na kukufikisha kwenye Mwamori, na Mhiti, na Mperizi, na Mkanaani, na Mhivi, na Myebusi; nami nitawakatilia mbali. Usiisujudie miungu yao, wala kuitumikia; wala usitende mfano wa matendo yao; bali utaiangamiza kabisa, na nguzo zao utazivunja vipande vipande. Nanyi mtamtumikia BWANA, Mungu wenu, naye atakibarikia chakula chako, na maji yako; nami nitakuondolea ugonjwa kati yako. Hapatakuwa na mwenye kuharibu mimba, wala aliye tasa, katika nchi yako; na hesabu ya siku zako nitaitimiza.”

Kwa hiyo kama wanafunzi wa Biblia utakuwa umegundua kuwa neno kusikia, sikia, msikilizeni, tiini, linaambatana na baraka kubwa sana ulimwenguni, endapo watu wa Mungu watajifunza na kuelewa kuwa kusikia, kuna maana ya kutii, kutunza, kufanya, kuishi, kuamini na kufuata na ndani ya neno hili kuna siri kubwa sana ya Baraka za Mungu ni kama Baraka zote zimefungwa katika kusikiliza kunakotajwa kimaandiko yaani SHEMA basi kumsikia Yesu ni Baraka.

Kwa hiyo Sauti ya Mungu Baba iliposikika kwa Petro, Yakobo na Yohana Huyu ndiye mwanangu mpendwa msikieni yeye, wanafunzi hawa wa Yesu Kristo kwa kuwa walikuwa Wayahudi walikuwa na uelewa mpana wa kile ambacho mbingu zilikuwa zinakimaanisha kuhusu Yesu Kristo, mwanaye ni kwamba uko ulazima au amri kuwa yeye ni wa kuaminiwa, yeye ndiye wa kumtii, yeye ndiye wa kumfuata, yeye ndiye wa kumtegemea, yeye ndiye wa kusikilizwa, yeye ndiye wa kufuata maagizo yake yeye ndiye wa kutekeleza asemayo na hakuna mwingine kabla yake wala baada yake, Ni lazima wafuate mafundisho yake na kwa kumtii yeye Baraka zote zilizoahidiwa katika maandiko zitatufuata

Umuhimu wa Yesu Kristo kwa wanadamu.

Mathayo 17:1-5 “Na baada ya siku sita Yesu akawatwaa Petro, na Yakobo, na Yohana nduguye, akawaleta juu ya mlima mrefu faraghani; akageuka sura yake mbele yao; uso wake ukang'aa kama jua, mavazi yake yakawa meupe kama nuru. Na tazama, wakatokewa na Musa na Eliya, wakizungumza naye. Petro akajibu akamwambia Yesu, Bwana, ni vizuri sisi kuwapo hapa; ukitaka, nitafanya hapa vibanda vitatu, kimoja chako wewe, na kimoja cha Musa, na kimoja cha Eliya. Alipokuwa katika kusema, tazama, wingu jeupe likawatia uvuli; na tazama, sauti ikatoka katika lile wingu, ikasema, Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, ninayependezwa naye; MSIKIENI yeye.”

Tukio hili katika maandiko ni tukio la kipekee lisiloweza kusahaulika, Petro katika maisha yake yote aliweza kumtumikia Mungu kwa jina la Yesu na hata miaka mingi sana ilipopita bado aliendelea kulikumbuka tukio hili lililokuwa limemfunua Yesu Kristo katika ubora wake na kama Bwana aliyekubalika kwa mamlaka kubwa zaidi kuliko yeyote yule, hata wale walioheshimika sana  katika jamii ya Israel kama Musa na Eliya akam manabii wakubwa na muhimu sana, Petro hata alipokuwa anakaribia kufa bado alikumbuka tukio lile la kipekee, la kufunuliwa kwa heshima na utukufu na kuthibitishiwa ukuu wa Yesu Kristo kuliko manabii wote, kulikofanywa na Mungu Baba:-

2Petro 1:16-18 “Maana hatukufuata hadithi zilizotungwa kwa werevu, tulipowajulisha ninyi nguvu zake Bwana wetu Yesu Kristo na kuja kwake; bali tulikuwa tumeuona wenyewe ukuu wake. Maana alipata kwa Mungu Baba heshima na utukufu, hapo alipoletewa sauti iliyotoka katika utukufu mkuu, Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, ninayependezwa naye. NA SAUTI HIYO SISI TULIISIKIA ikitoka mbinguni tulipokuwa pamoja naye katika mlima ule mtakatifu”.

Mungu alitaka Petro, Yakobo na Yohana na walimwengu wote baada yao, kuwa na uelewa huu mkubwa kuhusu Yesu Kristo ili asitokee mtu akamvunjia Yesu Heshima, Yesu ni mkuu na mbora kuliko nabii Musa, Eliya na wengine wote, sio tu kuwa torati na manabii zilizungumza habari zake lakini hata Mungu Baba mwenyewe alithibitisha habari zake na kina Petro waliisikia sauti, iliyowathibitishia kuwa sifa za Yesu sio hadithi za kutungwa kwa werevu bali ni uthibitisho kutoka mbinguni kuwa Yesu ni mwana wa Mungu na ulimwengu unapaswa kumuamini yeye na kumtii;-

-          Maandiko yote yanaelekeza kwa Yesu Kristo – Unapoyachambua maandiko yote kutoka agano la kale mpaka mwisho kuanzia Torati na manabii wote walielekeza watu kwa Yesu Kristo na ukiona nabii anaelekeza watu kwa mtu mwingine na sio Kristo huyo ni nabii wa uongo, au ukiona nabii anaelekeza watu wamwamini yeye na sio Yesu Kristo basi huyo ni nabii wa uongo, Yesu Kristo ndio ufunuo wa mwisho wa Mungu kwa wanadamu wote.

Luka 24:25-31 “Akawaambia, Enyi msiofahamu, wenye mioyo mizito ya kuamini yote waliyoyasema manabii! Je! Haikumpasa Kristo kupata mateso haya na kuingia katika utukufu wake? Akaanza kutoka Musa na manabii wote, akawaeleza katika maandiko yote mambo yaliyomhusu yeye mwenyewe. Wakakikaribia kile kijiji walichokuwa wakienda, naye alifanya kama anataka kuendelea mbele.Wakamshawishi wakisema, Kaa pamoja nasi, kwa kuwa kumekuchwa, na mchana unakwisha. Akaingia ndani kukaa nao. Ikawa alipokuwa ameketi nao chakulani, alitwaa mkate, akaubariki, akaumega, akawapa. Yakafumbuliwa macho yao, wakamtambua; kisha akatoweka mbele yao.”

-          Musa ingawa alikuwa nabii mkubwa lakini aliwaelekeza watu kwa Yesu – Na kuamuru watu wote wamsikilize yeye yaani wamwamini, wamtii na kuyashika mafundisho yake, mtu awaye yote ambaye hatamsikiliza atakufa

Kumbukumbu 18:15-18 “Bwana, Mungu wako, atakuondokeshea nabii miongoni mwa ndugu zako kama nilivyo mimi; MSIKILIZENI YEYE. Kama vile ulivyotaka kwa Bwana, Mungu wako, huko Horebu, siku ya kusanyiko, ukisema, Nisisikie tena sauti ya Bwana, Mungu wangu, wala nisiuone tena moto huu mkubwa, nisije nikafa. Bwana akaniambia, Wametenda vema kusema walivyosema. Mimi nitawaondokeshea nabii miongoni mwa ndugu zao mfano wako wewe, nami nitatia maneno yangu kinywani mwake, naye atawaambia yote nitakayomwamuru.”

Matendo 3:22-24 “Kwa maana Musa kweli alisema ya kwamba, Bwana Mungu wenu atawainulieni nabii, katika ndugu zenu, kama MIMI; MSIKIENI YEYE katika mambo yote atakayonena nanyi. Na itakuwa ya kwamba kila mtu ASIYEMSIKILIZA NABII HUYO ATAANGAMIZWA na kutengwa na watu wake. Naam, na manabii wote tangu Samweli na wale waliokuja baada yake, wote walionena, walihubiri habari za siku hizi.”

-          Isaya alimuhubiri Kristo – Isaya alijulikana kama muhubiri mkubwa sana wa nyakati za agano la kale watu wengi wanamuita nabii wa Masihi au mwinjilishi wa agano la kale yeye alipewa neema ya kutoa unabii ulio wazi sana kuhusu Yesu Kristo ikiwepo mamlaka yake, kuzaliwa kwake na mateso yake akimuelezea Kristo miaka 700 kabla yake kwa uweza wa ajabu sana Isaya alimuhubiri Kristo na kumtaja kama mshauri wa ajabu, Mungu mwenye nguvu, baba wa milele na mfalme wa Amani, sasa utapata wapi uzima na uponyaji na wokovu kama humsikilizi?

Isaya 7:14 “Kwa hiyo Bwana mwenyewe atawapa ishara. Tazama, bikira atachukua mimba, atazaa mtoto mwanamume, naye atamwita jina lake Imanueli.”

Isaya 9:6 “Maana kwa ajili yetu mtoto amezaliwa, Tumepewa mtoto mwanamume; Na uweza wa kifalme utakuwa begani mwake; Naye ataitwa jina lake, Mshauri wa ajabu, Mungu mwenye nguvu, Baba wa milele, Mfalme wa amani.”

Isaya 53:1-9 “Ni nani aliyesadiki habari tuliyoileta? Na mkono wa Bwana amefunuliwa nani? Maana alikua mbele zake kama mche mwororo, Na kama mzizi katika nchi kavu; Yeye hana umbo wala uzuri; Na tumwonapo hana uzuri hata tumtamani. Alidharauliwa na kukataliwa na watu; Mtu wa huzuni nyingi, ajuaye sikitiko; Na kama mtu ambaye watu humficha nyuso zao, Alidharauliwa wala hatukumhesabu kuwa kitu.Hakika ameyachukua masikitiko yetu, Amejitwika huzuni zetu; Lakini tulimdhania ya kuwa amepigwa, Amepigwa na Mungu, na kuteswa. Bali alijeruhiwa kwa makosa yetu, Alichubuliwa kwa maovu yetu; Adhabu ya amani yetu ilikuwa juu yake, Na kwa kupigwa kwake sisi tumepona.Sisi sote kama kondoo tumepotea; Kila mmoja wetu amegeukia njia yake mwenyewe; Na Bwana ameweka juu yake Maovu yetu sisi sote.Alionewa, lakini alinyenyekea, Wala hakufunua kinywa chake; Kama mwana-kondoo apelekwaye machinjoni, Na kama vile kondoo anyamazavyo Mbele yao wakatao manyoya yake; Naam, hakufunua kinywa chake. Kwa kuonewa na kuhukumiwa aliondolewa; Na maisha yake ni nani atakayeisimulia? Maana amekatiliwa mbali na nchi ya walio hai; Alipigwa kwa sababu ya makosa ya watu wangu. Wakamfanyia kaburi pamoja na wabaya; Na pamoja na matajiri katika kufa kwake; Ingawa hakutenda jeuri, Wala hapakuwa na hila kinywani mwake.”

-          Yohana mbatizaji alimuhubiri Kristo na kuonyesha kuwa ni mwenye mamlaka kuu  – Yohana 1:26-30 “Yohana akawajibu akisema, Mimi nabatiza kwa maji. Katikati yenu amesimama yeye msiyemjua ninyi. Ndiye yule ajaye nyuma yangu, ambaye mimi sistahili kuilegeza gidamu ya kiatu chake. Hayo yalifanyika huko Bethania ng'ambo ya Yordani, alikokuwako Yohana akibatiza. Siku ya pili yake amwona Yesu anakuja kwake, akasema, TAZAMA, MWANA-KONDOO WA MUNGU, aichukuaye dhambi ya ulimwengu! Huyu ndiye niliyenena habari zake ya kwamba, Yuaja mtu nyuma yangu, ambaye amekuwa mbele yangu; kwa maana alikuwa kabla yangu.”

Yohana 3:26-31 “Wakamwendea Yohana, wakamwambia, Rabi, yeye aliyekuwa pamoja nawe ng'ambo ya Yordani, yeye uliyemshuhudia, tazama, huyo anabatiza na watu wote wanamwendea.Yohana akajibu, akasema, Hawezi mtu kupokea neno lo lote isipokuwa amepewa kutoka mbinguni. Ninyi wenyewe mwanishuhudia ya kwamba nalisema, Mimi siye Kristo, bali nimetumwa mbele yake. Aliye naye bibi arusi ndiye bwana arusi; lakini rafiki yake bwana arusi, yeye anayesimama na kumsikia, aifurahia sana sauti yake bwana arusi. Basi hii furaha yangu imetimia. Yeye hana budi kuzidi, bali mimi kupungua. Yeye ajaye kutoka juu, huyo yu juu ya yote. Yeye aliye wa dunia, asili yake ni ya dunia, naye anena mambo ya duniani. Yeye ajaye kutoka mbinguni yu juu ya yote.”           

-          Daudi – alihubiri na kutabiri kwa kina sana kwa habari ya mambo mengi kuhusu Yesu Kristo, na alimuita Bwana na kutabiri swala zima la kuketi katika mkono wa kuume wa Mungu huko mbinguni ona :-

 

Zaburi 110:1-2 “Neno la Bwana kwa Bwana wangu, Uketi mkono wangu wa kuume, Hata niwafanyapo adui zako Kuwa chini ya miguu yako. Bwana atainyosha toka Sayuni Fimbo ya nguvu zako. Uwe na enzi kati ya adui zako;”

Mathayo 22:41-46 “Na Mafarisayo walipokusanyika, Yesu aliwauliza, akisema, Mwaonaje katika habari za Kristo? Ni mwana wa nani? Wakamwambia, Ni wa Daudi. Akawauliza, Imekuwaje basi Daudi katika Roho kumwita Bwana, akisema, Bwana alimwambia Bwana wangu, Uketi mkono wangu wa kuume, Hata niwawekapo adui zako Kuwa chini ya miguu yako? Basi, Daudi akimwita Bwana, amekuwaje ni mwanawe? Wala hakuweza mtu kumjibu neno; wala hakuthubutu mtu ye yote tangu siku ile kumwuliza neno tena.”

-          Paulo mtume alimuelezea Yesu kwa kina sana - Wafilipi 2:5-11 “Iweni na nia iyo hiyo ndani yenu ambayo ilikuwamo pia ndani ya Kristo Yesu; ambaye yeye mwanzo alikuwa yuna namna ya Mungu, naye hakuona kule kuwa sawa na Mungu kuwa ni kitu cha kushikamana nacho; bali alijifanya kuwa hana utukufu, akatwaa namna ya mtumwa, akawa ana mfano wa wanadamu; tena, alipoonekana ana umbo kama mwanadamu, alijinyenyekeza akawa mtii hata mauti, naam, mauti ya msalaba. Kwa hiyo tena Mungu alimwadhimisha mno, akamkirimia Jina lile lipitalo kila jina; ili kwa jina la Yesu kila goti lipigwe, la vitu vya mbinguni, na vya duniani, na vya chini ya nchi; na kila ulimi ukiri ya kuwa YESU KRISTO NI BWANA, kwa utukufu wa Mungu Baba.”

Kila muhubiri nyakati za kanisa la kwanza alimuhubiri Kristo, kujulikana kwetu, kuheshimika kwetu hakutakuja kwa sababu ya kujijengea jina kutakuja kama tunamuinua Yesu Kristo katika maisha yetu na mahubiri yetu, kazi ya kila mtumishi wa Mungu ni kuwaelekeza watu wa Mungu kwa Yesu Kristo, nje ya Yesu Kristo huwezi kupata matokeo yanayokusudiwa, Mungu aliyemthibitisha Yesu kwa wanafunzi wake hawezi kumthibitisha kwa wasiomsikiliza au kumtii, kama tunataka kuona matokeo makubwa sana katika injili basi tumuhubiri Yesu Kristo:-

Filipo aliposhuka Samaria alimuhubiri Kristo na watu waliposikia waliponywa na kufunguliwa na kuokolewa - Matendo 8:5-8. “Filipo akatelemka akaingia mji wa Samaria, AKAWAHUBIRI KRISTO. Na makutano kwa nia moja WAKASIKILIZA maneno yale yaliyosemwa na Filipo walipoyasikia na kuziona ishara alizokuwa akizifanya. Kwa maana pepo wachafu wakawatoka wengi waliopagawa nao, wakilia kwa sauti kuu; na watu wengi waliopooza, na viwete, wakaponywa. Ikawa furaha kubwa katika mji ule.”

-          Ni Yesu Kristo pekee ndiye mwenye maneno ya uzima wa milele – watu wengi wanaweza kuwa na maneno ya Hekima “Falasafa”, lakini maneno hayo hayana uwezo wa kutoa uzima huu wala wa milele Yesu Kristo anayo maneno ya uzima wa milele, kila mtu anayemsikiliza anapewa uwezo wa kuwa na uzima wa milele

Yoahan 6:68-69 “Basi Simoni Petro akamjibu, Bwana! Twende kwa nani? Wewe unayo maneno ya uzima wa milele.Nasi tumesadiki, tena tumejua, ya kuwa wewe ndiwe Mtakatifu wa Mungu.”

-          Ni Yesu Kristo pekee ambaye anatajwa kuwa ndio njia na kweli na uzima, Mungu anataka watu wasimsikilize mwingine bali wamsikilize Yesu kwani wakimsikiliza yeye hawatapotea, Mungu hataki wanadamu wasikilize njia nyingine zinazopingana na Kristo au kuwaongoza kwenda upotevuni. Unataka uzima mwamini Bwana Yesu, mtii.

 Yohana 14:6 “Yesu akamwambia, Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi.”

-          Ni Yesu Kristo pekee ambaye amepewa mamlaka yote mbinguni na Duniani. Na jina kubwa kuliko majina yote iwe ni ya mbinguni au duniani uwezi kumfananisha Yesu Kristo na nabii mwingine yeyote, yeyote.

Mathayo 28:18 “Yesu akaja kwao, akasema nao, akawaambia, Nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani.”

Wafilipi 2:9-11 “Kwa hiyo tena Mungu alimwadhimisha mno, akamkirimia Jina lile lipitalo kila jina; ili kwa jina la Yesu kila goti lipigwe, la vitu vya mbinguni, na vya duniani, na vya chini ya nchi; na kila ulimi ukiri ya kuwa YESU KRISTO NI BWANA, kwa utukufu wa Mungu Baba.”     

Huyu ndiye Mwanangu mpendwa msikieni yeye.

Mathayo 17:1-5 “Na baada ya siku sita Yesu akawatwaa Petro, na Yakobo, na Yohana nduguye, akawaleta juu ya mlima mrefu faraghani; akageuka sura yake mbele yao; uso wake ukang'aa kama jua, mavazi yake yakawa meupe kama nuru. Na tazama, wakatokewa na Musa na Eliya, wakizungumza naye. Petro akajibu akamwambia Yesu, Bwana, ni vizuri sisi kuwapo hapa; ukitaka, nitafanya hapa vibanda vitatu, kimoja chako wewe, na kimoja cha Musa, na kimoja cha Eliya. Alipokuwa katika kusema, tazama, wingu jeupe likawatia uvuli; na tazama, sauti ikatoka katika lile wingu, ikasema, Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, ninayependezwa naye; MSIKIENI yeye.”

Wakati Mungu anasema maneno haya ya muhimu sana mapema katika tukio hilo, Musa na Eliya walikuwa wameonekana wakizungumza na Yesu akiwa katikati yao, kimsingi Musa anawakilisha Sheria au Torati na Eliya anawakilisha Manabii, Katika hali ya sintofahamu Petro alitoa ushauri ambao Mbingu ziliukataa na kutamka maneno hayo mazito,  Petro alisema ni vema wakikaa hapo na vikajengwa vibanda vitatu kimoja cha Kristo, kingine cha Musa na kingine cha Eliya, unajua ni kwanini Petro alitamka haya katika mawazo yake alifikiri kuwa Musa na Eliya wako sawasawa na Yesu na hapo ndipo Mungu alipoingilia kati kumjulisha Petro na wenzake kuwa manabii hao ni tofauti na Bwana Yesu “HUYU NDIYE MWANANGU MPENDWA NINAYEPENDEZWA NAYE MSIKIENI YEYE” maneno haya yalikuwa yanafunua uwazi wa Mungu Baba kuwa Yesu ni mkuu kuliko Musa, Yesu ni mkuu kuliko Eliya, Yesu ni zaidi ya manabii wote, Yesu ndiye utimilifu wa Sheria na manabii, kwa hiyo yeye ndiye wa kusikilizwa, yeye ndiye wa kuaminiwa, yeye ndiye wa kumtii, yeye ndiye wa kufuata yeye ndiye wa kuyashika mafundisho yake, yeye ndiye mtekeleze maagizo yake, yeye ndiye wa kutegemewa, kumlinganisha Yesu na Musa ni sawa na kumlinganisha mtimishi mwaminifu na Mwana mwaminifu katika nyumba ya Mungu.

Waebrania 3:3-6 “Kwa maana huyo amehesabiwa kuwa amestahili utukufu zaidi kuliko Musa, kama vile yeye aitengenezaye nyumba alivyo na heshima zaidi ya hiyo nyumba. Maana kila nyumba imetengenezwa na mtu; ila yeye aliyevitengeneza vitu vyote ni Mungu. Na Musa kweli alikuwa mwaminifu katika nyumba yote ya Mungu kama mtumishi, awe ushuhuda wa mambo yatakayonenwa baadaye; bali Kristo, kama mwana, juu ya nyumba ya Mungu; ambaye nyumba yake ni sisi, kama tukishikamana sana na ujasiri wetu na fahari ya taraja letu mpaka mwisho.”                

Kwa msingi huo mtu awaye yote ambaye hatamsikiliza Yesu Kristo huyo atakatiliwa mbali na watu wake, ataangamia

Matendo 3:22-23 “Kwa maana Musa kweli alisema ya kwamba, Bwana Mungu wenu atawainulieni nabii, katika ndugu zenu, kama mimi; msikieni yeye katika mambo yote atakayonena nanyi.Na itakuwa ya kwamba kila mtu asiyemsikiliza nabii huyo ataangamizwa na kutengwa na watu wake.”

Kwa hiyo maneno HUYU NDIYE MWANANGU MPENDWA NINAYEPENDEZWA NAYE MSIKILIZENI YEYE  Ni tamko la mamlaka ya kimbinguni linalomtangaza Yesu Kristo kuwa ndiye Masihi na Mwokozi wa ulimwengu na hakuna nabii mwingine yeyote ambaye ni mkubwa au ana heshima kubwa kuliko yeye tena wala hakuna mbadala wake, huyu ndiye Alfa na Omega kwa hiyo wito huo haukuwa wa Petro, Yakobo na Yohana bali ulikuwa ni wito kwa ulimwengu mzima kwamba macho na masikio yetu, mioyo yetu, imani yetu na utii wetu uelekezwe kwa Yesu, Musa alielekeza watu kwa Yesu, Manabii wote walielekeza kwa Yesu, Mitume walimuhubiri Kristo, na Roho Mtakatifu anamshuhudia Kristo, kwa hiyo hili lilikuwa onyo pia la wazi kwa wanadamu kwamba ole wako umwanimi mwingine au atakayekuja nyuma ya Yesu na kujifanya ni nabii au mjumbe wa mwenyezi Mungu, ni ujumbe unaowasaidia wakristo kutambua wazi nani ni nabii wa kweli na nani ni nabii wa uongo. Ole wako umuhubiri Siddhartha Gautama Budha wa Budha, ole wako umuhubiri Guru Nanak wa Sikhism, Ole wako umuhubiri Lao Tzu wa Taoisim, Ole wako Umuhubiri Master Confucius, wa Confucianism, Ole wako umuhubiri Zoroaster wa Zoroastrianism, Ole wako umuhubiri Bahaulah wa Bahai, Ole wako umuhubiri Muhamad wa Uislamu, mitume na watumishi wa Mungu wa kweli wanamuhubiri Kristo, sisi tunamuhubiri Yesu Kristo ya kuwa ni Bwana, ni hatari sana kumlinganisha Yesu na wanafalasafa wengine duniani.

2Wakorintho 4:3-5 “Lakini ikiwa injili yetu imesitirika, imesitirika kwa hao wanaopotea; ambao ndani yao mungu wa dunia hii amepofusha fikira zao wasioamini, isiwazukie nuru ya injili ya utukufu wake Kristo aliye sura yake Mungu. Kwa maana hatujihubiri wenyewe, bali Kristo Yesu ya kuwa ni Bwana; na sisi wenyewe kuwa tu watumishi wenu kwa ajili ya Yesu.”

Na Rev. Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima. 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni