Jumapili, 15 Machi 2026

Akilishika neno la imani vile vile kama alivyofundishwa!


Tito 1:7-9 “Maana imempasa askofu awe mtu asiyeshitakiwa neno, kwa kuwa ni wakili wa MUNGU; asiwe mtu wa kujipendeza nafsi yake, asiwe mwepesi wa hasira, asiwe mlevi wala mgomvi, asiwe mpenda mapato ya aibu.bali awe mkaribishaji, mpenda wema, mwenye kiasi, mwenye haki, mtakatifu, mwenye kudhibiti nafsi yake; akilishika lile neno la imani vile vile kama alivyofundishwa, apate kuweza kuwaonya watu kwa mafundisho yenye uzima, na kuwashinda wenye kupinga.”



Utangulizi:

Mojawapo ya sifa muhimu za viongozi wa kanisa ni pamoja na kuwa waaminifu katika mafundisho sahihi ya imani yetu (Sound Doctrine) na neno la Mungu, Paulo mtume alikuwa amemuacha Tito mtenda kazi pamoja naye katika makanisa yaliyokuwa katika kisiwa cha Krete moja ya kisiwa kikubwa na maarufu sana katika nchi ya Ugiriki, kwa kusudi la kuweka viongozi zamani waliitwa wazee (yaani wachungaji) katika makanisa yaliyokuwako huko.

Tito 1:4-5 “kwa Tito, mwanangu hasa katika imani tuishirikiyo. Neema na iwe kwako na amani zitokazo kwa Mungu Baba na kwa Kristo Yesu Mwokozi wetu. Kwa sababu hii nalikuacha Krete, ili uyatengeneze yaliyopunguka, na kuweka wazee katika kila mji kama vile nilivyokuamuru;”

Hata hivyo katika sifa kadhaa zilizoainishwa na Paulo Mtume kwaajili ya kuchagua viongozi mojawapo ya sifa muhimu sana ilikuwa inahusu kuchagua au kuweka watu ambao watalifundisha neno la Mungu vile vile kama wao walivyofundishwa, hili ilikuwa ni agizo muhimu sana kwa sababu Mafundisho sahihi ni sawa kabisa na mlo kamili wa chakula chenye virutubisho vyote muhimu vinavyohitajika katika mwili wa mwanadamu na mafundisho sahihi vile vile ni ya muhimu katika kanisa la Mungu kwa mustakabali wa kanisa kuwa na Afya njema, ukuaji mzuri wa kiroho, uhakika wa wokovu, na ulinzi wa kanisa dhidi ya mafundisho potofu, kuwanoa waamini, kukuza umoja wa kanisa na kuutunza utakatifu na maisha ya haki kutendeka kwa kazi ya huduma. Kwa msingi huo Kanisa linapochagua watenda kazi, wanafunzi na wenye hekima linapaswa kuhakikisha kuwa watu hao wanateuliwa kwa sababu wameshiba mafundisho yaliyo sahihi na wako tayari kwa huduma na si kwa sababu wana cheo, pesa na heshima fulani huko duniani, kwa Msingi huo leo tutachukua muda kujifunza somo hili muhimu “Akilishika neno la Imani vile vile kama alivyofundishwa!”, na tutajifunza somo hili kwa kuzingatia vipengele vitatu vifuatavyo:-

·         Maana ya kulishika neno la Imani vile vile.

·         Umuhimu wa kulishika neno la Imani vile vile kama ulivyofundishwa.

·         Akilishika neno la Imani vile vile kama alivyofundishwa!,

Maana ya kulishika neno vile vile.

Ni muhimu kufahamu kuwa kulishika neno la Mungu vile vile kama unavyofundishwa maana yake kwa Kiyunani  linatumika neno “antechomenon” au “antechomai” ambalo kwa kiingereza linatumika neno “holding fast to” au “adhering to” au “clinging” au “to hold firm” kwa lugha nzuri ya Kiswahili maana yake ni kushikamana, kung’ang’ania  au kutetea kwa uthabiti, kwa hiyo moja ya sifa ya kiongozi wa kanisa anapaswa kuwa king’ang’anizi, linapokuja swala la kushikamana na Mungu au mafundisho yake hapaswi kuwa mtu unayeyumbishwa, anapaswa kuwa mtu mwenye uwezo wa kusimamia kile unachokiamini kwa nguvu na hakuna mtu wa kukubadilisha.

Ayubu 2:9-10 “Ndipo mkewe akamwambia, Je! Wewe hata sasa washikamana na utimilifu wako? Umkufuru Mungu, ukafe. Lakini yeye akamwambia, Wewe wanena kama mmoja wa hao wanawake wapumbavu anenavyo. Je! Tupate mema mkononi mwa Mungu, nasi tusipate na mabaya? Katika mambo hayo yote Ayubu hakufanya dhambi kwa midomo yake.”

Sifa ya kushikamana na mafundisho ya mitume au injili ya kweli na mafundisho yaliyo sahihi ilikuwa na umuhimu mkubwa sana nyakati za kanisa la kwanza kama ilivyo na umuhimu mkubwa zaidi katika nyakati za leo, kwa hiyo mtu aliyependekezwa kuwa kiongozi alipaswa kuwa na sifa ya kuenenda vile vile kama alivyofundishwa, hakuna uhuru wa kuibadili injili, kwa hiyo kiongozi alikuwa hawezi kupotoshwa wala kuyumbishwa na hawezi kuogopa au kusita kuukemea uwongo, Lengo la kuwafanya wakristo kuwa wanafunzi ni ili wasivutwe kufuata mafundisho ya uongo.

Waefeso 4:11-14 “Naye alitoa wengine kuwa mitume, na wengine kuwa manabii; na wengine kuwa wainjilisti na wengine kuwa wachungaji na waalimu; kwa kusudi la kuwakamilisha watakatifu, hata kazi ya huduma itendeke, hata mwili wa Kristo ujengwe; hata na sisi sote tutakapoufikia umoja wa imani na kumfahamu sana Mwana wa Mungu, hata kuwa mtu mkamilifu, hata kufika kwenye cheo cha kimo cha utimilifu wa Kristo; ili tusiwe tena watoto wachanga, tukitupwa huku na huku, na kuchukuliwa na kila upepo wa elimu, kwa hila ya watu, kwa ujanja, tukizifuata njia za udanganyifu.”

2Timotheo 4:2-4 “lihubiri neno, uwe tayari, wakati ukufaao na wakati usiokufaa, karipia, kemea, na kuonya kwa uvumilivu wote na mafundisho. Maana utakuja wakati watakapoyakataa mafundisho yenye uzima; ila kwa kuzifuata nia zao wenyewe watajipatia waalimu makundi makundi, kwa kuwa wana masikio ya utafiti; nao watajiepusha wasisikie yaliyo kweli, na kuzigeukia hadithi za uongo.”  

Nyakati za kanisa la kwanza walikuwa makini sana kuhakikisha kuwa mtu wanayemkaribisha anakuwa na imani ile ile iliyofundishwa na kukubalika na mitume, Mitume waliagiza kuwa hakukuwa na sababu ya kumchekea mtu ambaye hakai au haleti mafundisho yao, walikazia kuwa mtu wa namna hiyo ikiwezekana wasimkaribishe wala hata wasimsalimie, mwenye dhambi anaweza kubadilika hata pole pole, lakini mafundisho ya uongo hata salamu asipewe

2Yohana 1:8-11 “Jiangalieni nafsi zenu msiyapoteze mliyoyatenda, bali mpokee thawabu timilifu. Kila apitaye cheo, wala asidumu katika mafundisho ya Kristo, yeye hana Mungu. Yeye adumuye katika mafundisho hayo, huyo ana Baba na Mwana pia. Mtu akija kwenu, naye haleti mafundisho hayo, msimkaribishe nyumbani mwenu, wala msimpe salamu. Maana yeye ampaye salamu azishiriki kazi zake mbovu.”

Kanisa linapaswa kusimamia msimamo huu, kuhakikisha kuwa kila mtu anayekaribishwa katika kanisa letu anakuja na fundisho lililo sahihi, anakuja na msimamo ule ule waliokuwa nao mitume wa Bwana wetu Yesu Kristo, au mtu anayechaguliwa kuwa kiongozi katika kanisa analishika neno la imani vile vile kama tulivyofundishwa na sio vinginevyo, mafundisho ya mitume yanapaswa kushikiliwa kama mila na desturi ya kanisa na kurithishwa katika kizazi kinachokuja hata akifufuka Paulo mtume leo atatukuta tukihubiri injili ile ile aliyoiacha na atatukuta hatujaichakachua injili wala hatuhubiri injili nyingine, na tutakemea kwa Mamlaka yote, kuonya na kukaripia. Kwa mafundisho yenye uzima. Haiwezekani Leo kiongozi mkubwa kabisa wa imani hatambui utatu na anachekewa

Umuhimu wa kulishika neno la imani vile vile kama ulivyofundishwa

Ni muhimu kufahamu kuwa mitume walikuwa wakali sana na swala zima la mfundisho ya uwongo kuliko tunavyofikiri, kwa bahati mbaya makanisa mengi leo wamekuwa wakali kwa dhambi jambo ambalo sio baya, kuliko kwa mafundisho potofu, dhambi inaweza kutubiwa na mwenye dhambi anaweza kubadilika, ukuaji wa kiroho ni mchakato na sio jambo la hatari kwa kanisa kwa sabahu Kristo alikuja kuokoa, lakini mafundisho potofu ni chachu na inaweza kubadilisha na kuathiri muelekeo mzima wa mwili wa Kristo na kwa sababu hiyo mitume walikuwa wakali sana na watu wanaofundisha uongo, Paulo mtume anamwagiza Tito kuwa makini kuwachagua watu wenye msimamo katika mafundisho yetu kwa sababu kisiwa cha Krete kilikuwa ni miongoni mwa sehemu zilizoathiriwa na mafundisho ya uongo kwa hiyo waliopendekezwa kuchaguliwa kuwa viongozi walipaswa kuwa watu hodari ambao wanauwezo wa kufundisha, kukemea, kuonya  na kuwazidi wale wanaowapinga au wale wanaoipinga kweli

Tito 1:4-5 “kwa Tito, mwanangu hasa katika imani tuishirikiyo. Neema na iwe kwako na amani zitokazo kwa Mungu Baba na kwa Kristo Yesu Mwokozi wetu. Kwa sababu hii nalikuacha Krete, ili uyatengeneze yaliyopunguka, na kuweka wazee katika kila mji kama vile nilivyokuamuru;”

Tito 1:7-9 “Maana imempasa askofu awe mtu asiyeshitakiwa neno, kwa kuwa ni wakili wa MUNGU; asiwe mtu wa kujipendeza nafsi yake, asiwe mwepesi wa hasira, asiwe mlevi wala mgomvi, asiwe mpenda mapato ya aibu.bali awe mkaribishaji, mpenda wema, mwenye kiasi, mwenye haki, mtakatifu, mwenye kudhibiti nafsi yake; AKILISHIKA LILE NENO LA IMANI VILE VILE KAMA ALIVYOFUNDISHWA, apate kuweza kuwaonya watu kwa mafundisho yenye uzima, na kuwashinda wenye kupinga.”

Kulikuwa na walimu wa uongo kule Krete, watu walikazia sheria ya Musa na mafundisho ya tohara, na pia watu walijitafutia mapato kupitia dini, kwa sababu hiyo suluhisho halikuwa miujiza bali suluhisho lilikuwa ni kupata watu sahihi watakaosimamia misingi ya Imani ya mitume na kuifundisha vile vile kama walivyofundishwa na wenye sifa ya kuweza kung’amua na kuyapinga au kuwashinda wale wenye kupinga kama alivyokuwa mtu wa Mungu Stefano, Paulo alikuwa anataka viongozi wawe wakali kwenye fundisho sahihi wenye sifa za ugumu wa kusimamia Imani na kupinga mafundisho ya uongo na kuwakemea waongo kwa nguvu zao zote, watu wenye uwezo wa kuwashinda wapingao na kuisimamia Imani kwa uaminifu hata kaa itawagharimu kufa 

Tito 1:10-14 “Kwa maana kuna wengi wasiotii, wenye maneno yasiyo na maana, wadanganyaji, na hasa wale wa tohara, ambao yapasa wazibwe vinywa vyao. Hao wanapindua watu wa nyumba nzima, wakifundisha yasiyowapasa kwa ajili ya mapato ya aibu. Mtu wa kwao, nabii wao wenyewe, amesema, Wakrete ni waongo siku zote, hayawani wabaya, walafi wavivu. Ushuhuda huo ni kweli. Kwa sababu hiyo uwakemee kwa ukali, ili wapate kuwa wazima katika imani; wasisikilize hadithi za Kiyahudi, wala maagizo ya watu wajiepushao na yaliyo kweli.”

Matendo 6:8-10 “Na Stefano, akijaa neema na uwezo, alikuwa akifanya maajabu na ishara kubwa katika watu. Lakini baadhi ya watu wa sinagogi lililoitwa sinagogi la Mahuru, na la Wakirene, na la Waiskanderia, na la wale wa Kilikia na Asia, wakaondoka na kujadiliana na Stefano;lakini hawakuweza kushindana na hiyo hekima na huyo Roho aliyesema naye.”

Kanisa linapaswa kuwa makini kuhakikisha kuwa linasimamisha watu waliojaa neno la Mungu, watu wenye injili iliyosahihi, watu wanaofunzwa vizuri ili kuirithisha Imani iliyosahihi kwa kizazi kinachokuja, leo hii kumejaa upuuzi wa kila aina kila kona kwa sababu ya uzembe wa Kanisa, Kanisa linafukuzana na mambo mengine na linaacha kuwafanya watu kuwa wanafunzi wa neno la Mungu, ni lazima tuikabidhi injili kwa watu waaminifu watakaofaa kuwafundisha na wengine vile vile kama walivyofundishwa, dunia ikijawa na mafundisho ya uongo leo sababu kubwa ni uzembe wa Kanisa kutokuwafundisha watu neno la Mungu, Kanisa ni lazima liwe kama shule ukiachanana maombezi na miujiza ambayo nayo ni ya muhimu lakini bila kusahau kuwafundisha watu neno, watu ni lazima wajae neno, dunia ni lazima ijawe na mafundisho yetu mpaka wakuu wa dini pinzani walalamike kama ilivyotokea kwa Masadukayo. 

2Timotheo 2:2 “Na mambo yale uliyoyasikia kwangu mbele ya mashahidi wengi, hayo uwakabidhi watu waaminifu watakaofaa kuwafundisha na wengine.”

Matendo 5:27-29 “Walipowaleta, wakawaweka katika baraza. Kuhani Mkuu akawauliza, akisema, Je! Hatukuwaamuru ninyi kwa nguvu, msifundishe kwa jina hili? Nanyi, tazameni, mmeijaza Yerusalemu mafundisho yenu, na mnataka kuileta damu ya mtu yule juu yetu. Petro na mitume wakajibu, wakisema, Imetupasa kumtii Mungu kuliko wanadamu.”

Kila kanisa ambalo linaamini kuwa lina mafundisho ya kweli basi lina wajibu wa kuijaza dunia na mafundisho hayo ya kweli kwa kuihubiri injili kila mahali, kufanya wanafunzi na kuijaza dunia na mafundisho yetu, kama hatufanyi kazi hiyo itafanywa kwa uaminifu na mashahidi wa Yehova, Mormonisim, Wasabato, na imani nyinginezo nyingi, injili za mafanikio, injili za neema iliyozidi, injili za sheria, na injili nyingine nyingi na usikasirike wakiwa na televisheni, magazeti na washuhudiaji wanapita nyumba kwa nyumba wakieneza mafundisho yao maana wewe hutaki na mafundisho yako lakini pembeni pembeni unadai una Imani ya kweli lakini umekaa nayo kimya na kazi yako ni kukosoa tu pembeni utasikia jihadharini na mafundisho ya mitandaoni, ahaaaa we ya kwako ya mitandaoni yako wapi na kwa nini hurushi? Kwa hiyo wadhani Kristo hana wanaohubiri kweli mitandaoni? Mwone kwanza lihubiri neno fundisha kweli eneza kweli kwa njia zozote, wafundishe washirika kupambanua mchele na chuya!   

Akilishika neno la Imani vile vile kama alivyofundishwa!.

Unadhani kuna faida gani ya kuwa na umati mkubwa wa watu, kuwa na sauti nzuri, kuwa na karama za kila aina, kutajirika na kubarikiwa sana na kuwa na walinzi na msafara wa magari lakini ukawa hauifundishi kweli? Kiongozi wa kweli wa imani ni lazima awe mwanafunzi mzuri wa neno la Mungu, awe mtetezi wa kweli wa imani, awe na uwezo wa kung’amua uongo na kuukemea kwa nguvu na kuukaripia au kuujibu kwa neno la Mungu, lakini zaidi sana awe mwaminifu kwa mafundisho ya mitume, na sio kwa sababu umerithi tu bali pia kwa sababu umelichunguza na kujithibitishia kuwa unaamini jambo lililo sahihi, mmesikia siku za Karibuni katika mitandao wahubiri wakubwa kabisa wenye umati mkubwa wa watu wakikanusha na kuushambulia na kupinga fundisho la utatu wa Mungu na watu wenye kweli wamekaa kimya tu hii ni mojawapo ya hatari iliyo wazi kuwa nyakati za leo tuna watu wengi tu wanaofuata mkumbo, kama watu wangekuwa wanafundishwa kweli ya Mungu kwa usahihi  na wakawa na uwezo mkubwa wa kupambanua nadhani siku ile wanamsikia kiongozi wao akisema hakuna Utatu ingekuwa ndio siku ya mwisho kuabudu hapo, lakini dunia imejaa vipofu, na viongozi wa vipofu, wala hawaoni kuwa hili ni tatizo kubwa!.

Kama kanisa tangu mwanzo lingezalisha watu wasioyumbishwa, imani yetu ingebaki kama ilivyokuwa nyakati za baba zetu, lakini siku za leo kumejaa nyumbu wengi makanisani ambao wanayumbishwa kila kukicha na Imani mbalimbali na imekuwa ngumu kwao leo kujua ipi ni sahihi na ipi ni potofu watu hawajui kupambanua. Mtu anayeishika Imani vile vile ni mtu asiyetikisika kwa sababu anajua alichokiamini na hawatikiswi na lolote wanashikamana na kile walichokiamini bila kujali wanapitia nini

-          2Timotheo 1:12-14 “Kwa sababu hiyo nimepatikana na mateso haya, wala sitahayari; kwa maana namjua yeye niliyemwamini, na kusadiki ya kwamba aweza kukilinda kile nilichokiweka amana kwake hata siku ile. Shika kielelezo cha maneno yenye uzima uliyoyasikia kwangu, katika imani na upendo ulio katika Kristo Yesu. Ilinde ile amana nzuri kwa Roho Mtakatifu akaaye ndani yetu.”

 

-          Matendo 5:27-29. “Walipowaleta, wakawaweka katika baraza. Kuhani Mkuu akawauliza, akisema, Je! Hatukuwaamuru ninyi kwa nguvu, msifundishe kwa jina hili? Nanyi, tazameni, mmeijaza Yerusalemu mafundisho yenu, na mnataka kuileta damu ya mtu yule juu yetu. Petro na mitume wakajibu, wakisema, Imetupasa kumtii Mungu kuliko wanadamu.”

 

Kanisa ni lazima tujikite katika kuandaa viongozi ambao watakuwa watata, wenye kumfuata Yesu na kukataa kuyachakachua maneno ya Mungu kwa gharama yoyote hata kama itawagharimu kuteseka na kuuawa, lazima tuzalishe viongozi mahiri wenye uwezo wa kumuigiza Yesu, kuwa hatukuja duniani kuwapendeza wanadamu bali tumekuja kuwatumikia watu kama yeye mwenyewe, lazima tuzalishe watu wenye nguvu, wenye akili wanaolijua neno ambao watasimama kuitetea Imani hata wakati wa mambo magumu na kuwasaidia watu kuijua kweli na kuisimamimai kwa gharama yoyote kwa sababu hiyo pamoja na sifa nyingine isisahahulike sifa hii muhimu ya kwamba imempasa askofu au kiongozi wa kanisa awe mtu anayeisimamia Imani vile vile kama alivyofundishwa .

Tito 1:7-9 “Maana imempasa askofu awe mtu asiyeshitakiwa neno, kwa kuwa ni wakili wa MUNGU; asiwe mtu wa kujipendeza nafsi yake, asiwe mwepesi wa hasira, asiwe mlevi wala mgomvi, asiwe mpenda mapato ya aibu.bali awe mkaribishaji, mpenda wema, mwenye kiasi, mwenye haki, mtakatifu, mwenye kudhibiti nafsi yake; akilishika lile neno la imani vile vile kama alivyofundishwa, apate kuweza kuwaonya watu kwa mafundisho yenye uzima, na kuwashinda wenye kupinga.”

Na. Rev. Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi mqwenye Hekima

Jumapili, 8 Machi 2026

Dema aliniacha, akiupenda ulimwengu huu wa sasa


2Timotheo 4:9-11 “Jitahidi kuja kwangu upesi. Maana Dema aliniacha, akiupenda ulimwengu huu wa sasa, akasafiri kwenda Thesalonike; Kreske amekwenda Galatia; Tito amekwenda Dalmatia. Luka peke yake yupo hapa pamoja nami. Umtwae Marko, umlete pamoja nawe, maana anifaa kwa utumishi.”



Utangulizi:

Ni maneno ya huzuni na masikitiko makubwa sana kutoka kwa mtume Paulo, akiwa kifungoni katika siku zake za mwisho, kabla kidogo ya kuhukumiwa kifo. Akiwa katika gereza lenye kutisha liitwalo “Mamertine Prison” akisubiria hukumu yake ya kifo, Katika wakati huo Mgumu anaachwa na mtenda kazi maarufu sana aliyewahi kuwa karibu sana na mtendakazi pamoja naye katika kazi ya injili aliyejulikana kwa jina la Dema, Ni katika namna ya kusikitisha sana Paulo akiwa katika maumivu hayo Dema anaamua kuachana na injili na kwenda katika jiji la Thesalonike Ugiriki ya leo, kwenda kuishi maisha ya kutanua na kustarehe, “Dema aliniacha akiupenda ulimwengu huu wa sasa”, ni ujumbe unaobeba fundisho muhimu sana kuhusu hatari ya kuanza vizuri na kumaliza vibaya! Wakati Paulo akiwa anafurahia kumaliza vizuri huduma yake Dema anamaliza vibaya kwa kurudi nyuma na kwenda kujirusha duniani.

Matendo 20:22-24 “Basi sasa, angalieni, nashika njia kwenda Yerusalemu hali nimefungwa rohoni, nisiyajue mambo yatakayonikuta huko; isipokuwa Roho Mtakatifu mji kwa mji hunishuhudia akisema, ya kwamba vifungo na dhiki vyaningoja. Lakini siyahesabu maisha yangu kuwa kitu cha thamani kwangu kama kuumaliza mwendo wangu na huduma ile niliyopokea kwa Bwana Yesu, kuishuhudia Habari Njema ya neema ya Mungu.”

Tuitajifunza somo hili Dema aliniacha akiupenda ulimwengu huu wa sasa kwa kuzingatia vipengele vitatu vifuatavyo:-


·         Dema ni nani na alikuwa nani?

·         Dema aliniacha akiupenda ulimwengu huu wa sasa.

·         Mambo ya kujifunza kutoka kwa Dema.


Dema ni nani na alikuwa nani?

Jina Dema kwa asili limetokana na jina la Kiyunani Dēmos ambalo maana yake kwa kiingereza ni “The people”  mzizi mmoja na jina Nicodemus ambalo kwa kiingereza ni “Victory of the people” kwa hiyo jina Dema maana yake ni watu.  Na Nicodemo maana yake ushindi wa watu. Dema hakuwa mshirika wa kawaida tu kanisani na katika huduma, Yeye alikuwa ni Mtumishi wa Mungu katika timu ya umisheni pamoja na Paulo Mtume  na anatajwa pamoja na Luka yule tabibu mpendwa, mwandishi wa Injili ya Luka na kitabu cha Matendo ya mitume pamoja na kina Epafra mwanzilishi wa makanisa ya Kolosai, Laodikia na  Hierapoli.

Wakolosai 4:12-14 “Epafra, aliye mtu wa kwenu, mtumwa wa Yesu Kristo, awasalimu, akifanya bidii siku zote kwa ajili yenu katika maombi yake, ili kwamba msimame wakamilifu na kuthibitika sana katika mapenzi yote ya Mungu. Maana namshuhudia kwamba ana juhudi nyingi kwa ajili yenu, na kwa ajili ya hao walioko Laodikia, na kwa ajili ya hao walioko Hierapoli. Luka, yule tabibu mpendwa, na Dema, wanawasalimu.”

Maandiko yanamtaja Dema pamoja na watumishi wa Mungu wa ngazi ya juu kabisa wenye sifa njema, na wote tunajua jinsi ambavyo Paulo mtume alikuwa makini sana katika kuchagua watu wema wa kuambatana naye katika kazi ya injili, kwa hiyo iko wazi kuwa Dema alikuwa sehemu muhimu ya timu ya wamishionari na mtendakazi, Pamoja na Paulo mtume. Na alijulikana sana kuwa aliitenda kazi ya Mungu pamoja na watu wengine maarufu katika watendakazi wenza pamoja na Paulo mtume, Dema alikuwa pia katika timu moja na Marko mwandishi wa Injili ya Marko na pia Aristrarko, na wengineo, alikuwa muhubiri wa injili, alikuwa mmishionari, alikuwa mpanda makanisa kwa hiyo ni dhahiri kuwa alikuwa mtendakazi aliyeweza kustahimili magumu mengi katika safari ya injili, kimsingi aliianza kazi hii vizuri.

Filemoni 1:22-24 “Na pamoja na hayo uniwekee tayari mahali pa kukaa; maana nataraji ya kwamba kwa maombi yenu mtajaliwa kunipata. Epafra, aliyefungwa pamoja nami katika Kristo Yesu, akusalimu; na Marko, na Aristarko, na Dema, na Luka, watendao kazi pamoja nami.”

Hata hivyo katika mazingira ya kustaajabisha na ya kusikitisha sana mtumishi huyu wa Mungu maarufu namna hii tunataarifiwa kuwa alirudi nyuma alimuacha Mtume Paulo akiwa gerezani kisha akaenda zake jijini Thesalonike kwenda kufanya biashara zake akiupenda ulimwengu wa sasa hii maana yake ni nini? Hilo linatupa nafasi kutafakari kipengele cha pili cha somo hili Dema aliniacha akiupenda ulimwengu huu wa sasa, kama Dema angemuacha Paulo mtume na kwenda kuhubiri sehemu nyingine hiyo ingekuwa njema na Paulo asingelihuzunika lakini Dema aliupenda ulimwengu huu ni msiba hasa kwa Paulo kwa kuwa Dema hakwenda kuihubiri injili bali alirudi duniani huko Ugiriki.

Dema aliniacha akiupenda ulimwengu huu wa sasa.

Biblia haitoi maelezo mengi kwanini Dema alirejea nyuma, akiiacha kazi ya Mungu na mateso ya Mtume Paulo gerezani, lakini ufafanuzi wa maneno ya Paulo unatupa picha kubwa na ya kutisha  na kusikitisha kuhusu mkasa wa Dema, Kimsingi mstari wa “10” 2Timotheo 4:10 “Maana Dema aliniacha, akiupenda ulimwengu huu wa sasa, akasafiri kwenda Thesalonike; Kreske amekwenda Galatia; Tito amekwenda Dalmatia.” Unasomeka hivi katika Kiyunani “yáp Dēmas egkataleipō, agapaō ton nun aiona”  Katika maneno hayo ya Kiyunani neno Agapaō linamaanisha “sacrificial love” kujidhabihu kwa hiyo Dema alikuwa amejidhabihu kwa dunia badala ya kazi ya Mungu, hii maana yake aliipenda sana dunia, alikubali kuvutiwa nayo, alishikamana na dunia kwa moyo wake wote  na neno “Aiona” yaani ulimwengu wa sasa linamaanisha alishikamana na mfumo wa sasa wa dunia hii ikimaanisha kutafuta Heshima, kutafuta mali, na usalama wa kidunia Dema aliamua kufanya hivyo kwa sababu wakati huu ulikuwa ni wakati wa hatari sana kujitoa kwaajili ya injili, mateso kutoka utawala wa kirumi yalikuwa yamepamba moto kinyume na Ukristo na injili yake, wakristo walikuwa wanateswa, kuuawa na hata kufungwa kwa hiyo Dema aliogopa alikimbilia katika jiji kubwa la kibiashara la Thesalonike huko Ulaya Ugiriki ambako kulikuwa na kanisa letu huko lakini hakurudi kanisani na badala yake alirudi katika maisha yake ya kawaida na kufanya biashara akiishi maisha ya kawaida akiachana  na huduma ambayo kimsingi ilikuwa inagharimu maisha ya watu, aliogopa kuifia injili.

1Yohana 2:15-17 “Msiipende dunia, wala mambo yaliyomo katika dunia. Mtu akiipenda dunia, kumpenda Baba hakumo ndani yake. Maana kila kilichomo duniani, yaani, tamaa ya mwili, na tamaa ya macho, na kiburi cha uzima, havitokani na Baba, bali vyatokana na dunia. Na dunia inapita, pamoja na tamaa zake, bali yeye afanyaye mapenzi ya Mungu adumu hata milele.”

Warumi 12:1-2 “Basi, ndugu zangu, nawasihi, kwa huruma zake Mungu, itoeni miili yenu iwe dhabihu iliyo hai, takatifu, ya kumpendeza Mungu, ndiyo ibada yenu yenye maana. Wala msiifuatishe namna ya dunia hii; bali mgeuzwe kwa kufanywa upya nia zenu, mpate kujua hakika mapenzi ya Mungu yaliyo mema, ya kumpendeza, na ukamilifu.”

Dema hakuwa mshirika wa kawaida alikuwa mtumishi wa Mungu alishiriki katika kazi ya injili, sio wakati wote mazingira yalikuwa rahisi lakini alivumilia kurudi nyuma kwa Mtumishi wa Mungu kama Dema ni swala la kusikitisha sana na ni swala lenye kuogopesha, Dema alikuwa askari wa mstari wa mbele, Kadiri tunavyokua na kuinuliwa katika imani  na kushinka nafasi za kitumishi hatunabudi kuongeza kiwango chetu cha kujitoa kwa Mungu na kumpenda Yesu, Shetani haogopi kuwa umefikia ngazi gani ya kiroho anaweza kukurejesha Duniani, kwa uwazi au kimya kimya.

Mambo ya kujifunza kutoka kwa Dema

Kumfuata Yesu kunahitaji kujikana nafsi – Leo tunamuhubiri Kristo na tunaweza tusisikie wahubiri wakirudi nyuma kwa sababu kwanza injili inalipa, watu wengi sana wamebarikiwa kutokana na kuihubiri injili katika wakati huu wa Amani, lakini yako mazingira ambapo mambo yanaweza kuwa magumu na mateso yakazidi hapo waoga wote wataondoka kwenye mfumo, tujikumbushe kuwa kumfuata Yesu kunahitaji kujikana  na kubeba Msalaba

 

Luka 9:23-25 “Akawaambia wote, Mtu ye yote akitaka kunifuata, na ajikane mwenyewe, ajitwike msalaba wake kila siku, anifuate. Kwa kuwa mtu atakaye kuiponya nafsi yake ataiangamiza, na mtu atakayeiangamiza nafsi yake kwa ajili yangu ndiye atakayeisalimisha. Kwa kuwa yamfaa nini mtu kuupata ulimwengu wote, kama akijiangamiza, au kujipoteza mwenyewe?

 

Kumfuata Yesu kunahitaji kuhesabu gharama – Yesu anawataka wanafunzi wake watambue kuwa kumfuata Yesu ni gharama ni sawa na mtu anayetaka kujenga mnara, ni lazima ukae upige hesabu na kufanya maandalizi ya kutosha ili usije ukawa dhihaka kwa kushindwa kukamilisha mradi wako, Dema alishindwa kukamilisha mradi.

 

Luka 14:28-30 “Maana ni nani katika ninyi, kama akitaka kujenga mnara, asiyeketi kwanza na kuhesabu gharama, kwamba anavyo vya kuumalizia? Asije akashindwa kuumaliza baada ya kuupiga msingi, watu wote waonao wakaanza kumdhihaki, wakisema, Mtu huyu alianza kujenga, akawa hana nguvu za kumaliza.”

 

Kumfuata Yesu ni kama kuanzisha vita – taifa lolote linapoanzisha vita na taifa lingine au ufalme wowote unapoanzisha vita na ufalme mwingine ni lazima taifa hilo au ufalme huo ukae chini na kupiga hesabu zake vizuri na kufanya mashauri au upelelezi wa kutosha kama unaweza kupigana na upande wa pili na kupata ushindi na ukiona vita inakuwia ngumu basi omba agano la Amani

 

Luka 14:31-33 “Au kuna mfalme gani, akitaka kwenda kupigana na mfalme mwingine, asiyeketi kwanza na kufanya shauri, kwamba yeye pamoja na watu elfu kumi ataweza kukutana na yule anayekuja juu yake na watu elfu ishirini? Na kama akiona hawezi, hutuma ujumbe kutaka sharti za amani, mtu yule akali mbali. Basi, kadhalika kila mmoja wenu asiyeacha vyote alivyo navyo, hawezi kuwa mwanafunzi wangu.”

 

Kumfuata Yesu ni kama kulima kwa jembe la kukokotwa na wanyama – Jembe la kukokotwa na wanyama kama ng’ombe kwa kawaida mtu anapolitumia kwenye kulima haliruhusu kusimama au kuangalia nyuma, mkulima wa jembe la kukokotwa na ngombe ni lazima aangalie pale anapolima ni lazima aangalie mbele asiondoe mawazo yake katika shughuli hiyo kwani kuangalia nyuma kunapoteza sifa ya mkulima wa aina hiyo hali kadhalika mtu anayemfuata Yesu

 

Luka 9:61-62 “Mtu mwingine pia akamwambia, Bwana, nitakufuata; lakini, nipe ruhusa kwanza nikawaage watu wa nyumbani mwangu. Yesu akamwambia, Mtu aliyetia mkono wake kulima, kisha akaangalia nyuma, hafai kwa ufalme wa Mungu.”

 

Kumfuata Yesu kunahitaji uaminifu hata kufa – Mungu kweli atatukoa wakati mwingine katika mitego ya adui, na vita za aina mbalimbali kama ilivyokuwa kwa Dema, tunakuwa salama wakati wote Bwana akiwa upande wetu hata hivyo yako mazingira kama haya ambayo Paulo mtume alikuwa anakabiliwa na kifo ni ukweli ulio wazi wengi walimuacha, kuna wakati tunapaswa kuwa waaminifu hata kufa lakini sio kila mtu anataka kifo, kuwa tayari kwa hilo kwaajili ya Kristo ni dhabihu ya hali ya juu sana ni kukubali kuwa shahidi wa Yesu Kristo uliye mwaminifu  

 

2Timotheo 4:16-17 “Katika jawabu langu la kwanza hakuna mtu aliyesimama upande wangu, bali wote waliniacha; naomba wasihesabiwe hatia kwa jambo hilo. Lakini Bwana alisimama pamoja nami akanitia nguvu, ili kwa kazi yangu ule ujumbe utangazwe kwa utimilifu, hata wasikie Mataifa yote; nami nikaokolewa katika kinywa cha simba.”

 

Ufunuo 2:9-10 “Naijua dhiki yako na umaskini wako, (lakini u tajiri) najua na matukano ya hao wasemao ya kuwa ni Wayahudi, nao sio, bali ni sinagogi la Shetani. Usiogope mambo yatakayokupata; tazama, huyo Ibilisi atawatupa baadhi yenu gerezani ili mjaribiwe, nanyi mtakuwa na dhiki siku kumi. Uwe mwaminifu hata kufa, nami nitakupa taji ya uzima.”

 

Matendo 21:10-14 “Basi tulipokuwa tukikaa huko siku nyingi, nabii mmoja jina lake Agabo akashuka kutoka Uyahudi. Alipotufikia akautwaa mshipi wa Paulo, akajifunga miguu na mikono, akasema, Roho Mtakatifu asema hivi, Hivyo ndivyo Wayahudi wa Yerusalemu watakavyomfunga mtu mwenye mshipi huu, nao watamtia katika mikono ya watu wa Mataifa. Basi tuliposikia haya, sisi na watu wa mahali pale, tukamsihi asipande kwenda Yerusalemu. Ndipo Paulo alipojibu, Mnafanya nini, kulia na kunivunja moyo? Kwa maana mimi, licha ya kufungwa, ni tayari hata kuuawa katika Yerusalemu kwa ajili ya jina lake Bwana Yesu. Alipokataa shauri letu, tukanyamaza tukisema, Mapenzi ya Bwana na yatendeke.”             

 

Kumfuata Yesu kunahitaji uwe imara – Kila mwanafunzi wa Yesu anapaswa kukumbuka wakati wote kujiimarisha katika Imani ili kuhakikisha kuwa kila siku tunapiga hatua na kukua kiroho, hata pamoja na kuwa tunamtumikia Mungu, Dema alijisahau, Paulo mtume anasema hakujihesabu kuwa amefika lakini kila wakati alikuwa akiendelea na mazoezi muhimu ya kiroho ili asifanye kazi ya kuhubiri tu wengine kisha yeye akawa mtu wa kukataliwa, uzoefu na kurudi nyuma kwa Dema kunatukumbusha kwamba tunapaswa kuhakikisha kuwa tunajiimarisha kila iitwapo leo

 

Wafilipi 3:12-14 “Si kwamba nimekwisha kufika, au nimekwisha kuwa mkamilifu; la! Bali nakaza mwendo ili nipate kulishika lile ambalo kwa ajili yake nimeshikwa na Kristo Yesu. Ndugu, sijidhanii nafsi yangu kwamba nimekwisha kushika; ila natenda neno moja tu; nikiyasahau yaliyo nyuma, nikiyachuchumilia yaliyo mbele; nakaza mwendo, niifikilie mede ya thawabu ya mwito mkuu wa Mungu katika Kristo Yesu.”

 

Mathayo 7:2-27 “Na kila asikiaye hayo maneno yangu asiyafanye, atafananishwa na mtu mpumbavu, aliyejenga nyumba yake juu ya mchanga; mvua ikanyesha, mafuriko yakaja, pepo zikavuma, zikaipiga nyumba ile, ikaanguka; nalo anguko lake likawa kubwa.”

 

Mathayo 13:20-21 “Naye aliyepandwa penye miamba, huyo ndiye alisikiaye lile neno, akalipokea mara kwa furaha; lakini hana mizizi ndani yake, bali hudumu kwa muda; ikitukia dhiki au udhia kwa ajili ya lile neno, mara huchukizwa.”

 

Watu wa Mungu tunaowajibu wa kuhakikisha kuwa tunamaliza vizuri, inasikitisha sana kuona mtu mkubwa aliyembatana na muhubiri mkubwa kama Dema akirudi nyuma, na kuipenda dunia, Shetani haogopi kuwa umefikia ngazi gani ya kiroho, kwa sababu hiyo kila wakati tujilinde katika neema ya Mungu, na kuendelea kujidhabihu na kutokukata tamaa kwa sababu ya dhiki na mambo mengineyo, na badala yake tujiimarishe katika Bwana ili kila mmoja wetu aweze kumaliza vizuri, tamaa ya mwili, tamaa ya macho na kiburi cha uzima kipo na ni rahisi kuvutwa kwenye ulimwengu huu kama hatutashikamana na utimilifu wetu wa Imani mpaka mwisho.                


Na. Rev. Innocent Samuel Kamote

 

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima

Jumapili, 1 Machi 2026

Umuhimu wa kutunza siri!


Mithali 11:12-14 “Asiye na akili humdharau mwenziwe; Bali mtu aliye na ufahamu hunyamaza. Mwenye kitango akisingizia hufunua siri; Bali mwenye roho ya uaminifu husitiri mambo. Pasipo mashauri taifa huanguka; Bali kwa wingi wa washauri huja wokovu.”



tangulizi:

Kutunza siri ni mojawapo ya jambo la msingi na la muhimu sana katika jamii, siri zinatunzwa kwa sababu ya kuheshimu utu wa mtu, kujenga jamii, kulinda taifa, kutunza na kuonyesha uaminifu, kuudumisha mahusiano, kuepuka kuleta migogoro, kutunza taarifa nyeti na za muhimu, kulinda usalama wa taifa, kulinda heshima ya mtu, kulinda jamii serikali, taasisi au watu dhidi ya madhara mbalimbali, aidha siri hutunzwa kwa makusudi ya kuepusha kumuharibia mtu, kumuaibisha mtu, kusababisha mtu ahukumiwe na jamii, au kukataliwa na jamii, au kutunza ubora wa taarifa za mtu, kutunza siri ni heshima na siri inaweza pia kutunza uhai wa mtu na kuonyesha ukomavu wa Msiri.

Mathayo 1:18-19 “Kuzaliwa kwake Yesu Kristo kulikuwa hivi. Mariamu mama yake alipokuwa ameposwa na Yusufu, kabla hawajakaribiana, alionekana ana mimba kwa uweza wa Roho Mtakatifu. Naye Yusufu, mumewe, kwa vile alivyokuwa mtu wa haki, asitake kumwaibisha, aliazimu kumwacha kwa siri.”

Kutunza siri ni kiwango cha juu sana cha uadilifu, mtu anapokueleza siri yake maana yake amekuamini, kutunza siri wakati mwingine kunasaidia kutunza uhusiano, kunazuia kusambaa kwa taarifa za mafununu, na kunawalinda wengine au taifa au kanisa kupata madhara na kunatunza heshima ya wengine, utunzaji wa siri unawapa watu maisha unampa mtu ujasiri wa kuendelea na maisha mengine na kujiamini, hakuna fani yeyote ile ambayo haina siri, Madaktari na wauguzi wanaapa kutunza siri za wagonjwa, Magereza kuna siri, Polisi kuna siri, waalimu wana siri, wachungaji wanapaswa pia kutunza siri lakini serikalini pia kuna siri, vyombo vyote vya ulinzi na usalama na fani za upelelezi wakati mwingine katika mazingira fulani hasa ya kichunguzi wanapaswa kuwa na siri.

Leo tutachukua muda basi kujifunza somo hili muhimu sana katika maisha, Umuhimu wa kutunza siri na tutajifunza somo hili kwa kuzingatia vipengele vitatu vifuatavyo:-


·         Maana ya neno siri

·         Umuhimu wa kutunza siri

·         Hatari za kutoa siri


Maana ya neno siri

Mithali 25:7-9 “Kwa maana ni heri kuambiwa, Njoo huku mbele; Kuliko kuwekwa nyuma machoni pa mkuu. Yale uliyoyaona kwa macho, Usitoke nje kwa haraka ili kuyashindania; Usije ukakosa kujua la kutenda hatimaye, Mwenzako atakapokuwa amekuaibisha. Ujitetee na mwenzako peke yake; Bali usiifunue siri ya mtu mwingine;”

Neno la Mungu linaonya na kuagiza juu ya kutokuifunua siri ya mtu mwingine, kimsingi neno la Mungu linatufundisha kuwa hapa duniani ziko siri au yako mambo ambayo kimsingi kama yatawekwa wazi yote yanaweza kusababisha madhara makubwa katika jamii kwa hiyo sio kila jambo linaweza kuwekwa wazi, hii ni kuanzia katika ngazi ya ndoa na familia mpaka ngazi ya taifa sasa basi tunapotaka kujifunza somo hili umuhimu wa kutunza siri kwanza ni muhimu kwetu kuelewa maana ya neno siri, Siri ni nini hasa kwa mujibu wa tafasiri za kibiblia.

Neno SIRI Katika Biblia ya Kiebrania linasomeka kama neno “Sôd” au “Sâthar” Neno hili limejitokeza katika biblia ya KJV mara 82 likitajwa katika kiingereza kama neno “Hide”, mara 72, “Secret” mara 4 “Close” mara 2, “Conceal” mara 1 na “Variant” mara 1 “Absent” 1 na “Surely” mara 1 kwa hiyo neno siri maana yake ni Mazungunzo au maandishi au maneno au sauti, au taarifa zilizofichwa, ni taarifa za siri, ni taarifa zilizofungwa, au taariza zinazolindwa, au zisizotakiwa kuwekwa wazi, zisizotakiwa kufunuliwa, kwa kiyunani ni “Mystērion” sawa na neno la kiingereza “mystery  yaani mambo ambayo hayajawekwa wazi, mambo ambayo yamefichwa aidha na Mungu au Serikali au na mtu binafsi. Kuficha, kufunga mdomo, kufanya kazi chini ya njia za kificho “undercover”, kuendesha chini chini, usiri.

Kumbukumbu 29:29 “Mambo ya siri ni ya Bwana, Mungu wetu; lakini mambo yaliyofunuliwa ni yetu sisi na watoto wetu milele, ili tuyafanye maneno yote ya sheria hii.”

Kwa hiyo jambo linapokuwa siri maana yake limekusudiwa kubaki kati ya mtu ama kundi fulani tu, na halipaswi kujulikana na wengine ama linabaki na mtu fulani bila mtu huyo kuliweka wazi kwa wengine, siri ni jambo la ndani, linaishia huko huko,  hulitangazwi, au huwezi kulisema kabla ya wakati, au halipaswi kusemwa kwa yeyote wala kujulikana na wakati mwingine ili kulitunza linaweza kuhusisha kiapo, swala linalopaswa kuheshimiwa na kusitiriwa isipokuwa kwa idhini tu, Mungu ni msiri kwa hiyo usiri ni tabia ya uadilifu, fikiria kama Mungu angeamua kuweka wazi mambo ya kila mtu duniani ingekuwaje? Au fikiria kama mitandao ya kijamii au ya simu za mkononi ikiamua kuweka wazi au kuutangazia umma kila ulichowasiliana kwa maneno au kwa maandishi je unadhani ingekuwaje kwa hiyo utakubaliana na maandiko kuwa kuficha siri ni kwaajili ya utukufu wa Mungu pia na ni uadilifu wa hali ya juu.

Mithali 25:2-3. “Ni utukufu wa Mungu kuficha jambo; Bali ni utukufu wa mfalme kuchunguza jambo. Mbingu huenda juu sana, na nchi huenda chini; Lakini mioyo ya wafalme haichunguziki.”

Umuhimu wa kutunza siri.

Nadhani mpaka sasa baada ya kuwa umefahamu maana ya siri vilevile utakuwa umeanza kuelewa umuhimu wa kutunza siri na hatari ya kuvujisha siri, siri zinaweza kuwa na maana kubwa sana endapo zitatunzwa na vilevile zinaweza kuwa na madhara makubwa sana endapo zitawekwa wazi, siri zinalinda usalama wa ndoa, usalama wa jamii, usalama wa mtu, usalama wa taasisi na usalama wa taifa, na kadhalika, kwa ujumla kutunza siri kuna uhusiano wa moja kwa moja na maswala ya uadilifu, chukulia kuwa umeugua jipu sehemu za siri, na muuguzi akakutibu kwa kulipasua jipu lako, kisha baada ya kukuhudumia habari za maumbile yako na utupu wako zikawa nimeenea mtaani? Au chukulia kuwa umekwenda kuungama na kutubu kwa mchungaji fulani, kisha baada ya muda habari za maungamo yako na toba yako zikawa zimeanikwa nje ya ofisi, au Serikali imetengeneza mitihani kwaajili ya darasa fulani kwa nchi nzima kisha mtihani wa somo fulani ukavuja kabla ya wakati wake  na labda watahiniwa wako milioni moja nukta mbili 1.2 nchi nzima kwa mwaka huo, Baraza la mitihani litatakiwa kuubadilisha mtihani huo kwa nchi nzima na kuuchapa tena na kuusambaza tena kwa wakati, unadhani serikali itapata hasara kiasi gani kwa mtihani mmoja kuvuja? Ambao ulifungwa usijulikane kabla ya wakati wake?  hapo ndipo tunapoelewa na kufahamu kuwa kutunza siri ni swala nyeti sana, hata katika ngazi ya familia na ndoa, chukulia kila unachokifanya mkeo anakwenda kukielezea kwa mama yake yaani mama mkwe wako kwa undani kabisa kisha ukakisikia utajisikiaje?, kuna mambo yakiwa siri yanaleta manufaa kwa jamii, chukulia kijana amebakwa au kulawitiwa kisha akatajwa wazi kwa jina lake halisi na akapigwa picha zake na zikawa wazi au jina lake likatajwa kama lilivyo katika vyombo vya habari, je hakuna madhara kwa makuzi ya huyo kijana? Na jamii yake je itakuwaje kesho yake na maisha yake hapo ndipo tunapopata ujuzi na hekima ya umuhimu wa kutunza siri, inawezekana katika maisha haya kuna mambo ambayo wewe hungependa yafunuliwe au watu wayajue kwa sababu yanaweza kukuaibisha au kufanya wewe upotee au kuchukua maamuzi mabaya sana ambayo hungeyachukua kama siri isingeliwekwa wazi aidha mambo hayo umeyafanya au umefanyiwa kila mwanadamu anayo siri fulani kwa hiyo siri ni sehemu ya maisha ya mwanadamu kwa hiyo yako mambo ambayo kila mwanadamu hangependa hata yeye mwenyewe kuyakumbuka au kukumbushwa,  kwa hiyo siri ina umuhimu katika maisha ikitunzwa, kufichua siri kulileta laana kwa Kanaani mtoto wa Hamu kwa sababu baba yake yaani Nuhu alipokunywa mvinyo akalewa na alipokaa uchi yeye hakuitunza siri na badala yake akaianika kwa kila mtu Nuhu alipoamka usingizini alimlaani aliyetoa siri na aliwabariki walioficha siri, Hakuna anayependa kuanikwa

Mwanzo 9:20-27 “Nuhu akaanza kuwa mkulima, akapanda mizabibu; akanywa divai, akalewa; akawa uchi katika hema yake. Hamu, baba wa Kanaani, akauona uchi wa baba yake, akawaeleza ndugu zake wawili waliokuwa nje. Shemu na Yafethi wakatwaa vazi, wakalitanda mabegani mwao wote wawili, wakaenda kinyumenyume, wakaufunika uchi wa baba yao; na nyuso zao zilielekea nyuma, wala hawakuuona uchi wa baba yao. Nuhu akalevuka katika ulevi wake, akajua mwana wake mdogo alivyomtendea. Akasema, Na alaaniwe Kaanani; Atakuwa mtumwa kabisa kwa ndugu zake. Akasema, Na atukuzwe BWANA, Mungu wa Shemu; Na Kaanani awe mtumwa wake.Mungu akamnafisishe Yafethi, Na akae katika hema za Shemu; Na Kaanani awe mtumwa wake.”

-          Kutunza siri ni ishara ya ukomavu, uadilifu na uaminifu – Mtu yeyote mkomavu wa busara na mkomavu wa kiroho anawajibu wa kuwa mtu wa kutunza siri, Kimsingi hata Mungu mwenyewe huweka siri zake kwa watu waminifu, kibiblia mtu asiyetunza siri huitwa mtu asiye na akili, wasiotunza siri katika jamii hupewa majina ya dharau na kutokuheshimika, huitwa wambeya, huitwa watu wasio na kifua, huitwa watu wenye friji haligandishi.

Mithali 11:12-13 “Asiye na akili humdharau mwenziwe; Bali mtu aliye na ufahamu hunyamaza. Mwenye kitango (Msengenyaji) akisingizia hufunua siri; Bali mwenye roho ya uaminifu husitiri mambo.”

-          Kutunza siri ni ishara ya kuwa mtu wa haki  - Maandiko yanamtaja Yusufu mumewe Mariamu mama yake Yesu kuwa alikuwa mtu wa haki, yeye alikuwa na ukomavu ya kuwa kila mwanadamu anakosea na hakuna mtu mkamilifu, alimpenda sana Mariamu na alipokuwa amemchumbia aligundua kuwa ana mimba, kwa mujibu wa torati ya Musa kama sio ufafanuzi wa Malaika kuwa ilikuwa mimba kwa uwezo wa Roho Mtakatifu, Mariamu alipaswa kutolewa kuulizwa na kupigwa mawe kwa dhambi ya zinaa, lakini Yusufu hakutaka Mariamu aaibishwe na pia alifikiri sana kuhusu maisha ya Mariamu na mwanae aliona aache maisha yaendelee yeye angeliweza kuoa mke mwingine, watu wasio na haki huaibisha wengine kwa kuanika wazi siri zao na kuwadhalilisha wengine.

Mathayo 1:18-21. “Kuzaliwa kwake Yesu Kristo kulikuwa hivi. Mariamu mama yake alipokuwa ameposwa na Yusufu, kabla hawajakaribiana, alionekana ana mimba kwa uweza wa Roho Mtakatifu. Naye Yusufu, mumewe, kwa vile alivyokuwa mtu wa haki, asitake kumwaibisha, aliazimu kumwacha kwa siri.Basi alipokuwa akifikiri hayo, tazama, malaika wa Bwana alimtokea katika ndoto, akisema, Yusufu, mwana wa Daudi, usihofu kumchukua Mariamu mkeo, maana mimba yake ni kwa uweza wa Roho Mtakatifu. Naye atazaa mwana, nawe utamwita jina lake Yesu, maana, yeye ndiye atakayewaokoa watu wake na dhambi zao.”

-          Kutunza siri kunadumisha mahusiano – Watu wanaotunza siri katika jamii wanaheshimika sana lakini wale wasiotunza siri wanaitwa hawana akili, wapumbavu, katika jamii yetu sisi wanaitwa wambeya, kuti kavu au watu ambao wana friji bovu, yaani friji lisilogandisha, ni nani atakufurahia kama anakuelezea mambo yake kisha unakwenda kumuanika, hii imekuwako hata makanisani, unamwamini mtu fulani unakwenda kukiri na kuungama dhambi zako kwake kesho kutwa anakuanika na kukutoa kwenye bomba, mnakwenda kupatanisha ndoa yenu kesho kutwa unatolewa mfano kwenye mahubiri, ukitunza siri za watu utaheshimiwa, kwa kuwa unatunza mahusiano mazuri ya watu kinyume cha hapo unaweza kusababisha fitina na mafarakano katika jamii

Mithali 25:8-9 “Usitoke nje kwa haraka ili kuyashindania; Usije ukakosa kujua la kutenda hatimaye, Mwenzako atakapokuwa amekuaibisha. Ujitetee na mwenzako peke yake; Bali usiifunue siri ya mtu mwingine;”

-          Kutunza siri kunakufanya uaminiwe na Mungu – Kuna mambo mengi sana ambayo Mungu aliyaweka wazi kwa Mariamu kuhusu mtoto Yesu na kama Mariamu asingelikuwa na kifua, Yesu angehujumiwa mapema sana Lakini Mariamu alikuwa mtu wa siri aliweka mambo moyoni, wakati mwingine Mungu hukufunulia jambo fulani ambalo labda unatakiwa kuliombea au ni maono ya siku zijazo na kwa sababu hiyo hayapaswi kusemwa, lakini kwa bahati mbaya ili watu wajionyeshe kuwa wao ni maalumu sana wanaweka wazi maono hayo badala ya kuyaweka moyoni na wamejikuta wanapoteza hata huduma zao au wanachukiwa kwa sababu ya kuropoka ropoka hivyo, Marimau alitunza moyoni mwake, maana yake alikuwa na siri kuhusu mambo makuu ya mwanaye yaani Yesu

Luka 2:15-19 “Ikawa, malaika hao walipoondoka kwenda zao mbinguni, wale wachungaji waliambiana, Haya, na twendeni mpaka Bethlehemu, tukalione hilo lililofanyika, alilotujulisha Bwana. Wakaenda kwa haraka wakamkuta Mariamu na Yusufu, na yule mtoto mchanga amelala horini. Walipomwona wakatoa habari waliyoambiwa juu ya huyo mtoto.Wote waliosikia wakastaajabu kwa hayo waliyoambiwa na wachungaji. Lakini Mariamu akayaweka maneno hayo yote, akiyafikiri moyoni mwake.”

-          Kutunza siri kunaepusha migogoro, mafarakano na hasara – watu wasioweza kuficha siri husababisha migogoro, mafarakano na hasara, daraja la chuki hujengeka kati ya watu waliowekwa wazi siri zao na aliyeweka wazi siri, usalama wa ndoa, familia, na hata taifa na taasisi, unaweza kuyumbishwa sana endapo watu watatoa siri na ndio maana wakati mwingine ili kutunza siri hizo viapo vinahusika katika kuhakikisha kuwa mtu ana apa kwa imani yake ili kutunza siri, hata hivyo kwa bahati mbaya wanadamu wanapenda umbeya na mtu akiwa na kitu moyoni hudhani kuwa akikitoa ndio atapata umaarufu kumbe anajivunjia heshima usitoe siri za watu.

Mithali 16:27-28 “Mtu asiyefaa kitu huchimba shimo la madhara; Katika midomo yake mna moto uteketezao. Mtu mshupavu huondokesha fitina; Na mchongezi huwafarakanisha rafiki.”

-          Kutunza siri kunahifadhi Usalama wa taifa na nchi – Serikali ina mambo nyeti, yanayohusu utunzaji wa nyaraka, ulinzi na usalama, mipango mikakati ya kitaifa, Serikali ina siri za kiusalama, siri za kiuchunguzi, siri za maamuzi ya ndani, na siri za watu,  siri hizo lazima zilindwe kwa sababu zinahusisha ustawi wa wengi na zinaweza kuleta madhara makubwa endapo zitavuja, sasa kama mambo yatavuja usalama wa nchi raia na viongozi unaweza kuwapo hatarini,  kwa hiyo kama u mfanya kazi katika sekta ya umma au serikalini na katika taasisi yoyote ile basi unapaswa kuwa na uwezo wa kutunza siri kwa kuheshimu mamlaka zilizoko, aidha watu wanaofanya kazi za za kikatibu au kwenye steshenari wanapaswa kuwa wasiri wa nyaraka za watu kwa uaminifu unapoapishwa usifanye tofauti na kiapo chako kiapo ni nadhiri hivyo ukishindwa kutimiza nadhiri umefanya upumbavu, kuweka nadhiri maana yake ni kujifunga au kuweka kiapo ya kuwa utafanya jambo kwa jina la Bwana hivyo kutokutimiza ahadi yako kwa Mungu kunaweza kukuponza, tafadhali sana hakikisha unatunza siri za kazini kwako, taifa lako na familia yako, rafiki zako, ndugu zako na kadhalika.

Kumbukumbu 23:21-23 “Utakapoweka nadhiri kwa Bwana, Mungu wako, usiwe mlegevu katika kuiondoa; kwa kuwa Bwana, Mungu wako, hataacha kuitaka kwako; nayo hivi itakuwa dhambi kwako. Lakini ukijizuia usiweke nadhiri, haitakuwa dhambi kwako. Yaliyotoka midomoni mwako yashike kuyafanya; kwa mfano wa ulivyomwekea nadhiri Bwana, Mungu wako, ni sadaka ya hiari uliyoahidi kwa kinywa chako.”

Muhubiri 5:4-6 “Wewe ukimwekea Mungu nadhiri, usikawie kuiondoa; kwa kuwa yeye hawi radhi na wapumbavu; basi, uiondoe hiyo uliyoiweka nadhiri. Ni afadhali usiweke nadhiri, Kuliko kuiweka usiiondoe. Usikiache kinywa chako kuukosesha mwili wako; wala usiseme mbele ya huyo malaika ya kwamba umepitiliwa; kwani Mungu akukasirikie sauti yako, na kuiharibu kazi ya mikono yako?              

-          Kutunza siri ni kuvuta muda mpaka baada ya wakati – Kuna siri ambazo haziwezi kufunuliwa kwa wakati fulani ili kuepusha madhara, na zinaweza kufunuliwa wakati muafaka ukifika ili mambo yasiharibike, kwa mfano mtihani unakuwa ni nyaraka ya siri kabla haujafanyika na siri ya mtihani huishia katika chumba cha mtihani na kisha karatasi za majibu hugeuka kuwa nyaraka ya siri mpaka mtihani utakaposahihishwa, baada ya majibu siri ya mtihani humalizika na mitihani hugeuka kuwa mitihani iliyopita maarifu kama Past papers, Yohana mbatizaji alipotaka kuzaliwa ililazimika baba yake kuwa bubu kwanza mpaka kijana alipozaliwa ndipo siri ilipowekwa wazi,kuwa alitokewa na malaika, tunajifunza hapo kuwa kuna mambo mengine hayapaswi kusemwa kwanza mpaka wakati wake utakapofika ndipo inapoweza kuwekwa wazi kwani mtu anaweza kuropoka kwa kiwewe kabala ya wakati, Malaika alijua kuwa Zekaria anaweza kuropoka maneno ya kutikuwa na imani hivyo mbingu zilitaka awe kimya mpaka mtoto alipozaliwa kwa hiyo nabii Zekaria alikuwa bubu mpaka Yohana alipozaliwa.

Luka 1:5-20 “Zamani za Herode, mfalme wa Uyahudi, palikuwa na kuhani mmoja, jina lake Zakaria, wa zamu ya Abiya, na mkewe alikuwa mmojawapo wa uzao wa Haruni, jina lake Elisabeti. Na wote wawili walikuwa wenye haki mbele za Mungu, wakiendelea katika amri zote za Bwana na maagizo yake bila lawama.Nao walikuwa hawana mtoto, maana Elisabeti alikuwa tasa, na wote wawili ni wazee sana. Basi ikawa, alipokuwa akifanya kazi ya ukuhani katika taratibu ya zamu yake mbele za Mungu, kama ilivyokuwa desturi ya ukuhani, kura ilimwangukia kuingia katika hekalu la Bwana ili kufukiza uvumba. Na makutano yote ya watu walikuwa wakisali nje saa ya kufukiza uvumba. Akatokewa na malaika wa Bwana, amesimama upande wa kuume wa madhabahu ya kufukizia. Zakaria alipomwona alifadhaika, hofu ikamwingia. Lakini yule malaika akamwambia, Usiogope, Zakaria, maana dua yako imesikiwa, na mkeo Elisabeti atakuzalia mtoto mwanamume, na jina lake utamwita Yohana. Nawe utakuwa na furaha na shangwe, na watu wengi watakufurahia kuzaliwa kwake. Kwa sababu atakuwa mkuu mbele za Bwana; hatakunywa divai wala kileo; naye atajazwa Roho Mtakatifu hata tangu tumboni mwa mamaye. Na wengi katika Waisraeli atawarejeza kwa Bwana Mungu wao.Naye atatangulia mbele zake katika roho ya Eliya, na nguvu zake, ili kuigeuza mioyo ya baba iwaelekee watoto, na kuwatilia waasi akili za wenye haki, na kumwekea Bwana tayari watu waliotengenezwa.  Zakaria akamwambia malaika, Nitajuaje neno hilo? Maana mimi ni mzee, na mke wangu ni mkongwe wa siku nyingi. Malaika akamjibu akamwambia, Mimi ni Gabrieli, nisimamaye mbele za Mungu; nami nimetumwa niseme nawe, na kukupasha habari hizi njema. Na tazama! Utakuwa bubu, usiweze kusema, mpaka siku ile yatakapotukia hayo, kwa sababu hukuyasadiki maneno yangu; nayo yatatimizwa kwa wakati wake.”

Habakuki 2:2-3 “Bwana akanijibu, akasema, Iandike njozi ukaifanye iwe wazi sana katika vibao, ili aisomaye apate kuisoma kama maji. Maana njozi hii bado ni kwa wakati ulioamriwa, inafanya haraka ili kuufikilia mwisho wake, wala haitasema uongo; ijapokawia, ingojee; kwa kuwa haina budi kuja, haitakawia.”

Hatari za kutoa siri.

Nadhani kama umefuatilia vizuri somo hili hatua kwa hatua utakuwa unaona pia madhara ya kutoa siri au hatari za kutoa siri, kutoa siri za mtu kunaweza kusababisha madhara makubwa na hata kusababisha kifo, watu wote duniani wana siri zinaweza kuwa siri nzuri au zinaaweza kuwa siri mbaya, kutoa siri kunaweza kukugharimu sana maisha yako, kunaweza kukujenga au kunaweza kukuharibu  na kunaweza kukubomoa, kwa hiyo mtu anapotaka kutoa siri ni lazima ajiulize mara mbilimbili anaitoa kwa nani na kwa manufaa gani na kama umeapishwa kutokutoa siri basi usizitoe kwa usalama wako, kwa nini usitoe siri?.

-          Kutoa siri ni ishara ya kukosa uaminifu na uadilifu – Ulimwamini mtu ukampa siri yako kisha yeye akaamua kukuanika na kuitoa ni Ishara ya kuwa mtu huyu sio mwaminifu na hana uadilifu, anapoitoa siri hiyo inaweza kuyagharimu maisha yako, usalama wako na hata kusababisha kifo, huu ni usaliti wa hali ya juu, sawa tu na jinsi Yuda alivyowaongoza watu waliokuja kumkamata Yesu, kwa sababu alijua kuwa Yesu atakuwa eneo gani na sehemu gani, anapatikana wapi na mida gani na akawaongoza maadui, wa Yesu mpaka kwenye bustani ya Geththemane. Watu wengi wamedhuriwa na wale waliowaamini, waliodhani kuwa watawatunzia siri zao hao hao ndio wakawa sababu ya uharibifu na maumivu mengi katika maisha, kwa hiyo tunajifunza pia usimpe siri yako mtu ambaye bado hujamuelewa, mtu anayeweza kukudhuru ni yule ambaye anakujua nje ndani ndani nje lakini sio hivyo tu Shetani hupenda kuwatumia watu wanaotujua vema ili kukuharibia maisha yako na kukuletea uhungu mkubwa katika maisha kwa hiyo usimuamini kila mtu wala usitoe siri yako kwa kila mtu, na kama unajua mambo ya mtu usiyatoe mpaka kwa idhini yake au umuone yeye mwenyewe kwanza ili kupata uhakika.

Zaburi 41:9 “Msiri wangu tena niliyemtumaini, Aliyekula chakula changu, Ameniinulia kisigino chake.”

Luka 22:47-48 “Basi alipokuwa katika kusema, tazama, mkutano wa watu, na yule aitwaye Yuda, ambaye ni mmoja wa wale Thenashara, amewatangulia. Akamkaribia Yesu ili kumbusu.Yesu akamwambia, Yuda, wamsaliti Mwana wa Adamu kwa kumbusu?

-          Kutoa siri kunaweza kusababisha madhara na hasara kwa wengine na taifa – Ziko siri ambazo zikitolewa zinaweza kuwa na madhara makubwa kwa mtu, watu au taifa na kusababisha hasara, upotevu na uharibifu au uvunjifu wa mahusiano, kama kifua chako hakiwezi kustahimili kutunza vitu basi ni muhimu kwako ukafanya tathimini kwanza kabla ya kuropoka unayotaka kuyaropoka, Samsoni alitoa siri yake kwa mwanamke wa kifilisti aliyekuwa mpelelezi ambaye aliweza kusababisha madhara kwa Samsoni na kuharibu maisha yake na huduma.

Waamuzi 16:15-21 “Mwanamke akamwambia, Wawezaje kusema, Nakupenda; na moyo wako haupo pamoja nami? Umenidhihaki mara hizi tatu, wala hukuniambia asili ya nguvu zako nyingi. Ikawa, kwa vile alivyomsumbua kwa maneno yake kila siku, na kumwudhi, roho yake ikadhikika hata kufa.Ndipo alipomwambia yote yaliyokuwa moyoni mwake, akamwambia, Wembe haukupita juu ya kichwa changu kamwe; maana mimi nimekuwa Mnadhiri wa Mungu, tangu tumboni mwa mama yangu; nikinyolewa, ndipo nguvu zangu zitanitoka, nami nitakuwa dhaifu, nitakuwa kama wanadamu wenzangu. Delila alipoona ya kuwa amemwambia yote yaliyokuwa moyoni mwake, akatuma mtu akawaita wakuu wa Wafilisti, akisema, Njoni huku mara hii tu, maana ameniambia yote aliyo nayo moyoni mwake. Ndipo wakuu wa Wafilisti wakamwendea wakachukua ile fedha mikononi mwao.Naye akamlaza usingizi magotini pake. Kisha akamwita mtu akavinyoa vile vishungi saba vya nywele za kichwa chake; akaanza kumsumbua, nguvu zake zikamtoka. Kisha akasema, Samsoni, Wafilisti wanakujia. Akaamka katika usingizi wake, akasema, Nitakwenda nje kama siku nyingine, na kujinyosha. Lakini hakujua ya kuwa Bwana amemwacha. Wafilisti wakamkamata, wakamng'oa macho; wakatelemka naye mpaka Gaza, wakamfunga kwa vifungo vya shaba; naye alikuwa akisaga ngano katika gereza.”

-          Kutoa siri kunaweza wakati mwingine kusababisha kumkosea Mungu – Yako mambo ambayo Mungu anaweza kuyafunua kwako au kuyaeleza kwako kama siri na wakati wake ukawa bado, na kama utalisema kabla ya wakati unaweza kuharibu mambo, na kuvuruga mpango wa Mungu, kwani Mungu anao Muda maalumu labda wa kufunuliwa kwa jambo hilo, jua basi ni wakati gani wa kusema na ni wakati gani wa kunyamaza.

Mathayo 17:9 “Na walipokuwa wakishuka mlimani, Yesu aliwaagiza, akasema, Msimwambie mtu ye yote habari ya maono hayo, hata Mwana wa Adamu atakapofufuka katika wafu.”

Muhubiri 3:1-7 “Kwa kila jambo kuna majira yake, Na wakati kwa kila kusudi chini ya mbingu. Wakati wa kuzaliwa, na wakati wa kufa; Wakati wa kupanda, na wakati wa kung'oa yaliyopandwa; Wakati wa kuua, na wakati wa kupoza; Wakati wa kubomoa, na wakati wa kujenga; Wakati wa kulia, na wakati wa kucheka; Wakati wa kuomboleza, na wakati wa kucheza; Wakati wa kutupa mawe, na wakati wa kukusanya mawe; Wakati wa kukumbatia, na wakati wa kutokumbatia; Wakati wa kutafuta, na wakati wa kupoteza; Wakati wa kuweka, na wakati wa kutupa; Wakati wa kurarua, na wakati wa kushona; Wakati wa kunyamaza, na wakati wa kunena;”

-          Kutoa siri kunaweza kusababisha fedheha – Kutoa siri kunaweza kumsababishia mtu mwingine fedheha au wewe unayetoa siri ukajikuta unafedheheka, kutunza siri ni hekima uaminifu na heshima unapokuwa mwaminifu kutunza siri utaaminiwa sio tu na wanadamu bali hata Mungu pia,

Mithali 13:2-3 “Mtu atakula mema kwa matunda ya kinywa chake; Bali nafsi ya mtu haini itakula jeuri.Yeye alindaye kinywa chake huilinda nafsi yake; Bali afunuaye midomo yake atapata uharibifu.”

Yakobo 3:2-5 “Angalieni, twatia lijamu katika vinywa vya farasi, ili wamtii, hivi twageuza mwili wao wote. Tena angalieni merikebu; ingawa ni kubwa kama nini, na kuchukuliwa na pepo kali, zageuzwa na usukani mdogo sana, ko kote anakoazimia kwenda nahodha. Vivyo hivyo ulimi nao ni kiungo kidogo, nao hujivuna majivuno makuu. Angalieni jinsi moto mdogo uwashavyo msitu mkubwa sana.”

-          Kutoa siri kunaharibu uhusiano na kubomoa kuaminika – Mithali 17:9 “Afunikaye kosa hutafuta kupendwa; Bali yeye akashifuye neno hutenga rafiki.” Una rafiki umemuamini unajifunua kwake na kumueleza kila kitu chako kisha kesho unasikia habari zimeenea mtaani, ni wazi kuwa kama hukutaka siri hiyo ifunuliwe kwa watu, kutasababisha mafarakano mgawanyiko na maumivu lakini pia kuvunjika kwa urafiki na uhusiano, kimsingi mtu anapotoa siri zako pia ni kama anatangaza kuwa hakupendi na anakuchukia, neno la Mungu linasema upendo husitiri wingi wa dhambi, kama mtu unampenda hutapenda kuweka wazi mambo yake hata kama ni mabaya kwa hiyo kuanika siri za mtu ni ishara ya kuwa unamchukia mtu huyo, ziko kanuni kwa mfano ambazo haziwezi kutolewa bila kibali cha wenyewe? Kanuni kwa mfano za kutengeneza Cocacola, au Colgate na kadhalika ni siri ya viwanda husika hata katika bidhaa ndogo ndogo watu wana kanuni zao mpaka za kutengeneza maandazi n.k.

1Petro 4:8 “Zaidi ya yote iweni na juhudi nyingi katika kupendana; kwa sababu upendano husitiri wingi wa dhambi.”

-          Kutoa siri ni kujivunjia heshima – wengi wa watu wanaotoa siri Fulani wanadhani watapata heshima lakini badala yake wanajivunjia heshima, neno la Mungu linasema watu watakaposikia hawatamdharau uliyemtolea siri badala yake utadharauliwa wewe uliyetoa siri, unatoa siri kwa lengo gani? Ni ili mtu asikubalike? ni ili kumchafua mtu? Ni ili wewe uonekane kuwa ni mtu maalumu sana

Mithali 18:6-8 “Midomo ya mpumbavu huingia katika fitina, Na kinywa chake huita mapigo. Kinywa cha mpumbavu ni uharibifu wake, Na midomo yake ni mtego wa nafsi yake. Maneno ya mchongezi ni kama vitoweo; Nayo hushukia pande za ndani za tumbo.”

Neno la Mungu linakutaka kama una neno na mtu muitane ninyi wenyewe na kuyamaliza wenyewe, kwa hiyo unaposikia neno kuhusu mtu mwite yeye mwenyewe kwa ufafanuzi na maonyo na mkilelewana umempata nduguyo mpaka ikishinidkana basi unaweza kumuhesabu kama mtu asiye na lolote

Mathayo 18:15-17 “Na ndugu yako akikukosa, enenda ukamwonye, wewe na yeye peke yenu; akikusikia, umempata nduguyo. La, kama hasikii, chukua pamoja nawe tena mtu mmoja au wawili, ili kwa vinywa vya mashahidi wawili au watatu kila neno lithibitike. Na asipowasikiliza wao, liambie kanisa; na asipolisikiliza kanisa pia, na awe kwako kama mtu wa mataifa na mtoza ushuru.”

-          Kutoa siri katika mapenzi ya Mungu – Katika mazingira Fulani mtu anaweza kutoa siri katika mapenzi ya Mungu japo sio hekima kufanya hivyo kwani kunaweza kuhatarisha maisha yako lakini watu wa Mungu wakati mwingine tunapaswa kuwa waaminifu hata kufa, Hatuwezi kufumbia macho uovu, Serikali au taasisi zinazoongozwa na watu, na watu hawa wana Imani na wakati mwingine watu wanaweza kuwa waovu, kama kutakuwa na Rushwa, ufisadi, wizi wa kura, uonevu mauaji, na vitendo vyovyote vile vinavyopingana na haki za binadamu na mambo yote yanayohusisha dhambi na uovu na mambo hayo yako kinyume na mapenzi ya Mungu. Utamuomba Mungu na utatumia hekima au utaratibu wa kisheria, si kwa fujo wala uasi utaionya na kukemea serikali au kutoa taarifa zenye ushahidi juu ya uovu wote unaofanywa na serikali au viongozi wake lakini sio kwa tamaa chuki au uzembe au kwa kusudi la kumchafua mtu, au kutaka sifa, kemea uovu huo, ingawa inaweza kugharimu maisha yako

Matendo 5:26-29 “Ndipo yule jemadari akaenda pamoja na watumishi, wakawaleta, lakini si kwa nguvu, kwa maana waliogopa watu wasije wakawapiga kwa mawe. Walipowaleta, wakawaweka katika baraza. Kuhani Mkuu akawauliza, akisema, Je! Hatukuwaamuru ninyi kwa nguvu, msifundishe kwa jina hili? Nanyi, tazameni, mmeijaza Yerusalemu mafundisho yenu, na mnataka kuileta damu ya mtu yule juu yetu. Petro na mitume wakajibu, wakisema, Imetupasa kumtii Mungu kuliko wanadamu.”

Mathayo 14:3-4 “Maana Herode alikuwa amemkamata Yohana, akamfunga, akamtia gerezani, kwa ajili ya Herodia, mke wa Filipo nduguye. Kwa sababu Yohana alimwambia, Si halali kwako kuwa naye.”

Serikali ina haki ya kulinda siri na kuadhibu wale wanaozivunja kwa mujibu wa sheria, lakini serikali haina mamlaka ya kumuua mtu kwa kosa la kuvujisha siri, Mungu anachukizwa na mauaji yanayofanywa kwa jina la kimamlaka kwa sababu uhai ni mali ya Mungu kwa hiyo hakuna mtu mwenye haki ya kuondoa uhai wa mwingine, Mtu akivunja kiapo cha utoaji siri ataadhibiwa kwa mujibu wa sheria ziliowekwa kwa haki, lakini swala la hukumu ya kifo sio haki ya mwanadamu kwa sababu uhai wa mtu ni mali ya Mungu, Uhai ni mali ya Mungu.

Narudia tena ni makosa kutoa siri hata  hivyo si halali kumuua mtu kwa sababu ya kutoa siri na badala yake mtu aliyetoa siri au atakayetoa siri anaweza kushitakiwa kwa kanuni za haki za binadamu, swala la uhai wa binadamu liko mikononi mwa Mungu yeye ndiye mwamuzi mwenye haki, hivyo serikali yoyote ile hairuhusiwi kumuua mtu kwa sababu ametoa siri, badala yake adhabu za kisheria zinapaswa kuchukua mkondo wake hasa kama amehatarisha usalama wa taifa lakini kimaandiko uhai ni mali ya Mungu na hakuna mtu anatakiwa kufa kwa hilo

Yakobo 4:11-12 “Ndugu, msisingiziane; amsingiziaye ndugu yake, au kumhukumu ndugu yake, huisingizia sheria na kuihukumu sheria. Lakini ukiihukumu sheria, huwi mtenda sheria, bali umekuwa hakimu.Mtoa sheria na mwenye kuhukumu ni mmoja tu, ndiye awezaye kuokoa na kuangamiza. U nani wewe umhukumuye mtu mwingine?

Wewe mwenyewe pia unayo haki ya kuweka dhambi zako wazi na kuziungama mbele za Mungu endapo umemkosea Mungu huko utaeleza siri zako na Mungu ni mwaminifu atakupa rehema, kwa sababu kama tunaishi kwa unafiki Mungu sio mnafiki siku ya hukumu ataleta hukumuni kila jambo na kila tendo la siri  

Mithali 28:13 “Afichaye dhambi zake hatafanikiwa; Bali yeye aziungamaye na kuziacha atapata rehema.”

1Yohana 1:8-10 “Tukisema kwamba hatuna dhambi, twajidanganya wenyewe, wala kweli haimo mwetu. Tukiziungama dhambi zetu, Yeye ni mwaminifu na wa haki hata atuondolee dhambi zetu, na kutusafisha na udhalimu wote.Tukisema kwamba hatukutenda dhambi, twamfanya Yeye kuwa mwongo wala neno lake halimo mwetu.”

Muhubiri 12:14 “Kwa maana Mungu ataleta hukumuni kila kazi, pamoja na kila neno la siri, likiwa jema au likiwa baya.”          

 

Na. Rev. Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima