Tito 1:7-9 “Maana imempasa askofu awe mtu asiyeshitakiwa neno, kwa kuwa ni wakili wa MUNGU; asiwe mtu wa kujipendeza nafsi yake, asiwe mwepesi wa hasira, asiwe mlevi wala mgomvi, asiwe mpenda mapato ya aibu.bali awe mkaribishaji, mpenda wema, mwenye kiasi, mwenye haki, mtakatifu, mwenye kudhibiti nafsi yake; akilishika lile neno la imani vile vile kama alivyofundishwa, apate kuweza kuwaonya watu kwa mafundisho yenye uzima, na kuwashinda wenye kupinga.”
Utangulizi:
Mojawapo ya sifa muhimu za
viongozi wa kanisa ni pamoja na kuwa waaminifu katika mafundisho sahihi ya
imani yetu (Sound Doctrine) na neno
la Mungu, Paulo mtume alikuwa amemuacha Tito mtenda kazi pamoja naye katika
makanisa yaliyokuwa katika kisiwa cha Krete moja ya kisiwa kikubwa na maarufu
sana katika nchi ya Ugiriki, kwa kusudi la kuweka viongozi zamani waliitwa
wazee (yaani wachungaji) katika makanisa yaliyokuwako huko.
Tito 1:4-5 “kwa Tito, mwanangu hasa katika
imani tuishirikiyo. Neema na iwe kwako na amani zitokazo kwa Mungu Baba na kwa
Kristo Yesu Mwokozi wetu. Kwa sababu hii nalikuacha Krete, ili uyatengeneze
yaliyopunguka, na kuweka wazee katika kila mji kama vile nilivyokuamuru;”
Hata hivyo katika sifa kadhaa
zilizoainishwa na Paulo Mtume kwaajili ya kuchagua viongozi mojawapo ya sifa muhimu
sana ilikuwa inahusu kuchagua au kuweka watu ambao watalifundisha neno la Mungu
vile vile kama wao walivyofundishwa, hili ilikuwa ni agizo muhimu sana kwa
sababu Mafundisho sahihi ni sawa kabisa na mlo kamili wa chakula chenye
virutubisho vyote muhimu vinavyohitajika katika mwili wa mwanadamu na
mafundisho sahihi vile vile ni ya muhimu katika kanisa la Mungu kwa mustakabali
wa kanisa kuwa na Afya njema, ukuaji mzuri wa kiroho, uhakika wa wokovu, na
ulinzi wa kanisa dhidi ya mafundisho potofu, kuwanoa waamini, kukuza umoja wa
kanisa na kuutunza utakatifu na maisha ya haki kutendeka kwa kazi ya huduma.
Kwa msingi huo Kanisa linapochagua watenda kazi, wanafunzi na wenye hekima
linapaswa kuhakikisha kuwa watu hao wanateuliwa kwa sababu wameshiba mafundisho
yaliyo sahihi na wako tayari kwa huduma na si kwa sababu wana cheo, pesa na
heshima fulani huko duniani, kwa Msingi huo leo tutachukua muda kujifunza somo
hili muhimu “Akilishika neno la Imani
vile vile kama alivyofundishwa!”, na tutajifunza somo hili kwa kuzingatia
vipengele vitatu vifuatavyo:-
·
Maana ya
kulishika neno la Imani vile vile.
·
Umuhimu
wa kulishika neno la Imani vile vile kama ulivyofundishwa.
·
Akilishika
neno la Imani vile vile kama alivyofundishwa!,
Maana ya kulishika neno vile vile.
Ni muhimu kufahamu kuwa kulishika
neno la Mungu vile vile kama unavyofundishwa maana yake kwa Kiyunani linatumika neno “antechomenon” au “antechomai” ambalo kwa kiingereza linatumika
neno “holding fast to” au “adhering to” au “clinging” au “to hold
firm” kwa lugha nzuri ya Kiswahili maana yake ni kushikamana, kung’ang’ania au
kutetea kwa uthabiti, kwa hiyo moja ya sifa ya kiongozi wa kanisa anapaswa
kuwa king’ang’anizi, linapokuja
swala la kushikamana na Mungu au
mafundisho yake hapaswi kuwa mtu unayeyumbishwa, anapaswa kuwa mtu mwenye uwezo
wa kusimamia kile unachokiamini kwa nguvu na hakuna mtu wa kukubadilisha.
Ayubu 2:9-10 “Ndipo mkewe akamwambia, Je!
Wewe hata sasa washikamana na utimilifu wako? Umkufuru Mungu, ukafe. Lakini
yeye akamwambia, Wewe wanena kama mmoja wa hao wanawake wapumbavu anenavyo. Je!
Tupate mema mkononi mwa Mungu, nasi tusipate na mabaya? Katika mambo hayo yote
Ayubu hakufanya dhambi kwa midomo yake.”
Sifa ya kushikamana na mafundisho
ya mitume au injili ya kweli na mafundisho yaliyo sahihi ilikuwa na umuhimu
mkubwa sana nyakati za kanisa la kwanza kama ilivyo na umuhimu mkubwa zaidi
katika nyakati za leo, kwa hiyo mtu aliyependekezwa kuwa kiongozi alipaswa kuwa
na sifa ya kuenenda vile vile kama alivyofundishwa, hakuna uhuru wa kuibadili
injili, kwa hiyo kiongozi alikuwa hawezi kupotoshwa wala kuyumbishwa na hawezi
kuogopa au kusita kuukemea uwongo, Lengo la kuwafanya wakristo kuwa wanafunzi
ni ili wasivutwe kufuata mafundisho ya uongo.
Waefeso 4:11-14 “Naye alitoa wengine kuwa
mitume, na wengine kuwa manabii; na wengine kuwa wainjilisti na wengine kuwa
wachungaji na waalimu; kwa kusudi la kuwakamilisha watakatifu, hata kazi ya
huduma itendeke, hata mwili wa Kristo ujengwe; hata na sisi sote tutakapoufikia
umoja wa imani na kumfahamu sana Mwana wa Mungu, hata kuwa mtu mkamilifu, hata
kufika kwenye cheo cha kimo cha utimilifu wa Kristo; ili tusiwe tena watoto
wachanga, tukitupwa huku na huku, na kuchukuliwa na kila upepo wa elimu, kwa
hila ya watu, kwa ujanja, tukizifuata njia za udanganyifu.”
2Timotheo 4:2-4 “lihubiri neno, uwe tayari,
wakati ukufaao na wakati usiokufaa, karipia, kemea, na kuonya kwa uvumilivu
wote na mafundisho. Maana utakuja wakati watakapoyakataa mafundisho yenye
uzima; ila kwa kuzifuata nia zao wenyewe watajipatia waalimu makundi makundi,
kwa kuwa wana masikio ya utafiti; nao watajiepusha wasisikie yaliyo kweli, na
kuzigeukia hadithi za uongo.”
Nyakati za kanisa la kwanza
walikuwa makini sana kuhakikisha kuwa mtu wanayemkaribisha anakuwa na imani ile
ile iliyofundishwa na kukubalika na mitume, Mitume waliagiza kuwa hakukuwa na
sababu ya kumchekea mtu ambaye hakai au haleti mafundisho yao, walikazia kuwa
mtu wa namna hiyo ikiwezekana wasimkaribishe wala hata wasimsalimie, mwenye
dhambi anaweza kubadilika hata pole pole, lakini mafundisho ya uongo hata
salamu asipewe
2Yohana 1:8-11 “Jiangalieni nafsi zenu
msiyapoteze mliyoyatenda, bali mpokee thawabu timilifu. Kila apitaye cheo, wala
asidumu katika mafundisho ya Kristo, yeye hana Mungu. Yeye adumuye katika
mafundisho hayo, huyo ana Baba na Mwana pia. Mtu akija kwenu, naye haleti
mafundisho hayo, msimkaribishe nyumbani mwenu, wala msimpe salamu. Maana yeye
ampaye salamu azishiriki kazi zake mbovu.”
Kanisa linapaswa kusimamia
msimamo huu, kuhakikisha kuwa kila mtu anayekaribishwa katika kanisa letu
anakuja na fundisho lililo sahihi, anakuja na msimamo ule ule waliokuwa nao
mitume wa Bwana wetu Yesu Kristo, au mtu anayechaguliwa kuwa kiongozi katika
kanisa analishika neno la imani vile vile kama tulivyofundishwa na sio
vinginevyo, mafundisho ya mitume yanapaswa kushikiliwa kama mila na desturi ya
kanisa na kurithishwa katika kizazi kinachokuja hata akifufuka Paulo mtume leo
atatukuta tukihubiri injili ile ile aliyoiacha na atatukuta hatujaichakachua
injili wala hatuhubiri injili nyingine, na tutakemea kwa Mamlaka yote, kuonya
na kukaripia. Kwa mafundisho yenye uzima. Haiwezekani Leo kiongozi mkubwa
kabisa wa imani hatambui utatu na anachekewa
Umuhimu wa kulishika neno la imani vile vile kama ulivyofundishwa
Ni muhimu kufahamu kuwa mitume
walikuwa wakali sana na swala zima la mfundisho ya uwongo kuliko tunavyofikiri,
kwa bahati mbaya makanisa mengi leo wamekuwa wakali kwa dhambi jambo ambalo sio
baya, kuliko kwa mafundisho potofu, dhambi inaweza kutubiwa na mwenye dhambi
anaweza kubadilika, ukuaji wa kiroho ni mchakato na sio jambo la hatari kwa
kanisa kwa sabahu Kristo alikuja kuokoa, lakini mafundisho potofu ni chachu na
inaweza kubadilisha na kuathiri muelekeo mzima wa mwili wa Kristo na kwa sababu
hiyo mitume walikuwa wakali sana na watu wanaofundisha uongo, Paulo mtume
anamwagiza Tito kuwa makini kuwachagua watu wenye msimamo katika mafundisho yetu
kwa sababu kisiwa cha Krete kilikuwa ni miongoni mwa sehemu zilizoathiriwa na
mafundisho ya uongo kwa hiyo waliopendekezwa kuchaguliwa kuwa viongozi
walipaswa kuwa watu hodari ambao wanauwezo wa kufundisha, kukemea, kuonya na kuwazidi wale wanaowapinga au wale
wanaoipinga kweli
Tito 1:4-5 “kwa Tito, mwanangu hasa katika
imani tuishirikiyo. Neema na iwe kwako na amani zitokazo kwa Mungu Baba na kwa
Kristo Yesu Mwokozi wetu. Kwa sababu hii nalikuacha Krete, ili uyatengeneze
yaliyopunguka, na kuweka wazee katika kila mji kama vile nilivyokuamuru;”
Tito 1:7-9 “Maana imempasa askofu awe mtu
asiyeshitakiwa neno, kwa kuwa ni wakili wa MUNGU; asiwe mtu wa kujipendeza
nafsi yake, asiwe mwepesi wa hasira, asiwe mlevi wala mgomvi, asiwe mpenda
mapato ya aibu.bali awe mkaribishaji, mpenda wema, mwenye kiasi, mwenye haki,
mtakatifu, mwenye kudhibiti nafsi yake; AKILISHIKA LILE NENO LA IMANI VILE VILE
KAMA ALIVYOFUNDISHWA, apate kuweza kuwaonya watu kwa mafundisho yenye uzima, na
kuwashinda wenye kupinga.”
Kulikuwa na walimu wa uongo kule
Krete, watu walikazia sheria ya Musa na mafundisho ya tohara, na pia watu
walijitafutia mapato kupitia dini, kwa sababu hiyo suluhisho halikuwa miujiza
bali suluhisho lilikuwa ni kupata watu sahihi watakaosimamia misingi ya Imani
ya mitume na kuifundisha vile vile kama walivyofundishwa na wenye sifa ya
kuweza kung’amua na kuyapinga au kuwashinda wale wenye kupinga kama alivyokuwa
mtu wa Mungu Stefano, Paulo alikuwa anataka viongozi wawe wakali kwenye
fundisho sahihi wenye sifa za ugumu wa kusimamia Imani na kupinga mafundisho ya
uongo na kuwakemea waongo kwa nguvu zao zote, watu wenye uwezo wa kuwashinda
wapingao na kuisimamia Imani kwa uaminifu hata kaa itawagharimu kufa
Tito 1:10-14 “Kwa maana kuna wengi
wasiotii, wenye maneno yasiyo na maana, wadanganyaji, na hasa wale wa tohara,
ambao yapasa wazibwe vinywa vyao. Hao wanapindua watu wa nyumba nzima,
wakifundisha yasiyowapasa kwa ajili ya mapato ya aibu. Mtu wa kwao, nabii wao
wenyewe, amesema, Wakrete ni waongo siku zote, hayawani wabaya, walafi wavivu.
Ushuhuda huo ni kweli. Kwa sababu hiyo uwakemee kwa ukali, ili wapate kuwa
wazima katika imani; wasisikilize hadithi za Kiyahudi, wala maagizo ya watu
wajiepushao na yaliyo kweli.”
Matendo 6:8-10 “Na Stefano, akijaa neema na
uwezo, alikuwa akifanya maajabu na ishara kubwa katika watu. Lakini baadhi ya
watu wa sinagogi lililoitwa sinagogi la Mahuru, na la Wakirene, na la
Waiskanderia, na la wale wa Kilikia na Asia, wakaondoka na kujadiliana na
Stefano;lakini hawakuweza kushindana na hiyo hekima na huyo Roho aliyesema naye.”
Kanisa linapaswa kuwa makini kuhakikisha
kuwa linasimamisha watu waliojaa neno la Mungu, watu wenye injili iliyosahihi,
watu wanaofunzwa vizuri ili kuirithisha Imani iliyosahihi kwa kizazi
kinachokuja, leo hii kumejaa upuuzi wa kila aina kila kona kwa sababu ya uzembe
wa Kanisa, Kanisa linafukuzana na mambo mengine na linaacha kuwafanya watu kuwa
wanafunzi wa neno la Mungu, ni lazima tuikabidhi injili kwa watu waaminifu
watakaofaa kuwafundisha na wengine vile vile kama walivyofundishwa, dunia
ikijawa na mafundisho ya uongo leo sababu kubwa ni uzembe wa Kanisa kutokuwafundisha
watu neno la Mungu, Kanisa ni lazima liwe kama shule ukiachanana maombezi na miujiza
ambayo nayo ni ya muhimu lakini bila kusahau kuwafundisha watu neno, watu ni
lazima wajae neno, dunia ni lazima ijawe na mafundisho yetu mpaka wakuu wa dini
pinzani walalamike kama ilivyotokea kwa Masadukayo.
2Timotheo 2:2 “Na mambo yale uliyoyasikia
kwangu mbele ya mashahidi wengi, hayo uwakabidhi watu waaminifu watakaofaa
kuwafundisha na wengine.”
Matendo 5:27-29 “Walipowaleta, wakawaweka
katika baraza. Kuhani Mkuu akawauliza, akisema, Je! Hatukuwaamuru ninyi kwa
nguvu, msifundishe kwa jina hili? Nanyi, tazameni, mmeijaza Yerusalemu
mafundisho yenu, na mnataka kuileta damu ya mtu yule juu yetu. Petro na mitume
wakajibu, wakisema, Imetupasa kumtii Mungu kuliko wanadamu.”
Kila kanisa ambalo linaamini kuwa
lina mafundisho ya kweli basi lina wajibu wa kuijaza dunia na mafundisho hayo
ya kweli kwa kuihubiri injili kila mahali, kufanya wanafunzi na kuijaza dunia
na mafundisho yetu, kama hatufanyi kazi hiyo itafanywa kwa uaminifu na
mashahidi wa Yehova, Mormonisim, Wasabato, na imani nyinginezo nyingi, injili
za mafanikio, injili za neema iliyozidi, injili za sheria, na injili nyingine
nyingi na usikasirike wakiwa na televisheni, magazeti na washuhudiaji wanapita
nyumba kwa nyumba wakieneza mafundisho yao maana wewe hutaki na mafundisho yako
lakini pembeni pembeni unadai una Imani ya kweli lakini umekaa nayo kimya na
kazi yako ni kukosoa tu pembeni utasikia jihadharini na mafundisho ya
mitandaoni, ahaaaa we ya kwako ya mitandaoni yako wapi na kwa nini hurushi? Kwa
hiyo wadhani Kristo hana wanaohubiri kweli mitandaoni? Mwone kwanza lihubiri
neno fundisha kweli eneza kweli kwa njia zozote, wafundishe washirika
kupambanua mchele na chuya!
Akilishika neno la Imani vile vile kama alivyofundishwa!.
Unadhani kuna faida gani ya kuwa
na umati mkubwa wa watu, kuwa na sauti nzuri, kuwa na karama za kila aina, kutajirika
na kubarikiwa sana na kuwa na walinzi na msafara wa magari lakini ukawa
hauifundishi kweli? Kiongozi wa kweli wa imani ni lazima awe mwanafunzi mzuri
wa neno la Mungu, awe mtetezi wa kweli wa imani, awe na uwezo wa kung’amua
uongo na kuukemea kwa nguvu na kuukaripia au kuujibu kwa neno la Mungu, lakini
zaidi sana awe mwaminifu kwa mafundisho ya mitume, na sio kwa sababu umerithi
tu bali pia kwa sababu umelichunguza na kujithibitishia kuwa unaamini jambo
lililo sahihi, mmesikia siku za Karibuni katika mitandao wahubiri wakubwa
kabisa wenye umati mkubwa wa watu wakikanusha na kuushambulia na kupinga fundisho
la utatu wa Mungu na watu wenye kweli wamekaa kimya tu hii ni mojawapo ya
hatari iliyo wazi kuwa nyakati za leo tuna watu wengi tu wanaofuata mkumbo,
kama watu wangekuwa wanafundishwa kweli ya Mungu kwa usahihi na wakawa na uwezo mkubwa wa kupambanua nadhani
siku ile wanamsikia kiongozi wao akisema hakuna Utatu ingekuwa ndio siku ya
mwisho kuabudu hapo, lakini dunia imejaa vipofu, na viongozi wa vipofu, wala
hawaoni kuwa hili ni tatizo kubwa!.
Kama kanisa tangu mwanzo
lingezalisha watu wasioyumbishwa, imani yetu ingebaki kama ilivyokuwa nyakati
za baba zetu, lakini siku za leo kumejaa nyumbu wengi makanisani ambao
wanayumbishwa kila kukicha na Imani mbalimbali na imekuwa ngumu kwao leo kujua
ipi ni sahihi na ipi ni potofu watu hawajui kupambanua. Mtu anayeishika Imani
vile vile ni mtu asiyetikisika kwa sababu anajua alichokiamini na hawatikiswi
na lolote wanashikamana na kile walichokiamini bila kujali wanapitia nini
-
2Timotheo
1:12-14 “Kwa sababu hiyo nimepatikana na mateso
haya, wala sitahayari; kwa maana namjua yeye niliyemwamini, na kusadiki ya
kwamba aweza kukilinda kile nilichokiweka amana kwake hata siku ile. Shika
kielelezo cha maneno yenye uzima uliyoyasikia kwangu, katika imani na upendo
ulio katika Kristo Yesu. Ilinde ile amana nzuri kwa Roho Mtakatifu akaaye ndani
yetu.”
-
Matendo
5:27-29. “Walipowaleta, wakawaweka katika baraza.
Kuhani Mkuu akawauliza, akisema, Je! Hatukuwaamuru ninyi kwa nguvu, msifundishe
kwa jina hili? Nanyi, tazameni, mmeijaza Yerusalemu mafundisho yenu, na mnataka
kuileta damu ya mtu yule juu yetu. Petro na mitume wakajibu, wakisema,
Imetupasa kumtii Mungu kuliko wanadamu.”
Kanisa ni lazima tujikite katika
kuandaa viongozi ambao watakuwa watata, wenye kumfuata Yesu na kukataa
kuyachakachua maneno ya Mungu kwa gharama yoyote hata kama itawagharimu
kuteseka na kuuawa, lazima tuzalishe viongozi mahiri wenye uwezo wa kumuigiza
Yesu, kuwa hatukuja duniani kuwapendeza wanadamu bali tumekuja kuwatumikia watu
kama yeye mwenyewe, lazima tuzalishe watu wenye nguvu, wenye akili wanaolijua
neno ambao watasimama kuitetea Imani hata wakati wa mambo magumu na kuwasaidia
watu kuijua kweli na kuisimamimai kwa gharama yoyote kwa sababu hiyo pamoja na
sifa nyingine isisahahulike sifa hii muhimu ya kwamba imempasa askofu au
kiongozi wa kanisa awe mtu anayeisimamia Imani vile vile kama alivyofundishwa .
Tito 1:7-9 “Maana imempasa askofu awe mtu
asiyeshitakiwa neno, kwa kuwa ni wakili wa MUNGU; asiwe mtu wa kujipendeza
nafsi yake, asiwe mwepesi wa hasira, asiwe mlevi wala mgomvi, asiwe mpenda
mapato ya aibu.bali awe mkaribishaji, mpenda wema, mwenye kiasi, mwenye haki,
mtakatifu, mwenye kudhibiti nafsi yake; akilishika lile neno la imani vile vile
kama alivyofundishwa, apate kuweza kuwaonya watu kwa mafundisho yenye uzima, na
kuwashinda wenye kupinga.”
Na. Rev. Innocent Samuel Kamote
Mkuu wa wajenzi mqwenye Hekima


